Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Kuporomoka kwa Lira ya Uturuki Kufikia Kiwango cha Chini Kabisa na Athari Zake kwa Uchaguzi wa Rais wa Mwaka 2023

December 12, 2021
2999

Jibu la Swali

Swali: Lira ya Uturuki imeporomoka hadi kufikia viwango vyake vya chini kabisa katika kipindi kifupi, ambapo imepoteza zaidi ya 30% ya thamani yake katika muda usiozidi miezi miwili, na zaidi ya 45% tangu kuanza kwa mwaka huu. Mfumuko wa bei umeongezeka maradufu hadi takriban 21% na bei za bidhaa zimepanda kwa kiasi kikubwa. Ikumbukwe kuwa sarafu hiyo imekuwa ikishuka mfululizo tangu mwaka 2013. Je, ni zipi sababu za hali hii? Mgogoro huu unaweza kutatuliwaje na kudhibiti anguko hili? Na ni zipi athari zake kwa uchaguzi wa mwaka 2023?

Jibu: Ili kufahamu sababu za hali hii na matokeo yake, tunapitia mambo yafuatayo:

1- Ni kweli kwamba sarafu imepoteza takriban 45% ya thamani yake dhidi ya dola tangu kuanza kwa mwaka huu, na takriban 30% tangu mwishoni mwa mwezi Oktoba. Haya yote yanatokana na kuongezeka kwa madeni, kufika kwa muda wa kulipa madeni ya dharura, na kushindwa kulipa madeni hayo yanapofika muda wake; mambo haya yana mchango mkubwa katika kushuka kwa thamani ya sarafu. Kwa mujibu wa Wizara ya Fedha ya Uturuki tarehe 31/03/2021, deni la nje lilifikia takriban dola bilioni 448.4, huku deni la msingi likiwa ni dola bilioni 262.1, ambalo limeongezeka maradufu kutokana na riba pamoja na malipo ya bima ya madeni. Madeni ya dharura ambayo Uturuki inatakiwa kuyalipa ndani ya mwaka mmoja yalifikia takriban dola bilioni 168.7. Ili kulipa madeni hayo, inahitaji kukopa kutoka kwa pande nyingine, na hivyo kubaki katika mzunguko wa kulipa madeni. Inaonekana kuna upungufu katika kulipa madeni haya ya dharura, ambayo yanalipwa kwa fedha za kigeni (hard currency) kama inavyojulikana. Upangaji wa malipo ya madeni unaupa shinikizo uchumi wa Uturuki. Upungufu wa malipo uliongezeka mwezi Oktoba uliopita kutoka dola bilioni 3.7 hadi dola bilioni 12 mwezi Novemba. Inatarajiwa kuwa upungufu mwezi huu wa Desemba utakuwa takriban dola bilioni 10.4. Inatabiriwa kuwa upungufu hadi miezi ya kiangazi ijayo utakuwa wastani wa dola bilioni 9 kwa mwezi, kwa mujibu wa utabiri wa baadhi ya wachumi wa Uturuki wanaofanya kazi benki. Erdogan alijaribu kulaumu pande zisizojulikana zinazonunua fedha za kigeni na kuziondoa sokoni ili zisifikie Benki Kuu. ("Erdogan alielekeza Baraza la Ukaguzi la Serikali kubainisha taasisi zilizonunua kiasi kikubwa cha fedha za kigeni na kubaini ikiwa kuna ujanja wowote uliofanyika." Alisema "Nchi yetu inapigana vita vya uhuru wa kiuchumi na haitashindwa na shinikizo za kubadili mkondo. Tunashuhudia ujanja kwenye kiwango cha ubadilishaji fedha, viwango vya riba, na kupanda kwa bei kunakofanywa na wale wanaotaka kuiondoa Uturuki kwenye ramani"... Asharq Al-Awsat 27/11/2021). Maneno haya yote ni jaribio la kukwepa majukumu na kufunika ukweli; kwani upungufu ni wa kweli, na milango imefunguliwa kwa pande mbalimbali kukopa nje kwa riba, iwe ni serikali, makampuni, au watu binafsi kupitia kadi za mkopo. Madeni yanalipwa kwa fedha za kigeni, na yote haya yanasababisha mgogoro wa kweli, ambapo sarafu inashuka na umaskini unaongezeka. Benki na taasisi za kifedha zinazotoa mikopo zitajaza hazina zao, huku nchi zao, hasa zile za kibeberu, zitaongeza uingiliaji wao katika masuala ya nchi na kulazimisha utawala zaidi juu yake.

