Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Ukweli wa Mgogoro wa Ukraine, Vipimo na Motisha Zake

December 22, 2021
9123

Swali:

Al-Jazeera ilichapisha mnamo 20/12/2021 kwenye tovuti yake: [Jeshi la Ukraine na waasi wanaoiunga mkono Moscow wamebadilishana risasi, jambo lililosababisha vifo kwa pande zote mbili... Maendeleo haya yanakuja siku moja baada ya Katibu wa Baraza la Usalama wa Taifa na Ulinzi la Ukraine, Oleksiy Danilov, kutangaza kuwa nchi yake imeandaa mpango wa utekelezaji wa kina unaohusisha mashirika yote na sekta za jeshi, kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hiyo, kujiandaa na uvamizi wowote kutoka kwa Urusi, kama alivyosema. Ukraine iliishutumu Urusi kwa kukusanya wanajeshi wapatao 100,000 karibu na mpaka wake kwa ajili ya maandalizi ya kuishambulia kufikia mwisho wa Januari ijayo... Hata hivyo, Urusi ilikanusha kuwa inapanga kuivamia Ukraine... Al-Jazeera 20/12/2021]. Je, ni upi ukweli wa mgogoro huu, vipimo vyake na vichocheo vyake? Na nini kinachotarajiwa kutokana na ushindani huu, hasa kati ya Urusi na Marekani?

Jibu:

Ili jibu liwe wazi, tunapitia mambo yafuatayo:

1- Urusi ya kifalme (Czarist Russia) ilidhibiti ardhi ya Ukraine wakati wa karne ya kumi na sita, kisha watu wa Ukraine wakaanza kushirikiana na Warusi katika ukoloni wao kwa maeneo mengine na kuwasaidia kutawala mataifa mengine, kiasi kwamba mataifa yaliyotawaliwa mara chache yaliweza kutofautisha kati ya Warusi na Waukraine, hasa kwa kuwa wote wawili wanatokana na jamii ya Waslavu (Slavic race). Wakati Umoja wa Kisovieti uliposambaratika mnamo 1991, na Ukraine kupata uhuru wake mwaka huo huo, ikawa nchi ya pili katika eneo la "Umoja wa Kisovieti" ikiwa na eneo la kipekee kaskazini mwa Bahari Nyeusi, idadi kubwa ya watu iliyofikia milioni 40, muundo wa kiviwanda usiopungua ule wa Urusi, na ghala la silaha za nyuklia lililowakilisha theluthi moja ya urithi wa Kisovieti. Hiyo ilikuwa kabla ya kunyang'anywa silaha hizo kwa mujibu wa makubaliano ya Marekani na Urusi na Ukraine mkabala na ahadi ya Marekani na Urusi kulinda umoja wa ardhi ya Ukraine na kuhifadhi uhuru wake. Ukraine ilipitia mazungumzo marefu na magumu na Urusi kuhusu meli za kivita za Bahari Nyeusi za "Kisovieti", ambazo Urusi ilirithi sehemu kubwa na zikaendelea kuwekwa katika bandari ya Sevastopol katika rasi ya Crimea ndani ya Ukraine kwa mujibu wa mkataba wa upangaji.

2- Nguvu ya Urusi ilikuwa ikishindwa kuirudisha Ukraine kwenye himaya yake katika kila mzozo, iwe ni katika suala la kugawana meli za Bahari Nyeusi mwanzoni mwa miaka ya tisini, au katika suala la mabomba marefu ya gesi ambayo Umoja wa Kisovieti ulikuwa ameyajenga ndani ya Ukraine kusafirisha gesi kutoka ardhi ya Urusi kwenda Ulaya, na kilichojitokeza baada ya suala hili ni hitaji la Urusi la njia mbadala kama vile bomba la TurkStream kupitia Bahari Nyeusi au Nord Stream kupitia Bahari ya Baltic kwenda Ujerumani. Pia katika masuala ya kibiashara ambapo soko la Urusi lina uhitaji mkubwa wa sukari na mafuta yanayozalishwa na ardhi yenye rutuba ya Ukraine, au suala la uanachama wa Ukraine katika taasisi mbalimbali zilizoundwa na Urusi kwa nchi za zamani za mfumo wa Kisovieti, au baada ya hapo kwa kujitokeza kwa mwelekeo wa Ukraine kuelekea Umoja wa Ulaya na Nato. Migogoro hii yote ya Urusi na Ukraine haikuifanya Urusi iweze kurejesha utawala wake juu ya Ukraine katika miongo mitatu iliyopita licha ya ubora wa kijeshi wa Urusi...

