Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Kashfa ya Ufisadi wa Kisiasa na Kifedha Inayoitingisha Serikali ya Uturuki

December 29, 2013
3171

Swali:

Mnamo tarehe 25/12/2013, Erdogan alitangaza kuundwa kwa serikali mpya, ambapo alibadilisha mawaziri kumi, baada ya mawaziri watatu kujiuzulu, akiwemo Waziri wa Mazingira ambaye naye alimtaka Erdogan kujiuzulu. Hii ilitokana na kashfa ya ufisadi wa kisiasa na kifedha ambayo imekuwa ikiitingisha serikali ya Uturuki kwa takriban siku kumi. Kabla ya hapo, tarehe 20/12/2013, watu 24 walikamatwa kati ya 49 wa karibu na serikali na chama chake ambao walikuwa wamefikishwa kwenye uchunguzi tarehe 17/12/2013 kwa tuhuma za kufanya vitendo vya ufisadi... Kufuatia hilo, Waziri Mkuu alianzisha shambulio kali dhidi ya wale waliosababisha kufichuliwa kwa watu hao na kupelekea kukamatwa kwao, na aliwaondoa makumi ya wakuu wa usalama ambao wanachukuliwa kuwa ni wafuasi wa kundi la Fethullah Gülen, na akaelekeza ghadhabu yake yote kwa kundi hili... Vilevile alimkosoa Balozi wa Marekani nchini Uturuki. Swali ni: Ni nini kimetokea mpaka uhusiano wa ushirikiano na uungaji mkono kati ya Erdogan na kundi la Fethullah Gülen kugeuka kuwa uhusiano wa uhasama? Naomba ufafanuzi wa kina kadiri inavyowezekana kwani mambo yametuchanganya baada ya mienendo ya Erdogan dhidi ya kundi hilo. Kisha, nini maana ya tamko la Erdogan dhidi ya Balozi wa Marekani, ikizingatiwa kuwa uhusiano wa Erdogan na Marekani ni wa karibu sana kiasi cha kusifiwa kuwa yeye ni mtu wa Marekani nchini Uturuki?

Jibu:

Kwa kupitia matukio yaliyotangulia na matokeo yake, jibu la swali hapo juu linabainika:

1- Kutangazwa kwa uchunguzi huu na kukamatwa kwa watu kulichochea serikali, chama chake, na kiongozi wake Erdogan kwa sababu kulikuwa kumeulenga watu wa karibu na serikali na chama tawala. Miongoni mwao ni watoto wanne wa mawaziri serikalini, mkuu wa manispaa ya eneo la Fatih huko Istanbul, na mkurugenzi wa Halkbank... Miongoni mwao pia ni wafanyabiashara wa karibu na chama hiki. Hili linakuja wakati Uturuki ikijiandaa kwa uchaguzi wa serikali za mitaa baada ya miezi mitatu tarehe 30/3/2014, ambapo Erdogan alikuwa akitumaini kuimarisha umaarufu wake kwa ajili ya kugombea urais wa Jamhuri utakaofanyika miezi michache baadaye tarehe 26/8/2014. Upigaji kura wa urais utakuwa wa moja kwa moja na wananchi, tofauti na ilivyokuwa ikifanyika hadi sasa ambapo Rais alikuwa akichaguliwa na bunge. Kwa sababu hii, hisia za Erdogan zilikuwa za ghadhabu sana, akafanya mabadiliko ya wakuu wa usalama wafuasi wa kundi la Fethullah Gülen, na akawatishia watu wa kundi hilo katika idara ya mahakama kama ilivyoelezwa katika gazeti la Milliyet tarehe 18/12/2013 kwa kusema: "Lakini wafanyakazi katika nyanja ya mahakama lazima waheshimu haki na sheria, na wasichukue hatua kwa maelekezo kutoka kwa upande fulani... Kwani hakuna haki kwa yeyote anayefanya kazi katika nyanja ya mahakama kufanya shinikizo na kutoa amri na maelekezo kwa mamlaka ya utendaji (serikali) kwa namna isiyo ya kawaida. Ikiwa mtaielekeza mahakama ili kuleta aina fulani ya shinikizo kwa watu, basi tutafanya kile tunachopaswa kufanya, na tumekwishakifanya," akiashiria kwa kusema: "na tumekwishakifanya" kuondolewa kwa idadi ya wakuu wa usalama... Na ili Erdogan apate uungaji mkono kwa msimamo wake dhidi ya kundi la Gülen, alitoa tamko linaloashiria kuwa kuna njama ya nje, akisema: "Matukio yaliyotokea siku za hivi karibuni yana mwelekeo wa kimataifa, kwani ni operesheni iliyofanywa na watekelezaji wa ndani wanaofuata maelekezo ya nje" kama ilivyoelezwa katika gazeti hilo hilo... Kisha baadaye akiwa Samsun wakati wa ziara yake ya kuhamasisha maoni ya umma upande wake tarehe 20/12/2013 alitamka: "Balozi anaingia katika mzunguko wa baadhi ya vitendo vya njama. Kwa hiyo namuambia: afanye kazi yake, ikiwa mmetoka (enyi Balozi) nje ya mzunguko wa kazi yenu, basi serikali yetu itakwenda katika njia yake hadi kufikia mwisho wa mamlaka iliyo nayo..." (Milliyet 21/12/2013). Hapa alikuwa akimashiria Balozi wa Marekani, akitolea maoni habari iliyochapishwa na baadhi ya magazeti ya Uturuki (Star, Yeni Şafak, na Akşam) kuhusu mkutano wa Balozi wa Marekani huko Ankara, Ricciardone, na baadhi ya wawakilishi wa Umoja wa Ulaya tarehe 17/12/2013... Habari hiyo ilikuwa na ishara za kuingilia kati kwa Balozi wa Marekani katika matukio hayo... Hivyo, Erdogan alikuwa katika kilele cha ghadhabu katika matamshi yake dhidi ya kundi la Gülen, na katika kilele cha tahadhari dhidi ya Balozi wa Marekani.

