Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Waqf katika Ardhi ya Kharaj

December 23, 2019
3651

Silsila ya Majibu ya Mwanachuoni Mheshimiwa Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Wageni kwenye Ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi"

Kwa Yusuf Abu Islam

Swali:

Barakallahu fika na Mwenyezi Mungu atunufaishe kwa elimu yako. Lakini Sheikh wetu, nina maswali mawili ukitukirimia: Kwanza: Ni upi ushahidi wa kwamba katika waqf inashartiwa mwenye kutoa waqf awe anamiliki dhati ya kile anachokitoa waqf? Pili: Je, kuna hukumu nyingine kando na waqf zinazotofautisha katika utendaji kwenye ardhi kati ya kuwa ni ya 'Ushri au Kharaji? Mwenyezi Mungu atubariki sisi na Hizb yetu katika umri wako na afya yako, na afungue kheri kupitia mikono yako.

Jibu:

Wa Alaykum Salaam Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh,

Kwanza: Suala la waqf katika ardhi ya Kharaj lina khilaf (utofauti wa kifikra) miongoni mwa mafaqihi:

1- Kuna miongoni mwao wanaojuzisha waqf katika yale yanayojengwa juu yake kama majengo au mimea. Hivyo, ikiwa mtu atajenga shule juu ya ardhi ya Kharaj anayoimiliki, inajuzu kwake kuifanya shule hiyo kuwa waqf kwa ajili ya wanafunzi... au ikiwa atapanda mizeituni kwa mfano, inajuzu kwake kuifanya matunda yake kuwa waqf kwa ajili ya mafukara na wahitaji, mradi tu waqf huu uwe wa kudumu:

Imekuja katika Al-Mawsu'ah al-Fiqhiyyah al-Kuwaitiyyah: [Ibn Abidin amepokea kutoka kwa Al-Khassaf kwamba amesema: (Hakika waqf ya maduka ya masokoni inajuzu ikiwa ardhi iko mikononi mwa wale waliojenga kwa kukodisha ambapo Sultani hawaondoi kwayo, kwa sababu tumeona iko mikononi mwa wamiliki wa majengo wakirithiana na kugawana miongoni mwao bila Sultani kuwaingilia wala kuwahamisha, isipokuwa tu anachukua mapato kutoka kwao na wanarithiana kizazi baada ya kizazi, na kupita zama nyingi huku ikiwa mikononi mwao wakiiuziana, kuikodisha, na inajuzu katika wasia wao, na wanabomoa majengo yake na kuyajenga upya, na kujenga mengineyo, basi kadhalika waqf inajuzu). Ibn Abidin amesema: Na akaidhinisha hilo katika Al-Fath na sababu yake ni kubakia kwa udumishaji.

Na ikiwa kile alichoweka katika ardhi ni mimea, basi hukumu ya waqf yake ni sawa na hukumu ya jengo. Ama ikiwa kile alichofanya katika ardhi ni kuongeza tu udongo au mbolea, basi waqf yake haisihi.] Mwisho.

2- Na kuna miongoni mwao wanaojuzisha waqf ya manufaa hata ikiwa ni kwa muda, hivyo ikiwa mtu atakodisha nyumba kwa muda wa mwaka mmoja, inajuzu kwake kuifanya nyumba hiyo kuwa waqf kwa ajili ya wahitaji kwa muda wa mwaka huo uliotajwa katika mkataba wa upangaji... au kukodisha shamba la mimea kwa muda wa kuisha kwa mavuno na akalifanya waqf kwa wahitaji kwa muda wa mavuno hayo kulingana na mkataba wa upangaji. Yaani, anajuzisha waqf ya manufaa na si sharti iwe ya kudumu bali hata ya muda pia:

Imekuja katika Al-Mawsu'ah al-Fiqhiyyah al-Kuwaitiyyah: [Jamhuri ya mafaqihi wa Hanafi, Shafi'i, na Hanbali wameelekea kwenye kutokujuzu kwa waqf ya manufaa kwani wanashartiwa kuwa kitu kinachowekwa waqf kiwe ni dhati ya kitu kinachonufaisha huku dhati yake ikibaki, kama vile wanavyoshartia udumishaji wa waqf (1)... Na Maliki wameelekea kwenye kujuzu kwa waqf ya manufaa, hivyo yeyote aliyekodisha nyumba kwa muda maalumu inajuzu kwake kuweka waqf manufaa yake katika muda huo, na waqf itaisha kwa kuisha kwa muda huo, kwa sababu kwao haishartiwi udumishaji wa waqf (2)...