3- Ukraine ni bustani ya mbele ya Urusi, na kwa Urusi, Ukraine si kama Asia ya Kati, kwa mfano, ambayo ni bustani ya nyuma kwa upande wa eneo, mafungamano ya kitaifa, dini na historia. Ukraine ndiyo sura ya mbele ya Urusi na nafasi yake ya kimataifa; inatazama Bahari Nyeusi na kuidhibiti, mbali na mtazamo wake juu ya maeneo ya Kiislamu ya Caucasus ambayo Urusi iliyanyakua katika historia yote. Kutokana na ardhi yenye rutuba ya Ukraine, Urusi inapata usalama wake wa chakula katika bidhaa za msingi zinazoikinga na mabadiliko ya uhusiano wake na Magharibi, na kupitia Ukraine inapita kwenda Ulaya Mashariki iwe kwa mabomba ya gesi au vinginevyo. Zaidi ya hayo yote, Ukraine leo inawakilisha eneo la mwisho la bafa (buffer zone) kutatua fundo la kihistoria la Urusi linalowakilishwa na hofu dhidi ya Ulaya ambayo ilivamiwa kwayo mara mbili (Napoleon na Hitler). Ikiwa udhaifu wa dola ya Kisovieti uliilazimisha kuachana na Ulaya Mashariki kama eneo la bafa, basi mbele ya kusonga mbele kwa muungano wa Nato kuelekea Ulaya Mashariki, Urusi inataka angalau kutoka kwa majirani zake wawili, Ukraine na Belarus, waipatie eneo linaloitenga na hatari za Nato na kusonga mbele kwa zana zake za kijeshi kuelekea Mashariki. Urusi leo inataka kuizuia Ukraine kujiunga na muungano wa Atlantiki ya Kaskazini "Nato", au kuungwa mkono nayo (Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergey Ryabkov, alizingatia msaada wa kijeshi wa Marekani kwa Ukraine kama "changamoto kubwa kwa usalama wa Urusi"... Al-Ain News, 13/4/2021).

4- Magharibi, na hasa Marekani, walitambua ukweli wa fundo hili la Ukraine katika siasa za Urusi, na kwamba Ukraine inawakilisha ubavu dhaifu zaidi wa Urusi, hasa baada ya kuimarika kwa harakati za kitaifa nchini Ukraine na kukita kwa uadui wao dhidi ya Urusi. Kwa hiyo, Ukraine imekuwa kwa miongo miwili kitovu cha msuguano wa Marekani na Ulaya dhidi ya Urusi. Kufuatia Mapinduzi ya Machungwa yaliyomwondoa Rais wa Ukraine Yanukovych anayeiunga mkono Urusi mnamo 2014, Moscow ilijibu mwaka huo huo kwa kuimega rasi ya Crimea iliyo kusini mwa Ukraine na kuiunganisha na Urusi, ambayo inamiliki kambi kubwa za kijeshi za kimkakati katika rasi hiyo. Haikuishia hapo, bali iliwasukuma waasi wa Kirusi nchini Ukraine kuchochea maeneo ya mashariki na kutangaza uhuru wa mikoa miwili (Donetsk na Luhansk) ili Warusi wajitegemee kwa jina la "Urusi Ndogo", na kuwapa msaada wa kijeshi. Haya yote yaliisukuma Ukraine kwenye mikono ya Magharibi, na baada ya hapo Ukraine ikaanza kudai na kusisitiza kujiunga na muungano wa Nato kwa matumaini kuwa utailinda dhidi ya uchokozi wa Urusi. Magharibi ilianza kuikaribisha na kuonekana kama mtetezi wake, hivyo Ukraine ikaanza kualikwa kwenye mikutano ya Ulaya na mikutano ya "Nato" hasa wakati migogoro na Urusi inapozidi, bila ya kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya au "Nato". Marekani ilianza kuipatia silaha na misaada ya kijeshi ya mabilioni ya dola na kuanza kulifunza jeshi lake...

