Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Hukumu ya Kushiriki katika Uchaguzi wa Mtawala Anayetawala kwa Kufuru

February 04, 2016
7352

P

(Sura ya Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Ameer wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Wageni wa Ukurasa Wake wa Facebook "Fiqhi")

Jibu la Swali Hukumu ya Kushiriki katika Uchaguzi wa Mtawala Anayetawala kwa Kufuru Kwa Mouadh Seif Elmi

Swali:

Assalamu Alaikum Sheikh wetu, nina swali: Je, ni kweli kwamba Maswahaba waliohamia Habasha walipigana pamoja na Najashi dhidi ya adui yake na wakatamani ushindi wa Najashi na wakafurahia ushindi wake? Kwa sababu kisa hiki kinatumiwa kama ushahidi na baadhi ya masheikh nchini Tunisia kuhusu kuruhusiwa kwa uchaguzi wa bunge na urais, na wanatoa wito wa kuchagua vyama vyenye shari ndogo. Pamoja na shukrani.

Jibu:

Wa Alaikum Salaam Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh,

Kabla ya kuanza kujibu, ningependa kuashiria kuwa Mujtahid anapotafuta hukumu ya kisheria katika suala lolote, ni wajibu wake baada ya kufahamu uhalisia wa suala hilo (waqi’), atafute ushahidi wake katika maandiko ya kisheria (nusus ash-shar’iyyah), kisha achimbue (yastanbit) hukumu ya kisheria ya suala hilo baada ya kuangalia ushahidi unaohusiana nalo... Haifai kuweka maoni katika suala fulani kisha baada ya hapo ndipo aanze kutafuta ushahidi unaoweza kuunga mkono maoni aliyoyachukua. Hii ni kwa sababu kinachotakiwa kisheria ni kuifanya sheria kuwa mwamuzi, yaani kuchukua hukumu kutoka kwenye ushahidi, na sio kutoa maoni kutoka kwa "Mujtahid" kwanza kisha kutafuta ushahidi wa kuunga mkono kauli hiyo. Kitendo hiki si kufuata sheria na wala si kutafuta hukumu ya kisheria, bali ni kufuata matamanio (hawa)...

Anayezingatia kauli za wale wanaoruhusu kushiriki katika mifumo inayotawala kwa sheria za kufuru, na wanaoruhusu kuchagua watawala na wabunge wanaotawala kwa yasiyokuwa sheria za Allah na kuwatungia watu mifumo ya kibinadamu bila mwongozo kutoka kwa Allah, anayezingatia kauli zao atawakuta wakitafiti maandiko ya kisheria huku na kule mpaka wapate kile ambacho ni kidogo kuliko shubhu ya ushahidi ili kuunga mkono kauli yao... Na cha ajabu ni kwamba wanaacha ushahidi wa mkato (qat’i), uliopokelewa kwa wingi (mutawatir) na ulioenea katika Kitabu na Sunnah, na wanatafuta mambo yasiyokuwa wazi ili kutoa maoni yao...

Sasa tunajibu suala lililotajwa katika swali:

Kwa kurejea vitabu vya Seerah (historia ya Mtume), inabainika kuwa haijathibiti chochote kinachoonyesha kuwa Maswahaba walipigana pamoja na Najashi dhidi ya adui yake. Kuna masimulizi yaliyopokewa katika vitabu vya Seerah kuhusu msimamo wa Maswahaba kwenye kadhia ya Najashi na maadui zake, ambayo yanakaribiana ikiwa hayatofanana kabisa. Namnukulu muulizaji hapa riwaya ya Imam Ahmad bin Hanbal katika Musnad yake baada ya kutaja kisa cha Waislamu na Najashi na jinsi alivyowafanyia uadilifu, palikuja yafuatayo:

