Silsila ya majibu ya mwanachuoni mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook "Fikri"
Jibu la Swali
Kwenda kwa Hamid Shahin
Swali:
Assalamu Alaikum Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh,
Salamu njema, kisha:
Namuomba Mwenyezi Mungu uwe katika hali nzuri na afya, Amir wetu mpendwa,
Swali langu linahusu thamani (kima). Swali ni kuhusu thamani inayotimizwa na Hizb katika kuanza tena maisha ya Kiislamu; je, kuanza tena maisha ya Kiislamu kunatimiza "thamani ya kiubinadamu" kwa kuwa ni kazi inayookoa ubinadamu itakapofikiwa, au kunatimiza "thamani ya kiroho" kwa kuwa kuanza tena maisha ya Kiislamu kumesimama juu ya msingi wa kisheria (si wa kisilika) unaohusiana na kuhukumu kwa Uislamu na wajibu wa kutoa bai'ah kwa Khalifa... n.k? Mwenyezi Mungu akubariki.
Pia, je thamani ya kiroho inahusiana tu na ibada pekee na si vinginevyo?
Jibu:
Walaikum Assalam Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh
Kwanza: Kabla ya kujibu, ni lazima kufafanua mambo mawili yanayohusiana na thamani:
- Jambo la kwanza ni kwamba thamani ni kusudio (qasd) la kitendo na si matokeo yanayopatikana kutokana na kutekeleza kitendo hicho. Thamani inaweza kuwa ya kiroho lakini matokeo yakawa yanahisika au hayahisiki. Kwa mfano, wewe unafanya Jihadi na kusudio lako ni thamani ya kiroho, lakini matokeo ya kitendo hicho ni matokeo yanayohisika kama vile kukomboa nchi au ngome... Na wewe unaomba dua na kusudio lako ni kutimiza thamani ya kiroho, na matokeo yake hayahisiki ikiwa dua katika hali hiyo si sehemu ya njia (tariqah), bali njia ya kisheria ni nyingine tofauti na dua; hivyo matokeo yanakuwa ni kupata thawabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu (swt). Imekuja katika kitabu cha Al-Mafahim: (...Kwa mfano, dua ni kitendo kinachotimiza thamani ya kiroho, na Jihadi ni kitendo cha kimaada kinachotimiza thamani ya kiroho. Lakini dua, ingawa ni kitendo cha kimaada, inatokeza matokeo yasiyohisika, nayo ni thawabu, hata ikiwa kusudio la anayefanya dua ni kutimiza thamani ya kiroho. Hii ni tofauti na Jihadi, kwani ni kupigana na maadui, nacho ni kitendo cha kimaada kinachotokeza matokeo yanayohisika kama vile kukomboa ngome au mji au kuua adui na mfano wa hayo, hata ikiwa kusudio la mujahid ni kutimiza thamani ya kiroho...).
Ama dua katika hali nyingine "ambayo haina njia ya kisheria mahususi", inaweza kuleta matokeo yanayohisika. Imekuja katika jibu la swali la tarehe 25/10/2014: (......Na haikuja katika "Al-Mafahim" kuhusu dua chochote katika hali nyinginezo, bali hizo zinajumuishwa na hadith ya jumla aliyoitoa Ahmad katika Musnad yake: Kutoka kwa Abi al-Mutawakkil, kutoka kwa Abi Said, kwamba Mtume ﷺ amesema:
مَا مِنْ مُسْلِمٍ يَدْعُو بِدَعْوَةٍ لَيْسَ فِيهَا إِثْمٌ، وَلَا قَطِيعَةُ رَحِمٍ، إِلَّا أَعْطَاهُ اللَّهُ بِهَا إِحْدَى ثَلَاثٍ: إِمَّا أَنْ تُعَجَّلَ لَهُ دَعْوَتُهُ، وَإِمَّا أَنْ يَدَّخِرَهَا لَهُ فِي الْآخِرَةِ، وَإِمَّا أَنْ يَصْرِفَ عَنْهُ مِنَ السُّوءِ مِثْلَهَا
"Hapana Muislamu yeyote anayeomba dua ambayo haina dhambi ndani yake, wala kukata udugu, isipokuwa Mwenyezi Mungu humpa kwayo moja ya mambo matatu: Ama amharakishie dua yake, au amuekee akiba kwa ajili ya Akhera, au amuepushe na ubaya mfano wake." Wakasema: "Basi tutazidisha (kuomba)," akasema: "Mwenyezi Mungu ni zaidi (wa kutoa)."
