Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

JIBU LA SWALI: Je, Imani Inazidi na Kupungua?

July 02, 2013
8226

(Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook)

Kwa Al-Wathiq bin Nasrullah

Swali:

Assalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh... Naomba jibu la swali langu: "Je, imani inazidi na kupungua?" Na ningependa kuongeza swali lingine linalofuatana nalo: "Je, imani inatofautiana kati ya muumini mmoja na mwingine?"

Jibu:

Wa Alaikum Salaam Warahmatullahi Wabarakatuh.

1- Iman ni kusadikisha kwa yakini (at-tasdiq al-jazim) kunakowafikiana na uhalisia kutokana na ushahidi (dalili). Kusadikisha kwa yakini maana yake ni kukinai (kuridhika kiakili) kwa kukata shauri kusikoweza kubeba shaka yoyote, na hii ndiyo maana yenyewe ya kilugha ya imani, yaani kusadikisha kwa yakini. Na kunakowafikiana na uhalisia maana yake ni kwamba ukweli unaohisiwa unaisadikisha na hauipingi. Na ili iwe kusadikisha kwa yakini na kunakowafikiana na uhalisia, ni lazima iwe imetokana na ushahidi (dalili) uliokatwa (wa mkato) usahihi wake; iwe ushahidi huo ni wa kiakili (aqli), yaani matokeo ya utafiti wa kiakili katika mambo yanayohisiwa kama vile kutafiti viumbe vinavyohisiwa ili kutolea ushahidi kuwepo kwa Allah (swt) Muumba wao, au kwa kutafiti maneno ya Allah yaliyoteremshwa – Qur’an Tukufu – ili kutolea ushahidi kuwa ni maneno ya Allah (swt) na si maneno ya mwanadamu, na kisha kutolea ushahidi kuwa (Muhammad) aliyekuja na maneno ya Allah ni Mtume kutoka kwa Allah. Au ushahidi huo uwe wa kunukuliwa (naqli), yaani kupitia njia ya mapokezi ya mkato kutoka kwa Allah (swt) katika Kitabu Chake kitukufu au kutoka kwa Mtume Wake (saw) katika hadith zake Mutawatir (zilizopokelewa na wengi), na hiyo ni kama kuamini mambo ya ghaibu, malaika, vitabu vilivyoteremshwa hapo awali, mitume waliopita, Siku ya Mwisho, na Qadar (kadari) kheri yake na shari yake. Allah (swt) anasema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا آمِنُوا بِاللَّهِ وَرَسُولِهِ وَالْكِتَابِ الَّذِي نَزَّلَ عَلَى رَسُولِهِ وَالْكِتَابِ الَّذِي أَنْزَلَ مِنْ قَبْلُ وَمَنْ يَكْفُرْ بِاللَّهِ وَمَلَائِكَتِهِ وَكُتُبِهِ وَرُسُلِهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا بَعِيدًا

"Enyi mlioamini! Mwaminini Allah na Mtume wake, na Kitabu alichokiteremsha kwa Mtume wake, na Kitabu alichokiteremsha kabla yake. Na anayemkataa Allah, na Malaika wake, na Vitabu vyake, na Mitume wake, na Siku ya Mwisho, basi huyo amepotea upotevu wa mbali." (QS. An-Nisa [4]: 136)

Na Mtume (saw) anasema katika hadith ya Muslim kutoka kwa Abdullah bin Umar akisema: Alinihadithia baba yangu Umar bin al-Khattab akasema: Siku moja tulipokuwa tumekaa na Mtume wa Allah (saw), ghafla alitutokezea mtu aliyevaa nguo nyeupe sana, mwenye nywele nyeusi sana... akasema: Ewe Muhammad... nieleze kuhusu imani (iman). Akasema:

أَنْ تُؤْمِنَ بِاللهِ، وَمَلَائِكَتِهِ، وَكُتُبِهِ، وَرُسُلِهِ، وَالْيَوْمِ الْآخِرِ، وَتُؤْمِنَ بِالْقَدَرِ خَيْرِهِ وَشَرِّهِ

"Ni kumuamini Allah, na Malaika Wake, na Vitabu Vyake, na Mitume Wake, na Siku ya Mwisho, na kuamini Qadar, kheri yake na shari yake."

