Swali:
Mnamo tarehe 20/02/2014, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, alitaka kutumwa kwa haraka vikosi vya ziada vya kijeshi nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati ili kuzuia kuzorota kwa hali ya usalama. Ikumbukwe kwamba Ufaransa tayari ilituma wanajeshi 2000 kando ya vikosi vya Afrika vilivyozidi wanajeshi 5000, baada ya Baraza la Usalama kutoa azimio mnamo 05/12/2013 la kuingilia kati kijeshi nchini humo. Makundi ya wanamgambo wa Kikristo yamefanya vitendo vya kinyama na vya kutisha dhidi ya Waislamu, ikiwemo mauaji, kuchomwa moto, kula nyama za watu, kuharibu nyumba zao, kupora mali zao, na kuwafukuza makwao. Michel Djotodia, rais wa kwanza mwenye asili ya Kiislamu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, alijiuzulu mnamo 10/01/2014, na kuchaguliwa kwa Catherine Samba-Panza kama rais wa Jamhuri hiyo kulitangazwa mnamo 20/01/2014. Marekani imetangaza kuunga mkono kikosi cha Afrika na kutoa wito wa kufanyika kwa uchaguzi kabla ya Februari 2015. Je, ni upi ukweli wa mgogoro huko? Hali hiyo ililipukaje? Ni nini sababu za mgogoro huo? Na unaelekea wapi?
Jibu:
Ili kujibu swali hilo, ni lazima kwanza tuangalie hali ya Waislamu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, na kuelezea historia ya mapinduzi nchini humo na uhusiano wake na ushindani wa kimataifa pamoja na yale yaliyotokana na ushindani huo:
1- Idadi ya Waislamu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati inakadiriwa kuwa kati ya 15% hadi 20% ya jumla ya wakazi wapatao milioni 5. Lakini asilimia hii inatiliwa shaka kutokana na kiwango cha kuenea kwa Waislamu nchini humo. Takwimu hizi si za upande wowote wala si za uaminifu, kwani mara nyingi kuna mwelekeo wa kupunguza asilimia ya Waislamu kwa sababu mbalimbali... Hivyo basi, uwezekano mkubwa ni kwamba asilimia ya Waislamu inazidi makadirio haya... Asilimia iliyobaki imegawanywa kati ya Wakristo na wapagani... Waislamu wameenea katika mji mkuu wa Bangui, ambapo wamejenga idadi kubwa ya misikiti na shule za kufundishia Qur'ani. Pia wameenea katika miji na mikoa mingine mingi mikuu, hasa kaskazini mwa nchi ambapo utawala wa Kiislamu (Sultanate) ulianzishwa mwishoni mwa karne ya kumi na saba wakati masultani kadhaa wa utawala wa Kiislamu wa Baguirmi kusini mwa Chad walipohamia huko baada ya kuanguka kwa utawala wao na kuhama kutoka kusini mwa Chad kwenda kaskazini mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Watu wengi wapagani walisilimu mikononi mwao, kama vile wengi walivyosilimu mikononi mwao kusini mwa Chad. Ikumbukwe kwamba Uislamu uliingia katika eneo la kaskazini mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati katika karne ya kumi na tatu, na baadhi ya makabila yalisilimu kama vile kabila la Runga linalopatikana katika eneo la Ndélé, mji mkuu wa kaskazini, na kabila la Vakaga linalopatikana katika mji wa Birao, mji mkuu wa kaskazini-mashariki, ambalo ni miongoni mwa maeneo tajiri zaidi kwa dhahabu, almasi, na urani. Kuna makundi ya Waislamu waliohamia maeneo haya katika karne ya kumi na nane na kumi na tisa kwa sababu mbalimbali na walishirikiana na ndugu zao katika harakati za kuufukuza ukoloni wa Kifaransa nchini humo. Vilevile, walihamia huko Waislamu kutoka Afrika Magharibi wa makabila ya Hausa na Fulani (Fulata) na wanaunda asilimia kubwa katika maeneo ya kusini-magharibi yanayopakana na Kamerun. Serikali kwa msaada wa Ufaransa, na hasa utawala wa Patassé, ilifanya kazi ya kuwatenga Waislamu kutoka kwa wapagani kwa hofu ya kuenea kwa Uislamu miongoni mwao; bali ilifanya operesheni ya kuwaondoa Waislamu serikalini na katika kazi za umma. Hivyo, Waislamu walielekea kwenye biashara, na matokeo yake, baada ya mauaji dhidi ya wafanyabiashara wa Kiislamu, biashara ilisimama na kukatokea uhaba mkubwa wa chakula kwa wakazi wa mji mkuu wa Bangui.
