Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Harakati za Umma nchini Iraq, Lebanon na Iran

December 05, 2019
5133

Swali:

Tunafahamu kuwa harakati za umma nchini Iraq, Lebanon na Iran zilianza kwa hiari (bila kupangwa) kama ilivyoelezwa katika muhtasari wa tarehe 05/11/2019, je, bado ziko hivyo? Na je, kuna nafasi yoyote ya Ulaya katika nchi hizi tatu ambazo Marekani ndiyo yenye ushawishi mkuu? Je, hali katika nchi hizi tatu itabaki kama ilivyo, au Marekani iko katika mchakato wa kubadilisha vibaraka hawa au baadhi yao kupitia mabadiliko ya kawaida au kupitia jeshi kama ilivyofanya nchini Misri na Sudan? Jazaakallahu khayran.

Jibu:

Ili kuweka wazi jibu la maswali yaliyo hapo juu, tunapitia mambo yafuatayo:

Kwanza: Sababu za maandamano na vichocheo vyake:

Ndiyo, maandamano yalianza kwa hiari katika nchi zote tatu, na vichocheo vyake kwa ufupi ni kama ifuatavyo:

  1. Maandamano ya Iraq: Maandamano ya umma nchini Iraq yalizuka mapema mwezi Oktoba 2019 katika mfumo wa maandamano na migogoro iliyopelekea kufungwa kwa madaraja mjini Baghdad na barabara nyingine kuu. Hii ilikuwa ni kupinga kuzorota kwa hali ya kiuchumi ya nchi hiyo, kuenea kwa ufisadi wa kiutawala na kifedha katika vyombo vya serikali, na kuenea kwa ukosefu wa ajira. Yalianza kwa hiari baada ya hali kuwa mbaya sana na maisha ya watu kuwa magumu... serikali haikuweza kutatua suala la umeme kwa kipindi cha miaka 16, wala kutoa nafasi za kazi kwa vijana na wahitimu, wala kukidhi mahitaji ya watu licha ya utajiri mkubwa wa mafuta... kisha maandamano yakalipuka na kusababisha vifo vya takriban watu 350, mbali na maelfu ya waliojeruhiwa na waliokamatwa. Ofisi za vyama vinavyoshiriki serikalini vinavyoiunga mkono Iran zilichomwa moto, kisha ubalozi mdogo wa Iran huko Karbala ukachomwa moto tarehe 04/11/2019 na kupigwa mawe huku kukiwa na madai ya kuondolewa kwao mjini humo, na ubalozi mdogo wa Iran huko Najaf ukachomwa moto tarehe 27/11/2019... Jambo lililoichanganya zaidi serikali ya Iraq ni kwamba maandamano haya yalienea katika miji ya Baghdad, Nasiriyah, Karbala, Najaf na miji mingine ya kusini, maeneo ambayo serikali inayachukulia kuwa ni ngome zake za kijamii. Kutokana na ukubwa wa athari zake, Abdul-Mahdi hakuweza kuendelea kung'ang'ania madaraka, hivyo akajiuzulu tarehe 30/11/2019 na Bunge likaidhinisha kujiuzulu huko tarehe 01/12/2019.

  2. Maandamano ya Lebanon: Hali ya kiuchumi nchini Lebanon iligusa ukingo wa kuporomoka kabisa au karibu na hivyo! Deni la taifa la Lebanon lilifikia "dola bilioni 85.32" mapema mwaka 2019 (Al-Araby Al-Jadeed, 15/03/2019). Hili ni deni kubwa ambalo riba yake pekee inateketeza takriban nusu ya mapato ya serikali nchini Lebanon. "Uwiano wa deni la nchi kwa pato la taifa ni asilimia 152, na riba ya deni hilo inateketeza takriban nusu ya mapato ya nchi" (BBC, 28/10/2019). Uhalifu huu wa kirasimali umeacha "kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira nchini Lebanon kinachokadiriwa kuwa asilimia 37 kwa wale walio chini ya umri wa miaka 35..." (BBC, 26/11/2019). Mbele ya uharibifu huu wa kiuchumi ulioachwa na tabaka la kisiasa kwa wananchi, cheche ya kodi ya "WhatsApp" mnamo 17/10/2019 iliwasha mitaa ya Lebanon. Ofisi za wabunge zilichomwa moto hasa kusini mwa Lebanon, na Beirut, Nabatieh, na Tyre ziliwaka moto, na maandamano makubwa yakatokea... kisha haraka yakageuka kuwa madai ya kujiuzulu kwa serikali, na hata kubadilishwa kwa wasomi wote wa kisiasa nchini Lebanon... Kwa kutumia fikra za kiusalama ambazo serikali na wafuasi wake nchini Lebanon wanazitumia, wafuasi wa chama cha Iran walijaribu kuwatisha waandamanaji mnamo tarehe 24 na 25/10/2019 kwa kuvamia viwanja vya maandamano, kisha wafuasi wa chama cha Iran na harakati ya Amal walijaribu tena mjini Beirut!