... Kisha akaniambia: "Ewe Umar, je, unamjua yule muulizaji?" Nikasema: Allah na Mtume Wake wanajua zaidi. Akasema: "Hakika huyo ni Jibril, amekujieni kuwafundisha dini yenu."

2- Hii ndiyo imani, na kwa maana hii ni kinyume cha ukafiri (kufr). Hivyo, asiyekuwa muumini ni kafiri kwa yakini, na hakuna nusu muumini wala nusu kafiri. Allah (swt) anasema akilinganisha imani na ukafiri:

إِنَّ اللَّهَ لَا يَسْتَحْيِي أَنْ يَضْرِبَ مَثَلًا مَا بَعُوضَةً فَمَا فَوْقَهَا فَأَمَّا الَّذِينَ آمَنُوا فَيَعْلَمُونَ أَنَّهُ الْحَقُّ مِنْ رَبِّهِمْ وَأَمَّا الَّذِينَ كَفَرُوا فَيَقُولُونَ مَاذَا أَرَادَ اللَّهُ بِهَذَا مَثَلًا

"Hakika Allah haoni haya kupiga mfano hata wa mbu na ulio juu yake. Ama wale walioamini wanajua kuwa hiyo ni haki inayotoka kwa Mola wao Mlezi; na ama wale waliokufuru husema: Allah amekusudia nini kwa mfano huu?" (QS. Al-Baqarah [2]: 26)

Na Anasema (swt):

إِنَّ الَّذِينَ اشْتَرَوُا الْكُفْرَ بِالْإِيمَانِ لَنْ يَضُرُّوا اللَّهَ شَيْئًا وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ

"Hakika wale walionunua ukafiri kwa imani, hawatamdhuru Allah chochote, na watapata adhabu chungu." (QS. Ali-Imran [3]: 177)

Na Anasema Aliyetukuka:

وَلَكِنِ اخْتَلَفُوا فَمِنْهُمْ مَنْ آمَنَ وَمِنْهُمْ مَنْ كَفَرَ

"Lakini walikhitilafiana; basi wapo miongoni mwao walioamini, na wapo miongoni mwao waliokufuru." (QS. Al-Baqarah [2]: 253)

Na kuna aya nyingine nyingi zinazolinganisha imani na ukafiri.

3- Imani kwa maana hii tuliyoitaja (kusadikisha kwa yakini kunakowafikiana na uhalisia kutokana na ushahidi) haizidi wala haipungui kwa sababu ni kusadikisha kwa yakini, na yakini (mkato) haiwi isipokuwa kamilifu. Hivyo, hakuna imani ya asilimia 90% kisha ikazidi hadi 95% au 100%, na wala hakuna imani ya 100% kisha ikapungua hadi 95% au 90%, kwa sababu upungufu huu maana yake ni kukosekana kwa yakini (kutokukata shauri) yaani ni shaka, na hapo haitakuwa imani bali ni ukafiri.

4- Na ili picha iwe wazi tunasema:

Maneno ya kuzidi na kupungua ni miongoni mwa maneno yenye maana zaidi ya moja kilugha (alfadh mushtarakah). Huja kwa maana ya kuongezeka na kupungua kwa kiasi (idadi), yaani katika upana na ukubwa, na huja kwa maana ya nguvu na udhaifu (quwwah wa dha'f). Kiashiria cha maneno (qarinah) ndicho kinachoamua ni maana gani inayokusudiwa. Ikiwa kuzidi na kupungua kumehusishwa na imani, basi maana yake ni kwa upande wa nguvu na udhaifu, kwa sababu kusadikisha kwa yakini haisahihi kwake kuongezeka au kupungua kwa kiasi (idadi). Kwa sura hii, aya hizi zinaeleweka:

الَّذِينَ قَالَ لَهُمُ النَّاسُ إِنَّ النَّاسَ قَدْ جَمَعُوا لَكُمْ فَاخْشَوْهُمْ فَزَادَهُمْ إِيمَانًا وَقَالُوا حَسْبُنَا اللَّهُ وَنِعْمَ الْوَكِيلُ