2- Kuhusu kundi la Gülen, inajulikana kuwa kundi hili limemuunga mkono Erdogan na chama chake tangu aliposhika madaraka mwaka 2002... Serikali ililiruhusu kuingia katika taasisi nyingi, mbali na kusimamia idadi kubwa ya vituo vya masomo ya ziada (tuiton) ambavyo vilikuwa vikilikusanyia kundi hilo pesa kutoka kwa ada za wanafunzi, na wakati huo huo kuwatayarisha wanafunzi wengi miongoni mwao kufanya kazi na kundi hilo... Haya yote yalikuwa wazi na si siri, na Erdogan alikuwa haogopi hatari yoyote kutoka kwao, hasa kwa kuwa uhalisia wa kundi hilo ni sawa na sheikh na wafuasi wake, yaani si shirika la kisiasa lenye programu na linaloshindania utawala ili kuzitekeleza... Kwa sababu hiyo, Erdogan alikuwa hawapi umuhimu mkubwa, hasa kwa kuwa kundi hilo lilikuwa ni mkono wa Marekani kama alivyo Erdogan, ingawa mbinu na majukumu vilitofautiana... Wote wawili walishiriki katika kudhibiti taasisi na kuvunja muundo wa kutaifa (nationalist) wenye usetiri wa Waingereza. Hilo lilifanyika kwa Marekani kuweza kupenya katika taasisi kupitia kundi hilo, na pia Marekani kuweza kupenya jeshini na katika duru za kisiasa kupitia Erdogan na chama chake... Hivyo, chama na kundi hilo walikuwa ni mikono miwili ya Marekani nchini Uturuki, na uhusiano wao ulikuwa wa ushirikiano, urafiki, na uaminifu kwa marejeo mmoja... Hii ni pamoja na kwamba Marekani mwanzoni mwa utawala wa Erdogan ilikuwa ikitaka umoja wenye nguvu wa watu wake nchini Uturuki kwa sababu nguvu za Waingereza wakati huo zilikuwa bado zina ushawishi katika mahakama na jeshini, jambo ambalo Marekani ilikuwa ikiliogopa... Haya yote yaliifanya Marekani kuwa na hamu ya uhusiano kati ya Erdogan na chama chake na kati ya kundi la Fethullah Gülen uwe tulivu bila mivutano, na hali hiyo iliendelea hadi mwanzoni mwa mwaka 2010... Ambapo yalitokea matukio mwaka huo yaliyopandikiza mbegu za tofauti kati ya Erdogan na Fethullah Gülen. La kwanza lilikuwa ujumbe wa Fethullah Gülen kuhusu tukio la meli ya Mavi Marmara iliyoshambuliwa na umbile la Kiyahudi alfajiri ya tarehe 31/5/2010. Gülen alisema katika ujumbe wake: "Kusafiri kwa meli hiyo na kuingia kwake katika maji ya kimataifa ya Israel ni kosa kubwa, na ilikuwa ni lazima kupata idhini kutoka Tel Aviv." Kwa hiyo alikuwa akilaumu msimamo wa meli hiyo, na kusimama upande wa kitendo cha umbile la Kiyahudi na haki yao ya kuua baadhi ya abiria wake, wakati huo Erdogan alikuwa akisimama upande wa meli na abiria. Erdogan alichukulia ujumbe wa Fethullah Gülen kama ulioelekezwa kwake binafsi. Pamoja na hayo, wote wawili walivuka yaliyotokea, na uhusiano mzuri ulirejea kati yao, na Fethullah alikuwa muungaji mkono wa kura ya maoni aliyoitisha Erdogan tarehe 12/9/2010 kuhusu marekebisho ya katiba... Ambapo Fethullah Gülen alikuwa na mchango katika kupendelea upande wa "ndiyo" katika kura hiyo. Gülen alitoa wito kutoka makazi yake Marekani kwa watu wa Uturuki, wiki chache kabla ya tarehe ya kura ya maoni, kukubali marekebisho ya katiba akieleza kuwa "marekebisho haya, ingawa ni madogo, yana mambo makubwa yatakayofuata na ni hatua kuelekea uhuru zaidi na utekelezaji wa kidemokrasia." Erdogan alishinda katika kura hiyo ya maoni ambapo kukubaliwa kwa marekebisho ya katiba kulifikia 58% na sherehe kubwa ilifanyika mbele ya makao makuu ya chama tawala.

