Jibu la Swali
Swali:
Tovuti ya Al-Arabiya mnamo tarehe 27/02/2023 iliripoti kuwa (Kremlin: Tunakaribisha mpango wa amani wa China lakini suluhu bado iko mbali). Vilevile, tovuti ya kituo cha Al-Youm mnamo 27/02/2023 iliripoti kuwa (Kremlin ilisema kuwa Urusi inatazama kwa umakini mpango wa amani wa China nchini Ukraine, ikibainisha kuwa maelezo ya pendekezo hilo yanahitaji uchambuzi na mahesabu ya kina kulingana na maelezo yake). Rais Putin mnamo 21/02/2023 alikuwa ametangaza ("kwamba Urusi imesitisha ushiriki wake katika mkataba wa New START uliotiwa saini na Marekani"... Anadolu, 21/02/2023). Matamko haya yalikuja baada ya ziara ya Biden huko Kyiv mnamo 20/02/2023 na mkutano wake na Rais wa Ukraine Zelensky ambapo Biden alisema (kwamba Ukraine itapokea kifurushi kipya cha msaada wa kijeshi chenye thamani ya dola milioni 500 kitakachotangazwa Jumanne... Sky News Arabia, 20/02/2023). Matamko haya yalitanguliwa na tangazo la Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi, wakati wa Mkutano wa Usalama wa Munich kwamba China ina mpango wa amani nchini Ukraine, akisema ("Vita hivi haviwezi kuendelea kuwaka"... CNN Arabic, 18/02/2023).
Swali ni: Je, China ina uwezo wa kusitisha vita nchini Ukraine? Na kwa nini China inatoa mpango huu baada ya kupita mwaka mmoja tangu kuanza kwa vita? Kisha, kwa nini Urusi inakaribisha mpango huo kisha inasema suluhu iko mbali? Na una nafasi gani ya kufanikiwa?
Jibu:
Ili kubainisha jibu la maswali yaliyo hapo juu, tunatathmini mambo yafuatayo:
Kwanza: Mataifa yenye ushawishi kuhusiana na vita vya Urusi na Ukraine:
1- Marekani: Marekani, chini ya uongozi wa Rais Biden, imefanikiwa kuondoa mashaka ya Ulaya kuhusu uongozi wa Marekani kwa ulimwengu wa Magharibi. Serikali ya Biden iliunganisha juhudi za Magharibi kutoa misaada ya kijeshi na isiyo ya kijeshi kwa Ukraine ili iweze kustahimili mashambulizi ya Urusi. Iliwajumuisha Magharibi katika kuweka vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Urusi, na kufanikiwa kukata mishipa ya nishati ya Urusi kuelekea Ulaya. Aidha, iliyashirikisha mataifa yaliyo mbali na Ulaya katika vikwazo hivyo, kama vile Japan, Korea Kusini, na Australia, na kuuhuisha muungano wa NATO baada ya kuwa katika mashaka wakati wa serikali ya Trump. Serikali ya Biden imeendelea kuongeza silaha kwa Ukraine na kutangaza kuwa lengo lake ni kuishinda Urusi nchini Ukraine.
2- Mataifa makubwa ya Ulaya: Wakati msimamo wa Uingereza hauwezi tena kutofautishwa na msimamo wa Marekani dhidi ya Urusi, Ujerumani na Ufaransa nazo zimefuata mkondo huo. Kwa kila mshipa wa nishati wa Urusi uliokatwa kuelekea Ulaya, Ujerumani ilizidisha msimamo wake dhidi ya Urusi, kiasi kwamba Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Baerbock, alisema katika jitihada za kuunganisha misimamo ya Ulaya kuhusu kuipa Ukraine vifaru: (Tunapigana vita dhidi ya Urusi na si dhidi yetu wenyewe... Al-Shorouk, 24/01/2023), jambo ambalo lilimfanya Rais wa zamani wa Urusi, Medvedev, kumwita "mjinga mwenye faida" (Anadolu, 29/01/2023), akimaanisha kuwa anakiri Ulaya ni upande katika mzozo wa Ukraine. Ama Ufaransa, ambayo ilikabiliwa na ukosoaji kutoka kwa washirika wake kutokana na mawasiliano ya rais wake na Rais wa Urusi, hatimaye imeanza kupanda treni ileile ambayo mataifa mengine ya Ulaya yalipanda nyuma ya mabehewa ya Marekani dhidi ya Urusi. Rais wake Macron, alipokuwa akirejea kutoka Mkutano wa Munich, alisema kulingana na Sky News Arabia, 19/02/2023: (Nataka Urusi ishindwe nchini Ukraine na nataka Ukraine iweze kulinda msimamo wake).
