Swali:
Mnamo tarehe 5/8/2024, ilitangazwa kujiuzulu kwa Waziri Mkuu wa Bangladesh na kukimbia kwake nje ya nchi baada ya maandamano dhidi ya mfumo wa upendeleo wa nafasi za kazi (quota system) katika sekta ya umma tangu kuanza kwa mwezi uliopita. Maandamano hayo yaligeuka kuwa ya umwagaji damu tangu katikati ya mwezi uliopita huku wafuasi wa chama tawala wakikabiliana na waandamanaji. Jeshi lilitangaza kuchukua mamlaka, na Rais wa nchi hiyo akatangaza kuvunja bunge na kuteua serikali ya mpito. Je, maandamano haya yalikuwa yamepangwa? Je, kuingilia kati kwa jeshi kulikuja kwa makubaliano? Na je, jambo hili lina uhusiano na ushindani wa kimataifa nchini humo?
Jibu:
Ili kubainisha jibu la maswali yaliyo hapo juu, tunapitia mambo yafuatayo:
1- Bangladesh ni nchi ya Kiislamu. Katika miaka ya kwanza ya karne ya kumi na tatu Miladi, Waislamu waliikomboa ardhi ya Bengal wakati wa kampeni ya Muhammad Al-Ghori mwishoni mwa mwaka 1192 M ambayo ilienea kote Kaskazini mwa India. Bangladesh, ambayo ni nchi ya nane kwa ukubwa duniani kwa idadi ya watu ikiwa na takriban watu milioni 171, ipo Kusini mwa Asia na inapakana na Myanmar na India. Zaidi ya 90% ya idadi ya watu ni Waislamu na dini rasmi ya nchi hiyo ni Uislamu. Kama sehemu ya sera ya "divide and rule" (gawa utawale) iliyofuatwa na Uingereza, chama cha Awami League kilichokuwa na makao yake makuu Mashariki mwa Pakistan kikiongozwa na Sheikh Mujibur Rahman, wakala wa Uingereza na kwa msaada wa Waingereza, kilitangaza uhuru wake kutoka kwa Pakistan baada ya vita na Pakistan mnamo 1971.
2- Waziri Mkuu wa Bangladesh, Hasina, alirithi utiifu kwa Uingereza—mkoloni wa zamani wa nchi hiyo—kutoka kwa baba yake, aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani wa Bangladesh, Mujibur Rahman, kiongozi wa chama cha Awami, ambaye aliuawa pamoja na wanafamilia yake mnamo 1975 na maafisa waliofanya mapinduzi dhidi yake. Hasina alinusurika kwa sababu alikuwa nje ya nchi wakati wa mapinduzi hayo. Aliishi India hadi aliporuhusiwa kurejea nchini kwake na kuanza shughuli za kisiasa mnamo 1981. Alishika wadhifa wa Waziri Mkuu kwa mara ya kwanza kati ya mwaka 1996 na 2001, na baada ya hapo akaongoza serikali tangu 2009 hadi leo. Alituhumiwa kwa kuiba kura katika uchaguzi uliofanyika mapema mwaka huu, ambapo alipata ushindi mkubwa katika bunge lililoundwa na chama chake cha Awami League, ambapo idadi ya washindi ilifikia wabunge 233 kati ya 300, pamoja na wanachama 9 kutoka chama kilichoungana na chama chake. Vyama vingine vilikataa matokeo hayo na kuyaona kama uchaguzi wa kiini macho, na Amerika pia ilikosoa uchaguzi huo. Hata hivyo, utawala wa Hasina ulitangaza rasmi ushindi wake!