Kufuatia kukubaliwa huku, mabadiliko makubwa yalitokea katika taasisi yaliyopelekea kujazwa kwa nafasi zilizoachwa wazi na watu wa kutaifa kwa kuajiri watu wa kundi la Gülen. Vilevile palikuwa na mabadiliko katika muundo wa Baraza Kuu la Majaji na Waendesha Mashtaka, na nafasi mpya zilizoanzishwa, ambazo zote zilikuwa kwa faida ya kundi hilo, jambo lililolifanya kuwa na ushawishi mkubwa katika taasisi hizi madhubuti, na kundi likawa linadhibiti idadi ya mahakama muhimu na mahakama maalum zilizo chini ya Baraza Kuu la Majaji na Waendesha Mashtaka.

3- Kisha mambo yakawa magumu kati yao baada ya hapo mwanzoni mwa 2011 ambapo Erdogan aligundua kuwa kupenya kwa kundi hilo katika usalama na mahakama kumeanza kumsumbua, na ni jaribio la kutawala... na si kama ilivyokuwa awali kama uungaji mkono kutoka kwa kundi kwake. Tangu wakati huo, hatua na majibu ya kishindani yalianza kati ya Erdogan na kundi la Gülen:

a- Tangu mwanzoni mwa mwaka 2011, Erdogan alianza kufanya kazi ya kudhoofisha ushawishi wa kundi hili, akawaondoa wanachama wa kundi hili kwenye orodha ya wagombea wa bunge katika uchaguzi wa 2011, kisha akaanza kuwaondoa baadhi ya wanachama wa kundi hili kutoka vituo vya usalama na baadhi ya mahakama...

b- Kufuatia hilo, vyombo vya habari vya kundi hili vilianzisha shambulio dhidi ya Erdogan... Havikuishia hapo, bali vilifanya kampeni ya kukuza yaliyomo katika mkanda wa sauti uliovuja mnamo Septemba 2011 kuhusu mazungumzo ya mkuu wa shirika la ujasusi la taifa, Hakan Fidan, na viongozi wa chama cha PKK (chama cha Ocalan) huko Oslo kati ya mwaka 2009 na 2010 kwa ajili ya kutatua suala la Kikurdi. Mazungumzo hayo yalikuwa yakifanyika kwa siri wakati huo ili kuweka mazingira kabla ya kutangazwa... Vidole vya tuhuma vilielekezwa kwa kundi hili kwamba lina uhusiano na usambazaji wa mkanda huo. Mwendesha mashtaka mkuu anayeliunga mkono kundi hilo aliomba tarehe 7/2/2012 kufanya uchunguzi na Fidan, mkuu wa ujasusi...

c- Erdogan alichukulia suala hili kama la kufa na kupona kwake kwa sababu lingemgusa Waziri Mkuu na kufichua siri zinazohusiana na mawasiliano ya nchi kupitia idara yake ya ujasusi na chama cha PKK. Erdogan alimkinga mkuu wa ujasusi na ufuatiliaji wowote wa kisheria kwa kupitisha sheria bungeni inayohusiana na hilo: kwamba "hairuhusiwi kuwachunguza wafanyakazi katika sekta ya ujasusi na watu waliopewa jukumu la kufanya kazi maalum na Waziri Mkuu isipokuwa kwa idhini yake." Kufuatia hilo pia, Erdogan alifanya mchakato wa kusafisha idara za ujasusi huko Ankara, Istanbul, na Izmir, na pia alifanya usafishaji katika sekta ya elimu na sekta ya mahakama kwa watu waliohesabiwa kuwa ni wa kundi la Gülen...

