Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Marekani na Kubadilisha Vibaraka Vyake nchini Pakistan

May 06, 2022
2874

Jibu la Swali

Marekani na Kubadilisha Vibaraka Vyake nchini Pakistan

Swali:

(Bilawal Bhutto Zardari, mwanawe Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan Benazir Bhutto, leo Jumatano ameapishwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje katika serikali ya Waziri Mkuu Shehbaz Sharif, iliyoundwa baada ya kura ya kutokuwa na imani na Imran Khan. Bhutto Zardari (mwenye umri wa miaka 33) anaongoza Chama cha Watu wa Pakistan (PPP)... Al Jazeera 27/04/2022). Serikali ya Shehbaz Sharif, ambaye alimrithi kaka yake Nawaz katika uongozi wa chama cha Muslim League, ilikuwa imeapishwa mnamo 19/04/2022, ikiwa ni zaidi ya wiki moja baada ya kuondolewa kwa Imran Khan kwa kura ya kutokuwa na imani naye. Swali ni: ni nini sababu ya mabadiliko haya? Ikizingatiwa kuwa Bunge, likiungwa mkono na jeshi, lilikuwa limempa imani Imran wakati wa kuteuliwa kwake, na wakati huo vyama vya Muslim League na PPP vilikuwa vimekataliwa na jeshi. Ni nini kipya kilichotokea? Je, Marekani ina mkono katika suala hili, ikizingatiwa kuwa imekuwa nyuma ya utawala nchini Pakistan kwa miaka mingi?

Jibu:

Ili kuweka wazi jibu la maswali haya, tunapitia mambo yafuatayo:

Kwanza: Jinsi Imran Khan alivyofika mamlakani:

1- Jeshi ndilo lililompa Khan mamlaka, na Khan aliongoza serikali iliyokuwa tiifu kwa majenerali kwa kiwango kisicho na kifani. Khan alikosolewa kwa kuwa karibu sana na jeshi tangu alipoahidi kuanzisha "Pakistan Mpya" ili kuondokana na ufisadi na upendeleo baada ya ushindi wake katika uchaguzi wa 2018. Hadi hivi karibuni, Imran Khan alikuwa akielezewa kama mmoja wa mawaziri wakuu nchini Pakistan aliyekuwa na ushirikiano wa karibu zaidi na wanajeshi, na hata kushutumiwa kwa kuwa mfuasi wao. Isingekuwa msaada wa jeshi kwake, asingepata kura ya imani! Alitangaza mnamo mwaka 1996 kuundwa kwa chama chake cha kisiasa kiitwacho "Tehreek-e-Insaf Pakistan (PTI)", na mwaka 1997 Khan alishindwa kupata hata kiti kimoja katika Bunge la Kitaifa wakati wa uchaguzi mkuu. Ni mnamo mwaka 2013 pekee ambapo chama chake kiliweza kuleta athari katika siasa za Pakistan kutokana na uungaji mkono wa jeshi la Pakistan kwake. Chama chake kiliweza kushinda viti 30 katika Bunge la Kitaifa, kikawa chama cha tatu kwa ukubwa cha upinzani baada ya vyama vya Pakistan Muslim League na Pakistan Peoples Party. Kisha jeshi liliamua kumpa Khan nafasi ya kushinda katika uchaguzi wa 2018, lakini hiyo ilikuwa baada ya Khan kukubaliana na timu ya mkuu wa jeshi Qamar Bajwa kusimamia uchaguzi mkuu.

2- Jeshi na chombo cha ujasusi chini ya usimamizi wa Luteni Jenerali Faiz Hamid vilifanya kazi bila kuchoka ili kuboresha matarajio ya kisiasa ya Khan. Ujasusi wa Pakistan ulisaidia kupanga mikutano yake nchini kote na kumfanya kuwa mgombea mshindi. Jeshi liliwashawishi wanasiasa kutoka vyama vingine kuhama vyama vyao na kujiunga na chama cha Imran Khan pamoja na wapiga kura wao. Jeshi liliitisha vyombo vya habari kutoa habari chanya kwa chama cha Insaf huku likishambulia chama cha Muslim League, ambapo vyombo vya usalama viliwakamata, kuwaweka kizuizini na kuwanyanyasa wafanyakazi wa chama cha Pakistan Muslim League - Nawaz, na jeshi lilifanya kazi nyuma ya pazia kuwazuia wagombea wa Muslim League kugombea...