3- Wakati wa vipindi vyake vya utawala, Hasina alifanya kazi kuwapiga mawakala wa Amerika na kuimarisha ushawishi wa Waingereza jeshini, katika mazingira ya kisiasa, mahakamani na katika vituo vinginevyo. Alikuwa akishindana na kiongozi wa chama cha upinzani, mkuu wa chama cha Bangladesh Nationalist Party (BNP), Khaleda Zia, ambaye alirithi utiifu kwa Amerika kutoka kwa mume wake, Jenerali Ziaur Rahman, aliyeshika madaraka mnamo 1977 na kuuawa mnamo 1981 na mawakala wa Waingereza. Mke wake, Khaleda Zia, aliongoza serikali katika vipindi viwili kati ya 1991 na 1996, na kati ya 2001 na 2006. Baadaye alihukumiwa kwa makosa ya ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka. Aliachiliwa yeye na wafungwa wengine wakati wa maandamano ya hivi karibuni baada ya Hasina kukimbia tarehe 5/8/2024. Kwa sababu hiyo, kuna ushindani wa kimataifa nchini Bangladesh kati ya mkoloni wa zamani, Uingereza, mwenye ushawishi mkubwa, na mkoloni mpya, Amerika, ambayo imejitengenezea ushawishi kwa kuwapata mawakala jeshini tangu wakala wake Jenerali Ziaur Rahman alipochukua mamlaka mnamo 1977, na pia kupata mawakala katika mazingira ya kisiasa, haswa mke wa Jenerali Zia na chama cha BNP. Pamoja na hayo, ushawishi mkubwa bado ni wa Uingereza.
4- Hasina na serikali yake walifanya kazi ya kupiga vita wale wanaotafuta kurejesha Uislamu kwenye utawala kwa sababu yeye ni msekula na chama chake ni cha kisekula cha kizalendo. Kisiasa, yeye ni mfuasi wa mkoloni wa Magharibi anayepiga vita Uislamu na kurejea kwake madarakani. Alikipiga marufuku chama cha Hizb ut Tahrir mnamo tarehe 22/10/2009 kwa sababu kinadai kurejea kwa Uislamu kupitia kusimamisha dola ya Khilafah ya Rashida. Ikumbukwe kuwa Hizb ut Tahrir ni chama cha kisiasa ambacho msingi wake ni Uislamu na hakitumii njia za kimwili (mapambano ya silaha), bali hufanya mapambano ya kisiasa na mgongano wa kifikra. Pia alipiga marufuku makundi mengine manne ya Kiislamu. Aliwafunga gerezani vijana wengi wa Hizb ut Tahrir na makundi mengine, na kuwanyonga baadhi ya viongozi wa Kiislamu. Hasina Wajed alianza operesheni zake za kisiasa dhidi ya Jamaat-e-Islami tangu mwaka 2013 kwa kisingizio kuwa ni wahalifu wa kivita waliokataa uhuru wa Bangladesh, huku lengo likiwa ni kuondokana na mrengo wa Kiislamu. Miongoni mwa watu mashuhuri waliokamatwa na kunyongwa au kufia gerezani kutoka kwa viongozi wa Jamaat-e-Islami hadi sasa ni wanazuoni wakubwa saba, ambapo watano walinyongwa na wawili walifia gerezani kabla ya kuhukumiwa kunyongwa. (https://alestiklal.net/ 6/8/2024). Hasina alikuwa na uadui mkali dhidi ya Uislamu na wale wanaolingania kurejea kwake madarakani na umoja wa Waislamu katika dola moja. Aliongoza chama cha kisekula kilichoanzishwa na baba yake, ambaye alifanya usaliti mkubwa kwa kuitenganisha Pakistan Mashariki (Bangladesh) na Pakistan Magharibi kwa msaada wa Uingereza na mawakala wake nchini India mnamo 1971.
5- Bangladesh inakabiliwa na migogoro mikubwa ya kiuchumi isiyotibika kutokana na kukosekana kwa maendeleo ya kweli na kwa sababu ya kufungamanishwa kwake na nguvu za kigeni za kisiasa na kiuchumi. Makadirio yanaonyesha kuwa takriban vijana milioni 18 wa Bangladesh wanatafuta kazi, na wahitimu wa vyuo vikuu wanakabiliwa na viwango vya juu vya ukosefu wa ajira! Zaidi ya 40% ya idadi ya watu nchini Bangladesh wenye umri kati ya miaka 15 na 24 hawafanyi kazi na hawapati elimu. BBC ya Uingereza iliripoti mnamo 5/8/2024 mahojiano kuhusu hali ya kiuchumi nchini Bangladesh, ambapo Lutfey Siddiqi, profesa mgeni katika Shule ya Uchumi ya London (London School of Economics), alisema: "Kubadilika kwa utawala nchini Bangladesh ni jambo lisiloepukika kiuchumi, na kilichotokea ilikuwa ni suala la muda tu. Serikali ya Hasina ilipoteza haki na nguvu ya kutawala na rasilimali zinazohitajika kwa ajili hiyo pia zitaisha. Bangladesh ipo ukingoni mwa kuporomoka kiuchumi." Ikumbukwe kuwa serikali ya Hasina imeweka rehani uchumi wa nchi na rasilimali zake kwa kampuni za kigeni, haswa za Kiingereza, Kimarekani, Kichina na Kihindi. Ilianza kutegemea mikopo ya riba chini ya masharti magumu kutoka kwa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia, ambazo ni taasisi zinazotawaliwa na Amerika, pamoja na Benki ya Maendeleo ya Asia (ADB) ya China. Hii ina maana kwamba hali nchini Bangladesh ilikuwa mbaya na ilikuwa karibu kulipuka.
