Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Urusi Kujiunganishia Rasi ya Crimea

March 22, 2014
3044

Swali:

Urusi imejiunganishia Rasi ya Crimea, na Putin akatia saini hati ya hatua hiyo mnamo 2014/3/18. Je, hii inamaanisha kuwa kile kilichotokea ni hatua ya awali kwa Urusi kujiunganishia sehemu iliyobaki ya Ukraine, hususan ikizingatiwa kuwa mwitikio wa Magharibi ni dhaifu? Mwenyezi Mungu akujaze heri.

Jibu:

Tumeshataja hapo awali katika majibu yetu kwamba hali ya sasa ya kimataifa na kikanda haiwezeshi upande wowote kati ya pande tatu zinazohusika na Ukraine kuichukua Ukraine yote upande wake. Suluhu inayotarajiwa kati ya pande hizi tatu ni suluhu ya kati na kati... Kwa hivyo, Urusi kuichukua Ukraine yote ni jambo lisilowezekana kwa wakati huu, au angalau katika siku za usoni. Ikiwa Urusi itaweza kutulia katika Rasi ya Crimea, hii inamaanisha kuwa Magharibi, na hasa Amerika, itatulia katika sehemu iliyobaki ya Ukraine.

Kuhusu upande wowote kati ya pande tatu kuichukua Ukraine yote upande wake, jambo hili kama tulivyosema, ni gumu kwa sasa au angalau katika siku za usoni.

Inaonekana kwamba kile kinachoendelea hivi sasa kinatoa ishara ya suluhu ya kati na kati inayotekelezwa, ambayo ni Urusi kupanua ushawishi wake katika Rasi ya Crimea, na Magharibi, hususan Amerika, kupanua ushawishi wake katika sehemu iliyobaki ya Ukraine. Miongoni mwa ishara hizi ni:

  • Mawasiliano ya simu ya Waziri wa Ulinzi wa Urusi, Sergey Shoygu, na mwenzake wa Marekani, Chuck Hagel, mnamo Alhamisi 2014/3/20, ambapo Moscow ilisema haitashambulia mashariki mwa Ukraine. Alimwambia: "Kwamba vikosi vilivyokusanywa kando ya mpaka viko hapo tu kwa ajili ya kufanya mazoezi, na havina nia yoyote ya kuvuka mpaka kuingia Ukraine na kwamba havitaendesha kitendo chochote cha uchokozi."

  • Taarifa ya mamlaka ya mpito huko Kyiv ikisisitiza katika siku hiyo hiyo "kwamba itajibu 'kijeshi' kwa jaribio lolote la Urusi la kujiunganishia maeneo ya mashariki mwa Ukraine yanayozungumza Kirusi," ikifahamika kuwa ilikuwa imetoa tamko kuhusiana na Rasi ya Crimea hapo awali mnamo 2014/3/19 kuhusu utayari wa kuondoa vikosi vyake kutoka Crimea. Mkuu wa usalama nchini Ukraine alitangaza kuwa nchi yake inatayarisha mipango ya kuondoa vikosi na raia wake kutoka Rasi ya Crimea. Andriy Parubiy alisema kuwa lengo kuu ni kuhamisha vikosi na familia za Kiukreni kwa "njia za haraka na zenye ufanisi zaidi."

Hii inaonyesha sura ya suluhu ya kati na kati kwa kubadilishana kati ya Rasi hiyo na sehemu iliyobaki ya Ukraine! Na kwamba nia ya Ukraine katika maeneo ya mashariki ndilo jambo linalojitokeza zaidi, wakati kiwango cha nia katika Rasi hiyo kimepungua ikilinganishwa na maeneo ya mashariki.

Sura hizi zimezidi kuwa na nguvu zaidi kutokana na kile kilichotokea Ijumaa 2014/3/21 wakati wa mkutano wa kilele wa Ulaya uliofanyika Brussels, ambapo Umoja wa Ulaya na Waziri Mkuu wa mpito wa Ukraine, Arseniy Yatsenyuk, walitia saini vipengele vya kisiasa vya makubaliano ya ushirikiano. Haya ni makubaliano ambayo yataifanya Kyiv kuwa karibu na kupata uanachama katika umoja wa Ulaya. Makubaliano haya ndiyo yaliyosababisha mgogoro kati ya Ukraine na Urusi, na uamuzi wa Rais wa zamani wa Ukraine, Yanukovych, wa kutotia saini ulisababisha wimbi kubwa la maandamano na migomo kwa upande wa Waukreni...

Hizi zote ni ishara za aina ya suluhu ya kati na kati... Hata hivyo, kama tulivyosema katika majibu yetu ya awali, Ukraine itabaki kuwa bomu linaloweza kulipuka wakati wowote ambapo mazingira ya kimataifa au kikanda yatabadilika kwa faida ya Urusi au Magharibi. Wakati huo, kila upande utajaribu kuitazama Ukraine yote na kujaribu kuimiliki kulingana na mazingira ya kimataifa ya wakati huo... Kwani Ukraine ni ubavu wa Urusi, na wakati huo huo ni lango la Ulaya...

Hadi mazingira ya kimataifa na kikanda yabadilike, suluhu ya kati na kati itabaki kufanyiwa kazi, na inaweza kusababisha aina fulani ya utulivu, "utulivu wa muda mfupi"... Ama utulivu wa kudumu, hususan katika Rasi ya Crimea, hautakuwepo isipokuwa kwa kurejea kwake katika hali ilivyokuwa kabla ya kukaliwa kwa mabavu na Urusi tangu mwishoni mwa karne ya kumi na nane na mapema karne ya kumi na tisa, yaani, pale itakapokuwa sehemu ya Dola ya Khilafah inayokuja, InshaAllah.

Share Article

Share this article with your network