(1) Mughni al-Muhtaj 2/377, na Sharh Muntaha al-Iradat 2/492, na al-Bada'i 6/220, na Hashiyat Ibn Abidin 3/359... (2) al-Sharh al-Kabir na Hashiyat al-Dasuqi juu yake 4/76, na al-Sharh al-Saghir 2/298 chapa ya Al-Halabi.] Mwisho.

Pili: Na kuna maoni yenye nguvu zaidi (al-rajih) kwamba waqf haijuzu isipokuwa ikiwa shingo ya ardhi (raqabah) inamilikiwa na mwenye kutoa waqf na iwe kwa namna ya kudumu, na hili ndilo tunalolipendekeza katika suala hili kulingana na dalili sahihi katika maudhui haya, na hapa kuna ufafanuzi:

1- Imekuja katika Sharh al-Maddah 133 ya Muqaddimat al-Dustur, sehemu ya pili yafuatayo:

(Ardhi ya 'Ushri na Kharaji ina haki ya kubadilishana na kurithiwa kutoka kwa mmiliki wake kwa sababu ni milki ya kweli ya mmiliki wake, hivyo inatumika kwake hukumu zote za milki. Na hili kwa upande wa ardhi ya 'Ushri liko wazi, ama kwa upande wa ardhi ya Kharaji, milki yake ni kama milki ya ardhi ya 'Ushri sawasawa kwa upande wa umiliki, na hakuna tofauti kati yake isipokuwa katika mambo mawili pekee: moja ni kwa upande wa dhati ya kile kinachomilikiwa, na la pili ni kwa upande wa kile kinachowajibika juu ya ardhi.

Ama kwa upande wa dhati ya kile kinachomilikiwa, mmiliki wa ardhi ya 'Ushri anamiliki shingo yake (raqabah) na manufaa yake, na mmiliki wa ardhi ya Kharaji anamiliki manufaa yake pekee na hamiliki shingo yake. Inatokana na hili kwamba mmiliki wa ardhi ya 'Ushri akitaka kuweka waqf ardhi yake anayoimiliki, anaweza kufanya hivyo wakati wowote anaotaka, kwa sababu anamiliki dhati yake yaani shingo yake. Ama mmiliki wa ardhi ya Kharaji akitaka kuweka waqf ardhi yake anayoimiliki, hawezi kufanya hivyo, kwa sababu waqf inashartiwa ndani yake mwenye kutoa waqf awe mmiliki wa dhati ya kile anachoweka waqf, na mmiliki wa ardhi ya Kharaji hamiliki dhati ya ardhi yaani shingo yake bali anamiliki manufaa yake tu, kwa sababu shingo yake ni milki ya Baitul Mal.

Ama kwa upande wa kile kinachowajibika juu ya ardhi, ardhi ya 'Ushri inawajibika ndani yake 'Ushr (moja ya kumi) au nusu ya 'Ushr, yaani inawajibika ndani yake Zaka juu ya dhati ya kile kinachotoka ikiwa kimefikia nisabu. Ama ardhi ya Kharaji inawajibika ndani yake Kharaj, yaani kiasi ambacho dola inakipanga kila mwaka juu yake...) Mwisho. Na kama unavyoona, waqf haijuzu katika ardhi ya Kharaji kwa sababu waqf inashartiwa umiliki wa shingo ya ardhi, na ardhi ya Kharaji shingo yake ni ya Baitul Mal, hivyo mmiliki wake hamiliki bali anamiliki manufaa yake.