3- Ingawa chama cha Khan kilipata viti 149 katika Bunge la Kitaifa, bado kilikuwa pungufu ya viti 172 vinavyohitajika kuunda serikali ya wengi. Hata hivyo, kiliweza kufanya hivyo kwa mpangilio wa jeshi ili kuunda serikali ya mseto. Serikali ya mseto ilikuwa mpango wa jeshi la Pakistan ili kuhakikisha njia ya kurudi nyuma iwapo Khan angebadili nia na kufanya kazi dhidi ya jeshi. Vilevile, chombo cha ujasusi kilifanikiwa kuwavuta wanachama kutoka chama cha Pakistan Peoples Party kuingia katika serikali ya Khan. Hivyo, jumla ya wanachama 17 wa timu ya Khan waliteuliwa kwa ushawishi wa idara ya ujasusi ya Pakistan (ISI), na wanachama watatu tu katika baraza la mawaziri ndio walikuwa wafuasi wa vuguvugu la Insaf ambao hawakuwahi kujiunga na chama kingine chochote!

Pili: Baada ya Imran kufikia uwaziri mkuu, alitoa huduma nyingi kwa Marekani:

1- Kituo cha televisheni cha Pakistan Geo TV kilimnukuu Khan akisema kuwa ("alipokea barua kutoka kwa Rais wa Marekani Trump mapema leo 03/12/2018, akiiomba Pakistan kuchukua jukumu katika mazungumzo ya amani ya Afghanistan, na kusaidia kuwaleta Taliban kwenye meza ya mazungumzo"... Sputnik ya Urusi 03/12/2018). Kisha Khan akakutana siku mbili baadaye na mjumbe maalumu wa Marekani Khalilzad huko Islamabad akisisitiza kufuata kwa Pakistan mpango wa Marekani nchini Afghanistan!

2- Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa Pakistan, Khawaja Asif, alithibitisha usaliti wa watawala wa Pakistan, naye akiwa mmoja wao, alipoandika mnamo 19/11/2018 kwenye akaunti yake ya Twitter: "Pakistan bado inatoa damu kwa ajili ya Marekani kwa sababu ya kupigana vita ambavyo si vyetu. Tuliangamiza thamani za dini yetu ili kuifanya iendane na maslahi ya Marekani na tukaharibu roho yetu ya uvumilivu na kuibadilisha na ushabiki na kutovumiliana." Hakuna maneno yaliyo wazi zaidi kuliko haya: Pakistan ilipigana vita ambavyo si vyake... na ikamwaga damu za watoto wa Kiislamu kwa ajili ya Marekani... na ikaharibu thamani za dini yake ya Uislamu ili kutumikia maslahi ya Marekani...

3- Kadhalika hali ilikuwa hivyo kwa upande wa India, kwani alifanya uzembe mbele yake na kunyamazia hatua yake ya kuunganisha Kashmir isipokuwa kwa vitendo vinavyofanana na michezo ya fataki. Tulishasema katika jibu la swali la tarehe 18/08/2019: (Na wakati India ilipotangaza uamuzi wake wa hivi karibuni wa kufuta hadhi maalum ya Kashmir, msimamo wa Pakistan ulikuwa wa kusuasua pia, haukuvuka mipaka ya kulaani ili tu kujiondolea lawama. Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan ilitoa taarifa ikisema: "Pakistan inalaani vikali na kukataa tangazo lililotolewa Jumatatu tarehe 05/08/2019 kutoka New Delhi, na kwamba hakuna hatua yoyote ya upande mmoja kutoka kwa serikali ya India inayoweza kubadilisha hali ya mgogoro huo na kama sehemu ya mgogoro huu wa kimataifa Pakistan itafanya kila iwezalo kukabiliana na hatua hizo haramu"... AFP 05/08/2019"... Yaani, kama vile mamlaka ya Abbas na nchi za Kiarabu zinazoizunguka zinavyofanya pale wanapolaani na kupinga ukiukaji wa dola ya Kiyahudi dhidi ya Al-Quds katika ardhi iliyobarikiwa ya Palestina bila kusogeza majeshi kupigana, na Pakistan inakariri jukumu lile lile kwa kulaani bila kusogeza jeshi kupigana!)

