Jibu la Swali
Mabadiliko Mapya ya Kisiasa nchini Lebanon
Swali: Tovuti ya Al-Arabi Al-Jadeed ilichapisha mnamo tarehe 21/01/2025: (... Nawaf Salam alitoka baada ya kukutana na Rais wa Jamhuri Joseph Aoun jioni ya leo Jumanne, katika ikulu ya Baabda akiwa ameshikilia mkononi mwake faili nyeusi bila kufichua kama amewasilisha rasimu yoyote ya majina au muundo wa baraza la mawaziri...), ikifahamika kuwa: [Baada ya nafasi ya urais kubaki wazi kwa zaidi ya miaka miwili kutokana na mizozo ya kisiasa, Bunge la Lebanon lilimchagua Aoun kuwa rais wa nchi mnamo tarehe 09/01/2025. Siku nne baada ya kuchaguliwa kwake, Aoun alimteua Nawaf Salam kuunda serikali mpya ya Lebanon... Al Jazeera 20/01/2025]. Ni nini kinachoendelea nchini Lebanon kutokana na kasi hii ya makubaliano ya kumsimika mkuu wa jeshi Joseph Aoun kuwa rais mnamo tarehe 09/01/2025 baada ya nafasi hiyo kuwa wazi kwa zaidi ya miaka miwili, kisha baada ya siku chache kufikiwa makubaliano kwa Nawaf Salam kuwa Waziri Mkuu mnamo 13/01/2025? Je, mambo haya yote yamewezekanaje kwa kasi hii? Na je, kasi hii inamaanisha kuwa kuna kazi iliyokuwa ikiandaliwa na inaendelea kuandaliwa ili kubadilisha sura ya Lebanon ndani na nje, au ni mabadiliko ya kawaida kama yanavyotokea katika eneo hili?
Jibu: Ili kuweka wazi majibu ya maswali yaliyotajwa hapo juu, tunapitia yafuatayo:
Kwanza: Maendeleo makubwa ya kisiasa katika eneo hili na duniani ndiyo yaliyoongoza mabadiliko haya ya haraka nchini Lebanon, ambapo Aoun alichaguliwa kuwa rais wa Lebanon, na Nawaf Salam akateuliwa kuunda serikali. Ili kufafanua hilo, tunasema:
Mara tu baada ya mauaji yaliyofanywa na dola ya Kiyahudi dhidi ya viongozi wa Hizb la Iran na kabla ya usitishaji vita, kuliibuka wito nchini Lebanon wa kumchagua rais na kukomesha hali ya nafasi hiyo kuwa wazi. Wito huu uliongozwa na wapinzani wa Hizb la Iran, kama vile kikundi cha Samir Geagea ambacho kilitangaza wazi kukataa kwake kuiunga mkono Gaza katika vita. Huku kulikuwa ni kutumia fursa ya hali iliyotokana na vita na ilikuwa kwa ushauri wa wajumbe wa Ulaya waliokuwa wakizunguka Lebanon sambamba na ziara za mjumbe wa Marekani Hochstein, ambazo zilikuwa zikilenga usitishaji vita. Hizb la Iran lilikuwa likipinga wito huu kutoka kwa wapinzani wa Lebanon.
Baada ya vikao 12 vilivyofeli vya kumchagua rais nchini Lebanon katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, nguvu mbalimbali za kisiasa nchini Lebanon zilikubaliana kwa namna ya kushtukiza juu ya mkuu wa jeshi Joseph Aoun kuwa rais mpya ili kukomesha hali ya nafasi hiyo kuwa wazi. Hizb la Iran lilikuwa likitangaza kuwa mgombea wake ni Suleiman Frangieh (Al-Alam TV, 07/01/2025). Frangieh huyu anahesabiwa kuwa katika mhimili wa Iran na utawala wa Bashar uliopinduliwa. Kisha Suleiman Frangieh akatangaza kujiondoa kwenye kinyang'anyiro ili kupisha makubaliano.
Wafuasi wa mhimili wa Iran (Hizb lake na Harakati ya Amal) hawakumchagua Joseph Aoun katika kikao cha kwanza, yaani upigaji kura ulifeli kwa sababu ya kutopata asilimia ya theluthi mbili (kura 86). Kisha katika kikao cha pili na baada ya mkutano na makundi haya ya bunge, walimpigia kura na akapata kura 99. Hivyo basi, upigaji kura kwa Joseph Aoun katika kikao cha pili ulilenga kuonyesha kuwa bila kura za Hizb la Iran na Harakati ya Amal, Joseph asingeshinda urais. Ingawa hilo lina maana fulani kwamba ushawishi wa wafuasi wa Iran bado upo na kwamba wanaathiri upigaji kura, kitendo chao cha kuacha kukwamisha uchaguzi — na wanauwezo wa kufanya hivyo — kinamaanisha kurudi nyuma.
