Swali:
Taarifa ya pamoja ya Saudi, Iran, na China ilitolewa mnamo 2023/3/10 kuhusu kufikiwa kwa makubaliano ya kurejesha uhusiano kati ya Saudi Arabia na Iran na kufungua balozi ndani ya muda wa miezi miwili. Ili kuthibitisha makubaliano hayo, Mfalme wa Saudi mnamo 2023/3/19 alimualika Rais wa Iran kutembelea Saudi Arabia. Mazungumzo hayo yalifanyika kwa uenyeji na usimamizi wa China. Msimamo wa Marekani kuhusu makubaliano hayo ulikuwa wa chanya na kuukaribisha. Wakati huo huo, dola ya Kiyahudi ilionyesha kusononeka sana kufuatia hatua hiyo. Kwa nini China ilichukua jukumu hili na ni nani aliyeisukuma kufanya hivyo, na maslahi yake ni nini? Kwa nini Marekani yenyewe haikuchukua jukumu hili, na je, jambo hili linapingana na maslahi yake au lilifanyika kwa niaba yake? Na kwa nini kuna kusononeka huku kote kutoka kwa dola ya Kiyahudi kuelekea makubaliano haya? Mwenyezi Mungu akulipe kheri.
Jibu:
Ili kuweka wazi jibu la maswali yaliyotajwa hapo juu, tunapitia mambo yafuatayo:
1- Shirika la Habari la Saudi (SPA) lilichapisha mnamo 2023/3/10 taarifa ya pamoja iliyofikiwa kati ya Saudi na Iran, likieleza kuwa "pande hizo mbili zimekubaliana kurejesha uhusiano wa kidiplomasia kati yao na kufungua tena balozi na ofisi zao za uwakilishi ndani ya muda usiozidi miezi miwili." Walikubaliana "kuheshimu mamlaka ya nchi na kutoingilia masuala yao ya ndani, na kuamsha ushirikiano wa usalama uliotiwa saini kati yao mwaka 2001, pamoja na kuamsha makubaliano ya jumla ya ushirikiano katika nyanja za uchumi, biashara, uwekezaji, teknolojia, sayansi, utamaduni, michezo na vijana yaliyotiwa saini mwaka 1998. Makubaliano hayo yalijumuisha kufanyika kwa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Saudi na Iran ili kutekeleza hatua hizo, kuratibu ubadilishanaji wa mabalozi na kujadili njia za kuimarisha uhusiano kati yao."
Vilevile, ilielezwa katika taarifa hiyo ya pamoja kuwa "Saudi Arabia na Iran zinashukuru Iraq na Oman kwa kuwa wenyeji wa mazungumzo kati ya pande hizo mbili katika miaka ya 2021-2022." Ili kuimarisha na kuthibitisha makubaliano hayo, Mohammad Jamshidi, Msaidizi wa Kisiasa wa Rais wa Iran, alitangaza kupitia akaunti yake ya Twitter mnamo 19/3/2023 kuwa ("Rais Ebrahim Raisi amepokea mwaliko kutoka kwa Mfalme wa Saudi kutembelea Ufalme huo"... "na Raisi amekaribisha mwaliko huo"). Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, alisema kuwa ("Katika kipindi cha siku kumi zilizopita, tumebadilishana ujumbe kupitia Uswisi, na mmoja wa ujumbe huo ulitangaza utayari wa Iran kuhudhuria mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje na kupendekeza maeneo matatu ya kufanyia mkutano huo"). Aliashiria njia ambayo makubaliano hayo yalifikiwa, akisema "Tehran na Riyadh zilishiriki katika mizunguko mitano ya mazungumzo katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad, na mizunguko mitatu katika mji mkuu wa Oman, Muscat. Kisha Rais wa China alichukua uamuzi wa kutoa mpango wa kusukuma mchakato huu mbele, ambao ulizaa matokeo mnayoyajua." Alipoulizwa kuhusu Yemen, alisema: "Tunachukulia kama suala linalohusu watu wa Yemen, bila shaka lengo la amani katika eneo hilo lilikuwa sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa kati ya Iran na Riyadh"... Shirika la Habari la Tasnim la Iran, 2023/3/19). Pamoja na hayo, gazeti la The Wall Street Journal liliwanukuu maafisa wa Marekani na Saudi wakisema ("Iran imekubali kusitisha usafirishaji wa siri wa silaha kwa Wahouthi chini ya makubaliano yaliyopatanishwa na China"... BBC, 2023/3/19). Shirika la Habari la Iran (IRNA) lilikuwa limeeleza mnamo 2023/3/11 kwamba "upatanishi huu utaharakisha usitishaji vita na kusaidia kuanza kwa mazungumzo ya kitaifa na kuundwa kwa serikali ya kitaifa inayojumuisha wote nchini Yemen." Kisha Waziri wa Mambo ya Nje wa Yemen, Ahmed Awad bin Mubarak alisema ("Tunatumai kuwa makubaliano ya Saudi na Iran yatatengeneza hatua nzito ya uhusiano katika eneo hili itakayohitimisha uingiliaji kati wa Tehran katika masuala ya nchi za eneo hilo." Tovuti ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Yemen, 2023/3/17). Kwa hivyo, inabainika kuwa mazungumzo yalikuwa yameiva nchini Iraq na Oman hapo awali katika miaka ya 2021-2022, lakini utiaji saini haukufanyika katika nchi yoyote kati ya hizo, bali Beijing ndiyo ilikuwa sehemu ya utiaji saini!
