Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Ameer wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Watembeleaji wa Ukurasa Wake wa Facebook "Fiqhi"
Jibu la Swali
Kwa Ahmed Al-Qairawan
Swali:
Assalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh Sheikh Ata, nina swali muhimu sana nalo ni: Je, hukumu ya rajm (kupigwa mawe) imetajwa ndani ya Qur’ani au katika hadith sahihi mutawatir? Nimefanya utafiti kuhusu hili na sikuelewa kwa nini hukumu hii inaingizwa katika sheria wakati haikutajwa ndani ya Qur’ani kama vile mwizi mwanamume na mwizi mwanamke basi ikateni mikono yao, au mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume basi wapigeni mijeledi... n.k miongoni mwa hukumu? Na je, sisi tunafuata sheria na kanuni zake kutoka kwenye Qur’ani au kutoka kwenye hadith? Utaniambia kwa nini kwa mfano mienendo ya swala au udhu haikutajwa ndani ya Qur’ani na kwamba si kila kitu kimetajwa ndani ya Qur’ani... n.k, lakini hii ni hukumu ya mkataa yaani ya msingi kama kanuni ya hesabu 1+1 ni sawa na 2. Yaani kila jambo lililopo ndani ya Qur’ani tunalihukumu na lisilokuwepo hatulifanyi kuwa kanuni ya msingi. Naam, tunaweza kufanya utafiti na ijtihad katika maelezo ya ndani (tafasil) na hadith inaweza kuchukuliwa katika maelezo hayo, lakini haiwezekani kuchukua msingi (asl) kutoka kwenye hadith na kuuacha asili (Qur'ani). Asante.
Jibu:
Wa Alaikum Salaam Warahmatullahi Wabarakatuh,
Kwanza: Hakika yale yaliyokuja katika swali lako kuwa: (kila jambo lililopo ndani ya Qur’ani tunalihukumu na lisilokuwepo hatulifanyi kuwa kanuni ya msingi), ni jambo geni kwa Uislamu na Waislamu. Muislamu anaamini kuwa Sunnah ya Mtume ni dalili ya kisheria sawa kabisa na Qur'ani Tukufu, na anaamini kuwa yale yaliyokuja katika Sunnah ni wahyi kutoka kwa Allah (swt) na ni wajibu kuyafuata bila ya kufanya utofauti kati yake na yale yaliyokuja ndani ya Qur'ani Tukufu... Na huu ndio msimamo wa Waislamu tangu zama za Maswahaba watukufu (ra) mpaka leo hii... Tumelifafanua suala hili katika kitabu cha Ash-Shakhsiyyah al-Islamiyyah (Shakhsia ya Kiislamu) katika mada za: "Sunnah ni dalili ya kisheria kama Qur'ani", "Kutoa dalili kwa Sunnah", na pia katika kitabu cha Ash-Shakhsiyyah al-Islamiyyah Juzuu ya Tatu katika mada ya "Dalili ya Pili: Sunnah". Rejea huko, kuna upembuzi wa kutosha akipenda Allah. Na nakunukulia yale yaliyokuja katika mada ya "Sunnah ni dalili ya kisheria kama Qur'ani" katika kitabu cha Ash-Shakhsiyyah al-Islamiyyah Juzuu ya Kwanza:
[Sunnah ni dalili ya kisheria kama Qur'ani, nayo ni wahyi kutoka kwa Allah Mtukufu. Na kutosheka na Qur'ani pekee na kuacha Sunnah ni ukafiri wa wazi, na hayo ni maoni ya wale waliojitenga na Uislamu. Ama kuhusu kuwa Sunnah ni wahyi kutoka kwa Allah Mtukufu, jambo hilo liko wazi ndani ya Qur'ani Tukufu. Allah Mtukufu amesema:
قُلْ إِنَّمَا أُنذِرُكُم بِالْوَحْيِ
"Sema: Hakika mimi nakuonyeni kwa wahyi pekee." (QS Al-Anbiya [21]: 45)
Na akasema:
إِن يُوحَى إِلَيَّ إِلَّا أَنَّمَا أَنَا نَذِيرٌ مُّبِينٌ
"Haifunuliwi kwangu isipokuwa kwamba mimi ni mwonyaji bayana." (QS Saad [38]: 70)
Na akasema:
إِنْ أَتَّبِعُ إِلَّا مَا يُوحَى إِلَيَّ
"Sifuati isipokuwa yale yanayofunuliwa kwangu." (QS Al-An'am [6]: 50)
Na akasema:
قُلْ إِنَّمَا أَتَّبِعُ مَا يِوحَى إِلَيَّ مِن رَّبِّي
"Sema: Hakika mimi nafuata yale yanayofunuliwa kwangu kutoka kwa Mola wangu." (QS Al-A'raf [7]: 203)
Na akasema:
وَمَا يَنطِقُ عَنِ الْهَوَى * إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَى
"Wala hazungumzi kwa matamanio. Hayo si chochote ila ni wahyi unaofunuliwa." (QS An-Najm [53]: 3-4)
Aya hizi ni qat'iyyat ath-thubut (zenye uthabiti wa yakini) na qat'iyyat ad-dalalah (zenye maana ya yakini) katika kudhibiti yale anayokuja nayo Mtume na anayoonya kwayo na anayoyatamka, kuwa yanatokana na wahyi na hayakubali tafsiri nyingine yoyote. Hivyo, Sunnah ni wahyi kama Qur'ani.