Mnamo tarehe 13/01/2025, Waziri Mkuu mpya wa Lebanon, Nawaf Salam, aliteuliwa. Alipigiwa debe kama mgombea wa makubaliano ya kisiasa; yeye si Najib Mikati (mgombea wa Hizb la Iran na washirika wake) wala si Fouad Makhzoumi (mgombea wa kikundi cha Samir Geagea, yaani wapinzani wa Hizb la Iran). Hivyo ndivyo Nawaf Salam alivyoteuliwa kuwa Waziri Mkuu nchini Lebanon.
Nawaf Salam alikuwa mgombea aliyekataliwa na Hizb la Iran na nguvu zilizoungana nalo nchini Lebanon. Hizb la Iran lilimkataa mwaka 2019 baada ya kujiuzulu kwa Saad Hariri na wakati huo lilimuita "mgombea wa Marekani", na Hassan Diab akateuliwa wakati huo. Chama hicho kilikataa tena uteuzi wake mwaka uliofuata baada ya mlipuko wa bandari ya Beirut mnamo 04/08/2020.
Inaonekana kuwa chaguo hili limeikasirisha Hizb la Iran na Harakati ya Amal: (Mwandishi wa Al Jazeera aliripoti mnamo 13/01/2025 kuwa kundi la bunge la Hezbollah halikumtaja mgombea yeyote wa nafasi ya Waziri Mkuu wa Lebanon. Kufuatia mkutano wa wabunge wa Hezbollah na Rais wa Lebanon kwa ajili ya kumteua Waziri Mkuu, mbunge wa chama hicho Mohammad Raad alielezea masikitiko yake na kusema kuwa baadhi ya watu wanafanya kazi ya kuitenga harakati hiyo na kuifuta. Aliongeza, katika taarifa kwa waandishi wa habari, "Tulipiga hatua chanya katika mkutano wetu na Rais wa Jamhuri, lakini hatukupata mkono wa ushirikiano," akisisitiza kuwa harakati hiyo itatenda kwa utulivu na hekima kwa ajili ya maslahi ya kitaifa. Chanzo kilicho karibu na Hezbollah kilieleza kuwa chama hicho na mshirika wake Harakati ya Amal, inayoongozwa na Spika wa Bunge Nabih Berri, walikuwa wakiunga mkono kuteuliwa tena kwa Mikati. Alifafanua kuwa kuteuliwa tena kwa Mikati "ni sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa na mjumbe wa Saudi Arabia nchini Lebanon, Yezid bin Mohammed bin Fahd Al Farhan, ambayo yalipelekea Hezbollah na Amal kuendelea na uchaguzi wa Aoun kama rais siku ya Alhamisi iliyopita"). Kwa maana hiyo hiyo, BBC mnamo 13/01/2025 ilinukuu mkuu wa kundi la Hizb la Iran bungeni akisema kuwa kumteua Aoun ni "sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa na mjumbe wa Saudi Arabia nchini Lebanon, ambayo yalipelekea Hezbollah na Amal kuendelea na uchaguzi wa Aoun kuwa rais".
Pili: Hivyo ndivyo mambo yalivyokwenda nchini Lebanon; bunge likamchagua rais mpya na Waziri Mkuu mpya kuteuliwa pia. Kwa kuangalia kwa umakini tunapata yafuatayo:
Tunakuta kuwa Marekani imeridhika kikamilifu na maendeleo mapya ya kisiasa nchini Lebanon, bali kwa usahihi zaidi ni kwamba yeye ndiye aliye nyuma yake. Rais Biden alisema katika taarifa yake: ("Nampongeza kwa kuchaguliwa kwake kuwa rais wa Lebanon", na akaendelea: "Rais Aoun atatoa uongozi madhubuti wakati Lebanon na (Israel) zikitekeleza usitishaji kamili wa mapigano na kurejea kwa mamia ya maelfu ya watu katika nyumba zao na wakati Lebanon ikipona na kujijenga upya. Rais Aoun ana imani yangu. Naamini kwa dhati kuwa yeye ndiye kiongozi sahihi kwa wakati huu". CNN Arabic, 09/01/2025). Kadhalika, kibaraka wa Marekani Mohammed bin Salman nchini Saudi Arabia alimpongeza (Alhurra, 09/01/2025).