4- Alishirikiana na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), na shirika hili liko chini ya utawala wa Marekani na linatekeleza sera zake. Hii ni baada ya kutoa tamko dhidi ya kushirikiana nalo katika kampeni yake ya uchaguzi, ambapo alikuwa amesema kuwa (atapatiliza nafsi yake "nitajiua" kabla ya kuchukua mkopo kutoka IMF) kisha akarejea na kuvunja ahadi yake! Akaanza mazungumzo na IMF. Na mnamo tarehe 3 Julai 2019, IMF iliidhinisha Pakistan kupata mkopo wa dola bilioni 6 chini ya mpango wa muda wa miezi 39...

5- Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan alitamka akikumbusha huduma zao kwa Marekani katika mahojiano na kituo cha Fox News Jumatatu 22/07/2019: (kwamba ujasusi wa Pakistan uliipa Idara ya Ujasusi ya Marekani (CIA) habari iliyoiruhusu kumpata na kumuua muasisi wa Al-Qaeda Osama bin Laden. Hii ilikuwa ziara ya kwanza ya bingwa huyo wa zamani wa kriketi katika Ikulu ya Marekani tangu alipochaguliwa mwaka mmoja uliopita nchini Pakistan ambapo alikutana na Rais wa Marekani Donald Trump Jumapili... Al-Quds Al-Arabi, 23/07/2019).

Tatu: Mvutano katika uhusiano kati ya Imran na uongozi wa jeshi na kisha Marekani:

Imran Khan aliendelea kuwa mtiifu kwa uongozi wa jeshi na nyuma yake ikiwa ni Marekani kwa takriban miaka mitatu ya utawala wake. Mwishoni mwa mwaka wa tatu, uhusiano kati yake na mkuu wa jeshi Bajwa ulivunjika, na baadaye na Marekani kutokana na kuunga mkono msimamo wa jeshi... Imran alikataa kuidhinisha mgombea wa jeshi kwa nafasi ya mkuu wa ujasusi wa kijeshi (ISI), Luteni Jenerali Nadeem Anjum, na alichelewesha uteuzi huo kwa muda mrefu, jambo ambalo lilipelekea hali ya kutoridhika ndani ya jeshi... (Anjum atachukua nafasi yake mpya kuanzia Novemba 20. Na mnamo Oktoba 6 mwaka huu, Bajwa alimteua Anjum kuchukua nafasi ya mkuu wa ujasusi wa Pakistan, Luteni Jenerali Faiz Hamid. Anjum alikuwa akihudumu kama kamanda wa kikosi cha jeshi katika mji wa pwani wa kusini wa Karachi, na Bajwa alimteua Hamid kuwa kamanda wa kikosi katika mji wa Peshawar mwezi huu. Tovuti ya kituo cha Al-Manar, 27/10/2021). Na Imran Khan alikuwa akitangaza waziwazi uungaji mkono wake kwa Faiz Hamid kuendelea kuongoza usalama wa ndani. Hivyo, uhusiano wa serikali ya Imran na jeshi ulikumbwa na mivutano kufuatia kuteuliwa kwa Anjum badala ya Faiz Hamid, hasa kwa vile kulikuwa na uvumi mkubwa kwamba Khan angemteua Hamid kuchukua nafasi ya Qamar Javed Bajwa ambaye kipindi chake cha pili madarakani kinamalizika mwaka 2022. Na kwa asili, Marekani iko nyuma ya mkuu wa jeshi, na hivyo uamuzi ukachukuliwa wa kuandaa mazingira ya kura ya kutokuwa na imani na Imran Khan na kutafuta mbadala wake. Imran Khan alipata baadhi ya habari hizo na akajaribu kurekebisha mambo na uongozi wa jeshi kwa kukubali kuteuliwa kwa Anjum badala ya rafiki yake Faiz Hamid, lakini uongozi wa jeshi ukisisitizwa na uungaji mkono wa Marekani ulisisitiza kumuondoa kwenye uwaziri mkuu na kumteua mwingine! Jeshi na Marekani walihofia kuwa ukiukaji huo wa uamuzi wa jeshi ungekuwa mwanzo wa kujitenga na maamuzi ya jeshi yanayoungwa mkono na Marekani, na hivyo wakasisitiza kumuondoa...