Ama kuhusu kuwa Sunnah ni wajibu kufuata kama Qur'ani Tukufu, hilo pia liko wazi ndani ya Qur'ani. Allah Mtukufu amesema:
وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا
"Na kile anachokupeni Mtume, kichukueni, na anachokukatazeni, jiepusheni nacho." (QS Al-Hashr [59]: 7)
Na akasema:
مَّنْ يُطِعِ الرَّسُولُ فَقَدْ أَطَاعَ اللّهَ
"Mwenye kumtii Mtume, basi hakika amemtii Allah." (QS An-Nisa [4]: 80)
Na akasema:
فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ
"Basi na waonye wale wanaokwenda kinyume na amri yake, isije ikawapata fitna au ikawapata adhabu iumizayo." (QS An-Nur [24]: 63)
Na akasema:
وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَمْراً أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ
"Haiwi kwa Muumini mwanamume wala Muumini mwanamke, Allah na Mtume Wake wanapokata shauri, wawe na hiyari katika shauri lao." (QS Al-Ahzab [33]: 36)
Na akasema:
فَلاَ وَرَبِّكَ لاَ يُؤْمِنُونَ حَتَّىَ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لاَ يَجِدُواْ فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجاً مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُواْ تَسْلِيماً
"La! Naapa kwa Mola wako, hawaamini mpaka wakufanye wewe kuwa mwamuzi katika yale wanayozozana, kisha wasione uzito katika nafsi zao kwa ulichokihukumu na wasalimu amri kwa unyenyekevu." (QS An-Nisa [4]: 65)
Na akasema:
أَطِيعُوا اللَّهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ
"Mtiini Allah na mtiini Mtume." (QS An-Nisa [4]: 59)
Na akasema:
قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللّهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللّهُ
"Sema: Ikiwa nanyi mnamfanyia mapenzi Allah, basi nifuateni mimi, Allah atawapenda." (QS Ali 'Imran [3]: 31)
Haya yote yako wazi kabisa katika kuwajibisha kumfuata Mtume katika yale anayokuja nayo, na katika kuzingatia utiifu kwake kuwa ni utiifu kwa Allah Mtukufu.
Hivyo, Qur'ani na hadith kwa upande wa kuwajibika kufuata yale yaliyokuja ndani yake ni dalili mbili za kisheria, na hadith ni kama Qur'ani katika maudhui haya. Na kwa sababu hiyo, haijuzu kusema kuwa tuna Kitabu cha Allah tunachokichukua, kwa sababu hiyo inaeleweka kuwa ni kuacha Sunnah. Bali ni lazima kuiunganisha Sunnah na Kitabu (Qur'ani), hivyo hadith inachukuliwa kama dalili ya kisheria kama inavyochukuliwa Qur'ani, na haijuzu kwa Muislamu kutoa kauli inayohisiwa kuwa anatosheka na Qur'ani pekee bila hadith. Na Mtume ﷺ ametahadharisha kuhusu hilo. Imepokelewa kuwa Mtume ﷺ amesema:
يُوشِكُ أَنْ يَقْعُدَ الرَّجُلُ مِنْكُمْ عَلَى أَرِيكَتِهِ يُحَدِّثُ بِحَدِيثِي، فَيَقُولُ: بَيْنِي وَبَيْنَكُمْ كِتَابُ اللَّهِ، فَمَا وَجَدْنَا فِيهِ حَلَالاً اسْتَحْلَلْنَاهُ، وَمَا وَجَدْنَا فِيهِ حَرَاماً حَرَّمْنَاهُ، وَإِنَّ مَا حَرَّمَ رَسُولُ اللَّهِ كَمَا حَرَّمَ اللَّهُ
"Anakaribia mtu mmoja wenu kuketi juu ya kochi lake akihadithiwa hadith yangu, kisha anasema: Baina yangu na ninyi ni Kitabu cha Allah, kile tulichokipata humo kuwa ni halali tunakifanya halali, na kile tulichokipata humo kuwa ni haramu tunakifanya haramu. Hakika kile alichokiharamisha Mtume wa Allah ni sawa na alichokiharamisha Allah." (Imepokelewa na Al-Hakim na Al-Bayhaqi).