3- Urusi: Baada ya taswira ya nguvu iliyokuwa ikilikunika jeshi la Urusi kimataifa, vita nchini Ukraine vimefichua udhaifu mkubwa ulioshusha hadhi ya jeshi hilo, ambalo lilishindwa maeneo ya karibu na Kyiv, Kharkiv, na hatimaye Kherson. Baada ya jeshi la Urusi kuwa nguzo ya ukuu wa Urusi, sasa limebakiza tu nguvu za kinyuklia kama msingi wa kimataifa wa ukuu wake. Ama uchumi wa Urusi, asili yake ni dhaifu. Kisiasa, Marekani na Ulaya zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuiwekea Urusi kutengwa kimataifa, mbali na kukosekana kwa makubaliano ya ndani nchini Urusi kuhusu vita hivyo; kwani wakati wa kampeni ya kuandikisha askari kwa nguvu, Warusi wengi walitorokea nje ya nchi!
Pili: Athari za mabadiliko haya yote ya kimataifa kwa China:
1- China inatambua kuwa yenyewe iko kileleni mwa orodha ya vipaumbele vya Marekani, yaani kabla ya Urusi. Marekani inaichangamoto China kuhusu Taiwan, na kuiaibisha kwa hilo. Inaikabili kupitia mazoezi ya kijeshi yasiyo na kifani na Korea Kusini, na kuikabili ikiwa itajaribu kuifidia Urusi kwa hasara zake kutokana na vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Moscow, au ikiwa itatoa msaada wa kijeshi wenye kuua kwa Urusi. Pia inaikabili kwa kuuzingira uchumi wake kwa siri kama ilivyo katika vita vya kiuchumi vinavyoendeshwa na Marekani dhidi ya kampuni ya China ya Huawei na makampuni mengine ya teknolojia. Hata hadharani Marekani ilikata usambazaji wa chips za kielektroniki kwa kisingizio cha matumizi yake ya kijeshi na kwamba China inatishia usalama wa taifa wa Marekani. China inaona Marekani ikiipa Japan silaha na kuifanya kuwa kero ubavuni mwake, na pengine Marekani ikaiendeleza Japan kuwa kero katika moyo wa China. Vilevile, kuna miungano mingine ya kijeshi ambayo Marekani inaianzisha barani Asia kama vile AUKUS na QUAD. Haya yote yanaweka changamoto kubwa kwa China na jeshi lake.
2- Ama mataifa ya Ulaya ambayo ni washirika wakubwa wa kiuchumi wa China kama ilivyo kwa Marekani, yenyewe yameitikia matakwa ya Washington kwa uratibu wa pamoja. Uratibu huu ulihuishwa baada ya Urusi kuanzisha vita nchini Ukraine na kujitokeza kwa hitaji la dharura la Ulaya la mwavuli wa usalama wa Marekani kulinda bara hilo dhidi ya vitisho vya Urusi. China imeshuhudia kuwa uongozi wa Marekani kwa mataifa ya Ulaya, uliorejeshewa uhai kutokana na vita vya Urusi nchini Ukraine, umeanza kuyavuta mataifa hayo kufuata misimamo ya Marekani dhidi ya China. Imeibuka istilahi ya mataifa yenye "fikra zinazofanana" ikirejelea mataifa ya kibeberu na wafuasi wao "waliopumbazwa na Magharibi" mashariki mwa Asia. Hata mazungumzo kuhusu nafasi ya muungano wa NATO mashariki mwa Asia yameanza kuenea, na hili ni tishio hatari kwa China kwamba Marekani ina uwezo wa kuyavuta mataifa mengi dhidi ya Beijing.