فَوَاللهِ إِنَّا عَلَى ذَلِكَ إِذْ نَزَلَ بِهِ - يَعْنِي مَنْ يُنَازِعُهُ فِي مُلْكِهِ - قَالَ: فَوَاللهِ مَا عَلِمْنَا حُزْنًا قَطُّ كَانَ أَشَدَّ مِنْ حُزْنٍ حَزِنَّاهُ عِنْدَ ذَلِكَ، تَخَوُّفًا أَنْ يَظْهَرَ ذَلِكَ عَلَى النَّجَاشِيِّ، فَيَأْتِيَ رَجُلٌ لَا يَعْرِفُ مِنْ حَقِّنَا مَا كَانَ النَّجَاشِيُّ يَعْرِفُ مِنْهُ. قَالَتْ: وَسَارَ النَّجَاشِيُّ وَبَيْنَهُمَا عُرْضُ النِّيلِ، قَالَتْ: فَقَالَ أَصْحَابُ رَسُولِ اللهِ ﷺ: مَنْ رَجُلٌ يَخْرُجُ حَتَّى يَحْضُرَ وَقْعَةَ الْقَوْمِ ثُمَّ يَأْتِيَنَا بِالْخَبَرِ؟ قَالَتْ: فَقَالَ الزُّبَيْرُ بْنُ الْعَوَّامِ: أَنَا، قَالَتْ: وَكَانَ مِنْ أَحْدَثِ الْقَوْمِ سِنًّا، قَالَتْ: فَنَفَخُوا لَهُ قِرْبَةً، فَجَعَلَهَا فِي صَدْرِهِ ثُمَّ سَبَحَ عَلَيْهَا حَتَّى خَرَجَ إِلَى نَاحِيَةِ النِّيلِ الَّتِي بِهَا مُلْتَقَى الْقَوْمِ، ثُمَّ انْطَلَقَ حَتَّى حَضَرَهُمْ. قَالَتْ: وَدَعَوْنَا اللهَ لِلنَّجَاشِيِّ بِالظُّهُورِ عَلَى عَدُوِّهِ، وَالتَّمْكِينِ لَهُ فِي بِلادِهِ، وَاسْتَوْسَقَ عَلَيْهِ أَمْرُ الْحَبَشَةِ، فَكُنَّا عِنْدَهُ فِي خَيْرِ مَنْزِلٍ، حَتَّى قَدِمْنَا عَلَى رَسُولِ اللهِ ﷺ، وَهُوَ بِمَكَّةَ

"... Na tulikaa kwake katika nyumba bora na jirani bora. Akasema: Wallahi tulikuwa katika hali hiyo ghafla akavamiwa na mtu anayemnyang'anya ufalme wake. Akasema: Wallahi hatujapata kujua huzuni yoyote iliyokuwa kali kuliko huzuni tuliyoipata wakati huo, kwa kuhofia kwamba yule adui angemshinda Najashi, kisha akaja mtu asiyejua haki yetu kama Najashi alivyokuwa akiijua. Akasema: Najashi akasafiri (kwenda kupigana) na baina yao palikuwa na upana wa mto wa Nile. Akasema: Maswahaba wa Mtume wa Allah ﷺ wakasema: Ni nani atakayetoka kwenda kushuhudia mapigano ya watu hao kisha atuletee habari? Akasema: Az-Zubayr bin Al-Awwam akasema: Mimi. Akasema: Na yeye alikuwa miongoni mwa vijana wadogo zaidi. Akasema: Wakampulizia kiriba cha maji akakiweka kifuani kwake kisha akaogelea kwayo mpaka akafika upande mwingine wa Nile ambapo watu walikuwa wamekutana, kisha akaenda mpaka akawafikia. Akasema: Tukamuomba Allah amnusuru Najashi dhidi ya adui yake, na kumuimarisha katika nchi yake, na mambo ya Habasha yakatulia kwake, tukawa kwake katika makazi bora, mpaka tulipomrudia Mtume wa Allah ﷺ akiwa Makka." (Mwisho).

Na ilikuja katika Al-Bidaya wan-Nihaya ya Ibn Kathir yafuatayo:

قَالَتْ: فَأَقَمْنَا مَعَ خَيْرِ جَارٍ فِي خَيْرِ دار، فلم نشب أَنْ خَرَجَ عَلَيْهِ رَجُلٌ مِنَ الْحَبَشَةِ يُنَازِعُهُ في مِلْكِهِ، فَوَاللَّهِ مَا عَلِمْنَا حُزْنًا حَزِنَّا قَطُّ هُوَ أَشَدُّ مِنْهُ، فَرَقًا مِنْ أَنْ يَظْهَرَ ذَلِكَ الْمَلِكُ عَلَيْهِ فَيَأْتِي مَلِكٌ لَا يَعْرِفُ مِنْ حقنا ما كان يعرفه، فجعلنا ندعو اللَّهَ وَنَسْتَنْصِرُهُ لِلنَّجَاشِيِّ فَخَرَجَ إِلَيْهِ سَائِرًا فَقَالَ أَصْحَابُ رَسُولِ اللَّهِ ﷺ بعضهم لبعض: من يَخْرُجُ فَيَحْضُرُ الْوَقْعَةَ حَتَّى يَنْظُرَ عَلَى مَنْ تكون؟ وقال الزُّبَيْرُ - وَكَانَ مِنْ أَحْدَثِهِمْ سِنًّا - أَنَا، فَنَفَخُوا له قربة فجعلها في صدره، فجعل يَسْبَحُ عَلَيْهَا فِي النِّيلِ حَتَّى خَرَجَ مِنْ شِقِّهِ الْآخَرِ إِلَى حَيْثُ الْتَقَى النَّاسُ، فَحَضَرَ الْوَقْعَةَ فَهَزَمَ اللَّهُ ذَلِكَ الْمَلِكَ وَقَتَلَهُ، وَظَهَرَ النجاشي عليه. فجاءنا الزبير فجعل يليح لَنَا بِرِدَائِهِ وَيَقُولُ أَلَا فَأَبْشِرُوا، فَقَدْ أَظْهَرَ اللَّهُ النَّجَاشِيَّ. قُلْتُ: فَوَاللَّهِ مَا عَلِمْنَا فرحنا بشيء قَطُّ فَرَحَنَا بِظُهُورِ النَّجَاشِيِّ ثُمَّ أَقَمْنَا عِنْدَهُ حتى خرج من خرج منا إِلَى مَكَّةَ، وَأَقَامَ مَنْ أَقَامَ.