2- Kutokana na hayo, bei zimepanda kwa kiasi kikubwa. Shirika la Takwimu la Uturuki lilitangaza mnamo 03/12/2021 (kwamba "kiwango cha mfumuko wa bei nchini kwa mwaka kilifikia 21.31% katika mwezi Novemba"... Anadolu 03/12/2021). Hii inasababisha kusinyaa kwa uchumi (economic contraction), na kiwango hiki ni mara nne zaidi ya lengo lililowekwa na serikali ya Erdogan, jambo linalofanya gharama za maisha kuwa ghali kwa familia nyingi, na kushindwa kwa watu wengi kulipa madeni yao. Urais wa Bajeti na Mikakati wa Jamhuri ya Uturuki ulitangaza katika ripoti iliyotolewa mnamo 02/12/2021 ("kwamba idadi ya watumiaji wanaoshindwa kulipa madeni yao ya riba iliongezeka mwaka huu hadi 127.2% ikilinganishwa na mwaka jana. Ikumbukwe kuwa idadi ya watu wanaotumia kadi za mkopo au mikopo ya riba nchini Uturuki, yaani wanaokopa kwa riba, ni takriban watu milioni 35. Waziri wa Hazina na Fedha, Lütfi Elvan, alieleza kuwa idadi ya wanaotumia kadi za mkopo inafikia watu milioni 34, laki moja na elfu kumi na tisa na mia mbili na hamsini. Na wana madeni ya takriban Lira za Uturuki bilioni 874 na milioni 300"... BBC Turk 14/09/2021).

3- Serikali, Rais wake, na taasisi zake wanawahimiza watu kutumia (consumption) ili kuleta ukuaji wa uchumi, na hii inawapelekea kukopa, jambo ambalo haliwezekani isipokuwa kupitia riba yenye madhara na iliyoharamishwa. Hali hiyo haibadiliki hata kama Benki Kuu, kwa ombi la Erdogan, itapunguza kiwango cha riba kutoka 24% hadi 19% na kisha kushuka hadi 15% katika miezi ya hivi karibuni. Rais alijaribu kupitia hatua hiyo kutumia hisia za Waislamu kwa kusema mbele ya kundi la wabunge wa chama chake mnamo 17/11/2021: ("Riba ndiyo sababu na mfumuko wa bei ndiyo matokeo, na kwa sababu hiyo tutapambana na mfumuko wa bei na hatutaruhusu riba iwakandamize watu wetu"...). Hakuna tofauti katika riba iwe ni 24%, 19%, au 15%; kwani riba, iwe kidogo au nyingi, ni haramu. Na yule anayeila, anayeihalalisha, na anayeihimiza, basi ametangaza vita na Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Amewatumbukiza watu wengi kwenye riba kwa muda wa miaka 19 ya utawala wake na chama chake tangu mwaka 2002, kwa msingi wa kwamba yeye ni wa Kiislamu! Alihimiza mikopo ya riba ili gurudumu la uchumi litembee na kuongeza ukuaji, jambo ambalo linamaanisha kuongezeka kwa harakati za soko katika kuuza, kununua, kuwekeza, na kupunguza ukosefu wa ajira. Lakini yote haya yamewageuka watu wa Uturuki walipokimbilia matumizi kupitia madeni ya riba. Umaskini na taabu zao vimeongezeka, huku wenye mitaji wakizidi kuwa matajiri, na watu wameanza kulalamika na sauti zimeanza kupazwa dhidi yake. Umaarufu wake umeanza kushuka hadi viwango vya chini, huku uchuguzi wa Rais ukiwa mlangoni ambapo umepangwa kufanyika tarehe 18/06/2023. Mfumo wa kidemokrasia wa kisekular wa kibepari unaotumika sasa nchini Uturuki ndio kichocheo kikuu cha kuenea kwa riba kwa sababu ni miongoni mwa nguzo za mfumo huu.

