Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Kuporomoka kwa Lira ya Uturuki

August 23, 2018
7323

Jibu la Swali

Kuporomoka kwa Lira ya Uturuki

Swali: Lira ya Uturuki iliporomoka kwa asilimia 14 ndani ya siku moja mnamo 2018/08/10, baada ya kushuka kwa zaidi ya asilimia 21 tangu kuanza kwa mwaka huu mfululizo... Anguko hilo lilichochewa zaidi na hatua ya Marekani kuweka ushuru wa forodha kwa chuma na alumini zinazoagizwa kutoka Uturuki... na pia kuibuliwa kwa suala la kuzuiliwa kwa mchungaji wa Kimarekani nchini Uturuki tangu mwaka 2016, na kutaka aachiliwe huru... Ni nini sababu za yote haya? Kisha, mzozo huu unaelekea wapi? Na Mwenyezi Mungu akulipe kheri.

Jibu: Ili jibu liwe wazi, ni lazima kuzingatia mambo yafuatayo:

Kwanza: Mzozo wa Lira na kuporomoka kwake mfululizo kwa vipindi:

1- Matumizi ya Lira yalianza mwaka 1927 ikiwa na thamani ya takriban dola moja, na hiyo ilikuwa baada ya kuondolewa kwa Khilafah na sarafu yake iliyokuwa ikitegemea dhahabu na fedha... Kisha hadithi ya kuporomoka kwa Lira ilianza tangu mwaka 1933 ambapo dola ilikuwa sawa na Lira mbili... Baada ya hapo, mfululizo wa anguko uliongezeka kasi hadi dola ikawa sawa na Lira milioni moja na elfu 650 mwaka 2001. Nakisi katika uchumi wa Uturuki ilifikia kilele chake kutokana na shinikizo la Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), na serikali ya Ecevit kibaraka wa Waingereza ilianza kuyumba... Hivyo, uchaguzi wa mwaka 2002 ulifanyika ambapo Erdogan na chama chake walishinda na kuunda serikali kwa uungaji mkono wa Marekani. Serikali yake ilichukua uamuzi wa kufuta sufuri sita na bunge likaidhinisha, kisha ikaanza kutumika kuanzia 2005/01/01, ambapo dola ikawa sawa na Lira 1.79. Lakini hali hiyo haikutulia kwa muda mrefu, kwani tangu mwaka 2013 Lira ilianza kuanguka tena, na ikarekodi anguko kubwa ndani ya miezi tisa hadi mwanzoni mwa mwaka 2014 ambapo ilipoteza 30% ya thamani yake, na haijatulia hadi leo. Serikali ya Erdogan ilijaribu kuzuia anguko hilo na kudumisha utulivu lakini haikuweza. Lira ilianza kuanguka tangu mwanzoni mwa mwaka huu kwa kiasi kikubwa, ambapo hadi katikati ya mwaka 2018 ilikuwa imepoteza takriban 21% ya thamani yake ya mwanzoni mwa mwaka, yaani ndani ya miezi sita pekee...

2- Baada ya hapo, mnamo Julai 26 mwaka huu, mzozo ulijitokeza wazi kwa namna ya kushangaza wakati Trump na makamu wake Mike Pence walipotishia kuiwekea vikwazo Uturuki ikiwa Brunson hataachiliwa huru mara moja... Kisha Lira ilizidi kushuka mwishoni mwa mwezi Julai uliopita dhidi ya dola na kufikia Lira 4.91 ikilinganishwa na Lira 4.76 kabla ya kutolewa kwa uamuzi wa Benki Kuu ya Uturuki kubakisha kiwango cha riba (riba) kuwa 17.75% bila kuongeza (Benki Kuu ya Uturuki ilibakisha viwango vya riba bila mabadiliko siku ya Jumanne, kinyume na matarajio yaliyotabiri kupandishwa kwake baada ya mfumuko wa bei kupanda hadi kiwango cha juu zaidi katika miaka 14... Benki ilibakisha kiwango cha riba cha wiki moja kuwa 17.75%... Lira, ambayo imepoteza takriban 20% ya thamani yake tangu mwanzo wa mwaka huu, ilishuka hadi 4.91% dhidi ya dola baada ya uamuzi huo kutoka 4.7605 kabla yake... Chanzo: Sky News Arabic - Jumanne, Julai 24, 2018).