6- Bangladesh ilianza kushuhudia wimbi la maandamano ya wanafunzi tangu mwanzoni mwa mwezi uliopita, tarehe 1/7/2024, dhidi ya mfumo wa ajira. Maandamano hayo yalilenga kufuta mfumo wa upendeleo (quotas) katika sekta ya umma ambao unatenga takriban 56% ya kazi kwa makundi fulani maalum, ambao ulitumiwa na Waziri Mkuu na wasaidizi wake kuwaajiri jamaa zao na wafuasi wao na kuwanyima wapinzani. Miongoni mwa makundi haya maalum yaliyojumuishwa kwenye kazi hizo "ni wale walioshiriki pamoja na baba yake na watoto wao" katika usaliti mkubwa wa vita vya kujitenga kati ya Pakistan Mashariki (Bangladesh) na Pakistan Magharibi kwa msaada wa Uingereza na mawakala wake nchini India mnamo 1971. Huu ndio ulikuwa mfumo wa ajira ambao maandamano yalianza dhidi yake, ambapo wanafunzi walidai kuwa ajira iwe kulingana na uwezo wa mtu na si kwa vigezo vingine. Maandamano haya yalileta athari katika kufuta mfumo huu, ambapo Mahakama Kuu ya Bangladesh ilitangaza mnamo 21/7/2024 kuwa uamuzi wa kurejesha upendeleo wa kazi ulikuwa kinyume cha sheria. Lakini hiyo haikusaidia kuwanyamazisha waandamanaji. Tarehe 16/7/2024 ilishuhudia vifo vya kwanza katika maandamano haya wakati wanafunzi wafuasi wa chama cha Hasina walipokabiliana na waandamanaji huko Dhaka kwa fimbo na kurushiana mawe.
7- Ili kusimamisha maandamano haya, serikali ya Hasina iliamuru kufungwa kwa shule na vyuo vikuu nchi nzima, na Hasina alitoa matamshi akiwataka wanafunzi watulie na kuahidi kuadhibu kila uhalifu wa mauaji katika maandamano hayo. Lakini waandamanaji walikataa matamshi yake, na kuanza kumlenga yeye binafsi, wakipiga kelele "anguka dikteta," na wakachoma moto makao makuu ya shirika la utangazaji la serikali na makumi ya majengo mengine ya serikali. Serikali ilikata huduma za intaneti. Maandamano yalianza kushika kasi zaidi na zaidi, na idadi ya vifo na majeruhi iliongezeka kila siku. Amri ya kutotoka nje saa ishirini na nne ilitangazwa na wanajeshi walipelekwa mitaani. Polisi walifyatua risasi na mabomu ya machozi kwa waandamanaji. Jioni ya tarehe 19/7/2024, ilitangazwa kuwa watu 105 wameuawa. Naye Naeemul Islam Khan, msemaji wa ofisi ya Waziri Mkuu, alisema ("Serikali imeamua kuweka amri ya kutotoka nje na kupeleka jeshi kusaidia mamlaka za kiraia"... AFP 19/7/2024). Mawasiliano na utangazaji wa vituo vya habari na baadhi ya huduma za simu vilikatwa katika juhudi za kuzima maandamano. Waandamanaji walivamia gereza na kuwaachilia mamia ya wafungwa mnamo tarehe 19/7/2024 kabla ya kuchoma moto jengo hilo. Jumla ya vifo katika maandamano hayo nchini Bangladesh vilifikia takriban watu 409 kwa mujibu wa shirika la AFP likitegemea takwimu za polisi, maafisa wa serikali na madaktari. Inaonekana kuwa matukio haya yalilipuka kama maandamano ya hiari ya wanafunzi dhidi ya mfumo wa ajira ambapo walio wengi wananyimwa kazi. Maandamano hayakukomea kwa wanafunzi pekee, bali watu wa matabaka yote walianza kujiunga nayo kwa idadi iliyofikia takriban watu 400,000. Maandamano haya yalichukuliwa kama changamoto na tishio ambalo halijawahi kushuhudiwa kwa utawala wa kimabavu wa Hasina uliodumu kwa miaka 15.
