Swali:
Kulitokea mjadala katika moja ya vikao kuhusu mada ya dua, hususan yale yaliyokuja katika kitabu cha Al-Mafahim ukurasa wa 57 na 58... kukawa na kuvutana: Je, dua ni kwa ajili ya kuomba thawabu pekee? Au inaweza kuwa na matokeo yanayohisika? Na je, njia ya utekelezaji wa fikra ya Kiislamu haiingiliwi na dua, bali ni vitendo vya kimaada vinavyofikia matokeo yanayohisika? Je, kuoanisha vitendo hivi na dua ni kinyume na njia ya Uislamu (tariqah)? Na vipi kuhusu hadith ya Mtume (saw): «MÃ MIN MUSLIMIN YAD’U BI DA’WATIN LAYSA FIHA ITHMUN, WALA QATI’ATU RAHIMIN, ILLA A’TAHULLAHU BIHA IHDA THALATHIN: IMMA AN TUAJJALA LAHU DA’WATUHU, WA IMMA AN YADDAKHIRAHA LAHU FIL-AKHIRAH, WA IMMA AN YASRIFA ‘ANHU MINAS-SUI MITHLAHA» (Hakuna Muislamu yeyote anayeomba kwa dua ambayo ndani yake hamna dhambi wala kukata udugu, isipokuwa Allah humpa moja ya mambo matatu: ama amharakishie dua yake, au amuekee akiba kwa ajili ya Akhera, au amuepushe na ubaya mfano wa dua hiyo). Wakasema: "Basi tutaongeza (dua)". Akasema: «Allah ana vingi zaidi». Yaani kwamba kuna matokeo yanayohisika yanayotokea kutokana na dua kama vile Allah kuharakisha kutimizwa kwa haja ya mwombaji hapa duniani? Pia, Allah amewafadhili waja Wake kwamba Yeye (swt) anajibu dua ya mwenye dhiki anapomwomba katika aya tukufu:
أَمَّنْ يُجِيبُ الْمُضْطَرَّ إِذَا دَعَاهُ
"Au nani yule anayemjibu mwenye dhiki anapomwomba..." (QS. An-Naml [27]: 62).
Tunaomba ufafanuzi wa jambo hili na Allah akulipe kheri.
Jibu:
Inaonekana kuna mkanganyiko katika kuelewa yaliyomo katika kurasa za 57 na 58 za Al-Mafahim. Yale yaliyotajwa kuhusu dua humo, na kwamba inaleta matokeo yasiyohisika (thawabu), yalikuwa katika muktadha wa hali fulani mahususi, nayo ni pale ambapo maandiko ya kisheria (nusus) yamebainisha njia ya utekelezaji (tariqah) wa jambo fulani, kisha tusiitumie njia hiyo na badala yake kutosheka na dua pekee. Kitabu kimetoa mfano wa jihadi na dua kuelekea kufungua ngome au kupigana na adui...
Ama katika hali nyingine isiyo hiyo, dua inaweza kuleta matokeo yanayohisika kwa idhini ya Allah, pamoja na thawabu kama ilivyokuja katika hadith ya Mtume (saw) iliyotajwa katika swali.
Ili jambo hili liwe wazi, nitapitia yale yaliyokuja katika kurasa za 57 na 58 za Al-Mafahim:
1- Ilikuja mwanzoni mwa ukurasa wa 57: (Na anayechunguza kwa kina vitendo hivi ambavyo vimeonyeshwa na hukumu za kisheria zinazohusiana na tariqah (njia ya utekelezaji), atakuta kuwa ni vitendo vya kimaada vinavyofikia matokeo yanayohisika na si vitendo vinavyofikia matokeo yasiyohisika...) Mwisho.
Na hili ni sahihi, kwani kwa kufuatilia dalili imebainika kuwa vitendo vya tariqah hufikia matokeo yanayohisika.
