Jibu la Swali
Ukweli wa Mvutano kati ya Uturuki na Ugiriki, Hususan Migogoro kuhusu Visiwa vya Bahari ya Aegean
Swali:
Ilitajwa katika taarifa ya mwisho iliyotolewa na Umoja wa Ulaya katika mkutano wake mkuu mjini Brussels mnamo tarehe 23 na 24/06/2022 chini ya kichwa "Mashariki mwa Mediterania" kuhusu uhusiano wa Uturuki na Ugiriki, hasa mgogoro wa visiwa vya Bahari ya Aegean: ("Umoja wa Ulaya unaelezea wasiwasi wake mkubwa kutokana na matamshi na vitendo vya hivi karibuni vya Uturuki. Uturuki lazima ionyeshe heshima kwa mamlaka na uadilifu wa mipaka ya nchi zote wanachama wa Umoja wa Ulaya..." Voice of America 24/06/2022). Kwa upande mwingine, Uturuki ilisema katika taarifa iliyochapishwa na wizara yake ya mambo ya nje: ("Kuchukua msimamo wa upendeleo, usio na maono na uliotengwa na ukweli kuhusu nchi yetu katika maamuzi yaliyopitishwa wakati wa mkutano wa wakuu wa nchi na serikali wa Umoja wa Ulaya ni jambo la kusikitisha, na haikubaliki kwa Umoja wa Ulaya kujaribu kuhalalisha madai ya kithubutu na yanayokiuka sheria za kimataifa kuhusiana na Mashariki mwa Mediterania na Bahari ya Aegean..." Anadolu 24/06/2022). Je, hii inamaanisha kuwa mvutano umerudi tena katika uhusiano kati ya Uturuki na Ugiriki? Na je, inawezekana hili likapelekea vita kati yao huku wote wawili wakiwa katika muungano wa NATO? Kisha msimamo wa Amerika ni upi huku ikiongoza muungano huu? Je, inaweza kuondoa mvutano huu na kutuliza mambo, au mvutano huu utaendelea kuongezeka?
Jibu:
Ili jibu liwe wazi, tunapitia mambo yafuatayo:
Katika Bahari ya Aegean kuna takriban visiwa vidogo na vikubwa 1800 na miamba, ambapo takriban 100 kati yake vinakaliwa na watu na visiwa 24 tu vina eneo la zaidi ya kilomita mraba 100. Visiwa hivi vilianza kuingia chini ya mamlaka ya Uislamu na utawala wa Waislamu pamoja na nchi ya Ugiriki tangu Muhammad al-Fatih (rehema za Allah ziwe juu yake) alipoanza mashambulizi ya ukombozi huko kuanzia mwaka 1456 BK baada ya kufanya ukombozi mkuu wa Istanbul, mji mkuu wa Roma ya Mashariki mnamo 1453 BK. Lakini udhaifu ulipoanza kudhihirika katika Dola ya Ottoman kama dola ya Kiislamu, mataifa ya kikafiri yalitumia fursa hiyo na kuanza kuifanyia vitimbi Dola ya Kiislamu, yakawachochea Wagiriki kuasi dhidi yake. Hata Uingereza, Ufaransa na Urusi ziliingilia kati moja kwa moja katika vita vya majini dhidi yake ili kuitenganisha Ugiriki na Dola ya Ottoman hadi hilo lilipofanyika mnamo 1830 BK. Hata hivyo, mamlaka ya visiwa vingi yalibaki kwa Dola ya Ottoman, hadi Italia ilipokalia visiwa vya Menteshe