2- Tayari tulishatoa jibu la swali mnamo 13/02/2019 kuhusu mada hii, na huenda unaliashiria katika swali lako, ambapo ilikuja: (... kwa mfano waqf sharti katika usahihi wake ni umiliki wa dhati ya kitu kinachowekwa waqf, na hivyo mmiliki wa ardhi ya 'Ushri akitaka kuiweka waqf ardhi yake anayoimiliki, anaweza kufanya hivyo wakati wowote anaotaka, kwa sababu anamiliki dhati yake yaani shingo yake. Ama mmiliki wa ardhi ya Kharaji akitaka kuiweka waqf ardhi yake anayoimiliki, hawezi kufanya hivyo, kwa sababu mwenye kutoa waqf anashartiwa kuwa mmiliki wa dhati ya kile anachoweka waqf, na mmiliki wa ardhi ya Kharaji hamiliki dhati ya ardhi yaani shingo yake bali anamiliki manufaa yake tu, kwa sababu shingo yake ni milki ya Baitul Mal.) Mwisho.

3- Ama dalili za kushartiwa umiliki wa shingo (raqabah - asili ya manufaa) kwa ajili ya usahihi wa waqf ni pamoja na zifuatazo:

  • Al-Bukhari amepokea katika Sahih yake kutoka kwa Ibn Umar (ra):

أَنَّ عُمَرَ بْنَ الْخَطَّابِ أَصَابَ أَرْضاً بِخَيْبَرَ فَأَتَى النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم يَسْتَأْمِرُهُ فِيهَا فَقَالَ يَا رَسُولَ اللَّهِ إِنِّي أَصَبْتُ أَرْضاً بِخَيْبَرَ لَمْ أُصِبْ مَالاً قَطُّ أَنْفَسَ عِنْدِي مِنْهُ فَمَا تَأْمُرُ بِهِ قَالَ: «إِنْ شِئْتَ حَبَسْتَ أَصْلَهَا وَتَصَدَّقْتَ بِهَا» قَالَ فَتَصَدَّقَ بِهَا عُمَرُ أَنَّهُ لَا يُبَاعُ وَلَا يُوهَبُ وَلَا يُورَثُ وَتَصَدَّقَ بِهَا فِي الْفُقَرَاءِ وَفِي الْقُرْبَى وَفِي الرِّقَابِ وَفِي سَبِيلِ اللَّهِ وَابْنِ السَّبِيلِ وَالضَّيْفِ لَا جُنَاحَ عَلَى مَنْ وَلِيَهَا أَنْ يَأْكُلَ مِنْهَا بِالْمَعْرُوفِ وَيُطْعِمَ غَيْرَ مُتَمَوِّلٍ قَالَ فَحَدَّثْتُ بِهِ ابْنَ سِيرِينَ فَقَالَ غَيْرَ مُتأَثِّلٍ مَالاً.

"Kwamba Umar bin al-Khattab alipata ardhi huko Khaybar, akaja kwa Mtume (saw) kumtaka ushauri kwayo akasema: 'Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, nimepata ardhi huko Khaybar sijawahi kupata mali iliyo bora kwangu kuliko hiyo, basi unaniamrisha nini?' Akasema: 'Ukitaka, izuie asili yake na utoe sadaka kwayo.' Akasema: Basi Umar akaitoa sadaka kwamba haiuzwi, haitolewi zawadi, wala hairithiwi, na akaitoa sadaka kwa mafukara, jamaa wa karibu, katika kukomboa watumwa, katika njia ya Mwenyezi Mungu, msafiri, na mgeni, hakuna dhambi kwa anayeisimamia kula kwayo kwa wema na kulisha wengine bila kujilimbikizia mali.' Akasema: Nikamhadithia Ibn Sirin akasema: 'Bila kujichumia mali kwayo.'" (Sahih al-Bukhari)

  • Na Al-Bukhari amepokea katika Sahih yake kutoka kwa Ibn Umar (ra):

