Swali:
Shirika la habari la SUNA mnamo tarehe 23/03/2014 lilimnukuu Balozi Osman Dirar, mtaalamu wa kitaifa katika urais wa Jamhuri ya Sudan, akisema: "Msimamo wa Amerika kuhusu Hati ya Doha ya amani ya Darfur unagongana moja kwa moja na msimamo na matakwa ya wadau wa kweli ndani ya Darfur...". Alikuwa akitoa maoni yake kuhusu kauli ya mwakilishi wa Marekani katika Baraza la Usalama, Samantha Power, katika mchango wake mbele ya mkutano wa Baraza la Amani la Afrika huko Addis Ababa tarehe 10/03/2014 ambapo alisema: ("Hati ya Doha imepitwa na wakati na haitegemeki tena, na akalitaka Baraza kutafuta jukwaa jipya la kutatua suala la Darfur") akijua kwamba Amerika ndiyo iliyokuwa nyuma ya kusainiwa kwa hati hii huko Doha mnamo tarehe 14/07/2011. Je, hii inamaanisha kuwa Amerika imejitoa kwenye makubaliano ya Doha? Na ikiwa sivyo, ni vipi tunaweza kuelewa kauli ya mwakilishi wa Marekani katika Baraza la Usalama, Samantha Power? Mwenyezi Mungu akulipe kheri.
Jibu:
1- Ndiyo, Amerika ndiyo iliyokuwa nyuma ya kusainiwa kwa Makubaliano ya Doha, na ilifanya kila juhudi katika hilo. Lengo lilikuwa ni kuondoa ushawishi wa Wazungu; Amerika ilikuwa ikifanya kazi ya kushikilia nyuzi za suala la Darfur peke yake huku ikijitahidi kuziondoa Ufaransa na Uingereza na kuwaacha wao na mawakala wao nchini Chad na Qatar washiriki tu katika sherehe za utiaji saini, washuhudie kwa uongo, na washiriki katika kulipa gharama muhimu na fidia kwa wakimbizi, hususan Qatar ambayo inacheza nafasi fulani kwa maslahi ya Uingereza. Jukumu kubwa ambalo Amerika iliwapa ni kuwaweka katika kamati ya utaratibu wa ufuatiliaji wa utekelezaji wa kile kilichoamuliwa, yaani kama waangalizi wa kimataifa wanaotekeleza maamuzi ya Amerika katika hati inayohusu Darfur. Pamoja na hayo, Ulaya (Ufaransa na Uingereza) haitakubali kwa urahisi Amerika ijivunie Darfur peke yake kama ilivyofanya huko Kusini mwa Sudan. Ingawa wamelegeza msimamo wao kuelekea makubaliano hayo... si zaidi ya mapumziko ya mpiganaji mpaka Ulaya itakapopata fursa inayofaa kupenya makubaliano haya kwa namna ambayo itaweza kushika tena nyuzi za Darfur, hata kama si nyuzi zote.
2- Hati hiyo ni muhimu kwa Amerika, na Amerika imeichukulia kama mafanikio makubwa! Amerika haichukulii makubaliano haya kama ya mwisho, bali iliyaona kama hatua mbele kuelekea suluhisho la kudumu la mgogoro wa Darfur. Hii inamaanisha kuwa Amerika inasema kuwa itafuatiwa na hatua nyingine ambazo huenda zisitoshe tu kwa eneo la Darfur kufurahia utawala wa ndani wenye mamlaka mapana, bali jambo hilo linaweza kufikia kuiondoa Darfur kabisa kutoka Sudan kwa kutengeneza makubaliano mengine kwa mfano wa makubaliano ya Naivasha, kwa kutoa haki ya kujiamulia mustakabali kwa watu wa Darfur mpaka kura ya maoni itakapofanyika na kufuatiwa na kujitenga kama ilivyotokea Kusini mwa Sudan. Kwa hiyo, haiwezekani kwa Amerika kuacha vipengele vya msingi katika Hati ya Doha kwa sababu ni hatua mojawapo katika hatua zake za kuhodhi suala la Darfur, ikifuatiwa na hatua mpya.