2- Kutokana na hayo, ilielezwa pia katika taarifa hiyo ya pamoja: "Katika kipindi cha kuanzia Machi 6 hadi 10, 2023, mazungumzo yalifanyika Beijing kati ya jumbe za Saudi na Iran, ikiwa ni kuitikia mpango mwema wa Rais wa China Xi Jinping kwa uungaji mkono wa China kukuza uhusiano wa ujirani mwema kati ya Saudi na Iran. Makubaliano hayo yalifikiwa kulingana na makubaliano kati ya Rais Xi na viongozi wa Saudi na Iran kwamba China iwe mwenyeji na isimamie mazungumzo kati ya Saudi na Iran kwa hamu yao ya kutatua tofauti kupitia mazungumzo na diplomasia." China inachukulia Saudi Arabia na Iran kama washirika wake wakuu wa kibiashara, kwani imeanzisha ushirikiano wa kimkakati na kila mmoja wao; ilitia saini makubaliano kama hayo na Saudi Arabia mnamo Desemba 2022 na kutia saini na Iran makubaliano ya ushirikiano wa kibiashara na kimkakati mwaka 2020 ya muda wa miaka 25. Kutokana na hapa, mtu anaweza kuona kana kwamba China ina ushawishi juu ya nchi hizo mbili na kwamba inaweza kuzilazimisha makubaliano hayo. Lakini hali sivyo, kwani China haina nufudhi (ushawishi) wala nguvu katika Mashariki ya Kati, na haina uzoefu wa muda mrefu katika eneo hilo wala katika upatanishi wa kimataifa; na hii ni mara yake ya kwanza kufanya upatanishi kati ya nchi mbili katika Mashariki ya Kati. Inaeleweka kutokana na taarifa hiyo kuwa Saudi na Iran ndizo zilizoiomba China kufanya upatanishi kati yao (kwa hamu yao ya kutatua tofauti kupitia mazungumzo na diplomasia) kama ilivyoelezwa wazi katika taarifa hiyo! Mazungumzo kati yao yalikuwa yameiva katika miaka miwili iliyopita tangu Aprili 2021 wakati Iraq ilipokuwa mwenyeji wa mizunguko ya kwanza ya mazungumzo chini ya utawala wa Waziri Mkuu wa zamani wa Iraq, Mustafa al-Kadhimi, ambaye alikuwa mfuasi wa Marekani na alikuwa na uhusiano mzuri na pande zote mbili. Kisha Oman ikakaribisha mizunguko mingine, hivyo iliwezekana kutangazwa kwa makubaliano hayo iwe nchini Iraq au Oman, lakini yalitokea China!
3- Kuhusu kwa nini hili lilitokea, inaonekana kuwa Marekani, kwa njia ya hadaa, imeipa China jukumu la kukamilisha upatanishi na kutangaza makubaliano baada ya mazungumzo kuiva huko Baghdad na Muscat kwa sababu zifuatazo:
a- Kwa sababu Marekani haina uhusiano wa kidiplomasia na Iran, na pia haitaki kuonekana kama imeridhika na Iran, bali inajionyesha kuwa ni adui wake. Haitaki kuonyesha kuwa Iran inafuata mzunguko wake na kuitumikia katika sera mbalimbali kama walivyokiri maafisa wa Iran.
b- Inataka kuifanya China ijione ina deni kwake kwa kuifanya itekeleze kazi ya kimataifa, ili ya mwisho ijidanganye kuwa itakuwa dola kuu duniani. Kisha Marekani itaihadaa kwa kuitumia katika kazi maalum kama ilivyoitumia Urusi katika suala la Syria na masuala mengine.
