** (Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata bin Khalil Abu al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Wageni kwenye Ukurasa Wake wa Facebook "Siasa")**
Jibu la Swali: Nafasi ya Iran Katika Eneo Hili
Kwa Mais Bader
Swali:
Assalamu Alaikum wa Rahmatullahi wa Barakatuh. Sheikh wangu mtukufu, Mwenyezi Mungu akulinde na akuhifadhi. Swali: Kwa nini Marekani imeiruhusu Iran kupata ongezeko hili la kasi kiasi katika uwezo wake wa kijeshi wa aina mbalimbali mpaka imekuwa miongoni mwa nchi muhimu katika eneo hili kwa upande wa kucheza nafasi zenye ushawishi katika mkondo wa matukio nchini Iraq, Syria, Ghuba na eneo linalowaka moto kwa ujumla? Na ni ipi siasa ya Marekani katika kuidhibiti nafasi hii iliyoponyoka? Mwenyezi Mungu akulipe kheri...
Jibu:
1- Kusema kwamba Iran ina nafasi iliyoponyoka (isiyodhibitiwa) katika eneo hili ni kauli isiyo sahihi. Iran inakwenda sambamba na Marekani katika masuala yote ya eneo hili... Iran ni nchi kitovu katika siasa za Marekani katika eneo hili, na Marekani inaitegemea nchini Iraq, Syria, Yemen, Afghanistan, Lebanon na kwingineko... Na mwenye kuangalia matendo ya Iran kwa kina atalikuta hilo liko wazi. Viongozi kadhaa wa Iran wametamka wazi kuwa ushirikiano wa Iran na Marekani ndio ulioiwezesha Marekani kuikalia kwa mabavu Afghanistan na Iraq... Na hivyo ndivyo ilivyo katika masuala mengine.
2- Tulitoa jibu la swali mnamo tarehe 14 Shawwal 1434 AH sawia na 21/08/2013 BK lenye kichwa cha habari: "Ukweli wa Iran kuhusiana na siasa za Marekani?" Na tulibainisha humo kwa kina ukweli wa uhusiano wa Iran na Marekani na ushirikiano wa Iran nayo katika masuala ya eneo hili. Unaweza kurejea jibu hilo ili kufahamu yaliyomo, na hapa nakunukulia sehemu ya jibu hilo:
(- Vitendo vyote vya kisiasa katika eneo hili ambavyo Iran imevifanya, vyote vimefanyika kwa maelewano na uwiano na miradi ya Marekani:
Nchini Lebanon, ilianzisha chama (Hezbollah) kutokana na wafuasi wa madhehebu yake na kukipatia silaha mpaka kikawa jeshi maalumu huko lililotengana na jeshi la Lebanon, na utawala wa Lebanon ukakitambua chama hicho na silaha zake, huku ikifahamika kuwa utawala wa Lebanon ni wa kisekula unaofuata siasa za Marekani. Utawala wa Lebanon haukuruhusu vyama vingine kubeba silaha wala haukutambua silaha za vyama vingine. Na chama cha Iran nchini Lebanon kilifanya kazi ya kuuunga mkono utawala wa Syria uliofungamana na Marekani kama ilivyofanya Iran, na Marekani haukuuzuia utawala wa Lebanon kukiruhusu chama cha Iran kuingilia kati nchini Syria ili kuunusuru utawala wa Bashar Assad wa kisekula nchini humo. Bali kuna idhini ya Marekani ya kimya kimya kwa chama hicho kuingilia kati nchini Syria bila kuzuiliwa na jeshi la Lebanon.