  3. Maandamano ya Iran: Serikali ya Iran haikuwa katika hali bora zaidi kuliko nchi za mhimili wake - Iraq, Lebanon na kabla yake Syria. Inakosa mtazamo wa kichungaji (ri'ayah) katika kuiongoza nchi, jambo lililopelekea Walinzi wa Mapinduzi kudhibiti sekta kubwa za uchumi wa Iran, na kutengwa kwa maeneo yasiyo ya Kiajemi mipakani, jambo lililounda ukanda wa miji ya kimaskini pembezoni mwa nchi, na hali ya kiuchumi iliyo karibu kulipuka katika kitovu na pembezoni kwa pamoja. Ilikuwa ni aibu kwa serikali inayojivunia mpango wa nyuklia na makombora kuona maandamano ya umma yakizuka kwa sababu ya uhaba wa petroli! Uhaba huo ulitokana na ukosefu wa viwanda vya kusafisha mafuta, ambalo ni tasnia isiyo ngumu kwa nchi zinazojali masuala ya watu wake ipasavyo... Kisha, licha ya kuongezeka kwa matumizi ya petroli nchini Iran kwa takriban 40% tangu 2017 na kushindwa kwa kiwanda cha kusafisha mafuta katika mkoa wa Hormozgan, kiasi kikubwa cha petroli kinatoroshwa nje na magenge ambayo si vigumu kwa serikali kuyajua kwa sababu ya tofauti ya bei. Hii ni dhihirisho jingine la kushindwa kwa serikali katika kusimamia mojawapo ya rasilimali muhimu zaidi nchini humo, ambayo ni mafuta! Kisha serikali ikapandisha bei ya petroli kwa 300%, na maandamano yakazuka tarehe 15/11/2019 mjini Tehran na miji mingine mingi ya Iran. Maandamano hayo yalikuwa makali ambapo mabenki yalichomwa moto, taasisi za kidini za Iran (hawza), ofisi za usalama na za serikali zilishambuliwa. Serikali ilikata Internet ili kuzuia mawasiliano ya waandamanaji, na utawala huo ukatumia kiwango cha juu zaidi cha vurugu katika kukabiliana na harakati hii ya maandamano na kuizima kwa nguvu na moto. "Wakati vikosi vya usalama vya Iran vikiendelea na kampeni zao za ukandamizaji dhidi ya waandamanaji, upinzani wa Iran ulithibitisha mnamo tarehe 23 Novemba kuwa idadi ya vifo katika maandamano imezidi 300, ambapo majina 99 kati yao yameandikwa, na idadi ya waliojeruhiwa imezidi 4,000, huku idadi ya waliokamatwa ikizidi watu 10,000. Pia ilibainishwa kuwa Walinzi wa Mapinduzi waliondoa miili ya waliouawa kutoka mahospitalini na kuipeleka kusiko julikana" (Independent Arabia, 24/11/2019).

Pili: Je, maandamano bado ni ya hiari bila kuingiliwa na Ulaya?

Ulaya imejaribu kutumia maandamano haya... lakini haijawa na ufanisi au ushawishi katika kupenya ushawishi wa Marekani katika nchi hizi tatu, na ufafanuzi wake ni kama ifuatavyo:

  1. Majaribio ya Ulaya nchini Iraq: Kama tulivyotaja hapo awali, maandamano nchini Iraq, hasa katika maeneo ya kusini, yalikuwa yakiongezeka na kujikita katika maeneo ya Mashia. Haizuiliki kuwa Ulaya, hasa Uingereza, inaweza kuwa imejaribu kutumia maandamano hayo. Ingawa hapakuwa na ushahidi wa kutegemewa kuhusu kuwepo kwa uingiliaji kati wa Uingereza katika maandamano, Iran ilikuwa ikihofia jambo hili, na hata ilikuwa ni wasiwasi mkubwa kwake kiasi kwamba khatibu wa swala ya Ijumaa mjini Tehran, Mohammad Ali Movahedi Kermani, alisema wakati wa hotuba yake akiwataja waandamanaji wa Iraq "kuwa ni Mashia wa Waingereza," na kuongeza: "Baadhi ya makundi yaliyopotoka ambayo tunayaita Mashia wa Waingereza yamepenya katika safu za watu wa Iraq..." (Iran International, 01/11/2019). Kauli yake hiyo ilikuwa ni dhihirisho la hofu ya maafisa wa Iran kwamba Uingereza inaweza kutumia harakati za watu. Hii ni pamoja na jaribio la Iran la kuwatisha waandamanaji kwa kuwatuhumu kuwa ni mawakala wa Waingereza, hasa kwa vile msimamo wa Uingereza ulikuwa wazi katika kuunga mkono maandamano. "Ubalozi wa Uingereza ulisema kwenye ukurasa wake rasmi wa Twitter kwamba maandamano ya amani ni haki ya watu wa Iraq" na kuongeza: "Vurugu dhidi ya waandamanaji hazikubaliki"... "Maombi yetu ni kwa waliojeruhiwa na familia za wale waliopoteza maisha katika maandamano" (Shirika la Habari la Sputnik la Urusi, 05/11/2019). Huu ni msimamo ule ule ambao ulikuwa umeelezwa na Waziri wa Nchi wa Uingereza, Andrew Morrison, kama ulivyoripotiwa na tovuti ya Al-Ain News tarehe 27/10/2019.

  2. Majaribio ya Ulaya nchini Lebanon: Inafahamika kuwa Lebanon kuna wafuasi wa Marekani na wa Ulaya. Inafahamika pia kuwa wafuasi wa Marekani, iwe ni wa moja kwa moja kama Aoun na Berri, au wa njia isiyo ya moja kwa moja kama Hizbullah kupitia Iran, hawa ndio upande wenye nguvu zaidi kimali na kimwili... Ama wafuasi wa Ulaya (Uingereza na Ufaransa) ni upande dhaifu zaidi kama Geagea na Jumblatt... Ama Hariri ndiye dhaifu zaidi kwa sababu ana mguu mmoja Ulaya na mwingine Saudi Arabia inayofungamana na Marekani. Vibaraka hawa hawawezi kuamua, bali hufanya vitendo vya kuuchanganya upande mwingine. Kwa mfano, mawaziri wanne wa chama cha Lebanese Forces mnamo 19/10/2019 walijiuzulu kutoka kwa serikali ambayo waandamanaji wanadai ianguke. Waziri Mkuu Saad Hariri alitangaza tarehe 18/10/2019 muda wa saa 72 wa kushughulikia mgogoro huo, kisha akawasilisha kujiuzulu kwake tarehe 29/10/2019 kinyume na matakwa ya Rais wa nchi na matakwa ya chama cha Iran kinachodhibiti usalama nchini Lebanon... Kisha Ufaransa ikamtuma mjumbe wake nchini Lebanon, Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa, Christophe Farnaud, "ambaye alimfikishia Rais Aoun ujumbe kutoka kwa Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, na serikali ya Ufaransa ukithibitisha nia ya Ufaransa katika hali ya Lebanon na utayari wake wa kuisaidia Lebanon katika mazingira ya sasa" (Al-Arabiya, 13/11/2019). Ziara ya mjumbe huyo haikupokelewa vyema na wafuasi wa Marekani. Shirika la Taifa la Habari liliripoti kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje Bassil "kwamba alimfahamisha mjumbe wa Ufaransa juu ya ulazima wa kutokuingia upande wowote wa nje katika mgogoro wa Lebanon na kuutumia." Vilevile, Uingereza ilimtuma mjumbe wake Richard Moore ambaye alikutana na Aoun na kusema: "Uingereza imekuwa mshirika na muungaji mkono muhimu wa Lebanon kwa muda mrefu, kwa mfano, uwekezaji wa dola milioni 200 mwaka jana kusaidia usalama, utulivu, ustawi na mamlaka ya Lebanon." Aliendelea: "Ni muhimu kuendelea kuheshimu haki ya maandamano ya amani, na ukandamizaji wowote wa harakati ya maandamano kupitia vurugu au vitisho na upande wowote haukubaliki kabisa" (Independent Arabia, 25/11/2019).