4- Rais alimfuta kazi Gavana wa zamani wa Benki Kuu, Naci Ağbal, mnamo 19/03/2021 ambaye alikuwa akitetea sera ya riba ya juu, na kumteua Kavcıoğlu mahali pake ili kazi yake iwe kupunguza riba na kufanya kazi ya kurudisha uthabiti wa bei huku akiendeleza uchangamfu wa uchumi kabla ya uchaguzi ujao wa bunge na rais. Gavana wa Benki Kuu ya Uturuki, Şahap Kavcıoğlu, alisema ("kwamba lengo la uingiliaji wa Benki Kuu katika masoko ya fedha ni kuondoa kuyumba kunakotokea sokoni. Na athari limbikizi za msimamo wetu wa sera ya sasa ya kifedha tutaziona katika nusu ya kwanza ya mwaka 2022"... Anadolu 02/12/2021). Erdogan pia alimfuta kazi Waziri wa Hazina na Fedha, Lütfi Elvan, na kumteua Nureddin Nebati mahali pake, akitangaza hilo katika Gazeti la Serikali la Uturuki mnamo 02/12/2021. Ikumbukwe kuwa alikuwa amemteua mwaka mmoja tu uliopita baada ya kumfuta kazi mkwe wake, Berat Albayrak, mnamo 09/11/2020. Hii inaashiria mparaganyiko katika mwendo na kuchanganyikiwa katika sera na utoaji wa suluhisho, na jaribio la kutupa lawama za kufeli kwa watu wengine aliowateua.

5- Erdogan bado anatumikia sera za Amerika katika eneo hili na kutimiza maslahi yake, kwani anafuata mzunguko wake kikamilifu. Mkabil wa hilo, Amerika inafanya kazi ya kumsaidia kwa namna mbalimbali. Kwa sababu hiyo, makampuni ya kimataifa ya ukadiriaji wa mikopo (credit rating), ambayo ni makampuni ya Amerika, yalichapisha ripoti zao chanya kwa faida ya Erdogan. Wakala wa Amerika wa S&P Global Ratings ulichapisha mnamo 01/12/2021 utabiri wake kuhusu ukuaji wa uchumi wa Uturuki (ukapandisha utabiri wa ukuaji wa uchumi wa Uturuki mwaka huu kwa pointi 1.2 hadi 9.8%, huku ukiongeza utabiri wa ukuaji wa mwaka 2022 kwa pointi 0.4 hadi 3.7%. Ulikuwa umechapisha utabiri wake mwezi Septemba uliopita wa ukuaji wa uchumi wa Uturuki kwa mwaka 2021 kwa 8.6%... Anadolu 01/12/2021). Ikifuatiwa na wakala wa Amerika wa Fitch Ratings mnamo 02/12/2021 ambapo ulitoa taarifa iliyopitia tathmini kuhusu uchumi wa Uturuki kwa namna chanya. Taarifa yake ilitaja kuwa inatarajiwa uchumi wa Uturuki ukue mwaka huu kwa 10.5% badala ya 9.2% ambayo wakala huo ulitangaza mwezi Septemba uliopita. Pia ulipandisha utabiri wake wa ukuaji wa uchumi wa Uturuki mwaka 2022 kutoka 3.5% hadi 3.6%. Na ukabakisha ukadiriaji wake wa mkopo kwa Uturuki katika (BB-). Taarifa ya wakala huo iliashiria kuwa ("ukuaji wa uchumi wa Uturuki ni imara ikilinganishwa na wenzake, lakini pato la mtu mmoja mmoja linaelekea kushuka tangu mwaka 2013 kwa thamani ya dola"... Anadolu 03/12/2021). Wakala wa Amerika wa Moody's mnamo 03/12/2021 ulibakisha ukadiriaji wake katika daraja la B2 na mtazamo hasi wa siku zijazo, na ukaashiria kuwa ("hatari kuu za udhaifu wa nje za Uturuki zimepungua kutokana na upungufu wa akaunti ya sasa, jambo linalosaidia ujenzi wa taratibu wa akiba ya fedha za kigeni kwa msingi wa jumla na wavu, bila kujali udhaifu wa sasa wa sarafu ya ndani ya Lira... na kwamba Uturuki inafurahia uchumi mkubwa na wa aina mbalimbali, na inatarajiwa kuwa uchumi wa nchi utakua kwa 11% mwaka huu na 4% mnamo mwaka 2022 'Wakala huo ulikuwa umetabiri katika ripoti yake iliyochapishwa mwezi Novemba uliopita kuwa uchumi wa Uturuki ungekua kwa 9.2% mwaka huu'"... Anadolu 04/12/2021). Ripoti hizi za makampuni ya ukadiriaji ya Amerika zinachukuliwa kuwa msaada kwa Erdogan. Hii inamaanisha kuwa Amerika inamtaka ashinde katika uchaguzi ujao naye anaipatia huduma, na hakuna mbadala mwingine mwenye nguvu aliyejitokeza uwanjani hadi sasa.