Nne: Imran Khan alikasirika, hasa baada ya kutoa huduma kubwa kwa Marekani kama tulivyotaja, na pia alikuwa mtiifu kwa uongozi wa jeshi... Ni kana kwamba aliona haiwezekani kwa jeshi na Marekani kufanya kazi ya kumwondoa baada ya huduma hizo alizowapa, akisahau au kujisahaulisha kuwa nchi za kikafiri hazimruhusu kibaraka wake kupumua nje ya hewa yake! Vyovyote iwavyo, alikasirishwa na hilo na kutoa matamshi dhidi ya Marekani lakini baada ya muda kupita! Miongoni mwa matamshi hayo:

1- (Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan amesema leo Jumamosi kwa kikundi cha waandishi wa habari wa kigeni "Hatua ya kuniondoa madarakani ni uingiliaji wa wazi wa Marekani katika siasa za ndani". Euronews Arabic, 02/04/2022). Na vyombo vya habari vya ndani viliripoti (kuwa Khan alipokea barua kutoka kwa balozi wa Islamabad mjini Washington ikijumuisha rekodi ambayo afisa wa juu wa Marekani alisema "alisemekana kuwa Msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kwa masuala ya Asia Kusini na Kati Donald Lu" kwamba Marekani inahisi kuwa uhusiano unaweza kuwa bora ikiwa Khan ataondoka madarakani. Arabic Post, 03/04/2022).

2- Katika msimamo tofauti na msimamo wa Washington dhidi ya Urusi kuhusu shambulio lake dhidi ya Ukraine, alikataa kulaani shambulio hilo na hata akazuru Moscow, na kuonekana kando ya Rais wa Urusi Putin mnamo 24/02/2022, yaani siku ya kwanza ya Urusi kuanza vita vyake dhidi ya Ukraine, wakati ambapo mkuu wa jeshi la Pakistan Bajwa alilaani shambulio hilo akiafiki misimamo ya Marekani kwa uwazi kabisa, jambo linalopingana na matamshi ya hivi karibuni ya Khan (Mkuu wa jeshi la Pakistan amekosoa vita vya Urusi dhidi ya Ukraine, akitoa wito wa kusitishwa mara moja kwa kile alichokiita "msiba mkubwa" unaoikabili nchi ndogo. Jambo la kushangaza ni kwamba ukosoaji wa Jenerali Qamar Javed Bajwa dhidi ya Moscow ni kinyume na kile alichoelekeza Waziri Mkuu wa nchi yake, Imran Khan, ambaye alitetea umuhimu wa Islamabad kutofungamana na upande wowote kuelekea kile kinachotokea Ukraine, na akakataa kukosoa vitendo vya Rais wa Urusi Vladimir Putin. Al-Hurra, 02/04/2022).

3- Katika msimamo mwingine, Imran Khan alisema: ("Mabalozi wa Umoja wa Ulaya wameandika barua wakitutaka tulaani operesheni ya kijeshi ya Urusi nchini Ukraine... Nataka kuuliza kama mlipeleka barua yoyote kama hiyo kwa India". Aliongeza: "Je, sisi ni watumwa wenu.. tunafanya chochote mnachosema"? Afisa huyo wa Pakistan aliendelea kusema: "Wakati India ilipokiuka sheria za kimataifa katika Kashmir inayokaliwa kwa mabavu, je, kuna yeyote kati yenu aliyekata uhusiano na India au kusitisha biashara"? Al-Araby Al-Jadeed, 07/03/2022).