d- Kisha kukaja hatua iliyoliathiri kundi hilo kwa nguvu, ambayo ni mpango wa Erdogan wa kufuta vituo vya masomo ya ziada (tuiton), na kuvigeuza kuwa shule za binafsi zinazofundisha mtaala wa nchi au kuwa shule za sekondari. Takriban vituo elfu moja vilikuwa vikimilikiwa na kundi hilo, na vilikuwa vikitoza ada kubwa kutoka kwa wazazi wa wanafunzi waliokuwa wakihudhuria ili kuimarisha kiwango chao cha elimu kilichokuwa chini katika shule za serikali ili waweze kuingia vyuo vikuu. Kundi lilikuwa likilenga malengo makuu mawili: kupata pesa na kuwavuta wanafunzi hao kujiunga na kundi. Serikali ya Erdogan ilitaka kufanya mabadiliko katika mfumo wa elimu, na kuvigeuza vituo hivi kuwa shule za binafsi zinazofuata programu ya nchi, na kuwa chini ya uangalizi wake, na kubadilisha mfumo wa kuingia vyuo vikuu ili kufuta mwaka wa maandalizi ya kuingia vyuo vikuu baada ya kumaliza sekondari, jambo ambalo liliwafanya wazazi wengi kulazimika kuwapeleka watoto wao kwenye vituo hivyo ili waweze kuingia vyuo vikuu na kupata alama za juu zinazowawezesha kuingia kitivo wanachokipenda. Ikiwa vituo hivi vitafutwa au kufungwa, basi kundi hili litapoteza katika nyanja za kupata pesa na kupata wafuasi. Kwa sababu hiyo, kundi lilichanganyikiwa wakati Erdogan alipotangaza mpango wake wa kufuta vituo hivi na kuvigeuza kuwa shule za binafsi zinazofuata mtaala wa nchi... Ni kana kwamba kundi lilianza kufikiria kutoa jibu dhidi ya Erdogan na chama chake ili kuathiri ushindi wake katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika baada ya miezi mitatu tarehe 30/3/2014.

e- Baada ya hapo kukaja kashfa ya ufisadi na ukamataji uliowahusisha wanachama katika serikali ya Erdogan, chama chake, na watu wa karibu naye... Vidole vya tuhuma vilielekezwa kwa kundi la Fethullah Gülen, kwani majibu ya kundi la Gülen yalikuwa yakiwaashiria wao. Kundi lilionyesha furaha kubwa kwa kukamatwa huko na uchunguzi, na kulikuza kupitia vyombo vyake vya habari na kumkejeli Erdogan... Lakini hatua za haraka za Erdogan za mabadiliko aliyoyafanya kwa wakuu wa usalama kwa kuwafukuza na kuwahamisha... ambapo aliwafukuza idadi ya wakuu wa usalama waliofungamana nao... Mabadiliko haya yaligeuza furaha ya kundi kuwa huzuni na masikitiko, likajaribu kukwamisha au kuvuruga mabadiliko haya na kuashiria kuwa si halali au hayatekelezeki. Vyombo vya habari vinavyounga mkono kundi vilieneza habari kuwa uamuzi wa serikali wa kubadilisha wakuu wa usalama tangu Julai 2013 hadi leo umekataliwa na Rais wa Jamhuri na hakuupitisha. Ofisi ya Rais ilifanya haraka tarehe 20/12/2013 kutoa taarifa kutoka kwa Rais Abdullah Gül ikikanusha habari ya kundi la Gülen... Hivyo jaribio la kundi hilo la kuonyesha kuwa kuna tofauti na hitilafu kati ya Abdullah Gül na Erdogan lilifeli! Baada ya hapo kundi lililipuka kwa hasira dhidi ya Erdogan likihisi kuwa mabadiliko haya yameligusa pabaya, hivyo kiongozi wa kundi Fethullah Gülen kutoka makazi yake huko Pennsylvania, Marekani, alitoa hotuba ya sauti yenye hasira iliyochapishwa na vyombo vya habari vya kundi lake tarehe 21/12/2013 iliyojumuisha dua isemayo: "...Ee Mwenyezi Mungu, ididimize ardhi kwa wale waliowaacha huru wezi na kuwakamata wale waliowafuatilia wezi, na kwa wale waliofumbia macho wahalifu na kuchafua taswira ya wale waliowafuatilia wahalifu, na ziteketeze nyumba zao na kubomoa makazi yao na kusambaratisha mkusanyiko wao na kuwakatia mbali, na ujaalie uadui wao uwe miongoni mwao na unuru juu yao..." Inaonekana kuwa pigo lililoelekezwa kwa kundi lake lilikuwa lenye maumivu makali ikiwa si lenye kuvunja mgongo au kuua.