"Wale ambao watu waliwaambia: Hakika watu wamekwishakusanyeni, basi waogopeni! Hayo yakawazidishia imani, na wakasema: Allah anatutosha, naye ni Mlinzi bora kabisa." (QS. Ali-Imran [3]: 173)

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللَّهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَعَلَى رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ

"Hakika waumini ni wale ambao anapotajwa Allah nyoyo zao hujaa khofu, na wanaposomewa Aya zake huwazidishia imani, na wanamtegemea Mola wao pekee." (QS. Al-Anfal [8]: 2)

وَلَمَّا رَأَى الْمُؤْمِنُونَ الْأَحْزَابَ قَالُوا هَذَا مَا وَعَدَنَا اللَّهُ وَرَسُولُهُ وَصَدَقَ اللَّهُ وَرَسُولُهُ وَمَا زَادَهُمْ إِلَّا إِيمَانًا وَتَسْلِيمًا

"Na waumini walipoyaona makundi (ya maadui), walisema: Haya ndiyo aliyotuwahidi Allah na Mtume wake; na Allah na Mtume wake wamesema kweli. Na hayo hayakuwazidishia ila imani na unyenyekevu." (QS. Al-Ahzab [33]: 22)

Yaani waumini imani yao imekuwa na nguvu na imeshitadi (imeimarika) kwa sababu ya mambo haya ambayo Allah (swt) ameyaeleza katika aya zilizotangulia. Hivyo, imani inazidi na kupungua kwa matendo ya utiifu, kushikamana na hukumu za kisheria (ahkam shar'iyyah), khofu ya Allah, na kupigana Jihadi katika njia Yake... yote hayo ni kwa sababu imani kwa maana tuliyoieleza (kusadikisha kwa yakini kunakowafikiana na uhalisia kutokana na ushahidi) haisahihi kwake kuzidi au kupungua kwa maana ya kiasi, la sivyo isingekuwa ya yakini na ingegeuka kuwa shaka na kuwa ukafiri.

Inafaa kutaja kuwa (imani) inapokuja bila ya viashiria (qarina), maana yake ni ile tuliyoitaja hapo juu. Na ikija kwa maana nyingine, basi kiashiria kitafafanua, kwa mfano:

وَمَا كَانَ اللَّهُ لِيُضِيعَ إِيمَانَكُمْ

"Na Allah hakuwa wa kupoteza imani yenu (Sala zenu)." (QS. Al-Baqarah [2]: 143)

Hapa inamaanisha Sala zenu, kwa sababu Waislamu baada ya kubadilishiwa kibla, ilishuka aya hii kuwatuliza Waislamu kuwa Sala zao zilizotangulia kuelekea kibla cha kwanza zimekubaliwa na wanayo malipo yake. Na kwa mfano hadith ya Mtume (saw) aliyoitoa An-Nasa'i kutoka kwa Abu Hurairah akisema: Mtume wa Allah (saw) amesema:

الْإِيمَانُ بِضْعٌ وَسَبْعُونَ شُعْبَةً، أَفْضَلُهَا لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ، وَأَوْضَعُهَا إِمَاطَةُ الْأَذَى عَنِ الطَّرِيقِ

"Imani ina matawi sabini na kitu; lililo bora zaidi ni kusema La ilaha illa Allah (Hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila Allah), na la chini kabisa ni kuondoa kero njiani."

Na inajulikana kuwa kutokuondoa kero hakumfanyi mtu kuwa kafiri, na kwa hiyo imani hapa inamaanisha matendo ya utiifu kwa Allah kwa ujumla.

Tunamuomba Yeye (swt) azifanye nyoyo zetu ziwe na utulivu kwa imani, na tuwe katika kauli na vitendo vyetu wenye kushikamana na hukumu za Uislamu, na Allah (swt) atufufue pamoja na wale aliowaneemesha miongoni mwa Manabii, Masiddiqi, Mashahidi na Waja wema, na hao ndio marafiki bora kabisa.

Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

Link ya jibu kutoka kwa ukurasa wa Amir kwenye Facebook

Link ya jibu kutoka kwenye tovuti ya Amir

Link ya jibu kutoka kwa ukurasa wa Amir kwenye Google Plus

Share Article

Share this article with your network