2- Ukoloni wa Ufaransa ulianza kuingia Jamhuri ya Afrika ya Kati mnamo mwaka 1885, na Ufaransa ikaanzisha kambi yake mjini Bangui. Eneo hilo likawa koloni rasmi la Ufaransa mnamo 1894. Ufaransa ilipoipa nchi hiyo uhuru wa kishindo mnamo 1960, iliwakabidhi Wakristo mamlaka ya nchi, huku ushawishi wake na ukoloni wake ukibaki kama ulivyokuwa zamani. Ilikuwa ikiwaweka watawala wa Kikristo ama kwa mapinduzi au kwa kile kinachoitwa uchaguzi... Ufaransa ilimweka David Dacko kama rais wa kwanza wakati wa kuitoa uhuru huo wa bandia. Lakini baada ya miaka miwili tu ya utawala wake, udikteta ulianza kudhihirika na akaanza kampeni za ukandamizaji dhidi ya wapinzani wake. Marekani, ambayo ilikuwa ikijipenyeza kuelekea Afrika, ilitumia fursa hiyo, wakati huo Umoja wa Kisovieti ulikuwa ukifanya kazi ya kupambana na ukoloni mkongwe baada ya kukubaliana na Marekani mnamo 1961. Mataifa haya mawili yaliyotangaza sera ya maridhiano yalikuwa na ushawishi katika kuchochea mataifa ya Afrika dhidi ya wakoloni wakongwe. Ufaransa ikahofia ushawishi wake nchini humo, ikamchochea Mkuu wa Majeshi Jean-Bédel Bokassa mnamo 1966 kufanya mapinduzi na kushika hatamu za uongozi kwa mkono wa chuma, na baadaye akamteua rais wa zamani David Dacko kama mshauri wake. Hii inaonyesha kuwa mapinduzi hayo hayakuwa chochote isipokuwa mpango wa Ufaransa wa kukabiliana na shambulio la Marekani na Kisovieti, kwa kumteua mwanajeshi dikteta ili kuwakandamiza wote wanaopinga ushawishi wa Kifaransa. Bokassa aliendelea na udikteta wake na kuimarisha utawala wake ili kulinda ushawishi wa Kifaransa nchini humo hadi alipojitangaza kuwa mfalme (Emperor) mnamo 1976! Alikuwa akiwaheshimu sana Wafaransa kiasi kwamba alimwita De Gaulle, Rais wa Ufaransa wa wakati huo, kwa jina la "Baba" na kuifanya nchi yake kuwa uwanja wa Wafaransa. Tetesi nyingi zilienea kumhusu Bokassa, ikiwemo kula nyama za watu na kuua watoto, na hisia za umma ulimwenguni zilichochewa dhidi yake. Ufaransa ikaingilia kati kwa vikosi vyake vilivyokuwepo huko ili kumwondoa madarakani na kumteua David Dacko kwa mara ya pili kama rais wa nchi mnamo 1979. Kisha jeshi likiongozwa na Jenerali André Kolingba mnamo mwezi wa Septemba 1981 likafanya mapinduzi na kumwondoa Dacko madarakani. Baada ya Ufaransa kufanikiwa kumwangusha Habré aliyekuwa mtiifu kwa Marekani nchini Chad na kumleta kibaraka wake Idriss Déby mnamo 1990, nguvu ya Ufaransa iliongezeka katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa sababu Chad inachukuliwa kuwa nguzo ya kuunga mkono ushawishi wa Kifaransa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati... Hivyo Ufaransa ikaona ushawishi wake umeimarika, ikataka kuupaka rangi utawala wa nchi hii kwa rangi ya kidemokrasia! Ikaamua kuliondoa jeshi madarakani na kufanya uchaguzi upya. Uchaguzi wa rais ulifanyika mnamo 1993 na Ange-Félix Patassé aliyehusishwa na Ufaransa, ambaye alikuwa akiongoza upinzani, akatangazwa mshindi. Kilichoifanya Ufaransa kufanya hivyo ni kujaribu kudhibiti athari za wito wa demokrasia ambao Marekani ilikuwa ikiutilia mkazo barani Afrika ili kuangusha ukoloni mkongwe na kuchukua nafasi yake. Hivyo, Ufaransa iliunda utawala kupitia uchaguzi na upinzani ukiongozwa na mchungaji François Bozizé, uliokuwa na makundi mbalimbali ya kikabila ikiwemo Waislamu. Upinzani huo ulichukizwa na ufisadi wa Patassé na ukandamizaji wake kwa wapinzani, hususan Waislamu, na upinzani ukageuka kuwa uasi wa kijeshi... Ufaransa ikaona imbadilishe Patassé na ikamleta kiongozi wa upinzani, mchungaji Bozizé, kama rais wa Jamhuri mnamo 15/03/2003, na Waislamu walimsaidia kufika madarakani... Lakini Bozizé akawageuka wale