4- Na hivyo ndivyo mambo yalivyopinduka tangu 2010 kati ya Erdogan na Fethullah Gülen, na ukali wake kuongezeka katika miaka mitatu iliyofuata hadi leo... Inaonekana kuwa huduma ambazo kundi na kiongozi wake anayeishi Pennsylvania amezitoa kwa Marekani: uthubutu dhidi ya dini ya Mwenyezi Mungu, uadui dhidi ya mfumo wa Khilafah, kisha kuunga mkono maslahi ya Marekani hadi pumzi ya mwisho ya kundi hilo... Haya yote yalimfanya Gülen kudhani kuwa kwa huduma zake anazoshindana nazo na Erdogan na hata kuzizidisha, anadhani kuwa atapata radhi za Marekani, na itamfanya kuwa mbadala wa Erdogan, na kumuunga mkono katika mapambano yake... Hivyo akaanza kumsumbua Erdogan kama tulivyotaja hapo awali... Ama huduma za kundi kwa Marekani ambazo alidhania kuwa Marekani itamuunga mkono kama mbadala wa Erdogan, na kumtelekeza Erdogan, miongoni mwazo ni:

a- Wito wake wa haraka wa kile kinachoitwa Uislamu wa wastani, au kwa usahihi zaidi Uislamu uliofanyiwa marekebisho uliochanganywa na mawazo ya kisekula na kidemokrasia, na anayatetea mawazo haya kwa nguvu, na kuwaelekeza watu kwayo, na kutumia vyombo vya habari vya kundi katika hilo.

b- Shughuli za kundi katika suala la mazungumzo ya kidini, hasa na Mayahudi na Manasara, na kuwalinganisha na Waislamu kwa kuzingatia kuwa wote ni waumini, na wito wake wa kujenga mahekalu kwa ajili yao na kwa ajili ya Manusayri pembeni ya misikiti.

c- Kushambulia makundi yote yanayolingania kusimamisha Khilafah na dola ya Kiislamu, na kuyatuhumu kuwa ni ya msimamo mkali na ya kigaidi, na kueneza propaganda za kashfa dhidi yao kupitia vyombo vya habari vinavyomilikiwa na kundi na kuwachongea katika mamlaka za usalama na mahakama.

d- Kiongozi wake kuifanya Marekani kuwa makazi yake tangu mwaka 1999, na kupanua mikutano yake na maafisa wa Marekani na ujasusi wa Marekani... Kisha kutoa mihadhara nchini Marekani inayojumuisha misimamo, mawazo, na maoni yanayolinda maslahi ya Wamarekani. Yeye hapo awali hakulaani uvamizi wa Marekani huko Iraq na Afghanistan, na hivi sasa vyombo vyake vya habari vingi vinashambulia harakati za Kiislamu zinazoasi nchini Syria na kuziona kuwa ni za kigaidi na kufanya kazi ya kuchafua taswira yake, na kuunga mkono misimamo ya Marekani dhidi ya harakati hizo.

e- Misimamo yake ya kuunga mkono umbile la Kiyahudi, alilaani kutumwa kwa meli ya Mavi Marmara kusaidia watu wa Gaza mwishoni mwa mwezi Mei 2010 na akawapa haki Mayahudi kuipiga, na hakutoa mkono wa pole kwa wahanga wa Kituruki wala hakuwaona kuwa ni mashahidi. Hapo awali alilaani hatua ya Saddam kulipiga umbile la Kiyahudi mwaka 1991 na akatangaza kusikitishwa kwake na vifo vya Mayahudi vilivyotokana na hilo... Tovuti yake imechapisha picha yake (yaani ya Fethullah Gülen) akikutana na rabi wa Mayahudi wa Mashariki katika umbile la Kiyahudi, Eliyahu Doron, mwaka 1998.