3- Ama kuhusu Urusi, udhaifu wake unapelekea kuwa mshirika mdogo wa China, hasa wakati uwanja wa kimataifa unavyozidi kuibinya kidogo kidogo. Ulaya imeachana na mafuta na gesi yake, na kumesalia kiasi kidogo tu baada ya Urusi kuwa mshika hatamu wa nishati barani Ulaya. Wakati Ulaya na Marekani zikifunga milango yao kwa Urusi, zinaiandama kwenye milango ya mataifa mengine zikiyatafuta mataifa hayo yafuate ukomo wa bei ya mafuta uliowekwa dhidi ya Urusi. Haya yote yanaifanya Urusi kuitazama China kama mlango pekee unaoweza kutumika kupitishia vyanzo vyake vya nishati na malighafi, jambo ambalo Magharibi wanaliita "kuomba omba kwa biashara kwa Urusi mbele ya China." Hali hii inaleta usumbufu kwa China mbele ya Marekani na Ulaya ambazo ndizo soko muhimu zaidi kwa biashara yake.
4- Ama China yenyewe, licha ya kuendelea kwa utata wa misimamo yake iliyotangazwa kuhusu vita vya Ukraine, haina budi kuona kuwa matokeo ya vita hivyo hayafurahishi nafsi yake. China ilitia saini hati ya "muungano usio na mipaka" na Urusi muda mfupi kabla ya kuanza kwa vita nchini Ukraine. Wakati Marekani na mataifa ya Ulaya yalipoitaka China kuchukua msimamo dhidi ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, misimamo ya China ilikuwa ya utata. Kwa upande mmoja, haikutangaza kuunga mkono vita vya Urusi wala kutoa msaada kwa mshirika wake Urusi, na ilitosheka tu kwa kuilaumu Marekani kuwa inahusika na kuzuka kwa vita hivyo kwa sababu haikukubali kuipa Urusi dhamana za usalama. Ilikuwa ni kana kwamba China inasubiri Urusi iweke hali mpya ya mambo nchini Ukraine, na usalama utengamae ndani ya Ukraine ili kuyalazimisha mataifa ya Magharibi kutambua hadhi mpya ya kimataifa ya Urusi, jambo ambalo lingeweza kuchochea hisia za Wachina kuwa linaashiria hadhi bora ya kimataifa kwa China, hasa huko Taiwan. Hata hivyo, kutokana na kujitokeza kwa udhaifu wa jeshi la Urusi na kushindwa kulikopata kwenye medani za vita nchini Ukraine, misimamo ya China imekumbwa na hali ya kulegalega kana kwamba inajiondoa kwenye muungano wake na Urusi.
5- Misimamo hii yote ya Magharibi ambayo inanukia uadui dhidi ya China haikuifanya China kuchukua misimamo kama hiyo dhidi ya Marekani na mataifa ya Ulaya, wala China haikuonyesha kuunga mkono Urusi. Hiyo ni kwa sababu ukuaji wa China na hadhi yake mpya yote yanategemea biashara yake ya nje, ambapo masoko ya Marekani na mataifa ya Ulaya yanawakilisha mshipa mkuu wa ukuu wa China. Hili ni tofauti na Urusi ambayo urithi wake wa kijeshi kutoka kwa Umoja wa Kisovieti, na si uchumi wala biashara ya kimataifa, ndio msingi wa hadhi yake ya kimataifa. Lakini China, kwa upande mwingine, imeendelea kufanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi na Urusi katika bahari kuu barani Asia na nje ya Asia. Labda ilitaka kuwa katikati ili isimpoteze Urusi ambayo inaihitaji ikiwa jambo litatokea kati yake na Marekani, na wakati huo huo haitaki kuyapoteza mataifa ya Magharibi ambayo biashara nayo ndiyo mshipa wa uchumi wake.