أَنَّ عُمَرَ تَصَدَّقَ بِمَالٍ لَهُ عَلَى عَهْدِ رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم وَكَانَ يُقَالُ لَهُ ثَمْغٌ وَكَانَ نَخْلاً فَقَالَ عُمَرُ يَا رَسُولَ اللَّهِ إِنِّي اسْتَفَدْتُ مَالاً وَهُوَ عِنْدِي نَفِيسٌ فَأَرَدْتُ أَنْ أَتَصَدَّقَ بِهِ فَقَالَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم «تَصَدَّقْ بِأَصْلِهِ لَا يُبَاعُ وَلَا يُوهَبُ وَلَا يُورَثُ وَلَكِنْ يُنْفَقُ ثَمَرُهُ» فَتَصَدَّقَ بِهِ عُمَرُ فَصَدَقَتُهُ تِلْكَ فِي سَبِيلِ اللَّهِ وَفِي الرِّقَابِ وَالْمَسَاكِينِ وَالضَّيْفِ وَابْنِ السَّبِيلِ وَلِذِي الْقُرْبَى وَلَا جُنَاحَ عَلَى مَنْ وَلِيَهُ أَنْ يَأْكُلَ مِنْهُ بِالْمَعْرُوفِ أَوْ يُوكِلَ صَدِيقَهُ غَيْرَ مُتَمَوِّلٍ بِهِ.

"Kwamba Umar alitoa sadaka ya mali yake katika zama za Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (saw), na ilikuwa ikiitwa Thamgh na ilikuwa ni mitende, Umar akasema: 'Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, nimepata mali nayo kwangu ni bora, basi nilitaka kuitoa sadaka.' Mtume (saw) akasema: 'Toa sadaka ya asili yake, haiuzwi wala haitolewi zawadi wala hairithiwi, lakini unatumika mmea wake (matunda yake).' Basi Umar akaitoa sadaka hiyo katika njia ya Mwenyezi Mungu, katika kukomboa watumwa, maskini, mgeni, msafiri, na kwa wenye ujamaa, na hakuna dhambi kwa anayeisimamia kula kwayo kwa wema au kumlisha rafiki yake bila kujilimbikizia mali kwayo." (Sahih al-Bukhari)

  • Vilevile Muslim amepokea katika Sahih yake kutoka kwa Ibn Umar akisema:

أَصَابَ عُمَرُ أَرْضاً بِخَيْبَرَ فَأَتَى النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم يَسْتَأْمِرُهُ فِيهَا فَقَالَ يَا رَسُولَ اللَّهِ إِنِّي أَصَبْتُ أَرْضاً بِخَيْبَرَ لَمْ أُصِبْ مَالاً قَطُّ هُوَ أَنْفَسُ عِنْدِي مِنْهُ فَمَا تَأْمُرُنِي بِهِ قَالَ: «إِنْ شِئْتَ حَبَسْتَ أَصْلَهَا وَتَصَدَّقْتَ بِهَا» قَالَ فَتَصَدَّقَ بِهَا عُمَرُ أَنَّهُ لَا يُبَاعُ أَصْلُهَا وَلَا يُبْتَاعُ وَلَا يُورَثُ وَلَا يُوهَبُ قَالَ فَتَصَدَّقَ عُمَرُ فِي الْفُقَرَاءِ وَفِي الْقُرْبَى وَفِي الرِّقَابِ وَفِي سَبِيلِ اللَّهِ وَابْنِ السَّبِيلِ وَالضَّيْفِ لَا جُنَاحَ عَلَى مَنْ وَلِيَهَا أَنْ يَأْكُلَ مِنْهَا بِالْمَعْرُوفِ أَوْ يُطْعِمَ صَدِيقاً غَيْرَ مُتَمَوِّلٍ فِيهِ...

"Umar alipata ardhi huko Khaybar akamjia Mtume (saw) kumtaka ushauri kwayo, akasema: 'Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu nimepata ardhi huko Khaybar sijawahi kupata mali iliyo bora kwangu kuliko hiyo, basi unaniamrisha nini?' Akasema: 'Ukitaka, izuie asili yake na utoe sadaka kwayo.' Akasema: Umar akaitoa sadaka hiyo kwamba asili yake haiuzwi wala hainunuliwi wala hairithiwi wala haitolewi zawadi. Akasema: Umar akaitoa sadaka kwa mafukara, jamaa wa karibu, katika kukomboa watumwa, katika njia ya Mwenyezi Mungu, msafiri, na mgeni, hakuna dhambi kwa anayeisimamia kula kwayo kwa wema au kumlisha rafiki bila kujilimbikizia mali kwayo..." (Sahih Muslim)