5- Urusi imekumbwa na vikwazo vikali vya Magharibi (Ulaya na Marekani) tangu ilipoinyakua rasi ya Crimea, hivyo ilijaribu kufidia hilo kwa kuongeza uhusiano wake wa kiuchumi na Uchina. Ilitandaza mabomba ya kusafirisha mafuta na gesi kwenda Uchina, na kuifungulia Uchina njia ya nchi kavu (reli) kusafirisha bidhaa za Kichina moja kwa moja hadi Ulaya, yaani ilishirikiana nayo katika mfumo wa mradi mkubwa wa Uchina "Njia ya Hariri" (Silk Road). Zaidi ya hayo, ilianza kuondokana na akiba yake ya dhamana za Marekani na dola, na kukomboa biashara yake kwa kiasi kikubwa kutoka kwa dola. Ingawa Urusi si jitu la kibiashara kama Ulaya au Uchina, Marekani iliona kuwa Urusi inatoa changamoto kwa utawala wa kiuchumi wa Marekani na kuzichochea nchi nyingine kwa ujasiri kufanya hivyo. Hili linajitokeza katika mikataba mingi ya kibiashara ya Urusi, hasa na Uchina, kwa kutumia sarafu za ndani kama mbadala wa dola. Hili lilikuwa tishio kwa Marekani, ambalo liliongezewa hivi karibuni na kile Urusi ilichotuhumiwa nacho cha kupandisha bei za gesi ili iwe tatizo jipya la kiuchumi kwa Ulaya.

6- Urusi inatazama vipimo na faida kubwa za Ukraine kwa upande wa historia, utawala, uchumi na usalama, yaani eneo la bafa dhidi ya Nato. Hivyo, inaichukulia kama mstari mwekundu, (Putin aliuonya muungano wa Nato dhidi ya kupeleka vikosi na silaha zake nchini Ukraine, akisema: "Upanuzi wa miundombinu ya kijeshi ya Nato nchini Ukraine ni mstari mwekundu kwa Urusi na utasababisha jibu kali," lakini Rais wa Marekani Joe Biden alisema kuwa haheshimu mistari myekundu ya upande wowote kuhusu Ukraine. Noon Post, 4/12/2021). Kwa sababu hiyo yote, Urusi, wakati inadhibiti mgogoro wa sasa wa Ukraine, haina nia ya kuiacha Ukraine na kuiacha iwe mawindo rahisi kwa Marekani na Nato, hasa baada ya kujaribu vikwazo vya Magharibi na kuvistahimili. Zaidi ya hayo, inaona kuwa shughuli kuu ya Marekani leo ni kukabiliana na Uchina, ikimaanisha kuwa Marekani haitachukua hatua ya kuingiza Ukraine katika uanachama wa Nato kwa sababu ya rasilimali za Marekani zinazohitajika kuilinda Ukraine, kwani hilo litadhoofisha maandalizi ya Marekani katika Mashariki ya Mbali kukabiliana na Uchina... Pia Urusi haitoi uzito mkubwa kwa Ulaya ambayo ni dhaifu kijeshi na inategemea Urusi kwa kiasi kikubwa katika masuala ya nishati, ikimaanisha kuwa Urusi inahisi kuwa hali ya kimataifa ni nzuri kwake kupata mafanikio nchini Ukraine. Kwa sababu hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergey Lavrov, alimfahamisha mwenzake wa Marekani, Antony Blinken, kuwa Moscow inahitaji (dhamana za usalama za muda mrefu mipakani mwake upande wa magharibi ambazo zitazuia upanuzi wa muungano wa Atlantiki ya Kaskazini - Nato - kuelekea Mashariki... akiongeza "jambo ambalo lazima lichukuliwe kama takwa la lazima"), kama ilivyonukuliwa na lango la Al-Wasat la Libya, mnamo 2/12/2021.