Na akasema katika mapokezi kutoka kwa Jabir (marfuu'):
مَنْ بَلَغَهُ عَنِّي حَدِيثٌ فَكَذَّبَ بِهِ، فَقَدْ كَذَّبَ ثَلَاثَةً: اللَّهَ، وَرَسُولَهُ، وَالَّذِي حَدَّثَ بِهِ
"Mwenye kufikishiwa hadith kutoka kwangu kisha akaikanusha, basi amewakanusha watatu: Allah, Mtume Wake, na yule aliyeihadithia." (Majma' al-Zawaid kutoka kwa Jabir).
Na kutokana na hapa, lilikuwa ni kosa kusema kuwa tunaipima Qur'ani kwa hadith, na ikiwa haiendani nayo tunaiacha, kwa sababu hiyo inapelekea kuacha hadith ikiwa imekuja kuhusisha (mukhasis) Qur'ani au kuifunga (muqayyid), au kufafanua ujumla wake (mufassil li mujmalihi). Kwani inaweza kuonekana kuwa kile kilichokuja katika hadith hakiendani na Qur'ani, au hakipo ndani ya Qur'ani. Na hilo ni kama hadith zilizokuja kuunganisha matawi (furu') na asili (asl). Kwani yale yaliyokuja katika hadith miongoni mwa hukumu hayakuja ndani ya Qur'ani, hasa kwa kuwa hukumu nyingi zilizofafanuliwa hazikuja ndani ya Qur'ani bali zilikuja ndani ya hadith pekee. Kwa hivyo hadith haipimwi kwa Qur'ani, ili kikubalike kile kilichokuja humo na kukataliwa vinginevyo. Bali jambo lilivyo ni kwamba, ikija hadith inayopingana na yale yaliyokuja ndani ya Qur'ani yenye maana ya yakini (qat'iy al-ma'na), basi hadith hiyo hukataliwa kimasimulizi (dirayatan) yaani matini yake, kwa sababu maana yake inapingana na Qur'ani. Na hiyo ni kama ilivyopokelewa kutoka kwa Fatma bint Qays kuwa alisema:
طَلَّقَنِي زَوْجِي ثَلَاثاً عَلَى عهدِ رَسُولِ اللَّهِ ﷺ فَأَتَيْتُ النَّبِيَّ ﷺ فَلَمْ يَجْعَلْ لِي سُكْنَى، وَلَا نَفَقَةً
"Mume wangu alinitaliki talaka tatu katika zama za Mtume wa Allah ﷺ kisha nikamwendea Mtume ﷺ naye hakunifanyia makazi wala matumizi."
Basi hadith hii inakataliwa kwa sababu inapingana na Qur'ani, kwani inakinzana na kauli ya Allah Mtukufu:
أَسْكِنُوهُنَّ مِنْ حَيْثُ سَكَنتُم مِّن وُجْدِكُمْ
"Wawekeni (humo mnamokaa) pale mnamokaa kwa kadiri ya uwezo wenu." (QS At-Talaq [65]: 6)
Basi hadith inakataliwa wakati huo kwa sababu imepingana na Qur'ani ambayo ni qat'iyyat ath-thubut na qat'iyyat ad-dalalah. Ama ikiwa hadith haipingani na Qur'ani, kwa kuwa imejumuisha mambo ambayo hayakuja ndani ya Qur'ani au ziada ya yale yaliyomo ndani ya Qur'ani, basi hadith hiyo huchukuliwa na Qur'ani pia huchukuliwa. Na haisemwi kuwa tunatosheka na Qur'ani na yale yaliyokuja ndani ya Qur'ani, kwa sababu Allah ameamrisha vyote viwili pamoja na itikadi ni wajibu katika vyote viwili pamoja.] Mwisho wa nukuu kutoka kitabu cha Ash-Shakhsiyyah al-Islamiyyah Juzuu ya Kwanza.