6- Rais wa Uturuki anajaribu kusaidia uchumi na kulinda thamani ya sarafu kwa kuvutia uwekezaji wa nje na kutafuta uwekezaji wa Uturuki nje ya nchi, na sasa anaelekea kwenye nchi za Ghuba. Kwa sababu hiyo, ameanza kuitongoza Imarati ambayo kwa muda mrefu walikuwa wakirushiana maneno. Mwanamfalme wa Imarati, Mohammed bin Zayed, aliwasili Uturuki mnamo 24/11/2021 katika ziara rasmi kufuatia mwaliko wa Rais wa Uturuki Erdogan. Ikumbukwe kuwa walikuwa wamefanya mazungumzo kwa simu mnamo 31/08/2021 ambapo walijadili mahusiano ya pande mbili na masuala ya kikanda. Baada ya hapo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mevlüt Çavuşoğlu, aliashiria kuwa hali ya chanya imetanda kwenye mahusiano ya Uturuki na Imarati hivi karibuni. Katika ziara hii, Uturuki na Imarati zilitia saini mikataba 10 katika nyanja mbalimbali mbele ya Erdogan na Bin Zayed. Baada ya hapo, Bin Zayed aliandika kwenye akaunti yake ya Twitter: "Nimekutana leo mjini Ankara na Rais wa Uturuki Erdogan na tumefanya mazungumzo yenye tija. Mazungumzo hayo yalijikita kwenye fursa za kuimarisha mahusiano yetu ya kiuchumi", huku Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Uwekezaji ya Abu Dhabi (ADQ), Mohamed Hassan Al Suwaidi, akisema: ("Imarati imeamua kutenga dola bilioni 10 kwa ajili ya uwekezaji nchini Uturuki". Na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki alitangaza kuwa atafanya ziara mjini Abu Dhabi mwezi ujao... Anadolu 24/11/2021). Kufuatia hapo, Lira ya Uturuki ilipanda kidogo dhidi ya dola, kisha ikarudi kuporomoka. Tangu mwaka mmoja na nusu, Erdogan amekuwa akifanya kazi ya kusawazisha mahusiano na tawala ambazo alikuwa na uhasama nazo katika eneo hili; kwa sababu uhasama wake si wa kimfumo (kimbadili) bali unahusiana na maslahi na sera zilizofungamana na Amerika ambaye anafuata mzunguko wake. Imarati imefanya mapatano (normalization) na huluki ya Kiyahudi kama ambavyo Erdogan pia ana mapatano nayo na anasisitiza mapatano hayo. Wao na tawala nyingine za eneo hili ni wenye kula njama dhidi ya Palestina na wamekaa kimya juu ya unyakuzi wa Mayahudi juu yake.