8- Mkuu wa jeshi la Bangladesh, Jenerali Waker-uz-Zaman, alitangaza mnamo tarehe 5/8/2024 kuwa atachukua majukumu kamili baada ya kujiuzulu kwa Hasina na kukimbia kwake, na ataunda serikali ya mpito. Alisema kupitia televisheni ya taifa, "Naahidi kuwa malalamiko yote yatashughulikiwa" na kusema "Nchi imeteseka sana, uchumi umeathirika na idadi kubwa ya watu wameuawa, ni wakati wa kusitisha ghasia" (AFP 5/8/2024). Jenerali Waker-uz-Zaman alikuwa afisa katika kikosi cha watoto wa miguu, aliteuliwa mnamo Juni iliyopita kuwa mkuu wa jeshi na Hasina alimwamini kutokana na uhusiano wa mbali wa kifamilia uliopo kati yao, na alifanya kazi kama mshauri wake katika ofisi yake. Baba mkwe wake alikuwa mkuu wa jeshi katika kipindi cha kwanza cha utawala wa Hasina mnamo 1996 hadi 2001. Waker-uz-Zaman alipata mafunzo ya kijeshi nchini Uingereza na ana shahada ya uzamili katika masomo ya ulinzi kutoka Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Bangladesh na kutoka chuo cha Kiingereza cha "King's College" huko London. Hii inathibitisha kuwa yeye ni wa aina ya utawala wa Hasina unaoegemea Uingereza, ambayo ilimuelekeza kuchukua hatua na kulinda ushawishi wake nchini Bangladesh kwa kushika madaraka, na kwamba alikubaliana na Hasina aondoke ili kuokoa maisha yake kwa sababu kubaki kwake kungeongeza mgogoro na damu mpya ingemwagika. Baada ya hapo, jeshi lilijaribu kujikaribisha kwa waandamanaji ili kutuliza hali, na ndiyo maana jeshi liliruhusu maandamano katika siku ya mwisho kabla ya kuchukua mamlaka na kuzuia ufyatuaji risasi kwa muandamanaji yeyote kama njia ya kujisogeza kwao ili kutuliza hali.
9- Wakati mkuu wa jeshi, Jenerali Waker-uz-Zaman, alipotangaza kuchukua hatamu za uongozi nchini, aliahidi kuunda serikali ya mpito haraka iwezekanavyo, na kwamba atafanya mazungumzo na vyama vikuu vya upinzani na wanachama wa asasi za kiraia lakini bila chama cha Awami League, chama cha Hasina. Ili kuiridhisha Amerika na kuizuia isipate mwanya kupitia ujanja wa kisiasa wa Waingereza, urais nchini Bangladesh ulitangaza mnamo 7/8/2024 kuwa Muhammad Yunus, mshindi wa tuzo ya Nobel, ataongoza serikali ya mpito. Taarifa ya urais ilisema ("Uamuzi wa kuunda serikali ya mpito ikiongozwa na Yunus ulifikiwa wakati wa mkutano kati ya Rais wa Jamhuri Mohammed Shahabuddin, maafisa wakuu wa jeshi na viongozi wa 'kundi la wanafunzi dhidi ya ubaguzi'. Taarifa hiyo iliongeza: 'Rais amewataka wananchi kumsaidia kuvuka mgogoro huu. Na kwamba kuundwa kwa haraka kwa serikali ya mpito ilikuwa muhimu ili kushinda mgogoro huu'"... AFP 7/8/2024). Kufuatia hayo, Muhammad Yunus aliyekuwa Ulaya mwenye umri wa miaka 84 alitangaza kuwa yuko tayari kuongoza serikali ya mpito. Hivi ndivyo Waingereza walivyofanya kazi kujiokoa wasianguke na kulinda ushawishi wao wakati wakala wao alipokimbilia India kwa helikopta ya kijeshi chini ya shinikizo la maandamano. Serikali na bunge