Hayo yaliyotangulia ni machache tu kati ya mengi... Kundi limedhani kuwa kwa huduma hizo litapata upendeleo kwa Marekani utakaolifanya lipewe kipaumbele kuliko Erdogan. Inayopelekea usahihi ni kwamba dhana hii itawapeleka pabaya, kwani Marekani inamtazama Erdogan kama kiongozi wa chama cha kisiasa mwenye uwezo zaidi wa kutimiza maslahi yake kuliko kundi la Gülen na wafuasi wake...! Kisha Marekani haikuweza kufikia kile ilichokifikia ndani ya Uturuki na kuimarisha ushawishi wake huko isipokuwa kupitia chama cha kisiasa kinachoongozwa na Erdogan. Kwa sababu hiyo, inamuunga mkono ili kutekeleza mipango yake ya kisiasa kupitia yeye, hasa utekelezaji wa mpango wa Marekani unaohusiana na suala la Kikurdi, na mipango mingine ya Marekani ya ndani na nje, ikiwemo suala la Syria... Hata kama shinikizo litaongezeka kwa Erdogan na akajiuzulu kwa mfano, inaelekea kuwa Marekani itatafuta mtu mwingine mwenye nguvu kutoka chama cha AKP na si kwenda kwa Fethullah Gülen. Hii ni kwa sababu uhalisia wa kundi la Fethullah Gülen ni kwamba ni harakati isiyo ya kisiasa ambayo siku zote imekuwa ikijificha chini ya vyama vya kisiasa kwa kauli ya "yuko na mshindi". Lilishirikiana na chama cha Anavatan Partisi (ANAP) cha Turgut Özal katika miaka ya themanini ya karne iliyopita, na baada ya hapo likaunga mkono chama cha Refah, kisha chama cha Demokratik Sol Parti (DSP) kilichoongozwa na Ecevit mwaka 1998 baada ya kuanguka kwa chama cha Refah cha Erbakan. Na baada ya kuanzishwa chama cha AKP, likaingia chini ya kivuli chake. Kwa hiyo linatazamwa kuwa ni kundi lenye kutumia fursa (opportunistic) linalounga mkono vyama vya kisiasa tawala ili kutimiza maslahi yake binafsi. Kwa hiyo, inatarajiwa kuwa litafanya kazi ya kupatana na Erdogan kwa sababu litapoteza ikiwa halitafanya hivyo... Hili limeanza kuonekana kupitia mienendo ya kundi na wafuasi wake. Gülen amerudi nyuma kutoka kwenye shambulio la siri dhidi ya Erdogan, baada ya kumuelezea takriban mwezi mmoja uliopita kama Firauni na Nimrod, ambapo alisema katika sauti iliyorekodiwa akihutubia wafuasi wake: "Ikiwa Firauni na Nimrod wako dhidi yenu, basi nyinyi mko kwenye haki...", kisha akarudi nyuma zaidi wakati Gülen alipopendekeza hivi karibuni kuwa vituo vya masomo ya ziada vibaki na kuwekwa chini ya usimamizi wa nchi kama hatua ya kulegeza msimamo, lakini Erdogan alishikilia uamuzi wake... Hata watu wa Fethullah katika mahakama na usalama hawana mengi ya kufanya mbele ya Erdogan, kwani amewakamata idadi miongoni mwao na wale walioendelea na kazi zao wanayumba katika maamuzi yao. Baadhi ya mahakama zimekubali uamuzi wa Erdogan wa kutokubali mahakama kupokea kesi moja kwa moja kutoka kwa wakuu wa usalama bila idhini ya wakuu wao, na idadi ndogo ya mahakama ilijaribu kukwepa uamuzi huo kama ilivyoelezwa na kituo cha televisheni cha habari cha NTV tarehe 27/12/2013 kwamba "mahakama kuu ya Uturuki imefuta uamuzi wa serikali unaowataka maafisa wa polisi kuwajulisha wakuu wao kuhusu uchunguzi." Pamoja na hayo, Sky News Arabia iliripoti tarehe 26/12/2013 kuwa mwendesha mashtaka mkuu Muammer Akkaş, anayeongoza uchunguzi wa tuhuma za ufisadi zilizowahusu mawaziri katika serikali ya Uturuki, alisema kuwa "alikumbana na shinikizo nyingi" katika kesi hii, akiashiria kuwa "uchunguzi ulikwamishwa"...

Bado Erdogan anatishia na kuwaonya wasaidizi wa kundi hilo katika usalama na mahakama. Alisema wakati wa ziara yake katika wilaya ya Fatsa mkoani Ordu: "Natoa wito wangu kwa idara ya mahakama! Mnaiambia mamlaka ya utendaji: safisheni uchafu ulio miongoni mwenu. Lakini nanyi pia si wasafi kabisa. Na sisi tunayo tunayoyajua." (Hürriyet 21/12/2013). Hivyo basi, msimamo wa Erdogan ni wenye nguvu zaidi kuliko msimamo wa Fethullah Gülen angalau kwa muda unaoonekana, hasa kwa kuwa ushawishi wa Erdogan jeshini umekuwa mkubwa. Vyombo vya habari vya Uturuki vilitaja kuwa Jeshi la Uturuki lilitoa taarifa ikisema kuwa "linajitenga na maoni na makundi yoyote ya kisiasa na linalitumikia taifa la Uturuki kwa uaminifu." Kama ilivyoelezwa katika UPI na katika tovuti ya Al-Hayat tarehe 27/12/2013.