7- Rais wa Uturuki alielekea Qatar mnamo 06/12/2021, japo ziara hiyo ilikuja kutokana na mwaliko wa Amir wa Qatar kushiriki katika mkutano wa saba wa Kamati Kuu ya Mikakati kati ya nchi hizo mbili. Erdogan alisema katika mkutano na waandishi wa habari kabla ya kuelekea Qatar: ("Ukubwa wa miradi inayotekelezwa na wafanyabiashara wa Uturuki nchini Qatar unafikia takriban dola bilioni 15". Alisema: "Nchi hizi mbili zimeimarisha ushirikiano wao kwa msingi wa faida ya pande zote katika nyanja nyingi kuanzia uchumi hadi ulinzi, na kuanzia biashara hadi uwekezaji". Alisema: "Tutaendelea kuendeleza uhusiano wetu na ndugu zetu katika Ghuba bila ubaguzi katika mfumo wa maslahi yetu ya pamoja na kuheshimiana"... Anadolu 06/12/2021). Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Mohammed bin Abdulrahman Al Thani, alisema katika mkutano na waandishi wa habari na mwenzake wa Uturuki, Mevlüt Çavuşoğlu ("kuwa inatarajiwa kusainiwa kwa mikataba 12 kati ya Uturuki na Qatar wakati wa mkutano wa duru ya saba ya Kamati ya Mikakati" kabla ya ziara ya Erdogan mjini Doha... Anadolu 06/12/2021). Kisha mikataba 14 ya ushirikiano ilisainiwa kati ya Qatar na Uturuki: (Qatar na Uturuki zasaini mikataba 14 na Erdogan asisitiza nia ya Ankara kushirikiana na nchi za Ghuba... na kazi za duru ya saba zilifanyika chini ya uenyekiti wa Amir wa nchi ya Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, na Rais Erdogan anayezuru mji mkuu wa Qatar, Doha. Pande hizo mbili zilitia saini mikataba 14 ya ushirikiano katika nyanja mbalimbali kama vile uchumi, uwekezaji, viwanda, ulinzi, usalama, wakfu, habari, utamaduni, na michezo... Al Jazeera + Anadolu 07/12/2021). Haya ni majaribio ya Erdogan kusaidia uchumi wa Uturuki na jaribio la kuzuia kuporomoka kwa Lira ya Uturuki.