3- Baada ya hapo kukawa na tangazo la uamuzi wa vikwazo katika ujumbe wa Trump kwenye Twitter, na kisha kuporomoka kwa Lira ya Uturuki mbele ya dola kukashika kasi... Ili kudhibiti mzozo na Washington, Ankara ilifanya haraka kutuma ujumbe ukiongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki mnamo Agosti 7 kufanya mazungumzo na mwenzake wa Marekani ili kujadili mzozo wa mchungaji Brunson. Lakini mazungumzo kati ya pande hizo mbili hayakuzaa matunda. Mara tu ujumbe wa Uturuki ulipoanza safari ya kurejea nchini mwao mnamo Agosti 9, Trump alichochea moto kupitia ujumbe wake kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa "Twitter", Ijumaa, Agosti 10, kwa kuongeza ushuru kwa bidhaa za chuma na alumini kutoka Uturuki, kiasi kwamba ushuru wa alumini ukawa asilimia 20 na chuma asilimia 50, na kisha kuisukuma Lira kuanguka tena. Ilishuka hadi kiwango cha chini kabisa cha Lira 7.24 kwa dola katika miamala ya mapema huko Asia na Pasifiki. Sarafu ya Uturuki ilipoteza takriban asilimia 40 ya thamani yake tangu kuanza kwa mwaka huu; ndani ya wiki ya pili ya Agosti pekee, Lira ilipoteza kiasi cha asilimia 20 ya thamani yake mbele ya dola. (Trump aliongeza: "Nimeamuru hivi sasa kuongeza maradufu ushuru wa chuma na alumini... 2018/08/10 https://arabi21.com)

4- Hivyo basi, mzozo wa kifedha kati ya Marekani na Uturuki unaonekana kwa nje kama ni matokeo ya kadhia ya mchungaji Brunson, na hamu ya Rais wa Marekani ya kuridhisha sekta ya Kikristo ya msimamo mkali (evangelicals) miongoni mwa wapiga kura wake miezi michache tu kabla ya uchaguzi wa katikati ya muhula wa Kongresi. Lakini ukweli ni kwamba kadhia ya mchungaji Brunson ilitumiwa ili kufunika sababu za kweli za kuporomoka kwa Lira ya Uturuki, ambao ni mzozo wa kisiasa unaochochewa na Marekani ili kuipiga Ulaya kama tutakavyobainisha... Hii ni kwa sababu dalili za mzozo zilikuwepo hata kabla ya hitilafu ya Waturuki na Wamarekani, na kwamba serikali ya Uturuki ilisogeza mbele tarehe ya uchaguzi kutoka Novemba 2019 hadi Juni mwaka huu, ili kuwahi hali yoyote ya kuzorota kwa mzozo ambayo ingeweza kuathiri matokeo ya uchaguzi... Erdogan mwenyewe alikiri hilo akisema, "Shukrani kwa kusogeza mbele tarehe ya uchaguzi, tutajiandaa kwa athari za tetemeko la kiuchumi lenye kuharibu, la sivyo tusingeweza kutoka katika kipindi hiki bila kupata hasara." (Ukurasa wa habari za Uturuki 2018/04/20). Yaani kudorora kwa thamani ya Lira kulikuwepo kabla ya suala la mchungaji na kabla ya kupandishwa kwa ushuru... Hususan kwa kuwa Brunson amefungwa tangu mwaka 2016, hivyo haina maana kwa Marekani kukimbilia kuweka vikwazo dhidi ya Uturuki wakati huu kwa ajili ya Brunson, hasa inapojulikana jinsi Marekani ilivyo na maslahi madogo katika dini na haki za binadamu...