Yaani Mwenyezi Mungu (swt) anamuitikia muombaji kwa moja ya mambo matatu, na miongoni mwayo ni «ama amharakishie dua yake». Na haya ni matokeo yanayohisika.)
- Jambo la pili ni kwamba maudhui ya thamani yanahusiana na kusudio la mtu binafsi, yaani ni jambo la mtu mmoja mmoja (fardiy):
- Imekuja katika Al-Mafahim kuunganishwa kwa thamani na kusudio la mtu (binadamu kwa maana ya mtu au mtendaji), imekuja katika ukurasa wa 30-34 wa faili ya Word yafuatayo:
[...Ama kuhusu kusudio la kitendo, ni lazima kwa kila mtendaji awe na kusudio ambalo amefanya kitendo kwa ajili yake. Na kusudio hili ndilo thamani ya kitendo. Kwa hivyo, ilikuwa ni lazima kwa kila kitendo kuwa na thamani ambayo mwanadamu anazingatia kuitimiza wakati anapofanya kitendo hicho, la sivyo kingekuwa ni mchezo tu...
Kwa hivyo, ilikuwa ni lazima kwa Muislamu afanye juhudi zake kutimiza thamani inayokusudiwa kwa kila kitendo anachofanya wakati wa kukitekeleza na kukifanya, ili achangie katika ustawi wa jamii na utukufu wake, na kuhakikisha - wakati huo huo - ustawi wa nafsi yake na utulivu wake...
Na kwa ajili hiyo, ilikuwa ni makosa kumwachia mwanadamu akadirie thamani hizi, bali thamani lazima zikadiriwe na Muumba wa mwanadamu ambaye ni Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo, ilikuwa ni lazima kwa Sharia ndiyo imuainishie mwanadamu thamani hizi na iainishe wakati wa kuzitekeleza, na kwa mujibu wa hayo mwanadamu anazichukua...
Na kwa njia hiyo, thamani zinatimia katika jamii kwa kiasi kinachohitajika kama jamii fulani. Na jamii hii inapimwa kwa vigezo vyake. Na juu ya msingi huu, lazima kufanywe kazi ili kutimiza thamani hizo, ili kuwepo jamii ya Kiislamu kulingana na mtazamo wa Uislamu katika maisha.] Mwisho.
Hii ina maana kwamba thamani ya kitendo ni kusudio ambalo mtendaji amefanya kitendo kwa ajili yake. Kwa hivyo thamani ni kusudio la kitendo, na yule anayekuwa na kusudio la kitendo ni mwanadamu, yaani mtu binafsi aliyebainishwa kama Muhammad, Zainab, Fatima, na Khalid. Yeye anapofanya kitendo miongoni mwa vitendo, anakusudia kutimiza thamani fulani kutokana na kitendo chake. Ikiwa Muhammad atafanya biashara, basi anakusudia kutimiza faida ya kimaada ambayo ni thamani ya kimaada. Na ikiwa Zainab ataswali, basi anakusudia kutimiza thamani ya kimaanawi ambayo ni thamani ya kiroho. Na ikiwa Fatima atasema ukweli, basi anakusudia kutimiza thamani ambayo ni thamani ya kimaadili. Na ikiwa Khalid atamsaidia mwenye shida, basi anakusudia kutimiza thamani ambayo ni thamani ya kiubinadamu... Hivyo basi, thamani ni kusudio la mtu binafsi aliyebainishwa kutokana na kufanya kwake kitendo, yaani anayefanya kitendo kwa kusudio la kutimiza thamani ni mwanadamu "mtu binafsi".