3- Hata hivyo, mambo mawili yalitokea, ambapo kwayo Amerika ilijaribu kuipumbaza Ulaya kuwa Amerika hapingi kuishirikisha Ulaya katika suala la Darfur, na kujadili upya Makubaliano ya Doha kupitia kauli za hadaa. Kukubaliwa kwa kauli hizo na Ulaya kungesababisha majadiliano kuhusu Makubaliano ya Doha ambayo hayatapelekea kubadilisha vipengele vyake vya msingi, bali kuyapamba kwa baadhi ya marekebisho madogo ili kuridhisha pande nyingine na kisha kuyatia saini. Mambo hayo mawili ni:
Kwanza: Harakati ya Ukombozi na Uadilifu (Liberation and Justice Movement) iliyotia saini Makubaliano ya Doha inakumbwa na migogoro, kiasi kwamba habari zilienea kuhusu kujiuzulu kwa Naibu Rais wa harakati hiyo kwa masuala ya kisiasa, Ahmed Kaber Jibril, ambaye ni Naibu Gavana wa Darfur Mashariki. Katibu Mkuu wa harakati hiyo, Bahr Idriss Abu Garda, alikiri migogoro hii akisema: "Hali ndani ya harakati si shwari kutokana na changamoto kubwa zinazokabili mipango ya kiusalama na utekelezaji wa ratiba nyinginezo." Alibainisha kuwa "kuna mawasiliano na harakati ambazo hazikutia saini (Hati ya Doha ya amani) ili kujiunga na mchakato wa amani, kwa sababu amani haitakamilika bila kusainiwa kwa harakati zote za kijeshi huko Darfur (kwenye hati ya) amani." (27/02/2014 Akher Lahza). Harakati hii haijashikamana, bali ni mkusanyiko wa watu ili kuongeza idadi na kupata mafanikio fulani kwa haraka zaidi. Ni kama harakati nyingine za uasi nchini Sudan, zote zinatawaliwa na migawanyiko na migogoro kwa sababu viongozi wake wana mafungamano na mataifa ya nje, wanatafuta fedha na madaraka, na hawaongozwi na misingi wala fikra. Wanatumia vibaya hali mbaya ya watu kutokana na dhuluma na ukosefu wa huduma, bali kutokuwa na uwezo wa dola kutoa huduma na kushindwa kwake kusimamia mambo... Hivyo ndivyo harakati hizo zinavyotenda kwa kutegemea nchi za kikoloni moja kwa moja, ambapo nchi hizi hufanya kazi ya kutengeneza uongozi mpya utakaofuata utiifu wa kikaragosi na kutekeleza malengo yao ya kikoloni. Migogoro hii ndani ya Harakati ya Ukombozi na Uadilifu inaathiri mshikamano wake, nayo ni harakati ambayo Amerika iliitengeneza kutokana na waliojitenga na harakati nyingine za uasi ili kuongoza mazungumzo na kutia saini Hati ya Doha baada ya kuzitenga harakati nyingine zinazofuata Wazungu kama vile Harakati ya Uadilifu na Usawa na Harakati ya Ukombozi wa Sudan.
Pili: Machafuko ya kisiasa yanayoendelea dhidi ya serikali huko Khartoum, ambapo yameanza kushika kasi hivi karibuni kiasi cha kumfanya Rais wa serikali hiyo, Omar al-Bashir, kutafuta suluhu za kutuliza hali... Alikuwa katika hali ya msukosuko iliyomlazimisha kuwasiliana na viongozi wanaoiunga mkono Uingereza ambao alikuwa amekwisha waondoa madarakani! Hii inaashiria kuishiwa kwa suluhu kwa serikali hiyo na kwamba iko katika hali mbaya na hali ya kisiasa ni tete dhidi yake.