5- Ama sababu za kweli nyuma ya kuporomoka kwa kasi kwa sarafu ya Uturuki ni kutokana na mfululizo wa sababu, muhimu zaidi zikiwa:

a- Kiwango kikubwa cha mikopo, hususan kwa sekta binafsi, katika kipindi cha miaka kumi iliyopita... Kwani Hazina ya Uturuki ilitangaza mnamo Septemba 2017 kuwa jumla ya madeni ya nje ya Uturuki yamefikia dola bilioni 438... na kwamba inapanga kulipa takriban bilioni 11 kama huduma ya deni inayofikia takriban bilioni 43 wakati wa mwaka 2018: Hazina ya Uturuki ilitangaza katika taarifa iliyoitoa mnamo 2017/10/31 kwamba ("inapanga kulipa dola bilioni 10.92 kama sehemu ya kiasi kinachofikia takriban dola bilioni 43.1 kwa ajili ya huduma ya deni mnamo mwaka 2018"... na viwango vya mfumuko wa bei vilifikia hivi karibuni zaidi ya 10%"... Shirika la Anadolu 2017/10/31). Hivyo kengele za hatari zilianza kulia kwa nguvu, hadi pale Idara ya Hazina ya Uturuki ilipotangaza hivi karibuni kuwa ("jumla ya madeni ya nje ya Uturuki kwa robo ya kwanza ya mwaka kuanzia tarehe 2018/03/31 ni dola bilioni 466.1"... Shirika la Anadolu 2018/06/29). Hapa ni lazima kuashiria kuwa sehemu muhimu ya madeni haya yanatokana na miradi ya serikali kimsingi, lakini sekta binafsi ilichukua jukumu la kuitekeleza na kuifadhili... Kwa sababu serikali ya Rais Erdogan katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, ilijaribu kupunguza madeni ya serikali kwa kuikabidhi miradi hii kwa sekta binafsi, ambayo inakopa kutoka nje ili kuitekeleza... Hivyo basi, sekta binafsi leo hii inabeba sehemu ya madeni haya, na hii ni mbinu ya kisiasa ili serikali iweze daima kujisifu kwa uchache wa madeni yake ya nje!

b- Nakisi ya kibiashara kati ya mauzo na manunuzi ya nje iliongezeka hadi 37.5% ikilinganishwa na mwaka uliotangulia na kufikia dola bilioni 77.06 mnamo mwaka 2017 kama ilivyoonyeshwa na takwimu za Wizara ya Forodha na Biashara ya Uturuki mnamo 2018/01/02. Hizi hulipwa kwa fedha za kigeni. Thamani ya mauzo ya Uturuki ilikuwa dola bilioni 157.1 wakati manunuzi yalikuwa bilioni 234 + milioni 156 dola za Kimarekani kwa mwaka 2017 (Televisheni na Redio ya Uturuki 2018/01/02). Aidha, kiwango cha mfumuko wa bei kilichotangazwa nchini Uturuki kwa takwimu rasmi kutoka "Ofisi ya Takwimu ya Uturuki" mnamo 2018/08/03 kuhusu kiwango cha mfumuko wa bei nchini kilifikia 15.85% (Shirika la Anadolu 2018/08/03), nayo inapaa kwa mara ya kwanza kwa kiasi hiki tangu mwaka 2003 wakati chama cha Erdogan kilipoingia madarakani, ikijulikana kuwa lengo la Benki Kuu lilikuwa kufanya mfumuko wa bei uwe 5% ili kufikia vigezo vya Ulaya... Lakini ilishindwa kwani haikuweza kupata kiwango hiki na ilibaki kwenye 8% lakini upesi ikapanda hadi 10% mwaka jana na kufikia leo namba hii, yaani takriban 16%.