c- Kuashiria kwa China kwamba ikiwa inataka kuwa dola yenye ushawishi duniani, lazima ielewane na kushirikiana nayo na siyo na Urusi. Marekani inatumia ushawishi huo kama silaha dhidi ya China ikiwa itataka kukaidi sera zake, kwa kuinyima ushawishi wa kimataifa na kuizingira kama ilivyofanya kwa Urusi.
d- Marekani ilikuwa nyuma ya ombi la Saudi na Iran kwa China kusimamia makubaliano haya na kuyatia saini, ili Marekani isionekane inaendesha makubaliano haya moja kwa moja, bali China ionekane kuwa nyuma yake. Marekani inataka kwa kufanya hivyo kupata malengo mawili kwa jiwe moja:
Kwanza: Kufelisha mpango wa Mayahudi wa kuhalalisha uhusiano (normalization) na Saudi Arabia na kuishambulia Iran, jambo ambalo lingeiweka Marekani katika wakati mgumu wa kuwaunga mkono Mayahudi kutokana na ushawishi wa kundi la shinikizo la Kiyahudi nchini Marekani (Jewish Lobby), wakati Marekani ikiwa imetingwa na vita vya Urusi na Ukraine.
Pili: Kuonyesha kuwa China ndiyo inayosimamia makubaliano haya na si Marekani kutaizuia Lobby ya Kiyahudi kumpinga Biden wakati wa uchaguzi wa mwaka ujao, hasa kwa kuwa makubaliano haya yalikuwa pigo kubwa kwa dola ya Kiyahudi na yaliisababishia kusononeka. Hivyo, Marekani inaonekana haiko nyuma ya makubaliano haya, bali ni China! Hili halitoi sababu kwa Lobby ya Kiyahudi kuchochea harakati za ufanisi za uchaguzi dhidi ya Biden, au angalau kufanya hivyo kwa ufanisi mdogo.
4- Ama kuhusu kwa nini dola ya Kiyahudi imesononeka na makubaliano haya, ni kwa sababu yamefelisha kile ambacho dola hiyo ilikuwa ikipanga. Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa dola ya Kiyahudi, Netanyahu, alikuwa akizuru Italia na kupigia debe kuhalalisha uhusiano na Saudi, akashitukizwa na kuhalalishwa kwa uhusiano kati ya Saudi na Iran. Alipoteza mwelekeo na hadi sasa hajashindwa kutoa tamko lolote kuhusu makubaliano hayo, kwani lilikuwa pigo zito usoni mwake, na wizara yake ya mambo ya nje ilikataa kutoa maoni... Wachambuzi wa Kiyahudi waliona kuwa ukaribu wa Saudi na Iran ni pigo kwa (Israel) na waliuona kama kikwazo cha kuhalalisha uhusiano kati ya dola ya Kiyahudi na Saudi, na ni ujumbe kwa (Israel) kwamba hairuhusiwi kuishambulia Iran. (Magazeti na vyombo vya habari vya Israel vilijadili makubaliano ya Saudi na Iran, ambapo yalionekana kama pigo kwa Israel na kikwazo kwa matarajio ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ya kupanua mzunguko wa kuhalalisha uhusiano... Kabla ya kutangazwa rasmi kwa makubaliano — kwa upatanishi wa China — yanayofungua njia ya kurejea kwa uhusiano kati ya Riyadh na Tehran, kulikuwa na matamshi ya Netanyahu kutoka mji mkuu wa Italia, Roma, ambapo alieleza nia yake ya kuendeleza juhudi za kufikia lengo la serikali yake la kuhalalisha uhusiano kati ya Tel Aviv na Riyadh, kupitia ujenzi wa reli ya Hijaz na kuunganisha Haifa na Saudi Arabia kwa mradi wa treni kupitia Jordan... Al Jazeera, 2023/3/13). Serikali ya Netanyahu ilikuwa ikitegemea kuhalalisha uhusiano na Saudi na kuchochea uadui dhidi ya Iran na kuikabili Iran, ikihamasisha kuishambulia, huku Marekani ikikataa yote hayo. Ziara za maafisa wa Marekani hivi karibuni katika dola ya Kiyahudi zilikuwa katika mkondo huu, kutokana na "uasi" wa serikali ya Netanyahu dhidi ya utawala wa Marekani unaoongozwa na Wanachama wa Democratic. Netanyahu alichukulia kuhalalisha uhusiano na Saudi kama mafanikio yake makubwa zaidi na serikali yake, ambapo kuhalalisha huku kungekuwa ni ridhaa isiyo ya moja kwa moja kutoka kwa Saudi kwa kile ambacho Mayahudi wanakifanya Palestina na dhidi ya Iran. Tulifafanua yote hayo katika jibu la swali la tarehe 2023/3/10 lenye kichwa "Malengo ya ziara za maafisa wa kijeshi wa ngazi za juu wa Marekani katika dola ya Kiyahudi".