7- Huku ndiko ukweli wa madai kutoka upande wa Urusi yanayochochea mvutano huu nchini Ukraine. Urusi inaona kuwa Magharibi inaongeza silaha nchini Ukraine, na kwamba Magharibi inaweza kuisukuma Ukraine, baada ya kuimarisha jeshi lake, kuwaangamiza waasi wa Kirusi mashariki mwa Ukraine, na inaweza kuisukuma baada ya hapo kwenye vita katika rasi ya Crimea, na haya yote ni hatari kwa Urusi. Mkuu wa Majeshi ya Urusi, Valery Gerasimov, alisema, (kwamba kuipatia Ukraine ndege, droni na helikopta kutaifanya Kyiv kuchukua hatua hatari... lakini uchochezi wowote kutoka kwa Kyiv kutatua hali ya Donbas kwa nguvu utazimwa. RT, 9/12/2021). Hivyo, mgogoro wa sasa unafichua kuwa Urusi inalenga kwanza kutokuwa na shaka katika kubaki kwa Crimea kama sehemu yake, bali inataka hilo liwe jambo la kweli (de facto) kwa kutambuliwa kimataifa na Marekani na Ulaya. Lengo la pili ni mashariki mwa Ukraine kuwa nje ya mamlaka ya Ukraine na kuwa chini ya utawala wa Urusi. Lengo la tatu lenye ushawishi mkubwa zaidi ni kuzuia kujiunga kwa Ukraine kwenye Nato na kwamba inahitaji dhamana kwa hilo, hasa baada ya mazoezi ya kijeshi ya pamoja kati ya Nato na Ukraine katika Bahari Nyeusi ambapo Rais wa Urusi Vladimir Putin alisema wakati huo (kwamba mazoezi ya hivi karibuni yaliyofanywa na muungano wa Atlantiki ya Kaskazini "Nato" katika Bahari Nyeusi yamevuka mipaka yote, na akaona kuwa Magharibi haichukulii maonyo ya nchi yake kwa uzito wa kutosha. Katika hotuba aliyotoa mbele ya maafisa wa sera za mambo ya nje huko Moscow, Rais wa Urusi aliashiria kuwa kuruka kwa ndege za kivita za kimkakati za muungano wa Nato umbali wa kilomita 20 kutoka mpaka wa nchi yake kunavuka mipaka yote inayoruhusiwa. Alisema "Washirika wetu wa Magharibi wanazidisha hali kwa kuipatia Kyiv silaha za kisasa hatari na kufanya mazoezi ya kijeshi ya uchochezi." Al-Jazeera Net, 18/11/2021).

8- Marekani ilikubali madai ya Urusi kwa kufanya mkutano wa kilele kati ya Marais wawili, Putin wa Urusi na Biden wa Marekani. Mkutano huo ulifanyika mnamo 7/12/2021 na mgogoro wa Ukraine ulikuwa mada yake kuu lakini si pekee. Ilibainika wakati wa mkutano huo kuwa Urusi inadai Marekani itambue mistari myekundu inayochorwa nchini Ukraine, na ikabainika pia kuwa Marekani inaionya Urusi kwa vikwazo vya kiuchumi ikiwa itachukua hatua ya kuivamia Ukraine. Marekani haina chochote zaidi ya hapo, kwani Rais wa Marekani alisisitiza siku moja baada ya mkutano huo kuwa uingiliaji wa kijeshi wa Marekani katika hali ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine haupo. Marekani ilitishia kabla ya mkutano huo kupitia maafisa wengi vikwazo ambavyo Urusi haijawahi kuona mfano wake, na ikazungumzia kuzuia mtiririko wa gesi ya Urusi katika bomba la Nord Stream kwenda Ujerumani, na kwamba inazungumza na Wajerumani kuhusu hili, na kwamba kiwango cha juu walicho nacho ni kuiondoa Urusi na benki yake kuu kutoka mfumo wa uhamisho wa fedha wa nje (SWIFT) ingawa biashara nyingi za Urusi zimekuwa hazitumii dola.