Na ni wazi kutokana na yaliyotajwa hapo juu kuwa hukumu ya kisheria huchukuliwa kutoka kwenye Sunnah tukufu kama inavyochukuliwa kutoka kwenye Qur'ani Tukufu bila ya tofauti yoyote. Na si lazima hukumu iwe imetajwa ndani ya Qur'ani Tukufu ndipo iwe wajibu kuichukua, bali hukumu ya kisheria huchukuliwa hata kama Sunnah ya Mtume imehusika kuitaja... Pamoja na hayo, maudhui ya rajm (kupigwa mawe) kwa mzinifu mke au mume aliyekatika ndoa (muhsan) ni katika mlango wa ubainifu wa Sunnah kwa Qur'ani kwa sababu Sunnah inabainisha Qur'ani kwa kuhusisha ujumla wake (takhsis al-'amm), na rajm kwa mzinifu muhsan ni kuhusisha ujumla wa aya inayowajibisha kupigwa mijeledi mzinifu kama ilivyofafanuliwa hapa chini... Hivyo haisemwi kuwa Sunnah imejitegemea katika hukumu ya rajm kwa mzinifu kwa sababu hukumu hiyo ni sehemu ya adhabu ya mzinifu iliyobainishwa ndani ya Qur'ani. Yaani asili ya suala la adhabu ya mzinifu imebainishwa ndani ya Qur'ani, kisha ikaja Sunnah ikafafanua Qur'ani kwa kuhusisha ujumla wa aya husika, ikamtoa nje mzinifu muhsan na kufanya adhabu yake kuwa ni rajm mpaka kufa... Na kuhusisha ujumla wa Kitabu (Qur'ani) kwa Sunnah ni kwingi na hakuishii tu kwenye maudhui ya rajm kwa mzinifu muhsan...
Pili: Tulishawahi kujibu mnamo tarehe 12 Muharram 1441 H - 11/09/2019 M kuhusu maudhui ya rajm kwa mzinifu muhsan, na nakunukulia yale yaliyokuja katika jibu lililoashiriwa kwa sababu yana jibu la swali lako:
[Hakika wewe unauliza kuhusu adhabu ya mzinifu muhsan (aliyeoa/olewa), je, ni ya yakini (qat'iy) katika fikihi ya Kiislamu? Na je, ni miongoni mwa hudud (adhabu zilizowekwa na Allah) au si miongoni mwa hudud bali ni katika ta'zir (adhabu za utashi wa hakimu) kama wanavyosema baadhi ya wanachuoni katika zama hizi?
Jibu la swali lako ni kama ifuatavyo:
1- Hakika adhabu ya mzinifu muhsan kwa rajm mpaka kufa imeingia katika mlango wa hukumu za kisheria na si katika mlango wa itikadi (aqaid). Hivyo ni kama hukumu nyingine za kisheria, haishurutishwi dalili yake iwe ya yakini (qat'iy) ili ichukuliwe, bali inatosha katika hilo wingi wa dhana ya ukweli (ghalabat az-zann) kama inavyofahamika katika Usul al-Fiqh... Kwa hivyo, hakuna athari ya kuwa dalili ya adhabu hii ni ya yakini au si ya yakini katika kuichukua, bali jambo muhimu ni kudhibitiwa kwa dalili kutoka katika sheria juu yake. Na zimekuja dalili nyingi sahihi katika sheria zinazobainisha bila kuacha chembe ya shaka kuwa adhabu ya mzinifu muhsan ni rajm mpaka kufa kama ilivyotajwa hapa chini.
2- Inazingatiwa kwa baadhi ya wanachuoni katika zama hizi kwamba hawaendi mwendo sahihi katika kuchukua hukumu za kisheria kutoka kwenye dalili zake. Hiyo ni kwa sababu wanapopambana kutafuta hukumu ya kisheria, wanajitahidi kuendana na zama na kufikia maoni yanayoafikiana na yale yaliyotawala duniani miongoni mwa hukumu na maoni yaliyowekwa na ustaarabu wa Kimagharibi kwa watu kwa jina la sheria za kimataifa, mikataba ya haki za binadamu na mengineyo... Na jambo hili halisihi, kwa sababu kinachotakiwa ni hukumu ya Allah na si hukumu yoyote ile, wala hukumu inayoafikiana na yale yanayotawala duniani... Wajibu ni kuchukua hukumu ya kisheria kama ilivyo kutoka kwenye dalili zake na kuifanya kuwa ndiyo inayotekelezwa na kufanyiwa kazi, na kufanya ulinganifu na propaganda kwayo duniani kote. Kwani hiyo ndiyo hukumu inayofaa kwa wanadamu wote kwa sababu inatoka kwa Muumba wa wanadamu Mwenye kujua hali zao, Ametakasika:
أَلَا يَعْلَمُ مَنْ خَلَقَ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ
"Je! Asijue aliye umba, naye ndiye Mjuzi wa yaliyofichikana, Mwenye habari za kila kitu?" (QS Al-Mulk [67]: 14)
أَلَا لَهُ الْخَلْقُ وَالْأَمْرُ تَبَارَكَ اللَّهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ
"Fahamuni! Kuumba na amri ni Vyake. Ametukuka Allah Mola Mlezi wa walimwengu wote." (QS Al-A'raf [7]: 54)
Na kwa ajili hiyo, haifai kugeukia kauli za wale wanaong'ang'ania katika istinbat zao kuendana na zama na kuafikiana na ustaarabu wa Kimagharibi, wawe wanafanya hivyo chini ya shinikizo la uhalisia au kwa kuwaridhisha makafiri wa Kimagharibi...
