Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Je, Inajuzu kwa Bay'ah ya Khalifa Kuwa na Muda Maalum?

October 28, 2016
4355

(Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amiri wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Wageni kwenye Ukurasa Wake wa Facebook "Fiqhi")

Jibu la Swali

Kwa: Taqi Naser

Swali:

Assalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh Sheikh wetu mtukufu, salamu kisha:

Swali langu ni kuhusu bay'ah ambayo ni mkataba wa ridhaa kati ya Ummah na Khalifa, je, inajuzu kwa bay'ah hiyo kuwa na muda maalum kama vile miaka minne au mitano kama ilivyozoeleka katika mifumo ya sasa? Na je, wale wanaosema hivyo wana dalili au shaka ya dalili (shubhatu dalil)?

Barakallahu fika, na Mwenyezi Mungu atujalie sisi na nyinyi miongoni mwa wale ambao Mwenyezi Mungu anawatumia katika kunusuru Uislamu na kuupa tamkini.

Jibu:

Wa Alaikum Salaam Warahmatullahi Wabarakatuh,

1- Hakika maandiko ya bay'ah kwa Khalifa yanapingana na kuifunga kwa muda maalum, kwa sababu bay'ah kwa Mtume ﷺ na bay'ah kwa Makhalifa Waongofu ilikuwa ni juu ya kuhukumu kwa Kitabu cha Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta'aala) na Sunnah za Mtume Wake ﷺ. Hili ndilo sharti lake; hivyo basi, ikiwa Khalifa ataacha kuhukumu kwa Kitabu cha Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta'aala) na Sunnah za Mtume Wake ﷺ, basi mamlaka yake yanakoma kwa mujibu wa hukumu za kisheria zilizoelezwa katika hilo, ambazo zilifafanua namna ya kumvua Khalifa madarakani na mamlaka ya Mazhalim (Mahakama ya Malalamiko)... Na kuweka sharti lingine haijuzu kwa sababu linapingana na andiko la bay'ah, ambalo ni kuhukumu kwa Kitabu cha Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta'aala) na Sunnah za Mtume Wake ﷺ. Na hili limethibiti kupitia Sunnah na Ijma al-Sahaba (Maafikiano ya Maswahaba):

Ama Sunnah, Al-Bukhari amepokea kutoka kwa Ubadah bin al-Samit... akasema: Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ alituita tukampa bay'ah, na miongoni mwa yale aliyotuchukulia ahadi ni:

أَنْ بَايَعَنَا عَلَى السَّمْعِ وَالطَّاعَةِ فِي مَنْشَطِنَا وَمَكْرَهِنَا، وَعُسْرِنَا وَيُسْرِنَا، وَأَثَرَةٍ عَلَيْنَا، وَأَنْ لَا نُنَازِعَ الْأَمْرَ أَهْلَهُ... إِلَّا أَنْ تَرَوْا كُفْرًا بَوَاحًا عِنْدَكُمْ مِنَ اللهِ فِيهِ بُرْهَانٌ

"Kwamba alituchukulia bay'ah (ahadi) ya kusikia na kutii katika hali tunayopenda na tunayochukia, katika uzito wetu na wepesi wetu, na hata kama tutanyimwa haki yetu (upendeleo kwa wengine juu yetu), na kwamba tusiwakabili (tusigombee mamlaka) wenye jambo hilo... isipokuwa mkiona ukafiri wa wazi ambao mnao ushahidi kutoka kwa Mwenyezi Mungu juu yake." (Imepokewa na Muslim pia).

Na Muslim pia amepokea kutoka kwa Yahya bin Husain, kutoka kwa bibi yake Umm al-Husain, akasema: Nilimsikia akisema: Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ amesema:

إِنْ أُمِّرَ عَلَيْكُمْ عَبْدٌ مُجَدَّعٌ - حَسِبْتُهَا قَالَتْ - أَسْوَدُ، يَقُودُكُمْ بِكِتَابِ اللهِ تَعَالَى، فَاسْمَعُوا لَهُ وَأَطِيعُوا

"Ikiwa mtawekewa kiongozi mtumwa aliyekatwa viungo - nadhani alisema - mweusi, anayewaongoza kwa Kitabu cha Mwenyezi Mungu Mtukufu, basi msikilizeni na mumtii."

Ni wazi kutokana na yote hayo kuwa kuendelea kwa bay'ah na utii ni maadamu kuhukumu kunaendelea kwa Kitabu cha Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta'aala) na Sunnah za Mtume Wake ﷺ, isipokuwa panapotokea ukafiri wa wazi (kufr bawah), yaani ukiukaji wa dhahiri wa Sharia.

Ama Ijma al-Sahaba, hakika bay'ah ya Makhalifa Waongofu ilikuwa ni juu ya kuhukumu kwa Kitabu cha Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta'aala) na Sunnah za Mtume Wake ﷺ, na haikuwa kwa muda maalum. Na bay'ah yao ilikuwa mbele ya hadhara ya Maswahaba (Radhiya Allahu Anhum), hivyo ikawa ni Ijma (maafikiano) ya kutoainisha muda, bali kuendelea kwa Khalifa kunategemea utii wake kwa Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta'aala) na kwa Mtume Wake ﷺ, yaani kuhukumu kwa yale aliyoteremsha Mwenyezi Mungu. Ma'mar bin Rashid amepokea katika Jami' yake akisema: Abu Bakr alituhutubia akasema:

يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنِّي قَدْ وُلِّيتُ عَلَيْكُمْ وَلَسْتُ بِخَيْرِكُمْ... أَطِيعُونِي مَا أَطَعْتُ اللَّهَ وَرَسُولَهُ، فَإِذَا عَصَيْتُ اللَّهَ وَرَسُولَهُ فَلَا طَاعَةَ لِي عَلَيْكُمْ، قُومُوا إِلَى صَلَاتِكُمْ يَرْحَمْكُمُ اللَّهُ

"Enyi watu, hakika nimepewa mamlaka juu yenu na mimi si mbora wenu... Nitii mimi maadamu ninamtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, lakini nikimuasi Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, basi sina utii kwenu. Simameni kwa ajili ya swala yenu, Mwenyezi Mungu awarehemu."

Ni wazi kutokana na dalili hizi kwamba muda haujaainishwa, bali utii wa Khalifa kwa Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta'aala) na Mtume Wake ﷺ ndio uliotajwa. Kwa hivyo, maadamu Khalifa anahukumu kwa yale aliyoteremsha Mwenyezi Mungu, basi mamlaka yake yanaendelea. Ikiwa atakiuka andiko la mkato (la Sharia), basi mamlaka yake yanakoma hata kama yamedumu mwezi mmoja au miezi miwili... na hiyo ni kwa mujibu wa hukumu za kisheria zilizoelezwa kuhusu kumvua Khalifa na mamlaka ya Qadhi wa Mazhalim...

2- Ama kuhusu swali ikiwa wale wanaosema kuainisha muda wana dalili au shaka ya dalili, hakika sisi hatuoni kwao dalili yoyote wala shaka ya dalili. Tumelifafanua jambo hili kwa ukamilifu katika jibu la swali tulilolitoa tarehe 16 Jumada al-Akhira 1434 H sawia na 06/04/2013 M, hivyo linaweza kurejewa.

Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu al-Rashtah

26 Muharram 1438 H Sawia na 27/10/2016 M

Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amiri kwenye Facebook

Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amiri kwenye Google Plus

Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amiri kwenye Twitter

Kiungo cha jibu kutoka kwenye tovuti ya Amiri

Share Article

Share this article with your network