Marekani ilipoikalia kwa mabavu Iraq, ilikumbana na upinzani (resistance) ambao haukuutarajia, hivyo ikaiingiza Iran nchini Iraq ili kuisaidia kwa kuwashawishi wafuasi wa madhehebu yake ili kuwazuia wasichukue hatua dhidi ya uvamizi huo. Badala yake, iliwafanya wasimame dhidi ya upinzani na kuupinga, na kuupa utambuzi (legitimacy) uvamizi huo pamoja na utawala uliowekwa na Marekani huko, hususan baada ya mwaka 2005 wakati Marekani iliporuhusu muungano wa vyama vinavyoiunga mkono Iran kufika madarakani chini ya uongozi wa Ibrahim al-Jaafari na kisha Maliki. Serikali hizi ziliundwa na Marekani na zimefungamana nayo. Serikali ya Maliki, inayoungwa mkono na Iran, ilisaini mikataba ya kiusalama na kimkakati na Marekani ili kulinda ushawishi wake baada ya kumalizika kwa uvamizi wake nchini Iraq rasmi. Hilo linaashiria kuridhiwa na Marekani kwa nafasi ya Iran, ambayo maafisa wake walikiri kushirikiana na Marekani katika kuivamia Iraq na kufanya kazi ya kuhakikisha utulivu wa ushawishi wa Marekani nchini Iraq. Iran ilifungua ubalozi wake nchini Iraq mara tu baada ya uvamizi, na punde tu Jaafari alipochaguliwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran wa wakati huo, Kamal Kharrazi, alitembelea Baghdad mwaka 2005 wakati uvamizi ukiwa kileleni. Pande zote mbili zililaani harakati za upinzani dhidi ya uvamizi kwa kisingizio cha kulaani ugaidi nchini Iraq. Ziara ya Jaafari nchini Iran na kusainiwa kwa mikataba kadhaa, ukiwemo mkataba wa ushirikiano wa kiintelejensia kati yao kwa ajili ya kuweka usalama na kufuatilia vituo vya mpakani, na kuunganisha mji wa Basra na mtandao wa umeme wa Iran, na kujenga bomba la mafuta kati ya Basra na Abadan...
Ama uhusiano wa Iran na utawala wa Syria ni wa zamani tangu kulipuka kwa intifada ya kwanza mwanzoni mwa miaka ya themanini ya karne iliyopita, ambapo iliunga mkono utawala wa Syria katika kuwakandamiza watu wa Syria Waislamu katika kipindi hicho. Hilo lilikuwa ni kwa ajili ya kuuhifadhi utawala huo ndani ya mradi wa Marekani unaounga mkono utawala huo chini ya uongozi wa vibaraka wake, familia ya al-Assad. Iran inajua kuwa ni utawala wa kisekula, wa chama cha Ba'ath na wa kizalendo (nationalist), sawa na utawala wa Saddam ambao ilikuwa ikipigana nao, na hauna uhusiano na Uislamu. Bali unapigana na Uislamu na watu wake, na inatambua kuwa utawala huo umefungamana na Marekani. Hivyo, Iran haikuchukua jukumu la kutetea haki za Waislamu, bali ilifanya kinyume chake: ilipigana nao na kuunusuru utawala wa kikafiri wenye kijinai, na bado inaendelea kufanya hivyo mpaka sasa. Utawala wa Iran unadumisha uhusiano wa karibu na uongozi wa Syria, na uhusiano huo ulihusisha nyanja za kijeshi, kiuchumi na kisiasa. Iran ilisafirisha silaha nyingi kuunga mkono utawala wa Assad na kuupatia mafuta na gesi kwa bei nafuu kutokana na kukosekana kwa akiba ya nishati nchini Syria. Uhusiano wa kisiasa unaweza kuonekana hasa katika uingiliaji kati wa Iran katika mapinduzi ya Syria wakati utawala wa Assad ulipokuwa karibu kuanguka. Isingekuwa uingiliaji kati wa Iran kupitia kutuma vikosi vya Walinzi wa Mapinduzi (Revolutionary Guard), vikosi vya chama cha Iran (Hezbollah), na wanamgambo wa Maliki wafuasi wa Iran, basi Bashar na utawala wake ungeanguka. Mauaji ya kinyama ya Al-Qusayr, Homs, na leo mauaji ya kinyama ya kikemia huko Ghouta na mengineyo ni mashahidi wa uingiliaji kati huo.
Nchini Afghanistan, Iran iliunga mkono uvamizi wa Marekani na kuunga mkono katiba iliyowekwa na serikali iliyoundwa na Marekani chini ya uongozi wa Karzai, ikiwa ni huduma kwa Marekani. Iran ilihakikisha usalama kaskazini mwa nchi hiyo wakati Marekani iliposhindwa kuwashinda Taliban. Rais wa zamani wa Iran, Rafsanjani, alisema: "Kama vikosi vyetu visingesaidia katika kupigana na Taliban, Wamarekani wangezama katika kinamasi cha Afghanistan." (Gazeti la Asharq Al-Awsat 09/02/2002). Mohammad Ali Abtahi, Makamu wa Rais wa zamani wa Iran (Khatami) wa masuala ya kisheria na bunge, alisema katika mkutano wa "Ghuba na Changamoto za Baadaye" uliofanyika katika imarati ya Abu Dhabi jioni ya tarehe 13/01/2004: "Isingekuwa ushirikiano wa Iran, Kabul na Baghdad zisingeanguka kwa urahisi hivi. Lakini tulipata zawadi ya kuwa ndani ya mhimili wa uovu (axis of evil)!" (Islam Online Net 13/01/2004). Rais Ahmadinejad alikariri kauli kama hizo alipokuwa ziarani New York kuhudhuria mikutano ya Umoja wa Mataifa, katika mahojiano na gazeti la New York Times mnamo tarehe 26/09/2008 ambapo alisema: "Iran ilitoa msaada kwa Marekani kuhusiana na Afghanistan, na matokeo ya misaada hii yalikuwa ni Rais wa Marekani kutoa vitisho vya moja kwa moja vya kuanzisha mashambulizi ya kijeshi dhidi yetu. Pia nchi yetu imetoa misaada kwa Marekani katika kurejesha utulivu na usalama nchini Iraq.") Mwisho wa nukuu.
