Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

JAWABU LA SWALI: JE, INAJUZU KWA ARDHI KUWA NA MALIPO YA KIFEDHA?

May 27, 2016
5301

(Mfululizo wa majibu ya mwanachuoni mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi")

Jawabu la Swali

Kwa Saleh Natseh

Swali:

Assalamu Alaikum, nina swali kuhusu hukumu ya watu wawili kushirikiana katika kulima ardhi; wa kwanza ana ardhi na wa pili anailima, je jambo hili linaruhusiwa au ni Muzara’ah? Kwani jambo hili limenitatiza; miongoni mwa vijana wapo waliosema kuwa ni Muzara’ah, na wengine wakasema inajuzu, kwa kuwa mwenye ardhi anaweza kuiuza ndani ya miaka mitatu ambayo ni muda aliopewa kuilima. Allah awabariki.

Jawabu:

Wa Alaikum Salam Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh,

Muzara’ah ni kukodisha ardhi kwa ajili ya kuilima, na kumekuja dalili nyingi juu ya uharamu wa Muzara’ah, miongoni mwazo ni:

1- Al-Bukhari amepokea katika Sahih yake kutoka kwa Abu Hurairah (ra), amesema: Mtume wa Allah (saw) amesema:

مَنْ كَانَتْ لَهُ أَرْضٌ، فَلْيَزْرَعْهَا أَوْ لِيَمْنَحْهَا أَخَاهُ، فَإِنْ أَبَى، فَلْيُمْسِكْ أَرْضَهُ

"Mwenye kuwa na ardhi, basi na ailime au ampe ndugu yake, akigoma, basi na aiweke ardhi yake." (Sahih Bukhari)

2- Kutoka kwa Jabir (ra):

أَنَّ النَّبِيَّ ﷺ نَهَى عَنِ الْمُخَابَرَةِ

"Kwamba Mtume (saw) amekataza Al-Mukhabarah." (Imepokelewa na Muslim), na Al-Mukhabarah ni Muzara’ah.

3- Na katika Sahih Muslim kutoka kwa Jabir bin Abdullah, amesema:

نَهَى رَسُولُ اللهِ ﷺ أَنْ يُؤْخَذَ لِلْأَرْضِ أَجْرٌ، أَوْ حَظٌّ

"Mtume wa Allah (saw) amekataza kuchukuliwa kwa ajili ya ardhi ujira au fungu." (Sahih Muslim)

4- Amepokea Rafi’ bin Khadij amesema: Tulikuwa tukifanya Al-Mukhabarah wakati wa Mtume wa Allah (saw), akataja kuwa mmoja wa ami zake alimjia na kusema: Mtume wa Allah (saw) amekataza jambo ambalo lilikuwa na manufaa kwetu, lakini utiifu kwa Allah na Mtume wake ni wenye manufaa zaidi kwetu. Amesema: Tukasema, ni jambo gani hilo? Akasema: Mtume wa Allah (saw) amesema:

مَنْ كَانَتْ لَهُ أَرْضٌ فَلْيَزْرَعْهَا، أَوْ فَلْيُزْرِعْهَا أَخَاهُ، وَلَا يُكَارِيهَا بِثُلُثٍ وَلَا بِرُبُعٍ وَلَا بِطَعَامٍ مُسَمًّى

"Mwenye kuwa na ardhi basi na ailime, au ampe ndugu yake ailime, na wala asiikodishe kwa thuluthi (moja ya tatu), wala kwa robo, wala kwa chakula maalum." (Imetolewa na Abu Dawud).

5- Na katika Sunan An-Nasa'i kutoka kwa Usaid bin Zhuhair:

نَهَى رَسُولُ اللهِ ﷺ عَنْ كِرَاءِ الأَرْضِ، قُلْنَا: يَا رَسُولُ اللهِ، إِذًا نُكْرِيهَا بِشَيْءٍ مِنْ الْحَبِّ، قَالَ: لا، قَالَ: وَكُنَّا نُكْرِيهَا بِالتِّبْنِ، فَقَالَ: لا، وَكُنَّا نُكْرِيهَا عَلَى الرَّبِيعِ، قَالَ: لا، ازْرَعْهَا أَوْ امْنَحْهَا أَخَاكَ

"Mtume wa Allah (saw) amekataza kukodisha ardhi. Tukasema: Ewe Mtume wa Allah, basi tutaikodisha kwa sehemu ya nafaka? Akasema: Hapana. Akasema: Tulikuwa tukiikodisha kwa majani (ya ngano/shayiri), akasema: Hapana. Na tulikuwa tukiikodisha kwa sehemu ya kando ya mfereji (wa maji), akasema: Hapana, ilime au mpe ndugu yako." (Sunan An-Nasa'i). Na Al-Rabi’: Ni mto mdogo, yaani bonde, yaani tulikuwa tukiikodisha kwa kulima sehemu iliyo kando ya Al-Rabi’ yaani kando ya maji.

Ni wazi kutokana na hadithi hizi uhalisia wa Muzara’ah kuwa ni kukodisha ardhi, iwe ujira unaolipwa ni sehemu ya mazao au ni kitu kingine... kadhalika ni wazi kutokana nazo uharamu wa Muzara’ah...

Na dalili zilizotajwa hapo juu zinabainisha kuwa haijuzu kwa ardhi kuwa na malipo yoyote, hususan hadithi ya Muslim kwani iko wazi katika hilo: "Mtume wa Allah (saw) amekataza kuchukuliwa kwa ajili ya ardhi ujira au fungu", na kadhalika hadithi ya Al-Bukhari "Mwenye kuwa na ardhi, basi na ailime au ampe ndugu yake...", na hadithi ya An-Nasa'i "...ilime au mpe ndugu yako", kwa hivyo ardhi haijuzu kuwa na malipo.

* Kutokana na hayo, yale yaliyokuja katika swali lako (wa kwanza ana ardhi na wa pili anailima...) hapa ardhi imechukuliwa kama mali na ina fungu, yaani hukumu ya Muzara’ah inaitatua na haiafiki kuipatia jina la ushirika bali hiyo ni Muzara’ah na haijuzu. Vilevile, haiathiri katika hukumu ya kisheria ikiwa Muzara’ah hiyo itafanyika ndani ya miaka mitatu au baada yake, kwani hukumu ya kisheria inashughulikia mkataba wenyewe. Hivyo basi, mkataba huo ni batili madamu kumewekwa malipo ya kifedha kwa ajili ya ardhi hiyo ya aina yoyote ile kama ilivyofafanuliwa katika dalili zilizotajwa hapo awali...

Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

19 Sha'ban 1437 H Mwafaka na 26/05/2016 M

Kiungo cha jawabu kutoka kwa ukurasa wa Facebook wa Amir: ! facebook

Kiungo cha jawabu kutoka kwa ukurasa wa Google Plus wa Amir: ! Googleplus

Kiungo cha jawabu kutoka kwa ukurasa wa Twitter wa Amir: ! Twitter

Kiungo cha jawabu kutoka tovuti ya Amir

Share Article

Share this article with your network