Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Mazungumzo ya Sahaba Mtukufu Rib'iy bin 'Amir na Rustum, Kamanda wa Waajemi

February 19, 2022
5746
Mfululizo wa majibu ya mwanachuoni mtukufu Ata bin Khalil Abu al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wake kwenye ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi"
Jibu la Swali

Kwa Muhammad Al-Muslih

Swali:

Historia imeturekodia mazungumzo yaliyofanyika kati ya Sahaba mtukufu Rib’iy bin ‘Amir na Rustum, kamanda wa Waajemi, kuhusu fikra za jumla za Uislamu na Jihad. Ni nini kilisemwa katika mazungumzo hayo?

Wakati wa ufunguzi (fat-h) wa Waajemi (Fars) uliofanywa na Waislamu, Rustum, kamanda wa Waajemi, alituma ombi kwa Waislamu akitaka ujumbe wa kuzungumza naye; hii ni kutokana na hamu yake kubwa ya kutaka suluhu, au njia nyingine yoyote itakayofanya jeshi la Kiislamu lirrejee bila kuingia naye katika vita. Hivyo, Rib’iy bin ‘Amir akaenda kukutana na Rustum, na Rib’iy hakuwa miongoni mwa makamanda wa majeshi ya Kiislamu, bali alikuwa ni kiongozi katika watu wake.

Haya hapa ni mazungumzo hayo:

Rustum: Mruhuni aingie.

Rib’iy akaingia na farasi wake juu ya mazulia yaliyotandikwa mbele yake. Alipoingia na farasi wake, alikuta mito (mishago) ikiwa na dhahabu; akapasua mmoja wao, akapitisha kamba ya farasi wake na kumfunga kwayo. Kisha akachukua mkuki wake na kuelekea upande wa Rustum akiuegemea, na mkuki huo ulikuwa ukitoboa mazulia na kuyapasua. Watu wa Uajemi walisimama kimya, hali kadhalika Rustum. Wakati wakiwa wanawaza mahali atakapoketi, aliketi chini ardhini, akaweka mkuki wake mbele yake akiuegemea, na Rustum akaanza kuzungumza.

Rustum: Ni nini kimekupelekea kufanya hivi? (Yaani: Ni nini kimekusukuma uketi chini?)

Rib’iy: Sisi hatupendi kuketi juu ya pambo lenu.

Rustum: Ni nini kimewaleta?

Rib’iy: Allah ametutuma ili tuwatoe waja kutoka katika ibada ya kuabudu waja na kuwapeleka katika ibada ya kumwabudu Mola wa waja, na kutoka katika dhulma za dini mbalimbali kwenda katika uadilifu wa Uislamu, na kutoka katika dhiki ya dunia kwenda katika wasaa wa dunia na Akhera. Hivyo, atakayekubali hayo kutoka kwetu, tutamkubalia na kumwacha, na asiyekubali, tutapokea kutoka kwake Jizya, na akizikataa, tutapigana naye mpaka tupate ushindi.

Rustum: Huenda mkafa kabla ya hilo.

Rib’iy: Allah (swt) ametuahidi kuwa Pepo ni kwa yule atakayekufa miongoni mwetu juu ya hilo, na ushindi ni kwa atakayebaki miongoni mwetu.

Rustum: Nimeyasikia maneno yako (yaani nimeelewa lengo lako), basi je, unaweza kutupa muda kidogo mpaka tushauriane na viongozi wetu na watu wetu? (Anaomba muda wa kufikiri).

Rib’iy: Ndio, nakupa kiasi unachopenda: siku moja au siku mbili?

Rustum: Hapana, bali nipe zaidi; mimi nazungumza na watu wangu walioko Madain.

Rib’iy: Hakika Mtume wa Allah ametuwekea sunna ya kutowapa nafasi maadui zetu, na kutowachelewesha wakati wa kukutana zaidi ya siku tatu (yaani siku tatu tu ili wasiweze kujiimarisha na kujipanga upya). Basi nakupa siku tatu baada yake; chagua kusilimu kisha tuondoke kwako, au Jizya; na kama utahitaji msaada wetu tutakusaidia, na kama huna haja na msaada wetu tutakuacha, au kupigana katika siku ya nne. Na mimi ni mdhamini kwako kwa niaba ya watu wangu kuwa hatutaanza kukupiga vita mpaka siku ya nne, isipokuwa kama utaanza wewe (yaani: mimi nakuhakikishia kuwa Waislamu hawatakupiga vita mpaka siku ya nne).

Rustum: Je, wewe ndiye kiongozi wao? (Yaani: Je, wewe ndiye bwana wa watu hawa na rais wao mpaka unidhaminie kuwa hawatannipiga vita?).

