Mfululizo wa majibu ya mwanachuoni mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook "Fikri"
Kwa Abu Abdullah Sulayman
Swali:
Assalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh
Imeelezwa katika kitabu cha Ash-Shakhsiyyah al-Islamiyyah (Shakhsia ya Kiislamu) Juzuu ya Kwanza, mada ya "Haja ya Umma Leo kwa Wafasiri", mstari wa tisa na wa kumi: (kama kitabu cha kifikra, chenye fikra ya kina na inayoangaza (mustanirah)). Je, neno mustanirah ni sahihi?
Jibu:
Walaikum Salaam Warahmatullahi Wabarakatuh
Neno (mustanirah) ni sahihi, kwani fikra ziko za aina tatu:
Ya kijuujuu, ya kina, na inayoangaza... Maelezo ya kina ya jambo hili utayapata katika kitabu cha At-Tafkir (Kufikiri), ukurasa wa 86-92, na ninakunukulia kutoka humo:
[Kufikiri ima kuwe kwa kijuujuu, au kwa kina, au kuwe kunaangaza. Kufikiri kwa kijuujuu ni kufikiri kwa watu wa kawaida. Kufikiri kwa kina huwa kwa wanachuoni. Ama kufikiri kunakoangaza, mara nyingi huwa ni kufikiri kwa viongozi na watu walioangazika miongoni mwa wanachuoni na watu wa kawaida. Kufikiri kwa kijuujuu ni kuhamisha tu uhalisia (waqi') kwenda kwenye ubongo, bila kutafiti kingine, na bila kujaribu kuhisi kinachofungamana nao. Na kuunganisha hisia hii na taarifa zinazohusiana nayo, bila kujaribu kutafuta taarifa nyingine zinazohusiana nayo, kisha kutoa hukmu ya kijuujuu. Hili ndilo linalotawala makundi, na linalotawala wale wenye fikra za chini, na linalotawala wasiosoma na wasio na maarifa miongoni mwa watu werevu...
Ama fikra ya kina ni kuzama ndani katika kufikiri, yaani kuzama ndani katika kuhisi uhalisia, na kuzama ndani katika taarifa zinazounganishwa na hisia hii ili kuuelewa uhalisia. Haitosheki na hisia tupu na taarifa za awali tu za kuunganisha hisia, kama ilivyo katika kufikiri kwa kijuujuu, bali inarudia tena kuhisi uhalisia huo, na inajaribu kuhisi humo zaidi ya ilivyohisi mara ya kwanza, ima kwa njia ya majaribio au kwa kurudia kuhisi, na inarudia kutafuta taarifa nyingine pamoja na zile taarifa za awali, na inarudia kuunganisha taarifa na uhalisia zaidi ya ilivyokuwa imeunganishwa, ima kwa uangalizi na kuurudia au kwa kuunganisha tena mara nyingine. Hivyo, kutokana na aina hii ya hisia na aina hii ya muunganisho, au aina hii ya taarifa, hutoka fikra za kina, ziwe ni ukweli (haqaiq) au si ukweli. Na kwa kurudia jambo hilo na kulizoea, hupatikana kufikiri kwa kina. Hivyo basi, kufikiri kwa kina ni kutotosheka na hisia za awali, na kutotosheka na taarifa za awali, na kutotosheka na muunganisho wa awali. Hiyo ni hatua ya pili baada ya kufikiri kwa kijuujuu. Na huku ndiko kufikiri kwa wanachuoni na wanafikra, ingawa si lazima kuwe ni kufikiri kwa wasomi. Kwa hiyo, kufikiri kwa kina ni kuzama ndani katika hisia, taarifa, na muunganisho.
Ama kufikiri kunakoangaza, kwenyewe ni kule kufikiri kwa kina kwenyewe kukiwa kumeongezewa kufikiria kile kinachozunguka uhalisia na kinachofungamana nao ili kufikia matokeo ya kweli. Yaani, kufikiri kwa kina ni kuzama ndani katika fikra yenyewe, lakini kufikiri kunakoangaza ni kuwa, pamoja na kuzama ndani katika fikra, kuwe na kufikiria kile kinachozunguka uhalisia na kinachofungamana nao, kwa ajili ya lengo lililokusudiwa ambalo ni kufikia matokeo ya kweli. Kwa ajili hiyo, kila fikra inayoangaza ni kufikiri kwa kina, na haiwezekani kufikiri kunakoangaza kutokane na kufikiri kwa kijuujuu. Isipokuwa si kila kufikiri kwa kina ni kufikiri kunakoangaza. Kwa mfano, mwanasayansi wa atomu anapotafiti kuhusu mgawanyiko wa atomu, na mwanakemia anapotafiti muundo wa vitu, na mwanasheria wa Kiislamu (faqih) anapotafiti katika kutoa hukmu na kuweka sheria, wao na mfano wao wanapotafiti vitu na mambo, hakika wanavitafiti kwa kina, na lau si kina wasingefikia matokeo yale makubwa. Lakini wao si wanafikra wenye kufikiri kunakoangaza, na kufikiri kwao hakuchukuliwi kuwa ni kufikiri kunakoangaza. Hivyo usishangae unapomkuta mwanasayansi wa atomu akiswali mbele ya kipande cha mti, yaani msalaba, pamoja na kwamba mwangaza wa kawaida tu unamwonyesha kuwa mti huu haunufaishi wala kudhuru, na kwamba si kitu cha kuabudiwa. Na usishangae unapomkuta mwanasheria bingwa akiamini kuwepo kwa watakatifu, na akijisalimisha kwa mwanadamu kama yeye ili amsamehe madhambi yake. Kwa sababu mwanasayansi wa atomu na mwanasheria na mfano wao, wanafikiri kwa kina na si kufikiri kunakoangaza; na lau kufikiri kwao kungekuwa kunaangaza, wasingefika kwenye ule mti, wala wasingeamini kuwepo kwa watakatifu, wala wasingeomba msamaha kwa watu kama wao. Ni kweli kwamba anayefikiri kwa kina ni mwenye kina katika kile alichofikiria tu na si kinginecho; anaweza kuwa na kina anapofikiria mgawanyiko wa atomu au kuweka sheria, lakini akawa ni mpumbavu katika mambo mengine anapoyafikiria. Hilo ni kweli, lakini kuzoea kwa mwanafikra kufikiri kwa kina humfanya azame ndani katika mengi ya anayoyafikiria, hususan mambo yanayohusiana na tatizo kuu (al-uqdah al-kubra) au mtazamo wa kimaisha (wijhatun nadhar). Lakini kukosekana kwa mwangaza katika kufikiri kwake humfanya azoee kufikiri kwa kina, na azoee kufikiri kwa kijuujuu na hata kufikiri kwa kipumbavu. Kwa sababu hiyo, kufikiri kwa kina pekee hakutoshi kumuinua mwanadamu na kuinua kiwango chake cha kifikra, bali ni lazima, ili hilo lifanyike, kuwe na mwangaza katika fikra mpaka kupatikane mwinuko katika fikra...].
Na ukitaka ziada, basi rejea kwenye kitabu kilichotajwa, na Mwenyezi Mungu yu pamoja nawe.
Ndugu yenu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah
05 Shaaban 1445 Hijria Inayoafikiana na 15/02/2024 Miladia
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Mwenyezi Mungu amhifadhi) kwenye: Facebook