"... Akasema: Tulikaa na jirani bora katika nyumba bora, haukupita muda mrefu akatokea mtu miongoni mwa Waethiopia akimvunja katika ufalme wake. Wallahi hatujawahi kuhuzunika huzuni kali kama hiyo, kwa kuogopa kwamba mfalme yule angeshinda kisha akaja mfalme asiyejua haki yetu kama huyu anavyoijua. Tukawa tunamuomba Allah na kumuombea ushindi Najashi. Najashi akatoka kuelekea kwake, Maswahaba wa Mtume ﷺ wakaambiana wenyewe kwa wenyewe: Nani atatoka akashuhudie vita ili aone ushindi utakuwa kwa nani? Az-Zubayr akasema – na alikuwa mdogo wao zaidi – Mimi. Wakampulizia kiriba akakiweka kifuani kwake, akaanza kuogelea mtoni Nile mpaka akatokea upande wa pili mahali watu walipokutana. Akashuhudia vita, Allah akamshinda yule mfalme na akauawa, na Najashi akamshinda. Az-Zubayr akatujia akitupungia kwa vazi lake akisema: 'Furahini, kwani Allah amempa ushindi Najashi.' Akasema: Wallahi hatujapata kufurahi kwa jambo lolote kama tulivyofurahia ushindi wa Najashi, kisha tukakaa kwake mpaka walipotoka walioenda Makka na kubaki waliobaki." (Mwisho).

Sasa hawa watu wamechukua wapi kuwa inaruhusiwa kushiriki katika uchaguzi wa mtawala anayetawala kwa kufuru na kuchagua vyama ili viingie bungeni na kutunga sheria kando na Allah? Wamechukua wapi uhalali wa hayo wakati katika masimulizi haya hakuna sehemu inayosema Maswahaba walishiriki katika vita, wala hawakuwa na maamuzi katika jambo lolote, bali walikuwa wanyonge (mustad’afeen), na hawakufanya zaidi ya kumtuma mdogo wao ili afuatilie habari na kuona ushindi utakuwa wa nani:

  • "Maswahaba wa Mtume wa Allah ﷺ wakasema: Ni nani atakayetoka kwenda kushuhudia mapigano ya watu hao kisha atuletee habari?"

  • "Maswahaba wa Mtume wa Allah ﷺ wakaambiana wenyewe kwa wenyewe: Nani atatoka akashuhudie vita ili aone ushindi utakuwa kwa nani?"

Hivyo basi, ukweli wa jambo hili ni kwamba Maswahaba (ra) walipenda Najashi ashinde dhidi ya adui yake kwa sababu alikuwa mfalme mwadilifu ambaye hadhulumiwi mtu kwake kama alivyowaambia Mtume ﷺ na kama walivyojionea wao wenyewe... Na kwa kuhofia kuwa adui yake angeshinda na asiwatendee uadilifu kama alivyofanya Najashi:

"... Wallahi hatujapata kujua huzuni yoyote iliyokuwa kali kuliko huzuni tuliyoipata wakati huo, kwa kuhofia kwamba yule adui angemshinda Najashi, kisha akaja mtu asiyejua haki yetu kama Najashi alivyokuwa akiijua.", "...Wallahi hatujawahi kuhuzunika huzuni kali kama hiyo, kwa kuogopa kwamba mfalme yule angeshinda kisha akaja mfalme asiyejua haki yetu kama huyu anavyoijua. Tukawa tunamuomba Allah na kumuombea ushindi Najashi..."