4- Ulaya (Uingereza na Uaransa) imetumia mambo haya mawili na kuona fursa imepatikana ambapo inaweza kufidia kuondolewa kwake katika suala la Kusini mwa Sudan, ili idhibiti suala la Darfur, au angalau iwe na nafasi muhimu katika suluhisho. Kwa hivyo, mawakala wake walichukua jukumu la kufanya kazi kwa nguvu huko Kusini mwa Sudan ili kudhoofisha ushawishi wa Amerika huko na kuishughulisha hapo, na huko Darfur ili kuweka hali mpya ya kisiasa itakayoilazimisha Amerika kutoiondoa Ulaya katika kutatua tatizo la Darfur, na kisha iwe na maoni yenye uzito katika suluhisho. Maelezo ya hayo huko Kusini mwa Sudan na Darfur ni kama ifuatavyo:
a- Ama huko Darfur, katika kipindi cha hivi karibuni kumekuwa na maendeleo ya kushangaza ambapo baadhi ya harakati za uasi huko Darfur zimeongeza kasi ya matukio, wakati harakati hizi zilipoanza mashambulizi makali mwanzoni mwa mwezi uliopita, Februari 2014, kiasi kwamba El Fasher, mji mkuu wa Jimbo la Darfur Kaskazini, ukawa si salama, vilevile Nyala, mji mkuu wa Darfur Kusini. Wakaazi wa miji hiyo miwili wakawa katika hali ya hofu na wasiwasi baada ya waasi kudhibiti eneo la "Tawila" lililo umbali wa kilomita 60 kutoka El Fasher. Vilevile makundi ya kijeshi yalishambulia takriban vijiji 45 katika eneo lililo umbali wa kilomita 50 kutoka Nyala. Habari zimeeleza kuwa Harakati ya Ukombozi wa Sudan mrengo wa Minawi na kando yake Harakati ya Ukombozi na Uadilifu mrengo wa Ali Karbino ambao hawakutia saini Makubaliano ya Doha, walifanya shambulizi katika maeneo ya Haskanita na Al-Lait "Jar al-Nabi" na kwamba waliyadhibiti. Vilevile walifanya shambulizi huko Mellit na Al-Twaisha, mahali alipozaliwa Gavana Osman Kibir. Gavana wa Darfur Kaskazini, Osman Yusif Kibir, alinusurika jaribio la mauaji ambapo dereva wake na mmoja wa walinzi wake waliuawa. "Jeshi la Sudan lilikiri shambulizi hili na kulilaani, likiwatuhumu mamluki wa Minni Arko Minawi, kiongozi wa Harakati ya Ukombozi wa Sudan inayoasi huko Darfur, kwa kutekeleza jaribio hilo na kujaribu kuvuruga usalama na utulivu na kuwatisha wananchi katika mji wa Mellit katika jimbo la Darfur Kaskazini." "Vyanzo vya kuaminika vilisema kuwa Kibir aliyetembelea Jumamosi iliyopita (15/03/2014) eneo la Mellit lililoshambuliwa na waasi na wananchi wakakataa kumpokea, msafara wake ulishambuliwa kwa kuvamiwa na watu wenye silaha wakati akirejea kutoka mjini humo." (Al-Watan Saudi Arabia 18/03/2014). Kilichoongeza joto na athari ya matukio haya ni kwamba majeshi ya kulinda amani yanayoundwa na nchi nyingi hayakuweza kuzuia mashambulizi haya kama alivyobainisha mwakilishi wa Amerika, kwa sababu ndani ya majeshi haya kuna nguvu zinazofuata Wazungu na si zote ni nguvu za Amerika tupu. Hii ilimfanya mwakilishi wa Amerika kukosoa nafasi yao na kutotimiza wajibu wao wa kuzuia kuzuka kwa matukio ya hivi karibuni yaliyochochewa na harakati za uasi zinazofuata Wazungu.
b- Ama huko Kusini mwa Sudan, matukio ya Darfur yalienda sambamba na kile kilichotokea Kusini mwa Sudan katika miezi ya hivi karibuni ya uasi wa Riek Machar, wakala wa Waingereza, dhidi ya Salva Kiir, wakala wa Amerika. Uasi huu bado unaendelea na unaisumbua Amerika na haijaweza kuukomesha mpaka sasa...
Hivyo ndivyo Ulaya (Uingereza na Ufaransa) ilivyochochea harakati za uasi zinazoiunga mkono ili kuwasha moto wa vita upya huko Darfur baada ya utulivu wa kiasi tangu kusainiwa kwa Hati ya Doha... Ni wazi kutokana na harakati hizi kuwa zimepangwa ili kutengeneza hali mpya ya kisiasa inayolazimisha kushirikishwa kwa harakati ambazo hazikutia saini Hati ya Doha kwa njia yenye athari, na kwamba zirudi uwanjani upya. Kinachothibitisha kuwa harakati hizi za uasi zimefanya kazi kwa mpango ulioandaliwa na Wazungu ni kauli ya Abu Ubaida Abdullah al-Ta’ishi, Msaidizi wa Rais wa Harakati ya Jeshi la Ukombozi wa Sudan - mrengo wa Minawi kwa masuala ya habari na mahusiano ya umma, ambaye alisema: "Ushindi wa harakati hiyo katika jimbo la Darfur umeweka hali mpya ya kisiasa." (Ukurasa wa Sudan Tribune 18/03/2014).