Hivyo basi, maendeleo mapya ya kisiasa nchini Lebanon hayahusiani na mzozo wa kimataifa juu yake. Lebanon ilikuwa mikononi mwa Marekani wakati wa urais wa Michel Aoun, aliyeonekana kama sehemu ya mhimili wa Iran. Rais wa sasa, Joseph Aoun, aliteuliwa mnamo mwaka 2017 kuwa mkuu wa jeshi na kibaraka wa Marekani Michel Aoun. Hii ina maana kwamba Rais wa sasa Joseph Aoun asili yake ni katika kundi la vibaraka wa Marekani. Hata kabla ya nafasi ya urais kuwa wazi mwaka 2022 na baada ya hapo, Marekani ilikuwa ikitoa misaada ya kijeshi kwa jeshi la Lebanon, ikimaanisha kuwa ina uhusiano wa karibu na mkuu wa jeshi Joseph Aoun. Na hawezi kutoka nje ya mfumo huu pia Nawaf Salam, ambaye ametumia maisha yake kusoma na kufundisha katika vyuo vikuu vya Ufaransa na Marekani na taasisi za kimataifa, na mwisho akiwa Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ).
Kwa hiyo, Marekani leo inabadilisha kanuni za mchezo wake nchini Lebanon. Baada ya kuwa inategemea Iran na mhimili wake na nguvu zake nchini Lebanon ili kuimarisha ushawishi wake, leo inazitenga nguvu hizo kwa ajili ya kuibua shakhsia wapya ili kuendeleza ushawishi wake nchini Lebanon. Lebanon ilikuwa katika mtego wa Marekani na bado ipo, lakini Marekani inabadilisha tu sura na muonekano.
Ama nguvu zinazofuata nchi za Ulaya, zinajua kuwa ushawishi wao ni mdogo kuliko wa Marekani. Ufaransa, kupitia ushiriki wake katika Kamati ya Mataifa Matano, ilikuwa ikikataa jina la Joseph Aoun kama mgombea urais tangu mwaka 2023 wakati Marekani na Saudi Arabia zilipotaja jina lake mapema (Al-Arabi Al-Jadeed, 22/09/2023). Lakini mwishowe ililazimika kumkubali. Kwa upande mwingine, nchi za Ulaya zinakosa ushawishi wa kumfanya rais awe mfuasi wao. Samir Geagea, ambaye ana kundi kubwa zaidi la Wakristo bungeni, hakuonyesha hata nia ya kugombea urais kutokana na upinzani mkali dhidi yake kutoka kwa Hizb la Iran. Hizb la Iran lilisema (Hakuna kipingamizi kwa jina lolote isipokuwa Samir Geagea; kwa sababu mradi wake ni wa kuiangamiza Lebanon. Asharq Al-Awsat, 06/01/2025). Kadhalika, lilikataliwa jina la mgombea Fouad Makhzoumi kwa ajili ya nafasi ya Waziri Mkuu lililopendekezwa na vyama vya upinzani (RT, 13/01/2025). Kwa hiyo, nguvu zinazofuata Ulaya haziwezi kuhodhi yoyote kati ya nafasi tatu za uongozi nchini Lebanon na kwamba nafasi hizi zinabaki mikononi mwa wafuasi wa Marekani.
Lakini nchi za Ulaya zinakubali maendeleo mapya ya kisiasa nchini Lebanon, (Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, alimpongeza Aoun kwa kuchaguliwa kwake kuwa rais wa Lebanon, katika ujumbe aliouchapisha kupitia akaunti yake kwenye mtandao wa X. Macron aliona kuwa uchaguzi huu "unafungua njia ya mageuzi na kurejesha mamlaka ya Lebanon na ustawi wake". Alhurra, 10/01/2025). Alichokisema Rais wa Ufaransa kinaakisi hali ya nguvu za Ulaya na furaha yao kwa kupungua kwa kivuli cha Iran nchini Lebanon. Yaani, wanatosheka na kufikia sehemu ya matakwa yao ambayo ni kuiweka Lebanon kwenye njia iliyo mbali na Iran. Wanatosheka na kuwepo katika Kamati ya Mataifa Matano ya kuangalia masuala ya Lebanon iliyoundwa baada ya nafasi ya urais kuwa wazi. Ufaransa inakaa humo bega kwa bega na Marekani, Misri, na Saudi Arabia, huku Qatar ikiwakilisha maslahi ya Waingereza humo.