Hapa linajitokeza jukumu la Hizb katika kudhibiti thamani hizi kwa vijana wake, ziwe thamani hizi ni za kiroho, kimaadili, kiubinadamu, au kimaada, kwa kuwa thamani hizi ziwe kwa mujibu wa hukumu za Sharia. Hizb inatumia mbinu (uslub) zinazohitajika katika kuzidhibiti kupitia maelekezo au ufafanuzi kwa mujibu wa hukumu za Sharia. Ikiwa maelekezo na ufafanuzi havijafua dafu kudhibiti thamani kwa vijana na ikahitajika adhabu ya kiidara, basi hufanya hivyo, ili kuhakikisha utekelezaji wa vijana kwa thamani hizi ni kwa mujibu wa amri za Mwenyezi Mungu (swt) na makatazo Yake...
Kadhalika, linajitokeza jukumu la Dola kudhibiti thamani hizi kwa mujibu wa hukumu za Sharia. Na hakuna juu ya mwanadamu Muislamu katika sifa yake ya mtu binafsi (kama mtu au mtendaji) isipokuwa kufanya kazi ili kutimiza thamani hizi kwa mujibu wa amri za Mwenyezi Mungu na makatazo Yake... katika aina zote za thamani za kiroho, kimaadili, kiubinadamu, na kimaada.
Hili ndilo jukumu la Dola na nafasi yake katika kudhibiti utekelezaji wa watu binafsi katika kutimiza thamani kwa mujibu wa hukumu za Sharia, iwe thamani hiyo ni ya kiroho, kimaadili, kiubinadamu, au kimaada... Nayo inatumia mbinu zinazohitajika katika kuzidhibiti kupitia maelekezo au ufafanuzi kwa mujibu wa hukumu za Sharia. Ikiwa maelekezo na ufafanuzi havijafua dafu kurekebisha ukiukaji wa kisheria katika utekelezaji wa watu binafsi wa thamani hizi na ikahitajika adhabu, basi hufanya hivyo, ili kuhakikisha utekelezaji wa watu binafsi kwa thamani hizi ni kwa mujibu wa amri za Mwenyezi Mungu (swt) na makatazo Yake...
Pili: Na sasa nakujibu swali lako:
- Hakika mlinganiaji (hamil ad-da'wah) anayefanya kazi ya kuanza tena maisha ya Kiislamu kwa kusimamisha Khilafah yaongofu, anakusudia katika kitendo chake hiki kutimiza thamani ya kiroho ili kupata radhi za Mwenyezi Mungu (swt) na Mtume Wake ﷺ. Na matokeo ya kitendo chake yanakuwa ni matokeo yanayohisika kama vile utukufu, nusura, tamkin, ukombozi, na kueneza kheri popote itakapotua Khilafah.
وَأُخْرَى تُحِبُّونَهَا نَصْرٌ مِنَ اللَّهِ وَفَتْحٌ قَرِيبٌ وَبَشِّرِ الْمُؤْمِنِينَ
"Na (kuna) nyingine mnayoipenda, nayo ni nusura itokayo kwa Mwenyezi Mungu, na ushindi ulio karibu. Na wabashirie Waumini." (QS. As-Saff [61]: 13)
- Kusudia kutimiza thamani ni jambo la mtu binafsi, yaani linahusiana na watu binafsi. Fulani anakusudia kutimiza thamani ya kiroho, kimaadili, kiubinadamu, au kimaada... Hivyo ni kusudio la mtu binafsi. Ama Hizb, katika kazi yake ni kudhibiti vijana wake ili vitendo vyao visiwe mchezo tu, bali wafanye kazi ili kutimiza thamani hizi kwa mujibu wa hukumu za kisheria. Kadhalika, katika kazi ya Dola ni kudhibiti utimizaji wa thamani hizi kutoka kwa watu binafsi katika jamii kwa mujibu wa hukumu za kisheria.
Natumai jibu hili linatosheleza, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi zaidi na Mwenye hikma zaidi.
Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah
06 Rabi’ al-Akhar 1444 H Sawa na 31/10/2022 M
Kiungo cha jibu kutoka ukurasa wa Amir (Mwenyezi Mungu amhifadhi) kwenye Facebook
Kiungo cha jibu kutoka ukurasa wa Amir (Mwenyezi Mungu amhifadhi) kwenye Web