c- Mashirika ya ukadiriaji wa mikopo kushusha daraja la kiuchumi la Uturuki kulichochea shinikizo kwa Lira ya Uturuki na kudhoofisha imani kwake na kwa uchumi wa Uturuki... Shirika la ukadiriaji la "Moody's" mnamo 2018/04/14 lilionya dhidi ya udhaifu wa sarafu ya Uturuki na mfumuko wa madeni ya Uturuki, likisema: "Udhaifu wa kudumu wa sarafu ya Uturuki una athari mbaya kwa ukadiriaji wa madeni yake na ni tatizo kwa uchumi" na likaashiria "kupungua kwa akiba ya fedha za kigeni nchini Uturuki" (Reuters 2018/04/14), na "shirika hili lilishusha ukadiriaji wake kwa Uturuki kutoka (Ba1) hadi (Ba2) mnamo 2018/03/13". Erdogan alikasirika akisema: "Mashirika ya ukadiriaji wa mikopo yameshughulika na jitihada za kuisukuma Uturuki kwenye matatizo na kwamba masoko ya kifedha hayapaswi kuchukulia jambo hilo kwa uzito" (Turk Press 2018/03/13). Shirika la ukadiriaji la "Standard & Poor's" lilifuatia ambapo lilishusha ukadiriaji wa Uturuki mnamo 2018/05/02 katika hatua isiyotarajiwa... Shirika hili lilitangaza uamuzi wake wa kushusha ukadiriaji wa Uturuki kutoka (BB) hadi (BB-). Shirika hili lilisema: ("Kushuka kwa ukadiriaji kunatokana na wasiwasi wetu kuhusu kuzorota kwa matarajio ya mfumuko wa bei na kushuka kwa muda mrefu kwa thamani ya sarafu ya Uturuki na kuyumba kwake"... Reuters 2018/05/02). Shirika la ukadiriaji la "Fitch" nalo lilifuatia... likasema katika taarifa yake: ("Ukadiriaji wa mkopo wa Uturuki umeshuka kutoka "BB+" hadi "BB" kutokana na kuongezeka kwa mfumuko wa bei, nakisi katika akaunti ya sasa, na kutokuwa na uhakika katika sera ya kiuchumi ya Uturuki"... Turk Press 2018/07/14). Inajulikana kuwa mashirika haya ya ukadiriaji wa mikopo yanacheza mchezo katika kuathiri hali ya kiuchumi ambapo huficha matatizo ya kiuchumi ya nchi fulani na kutoyamulika kama yalivyofanya na Uturuki kwa miaka mingi, au kuyaibua na kuyakuza kama yanavyofanya na Uturuki sasa ili kutumikia malengo ya kisiasa, na kuwafanya wakopeshaji wawe na hofu ya kuikopesha Uturuki... Kisha kudai madeni yao... jambo ambalo huongeza mahitaji ya kukusanya fedha za kigeni sokoni ili kulipa madeni na hivyo Lira inashuka.

Pili: Na hapa ni lazima kujiuliza: Ikiwa mzozo wa Lira ulikuwepo tangu zamani... kwa nini basi shinikizo iongezwe katika kipindi hiki kwa mzozo wa mchungaji na kupandishwa kwa ushuru? Kisha kuonyeshwa kwa kuporomoka kwa Lira kwa kasi hii kana kwamba ni mvutano kati ya Uturuki na Marekani kwa lengo la kuipiga Lira? Hili ni jambo hatari kama kutangaza vita, ambalo linahitaji angalau kukatwa kwa uhusiano au kujiondoa NATO... nk, lakini hakuna lolote kati ya haya lililotokea! Nini ukweli wa mambo basi? Na ili ukweli ubainike tunataja mambo yafuatayo:

1- Kwamba utawala wa Trump daima umekuwa ukifuata sera ya dola yenye nguvu mbele ya fedha zenye ushawishi duniani, hususan Euro. Ulitegemea kushuka kwa riba katika kanda ya Euro na ukapandisha riba nchini humo ili kuchochea mitaji kuhama kutoka Ulaya kwenda Marekani ili kupata riba ya juu... Marekani ilikuwa ikitarajia kwamba kuhama kwa fedha kungeishusha Euro mbele ya dola, lakini matokeo hayakuwa kama walivyotaka, badala yake Euro iliendelea kupanda dhidi ya dola. Hii ni kwa sababu Benki Kuu ya Ulaya ilianza mipango madhubuti ya kukaza sera yake ya kifedha na kupunguza au kusitisha ununuzi wa dhamana katika kile kinachoitwa upanuzi wa kifedha (quantitative easing), jambo ambalo lilipelekea mitaji kuhama kutoka Marekani kwenda Ulaya na Asia kutafuta faida bora zaidi kwenye uwekezaji... Trump alipofeli katika hili, alielekea kwenye kupunguza manunuzi kutoka nje na kuongeza mauzo ili kurekebisha mizania ya biashara kwa maslahi yake ili dola iwe na nguvu. Alianza kwa kuweka ushuru kwa baadhi ya bidhaa zinazoingia (na kwa hiyo Waziri wa Biashara wa Marekani Wilbur Ross alitangaza Alhamisi, Mei 31, 2018 kuwa nchi yake itaweka kesho Ijumaa ushuru wa juu wa forodha kwa chuma na alumini vinavyoagizwa kutoka Umoja wa Ulaya, China, Mexico na Canada... 2018/05/31 www.dw.com).

2- Lakini sera hizi zote hazikumletea Trump kuimarisha dola mbele ya Euro... Inaonekana kuwa alipata alichokuwa akitafuta katika kuangazia kuporomoka kwa Lira ya Uturuki kwa kuongeza shinikizo zaidi juu yake, na kisha kuupiga soko la kifedha barani Ulaya kwa kuibua hofu ndani yake kutokana na wingi wa uhusiano wa kifedha kati ya Ulaya na Uturuki. Uwekezaji mwingi nchini Uturuki ni wa Ulaya, na umeongezeka mwaka 2017 kwa asilimia 42. Kiwango kikubwa zaidi cha biashara ya Uturuki ni na Ulaya ambapo kilifikia dola bilioni 160 mwaka 2017 na kimeegemea zaidi upande wa Ulaya. Pande hizo mbili zilianza kufanyia mabadiliko makubaliano ya Umoja wa Forodha yaliyotiwa saini mwaka 1995 kwa lengo la kupandisha biashara hadi kufikia dola bilioni 200 ndani ya mwaka mmoja na nusu na kufikia bilioni 500 ndani ya miaka mitano kama alivyotangaza Waziri wa Uchumi wa Uturuki Nihat Zeybekci (Asharq Al-Awsat 2017/09/29). Wakati kiwango cha biashara kati ya Uturuki na Marekani ni dola bilioni 18.7 kwa kuongezeka kwa mauzo ya Marekani kwenda Uturuki kwa asilimia 7.2 ndani ya miezi 11 ya kipindi cha Trump (Shirika la Anadolu 2018/01/21). Hivyo basi, mtikisiko wowote katika uchumi wa Uturuki na kisha Lira ya Uturuki utaibua hofu kubwa katika uchumi wa Ulaya... Na hofu hii ya kifedha, kama Trump anavyotarajia, itakuwa pigo karibu la kifo kwa Euro...

3- Soko la Ulaya limeathirika kweli na kushuka kwa Lira ya Uturuki:

a- Kwamba Benki Kuu ya Ulaya inahisi wasiwasi mkubwa unaoongezeka kuhusu mfiduo wa benki za kanda ya Euro kwa Uturuki, hususan benki ya BNP Paribas ya Ufaransa, benki ya BBVA ya Uhispania na benki ya UniCredit ya Italia. Benki hizi tatu zina miamala mikubwa nchini Uturuki, na hisa za benki hizo tatu zilishuka kwa takriban 3%. Hivyo Ulaya imeanza kuathirika na yanayotokea nchini Uturuki kutokana na uwekezaji wake huko, madeni inayoidai Uturuki, na wingi wa biashara kati ya pande hizo mbili.

b- (Kulingana na takwimu za hivi punde za Benki ya Makazi ya Kimataifa (BIS), madeni ya benki za Ulaya zinazoidai Uturuki yanafikia dola bilioni 224 (takriban Euro bilioni 200), mengi yakiwa ni ya benki za Uhispania. Benki hizo zinaogopa mfiduo wao kwa mzozo wa Uturuki, na hisa za baadhi ya benki hizo za Ulaya zimeanza kushuka kutokana na kuporomoka kwa Lira kwa viwango vinavyoanzia asilimia 10 hadi 20 kutokana na madeni yao nchini Uturuki) Sky News 2018/05/31.