9- Kwa kuangalia kwa umakini, tunaona kuwa Urusi inajisukuma katika mgogoro ambao unaweza kuigeukia. Marekani inaweza kumshinikiza Rais wa Ukraine kuichokoza Urusi hadi Urusi isipate nafasi au chaguo lingine isipokuwa kuivamia Ukraine, hivyo ikatumbukia kwenye matope ya Ukraine na kugombana na Ulaya. Ukraine si nchi mwanachama wa Nato kiasi kwamba Marekani iwe na wajibu wa kuingia kuilinda. Ikiwa Urusi itakosea na kuivamia Ukraine, itampatia Marekani sababu zote za kuzitiisha nchi za Ulaya na kuzirudisha chini ya mbawa za Marekani kwa kisingizio cha kusimama pamoja dhidi ya uchokozi wa Urusi, jambo ambalo linapingana na dhana ya ncha nyingi za kimataifa (multi-polarity) inayopigiwa debe na Urusi. Pia kuna upeo ambao Urusi hauoni; kama sehemu ya shinikizo la Marekani kwa Urusi ikiwa itaivamia Ukraine, Marekani itamiliki zana mpya ya kuvunja muungano unaochipuka kati ya Urusi na Uchina. Inaweza kuishinikiza Uchina na kuitishia biashara yake na Marekani ili ijitenge na Urusi iliyoivamia Ukraine: ikiwa Uchina itatii na kujitenga na Urusi, basi Marekani itakuwa imepata lengo kubwa. Na ikiwa Urusi itatii aina mbalimbali za vikwazo na kujiondoa Ukraine baada ya kuivamia, basi madai ya Marekani yataifuata mashariki mwa Ukraine, na hata katika rasi ya Crimea, jambo ambalo litainyima Urusi faida yoyote kutokana na uvamizi wake wa Ukraine, bali litailetea majanga. Hii ni mbali na Marekani kuzichochea nchi za Ulaya Mashariki na kuzifanya zitoe msaada wa kijeshi wenye ufanisi na ushawishi kuipiga Urusi nchini Ukraine. Labda uzoefu wa kuidhoofisha Urusi huko Afghanistan hauko mbali na kumbukumbu. Kwa sababu hiyo yote, Urusi inacheza mchezo hatari karibu na Ukraine ambao unaweza kuwa mtego mkubwa kwake na kuigeukia, yaani kama mpumbavu asiyetambua matokeo ya matendo yake!

10- Kuhusu mwelekeo wa mambo, suala ni kama ifuatavyo:

a- Nchi za Ulaya zinajitahidi kutuliza hali na kuizuia Urusi kuivamia Ukraine. Zinataka kulainisha uhusiano na Urusi ili kupunguza hatari zake na kuhakikisha kuendelea kwa mtiririko wa rasilimali za nishati ya Urusi kuelekea Ulaya kwa bei nzuri. Ufaransa, Ujerumani na Italia zinatoa wito wa Urusi kuhusika katika mazungumzo na Ukraine kutatua mgogoro huo. Kuhusu hili (Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Heiko Maas alisema kuwa nchi yake inatamani kuboresha uhusiano na Urusi. Waziri alisisitiza kuwa kufanikisha hilo kunahitaji kupiga hatua katika kutatua mzozo wa Donbas. RT, 23/11/2021). Lakini Uingereza inaweza kujitahidi kupandisha joto la hali hiyo kwa ajili ya ushindani wa kisiasa na Umoja wa Ulaya ambao ilijitoa! (Mkuu wa Jeshi la Uingereza Jenerali Nicholas Carter alisema kuwa kuna hatari kubwa zaidi kuliko wakati wowote tangu Vita Baridi, zinazotishia kuzuka kwa vita kati ya Magharibi na Urusi. Al-Jazeera Net, 13/11/2021). Alisema pia ("Lazima tuwe waangalifu" kuhusu uwezekano wa kuzuka kwa mzozo katika eneo hilo. Jenerali Nick Carter aliongeza kwa BBC kuwa anatumaini kweli kusiwe na vita na Urusi, lakini aliongeza kuwa Nato lazima iwe tayari kwa uwezekano huu. BBC, 5/12/2021). Matamshi kama haya kutoka kwa Uingereza ni kwa ajili ya kuvuruga zaidi kuliko kuwa ni ishara ya vita halisi.

b- Lakini jambo la uamuzi zaidi ni msimamo wa Marekani; inadhibiti kamba nyingi za serikali ya Ukraine. Kwa sababu hiyo, Urusi ilituma barua ya kudai dhamana za usalama kwa Marekani na si nchi nyingine yoyote, kwa kuzingatia kuwa nchi za muungano huo zinafuata nyayo zake. Hata kuchelewa kwa Marekani kujibu kuhusu dhamana za usalama, hasa suala la kujiunga kwa Ukraine kwenye muungano, kuchelewa huku kunaishughulisha: (Na huko Moscow, Sergey Ryabkov Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi alisema kuwa Moscow inahitaji jibu la haraka la Marekani kwa mapendekezo yake kwa sababu hali ni ngumu na inaweza kuwa tata na yenye mivutano zaidi... Al-Jazeera 20/12/2021). Hivyo basi:

  • Ikiwa Marekani itaamua kuipatia Urusi dhamana za usalama nchini Ukraine bila ya makubaliano nayo kuhusu Uchina, basi upande wa Urusi utakuwa na nguvu zaidi katika mgogoro huu, na kwamba kutoa dhamana hizi kutafichua udhaifu zaidi wa msimamo wa Marekani kwa sababu Marekani itakuwa imetii madai ya Urusi na kusikiliza madai ya Ulaya ya kutuliza hali. Hili ni jambo lisiloelekea kutokea isipokuwa itokee hatua ya Urusi kulegeza uhusiano wake na Uchina kwa maslahi ya Marekani.

  • Lakini ikiwa Marekani itaamua kuitumbukiza Urusi na kuisukuma kwenye vita nchini Ukraine, basi Urusi itakuwa imetumbukia au imetumbukizwa katika kamba za mpango wake yenyewe.

  • Kwa kuzingatia mambo haya, lenye uwezekano mkubwa ni kwamba vita vya moto kati ya Urusi na Ukraine havitarajiwi kutokea isipokuwa yakitokea maendeleo mapya ambayo Urusi itahadaika nayo kisha ianze vita na kutumbukia humo! Kutokutarajiwa kwa vita hakuzuii kutokea kwa msuguano mashariki mwa Ukraine mara kwa mara...

Vilevile haitarajiwi kuwa Marekani itapata hatua ya kuvunja kabisa uhusiano wa Urusi na Uchina... Na kwa upande mwingine, Urusi haitafanikiwa kufikia malengo yake matatu... Bali inawezekana, kwa njia ya wabeberu katika suluhu ya kati na kati, kukatokea kulainisha msimamo kutoka kwa Marekani kuelekea malengo matatu ya Urusi mkabala na kupunguza uhusiano wa Urusi na Uchina... Kisha Urusi itaondoa mikusanyiko ya majeshi yake mipakani mwa Ukraine, na kutosheka na kurudi bila ya kupata ngawira yoyote!

18 Jumada al-Ula 1443 H 22/12/2021 M

Share Article

Share this article with your network