Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Je, Hizb ut-Tahrir Inachukuliwa Kuwa ni ya Kiash’ari?

July 27, 2021
7353

Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mkubwa Ata bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir

kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook "Fikri"

Kwa Riyadh Abu Malik

Swali:

Mwenyezi Mungu akubariki Ewe Sheikh na akufungulie milango ya kheri. Nina swali ikiwa utaruhusu: Je, Hizb ut-Tahrir inachukuliwa kuwa ni ya Kiash'ari katika maudhui ya Aqidah, au ina ufahamu wake maalum katika maudhui ya Aqidah? Na shukrani.

Jibu:

Assalamu Alaikum Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh,

Kabla ya kujibu moja kwa moja swali lako, ningependa kusisitiza yafuatayo:

Kwanza: Ukweli wa Hizb ut-Tahrir:

1- Hizb ut-Tahrir imejitambulisha kama ifuatavyo: (Ni chama cha kisiasa ambacho mabda’ yake ni Uislamu. Siasa ni kazi yake, na Uislamu ni mabda’ yake. Kinafanya kazi miongoni mwa Umma na pamoja nao ili kuufanya Uislamu kuwa ndio kadhia yake kuu, na kuuongoza katika kurudisha Khilafah na utawala wa yale aliyoteremsha Mwenyezi Mungu katika maisha. Hizb ut-Tahrir ni mkusanyiko wa kisiasa, na si mkusanyiko wa kiroho, wala mkusanyiko wa kielimu, wala wa kutoa mafunzo, wala mkusanyiko wa kutoa misaada; na fikra ya Kiislamu ndiyo roho ya mwili wake, kiini chake na siri ya maisha yake). Kwa mujibu wa ufafanuzi huu, Hizb ut-Tahrir si shule ya kifikra, wala si kikundi cha elimu ya kalamu, wala si madhehebu ya kifikihi, bali ni chama cha kisiasa kinachochukua kadhia za Umma na kuzitetea, na kufanya kazi ya kusimamisha Uislamu katika maisha na kuulinda baada ya kusimamishwa kwake... Na chama kinaamini Aqidah ya Kiislamu na kinamchukulia kila anayeamini Aqidah ya Kiislamu kuwa ni ndugu yake:

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ

"Hakika Waumini ni ndugu." (QS. Al-Hujurat [49]: 10)

Na kinajadili naye katika nukta yoyote ya hitilafu kwa njia iliyo bora...

2- Hizb ut-Tahrir imetabanni (imechukua) fikra, hukmu, na rai zinazoilazimu kwa ajili ya kutekeleza kazi yake, na kuziweka ndani ya vitabu na matoleo yake... Lakini haikujadili kila suala na kila fikra, na haikutabanni katika masuala mengi, hususan katika masuala ya utafiti wa kiitikadi na ibada, kwa sababu hiyo haiilazimu katika kazi yake kama chama cha kisiasa kinacholenga kuuamsha Umma na kusimamisha Dola ya Khilafah, na kinachosimamia fikra na hisia za Umma... Kwa mfano, kimetabanni katika suala la 'Ismah (kuhifadhiwa na madhambi) kwa Manabii na Mitume, na kimetabanni katika suala la ijtihad ya Mtume ﷺ kwa sababu ya athari yake katika ufahamu wa kisheria (tashri’)... Lakini hakikutabanni katika masuala mengine mengi ambayo wanachuoni wa kalamu waliingia ndani yake...

3- Chama kimejifunga na nguvu ya dalili, na jambo hili limejitokeza wazi katika juhudi zake za kudumu za kupitia upya tsaqofah yake na tabanni zake na kutegemea nguvu ya dalili... Kimefanya marekebisho ya vitabu vyake na kuviboresha kulingana na hilo. Hakikung'ang'ania rai yoyote ambayo dalili yake ilibainika kuwa dhaifu na dalili ya rai nyingine kuwa yenye nguvu zaidi, bali kiliacha rai yenye dalili dhaifu na kuchukua rai iliyothibiti kuwa na dalili yenye nguvu. Hili liko wazi katika masahihisho na mabadiliko kadhaa ya vitabu vya chama, na pia katika mapitio kamili ya vitabu vyake ambayo hufanywa mara kwa mara...