  3. Majaribio ya Ulaya nchini Iran: Serikali ya Iran, kama kawaida yake, ilikuwa ikidai kwamba inakabiliana na njama na vitisho vya nje. "Kamanda wa Walinzi wa Mapinduzi ya Iran, Jenerali Hossein Salami, leo ametoa tishio la moja kwa moja kwa Marekani, Israel, Uingereza na Saudi Arabia, la 'kuangamizwa' endapo watavuka 'mistari myekundu' katika kushughulika na nchi yake. Salami alisema katika hotuba aliyoitoa mbele ya waandamanaji wanaoiunga mkono serikali mjini Tehran iliyorushwa na televisheni ya Iran: 'Naiambia Marekani, Israel, ukoo wa Saud na Uingereza kwamba mmetujaribu katika nyanja mbalimbali na hamkuweza kutujibu, na kila mtu amesikia makofi yetu.' Aliendelea: 'Tunawaambia msivuke mistari yetu myekundu, na mkivuka mistari yetu myekundu tutawaangamiza'" (RT, 25/11/2019). Serikali inataka kutoa picha kwamba maandamano yanachochewa na nguvu za nje na si kutoka kwa watu ambao wameonja machungu! Ikumbukwe kwamba ishara zote zinaonesha kuwa maandamano ya watu yanatoka katika mioyo yao na damu zao! Lakini inaonekana kuwa wimbo wa kuingiliwa na nje umekita mizizi katika serikali ya Iran kiasi kwamba khatibu wa Ijumaa mjini Tehran kama tulivyotaja hapo awali aliwatuhumu Mashia waandamanaji nchini Iraq kuwa ni Mashia wa Waingereza! Maandamano nchini Iran si ya kwanza na hayatakuwa ya mwisho, na uwezekano mkubwa ni kwamba ni ya hiari. Hakuna dalili zinazoashiria mikono ya kimataifa. Maandamano nchini Iran ni kama yale ya Syria, watu wanapambana dhidi ya watawala madikteta ambao siasa zao hazijajua ladha ya mafanikio katika kusimamia mambo ya Umma.

Tatu: Kuhusu mabadiliko ya vibaraka wa Marekani katika nchi hizi tatu, hali iko hivi:

  1. Ushawishi wa kweli katika nchi hizi tatu ni ushawishi wa Marekani, na Ulaya (Uingereza na Ufaransa) haijafanikiwa kushirikiana na Marekani katika ushawishi huu.

  2. Hadi Umma utakapoinuka kwa mwamko sahihi kwa msingi wa Uislamu na kisha kuleta mabadiliko ya kweli, hadi hapo itakapofanyika, watawala wa nchi hizi tatu wataendelea kuwa chini ya siasa za Marekani inayowabadilisha au kuwaweka...

  3. Nchi za kikafiri za kikoloni zinamtaka kibaraka atumikie maslahi yao. Ikitokea harakati ya watu na machafuko katika zama zake, humpa muda maalum. Ikiwa hawezi kupanga mambo yake katika utawala na kisha anakuwa hawezi kumtumikia bwana wake, basi humbadilisha... Chombo kinachotumika ni hadithi ya demokrasia ya uongo kwa kuleta kibaraka mpya mwenye sura isiyo na giza sana kuliko yule aliyefukuzwa. Hii ni ikiwa mgogoro si mkubwa sana, la sivyo chombo kinachotumika ni "jeshi" kama ilivyofanya Misri mwaka 2011 au Sudan mwaka 2019.

Nne: Kwa kuangalia mabadiliko yanayotarajiwa katika nchi hizi tatu kutokana na ukweli uliopo, inabainika yafuatayo:

  1. Kwa upande wa Iran: Marekani inatangaza waziwazi kwamba haitaki kubadilisha utawala nchini Iran. Yaani, hata mauaji yafikie kiasi gani katika maandamano, Marekani inaona kuwa utawala huu unatumikia maslahi yake! Wakati damu za Waislamu nchini Iran zikimwagika na utawala huo, maafisa wa Marekani walikuwa wakitangaza kuulinda utawala huo. "Afisa mkuu katika Ikulu ya Marekani alieleza Jumapili kuwa nchi yake haitaki kubadilisha utawala nchini Iran..." (Al-Arabiya Net, Jumapili 17/11/2019). Kwa hivyo, hakutarajiwi mabadiliko ya utawala nchini Iran kutokana na maandamano ya mwezi wa 11/2019 kama vile ambavyo hayakutokea mabadiliko kutokana na maandamano ya mwaka uliopita.

  2. Kwa upande wa Lebanon: Kama tulivyotaja, Lebanon ina wafuasi wa Marekani na wa Ulaya... na kwamba kundi la kwanza ndilo lenye nguvu, na hii inarahisisha makubaliano ya yule dhaifu kulingana na njia ya ufumbuzi wa kati (compromise). Pande hizo mbili zinatofautiana kuhusu serikali ya techno-political au serikali ya technocrat! Kwa vyovyote vile, inatarajiwa kuwa Marekani itabadilisha mizani ya utawala nchini Lebanon, ambapo uzito utakuwa kwa wafuasi wa Marekani na kuwashirikisha wafuasi wa Ulaya lakini kwa kiasi... kisha kuwashirikisha wananchi ili kuwatuliza.