c- Kuna upande mwingine unaotia wasiwasi kuhusu madeni ya Uturuki, nao ni kutokuwa na uwezo wa kulipa huduma za madeni... Wawekezaji wa Uturuki wanazidai benki za Uhispania kiasi cha dola bilioni 82.3, na benki za Ufaransa kiasi cha dola bilioni 38.4, wakati thamani ya mikopo ya Italia ni dola bilioni 17 katika mchanganyiko wa sarafu za ndani na kigeni. Kutoka hapa ndipo tahadhari zinatokea Ulaya, kwani benki ya Uhispania BBVA, UniCredit ya Italia na kampuni ya BNP Paribas ya Ufaransa zimepoteza thamani ya hisa zao: https://www.ft.com/content/51311230-9be7-11e8-9702-5946bae86e6d

Pia, kushuka kwa thamani ya Lira kunaibua uwezekano wa Uturuki kushindwa kulipa mikopo yake, jambo linalopelekea Ulaya kuathirika kwa upana...

d- Ripoti zilikuwa zimeashiria kuwa kampuni kubwa za Uturuki zinazodaiwa zaidi ya dola bilioni 220, ziliwasilisha maombi kwa serikali ya ulinzi dhidi ya wadai baada ya Lira kuanguka. Miongoni mwa kampuni hizo ni kundi la "Dogus" linaloendeshwa na bilionea Ferit Sahenk, ambaye aliziomba benki kuunda upya madeni ya fedha za kigeni yenye thamani ya mabilioni ya dola, na baadhi ya makadirio yalieleza kuwa jumla ya kiasi cha madeni anayoomba yaundwe upya ni takriban dola bilioni 20...

e- Umoja wa Vyumba vya Viwanda na Biashara nchini Ujerumani ulitangaza kuwa takriban kampuni 6,500 za Kijerumani ndani ya Uturuki zimeathirika kutokana na hali ya sintofahamu inayotanda katika uchumi wa Uturuki, ukiashiria kuwa kampuni za Kijerumani zimeanza kuacha mpango wa kuingiza uwekezaji mpya katika soko la Uturuki. "2018/08/13 www.lebanon24.com"

**Tatu: Hivyo basi, kuangazia mzozo wa Lira kwa kushuka huku kwa kasi kutokana na hatua za Marekani kulikuwa kwa ajili ya kuleta mtikisiko mkubwa katika uchumi wa Ulaya na kisha kuipiga Euro na kuishusha mbele ya dola... Ijapokuwa hatua za Marekani kwa kuishinikiza Lira zitaathiri maisha ya watu nchini Uturuki, Trump hajali jambo hili... Na ingawa mtu anaweza kuelewa kiburi cha Trump cha kupiga sarafu yoyote inayoshindana na dola kulingana na akili ya "cowboy" iliyochanganyika katika damu yake, lakini cha kushangaza ni kuwa Erdogan hatambui hilo na anashangazwa na alichokifanya Trump na kuona ajabu jinsi gani Trump anafanya hivyo kwa mshirika wake kwa ajili ya mchungaji?! Anasema mbele ya mkusanyiko katika mji wa Unye unaotazama Bahari Nyeusi ("Ni kosa kuthubutu na kujaribu kuifanya Uturuki isalimu amri kupitia kutoa vitisho kwa ajili ya mchungaji" na akaongeza "nawahutubia wale wa Marekani tena: aibu kwenu. Mnabadilisha mshirika wenu wa kimkakati katika muungano wa Atlantiki kwa mchungaji" Chanzo: Tovuti ya Al-Anba siku ya Jumapili mnamo 2018/08/12). Kisha anasema akimuhutubia Trump kwa kunyenyekea na huzuni kwamba Uturuki imetoa huduma nyingi kwa Marekani na kupigana kwa ajili yake! Hilo ni katika makala yenye anwani "Unauonaje mzozo na Marekani" iliyochapishwa katika gazeti la New York Times la Marekani mnamo 2018/08/11 ambapo Erdogan anasema: (... Kwamba Uturuki na Marekani ni washirika wa kimkakati na washirika katika NATO tangu miaka 60 na kwamba walikabiliana na matatizo ya pamoja katika kipindi cha Vita Baridi na baada yake... Uturuki imekimbilia kuisaidia Marekani kila wakati kwa miaka mingi... Na majeshi yetu yalipigana nao nchini Korea... Na katika nyakati ngumu zaidi za mzozo wa makombora na Cuba, tulichangia kutuliza mzozo kwa kuruhusu Marekani kuweka makombora ya Jupiter katika ardhi yetu. Na kwamba Uturuki ilituma majeshi yake Afghanistan ili kufanikisha misheni ya muungano wa Atlantiki ya Kaskazini (NATO) wakati Marekani ilipokuwa ikiwasubiri marafiki na washirika wake ili kuitikia mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11"). Hivyo Erdogan anaonyesha utii wake kwa Marekani adui wa Uislamu na Waislamu, na inamlipa kwa kutomthamini!