5- Haya yote yaliifanya Amerika kupitia kwa mwakilishi wake kutoa kauli hiyo ili kuipumbaza Ulaya kuwa Amerika iko tayari kuweka tena Makubaliano ya Doha mezani, na kukidhi matakwa ya harakati za uasi ambazo hazikutia saini ili ziwe na nafasi "yenye athari" kwa sasa kwa kufuta Hati ya Doha au kurekebisha vipengele vyake vya msingi... Ikijulikana kuwa Amerika kwa kweli inashikilia misingi mikuu katika hati hiyo kwani inaiona kama mafanikio muhimu na hatua ya kwanza katika njia ya mradi wake wa kuitenga Darfur. Lakini kauli hiyo inakusudiwa kuwa ni hadaa ili kuziingiza harakati ambazo hazikutia saini Makubaliano ya Doha mpaka zije kuzitia saini baada ya kuingiza baadhi ya mapambo. Kinachodhihirisha kuwa Amerika haitaki kuangusha misingi mikuu katika Hati ya Doha ya amani huko Darfur ni kutowekwa kwa ule msemo uliotajwa na mwakilishi wa Amerika Power mbele ya mkutano wa Amani na Usalama wa Afrika huko Addis Ababa ("Hati ya Doha imepitwa na wakati na haitegemeki tena, na akalitaka Baraza kutafuta jukwaa jipya la kutatua suala la Darfur"), kutoiweka katika taarifa yake rasmi aliyoitoa baada ya siku mbili ambayo ilichapishwa katika tovuti ya (IIP Digital, tovuti rasmi ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Amerika 14/03/2014). Hotuba yake aliyoitoa katika mkutano huo haikuchapishwa kwenye tovuti rasmi ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Amerika kama ilivyo kawaida, bali walitengeneza taarifa mpya iliyobeba kile alichokitaja katika mkutano huo isipokuwa ule msemo! Hii inaashiria mchezo wa maneno; aliutaja katika mchango wake, lakini hakuutaja katika tovuti rasmi ya Wizara ya Mambo ya Nje ili usichukuliwe rasmi dhidi yake kwa sababu kile kinachochapishwa kwenye tovuti kinakuwa ni hotuba rasmi inayoelezea sera ya utawala wa Amerika. Hivyo basi, Hati ya Doha ni mojawapo ya mafanikio ya Amerika yaliyoifanya ishike suala la Darfur ili kulihodhi peke yake, na imebatilisha makubaliano ambayo Ulaya ilikuwa na mkono ndani yake kama vile makubaliano ya Abuja mwaka 2006 na makubaliano ya mfumo na Harakati ya Uadilifu na Usawa mwaka 2009. Kwa hivyo, ni vigumu kwa Amerika kuacha vipengele vya msingi katika hati hii ambayo Amerika inapanga nyuma yake kufanya makubaliano ya amani ya kina kwa ajili ya kujiamulia mustakabali wa Darfur kwa mfano wa makubaliano ya Naivasha.