waliomsaidia miongoni mwa Waislamu na upinzani uliokuwa naye, na hakuwajali, bali aliwaona kama maadui! Alikabidhi ulinzi wake kwa kampuni ya usalama ya Kifaransa iliyoongozwa na Jenerali wa Kifaransa mstaafu Jean-Pierre Perez, kisha akafanya uchaguzi mnamo 2005 na 2011, na akatangaza ushindi wake katika kila mmoja wao... Katika kipindi hiki, uasi mpya ulitokea dhidi yake, na likajitokeza vuguvugu la Séléka (linalomaanisha muungano au makubaliano kati ya mashirika matano, ambayo viongozi wake ni Waislamu, na kubwa zaidi lilikuwa chini ya uongozi wa Djotodia...). Licha ya chaguzi zote za maigizo za Bozizé, hali haikutulia nchini na dhuluma ya Bozizé iliongezeka, hasa dhidi ya Waislamu ambapo utawala wake ulituma vikosi vyake kushambulia mali za Waislamu, na mamia ya wahanga walianguka wakijitetea wenyewe na mali zao...
3- Kufuatia hayo, mnamo 11/01/2013 mkutano ulifanyika mjini Libreville, mji mkuu wa Gabon, ulioshirikisha Rais Bozizé na vuguvugu la Séléka ili kufikia suluhu... Mkutano huo ulidhihirisha kiwango cha dhuluma wanachofanyiwa Waislamu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati ambapo hata haki zao za kimsingi zilikuwa zimeporwa... Kwa sababu hiyo walizidai, nazo zilikuwa madai rahisi: kutambuliwa kwa Uislamu kama dini nyinginezo, kuadhimishwa rasmi kwa sikukuu za Eid al-Fitr na Eid al-Adha, na kutokandamizwa kwa Waislamu... Lakini Bozizé alikuwa bingwa wa kupoteza muda, hivyo baada ya kukubaliana na baadhi ya madai ya Waislamu na Séléka, na kukubaliwa kuwa kibaraka huyu wa Kifaransa aendelee kutawala hadi 2016 - na licha ya kwamba makubaliano hayo yalivihakikishia utawala wa Bozizé kuendelea licha ya mauaji yake... na kwamba Marekani ilikuwa imeunga mkono makubaliano hayo kama ilivyoripotiwa na Shirika la Habari la Ufaransa (AFP)... licha ya hayo yote, Ufaransa na Bozizé walichelewa kutekeleza haki hizi rahisi, bali walizigeuka na kuanza tena vitendo vyao vya kinyama dhidi ya Waislamu. Hivyo Séléka ilielekea kwenye ikulu na kuiteka mnamo 24/03/2013 chini ya uongozi wa Michel Am-Nondokro Djotodia ambaye akawa rais... Hapa Ufaransa ilipiga kelele na kulalamika kwa sababu Djotodia ana asili ya Kiislamu, na ingawa alijaribu kuwaridhisha watu wa Magharibi tangu aliposhika madaraka, kama ilivyokuja katika matamko yake alipojitangaza kuwa rais wa muda: "Jamhuri ya Afrika ya Kati ni dola ya kisekula ambapo Wakristo na Waislamu wanaishi katika dola ya kisekula. Ni kweli mimi ni Mwislamu, lakini ni wajibu wangu kuitumikia nchi yangu na raia wote wa Jamhuri ya Afrika ya Kati." (31/03/2013 Al-Khaleej). Haya yote yalikuwa ni kuridhisha Magharibi na hasa Ufaransa pamoja na Wakristo, kiasi kwamba hakunyang'anya silaha wanamgambo wa Kikristo na akawaacha waendelee kufanya kazi. Hata hivyo, Ufaransa haikumtambua rais huyo mpya, na kadhalika vibaraka wake... Ufaransa ikaanza kufanya kazi dhidi yake kwa nguvu kwa sababu ana asili ya Kiislamu, na vibaraka wake wakaifuata katika hilo. Kisha Ufaransa ikawachochea viongozi wa Afrika ya Kati kufanya mkutano mjini N'Djamena, mji mkuu wa Chad tarehe 03/04/2013, na Idriss Déby, kibaraka maarufu wa Ufaransa, akawahutubia akisema: "Inaonekana haiwezekani kwetu kumtambua mtu aliyejiweka mwenyewe." (05/04/2013 Al-Wasat). Na ingawa baraza la mpito mnamo 13/04/2013 lilitangaza kumchagua Michel Djotodia kama rais wa nchi, yote hayo hayakumsaidia kwa sababu ya kuwa na asili ya Kiislamu. Ufaransa ikasitisha kutoa msaada kwa serikali hii, ingawa inapora maliasili za nchi hiyo kama urani, dhahabu, na almasi na kuzipangia serikali za Afrika ya Kati misaada na kuikata inapoona inafaa, ikichukulia maliasili hizo kama mali yake!