Hivyo, hadithi za Mtume (saw) ziko wazi katika kubainisha waqf kwamba ni kuzuia dhati ya kitu kinachowekwa waqf na kuachia manufaa yake, na kuizuia kunapelekea kuwa iwe inamilikiwa shingo yake na yule anayeizuia yaani mwenye kutoa waqf kabla ya kuizuia na kuiweka waqf, kwa sababu asiyemiliki kitu hawezi kukizuia. Basi kuzuia kitu hakuwi isipokuwa kwa mmiliki wake kwa sababu ni utendaji katika shingo ya kitu, ikiwa shingo ya kitu si yake basi atafanyaje utendaji kwayo kwa kuizuia?... Na Umar bin Al-Khattab (ra) alikuwa mmiliki wa shingo ya kile alichoamrishwa na Mtume (saw) kukizuia kama ilivyo katika hadithi hapo juu, kwani yeye (ra): "alipata ardhi huko Khaybar akamjia Mtume (saw) kumtaka ushauri kwayo akasema: Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu nimepata ardhi huko Khaybar sijawahi kupata mali iliyo bora kwangu kuliko hiyo, unaniamrisha nini?", yaani yeye (ra) alimiliki ardhi hiyo na ikawa ardhi yake yaani alimiliki shingo yake, kisha akaja kumuuliza Mtume (saw) kuhusu namna ya kuifanyia kazi... Kwa hiyo hadithi inayoonyesha uhalali wa waqf iko wazi kuwa mwenye kutoa waqf lazima awe mmiliki wa shingo ya kitu hicho... Mtume (saw) anasema kama ilivyo katika hadithi hapo juu:

«إِنْ شِئْتَ حَبَسْتَ أَصْلَهَا...»، «تَصَدَّقْ بِأَصْلِهِ...»، «إِنْ شِئْتَ حَبَسْتَ أَصْلَهَا...»

"Ukitaka, izuie asili yake...", "Toa sadaka ya asili yake...", "Ukitaka, izuie asili yake..." Na ardhi ya Kharaji imezuiwa shingo yake kwa ajili ya Baitul Mal ya Waislamu, hivyo shingo yake si milki ya mmiliki wake, na mmiliki wake anamiliki manufaa pekee. Maadamu mmiliki wake hamiliki shingo yake kwa sababu imezuiwa kwa ajili ya Baitul Mal, atawezaje basi kuizuia shingo yake?

4- Hili ndilo tunalolipendekeza na kulifuata kwa sababu ya kuafikiana kwa dalili za kisheria juu yake, yaani haijuzu kuweka waqf ardhi ya Kharaji, bali inajuzu kuiuza, kuitoa zawadi, kuitoa sadaka yenyewe au thamani yake na vitendo vyote vinavyojuzu kisheria, isipokuwa kama tulivyosema waqf ambayo inashartia umiliki wa shingo (raqabah), nayo katika ardhi ya Kharaji shingo yake inamilikiwa na Baitul Mal.

Tatu: Ama swali lako (Je, kuna hukumu nyingine kando na waqf zinazotofautisha katika utendaji kwenye ardhi kati ya kuwa ni ya 'Ushri au Kharaji?), jibu la hilo ni kwamba hatujapata tofauti nyingine zinazohusu utendaji katika ardhi ya Kharaji na 'Ushri isipokuwa mambo mawili yaliyotajwa hapo juu; yaani kinachowajibika katika ardhi ya 'Ushri ambacho ni Zaka na katika ardhi ya Kharaji ambacho ni Kharaj, na jambo la pili ni kujuzu kwa waqf katika ardhi ya 'Ushri na kutokujuzu kwake katika ardhi ya Kharaji.

Hili ndilo lenye nguvu kwetu na tunalolifuata, na Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi zaidi na Mwenye Hekima zaidi.

Ndugu yenu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

21 Rabi’ al-Akhar 1441 H Sawia na 18/12/2019 M

Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Mungu amhifadhi) kwenye Facebook

Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Mungu amhifadhi) kwenye Wavuti

Share Article

Share this article with your network