3- Hakika adhabu ya zinaa kwa muhsan ambayo ni rajm mpaka kufa, na kwa asiyekuwa muhsan ambayo ni kupigwa mijeledi mia, ni adhabu iliyoingia ndani ya Uislamu katika mlango wa hudud. Na tumebainisha hukumu za adhabu ya zinaa katika kitabu cha Nidham al-Uqubat (Mfumo wa Adhabu) kwa ufafanuzi wa kina na wa kutosha. Na nakunukulia kutoka kitabu cha Nidham al-Uqubat baadhi ya yaliyokuja katika mlango wa "Had ya Zinaa":
[Wanasema baadhi kuwa had ya mzinifu mwanamke na mwanamume ni mijeledi mia kwa muhsan na asiyekuwa muhsan sawasawa, na hakuna tofauti kati yao, kwa kauli ya Allah Mtukufu:
الزَّانِيَةُ وَالزَّانِي فَاجْلِدُوا كُلَّ وَاحِدٍ مِّنْهُمَا مِئَةَ جَلْدَةٍ وَلَا تَأْخُذْكُم بِهِمَا رَأْفَةٌ فِي دِينِ اللَّهِ
"Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mpigeni kila mmoja katika wao mijeledi mia, wala isiwashikeni huruma kwa ajili yao katika dini ya Allah." (QS An-Nur [24]: 2)
Wakasema: Haijuzu kuacha Kitabu cha Allah kwa njia ya yakini kwa ajili ya habari za mmoja mmoja (akhbar ahad) ambazo zinaweza kuwa na uongo, na kwa sababu hilo linapelekea kufuta (naskh) Kitabu kwa Sunnah na hilo halijuzu!
Na wanasema wanachuoni wote miongoni mwa Maswahaba, Tabiina, na waliokuja baada yao miongoni mwa wanachuoni wa miji katika karne zote kwamba asiyekuwa muhsan hupigwa mijeledi mia, na muhsan hupigwa mawe mpaka kufa kwa sababu Mtume ﷺ: "alimpiga mawe Ma'iz", na kwa yaliyopokelewa kutoka kwa Jabir bin Abdullah:
أَنَّ رَجُلاً زَنَى بِامْرَأَةٍ فَأَمَرَ بِهِ النَّبِيُّ ﷺ فَجُلِدَ الْحَدَّ، ثُمَّ أُخْبِرَ أَنَّهُ مُحْصَنٌ فَأَمَرَ بِهِ فَرُجِمَ
"Kwamba mtu mmoja alizini na mwanamke, basi Mtume ﷺ akaamuru apigwe mijeledi ya had, kisha akafahamishwa kuwa yeye ni muhsan, akaamuru apigwe mawe (akauawa)."
Na mwenye kutazama dalili anaona kuwa kauli ya Allah Mtukufu: "Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mpigeni kila mmoja katika wao mijeledi mia" ni ya jumla, kwani neno Az-Zaniya (Mzinifu mwanamke) na neno Az-Zani (Mzinifu mwanamume) ni miongoni mwa maneno ya ujumla, hivyo inajumuisha muhsan na asiyekuwa muhsan. Na ilipokuja hadith nayo ni kauli ya Mtume ﷺ:
وَاغْدُ يَا أُنَيْسُ إِلَى امْرَأَةِ هَذَا فَإِنْ اعْتَرَفَتْ فَارْجُمْهَا
"Na nenda asubuhi ewe Unais kwa mke wa huyu, akiri basi mpige mawe."