Yaani, Marekani ndiye mchezaji wa kimataifa mwenye nguvu nchini Lebanon leo, na ndiye anayebadilisha sura na muonekano, huku nchi za Ulaya zikitosheka na kuondolewa kwa kivuli cha Iran nchini Lebanon.
Tatu: Kuhusu kubadilisha sura ya Lebanon ndani na nje, hilo linaonekana kupitia mambo yafuatayo:
Ndani ya Lebanon, kuna uwezekano mkubwa kuwa vikwazo dhidi ya silaha za Hizb la Iran vitaongezeka. Neno "Mapambano" (Muqawama) ambalo hapo awali lilikuwa likiambatana na matamshi na taarifa za urais nchini Lebanon limetoweka katika matamshi ya rais mpya na taarifa zake:
a- (Tofauti na hotuba za kimapokeo zilizotambulisha vipindi vilivyopita baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Lebanon, hotuba ya Aoun ilikuja na jumbe za wazi, muhimu zaidi ikiwa ni msisitizo wake juu ya umuhimu wa "kuimarisha haki ya dola kuhodhi silaha" kama nguzo ya msingi ya kuimarisha mamlaka ya Lebanon. Alhurra, 10/01/2025), (Aoun alisema katika hotuba yake: Dola ya Lebanon — na narudia dola ya Lebanon — itajikomboa kutoka kwa uvamizi wa Israel, CNN Arabic, 10/01/2025).
b- (Nawaf Salam alizungumzia uvujishaji wa habari za vyombo vya habari kuhusu ugawaji wa wizara kwa vyama vya kimapokeo na kufuata masharti ya Hezbollah na Harakati ya Amal, hususan kuwapa wizara ya fedha... Salam aliongeza kuwa "hajajitolea kutoa wizara yoyote kwa upande wowote, na wizara ya fedha ni kama wizara nyinginezo si milki ya dhehebu fulani".. akisisitiza kuwa ana mwelekeo wa kuunda serikali ya mawaziri 24... Al-Arabi Al-Jadeed, 21 Januari 2025).
Kwa upande wa nje, kwa kutafakari yanayotokea, inaonekana yafuatayo:
a- Kinyume na ilivyozoeleka, hakukuonekana nafasi yoyote ya Iran katika kumchagua rais na Waziri Mkuu, ingawa kiini cha nafasi hii kipo nyuma ya msimamo wa chama chake nchini Lebanon. Na kwa sababu Hizb la Iran na washirika wake wanaweza kukwamisha maendeleo hayo na hawakufanya hivyo, basi mabadiliko haya ya Kimarekani yaliyotajwa kama mapinduzi yanafanyika kwa ridhaa ya kimya kimya ya Iran. Ushawishi wa Iran unapungua kweli katika eneo la Kiarabu, na Marekani imeikabidhi Uturuki suluhu ya kisiasa nchini Syria, na kuiondoa Iran humo kama ilivyoiondoa Urusi katika mzani wa Syria kabisa. Hii ndiyo sera mpya ya Marekani katika eneo hili, na hiki ndicho ilichokifanya nchini Lebanon. Na hii si sera ya utawala wa Biden pekee, bali utawala ujao una maono hayo hayo, na utafanya kazi ya kuimarisha hilo nchini Syria na Lebanon na kuipanua hadi Iraq. Sera hii ya Marekani inaendana kikamilifu na kile ambacho dola ya Kiyahudi inakitaka, na huenda ikawa ni miongoni mwa ahadi ambazo utawala wa Biden ulitoa kwa dola ya Kiyahudi ulipoishawishi kukubali usitishaji vita nchini Lebanon.
b- Inaonekana kuwa Rais mpya wa Lebanon anatambua kuwa Marekani inamleta katika hatua hii kwa ajili ya mabadiliko makubwa katika sura ya Lebanon, (Rais Aoun alisema mwanzoni mwa hotuba ya kiapo "Waheshimiwa wabunge wamenisherehesha kwa kunichagua kuwa Rais wa Jamhuri ya Lebanon, na ni nishani kuu ninayoibeba na majukumu makubwa zaidi, nikawa rais wa kwanza baada ya karne ya kwanza ya kuanzishwa kwa dola ya Lebanon Kuu, katikati ya tetemeko la Mashariki ya Kati ambapo miungano imepasuka na tawala zimeanguka na mipaka inaweza kubadilika". Independent Arabia, 11/01/2025). Kwa mujibu wa chanzo hicho hicho, ataelekea Saudi Arabia katika safari yake ya kwanza nje ya nchi, (Rais wa Lebanon Joseph Aoun amesema leo Jumamosi kuwa Saudi Arabia itakuwa kituo chake cha kwanza cha safari za nje, kufuatia mwaliko wa kuitembelea nchi hiyo aliopewa wakati wa mazungumzo ya simu na Mrithi wa Kiti cha Ufalme Mwanamfalme Mohammed bin Salman).