  3. Kwa upande wa Iraq: Marekani inaiongoza Iraq karibu moja kwa moja kutoka nyuma ya pazia. Idadi ya wafanyakazi wa ubalozi wake mjini Baghdad inafikia 16,000 wanaofuatilia kazi za wizara zote za Iraq, hasa mafuta na sekta ya usalama. Ni ubalozi mkubwa zaidi wa Marekani duniani, na ina kambi nyingi za kijeshi nchini Iraq, maarufu zaidi ikiwa ni kambi ya Ain al-Asad mkoani Anbar... Katika wiki ya mwisho ya mwezi uliopita, Marekani ilizidisha ujumbe wake, ambapo kulikuwa na ziara ya ghafla ya Makamu wa Rais wa Marekani Pence mnamo 23/11/2019 katika kambi ya Ain al-Asad. Kabla ya wiki kupita tangu ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani nchini Iraq, Marekani ilimtuma Mkuu wa Majeshi ya Marekani, Mark Milley, mjini Baghdad tarehe 27/11/2019. Huu ni ushahidi wa ufuatiliaji wa karibu wa Marekani, hasa kwa vile Iraq kwa Marekani ni jambo nyeti kwani iliikalia kwa mabavu na kudai kuwa inaiongoza kuelekea maendeleo, lakini ikaipeleka kwenye machafuko na kusambaratika... Sasa iko katika migogoro inayofuatana na haizuiliki kuwa ikiwa hali haitatulia hivi karibuni, Marekani inaweza kuleta mabadiliko kupitia "jeshi" na kuwashirikisha wananchi nao katika utawala kwa namna ilivyofanya nchini Misri au Sudan... Imeonekana kuwa Kikosi cha Kupambana na Ugaidi nchini Iraq, ambacho ni nguvu kubwa ya kijeshi iliyoundwa na Wamarekani na kupewa vifaa bora zaidi vya kijeshi, kiko mbali na siasa za ukandamizaji wa maandamano. Inaonekana kuwa waandamanaji katika uwanja wa Tahrir wanakitazama kikosi hiki kama mkombozi kutoka kwa wanasiasa wafisadi ambapo wanainua picha kubwa ya Jenerali Abdul-Wahab al-Saadi, mmoja wa makamanda wa kikosi hicho baada ya Abdul-Mahdi kumfuta kazi. Inaonekana kikosi hiki kinakubalika na waandamanaji ili kiwe na nafasi katika kupanga suluhu... Hii ni kwa upande mmoja, na kwa upande mwingine, mikutano ya kijeshi inayofanywa na Marekani mjini Baghdad, na kutuma wajumbe wake kwa ajili hiyo pamoja na harakati za ubalozi wake mkubwa mjini Baghdad, yote haya hayakosi mipango inayofanywa na Marekani inapohitajika...

Hata hivyo, kujiuzulu kwa Abdul-Mahdi na kuteuliwa kwa rais mpya hakuathiri jambo hilo kwani hili halitatui tatizo bali ni la muda, yaani jeraha linabaki wazi hadi lipone!

Kwa vyovyote vile, harakati za umma katika nchi hizi tatu zina mambo yanayozisaidia na mengine yanayozirudisha nyuma. Ama yanayozisaidia ni kwamba harakati zake ni za hiari, na bado ziko hivyo kwa kiasi kikubwa... Ama yanayozirudisha nyuma ni kwamba hadi sasa hazijajipatia uongozi wenye ikhlasi kwa Allah (swt) na mkweli kwa Mtume wake (saw) utakaowaangazia njia ya utawala wa Kiislamu, Khilafah ya kweli iliyoongoka (Rashidah)... Ikiwa harakati hizi zitaendelea bila uongozi wenye ikhlasi na kisha kuelekea pasipo na uongofu, basi jitihada zao na dhabihu zao zitapotea bure, na harakati wakati huo zitakuwa kama yule mwanamke aliyekatilia mbali nyuzi zake alizozisokota baada ya kuwa madhubuti! Na Allah ndiye Muongozaji kwenye njia iliyonyooka.

7 Rabi’ al-Akhir 1441 H Sawia na 04/12/2019 M.

Share Article

Share this article with your network