4- Ufaransa ilianza kuandaa mazingira ya kuingilia kati na kutengeneza matatizo ili kuhalalisha hatua hiyo. Ilifanikiwa kupata azimio kutoka kwa Baraza la Usalama mnamo 05/12/2013 likiipa mamlaka ya kuingilia kati kijeshi nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, na uingiliaji huo ukafanyika mnamo 08/12/2013. Rais wa Ufaransa François Hollande alitaka kujiuzulu kwa Michel Djotodia na kufanyika kwa uchaguzi wa mapema. Kwa ajili hiyo, Ufaransa iliandaa mkutano wa kilele wa kikanda wa Afrika katika mji mkuu wa Chad, N'Djamena, mnamo 10/01/2014 na ikatumia shinikizo kupitia mkutano huo kumlazimisha Djotodia kujiuzulu, naye akatangaza kujiuzulu kwake wakati wa mkutano huo. Kisha ikatangazwa kuchaguliwa kwa Samba-Panza, meya wa mji mkuu Bangui, kama rais wa muda wa nchi mnamo 20/01/2014. Hali hiyo ilifuatiwa na vitendo vya kinyama vilivyofanywa na wanamgambo wa Kikristo mbele ya macho na usimamizi wa vikosi vya Kifaransa, ambavyo vilikuwa vimenyang'anya silaha wapiganaji zaidi ya 7000 wa vuguvugu la Séléka kwa kisingizio cha kulinda usalama, lakini haikunyang'anya silaha wanamgambo wa Kikristo, hasa wale wanaoitwa "Anti-balaka", bali iliwaunga mkono! Kisha wanamgambo hawa baada ya kuangushwa kwa Rais Djotodia walifanya vitendo viovu zaidi kuliko wanyama, ikiwemo kuwaua na kuwachoma moto Waislamu, kula nyama zao, na kuharibu nyumba zao, misikiti, shule, na taasisi zao pamoja na kupora mali zao chini ya uangalizi wa vikosi vya Kifaransa na vya Afrika. Hata ripoti za Umoja wa Mataifa ziliituhumu Ufaransa kwa kuwaunga mkono wanamgambo wa Kikristo dhidi ya Waislamu wasio na ulinzi baada ya kuwapokonya silaha yoyote ambayo wangeweza kujilinda nayo... Kutokana na unyama wa uhalifu huu, rais mpya alikiri hilo akisema: "Anti-balaka wamepoteza maana ya ujumbe wao, leo wamekuwa wauaji." Na akasema: "Wanafikiri mimi ni dhaifu kwa sababu ni mwanamke, lakini kuanzia sasa wanamgambo wa Anti-balaka wanaotaka kuua watasakwa." (Radio BBC 12/02/2014). Redio hiyo iliongeza kusema: "Makumi ya maelfu ya Waislamu wamekimbia kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati kwenda Kamerun na Chad, huku sehemu yao wakikimbilia kwenye kambi ndani ya nchi. Shirika la Amnesty International lilisema kuwa mashambulizi ya wanamgambo yamesababisha msafara mkubwa wa Waislamu kwa viwango vya kihistoria. Ilielezea hali ya Afrika ya Kati kama utakaso wa kikabila." Hata hivyo, rais wa nchi alikataa maelezo hayo, na badala yake akadai kuwa "kinachoendelea nchini ni tatizo la kiusalama"!