Nne: Ama hatima ya mzozo huu kati ya Marekani na Uturuki na tatizo la Lira ya Uturuki, tunachotarajia ni kama ifuatavyo:

1- Kwa kuwa lengo la shinikizo la Marekani kwa Lira ya Uturuki lililopelekea kushuka kwa kasi kwa Lira... lengo hili ni kuleta hofu Ulaya ili kuvuruga uchumi wa Ulaya na kisha kuishusha Euro, kutokana na wingi wa uhusiano wa kifedha na kiuchumi kati ya Ulaya na Uturuki, na kwa kuwa hili limepelekea kweli kushuka kwa thamani ya Euro mbele ya dola: (... Na Euro iliathirika sana siku ya Ijumaa baada ya gazeti la Financial Times kunukuu vyanzo viwili vikisema kuwa Benki Kuu ya Ulaya ina wasiwasi kuhusu benki za Uhispania, Italia na Ufaransa na mfiduo wao kwa Uturuki. Na leo Euro imegusa dola 1.13655 ambayo ni kiwango cha chini kabisa mbele ya sarafu ya Marekani tangu Julai 2017, yaani tangu zaidi ya mwaka mmoja uliopita... Chanzo: Reuters - Jumatatu, 2018/08/13). Kwa hiyo Trump akifanikiwa kuipiga Euro kwa namna inayoridhisha kiburi chake, anaweza kurejesha uungaji mkono kwa Lira kwa kubadilisha mwelekeo wa mashirika ya ukadiriaji kama alivyofanya wakati wa kuingia Erdogan 2003 wakati Lira ilikuwa chini na uchumi ukiwa umeyumba katika kipindi cha Ecevit, na kisha akatengeneza "bubble" ya kupaa kwa uchumi kwa mikopo mfululizo kwa ushawishi wa Marekani na washirika wake na kupandisha ukadiriaji wa Uturuki... Kisha kukawa na utangazaji wa uchumi unaokua nchini Uturuki ijapokuwa umejengwa juu ya mikopo na madeni ya riba!

2- Ama kuhusu athari za ushuru, hazina athari kubwa, kwani mauzo ya chuma ya Uturuki kwenda Marekani yanazidi kidogo dola bilioni moja (Youm7 2018/08/02), na hiyo haina athari katika nchi ambayo mauzo yake mwaka 2017 yalifikia zaidi ya dola bilioni 157 (Al-Sharq 2018/01/02), na ni kana kwamba kilichokusudiwa kilikuwa ni kuleta mazingira ya kuvuruga uchumi wa Uturuki na kisha mazingira meusi kwa Lira ya Uturuki ambayo yatakuwa na mwangwi katika uchumi wa Ulaya na kisha Euro kutokana na wingi wa miamala ya kiuchumi na kifedha kati ya Uturuki na Ulaya, na hivyo ndivyo ilivyokuwa...