Tano: Kama tulivyosema hapo awali, Imran Khan hakutarajia kuwa huduma zake zote kwa jeshi na nyuma yake Marekani hazingemsaidia! Ni kana kwamba hakuelewa kuwa anayefika kwenye utawala kwa msaada wa makafiri wakoloni akiwa kibaraka kwao, basi anakuwa kwao kama kete ya chess wanayoichezesha wanavyotaka, bali hata kumuangusha wanavyotaka ikiwa hatatimiza maslahi yao bila kukeuka, na hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Imran Khan! Mahakama Kuu nchini Pakistan ilibatilisha mnamo tarehe 07/04/2022 uamuzi wa Naibu Spika wa Bunge wa kukataa kupiga kura juu ya pendekezo la upinzani kuhusu kura ya kutokuwa na imani na serikali ya Imran Khan, pia ilibatilisha uamuzi wa Rais wa Jamhuri wa kulivunja Bunge mnamo tarehe 03/04/2022 na kuelekea kwenye kufanya uchaguzi wa mapema kulingana na ushauri wa Waziri Mkuu Imran Khan kwake, na mahakama iliona hilo ni kinyume na katiba na kwamba hatua hiyo ni batili. Na ilimtaka Spika wa Bunge kuitisha kikao cha bunge mnamo tarehe 10/04/2022, ambapo bunge la Pakistan lenye viti 342 lilipiga kura kwa wingi wa kura 174 za kutokuwa na imani na Imran Khan... Na ni wazi kuwa katika matukio haya, jeshi ndilo lililokuwa likiongoza mambo nyuma ya pazia, kwani majaji wakuu hawachukui uamuzi kama huo bila uungaji mkono kamili kutoka kwa mkuu wa jeshi...

Sita: Siku iliyofuata tarehe 11/04/2022, Bunge lilimchagua Shehbaz Sharif kuwa Waziri Mkuu hadi wakati wa uchaguzi mkuu mnamo Agosti 2023. Shehbaz ni mdogo wake Nawaz Sharif ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa Pakistan hapo awali. Shehbaz amekuwa kiongozi wa upinzani katika Bunge la Kitaifa la Pakistan tangu mwaka 2018, na ameshika uongozi wa chama cha Pakistan Muslim League baada ya kaka yake Nawaz aliyeanzisha chama hicho. Na kwa kujitolea kwa Shehbaz kuwa mtiifu kwa jeshi na Marekani... hivyo wakamsaidia katika uchaguzi kuchukua nafasi ya Imran Khan. Kufuatia hilo, alifanya yafuatayo:

1- Shehbaz alianza sera yake kulingana na kile Marekani inachokitaka... alianza na lugha ya mapatano na India na kwamba yuko tayari kwa mazungumzo badala ya makabiliano. Katika hotuba yake ya kwanza, Shehbaz Sharif alisema: ("Pakistan inataka uhusiano bora na India. Lakini hakutakuwa na amani ya kudumu bila kusuluhisha hali ya Kashmir. Ni lazima kwa waziri mkuu wa India aturuhusu kutatua suala la Kashmir na kutoa nguvu zetu kwa ustawi wa nchi zetu"... Sky News 14/04/2022). Na Waziri Mkuu wa India Modi alimjibu kupitia akaunti yake ya Twitter akisema: ("Nampongeza Shehbaz Sharif kwa kuchaguliwa kwake kuwa waziri mkuu wa Pakistan. India inatamani amani na utulivu na katika eneo lisilo na ugaidi, ili tuweze kuzingatia maendeleo yetu na kuhakikisha ustawi na ufanisi wa watu wetu"). Ikumbukwe kuwa Waziri Mkuu wa India ana chuki na Uislamu na Waislamu, na anawachochea wafuasi wake Wahindu dhidi ya Waislamu nchini India na anawafanyia ukandamizaji na kutokubali kuishi kwa Waislamu katika nchi yao ya India na kuwakandamiza binti zao mashuleni katika suala la vazi la kisheria.

2- Habari zinataja kuwa Shehbaz Sharif alijitolea kufanya kazi na majenerali ikiwa atachaguliwa na akataja kuwa nchi inahitaji kusonga mbele na kuvuka tofauti na jeshi. Hapo awali alikuwa akikosoa jeshi katika mapinduzi yake dhidi ya kaka yake mkubwa, Waziri Mkuu wa zamani Nawaz Sharif, mnamo mwaka 1999. Shehbaz Sharif aligombea uchaguzi na kushindwa na Imran Khan. Na mnamo Desemba 2019, Idara ya Ukaguzi ilizuia mali 23 zinazomilikiwa na ndugu hao wawili na kuwafungulia mashtaka ya utakatishaji fedha, na mnamo Septemba 2020 Shehbaz alikamatwa kwa tuhuma za kuhusika na utakatishaji fedha na aliachiliwa mnamo Aprili 2021 kwa dhamana. Hivyo mapatano yake na jeshi ni moja ya sababu zilizomfanya kufika mamlakani.