mnamo 1912 BK wakati wa vita huko Libya, ambavyo huitwa Visiwa Kumi na Mbili (Dodecanese), ambavyo kiasili ni visiwa 14, pamoja na visiwa kumi vidogo na mikusanyiko ya miamba. Visiwa hivi vilipata umuhimu kwa kuwa karibu na mipaka ya Uturuki baada ya mgawanyo katika Mkataba wa Lausanne; vingine viko umbali wa takriban kilomita 3 kutoka Uturuki, huku vikiwa umbali wa takriban kilomita 500 kutoka pwani ya karibu ya Ugiriki. Visiwa hivi vilipewa Italia katika Mkataba wa Lausanne, uliotiwa saini na serikali ya Ankara chini ya uongozi wa Mustafa Kemal kupitia mjumbe wake Ismet Inonu, ambapo walisalimisha maeneo mapana ya Dola ya Ottoman na kutosheka na kile kinachoitwa Uturuki ya sasa iliyoainishwa na Washirika wakiongozwa na Uingereza. Italia ilipata utambuzi wa Uingereza kwa haki yake juu ya visiwa hivyo mkabala na kuingia katika Vita vya Kwanza vya Dunia upande wa Uingereza dhidi ya Ujerumani na Dola ya Ottoman. Mnamo 1947 BK, mkataba wa amani ulitiwa saini mjini Paris kati ya mataifa ya Washirika na Italia baada ya kushindwa kwa mwisho katika Vita vya Pili vya Dunia, na makubaliano hayo yalieleza kukabidhiwa kwa Italia visiwa vya Menteshe, Visiwa Kumi na Mbili kwa Ugiriki kwa sharti kwamba visiwa hivyo visiwe na silaha (demilitarized). Uturuki inadai kufanya mazungumzo ili kuamua hatima ya visiwa vingi vinavyozozaniwa, na visiwa vidogo ambavyo havikuhamishiwa kwa nchi yoyote chini ya mikataba iliyopita, huku Ugiriki ikidai haki yake katika visiwa vyote vya Bahari ya Aegean isipokuwa visiwa vichache vilivyorejeshwa kwa Uturuki chini ya Mkataba wa Lausanne pekee. Ugiriki inadai kuongeza maji yake ya kikanda kutoka maili 6 hadi maili 12. Uturuki bado iko chini ya Mkataba wa Paris na inaukubali ingawa haikuwa upande katika mkataba huo wala haikuutia saini! Waziri wake wa mambo ya nje, Cavusoglu, alisema katika mahojiano na gazeti la Hurriyet mnamo 26/05/2022: "Ugiriki lazima izingatie mkataba wa amani uliotiwa saini mwaka 1947 ambao hauruhusu chochote isipokuwa kitengo kidogo cha kijeshi cha askari wa Ugiriki kuwepo katika visiwa vya Dodecanese," na "Waziri alionya kuongezeka kwa hali hiyo iwapo Ugiriki haitazingatia masharti ya mkataba wa amani." Upande mwingine wa mgogoro unahusu haki zinazotokana na mamlaka hayo, ambazo ni maeneo ya ushawishi wa baharini, maeneo ya kiuchumi, na haki ya kutafuta vyanzo vya nishati kama mafuta na gesi karibu na visiwa hivi. Aidha, kuna suala la kuanzishwa kwa kambi za Marekani juu yake, pamoja na tamaa za Ulaya, hasa Ufaransa, katika eneo hili.