5- Ama dokezo la Erdogan katika tamko lake kuhusu Balozi wa Marekani kama lilivyochapishwa na gazeti la Milliyet 21/12/2013, suala ni kama ifuatavyo:

a- Wakati wa kampeni hii ya ukamataji katika kesi za ufisadi zilizotajwa... magazeti matatu (Star, Yeni Şafak, na Akşam) yalichapisha habari kuhusu mkutano wa Balozi wa Marekani huko Ankara, Ricciardone, na baadhi ya wawakilishi wa Umoja wa Ulaya tarehe 17/12/2013... Habari hiyo ilikuwa na ishara za kuingilia kati kwa Balozi wa Marekani katika matukio hayo, na magazeti haya yalidai kuwa Waziri wa Mambo ya Nje Davutoglu atampigia simu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry na kumuelezea kuchukizwa kwa Wizara ya Mambo ya Nje na duru za kidiplomasia na mienendo ya Balozi...

Licha ya kuwa Balozi wa Marekani mwenyewe Ricciardone alikanusha madai ya baadhi ya magazeti yaliyochapisha habari hii, na kukanusha uhusiano wowote wa Marekani na mchakato wa ukamataji unaohusiana na vitendo vya ufisadi, kupitia ukurasa wake wa Twitter, ambapo alisema: "Marekani haina uhusiano wowote na mchakato wa ukamataji unaohusiana na vitendo vya ufisadi kutokana na rushwa na njia zisizo halali. Habari hizo ni uongo na uzushi mtupu. Hakuna yeyote anayeweza kuweka uhusiano wa Uturuki na Marekani hatarini kwa madai yasiyo na msingi, na kwamba urafiki na ushirikiano kati ya nchi hizi mbili unapata umuhimu wa kufa na kupona kwa nchi zote mbili." (Milliyet 21/12/2013). Lakini Erdogan alitumia suala hili, kana kwamba alikuwa na ahadi na habari ya magazeti haya, jambo lililopelekea baadhi ya wachambuzi kusema kuwa haiondolewi uwezekano kuwa habari hiyo iliandaliwa kwa ajili ya Erdogan ili aitukie kusema kuwa matukio hayo yana mwelekeo wa kimataifa, ili kupata uungaji mkono wa watu kwa kuzingatia kuwa kuna njama ya nje! Kufuatia hilo, alitamka wakati wa ziara zake za kuhamasisha maoni ya umma... akisema akiwa Samsun tarehe 20/12/2013: "Balozi anaingia katika mzunguko wa baadhi ya vitendo vya njama. Kwa hiyo namuambia: afanye kazi yake, ikiwa mmetoka (enyi Balozi) nje ya mzunguko wa kazi yenu basi serikali yetu itakwenda katika njia yake hadi kufikia mwisho wa mamlaka iliyo nayo." (Milliyet 21/12/2013)... Lakini kilichotokea ni kwamba si Davutoglu aliyempigia simu Kerry, wala tamko la Erdogan halikuendelea kuwa hai kwa muda wowote, bali Naibu Rais wa chama cha AKP, Hüseyin Çelik, alitoa tamko lifuatalo: "Taarifa ya Balozi wa Marekani Francis Ricciardone kupitia Twitter inayokanusha habari zinazohusiana na matamshi yake yaliyochapishwa na baadhi ya magazeti inazingatiwa kwetu." (Hürriyet 21/12/2013).

b- Pamoja na kwamba ilivyozoeleka katika malalamiko ya nchi dhidi ya uingiliaji wa nchi nyingine ni Wizara ya Mambo ya Nje kutuma barua rasmi ya malalamiko kwa nchi nyingine, au kumuita Balozi... Na pia ilivyozoeleka wakati Balozi wa nchi yoyote anapokanusha habari kumhusu kutoka kwa nchi aliyopo ni kutuma barua kwa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo kukanusha habari... Lakini kilichotokea ni kwamba Waziri Mkuu alitoa tamko la maneno tu... na Balozi wa Marekani akachapisha majibu yake kwenye Twitter! Hili linaonyesha kuwa "malumbano" kati ya Erdogan na Marekani si zaidi ya maigizo yanayofanywa na waigizaji waliofeli wasio na weledi! Kinachothibitisha kuwa tamko la Erdogan "kali" dhidi ya Balozi wa Marekani ni kelele bila hatua, ni kwamba siku ambayo gazeti la Milliyet lilichapisha tamko la Erdogan yaani tarehe 21/12/2013, gazeti hilo hilo lilichapisha habari likisema: (Inavutia kuona kuwa wakati mchakato wa ufuatiliaji wa ufisadi wenye mwelekeo wa kimataifa ukiendelea, alifika Istanbul Mshauri wa Marekani anayehusika na ujasusi unaohusiana na ugaidi na fedha katika Wizara ya Hazina ya Marekani, David Cohen, anayejulikana kwa ukaribu wake na "Israel", na kisha akakutana na wakurugenzi wa benki nchini Uturuki... Mshauri huyo alijadili na wakurugenzi hao masuala ya kifedha na vikwazo dhidi ya Iran... bila mshauri huyu afisa wa Marekani kukutana na yeyote miongoni mwa wenye mamlaka serikalini)! Hili linaonyesha kuwa maneno ya Erdogan ni sawa na ganda tupu la kokwa lisilo na maana lakini linatoa sauti, kwani maafisa wa Marekani wanaingia nchini na kujadiliana na wanayewataka bila hata kukutana na afisa yeyote wa Uturuki!!