Tatu: Hivyo basi, misimamo hii imeifanya China kufikiria kuwa kama mpatanishi anayebeba mpango wa kutatua mgogoro kati ya pande mbili hata kama uhusiano wa China na pande hizo mbili hauko sawa. Maana ya haya yote ni kwamba China inaona mawingu mengi meusi yakitanda katika anga yake baada ya Urusi kuanzisha vita dhidi ya Ukraine. Mawingu haya yote yanaunda sehemu ya kwanza, au upande wa Kichina wa mpango wa amani wa China nchini Ukraine. Lakini upande huu usingeweza kuzaa mpango wowote makini isipokuwa kwa kuungana na upande wa pili, yaani upande wa Urusi. Kwa kuchunguza upande huu tunakuta:
1- Kwamba Urusi, ingawa imetangaza kampeni na kuandikisha takriban askari wapya nusu milioni, na pia ingawa imerejea kwenye mashambulizi kama ilivyo sasa karibu na mji wa Bakhmut huko Donbas, imeanza kutambua ugumu wa kushinda vita hivyo. Hiyo ni kwa sababu haipigani tu na jeshi la Ukraine, bali kulingana na maelezo yake "inapambana na uwezo wa muungano wa NATO" ambao unaipatia Ukraine msaada wa kijeshi wenye kuua kwa njia ya wazi na kwa lengo la wazi la kuishinda Urusi nchini Ukraine. Inavyoonekana Urusi imetambua kuwa inakabiliana na matakwa thabiti ya Marekani ya kuishinda nchini Ukraine, na hata kimataifa; kwani Finland na Sweden ziko karibu kuwa wanachama wapya wa muungano wa NATO, na hizi ndizo nchi za karibu zaidi kijiografia na Urusi. Na Ujerumani, adui mkubwa wa Urusi katika historia, imeanza kujiimarisha kijeshi kwa kasi. Na Mashariki, jeshi la Japan linaweza kuwa tishio kubwa kwa Urusi hivi karibuni, hasa kwa kuwa Japan inadai visiwa vya Kuril vilivyokaliwa na Urusi wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Maendeleo haya yote ya Ukraine na ya kimataifa yanaweka mizigo mikubwa ya usalama kwa Urusi na kufichua zaidi udhaifu wake, hasa ikiwa na vikwazo vya kiuchumi visivyo na kifani.
2- Ishara hizi za udhaifu wa Urusi, ambazo zinawakilisha ukiri mpya wa Urusi kuhusu matokeo ya vita vyake nchini Ukraine, na kutafuta njia ya kuzuia kuzorota kwa jeshi na uchumi wake na kuzuia kuzorota kwa mazingira ya kimataifa yanayomzunguka, yote hayo ni upande wa pili wa Kirusi ambao si chini ya umuhimu wa upande wa kwanza wa Kichina wa mpango wa amani. Hii ina maana kwamba Urusi inataka kusitisha vita nchini Ukraine lakini inataka kulinda heshima yake.
Kwa hiyo, kukutana kwa pande hizi mbili (athari hasi za kimataifa za vita kwa China, na kukata tamaa kwa Urusi kupata ushindi nchini Ukraine) ndiko kulikozaa mpango huu wa amani wa China nchini Ukraine. Hali hii haikuwepo mwaka mmoja uliopita mwanzoni mwa vita. Inaonekana China ilitarajia Urusi ingemaliza vita kwa faida yake haraka, ndiyo maana China ilisita mwanzoni mwa vita kutoa mpango. Lakini sasa, baada ya Urusi kukaribia kukata tamaa ya ushindi na kuonekana mwelekeo wa Urusi kwenye mazungumzo huku ikilinda heshima yake, baada ya hapo China ilitoa mpango huu.
Huu ndio ukweli wa mpango wa amani wa China nchini Ukraine, na hili ndilo linaloelezea wakati wake, hasa kilichojitokeza katika mpango huo cha kusisitiza kuheshimiwa kwa mamlaka ya mataifa ili kuwavutia Magharibi na Ukraine. Waziri wa Mambo ya Nje wa China alitangaza katika mpango huo kuunga mkono mamlaka ya Ukraine, akisema (kwamba umoja wa ardhi na mamlaka ya mataifa yote utaheshimiwa katika pendekezo la China... CNN Arabic, 18/02/2023), kama njia ya kuvutia Magharibi kwenye mazungumzo.
