Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Vichocheo vya Mapambano baina ya Madola

November 11, 2014
3823

** (Silsila ya Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Watembeleaji wa Ukurasa Wake wa Facebook "Fikri") **

Jibu la Swali

Vichocheo vya Mapambano baina ya Madola

Kwa: Bw. Ahmed Fouad Fouad

Swali:

Bismillahir Rahmanir Rahim, Assalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh. Imekuja katika kitabu cha Mafahim Siyasiyah (Dhana za Kisiasa) katika mada ya "Vichocheo vya Mapambano baina ya Madola" ukurasa wa 54, aya ya kwanza, mstari wa kwanza: "Mapambano ya kimataifa tangu kuchomoza kwa historia hadi kusimama kwa Saa (Qiyama) hayatoki nje ya moja ya vichocheo viwili: Ama kupenda enzi na ufahari, au kukimbilia manufaa ya kimaada." Kisha katika ukurasa huo huo, aya ya kabla ya mwisho, mstari wa 15 imeelezwa: "Na kichocheo hatari zaidi cha mapambano baina ya madola ni kichocheo cha ukoloni (Istiamar) kwa aina zake zote."

Swali: Katika aya ya kwanza, vichocheo vya mapambano baina ya madola vimeainishwa na kudhibitiwa katika vichocheo viwili pekee na si vinginevyo pale iliposemwa "hayatoki nje ya... moja ya vichocheo viwili," lakini katika aya ya pili kumetajwa kichocheo cha tatu ambacho hakikutajwa katika aya ya kwanza nacho ni "ukoloni". Na kwa njia nyingine: Je, vichocheo vya mapambano ya kimataifa ni viwili au vitatu? Kwani msomaji wa aya hizi mbili anahisi kuwepo kwa mgongano na tofauti baina yake, sasa inawezekanaje kuoanisha kati ya aya hizo? Kwani ikiwa vichocheo vya mapambano ya kimataifa ni viwili, kwa nini kimetajwa kichocheo kipya cha tatu ambacho ni ukoloni?

Jibu:

Wa Alaikum Salam Warahmatullahi Wabarakatuh.

Hakuna mgongano kati ya yale yaliyokuja katika kitabu cha Mafahim Siyasiyah ukurasa wa 54 mwanzoni mwake kwamba vichocheo vya mapambano ya kimataifa vimeishia katika vichocheo viwili navyo ni kichocheo cha kupenda enzi na ufahari na kichocheo cha kukimbilia manufaa ya kimaada, na yale yaliyokuja katika ukurasa huo huo baada ya hapo kwamba kichocheo cha ukoloni (Istiamar) kwa aina zake zote ni miongoni mwa vichocheo hatari zaidi vya mapambano ya madola. Hiyo ni kwa sababu kichocheo cha ukoloni kimeingia chini ya kichocheo cha kukimbilia manufaa ya kimaada; kwani ukoloni ni njia ya mfumo wa kibeberu (Capitalism) katika kupata manufaa kwa mujibu wa kipimo chao ambacho ni "unafuu" (Utilitarianism). Hii ina maana kwamba ukoloni unarudi kwenye kichocheo kilichotangulia kabla yake nacho ni kichocheo cha kukimbilia manufaa ya kimaada, na wala si kichocheo kipya tofauti na vile viwili vilivyotajwa mwanzoni mwa ukurasa. Na lau ungezingatia kwa makini ungekuta kuwa kimetajwa jambo jingine ambalo linaweza kudhaniwa kuwa ni kichocheo kingine... lakini maandishi yalirudisha jambo hilo kwenye kichocheo cha kupenda enzi na ufahari. Imekuja katika ukurasa huo huo yafuatayo:

"(Ama kichocheo cha kuzuia kukua kwa nguvu ya dola nyingine, kama ilivyotokea kwa mataifa dhidi ya Napoleon, na kama ilivyotokea kwa mataifa dhidi ya Dola ya Kiislamu, na kama ilivyotokea kwa mataifa dhidi ya Ujerumani ya Kinazi, hicho kinaingia katika kupenda enzi; kwa sababu ni kusimama mbele ya enzi ya wengine.)" Mwisho.

Hivyo, kama ambavyo kichocheo cha kuzuia kukua kwa nguvu ya dola nyingine hakikuhesabiwa kuwa ni kichocheo kilicho nje ya vichocheo viwili vilivyotajwa, vivyo hivyo ukoloni hauhesabiwi kuwa ni kichocheo kilicho nje ya vichocheo viwili vilivyotajwa; kwa sababu hivi vichocheo viwili ni vichocheo vikuu ambavyo chini yake huingia mambo mengine yanayofungamana navyo.

Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

Kiunganishi cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Facebook wa Amir

Kiunganishi cha jibu kutoka kwenye tovuti ya Amir

Kiunganishi cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Google Plus wa Amir

Share Article

Share this article with your network