Sasa wapi hapo kuna kuchagua mtawala ili atawale kwa kufuru au kuchagua vyama bungeni ili viwatungie watu sheria kando na Allah? Maswahaba walitamani, walipenda na kumuomba Allah amnusuru mfalme aliyewafanyia uadilifu dhidi ya adui yake ambaye huenda angewadhulumu. Hawakushiriki katika chochote kinachoashiria kumchagua mtu ili atawale kwa kufuru au kutunga sheria za kikafiri...

Kwa hiyo, kubatilika kwa kutolea ushahidi tukio hili kwa ajili ya kuruhusu ushiriki wa kumchagua mtawala anayetawala kwa kufuru na kuchagua vyama vya kutunga sheria kando na Allah, ni kubatilika kwa wazi kusikohitaji elimu nyingi au mazingatio makubwa... Hasa kwa kuwa ushahidi wa kuhukumu kwa aliyoyateremsha Allah ni wa mkato katika kuthibiti kwake (qat’i ath-thubut) na wa mkato katika maana yake (qat’i ad-dalalah), na miongoni mwa ushahidi huo ni:

Kauli yake Allah (swt):

وَأَنِ احْكُمْ بَيْنَهُمْ بِمَا أَنْزَلَ اللَّهُ وَلَا تَتَّبِعْ أَهْوَاءَهُمْ وَاحْذَرْهُمْ أَنْ يَفْتِنُوكَ عَنْ بَعْضِ مَا أَنْزَلَ اللَّهُ إِلَيْكَ

"Na uhukumu baina yao kwa aliyoyateremsha Allah, wala usifuate matamanio yao, na uwe na tahadhari nao wasije wakakushawishi ukaacha baadhi ya aliyokuteremshia Allah." (QS Al-Ma'idah [5]: 49)

إِنِ الْحُكْمُ إِلَّا لِلَّهِ

"Hukumu haiko ila kwa Allah tu." (QS Al-An'am [6]: 57)

فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّى يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنْفُسِهِمْ حَرَجًا مِمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا

"La! Naapa kwa Mola wako Mlezi! Hawataamini mpaka wakufanye wewe ndiye mwamuzi katika yale wanayozozana, kisha wasione uzito katika nyoyo zao kwa ulichokihukumu, na wajisalimishe kwa unyenyekevu." (QS An-Nisa [4]: 65)

أَفَحُكْمَ الْجَاهِلِيَّةِ يَبْغُونَ وَمَنْ أَحْسَنُ مِنَ اللَّهِ حُكْمًا لِقَوْمٍ يُوقِنُونَ

"Je, wanatafuta hukumu za kijahilia? Na nani aliye mbora wa kuhukumu kuliko Allah kwa watu wenye yakini?" (QS Al-Ma'idah [5]: 50)

...na aya nyinginezo.

Vilevile, makafiri wa Kikureishi walimpa ofa Mtume ﷺ kwamba wamtawaze kuwa mfalme wao kwa sheria zao bila ya Uislamu, lakini alikataa ﷺ:

Imekuja katika Seerah ya Ibn Ishaq "As-Siyar wal-Maghazi": (Kutoka kwa Ikrima kutoka kwa Ibn Abbas kwamba Utbah na Shaybah wana wa Rabia, na Abu Sufyan bin Harb, na An-Nadr bin Al-Harith... walikutana baada ya jua kuzama nyuma ya Al-Kaaba... wakasema: "Ewe Muhammad... ikiwa unachotafuta kwa jambo hili ni mali, tutakukusanyia mali zetu mpaka uwe tajiri zaidi yetu, na ikiwa unatafuta utukufu kati yetu, tutakufanya kuwa bwana wetu, na ikiwa unataka ufalme, tutakutawaza kuwa mfalme wetu..." Mtume ﷺ akawaambia: "Sijui mnayoyasema, sijawajia na haya niliyokuja nayo kwa ajili ya kutafuta mali zenu, wala utukufu kwenu, wala ufalme juu yenu. Lakini Allah amonituma kwenu niwe Mtume na akaniteremshia Kitabu, na akaniamrisha niwe mbashiri na mwonyaji kwenu. Nimeyafikisha kwenu ujumbe wa Mola wangu, na nimekunasihi. Mkikubali kutoka kwangu niliyokuja nayo, basi hilo ndilo fungu lenu duniani na Akhera. Na mkiyakataa, nitasubiri kwa amri ya Allah mpaka Allah ahukumu baina yangu nanyi.") Maelezo kama haya pia yamekuja katika Dala'il al-Nubuwwah ya Abu Nu'aym al-Asbahani na Seerah ya Ibn Kathir na vitabu vingine vya Seerah.