Nne: Kuhusu swali la uwezekano wa mpango huu wa China kufanikiwa, yaani kumaliza vita nchini Ukraine, hili linategemea mambo kadhaa yenye ushawishi:
1- Inategemea kwanza msimamo wa Marekani ambayo inafuatwa na misimamo ya mataifa ya Ulaya yanayoisaidia Ukraine, misimamo ambayo inawakilishwa na msimamo mkali unaotoka mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, na kutoka kwa Rais wa Ukraine Zelensky. Misimamo hii ya Ukraine na Magharibi inasisitiza ulazima wa jeshi la Urusi kujiondoa kwenye ardhi yote iliyokaliwa nchini Ukraine ikiwemo rasi ya Crimea kama sharti la mazungumzo ya amani. Yaani, mazungumzo na Urusi hayatakuwa kuhusu ardhi, bali kuhusu fidia na kuwafikisha wahalifu wa kivita kwenye mahakama ya kimataifa. Masharti haya yanakataliwa na Urusi ambayo inaashiria hali halisi iliyopo ardhini, yaani kusitisha mapigano kwenye mistari ya sasa ya mapigano, kisha kufanya mazungumzo. Hakika Urusi inataka kutoa makubaliano baada ya kusitisha mapigano kwa namna itakayolinda heshima yake kwa upande mmoja, na kwa upande mwingine kwa kuipa faida fulani za ardhi hata kama ni za ishara tu, pamoja na kuondolewa kwa vikwazo na kuachiwa kwa fedha zake zilizozuiliwa.
2- Na inavyoonekana leo mataifa ya Magharibi hayana hamu na mpango wa China na kwamba yanapanga kuishinda kabisa Urusi nchini Ukraine na yanasubiri jambo hilo. Rais wa Halmashauri ya Ulaya, Ursula von der Leyen, alisema: (Tunahitaji ushahidi zaidi kwamba China haifanyi kazi na Urusi, na hatuoni hilo sasa... CNN Arabic, 18/02/2023). Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani aliituhumu China kuwa inaunga mkono Urusi: (Blinken alisema katika mahojiano yaliyorushwa siku ya Jumapili kuwa China "inafikiria sana" kutuma risasi na silaha kwa Urusi wakati vita vyake dhidi ya Ukraine vikitimiza mwaka mmoja... Al-Quds Al-Arabi, 20/02/2023). Hizi ni ishara tosha kwamba Magharibi wanaendelea kuiunga mkono Ukraine ili kuishinda Urusi.
3- Kwa hayo yote, mpango wa amani wa China nchini Ukraine, licha ya kuashiria kuheshimu umoja wa ardhi ya mataifa, yaani kwamba Urusi inaweza kujiondoa... lakini mpango huu kulingana na mazingira ya leo haukubaliki kwa Marekani na wafuasi wake barani Ulaya pamoja na Ukraine ambayo haina uamuzi wowote. Hii ni kwa sababu Marekani inaiunga mkono Ukraine kwa njia thabiti na inayoongezeka katika aina ya silaha zinazotolewa, na inatangaza kupitia Rais wake Biden kwamba Rais wa Urusi hatashinda nchini Ukraine. Utashi huu thabiti wa Marekani unafuatwa na utashi kama huo nchini Uingereza na mataifa ya mashariki mwa bara la Ulaya kama vile Poland na mataifa ya Baltiki ambayo yana chuki kubwa dhidi ya Urusi. Maana yake ni kwamba mpango wa amani wa China haupati kibali wala kukaribishwa na Marekani. Inaonekana misimamo hii imeiaibisha Urusi, hivyo matamko yake kuhusu mpango huo yakaanza kuwa na lugha ya kukubali bila kuonyesha wazi, yaani inasonga mbele hatua moja na kurudi nyuma nyingine. Sky News Arabia mnamo 27/02/2023 iliripoti kwenye tovuti yake: [Kremlin inasema kuhusu mpango wa China: (Kwamba mazingira si mazuri kwa amani nchini Ukraine) lakini ikarejea na kusema: (Urusi inaonyesha kuthamini kwake mpango wa amani wa China...)] Vilevile, tovuti ya kituo cha Al-Youm mnamo 27/02/2023 iliripoti (Kremlin ilisema kuwa Urusi inatazama kwa umakini mpango wa amani wa China nchini Ukraine, ikibainisha kuwa maelezo ya pendekezo hilo yanahitaji uchambuzi na mahesabu ya kina kulingana na maelezo yake). Ni kana kwamba Urusi inajiwekea njia ya kutokea.