3- Ushahidi wa yote yaliyotangulia ni jinsi mazungumzo ya nyuklia yalivyoishia na msisitizo wa Marekani wa kufunga faili hili ili kuboresha uhusiano wa wazi na Iran ili kutekeleza kile ambacho Marekani imekipangia kama nafasi katika eneo hili kwa kisingizio cha maslahi ya pamoja, na bila kifuniko hata cha pazia nyembamba kama ilivyokuwa hapo awali! Rais wa Marekani alitoa hotuba mbele ya Ikulu ya Marekani (White House) iliyohusu makubaliano ya mwisho ya nyuklia na Iran, ambapo aliyataja makubaliano hayo kuwa "ni mazuri yanayofikia malengo yetu ya kimsingi" na akasema "kwa upande wa watu wa Iran, tuko tayari kufanya kazi kwa ajili ya maslahi ya pamoja" (Radio Sawa ya Kimarekani 02/04/2015)... Hivyo, matamshi ya Rais wa Marekani yako wazi kwamba anataka kufanya kazi na Iran chini ya jina la maslahi ya pamoja! Na ni maslahi gani ya pamoja na "Shetani Mkubwa" isipokuwa kufanikisha miradi ya Marekani katika eneo hili?!
4- Kisha kilichotokea na kinachoendelea kutokea katika mipango iliyooanishwa kati ya Marekani, Iran, na Wahouthi katika matukio ya Yemen! Ama kuhusu uhusiano wa Wahouthi na Iran, hauhitaji ushahidi, kwani unajulikana kama moto juu ya kilele cha mlima... Na ama kuhusu msaada wa Marekani kwa Wahouthi, kila mwenye macho na busara analitambua hilo. Marekani inatenda nchini Yemen kwa kiburi chake kinachojulikana, yaani kwa nguvu ya silaha na ukandamizaji. Wahouthi waliikalia kwa mabavu Sana'a na miji mingine, wakakamata na kuua kwa kisingizio cha "mapinduzi ya watu na kamati za watu...", na Marekani ilikuwa ikiunga mkono harakati hizi za Wahouthi kisiasa na kiusalama:
Kisiasa, Marekani haiwaoni Wahouthi kuwa ni magaidi kama Al-Qaeda, bali inawaona kama harakati ya kisiasa. Balozi wa Marekani Matthew Tueller alisema katika mkutano wake na waandishi wa habari mnamo 18/09/2014: "Tunatofautisha kati ya makundi yale yaliyoshiriki katika mchakato wa kisiasa. Harakati ya Kihouthi ilishiriki katika mkutano wa majadiliano ya kitaifa na hilo lilipelekea matokeo mengi chanya, na wana msimamo wa kisiasa na matamanio halali... Hivyo, tunamuunga mkono Houthi na harakati yake wafanye vitendo vile vile vinavyofanywa na makundi na vyama vya kisiasa" (Tovuti ya Monitor Press).
Kiusalama, Wahouthi walipoingia Sana'a, jeshi na polisi waliwapinga na kuwaua Wahouthi saba mnamo 09/09/2014, na mizani ilikuwa karibu kuegemea upande wa (Rais) Hadi. Lakini Marekani iliharakisha kumtuma Jamal Benomar, mjumbe wa Umoja wa Mataifa "au mjumbe wa Marekani kwa uhalisia," naye akamshinikiza Hadi na kufanya suala hilo kuwa la kusuasua kwa kutoa wito wa mazungumzo. Alitoa mwanga wa kijani kwa Wahouthi kuzidisha harakati zao wakati wa mazungumzo wakisaidiwa na shinikizo la Marekani kupitia Jamal Benomar dhidi ya Hadi.