Na ikathibiti kuwa Mtume wa Allah ﷺ alimpiga mawe Ma'iz baada ya kuuliza kuhusu ndoa yake (ihsan), na kumpiga mawe mwanamke wa Ghamidiyyah na mengineyo miongoni mwa hadith sahihi, basi hadith inakuwa ni yenye kuhusisha (mukhasis) aya hiyo. Hivyo hadith hizi zimehusisha ujumla huu uliomo ndani ya aya kwa asiyekuwa muhsan, na kumtoa nje ya ujumla huo yule muhsan. Hivyo hadith zimehusisha ujumla huu, na hazikufuta (kunaskh) Qur'ani. Na kuhusisha Qur'ani kwa Sunnah kunajuzu, na kumetokea katika aya nyingi ambazo zimekuja kwa ujumla kisha hadith ikaja na kuzihusisha.
Na hukumu ya kisheria ambayo dalili za kisheria zinaonyesha, yaani Kitabu na Sunnah, ni kwamba adhabu ya zinaa ni mijeledi mia kwa asiyekuwa muhsan kwa kufanyia kazi Kitabu cha Allah, na kufukuzwa mji mwaka mmoja kwa kufanyia kazi Sunnah ya Mtume wa Allah. Isipokuwa kufukuzwa mji ni jambo linalojuzu na si wajibu, na hilo limeachiwa kwa Imam; akitaka anampiga mijeledi na kumfukuza mji mwaka mmoja, na akitaka anampiga mijeledi na asimfukuze. Lakini haijuzu kumfukuza bila kumpiga mijeledi, kwa sababu adhabu yake ni mijeledi. Ama adhabu ya muhsan ni rajm mpaka kufa, kwa kufanyia kazi Sunnah ya Mtume wa Allah ﷺ iliyokuja kuhusisha Kitabu cha Allah. Na inajuzu kwa muhsan kukusanyiwa mijeledi na rajm; apigwe mijeledi kwanza kisha apigwe mawe. Na inajuzu kumpa adhabu ya rajm pekee asipigwe mijeledi, lakini haijuzu kumpa adhabu ya mijeledi pekee kwa sababu adhabu yake ya lazima ni rajm.
..........
Ama dalili ya adhabu ya muhsan ni hadith nyingi. Kutoka kwa Abu Hurairah na Zaid bin Khalid kwamba walisema kuwa mtu mmoja katika mabedui alimjia Mtume wa Allah ﷺ akasema:
يَا رَسُولَ اللَّهِ أَنْشُدُكَ اللَّهَ إِلَّا قَضَيْتَ لِي بِكِتَابِ اللَّهِ، وَقَالَ الْخَصْمُ الْآخَرُ وَهُوَ أَفْقَهُ مِنْهُ: نَعَمْ، فَاقْضِ بَيْنَنَا بِكِتَابِ اللَّهِ، وَائْذَنْ لِي، فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ ﷺ: قُلْ، قَالَ: إِنَّ ابْنِي كَانَ عَسِيفاً عَلَى هَذَا فَزَنَى بِامْرَأَتِهِ، وَإِنِّي أُخْبِرْتُ أَنَّ عَلَى ابْنِي الرَّجْمَ فَافْتَدَيْتُ مِنْهُ بِمِائَةِ شَاةٍ وَوَلِيدَةٍ، فَسَأَلْتُ أَهْلَ الْعِلْمِ فَأَخْبَرُونِي أَنَّمَا عَلَى ابْنِي جَلْدُ مِائَةٍ وَتَغْرِيبُ عَامٍ، وَأَنَّ عَلَى امْرَأَةِ هَذَا الرَّجْمَ. فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ ﷺ: وَالَّذِي نَفْسِي بِيَدِهِ لَأَقْضِيَنَّ بَيْنَكُمَا بِكِتَابِ اللَّهِ، الْوَلِيدَةُ وَالْغَنَمُ رَدٌّ، وَعَلَى ابْنِكَ جَلْدُ مِائَةٍ، وَتَغْرِيبُ عَامٍ، وَاغْدُ يَا أُنَيْسُ - لِرَجُلٍ مِنْ أَسْلَمَ - إِلَى امْرَأَةِ هَذَا فَإِنْ اعْتَرَفَتْ فَارْجُمْهَا، قَالَ: فَغَدَا عَلَيْهَا فَاعْتَرَفَتْ فَأَمَرَ بِهَا رَسُولُ اللَّهِ ﷺ فَرُجِمَتْ
"Ewe Mtume wa Allah, nakuomba kwa jina la Allah unihukumu kwa Kitabu cha Allah. Na mshitakiwa mwingine akasema - naye alikuwa na uelewa zaidi: Ndiyo, tuhukumu baina yetu kwa Kitabu cha Allah na niruhusu niseme. Mtume wa Allah ﷺ akasema: Sema. Akasema: Hakika mwanangu alikuwa mfanyakazi (kibarua) kwa huyu akazini na mke wake, nami nikahabariwa kuwa mwanangu anapaswa kupigwa mawe, nikajikomboa kwake kwa kondoo mia na kijakazi mmoja. Kisha nikawauliza watu wa elimu wakanihabari kuwa mwanangu anapaswa kupigwa mijeledi mia na kufukuzwa mji mwaka mmoja, na mke wa huyu anapaswa kupigwa mawe. Basi Mtume wa Allah ﷺ akasema: Naapa kwa Ambaye nafsi yangu iko mikononi Mwake, hakika nitahukumu baina yenu kwa Kitabu cha Allah. Yule kijakazi na kondoo warudishwe, na mwanao apigwe mijeledi mia na kufukuzwa mji mwaka mmoja. Na nenda asubuhi ewe Unais - kwa mtu kutoka kabila la Aslam - kwa mke wa huyu, akiri basi mpige mawe. Akasema: Akamwendea asubuhi akakiri, Mtume wa Allah ﷺ akaamuru apigwe mawe naye akapigwa mawe."