Pili: Baadhi ya Waislamu walizipa shule na madhehebu ya kifikra yaliyotofautiana katika tafiti zinazohusu matawi ya Aqidah na masuala ya kalamu majina maalum kama vile Ash’ariyah kwa kunasibishwa na Imam Al-Ash’ari (R.A), Maturidiyah kwa kunasibishwa na Imam Al-Maturidi (R.A), Salafiyah na nyinginezo... Na wakayaita maoni yao kuwa ni Aqidah, wakasema: Aqidah Ash’ariyah, Aqidah Maturidiyah, Aqidah Salafiyah na mfano wa hayo. Bali walitaja matini za wanachuoni fulani na vitabu vyao kuwa ni Aqidah, wakasema: Aqidah Tahawiyyah kwa kunasibishwa na Imam At-Tahawi (R.A), na wakasema: Aqidah Wasitiyyah kwa kunasibishwa na risala iliyoandikwa na Imam Ibn Taymiyyah (R.A) kwa watu wa Wasit... n.k. Ukweli ni kwamba kutumia neno Aqidah kwa hayo yote si jambo sahihi na haliko mahali pake, na husababisha mkanganyiko na mfarakano miongoni mwa Waislamu. Hii ni kwa sababu msimamo wa madhehebu kuhusu masuala yanayohusiana na tafiti za kiitikadi siyo Aqidah. Bali Aqidah ni ile Aqidah ya Kiislamu iliyothibiti katika Sharia kwa dalili za qat’i (zenye kukata) na hii hairuhusiwi kuwa na hitilafu ndani yake... Hivyo basi, hakuna kitu kinachoitwa Aqidah Ash’ariyah au Aqidah Salafiyah au Aqidah Tahawiyyah, bali kuna Aqidah ya Kiislamu pekee inayowaunganisha Waislamu wote kila mahali na kwa tofauti za madhehebu na rai zao. Na kuna rai tofauti miongoni mwa madhehebu na shule za kifikra kama vile Ash’ariyah, Maturidiyah, Salafiyah na nyinginezo katika tafiti zinazohusu masuala ya matawi yasiyokuwa Aqidah ya Kiislamu, na kila upande una rai yake ambayo haimtoi katika Aqidah ya Kiislamu.

Tatu: Manhaj (mbinu) ambayo chama kimeifuata katika kutabanni fikra, hukmu na rai ni kuchukua rai kulingana na nguvu ya dalili, iwe dalili ya kiakili au ya nakli (naqli), bila kuangalia nani aliyeisema. Kwa sababu hiyo, Hizb ut-Tahrir katika baadhi ya masuala ya matawi ya itikadi imetabanni mambo yaliyosemwa na Waash’ari, na imetabanni mambo mengine yaliyosemwa na wengineo... Na katika masuala ya kisheria imechukua rai kutoka katika madhehebu ya kifikihi mashuhuri na mengineyo bila kujifunga na madhehebu maalumu... Kwa hiyo, Hizb ut-Tahrir haisemwi kuwa ni Shafi’i au Hanafi kwa mfano, wala haisemwi kuwa ni Ash’ari au Salafi, wala Maturidi au Mu’tazili, wala haisemwi kuwa ni ya shule ya rai (Ahlur-Ra’y) au shule ya hadithi (Ahlul-Hadith)... n.k. Hizb ut-Tahrir si chochote katika hayo yote, bali ni chama cha kisiasa ambacho mabda’ yake ni Uislamu, na kinachukua rai kulingana na nguvu ya dalili yake kwa mujibu wa manhaj madhubuti iliyoitobanni katika vitabu vyake bila kujali msemaji wake. Katika rai zake kuna baadhi ya yale waliyoyasema Waash'ari, baadhi ya yale waliyoyasema Masalafi, na baadhi ya yale yaliyosemwa na shule nyinginezo. Hayo yote ni kwa kutegemea nguvu ya dalili, na si kwa kujifunga na rai za moja ya shule hizo na kufuata manhaj yake, fikra zake, au rai zake. Chama hakitambui migogoro iliyotokea kati ya Waislamu huko nyuma, bali kinawaona Waislamu kuwa ni Umma mmoja licha ya tofauti za madhehebu na mielekeo yao, na kinawaita kuitikia wito wake na kufanya kazi pamoja nacho kusimamisha Uislamu, kubeba Da’wah na kuunganisha Umma chini ya bendera ya Khilafah ya Kiislamu.

Nataraji jibu hili linatosheleza. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi zaidi na Mwenye Hekima zaidi.

Ndugu yenu Ata bin Khalil Abu Al-Rashtah

17 Dhul-Hijjah 1442 H Mswania 27/07/2021 M

Kiungo cha jibu kutoka katika ukurasa wa Amir (Mwenyezi Mungu amlinde) kwenye Facebook

Kiungo cha jibu kutoka katika ukurasa wa Amir (Mwenyezi Mungu amlinde) kwenye Web

Share Article

Share this article with your network