Ufaransa imeingia katika mstari huo na kuonyesha uungaji mkono wake kwa Ugiriki dhidi ya Uturuki kwa njia ya wazi. Ilitangaza upendeleo wake upande wa Ugiriki dhidi ya Uturuki katika mgogoro wa msimu wa joto wa 2020, na ikatuma ndege za Rafale na meli za kivita kukabiliana na kuenea kwa meli za kijeshi na shughuli za utafutaji za Uturuki katika Mashariki mwa Mediterania. Ilitia saini na Ugiriki mkataba wa ushirikiano wa pande mbili mnamo Septemba 2021 uliosema "msaada wa pande mbili kwa njia zote zinazofaa ikiwa nchi zote mbili zitabaini kwa pamoja kuwa kuna shambulio la silaha linalofanyika dhidi ya eneo la mmoja wao." Kisha Ufaransa ilichukua hatua kuimarisha makubaliano hayo kwa kutia saini mkataba wa ushirikiano wa kijeshi wa pamoja kati ya nchi hizo mbili mnamo Januari 2022 unaoeleza kuwa "ushirikiano wa kimkakati unaunganisha nchi hizo mbili katika ngazi ya kijeshi" kulingana na taarifa ya mkuu wa majeshi ya Ufaransa. Mkataba huu pia unaruhusu "kuimarisha uhusiano wa ulinzi wa kijeshi na kuupanga kwa muda mrefu, na kudhihirisha ushirikiano wa kijeshi wa pande mbili kati ya Ufaransa na Ugiriki katika ngazi za kimkakati na operesheni. Na kwamba ushirikiano wa kijeshi wa pande mbili utapanuliwa" (AFP 22/01/2022). Siku mbili kabla ya kutia saini mkataba huu, Ugiriki ilitangaza kupokea ndege za kivita 6 za aina ya Rafale kutoka Ufaransa kati ya ndege 18 ambazo Ugiriki ilitangaza kuzinunua kutoka Ufaransa mwaka jana pamoja na manowari 3 kwa gharama ya euro bilioni 5.5. Shirika la habari la AFP liliwanukuu wataalamu wakisema: "Mkataba huu wa ulinzi haujawahi kushuhudiwa na ni wa ajabu, kwa sababu unaunganisha nchi mbili wanachama wa NATO na unailenga Uturuki, mwanachama mwingine wa muungano huo." Ufaransa iliathiri Umoja wa Ulaya kwa msimamo wake huu, hivyo msimamo wake ulikuwa wa kuiunga mkono Ugiriki dhidi ya Uturuki.
Marekani haikunyamaza kimya mbele ya hatua hii ya Ufaransa, ilichukua hatua ili kubatilisha athari yake na kuipiga kibao kwanza Ugiriki. Ilitokea kwamba Ugiriki, Kupro na chombo cha Kiyahudi zilitangaza mnamo 20/12/2018 utayari wao wa kuanzisha mradi wa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Mashariki mwa Mediterania hadi Ulaya bila Uturuki na sehemu ya kaskazini ya Kituruki ya Kupro kuwa na mchango ndani yake. Bomba hilo lilitegemewa kutoa takriban mita za mchemraba bilioni 10 za gesi asilia kwa Ulaya. Lakini Marekani ilitangaza kusitisha uungaji mkono wake kwa mradi huo. Iliarifu chombo cha Kiyahudi na Ugiriki mnamo 10/01/2022 kuwa "haitaunga mkono mradi huo kisiasa na kifedha," na jambo hilo lilichukuliwa kama "ushindi kwa Uturuki ambayo ilikuwa imetengwa na mradi huo" (Asharq Al-Awsat 10/01/2022). Gazeti la kijeshi la Ugiriki katika ripoti iliyochapishwa mnamo 10/01/2022 liliashiria hilo kwa kusema: ("Mradi wa Athens wa kuongeza ushawishi wa kijiopolitika ili kuwa kitovu cha nishati na ushirikiano wa kihistoria na (Israel) ambao ulipelekea kuitenga Uturuki na kufikia malengo mengine umeporomoka kabisa... Na jambo hilo linatumika kwa sheria ya Maniatis inayoweka mipaka ya nje ya ukanda wa bahari wa Ugiriki, malengo yote mawili yameporomoka, na Uturuki imeivunja sheria ya Maniatis ambayo inaiita 'Blue Homeland', na ikaimarisha ukuu wake juu ya misimamo ya Ugiriki kwa makubaliano ya Uturuki na Libya, na sasa msimamo wa Washington umekuja kuipa fursa"). Na ikataja "kwamba Waziri Mkuu (wa Ugiriki) Mitsotakis hataki kufanya mazungumzo na Uturuki... na pia hakufanya mazungumzo na Marekani..." Ikaongeza kuwa "Marekani ilifanya kazi kupitia Ujerumani kuzuia kuwekwa kwa vikwazo dhidi ya Uturuki kutokana na mgogoro wa utafutaji gesi katika Mashariki mwa Mediterania mwaka jana"). Tukichunguza suala hili tunaona kwamba Marekani ilitaka kuipiga kibao Ugiriki kwa ushirikiano wake na Ufaransa na kubatilisha athari ya hatua ya Ufaransa katika eneo hilo, na Marekani ilitaka kuunganisha mradi huo na Uturuki, mshirika wake wa karibu ambaye yuko katika mzunguko wake, ili kuikabili Ufaransa.