5- Aidha, matukio ya hivi karibuni yanathibitisha uungaji mkono huu, na nakunukulia baadhi ya yaliyokuja katika jibu la swali la tarehe 27/03/2015 kuhusu suala hili (...Marekani imewapatia Wahouthi kupitia Iran aina mbalimbali za silaha na zana ili waweze kuitawala Yemen kwa nguvu kwa sababu inatambua kuwa tabaka la kisiasa kwa kiasi kikubwa ni zao la Waingereza... Hivyo Wahouthi walidhani kuwa wana nguvu itakayowafanya waitawale Yemen, wakamzingira Rais ili wachukue kutoka kwake kile wanachotaka kupitia sheria anazotoa. Alikuwa akikubali kisha anachelewa kutekeleza mpaka walipomuweka chini ya kizuizi cha nyumbani, akawatoroka na kwenda Aden, wakamfuata akawatoroka mara ya pili... Marekani ilitambua kuwa wafuasi wake, Wahouthi, wameingia katika mkwamo; wamesambaa nchini, hawawezi kutawala wala hawawezi kurejea kwenye nguvu waliyokuwa nayo huko walikotokea. Marekani ikaona iwaokoe kwa operesheni ya kijeshi yenye mipaka itakayoua ndege wawili kwa jiwe moja: iwaonyeshe kama waliodhulumiwa baada ya kukita katika fikra za watu kuwa wao ndio wavamizi, na kutengeneza mazingira ya mazungumzo yenye shinikizo ili kupata suluhu ya kati kama ilivyo desturi yake kwa lile ambalo haiwezi kulichukua peke yake... Hili limebainika kwa kufuatilia yaliyotokea na yanayoendelea; Saudi Arabia ilishauriana na Marekani kabla ya operesheni ya kijeshi, na wanaotekeleza nafasi ya kijeshi inayofanya kazi ni vibaraka wa Marekani, hususan Salman Mfalme wa Saudi Arabia na Sisi Rais wa Misri. Ama nchi nyingine za Ghuba, Jordan, na Morocco ziko karibu zaidi na nafasi ya kisiasa kulingana na desturi ya Uingereza ya kwenda sambamba na Marekani ili iwemo pichani na iwe na fungu katika mazungumzo yaliyopangwa, na kugawana keki ya ushawishi... Na ingawa operesheni za kijeshi zenye shinikizo wakati mwingine hufanikiwa kufungua mlango wa mazungumzo, lakini wakati mwingine hushindwa, na mambo huvurugika upya, na Yemen inayoungua moto huteseka, nchi ambayo ilikuwa yenye furaha siku si nyingi zilizopita... siku ambapo ardhi yake takatifu haikukanyagwa na vibaraka na makafiri wakoloni.) Mwisho wa nukuu.
Kwa kuzingatia yaliyotokea na matokeo yake, inabainika kuwa Marekani ndiyo iliyokuwa ikidhibiti mkondo wa mambo. Mashambulizi ya Saudi Arabia yalilenga silaha ambazo gharama yake ililipwa na Waislamu, na wahanga wengi ni raia na wachache ni Wahouthi... Na Iran haikuingilia kati bali ilibaki ikitazama kwa mbali ingawa sauti zilikuwa zikipiga kelele kuhusu operesheni ya Asifat al-Hazm (Dhoruba ya Maamuzi) inayoangukia vichwani mwa Wahouthi!
Hili linaonyesha kuwa mratibu (maestro) wa harakati hizi anadhibiti mdundo ili kufikia suluhu zinazowaokoa Wahouthi na si kuwaangamiza, na kuwapa fungu lenye uzito na si kuwatenga... Na kwamba Saudi Arabia inalitambua hilo na inaendesha operesheni zake za Asifat al-Hazm na tumaini lake kulingana na mdundo huu... Pia Iran inalitambua hilo na inatazama bila kuingilia kijeshi kulingana na mdundo huu...! Bali hata ilikubali kukaguliwa kwa meli zake zilizobeba misaada kwa ajili ya Yemen kabla ya kufika kwenye bandari za Yemen, kwa sababu Marekani inataka hivyo, na Iran ikatii...! Hivyo, kama vile Saudi Arabia inavyofuata nidhamu katika operesheni zake kulingana na maelekezo ya Marekani, ndivyo ilivyo Iran; wote wawili wanatambua lengo la vitendo hivi vya moto tulivyovibainisha. Na sasa wanaelekea kwenye utulivu wa moto unaotangulia suluhu za baridi!
6- Muhtasari ni kwamba Iran "haiponyoki" kutoka kwenye siasa za Marekani, bali haitoki nje yake, na yote hayo ni kwa kisingizio cha maslahi ya pamoja na "Shetani Mkubwa"!
Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu al-Rashtah
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir kwenye Facebook
Kiungo cha jibu kutoka kwenye tovuti ya Amir
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir kwenye Google Plus