5- Marekani ilijaribu kufaidika na mauaji ya Wafaransa na vibaraka wao nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati. Ilifanya kazi ya kuimarisha vikosi vya Afrika nchini humo ili viwe sawa na vikosi vya Kifaransa, na kwa njia hiyo kuondoa ukiritimba wa Ufaransa kama utangulizi wa kuiondoa na Marekani kuchukua nafasi yake au kushirikiana nayo... Watu walianza kuvituhumu vikosi vya Kifaransa kwa kushirikiana na wanamgambo wa Kikristo wa kiharifu, na madai ya kutaka vikosi vya Afrika badala ya Kifaransa yakaongezeka. Wito huo uliungwa mkono na vyanzo vya Marekani na pia vyanzo vya Umoja wa Mataifa ambavyo Marekani ina ushawishi mkubwa ndani yake... Mwenyekiti wa kamati inayohusika na masuala ya Afrika katika kamati ya mambo ya nje ya Bunge la Marekani (Congress), Christopher Coons, alisema: "Kamati imefanya kikao cha kusikilizwa ili kubaini kile Marekani inachoweza kufanya kusaidia juhudi za pande nyingi kuhakikisha kuwa vikosi vya Umoja wa Afrika vina uwezo unaohitajika kuimarisha usalama na kukomesha ghasia." (IIP Digital, tovuti ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, 23/12/2013). Mwakilishi wa kudumu wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Samantha Power, na msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kwa masuala ya Afrika, Linda Thomas-Greenfield, walitembelea Bangui mnamo 19/12/2013 kukutana na maafisa wa mpito huko. Greenfield alisema: "Tunaamini kuwa mamlaka yenye nguvu kwa ujumbe wa Umoja wa Afrika ili kuimarisha utulivu ndiyo yanayohitajika sasa kukabiliana na makundi na makundi ya silaha na kuyanyang'anya silaha." (Chanzo hicho hicho). Kwa upande mwingine, Ufaransa ilifanya kazi ya kuimarisha vikosi vya kimataifa kwa vikosi kutoka nchi za Ulaya ili kukabiliana na vikosi vya Afrika vilivyofikia idadi ya 4400 na vitaongezewa vikosi kutoka Rwanda vyenye wanajeshi 850. Kwa sababu hii, "Urais wa Ufaransa mnamo 14/02/2014 uliamua kutuma wanajeshi 400 wa ziada Jamhuri ya Afrika ya Kati ili kuimarisha kikosi chake kilichopo huko ili kufikia idadi ya wanajeshi 2000. Taarifa ya urais wa Ufaransa ilisema: Jitihada hii ya ziada ya wanajeshi 400 inajumuisha kutumwa mapema kwa vikosi vya mapigano vya Kifaransa ambavyo baadaye vitashiriki katika operesheni ya kijeshi ya Umoja wa Ulaya mara tu itakapotumwa. Iliongeza katika taarifa yake: Kwamba Ufaransa inautaka Umoja wa Ulaya kuharakisha kutumwa kwa kikosi cha EUFOR, ikiwemo kikosi cha askari wa kulinda usalama wa Ulaya (Gendarmerie). Vyanzo vya kidiplomasia vilieleza kuwa ushiriki wa Umoja wa Ulaya unaweza kuwa wanajeshi 900, yaani zaidi ya wanajeshi 500 waliokuwa wakitarajiwa." (AFP 14/02/2014). Marekani iliamua kufadhili vikosi vya Afrika; Marie Harf, Naibu Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, alisema: "Tunasikitishwa sana na kuongezeka kwa vitendo vya ghasia nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati ambavyo vimesababisha mgogoro unaokua wa kibinadamu na kuongezeka kwa hatari ya kufanywa kwa vitendo vya kinyama vya halaiki.