Na al-'asif ni kibarua. Basi Mtume akaamuru kupigwa mawe kwa muhsan na hakumpiga mijeledi. Na kutoka kwa Ash-Sha'bi:
أَنَّ عَلِيّاً رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ حِينَ رَجَمَ الْمَرْأَةَ ضَرَبَهَا يَوْمَ الْخَمِيسِ، وَرَجَمَهَا يَوْمَ الْجُمُعَةِ، وَقَالَ: جَلَدْتُهَا بِكِتَابِ اللَّهِ، وَرَجَمْتُهَا بِسُنَّةِ رَسُولِ اللَّهِ ﷺ
"Kwamba Ali (ra) alipompiga mawe mwanamke, alimpiga mijeledi siku ya Alhamisi, na kumpiga mawe siku ya Ijumaa, akasema: Nimempiga mijeledi kwa Kitabu cha Allah, na nimempiga mawe kwa Sunnah ya Mtume wa Allah ﷺ."
Na kutoka kwa Ubada bin Swamit amesema: Mtume wa Allah ﷺ amesema:
خُذُوا عَنِّي، خُذُوا عَنِّي، قَدْ جَعَلَ اللَّهُ لَهُنَّ سَبِيلاً الْبِكْرُ بِالْبِكْرِ جَلْدُ مِائَةٍ وَنَفْيُ سَنَةٍ، وَالثَّيِّبُ بِالثَّيِّبِ جَلْدُ مِائَةٍ وَالرَّجْمُ
"Chukueni kutoka kwangu, chukueni kutoka kwangu, hakika Allah ameshawafanyia njia; bikira kwa bikira (mzinifu asiyeoa/olewa) ni mijeledi mia na kufukuzwa mji mwaka mmoja, na mwanamke aliyewahi kuolewa kwa mwanamume aliyewahi kuoa (mzinifu muhsan) ni mijeledi mia na rajm."
Basi Mtume anasema kuwa adhabu ya muhsan ni mijeledi na rajm, na Ali anampiga mijeledi muhsan na kumpiga mawe. Na kutoka kwa Jabir bin Samura kwamba Mtume wa Allah ﷺ alimpiga mawe Ma'iz bin Malik na hakutaja mijeledi. Na katika Bukhari kutoka kwa Suleiman bin Buraida kwamba Mtume ﷺ alimpiga mawe yule mwanamke wa Ghamidiyyah na hakutaja mijeledi. Na katika Muslim kwamba Mtume ﷺ aliamrisha mwanamke kutoka kabila la Juhayna, nguo zake zikafungwa kisha akaamuru apigwe mawe na hakutaja mijeledi. Basi hiyo ikaonyesha kuwa Mtume alimpiga mawe muhsan na hakumpiga mijeledi, na kwamba alisema: "Mwanamke aliyewahi kuolewa kwa mwanamume aliyewahi kuoa ni mijeledi mia na rajm." Hiyo ikaonyesha kuwa rajm ni wajibu, ama mijeledi inajuzu na inaachiwa rai ya Khalifa. Na ikafanywa miongoni mwa had ya muhsan kuwa ni mijeledi pamoja na rajm ili kukusanya baina ya hadith. Na haisemwi kuwa hadith ya Samura katika kuto-mpiga mijeledi Ma'iz bali kutosheka na rajm yake ni yenye kufuta (nasikh) hadith ya Ubada bin Swamit inayosema: "Mwanamke aliyewahi kuolewa kwa mwanamume aliyewahi kuoa ni mijeledi mia na rajm". Haisemwi hivyo kwa sababu haikuthibiti kile kinachoonyesha kuwa hadith ya Ma'iz imekuja baada ya hadith ya Ubada. Na kwa kutokuthibiti kwa kuchelewa kwake, basi kuacha kutaja mijeledi hakuilazimishi kuifuta, wala kufuta hukumu yake. Hivyo kutokuthibiti kwa kipi kilichotangulia na kipi kilichochelewa miongoni mwa hadith hizi mbili kunakanusha kufutika (naskh), na hakuna chenye kutoa upendeleo kwa moja juu ya nyingine. Na yale yaliyokuja katika hadith miongoni mwa ziada juu ya rajm yanazingatiwa kuwa ni jambo linalojuzu na si wajibu, kwani wajibu ni rajm, na yaliyozidi juu ya hilo Imam ana hiyari kwayo ili kukusanya baina ya hadith...] Mwisho wa nukuu kutoka kitabu cha Nidham al-Uqubat.