Rib’iy: Hapana, bali mimi ni mtu miongoni mwa jeshi, lakini aliye duni zaidi miongoni mwetu anaweza kutoa dhamana kwa niaba ya aliye juu zaidi miongoni mwetu. (Anamaanisha kuwa mtu wa chini kabisa miongoni mwetu akisema neno, au akiahidi ahadi, ni lazima itekelezwe na aliye juu miongoni mwetu).

Rustum akarudi kuzungumza na wasaidizi wake tena...

Rustum: Je, mmeona mantiki yake?! Je, mmeona nguvu yake?! Je, mmeona ujasiri wake?! (Alikuwa akihutubia watu wake ili kuwashawishi wafanye suluhu na Waislamu; na kwa njia hiyo aepuke kuingia katika vita nao).

Lakini walikataa na wakang’ang’ania...

Na vita vikatokea...

Waislamu wakashinda na dola ya Waajemi ikafikia tamati.

Ndugu yangu, je, mazungumzo haya ni ya kweli au ni ya uongo?

Wassalamu Alaykum Warahmatullah.

Jibu:

Wa Alaykumussalam Warahmatullah Wabarakatuh,

Ewe ndugu yangu, huu ndio utukufu (izzah) wa Uislamu na kinga yake na kutokuwa na khofu isipokuwa kwa Allah, Mwenye Nguvu, Mwenye Kushinda... Na kisa hiki kipo katika vyanzo kadhaa kikiwa na tofauti ya baadhi ya maneno bila kubadilisha maana ya jumla, na miongoni mwa vyanzo vilivyokinakili ni:

  • Tarikh al-Tabari (3/ 33-40)
  • Al-Bidaya wan-Nihaya cha Ibn Kathir (7/ 46-47)
  • Tarikh Ibn Khaldun (2/ 94-95)

Na naam, kama ilivyokuja katika vyanzo hivi (...Mkalimani alimwambia: Ni nini kimewaleta? Akasema: Allah ametutuma ili tuwatoe waja Wake kutoka katika dhiki ya dunia kuelekea katika wasaa wake na kutoka katika dhulma ya dini mbalimbali kuelekea katika uadilifu wa Uislamu, na ametutuma na dini Yake kwa viumbe Vyake; basi atakayeikubali, tutamkubalia na kumwacha yeye na ardhi yake, na atakayekataa tutapigana naye mpaka tufikie Peponi au Ushindi. Rustum akasema: Je, mwaweza kutucheleweshea jambo hili mpaka tulitazame? Akasema: Ndio, unapenda muda gani, siku moja au mbili? Akasema: Hapana, bali mpaka tuwaandikie watu wetu wa mashauri na viongozi wa watu wetu. Akasema: Hakika katika yale aliyotuwekea sunna Mtume wa Allah ﷺ ni kutowapa maadui nafasi zaidi ya siku tatu, basi angalia jambo lako na jambo lao na uchague ima Uislamu nasi tukuache wewe na ardhi yako, au Jizya nasi tupokee na tujizuilie nawe na ukihitaji msaada wetu tutakunusuru, au vita katika siku ya nne ikiwa utakataa, nami ni mdhamini wa hili kwa niaba ya wenzangu. Rustum akasema: Je, wewe ndiye kiongozi wao? Akasema: Hapana, lakini Waislamu ni kama mwili mmoja, mmoja wao anaweza kutoa ahadi kwa niaba ya mwingine, aliye duni miongoni mwao anaweza kutoa dhamana kwa niaba ya aliye juu yao...)

Na naam, huu ndio utukufu wa Uislamu, ushindi duniani na Akhera.

يَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ وَيُدْخِلْكُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِنْ تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ وَمَسَاكِنَ طَيِّبَةً فِي جَنَّاتِ عَدْنٍ ذَلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ * وَأُخْرَى تُحِبُّونَهَا نَصْرٌ مِنَ اللَّهِ وَفَتْحٌ قَرِيبٌ وَبَشِّرِ الْمُؤْمِنِينَ

"Atawasamehe dhambi zenu, na atakuingizeni katika Bustani (Peponi) zipitazo mito chini yake, na maskani nzuri katika Bustani za Milele. Huko ndiko kufanikiwa kukubwa. Na (atakupeni) kingine mnachokipenda, nacho ni nusura itokayo kwa Mwenyezi Mungu, na ufunguzi (ushindi) ulio karibu. Na wabashirie Waumini." (QS As-Saff [61]: 12-13).

Ndugu yenu Ata bin Khalil Abu al-Rashtah

18 Rajab Al-Khair 1443 H Inayoambatana na 19/02/2022 M

Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Allah amhifadhi) kwenye: Facebook

Share Article

Share this article with your network