Tano: Hitimisho ni kwamba kipindi kijacho kitashuhudia mabadiliko mapya ambayo kichwa chake kitakuwa mpango wa China wa kumaliza vita nchini Ukraine. Juhudi hizi za China zimekuwa baada ya mwaka mmoja tangu kuanza kwa vita hivyo, kama tumaini kwa Urusi kutoka kwenye dimbwi la Ukraine ambalo ni hatari sana kwa hadhi yake ya kimataifa, mbali na juhudi hizo kuwa ni maslahi ya China kimsingi. Lakini Marekani, Ulaya, muungano wa NATO, na pia Ukraine zinakataa mpango huu na kuwa na shaka nao. Kwa hiyo, nafasi ya mpango huu kufanikiwa inaonekana kuwa katika kiwango cha chini kabisa isipokuwa mazingira ya kimataifa yabadilike au Urusi ithibitishe kuwa ina uwezo wa kuanzisha shambulio kubwa na lenye athari nchini Ukraine, jambo ambalo linaonekana kuwa gumu katika siku za karibu kutokana na Marekani na mataifa ya NATO kuitegea Urusi na mataifa haya kuwa tayari kuipatia Ukraine kila aina ya msaada wa mapigano kuzuia ushindi wa Urusi.
Mwishoni, mataifa haya ya kikafiri ya kikoloni yanayoitwa makubwa katika ulimwengu wa leo yanapigana kati yao si kwa ajili ya heri ya ulimwengu, bali kwa ajili ya shari na madhara. Urusi inaivamia Ukraine ili kumuua kila Myukraine anayejaribu kujihami, na Marekani na Magharibi wanapigana na uvamizi huo kwa kumtumia kila Myukraine na si kwa askari wao! Pande zote mbili zinapigana nchini Ukraine kwa kumuua kila Myukraine. Hivi ndivyo yalivyo mataifa haya yanayotafuta ufisadi katika ardhi, hayathamini wingi wa damu inayomwagika maadamu yanatimiza maslahi yao, bali hata sehemu ndogo ya maslahi yao. Ni kana kwamba historia inajirudia wakati dola za Kiajemi na Kirumi zilipokuwa zikipigana, huyu akishinda na yule akishindwa na hivyohivyo... na kila mmoja wao anafanya kama mashine inayofyonza damu za watu ili kutimiza maslahi yake mwenyewe. Hali hiyo iliendelea mpaka Mwenyezi Mungu alipowakirimu watu wa haki na uadilifu, Umma wa Kiislamu, kwa ushindi na ufunguzi ulio wazi, Uislamu na Waislamu wakawa na utukufu, na ukafiri na makafiri wakadhalilika. Na hakika hili litatokea tena kwa idhini ya Mwenyezi Mungu:
وَيَوْمَئِذٍ يَفْرَحُ الْمُؤْمِنُونَ * بِنَصْرِ اللَّهِ يَنْصُرُ مَنْ يَشَاءُ وَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ
"Na siku hiyo waumini watafurahi. Kwa nusura ya Mwenyezi Mungu; Humnusuru amtakaye, Naye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu." (QS. Ar-Rum [30]: 4-5)
9 Sha'ban 1444 Hijiria
01/03/2023 Miladi