Na jana tulipiga kura kuunga mkono azimio kali la pamoja katika Baraza la Usalama linalotoa kwa vikosi vya Umoja wa Afrika na vikosi vya Kifaransa vinavyounga mkono vikosi vya Umoja wa Afrika mamlaka chini ya Sura ya Saba ili kurejesha usalama na kuleta amani kwa watu walioteseka kwa muda mrefu sana. Tunakusudia kutoa dola milioni 40 kwa namna ya vifaa na mafunzo au msaada wa kilojistiki kwa vikosi vya Umoja wa Afrika na washirika wetu wa Kifaransa kwa muda mrefu kadiri hitaji litakapokuwepo." (IIP Digital 06/12/2013). Ni wazi kutokana na vitendo vya vikosi hivi, iwe ni kutoka nchi za Afrika ambazo Marekani ina ushawishi nazo, au vikosi vya Kifaransa vilivyoungwa mkono na vikosi vya Ulaya vinavyoifuata, ni wazi kutokana na vitendo vya vikosi hivi vinavyofikia takriban 8000 kwamba havipo kwa ajili ya kulinda usalama nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati. Havijafanya lolote kuzuia vitendo vya kinyama na mauaji ya kutisha dhidi ya Waislamu, ingawa kama vingekuwa na nia ya dhati vingeweza kwani nchi hiyo ina idadi ndogo ya watu... Bali huku ni kwa ajili ya ushindani kuhusu ushawishi wa Kifaransa na ushawishi wa Marekani unaofanya kila jitihada kuingiza ushawishi wake... Hivyo, damu za Waislamu zinazomwagika na nyama zao zinazolika... zimekuwa uwanja wa mashindano ambapo Ufaransa na Marekani wanacheza densi juu yake huku miguu yao ikizama katika damu za Waislamu.
6- Kwa mujibu wa hayo, Marekani inafanya kazi ya kuimarisha ushawishi wake nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati kupitia kuimarisha vikosi vya Afrika na kuimarisha majukumu ya vikosi hivyo. Kwa sababu hii, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, anayefuata sera za Marekani, alilitaka Baraza la Usalama: "Kutuma kwa haraka wanajeshi 3000 wa ziada ili kuweka usalama na kulinda raia..." (AFP 20/02/2014). Inajulikana kuwa watatoka katika vikosi vya Afrika... Inaonekana kuwa Marekani inataka hatimaye mchakato wa kisiasa kisha uchaguzi ambapo itatumia damu za Waislamu kugawana ushawishi na Ufaransa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati! Inatarajiwa pia kwamba Ufaransa itaenda sambamba na Marekani katika ufumbuzi wa kisiasa ili isipoteze kila kitu kwa sababu wakati huu ni mgumu zaidi kwake kuliko nyakati zote zilizopita, na hivyo itafanya kazi ya kufanikisha vibaraka wake kufika madarakani kupitia uchaguzi pia.
7- Kwa hitimisho, damu za Waislamu zimekuwa uwanja wa ushindani kati ya Marekani na Ufaransa kwa ajili ya ushawishi... Wala haiwajali wala kuwahusu ikiwa damu itatiririka kama mito kutoka kwa Waislamu, wala kuteswa kwa wazee, watoto, na wanawake, bali hata kuliwa wakiwa hai... Jambo muhimu kwa nchi hizi kafiri za kikoloni ni nani atasimama mwishoni akipiga makofi juu ya maiti na viungo hivyo... Makafiri wakoloni ni kundi moja, hawazingatii kwa Muumini udugu wala ahadi... Kwa hiyo, pande zote mbili zinazingatia kuua Waislamu hata kama mbinu na malengo yao yanatofautiana, lakini wanawaacha wanamgambo wa Kikristo wakizurura na kufurahia kumwaga damu za Waislamu...
Lakini jambo lenye kuumiza na kuhuzunisha ni kwamba Waislamu hawana wa kuwalilia, kwani damu zao zinamwagika kwa unyama nchini Palestina, Burma, Kashmir, Chechnya, Tatarstan, Syria, na sasa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati... n.k. Watawala katika nchi za Waislamu wanatumikia maslahi ya Magharibi, si maslahi ya Waislamu, hivyo wanatazama mauaji hayo kama yangekuwa katika nchi ya mbali sana au katika ulimwengu mwingine usio ulimwengu wao, wakati mauaji hayo hayako mbali na ardhi za udhibiti wa watawala hao hata kwa shubiri moja... Basi ole wao kwa yale wanayoyatenda.
Na mwisho wa hitimisho, Waislamu wanakosa ngao inayowazuia wavamizi, wanakosa Khalifa ambaye ni ngao na ulinzi.
إِنَّمَا الإِمَامُ جُنَّةٌ يُقَاتَلُ مِنْ وَرَائِهِ وَيُتَّقَى بِهِ
"Hakika Imamu ni ngao, ambapo watu hupigana nyuma yake na hujilinda kwake." (Imepokewa na Al-Bukhari kutoka kwa Abu Hurayrah r.a.)
وَيَقُولُونَ مَتَى هُوَ قُلْ عَسَى أَنْ يَكُونَ قَرِيبًا
"Na wanasema: 'Lini hayo?' Sema: 'Huenda yakawa karibu.'" (QS Al-Isra [17]: 51)