Kadhalika, walimpa ofa Mtume ﷺ kwamba washirikiane katika mambo yao yote, baadhi kutoka kwao na baadhi kutoka kwake ﷺ, waabudu Mungu wake mwaka mmoja na yeye aabudu miungu yao mwaka mmoja, lakini alikataa ﷺ isipokuwa Uislamu pekee:

Imekuja katika Tafsir ya Al-Qurtubi ya sura (Qul Ya Ayyuhal Kafirun):

(Ametaja Ibn Ishaq na wengineo kutoka kwa Ibn Abbas: Kwamba sababu ya kuteremka kwake ni kwamba Al-Walid bin Al-Mughirah, Al-Aas bin Wa'il, Al-Aswad bin Abd al-Muttalib, na Umayyah bin Khalaf walimkutana Mtume wa Allah ﷺ wakasema: Ewe Muhammad, njoo tuabudu unachokiabudu na wewe uabudu tunachokiabudu, na tushirikiane sisi na wewe katika mambo yetu yote, ikiwa kile ulichokuja nacho ni bora kuliko tulichonacho, basi tutakuwa tumeshirikiana nawe katika hilo na kuchukua fungu letu. Na ikiwa tulichonacho ni bora kuliko ulichonacho, basi utakuwa umeshirikiana nasi na kuchukua fungu lako. Allah (sw) akateremsha: Sema enyi makafiri...) mwisho.

Na imekuja katika Tafsir ya At-Tabari "Jami' al-Bayan" ya sura (Qul Ya Ayyuhal Kafirun):

(Kutoka kwa Ikrima, kutoka kwa Ibn Abbas: Kwamba Maquraishi walimwahidi Mtume wa Allah ﷺ... "Tunakupa chaguo moja ambalo ni kwa faida yako na faida yetu." Akasema: "Ni lipi hilo?" Wakasema: "Uabudu miungu yetu kwa mwaka mmoja: Al-Lat na Al-Uzza, na sisi tuabudu Mungu wako mwaka mmoja." Akasema: "Mpaka nione kitakachokuja kutoka kwa Mola wangu." Wahyi ukaja kutoka katika Lawh al-Mahfuz: (Qul Ya Ayyuhal Kafirun)) mwisho.

Na imekuja katika Fath al-Qadir ya Ash-Shawkani katika tafsir ya (Qul Ya Ayyuhal Kafirun):

(Ametoa Ibn Jarir, Ibn Abi Hatim na At-Tabarani kutoka kwa Ibn Abbas: "Kwamba Maquraishi walimlingania Mtume wa Allah ﷺ... wakasema: Ikiwa hufanyi hivyo basi tunakupa chaguo moja ambalo ndani yake mna heri kwako. Akasema: Ni lipi hilo? Wakasema: Uabudu miungu yetu mwaka mmoja na sisi tuabudu Mungu wako mwaka mmoja. Akasema: Mpaka nione kinachonijia kutoka kwa Mola wangu. Wahyi ukaja kutoka kwa Allah: (Qul Ya Ayyuhal Kafirun * La A'budu Ma Ta'budun) mpaka mwisho wa sura, na Allah akateremsha: (Sema: Je, mnamwamrisha nimwabudu asiyekuwa Allah enyi wajinga?) mpaka kauli yake: (Bali muabudu Allah pekee na uwe miongoni mwa wanaoshukuru)...) mwisho.

Na huu wote ni ushahidi wa wazi katika kukataza kwa mkato na ukali dhidi ya kuhukumu kwa yasiyoyateremsha Allah, na dhidi ya ushirikiano wowote katika hukumu hiyo. Na hakuna anayesimama dhidi ya ushahidi huu wa wazi isipokuwa yule anayemuasi Allah na Mtume wake ﷺ uasi wa wazi, na hoja yoyote nyingine anayokuja nayo ni hoja batili itakayomletea fedheha duniani, na adhabu ya Allah ni kubwa zaidi.

Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

Link ya jibu kutoka kwa ukurasa wa Facebook wa Ameer: Facebook

Link ya jibu kutoka kwa ukurasa wa Google Plus wa Ameer: Google Plus

Link ya jibu kutoka kwa ukurasa wa Twitter wa Ameer: Twitter

Link ya jibu kutoka tovuti ya Ameer: Al-Ameer

Share Article

Share this article with your network