3- Na ikiwa tutaashiria haraka ya Marekani kumpongeza Shehbaz Sharif ambapo Waziri wake wa Mambo ya Nje Blinken alisema: "Marekani inampongeza Waziri Mkuu mpya wa Pakistan aliyechaguliwa hivi karibuni Shehbaz Sharif, na tunatarajia kuendeleza ushirikiano wetu wa muda mrefu na serikali ya Pakistan" (Sky News 14/04/2022), basi hii inathibitisha kuwa Marekani imekubali mapatano yake na jeshi na ahadi yake ya kutekeleza sera yake na ikakubali kupanga ushindi wake katika kufika mamlakani baada ya kuwa imembana yeye na kaka yake Nawaz, na sasa imekubali baada ya kuwa amejiandaa kufanya kazi nayo kikamilifu na kupatana na jeshi tiifu kwake!

4- Serikali mpya ilitangaza tarehe 12/04/2022 kuwa "itashiriki kwa njia ya kujenga na chanya na Marekani ili kukuza malengo ya pamoja ya amani, usalama na maendeleo katika eneo" na ofisi ya Shehbaz Sharif ilithibitisha uhusiano wake na Marekani ambapo taarifa ya ofisi hiyo ilisema: "Tunakaribisha uthibitisho wa Marekani wa uhusiano wa muda mrefu na Pakistan... Tunatarajia kuimarisha uhusiano huu muhimu kwa msingi wa kanuni za usawa, maslahi ya pamoja na faida ya pande zote"... Na Psaki alisema "Utawala wa Biden unaunga mkono kuzingatia kwa amani misingi ya kidemokrasia ya kikatiba na hauungi mkono chama kimoja cha kisiasa kwa gharama ya kingine nchini Pakistan.. Tunathamini ushirikiano wetu wa muda mrefu na Pakistan na daima tunaona Pakistan yenye ustawi na ya kidemokrasia kuwa muhimu kwa maslahi ya Marekani.. na kwamba uhusiano mrefu, wenye nguvu na wa kudumu utaendelea chini ya viongozi wapya mjini Islamabad (Sauti ya Amerika 12/04/2022).

Hii inathibitisha kuwa Marekani ilikuwa nyuma ya kuanguka kwa kibaraka wake wa zamani Imran Khan na kuletwa kwa Shehbaz Sharif ambaye anatangaza kwa uwazi kabisa utayari wake wa kufanya kazi na Marekani kwa hima na bidii zaidi ya vile alivyokuwa Imran Khan!

Saba: Hakika vibaraka hawa hawajifunzi wala hawaelewi. Ikiwa Marekani itamwangusha mmoja wao, wanakimbilia kutafuta upendo wake na kujiandaa kutoa huduma kwake ili wafike mamlakani. Hawajitengi nayo, bali wanakimbilia kwayo ili iwarudishe tena mamlakani ikiwa itawaangusha! Kwani inawajua kuwa wao ni duni zaidi ya kuwa viongozi wa kisiasa wa kweli wenye itikadi; wao ni wasaka vyeo tu na si zaidi. Shehbaz Sharif hajajifunza jinsi Marekani ilivyomwangusha kaka yake zaidi ya mara moja na kisha yeye na kaka yake wakaadhibiwa kwa kufukuzwa nchini. Umma unahitaji wanasiasa wenye itikadi na wenye msimamo, ambao ni msimamo wa Umma, Uislamu ambao unatibu mambo yote kwa njia ya kimsingi na sahihi. Hawa ndio watakaookoa Umma na kuuamsha na kuufanya kuwa dola kuu na sio dola tiifu kwa Marekani. Na Pakistan ina sifa za kuwa kituo cha kuanzia cha dola hii kuu, dola ya Khilafah Rashidah, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.

إِنَّ فِي هَذَا لَبَلَاغاً لِقَوْمٍ عَابِدِينَ

"Hakika katika haya (yaliyotajwa) mna ujumbe tosha kwa watu wanaomwabudu (Mwenyezi Mungu)." (QS. Al-Anbiya [21]: 106)

5 Shawwal 1443 H 05/05/2022 M

Share Article

Share this article with your network