3- Ama mchungaji, amekuwa kizuizini kwa takriban miaka miwili na mambo yalikuwa shwari kati ya Uturuki na Marekani, na sasa Trump amemuibua kwa malengo ya uchaguzi, na pia kuleta hali ya mvutano kati ya Uturuki na Marekani ambayo inasaidia kuathiri masoko ya kifedha; yeye ni kipengele msaidizi katika vurugu hizi na si asili. Hivyo basi, pindi atakapotosheka na yaliyotokea kwa Euro, na inatarajiwa kuwa haitachukua muda mrefu... mchungaji huyo atakabidhiwa kwa Marekani huku Erdogan akihifadhi heshima yake au hata bila kuifadhi!

4- Ama mateso ya watu wa Uturuki kutokana na kuporomoka kwa Lira na kisha kupanda kwa bei na ugumu wa maisha... hili halimuhusu Trump wala haliwahusu wanaofuata mkondo wa Trump wala vibaraka... Huenda wafuasi hawa na wafuasi wao wakazinduka au wakaelewa kuwa hawana uzito wala thamani kwa mabwana zao ikiwa maslahi ya mabwana hao yatahitaji kuwafanyia watakavyo hata kama katika hilo kuna udhalilishaji kwa wafuasi hao au kuwaharibia sifa... Kwani anayedhalilika ni rahisi kwake kudhalilishwa...

Na muhtasari ni:

  • Kwamba mzozo uliotengenezwa na Trump kuanzia ushuru wa forodha, suala la mchungaji, kushushwa kwa ukadiriaji wa Uturuki na kufichuliwa kwa madeni ya Uturuki... nk, na kisha yaliyotokea kwa Lira ya kushuka kwa namna inayovutia macho... mzozo huu umekusudiwa kuleta hofu Ulaya ili kuvuruga uchumi wa Ulaya na kisha kuishusha Euro, kutokana na wingi wa uhusiano wa kifedha na kiuchumi kati ya Ulaya na Uturuki, na hili limepelekea kweli kushuka kwa thamani ya Euro mbele ya dola...

  • Na kwa kuwa Erdogan anafuata mkondo wa Marekani, haitarajiwi kuwa mzozo huu utachukua muda mrefu, bali ikiwa Trump atatosheka na kushuka kulikotokea katika Euro hata kama halitakuwa pigo la kifo kama alivyokuwa akitumaini, na kana kwamba hili haliko mbali... basi pindi Trump atakapoumaliza mzozo alioanzisha, ataufanya kwa namna ya kuhifadhi heshima kwa Erdogan au bila heshima yoyote... Na kisha mchungaji ataachiliwa huru na ushuru utafutwa au kupunguzwa, na mashirika ya ukadiriaji yatarejea na kurekebisha daraja la Uturuki baada ya kuahirisha deni kwa mikopo mipya, na kisha bei ya Lira itaimarika hata kama haitarudi kama ilivyokuwa kabla ya mzozo, na Trump na Erdogan watarejea kuzungumza kwa urafiki kana kwamba hakuna kilichotokea!! Na mzunguko utaendelea hivyo hivyo... Ikiwa maslahi ya mabwana zao yatahitaji kuwadhalilisha watafanya hivyo, bali hata ikihitajika kuwaondoa itakuwa, na kumeshatokea mfano wa hayo kwa wafuasi wao wa kabla, je hawakumbuki?

إِنَّ فِي ذَلِكَ لَذِكْرَى لِمَنْ كَانَ لَهُ قَلْبٌ أَوْ أَلْقَى السَّمْعَ وَهُوَ شَهِيدٌ

"Hakika katika hayo kuna mawaidha kwa mwenye moyo (wa kuzingatia) au anayetega sikio naye akawa anashuhudia (anazingatia)." (QS. Qaf [50]: 37)

12 Dhul-Hijjah 1439 H Inalingana na: 2018/08/23 M

Share Article

Share this article with your network