Hivyo basi, makubaliano haya yamesababisha kusononeka kwa Netanyahu na kuyaona kama jambo baya kwa dola yake (Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje na Usalama katika Knesset, Yuli Edelstein, alisema: "Iran na Saudi Arabia sasa zimekubaliana kurejesha uhusiano kati yao, na hili ni jambo baya sana kwa Israel na kwa ulimwengu wote huru... Al Jazeera, 2023/3/11). Bila shaka Netanyahu anajua ndani ya nafsi yake kuwa Marekani ndiyo iko nyuma ya makubaliano haya, lakini pia anatambua kuwa dola yake haiwezi kusimama bila (kamba kutoka kwa watu) na kamba hiyo kwa sasa ni Marekani, na ndiyo maana alinyamaza! Alitaka kuizuru Washington ili kujadili mambo haya, lakini alikataliwa! Ripoti zilieleza kuwa Netanyahu anafanya shinikizo hili kutokana na Rais wa Marekani Biden kumtenga, na kukataa kumwalika hadi sasa kutembelea Ikulu ya White House, na pia kukataa maombi ya Netanyahu ya mara kwa mara ya kuizuru Washington ambayo yamekuwa yakikataliwa kila mara. (Na kwamba Benjamin Netanyahu amekuwa akifanya kazi kwa wiki kadhaa kuratibu ziara ya Washington ili kuwa mgeni katika Ikulu ya White House, lakini maombi yake ya mara kwa mara yamekataliwa... Al-Masry Al-Youm, 2023/3/15). Hata mmoja wa mawaziri wake alipopoteza udhibiti wa hisia zake baada ya matamshi ya Biden akikosoa marekebisho ya mahakama, waziri huyo alisema: "Sisi siyo nyota nyingine katika bendera ya Marekani." Ofisi ya Netanyahu ilijibu ikisema: (Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel imeeleza kuwa Benjamin Netanyahu amewaagiza mawaziri katika serikali yake kutotoa maoni kuhusu matamshi ya Rais wa Marekani Joe Biden aliyoyataka ya kuachana na marekebisho ya mahakama... Na Netanyahu alisisitiza kuwa muungano wa Israel na Marekani ni imara na hautikisiki. Al Jazeera 2023/3/29)
Hivyo inabainika sababu ya kusononeka kwa Mayahudi kutokana na makubaliano ya Saudi na Iran, kisha sababu ya kunyamaza kwa dola ya Kiyahudi kufuatia kukataa kwa Biden kumkaribisha.
5- Kuhusu Marekani, imekaribisha makubaliano hayo. Msemaji wa Ikulu ya White House, Karine Jean-Pierre, alisema: ("Tunafahamu ripoti kuhusu makubaliano kati ya Iran na Saudi, na kwa ujumla tunakaribisha juhudi zozote za kusaidia kumaliza vita nchini Yemen na kupunguza mvutano katika eneo la Mashariki ya Kati. Hii ni moja ya sababu zilizomfanya Rais Biden kusafiri kwenda eneo hilo wakati wa majira ya joto yaliyopita kufanya mazungumzo").