Ugiriki ilitambua kuwa (imeikasirisha) Marekani kwa makubaliano yake na Ufaransa na kukaribiana nayo, na ili kurekebisha jambo hili, ilikubali kutia saini mkataba na Marekani ambao bunge la Ugiriki lilikuwa likichelewesha kuutia saini tangu 14/10/2021 hadi 13/05/2022 ambapo ulitiwa saini... Wakati wa upigaji kura, Waziri Mkuu wa Ugiriki Mitsotakis alitetea mkataba huo akisema: ["Mkataba wa ushirikiano wa ulinzi na Marekani unatumikia maslahi ya kitaifa ya nchi. Ni kura ya imani kwa Ugiriki, na ni muhimu kwa sababu kwanza unajumuisha ahadi ya wazi kwamba uwepo wa Marekani nchini Ugiriki utafanywa upya kila baada ya miaka 5 (badala ya mwaka mmoja kama ilivyokuwa hapo awali), kila upande una haki ya kuuvunja ukiona ni lazima. Pili, ushirikiano huu wa pande mbili na Marekani ni muhimu kwa sababu unapanuka sio tu kwa wakati muafaka bali pia mahali. Katika kambi ya majini ya Souda (katika kisiwa cha Crete), miundombinu yote inaboreshwa na kuimarishwa jukumu la kambi hiyo. Souda ni gatuzi pekee ambapo meli ya kubebea ndege ya Marekani inaweza kutia nanga katika Mashariki mwa Bahari ya Mediterania, pamoja na uwanja wa mazoezi ya risasi huko Litochoro na kambi mbili za kijeshi huko Volos na Alexandroupolis. Tatu, mkataba mpya ni muhimu kwa sababu unaeleza wazi utashi wa pamoja wa ulinzi wa pande mbili kwa mamlaka na uadilifu wa mipaka dhidi ya tishio lolote hata shambulio la silaha"... Youm7 kutoka mashirika ya habari 13/05/2022].
Hivyo ndivyo Marekani ilivyoifanya Ugiriki kufuata matakwa yake, ikaimarisha ushawishi wake huko na kudhoofisha ushirikiano wake na Ufaransa!
- Baada ya hapo, matamshi ya Ugiriki yalipungua kasi ambapo Waziri Mkuu wa Ugiriki alisema: ("Ni muhimu kuweka njia za mawasiliano wazi na Uturuki, licha ya matamshi makali yaliyopelekea kuongezeka kwa mvutano kati ya majirani wawili"... Al-Khaleej New 17/06/2022). Lakini hali hii imeufanya Umoja wa Ulaya kuwa katika hatari! Kwa hivyo, ili kulinda heshima yake, ulitosheka na tangazo lake la jumla lililopozwa kuelekea Uturuki huku ukionyesha uungaji mkono kwa Ugiriki kwa kuzingatia kuwa ni mwanachama wa Umoja huo: (Ilikuja katika taarifa ya mwisho iliyotolewa katika mkutano wake mkuu mjini Brussels mnamo tarehe 23 na 24/06/2022 chini ya kichwa "Mashariki mwa Mediterania": "Umoja wa Ulaya unaelezea wasiwasi wake mkubwa kutokana na matamshi na vitendo vya hivi karibuni vya Uturuki. Uturuki lazima ionyeshe heshima kwa mamlaka na uadilifu wa mipaka ya nchi zote wanachama wa Umoja wa Ulaya.")
Kufuatia hilo, Waziri Mkuu wa Ugiriki alisema: "Tunasimama kikamilifu nyuma ya kile kilichoelezwa katika taarifa ya mwisho ya Umoja wa Ulaya, na imemfanya Uturuki kuwajibika kuhusiana na mamlaka na uadilifu wa mipaka ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya na kumtaka apunguze mvutano kulingana na sheria za kimataifa. Natumai Uturuki itasikiliza wito huu safari hii. Kwa sababu hiyo ndiyo njia pekee ya kupunguza mvutano ambao uliongezwa kikamilifu na jirani yetu katika miezi miwili iliyopita katika Mashariki mwa Mediterania" (Voice of America 24/06/2022).