c- Inajulikana kuhusu Erdogan uhusiano wake na Marekani na utekelezaji wake wa mipango yake ndani ya Uturuki na nje yake. Mipango hii, hasa ya ndani, inahitaji yeye ili kukamilika, na ikiwa ataondoka labda itasimama... Marekani inamhesabu Erdogan kama mmoja wa watu wake wenye nguvu waliowezesha ushawishi wake nchini Uturuki tangu aliposhika madaraka. Ushawishi wa Waingereza kabla ya hapo ndio uliokuwa unatawala Uturuki kupitia jeshi kwa miongo iliyopita tangu Mustafa Kemal alipofuta Khilafah kufuatia matakwa ya Waingereza, adui mkubwa wa Uislamu na Waislamu, katika mkutano wa Lausanne mkabala wa kumfanya Mustafa Kemal kuwa Rais wa Jamhuri ya Uturuki... Tangu wakati huo ushawishi wa Waingereza umetawala utawala nchini Uturuki, na Marekani haikuweza kuuondoa ushawishi huu, hasa jeshini, isipokuwa baada ya Erdogan kushika madaraka ambapo ushawishi wa Waingereza ulidhoofika na kutoweka kwenye medani ya kisiasa, na vyama vya kisiasa vyenye asili ya Kiingereza, hususan chama cha CHP, vikawa dhaifu sana... Hivyo ushawishi wa Marekani ndio unaotawala sasa katika miaka ya utawala wa Erdogan, na ushawishi wa Marekani umekuwa dhahiri katika urais wa jamhuri na katika uwaziri mkuu... Kwa hiyo, tamko la maneno kutoka kwa Erdogan kuelekea Balozi wa Marekani bila kuwa na uhalisia wa kivitendo... tamko kama hilo Marekani inajua, na msemaji wake anajua, kuwa halina athari yoyote...

6- Na muhtasari:

a- Kwamba mgogoro wa sasa nchini Uturuki pande zake mbili ni kati ya vibaraka wa Marekani, Erdogan na Fethullah Gülen.

b- Marekani ilikuwa na hamu ya kubaki kwa Erdogan na Gülen kama nguvu moja bila ugomvi wakati Waingereza walipokuwa na nguvu inayohofiwa. Baada ya nguvu hiyo kudhoofika, Marekani ilikaa kimya kuhusu ugomvi wa chama cha AKP na kundi la Fethullah, na ikawaacha washindane katika uaminifu kwake na kutumikia maslahi yake.

c- Inayopelekea usahihi ni kuendelea kwa Erdogan angalau kwa muda unaoonekana, kwani bado anahifadhi umaarufu. Hata kama shinikizo litaongezeka kwake, Marekani itapendelea mtu mwingine kutoka chama cha AKP kuliko kundi la Gülen, kwa sababu inatambua kuwa kundi la Fethullah ni sawa na sheikh na wafuasi wake, lazima ili liendelee lijifiche chini ya chama cha kisiasa tawala, si liwe lenyewe katika utawala.

d- Hii ni katika makadirio ya Marekani na watu wake. Ama kile ambacho Umma unakifanyia kazi, ni kung’oa ushawishi wa Waingereza na Wamarekani na vibaraka wao na wafuasi wao... kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na kurejesha Khilafah upya kama alivyosema Swalla Allahu alayhi wa sallam:

«ثُمَّ تَكُونُ خِلَافَةٌ عَلَى مِنْهَاجِ النُّبُوَّةِ»

"...kisha kutakuwepo na Khilafah kwa njia ya Utume." (Imepokewa na Ahmad na Abu Dawud al-Tayalisi)

Na kila aliyepiga vita Khilafah na wale wanaoifanyia kazi, na kila aliyekwenda na makafiri wakoloni, wawe ni Waingereza au Wamarekani au Warusi au Wafaransa au wengineo... watapata udhalili duniani na unyonge na fedheha mikononi mwa waumini.

وَيَوْمَئِذٍ يَفْرَحُ الْمُؤْمِنُونَ * بِنَصْرِ اللَّهِ يَنْصُرُ مَنْ يَشَاءُ وَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ

"Na siku hiyo waumini watafurahi * kwa nusra ya Mwenyezi Mungu. Humnusuru amtakaye, Naye ni Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu." (QS. Ar-Rum [30]: 4-5)

Share Article

Share this article with your network