Aliongeza: "Kupunguza mivutano na diplomasia pamoja na uzuiaji (deterrence) ni nguzo kuu za sera iliyowekwa na Rais Biden wakati wa ziara yake katika eneo hilo mnamo Julai iliyopita. Hivyo kusitisha kuongezeka kwa mvutano Mashariki ya Kati ni kipaumbele na anakaribisha hilo"... CNN ya Marekani, 2023/3/11). John Kirby, mratibu wa mawasiliano katika Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani, alisema ("Wasaudi waliijulisha Washington kuhusu mawasiliano yao na Wairani lakini Marekani haikuwa na jukumu katika makubaliano hayo..." na akasema "Watu hawajali upatanishi wa China katika makubaliano hayo, hasa kwa kuwa ni upatanishi katika mgogoro mmoja na unaendana na matakwa ya Washington ya kutuliza Mashariki ya Kati"... Al-Khaleej Online, Al Jazeera, 2023/3/11). Kauli ya afisa wa Marekani kuwa Marekani haikuwa na jukumu katika makubaliano hayo inapingana na kauli yake kuwa Marekani ilikuwa ikiwasiliana na Wasaudi na kwamba jukumu la China linaendana na matakwa ya Marekani ya kutuliza hali ya mambo! Alitaka kuficha jukumu la Marekani lakini alijianika mwenyewe alipojigonga katika matamshi yake. Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani, Jake Sullivan, alithibitisha mnamo 2023/3/14 kuwa (Wasaudi walikuwa katika mawasiliano ya mara kwa mara na utawala wa Biden "wakati wa mazungumzo na makubaliano na Iran" na akasema "Washington inachukulia kuwa ni makubaliano chanya ya kusitisha mivutano katika eneo hilo na yamekuja kwa upatanishi wa China kwa sababu uhusiano wa Marekani na Iran hauko katika hali inayoiruhusu Marekani kupatanisha kutatua tofauti"... Al-Khaleej Online, 2023/3/16). Vilevile, chaneli ya "Al-Arabiya" ya Saudi ilinukuu mnamo 2023/3/16 kutoka kwa afisa wa Saudi kuwa "Ufalme wa Saudi Arabia uliwajulisha washirika wake ikiwemo Marekani kabla ya kutia saini Beijing makubaliano na Iran"... Hii inaongezea kile kilichonukuliwa na Al-Khaleej Online mnamo 2023/3/17 ikichapisha matamshi ya maafisa wa Marekani kuwa "kuna mazungumzo katika korido za siasa za Iraq kwamba Marekani ndiyo iliyoisukuma Riyadh kuharakisha makubaliano hayo." Hata kuna baadhi ya Wairani, wanasiasa, watu wenye habari na wataalamu wanaoelewa mchezo huo; tovuti ya "Middle East News" ya Iran ilinukuu mnamo 2023/3/21 kutoka tovuti ya "Fararu" ya Iran mahojiano yaliyofanywa na tovuti hiyo na Mahdi Motaharnia, profesa wa sayansi ya siasa na mtaalamu wa sera za kigeni akisema: "Hatua za hivi karibuni za China katika mfumo wa upatanishi kati ya Iran na Saudi Arabia zinahusiana na dhana ya makutano ya nguvu za kimataifa... kama mchambuzi siwezi kukubali wazo kwamba Wachina kwa mfano wanaweza kuchukua hatua ya mmoja mmoja kama hii bila uratibu na wanachama wenye ufanisi katika makutano ya nguvu za kimataifa kwa lengo la kupunguza mivutano kati ya Iran na Saudi Arabia." Anakusudia wanachama wenye ufanisi kuwa ni Marekani, kwani ndiyo mtekelezaji mkuu katika nyanja ya kimataifa na ndiyo mwenye ushawishi mkuu Mashariki ya Kati.
Yote haya yanathibitisha kuwa Marekani ndiyo iliyotaka makubaliano haya na ilitaka China iwe mpatanishi, na kwamba iko nyuma ya ombi la Iran na Saudi kwa China kusimamia makubaliano na utiaji saini.
6- Hivi ndivyo nchi za eneo hili zinavyofichuka na kuwa uchi kwa kufuata sera zilizopangwa kwa ajili yao na Marekani ambayo inashikilia hatamu za mambo, pindi inapowaomba washirika wake, iwe ni wafuasi wake au wale wanaofuata mzunguko wake, kuelewana na kutatua matatizo kati yao, wao hutekeleza kwa kutayarisha mazungumzo; na ikiwa itawaomba kinyume chake kwa kutengana au uadui, hufanya hivyo na kutengeneza sababu zake. Bila ya hivyo, Marekani isingeweza kufanya chochote katika eneo hili. Njia ya kujikwamua nayo ni kupitia kuangusha tawala hizi, na kisha kufanya kazi ya kusimamisha mfumo unaomridhisha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na Waumini, ambao utawaunganisha Waislamu katika dola moja, nao ni mfumo wa Khilafah kwa njia ya Utume ambayo Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Ta’ala ameahidi:
وَعَدَ اللَّهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنْكُمْ وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَيَسْتَخْلِفَنَّهُمْ فِي الْأَرْضِ كَمَا استَخْلَفَ الَّذِينَ مِنْ قَبْلِهِمْ
"Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na wakatenda mema, kwamba atawafanya makhalifa katika ardhi kama alivyowafanya makhalifa wale wa kabla yao." (QS. An-Nur [24]: 55)
Na akaitolea bishara Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ:
ثُمَّ تَكُونُ خِلَافَةً عَلَى مِنْهَاجِ النُّبُوَّةِ
"Kisha kutakuwepo na Khilafah kwa njia ya Utume." (Imepokelewa na Ahmad) - Kisha akanyamaza.
10 Ramadhan 1444 H 2023/4/1 M