vilivunjwa, na mkuu wa jeshi akashika hatamu huku wakiteua wakala wa Amerika mwenye umri mkubwa kama Muhammad Yunus kuongoza serikali ya mpito hadi uchaguzi ujao wa bunge na kuundwa kwa serikali mpya iliyochaguliwa. Kwa hili, walifanya kazi ya kuwanyamazisha waandamanaji kwa kumwondoa Hasina, na kuiridhisha Amerika kwa kumteua Muhammad Yunus ambaye ni mfuasi wake. Rais wa zamani wa Amerika Bill Clinton aliwahi kumsifu akisema anastahili tuzo ya Nobel: (Profesa Muhammad Yunus alipata tuzo ya Nobel mnamo 2006 akishirikiana na Benki ya Grameen... Rais wa Amerika Bill Clinton alikuwa akitetea kupewa tuzo ya Nobel kwa Muhammad Yunus, na katika hotuba aliyoitoa mwaka 2002, Rais Clinton alimtaja Yunus kuwa ni mtu ambaye alipaswa kushinda tuzo ya Nobel muda mrefu uliopita. Al-Jumhur, Jumanne 6/8/2024). Ikumbukwe kuwa Hasina alikuwa akimpiga vita, ambapo mahakama ya Bangladesh ilimhukumu mnamo 1/1/2024 kifungo cha miezi 6 kwa tuhuma za kukiuka sheria za kazi katika mji mkuu Dhaka (Asharq Al-Awsat, 1 Januari 2024). Hivyo basi, Muhammad Yunus alikuwa anakubalika na Amerika, na ujanja wa Kiingereza umeweza kuondoa maandamano kwa kumwondoa Hasina... na kuiridhisha Amerika kwa kumteua mfuasi wake aliyezeeka... huku Uingereza ikibaki ikishikilia utawala nchini Bangladesh kupitia mkuu wa jeshi kama ilivyokuwa kabla ya Hasina kukimbia!
10- Hivyo basi, ushindani wa kimataifa nchini Bangladesh bado unaendelea. Na wale mawakala wanaofuata mtazamo wa mkoloni, huyu au yule, na kutafuta kutumikia maslahi ya makafiri wakoloni ni miongoni mwa wenye kukhasirika duniani na Akhera. Ama duniani, ni udhalili unaozunguka shingo zao kutokana na makosa yao. Na ama Akhera, ni adhabu kali:
سَيُصِيبُ الَّذِينَ أَجْرَمُوا صَغَارٌ عِنْدَ اللَّهِ وَعَذَابٌ شَدِيدٌ بِمَا كَانُوا يَمْكُرُونَ
"Wale waliofanya uhalifu itawafika udhalili mbele ya Allah na adhabu kali kwa sababu ya vitimbi walivyokuwa wakivifanya." (QS Al-An'am [6]: 124)
Lau wangekuwa na akili, wangezingatia yaliyowafika mawakala kama wao katika kila nchi, haswa katika nchi za Kiislamu; ima wafungwe, wauawe au wakimbie nchi kwa udhalili! Hawazingatii yaliyowapata waliotangulia, bali wanaendelea katika upotevu wao wakitangatanga! Basi kwa nini wasirudi kwa Mola wao ili washikamane na dini yake na kuwanusuru wale wanaofanya kazi ya kusimamisha dini ikiwa imewakilishwa na dola yake, dola ya Khilafah ya Rashida kwa njia ya Utume ambayo Mtume wa Allah ﷺ aliibashiri katika hadith yake tukufu iliyopokelewa na Ahmad na At-Tayalisi:
ثُمَّ تَكُونُ خِلَافَةٌ عَلَى مِنْهَاجِ النُّبُوَّةِ
"Kisha itakuwepo Khilafah kwa njia ya Utume."
Basi kwa nini wasirudi kwa Mola wao lau wangekuwa na akili?!
إِنَّ فِي ذَلِكَ لَذِكْرَى لِمَنْ كَانَ لَهُ قَلْبٌ أَوْ أَلْقَى السَّمْعَ وَهُوَ شَهِيدٌ
"Hakika katika hayo kuna mawaidha kwa mwenye moyo (wa kuzingatia) au anayetega sikio naye yupo macho." (QS Qaf [50]: 37)
11 Safar 1446 H 16/8/2024 M