8- Haiwezekani kuzuia kuporomoka kwa sarafu hivi karibuni; kwani majaribio yamefanyika na yanaendelea kufanyika ili kuzuia kuporomoka kwake, lakini bila mafanikio kwa sababu msingi ambao majaribio haya yamejengwa juu yake ni mbovu na batili. Lira iliporomoka hapo awali hadi kufikia kiwango cha Lira milioni moja na laki saba na elfu tisini na saba mwishoni mwa mwaka 2004, na uamuzi ukachukuliwa wa kuondoa sufuri sita kuanzia 01/01/2005, hivyo dola ikawa sawa na Lira 1.79, lakini haikutulia kwa muda mrefu. Tangu mwaka 2013, thamani ya Lira ilianza kuanguka, na kuongeza kasi ya kuanguka. Kuporomoka kwa Lira kuna uhusiano na kudorora kwa hali ya uchumi wa Uturuki. Sababu za kudorora kwa hali ya uchumi wa Uturuki kimsingi zinarudi kwenye misingi uliyojengwa juu yake na sera zinazotekelezwa kulingana na misingi hiyo. Ikiwa misingi hii haitatatuliwa, basi watu wataendelea kuungua kwa moto wa mfumo huu ambao uchumi umejengwa juu yake na watataabika. Uchumi huo umejengwa juu ya misingi batili ya kibepari. Umetegemea kuongeza uzalishaji, ukuaji, na kuhimiza matumizi, na kwa ajili hiyo Erdogan na mfumo wake wa kisekular walifungua mlango wa kukopa na kuchukua mikopo ya riba, pamoja na kuwa ni haramu iliyokatazwa vikali katika Uislamu. Pia alifungua mlango wa uwekezaji wa kigeni ambapo makampuni haya yanafanya miradi ya umma kama vile ujenzi wa madaraja, barabara, mahandaki, treni za chini ya ardhi (metro), na viwanja vya ndege. Makampuni haya binafsi, yakiwemo ya kigeni, yanakusanya fedha kutoka kwa watu wa kawaida na kuvuna faida kutoka kwao. Ikumbukwe kuwa haya ni miongoni mwa huduma za umma ambazo ni wajibu kwa dola kuzitoa bure kwa watu wote kama Uislamu unavyoamrisha. Suluhisho la tatizo la kiuchumi liko katika kugawa mali ya umma na manufaa kwa raia wote na kuwawezesha kunufaika nayo. Ni lazima kuhakikisha kukidhi mahitaji yote ya kimsingi kwa kila mwanajamii mmoja mmoja kikamilifu, na kuhakikisha kuwa kila mmoja wao anaweza kukidhi mahitaji ya ziada (luxuries) katika kiwango cha juu kabisa kama inavyoelekezwa na vifungu vya Katiba ya Kiislamu vilivyostanbatishwa kutoka katika Kitabu (Qur'an) na Sunnah. Wakati huo huo, ni lazima kuvunja ufungamanishaji wa Lira ya Uturuki na dola, na kufanya msingi wake kuwa dhahabu na fedha kwa mujibu wa hukumu za Sharia. Kadhalika, kufungamanisha uchumi na nje na madeni ni jambo la hatari na lenye kuangamiza, hasa linapokuwa kwa riba. Mwenyezi Mungu amewaonya wanaofanya miamala ya riba kwa vita kutoka Kwake na kutoka kwa Mtume Wake ﷺ, pale Aliposema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ اتَّقُواْ اللّهَ وَذَرُواْ مَا بَقِيَ مِنَ الرِّبَا إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ * فَإِن لَّمْ تَفْعَلُواْ فَأْذَنُواْ بِحَرْبٍ مِّنَ اللّهِ وَرَسُولِهِ وَإِن تُبْتُمْ فَلَكُمْ رُؤُوسُ أَمْوَالِكُمْ لاَ تَظْلِمُونَ وَلاَ تُظْلَمُونَ

"Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu na acheni yaliyobakia katika riba, ikiwa nyinyi ni waumini. Na msipofanya hivyo, basi fahamuni mtatangaziwa vita na Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na mkitubu, basi haki yenu ni rasilimali zenu; msidhulumu wala msidhulumiwe." (QS. Al-Baqarah [2]: 278-279)

Na Ameahidi (Subhanahu wa Ta'ala) yule anayefuata uongofu Wake kupata furaha, na anayepuuza uongofu kupata taabu, akasema:

فَمَنِ اتَّبَعَ هُدَايَ فَلَا يَضِلُّ وَلَا يَشْقَى * وَمَنْ أَعْرَضَ عَن ذِكْرِي فَإِنَّ لَهُ مَعِيشَةً ضَنكاً

"Basi atakayefuata uongofu wangu, hatapotea wala hatataabika. Na atakayejiepusha na mawaidha yangu, basi kwa yakini atakuwa na maisha ya dhiki." (QS. Ta-Ha [20]: 123-124)

Na mwisho:

هَذَا بَيَانٌ لِلنَّاسِ وَهُدًى وَمَوْعِظَةٌ لِلْمُتَّقِينَ

"Huu ni ufafanuzi kwa watu, na ni uongofu na mawaidha kwa wachamungu." (QS. Ali-Imran [3]: 138)

7 Jumada al-Ula 1443 H 11/12/2021 M

Share Article

Share this article with your network