6- Kuhusu yale yaliyodhihirika katika kauli za Sudan za kupinga kauli za mwakilishi wa Amerika, hizo si zaidi ya kurusha mchanga machoni (hadia), na yote hayo si lolote bali ni kukamilisha hadaa ambayo Amerika imetengeneza nyuzi zake ili kuwaonyesha Wazungu kuwa inaandaa mpango utakaoiridhisha Ulaya na mawakala wake hata kama hautaridhisha serikali ya Sudan! Hiyo ni ili kuleta utulivu kuwa Amerika ni mkweli katika wito wake ili Ulaya iwasukume mawakala wake kushiriki katika mazungumzo kuhusu Hati ya Doha. Amerika inatambua kuwa wakiingia kwenye mazungumzo, watashughulika na marekebisho madogo kwenye makubaliano yatakayochukua muda mrefu wa kurekebisha hapa na kutorekebisha pale, kuvutana... Na wakati huo huo, harakati za kijeshi za waasi zitakuwa zimetulia kama si kutoweka kabisa! Hiyo ni kwa kisingizio cha kutovuruga hali ya mazungumzo. Kinachobainisha kuwa kauli za serikali nchini Sudan kuhusu kukerwa kwake na kauli za mwakilishi wa Amerika ni kelele tupu zisizo na matendo, ni kile alichotangaza mwakilishi mwenyewe katika taarifa yake ya tarehe 14/03/2014 ambapo alitaja utayari wa serikali ya Sudan kwa mazungumzo ya kisiasa na akaziita harakati za kijeshi kushiriki katika mazungumzo ya kisiasa yanayolenga kufikia suluhu ya kisiasa ya amani na ya kina. Na hivi ndivyo vilivyokuja katika taarifa ya mwakilishi iliyochapishwa mnamo 14/03/2014: "Tunaona kuwa serikali ya Sudan ilitaja katika mwezi wa Januari kuwa iko tayari kuongoza mazungumzo ya kisiasa yatakayojumuisha wadau wote katika uwanja wa kisiasa pamoja na makundi ya kijeshi yaliyokataa vurugu... Na sisi tunahimiza makundi yote ya kijeshi ikiwemo makundi yanayosaidiwa na serikali ya Sudan kukomesha mashambulizi yote ya vurugu na kushiriki katika mazungumzo ya kisiasa yanayolenga kufikia suluhu ya amani na ya kina kwa migogoro ya damu nchini Sudan ikijumuisha kutatua tofauti zilizobaki kuhusu Darfur...". (IIP Digital tovuti rasmi ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Amerika 14/03/2014). Hii inaashiria uratibu kamili kati ya serikali ya Sudan na Amerika... Na kwamba yeye, yaani Amerika, anataka kujionyesha kana kwamba yuko upande wa harakati hizi dhidi ya serikali ya Sudan na kwamba anataka kuifanya serikali itii matakwa ya harakati hizi ili harakati hizi zisitishe mashambulizi yao na kisha zije kufanya mazungumzo na serikali chini ya usimamizi wa Amerika.
7- Muhtasari ni kwamba kauli za mwakilishi wa Amerika dhidi ya Makubaliano ya Doha ni sehemu ya hadaa ili kuipumbaza Ulaya na mawakala wake kuwa Amerika iko siriazi katika kuwashirikisha kwenye suluhu ya tatizo la Darfur, na kwamba inakubali kujadiliwa kwa Makubaliano ya Doha kati ya makundi yaliyokusanyika ili kupata suluhu ya Darfur kwa ridhaa ya wote na bila kumtenga yeyote... Ukweli wa mambo ni kwamba inashikilia misingi mikuu katika Makubaliano ya Doha, na inataka kupitia kauli zake kuonyesha kuwa iko siriazi na kwamba iko pamoja na maslahi ya Ulaya na harakati ambazo hazikutia saini... Na ili kuwapumbaza na ukweli wake, kulikuwa na kauli hizo zinazoonyesha hitilafu na serikali ya Sudan! Yote hayo, kama tulivyosema, ni kwa ajili ya kuipumbaza Ulaya na mawakala wake ili waingie kwenye mazungumzo ya kisiasa kuhusu makubaliano ya kutatua tatizo la Darfur, na kisha kusitisha harakati za uasi vitendo vyao vya kijeshi huko Darfur kwa kisingizio cha kutovuruga hali ya mazungumzo.
Inasikitisha sana kuona kuwa masuala ya Waislamu yanadhibitiwa na mataifa ya kikafiri ya kikoloni mbele ya macho na masikio ya watawala madhalimu mawakala katika nchi za Waislamu. Wakoloni wanapanga njama dhidi ya Uislamu na watu wake waziwazi mchana kweupe, na hakuna mtawala yeyote katika nchi za Waislamu anayethubutu kusema hapana!
ذَلِكُمْ وَأَنَّ اللَّهَ مُوهِنُ كَيْدِ الْكَافِرِينَ
"Hivyo ndivyo, na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kudhoofisha hila za makafiri." (QS Al-Anfal [8]: 18)