Hivyo ndivyo Marekani ilivyoweza kupunguza makali ya mvutano kati ya Uturuki na Ugiriki, kwani Uturuki iko katika mzunguko wake, na Ugiriki imekuwa imeshikwa na mkataba wa ulinzi na Marekani, na ushawishi wa Umoja wa Ulaya na hasa Ufaransa juu ya Ugiriki umepungua. Kwa hivyo, ni vigumu kuwa na suluhisho lolote la mgogoro wa visiwa katika Bahari ya Aegean vikiwemo visiwa vya Menteshe katika siku za usoni, na utabaki mahali pake kama ulivyo kwa miongo mingi. Hata utawala wa Uturuki umekubali kwa njia isiyo ya moja kwa moja kupewa kwa Visiwa Kumi na Mbili kwa Ugiriki katika Mkataba wa Paris mwaka 1947 BK, hivyo utawala huu hauna mpango wa kuvirejesha, na vivyo hivyo visiwa vingine ambavyo umiliki wake haukuamuliwa rasmi kwa Ugiriki katika mikataba. Haitarajiwi kwa utawala wa kisekula wa Uturuki kufanya kazi yoyote ya dhati ya kurejesha visiwa hivi katika Bahari ya Aegean vinavyodhibitiwa na Ugiriki. Erdogan hafanyi chochote isipokuwa vita vya maneno na kisha anarudi nyuma kama ilivyotokea mwaka 2020 alipoondoa meli za utafutaji gesi katika Mashariki mwa Mediterania, na kufunga mjadala wa suala hilo. Kwa hivyo, haitarajiwi kutokea vita kati ya Uturuki na Ugiriki ili kurejesha visiwa hivi, kwani nyuzi za suala hili ziko mkononi mwa Marekani, na Uturuki iko katika mzunguko wake, na Ugiriki baada ya mkataba huo ushawishi wa Marekani umeanza kuongezeka ndani yake...
Mwisho, visiwa vya Bahari ya Aegean, na hata Ugiriki yenyewe, vilikuwa sehemu ya Dola ya Kiislamu (Ottoman). Baada ya ukombozi wa Constantinople mwaka 1453 BK, kusadikisha hadithi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ:
لَتُفْتَحَنَّ الْقُسْطَنْطِينِيَّةُ فَلَنِعْمَ الْأَمِيرُ أَمِيرُهَا وَلَنِعْمَ الْجَيْشُ ذَلِكَ الْجَيْشُ
"Hakika itafunguliwa Qustantiniyyah (Constantinople), kiongozi wake ndiye kiongozi bora na jeshi lake ndilo jeshi bora." (Imepokelewa na Ahmad katika Musnad yake)
Miaka mitatu baada ya hapo, yaani mnamo 1456 BK, harakati za ukombozi zilielekea Ugiriki na kuelekea visiwa hivyo na adhana ikapaa humo (Allahu Akbar Allahu Akbar). Na hakika vitarudi kwa idhini ya Mwenyezi Mungu katika siku ambayo waumini watafurahia ushindi wa Mwenyezi Mungu, siku ambayo Khalifa wao atawaongoza waumini, akiwahukumu kwa yale aliyoteremsha Mwenyezi Mungu na kupigana nao jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, ili kurejesha Dar al-Islam, asili yake na matawi yake. Kwani Khalifa ndiye ngao ya Umma na ulinzi wake dhidi ya maadui zake, na Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ amesema kweli:
إِنَّمَا الْإِمَامُ جُنَّةٌ يُقَاتَلُ مِنْ وَرَائِهِ وَيُتَّقَى بِهِ
"Hakika Imamu (Khalifa) ni kingao, watu hupigana nyuma yake na hujilinda kupitia kwake." (Muslim)
Tarehe 5 Dhul-Hijjah 1443 H Tarehe 04/07/2022 BK