Na hitimisho: Kwamba adhabu ya mzinifu muhsan ni rajm mpaka kufa na zimeonyesha hilo dalili sahihi thabiti kutoka katika Sunnah ya Mtume wa Allah ﷺ katika Sahih mbili (Bukhari na Muslim) na katika vitabu vingine vya hadith, nayo ni adhabu iliyoingia katika hudud na si katika mlango wa ta'zir.] Mwisho wa nukuu kutoka jibu la swali lililopita.
Na katika kumalizia, hakika wewe umejihukumu mwenyewe kwa nafsi yako kwani unasema: (Utaniambia kwa nini kwa mfano mienendo ya swala au udhu haikutajwa ndani ya Qur’ani na kwamba si kila kitu kimetajwa ndani ya Qur’ani... n.k, lakini hii ni hukumu ya mkataa yaani ya msingi kama kanuni ya hesabu 1+1 ni sawa na 2. Yaani kila jambo lililopo ndani ya Qur’ani tunalihukumu na lisilokuwepo hatulifanyi kuwa kanuni ya msingi. Naam tunaweza kufanya utafiti na ijtihad katika maelezo ya ndani na hadith inaweza kuchukuliwa katika maelezo hayo lakini haiwezekani kuchukua msingi kutoka kwenye hadith na kuuacha asili asante), basi wewe hapa unaruhusu tuchukue kutoka katika Sunnah kile kinachobainisha namna ya kutekeleza swala na unasema hili linajuzu kwa sababu ni thabiti kama 1+1=2! Wakati halina tofauti na kutoa dalili kwa Sunnah kwa upande wa mzinifu muhsan... Kwani katika hali ya swala, aya inasema: "Na simamisheni swala", basi huu ni ujumla (mujmal), na hadith zilizobainisha namna ya swala hata kama mujtahidina wametofautiana katika namna ya kurukuu, kusujudu na kusoma... basi hadith hizi ni ubainifu wa ujumla... na kadhalika aya "Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume"... basi ni ya jumla kwa sababu neno Az-Zaniya na Az-Zani ni maneno ya ujumla. Na hadith zinazohusiana na muhsan zimehusisha ujumla huu uliokuja ndani yake mijeledi, zimeuhusisha kwa mzinifu asiyekuwa muhsan. Hivyo suala hapa liko katika mlango wa kuhusisha ujumla (takhsis al-'amm)... Na ikiwa umesoma Usul (al-Fiqh) basi bila shaka utakuta kuwa kubainisha ujumla (bayan al-mujmal), kuhusisha ujumla (takhsis al-'amm), kufunga lile ambalo halijafungwa (taqyid al-mutlaq)... n.k vyote hivyo ni katika sehemu za Kitabu na Sunnah ambazo ni wajibu kuzitolea dalili kwa mujibu wa uhalisia wake wa kisheria.
Na kwa mujibu huo, kutofautisha kati ya kubainisha ujumla katika hali ya swala na kuhusisha ujumla katika hali ya zinaa ni utofautishaji ambao hausihi wala haujuzu, isipokuwa tu ikiwa huna elimu kamili ya Usul al-Fiqh. Na mimi namuomba Allah Mtukufu akuongoze kwenye jambo lililo sahihi zaidi na ujitahidi katika kufahamu Usul al-Fiqh ili swali liwe katika uwanja wake na si katika muktadha mwingine.
Natumai kuwa suala hili limeshafafanuka sasa.
Ndugu yenu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah
02 Jumada al-Akhira 1442 H Sawa na 15/01/2021 M
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Facebook wa Ameer (Mungu amuhifadhi) Kiungo cha jibu kutoka kwenye tovuti ya Ameer (Mungu amuhifadhi)