c- Inabainika kutokana na yote haya pia kuwa Marekani inaipa Saudi Arabia jukumu la kushughulikia masuala ya Lebanon wakati huu, baada ya Iran kuwa na jukumu hilo wakati uliopita. Kwa hiyo, nafasi ya Saudi Arabia itakuwa maarufu katika masuala ya Lebanon, na itakuwa na mchango mkubwa katika ujenzi mpya hasa kwa vile inatarajiwa kuwa Iran itakumbwa na shinikizo mpya za kibiashara na kifedha zitakazowekwa na utawala wa Trump. Hivyo Saudi Arabia itakuwa mbadala wa Iran nchini Lebanon, upande wa kisiasa na pia kifedha kwa ajili ya ujenzi mpya na kuunga mkono dola ili kuimarisha jeshi lake na kurahisisha upokonyaji silaha wa Hizb la Iran. Hilo linaweza kuivuta Lebanon kuelekea kwenye mahusiano ya kawaida (tatbi') na dola ya Kiyahudi hasa kwa vile Rais ajaye wa Marekani Trump anahimiza mahusiano ya Saudi Arabia na dola ya Kiyahudi.
Nne: Hali hii ya kutisha inatarajiwa kuendelea nchini Lebanon na karibu na Lebanon mpaka Allah atakapoleta jambo lililoahidiwa, itakaposimamishwa Dola ya Kiislamu, dola ya Khilafah, na kutoweka kwa nguvu hizi zote za kisiasa kutoka Lebanon na maeneo jirani, na kutoweka pamoja nazo dola ya Kiyahudi, kama ulivyotoweka utawala wa Assad nchini Syria. Hivyo ardhi ya Sham itarejea kama ilivyokuwa siku zote, kuwa moyo wa Umma wa Kiislamu mzima. Na sisi tuna uhakika na kurejea kwa Khilafah upya baada ya utawala huu wa kidikteta tunamoishi sasa.. Ahmad amepokea kutoka kwa Hudhayfah amesema: Mtume wa Allah ﷺ amesema:
ثُمَّ تَكُونُ مُلْكاً جَبْرِيَّةً فَتَكُونُ مَا شَاءَ اللهُ أَنْ تَكُونَ، ثُمَّ يَرْفَعُهَا إِذَا شَاءَ أَنْ يَرْفَعَهَا، ثُمَّ تَكُونُ خِلَافَةً عَلَى مِنْهَاجِ النُّبُوَّةِ. ثُمَّ سَكَتَ
"Kisha utakuwepo utawala wa kidikteta, na utakuwepo kwa muda anaotaka Allah uwepo, kisha Atauondoa Atapotaka Auondoe, kisha itakuwepo Khilafah kwa njia ya Utume. Kisha (Mtume) akanyamaza." (HR Ahmad)
Na kwamba mahali popote itakaposimama itafika Sham na kutulia humo. At-Tabarani amepokea kutoka kwa Salama bin Nufayl amesema: Mtume wa Allah ﷺ amesema:
عُقْرُ دَارِ الإِسْلامِ بِالشَّامِ
"Kiini cha nyumba ya Uislamu kiko Sham." (HR At-Tabarani)
Na itapigana na Mayahudi na kuiondoa dola yao inayokalia kwa mabavu ardhi takatifu na kuirejesha Palestina yote katika Darul Islam.. Na hakika kesho kwa anayeisubiri iko karibu.
Lakini kanuni ya Allah imetaka kuwa wasishuke malaika kutoka mbinguni kutusimamishia Khilafah itakayopigana na adui yetu huku sisi tukiwa tumekaa, bali huwateremsha malaika wake kama msaada na bishara ya ushindi wake kwa wanaume waliomwamini Mola wao na akawazidisha uongofu, askari Waislamu, wenye subira vitani, wanaojilinda kwa Imamu wao na kupigana nyuma yake dhidi ya maadui zao.. Kisha tutakuwa miongoni mwa walio haki ya kupata bishara:
نَصْرٌ مِنَ اللهِ وَفَتْحٌ قَرِيبٌ وَبَشِّرِ الْمُؤْمِنِينَ
"Nusuru itokayo kwa Allah na ushindi ulio karibu; na wabashirie Waumini." (QS. As-Saff [61]: 13)
23 Rajab 1446 H 23/01/2025 M