2- Kisha kitabu kulinganisha baada ya maandiko yaliyotangulia kati ya dua na jihadi katika hali ya kufungua ngome au mji au kuua adui, kikaona kuwa dua pekee si sehemu ya tariqah, na kwamba jihadi ndiyo tariqah katika hali hii, na hilo ni kwa mujibu wa dalili zilizokuja...
Ilikuja katika Al-Mafahim: (...Kwa mfano, dua ni kitendo kinachofikia thamani ya kiroho, na jihadi ni kitendo cha kimaada kinachofikia thamani ya kiroho, lakini dua ingawa ni kitendo cha kimaada, inafikia matokeo yasiyohisika nayo ni thawabu, hata kama kusudi la anayefanya dua ni kufikia thamani ya kiroho; tofauti na jihadi kwani ni kupigana na maadui na ni kitendo cha kimaada kinachofikia matokeo yanayohisika nayo ni kufungua ngome au mji au kuua adui na mfano wa hayo, hata kama kusudi la mujahid ni kufikia thamani ya kiroho...)
Hivyo ulinganifu hapa ni kati ya dua na jihadi wakati wa kupigana na maadui au kufungua ngome...:
Ikiwa dua itafanywa peke yake, basi inafikia matokeo yasiyohisika nayo ni thawabu, na hiyo ni kwa sababu tariqah iliyokuja katika hali hii ni jihadi na si dua. Kwa hiyo, mada ni ulinganifu wa dua ikiwa itatumiwa peke yake katika jambo fulani bila kutumia tariqah iliyobainishwa kwa jambo hilo.
Hairuhusiwi kueneza hali hii kwa kuifanya dua katika hali nyingine kuwa haina athari katika matokeo yanayohisika bali inaleta thawabu pekee! Kwani yaliyokuja katika aya iliyotangulia yanahusiana na jambo ambalo lina njia ya kivitendo katika Sharia ambalo halikuchukuliwa, bali badala yake ikachukuliwa dua pekee, hivyo dua ikawa na matokeo yasiyohisika nayo ni thawabu.
Inaonekana mkanganyiko umetokea kutokana na sentensi iliyokuja katika mfano uliotolewa, ambapo ilitajwa "lakini dua ingawa ni kitendo cha kimaada inafikia matokeo yasiyohisika nayo ni thawabu...", sentensi hii ikawa kwa baadhi yenu inadhaniwa kuwa ni ya kijumla, yaani kwamba dua katika hali zake zote haifikii isipokuwa matokeo yasiyohisika (thawabu), wakati ambapo muktadha wa mfano huo ni katika hali mahususi, nayo ni kutumia dua pekee katika kufungua ngome au kushinda adui bila kuchukua tariqah ambayo imekuja katika maandiko (Jihadi).
3- Ama kuhusu dua pamoja na kuchukua sababu (asbab), ina athari katika matokeo, na hivi ndivyo alivyokuwa Mtume (saw) na Maswahaba wake (ra). Mtume (saw) alikuwa akiandaa jeshi na kuingia katika kibanda chake (al-arish) akiomba, na Waislamu katika vita vya Al-Qadisiyyah walikuwa wakiandaa zana za kuvuka mto na Sa'd (ra) akimwelekea Allah kwa dua... na hivyo ndivyo waumini wa kweli wanavyojiandaa na kuanza kuomba. Mwenye kutafuta riziki anajitahidi na kutaabika huku akiomba, na mwanafunzi anasoma na kujitahidi huku akimwomba Allah (swt) mafanikio, na hilo linakuwa na athari katika matokeo kwa idhini ya Allah.
Ilikuja katika Al-Mafahim mwishoni mwa ukurasa wa 58: (Ila tu, ni lazima ijulikane kwamba hata kama kitendo kilichoonyeshwa na tariqah ni kitendo cha kimaada chenye matokeo yanayohisika, lakini ni lazima kitendo hicho kiongozwe na amri na makatazo ya Allah, na ikusudiwe katika kukiendesha kwa amri na makatazo ya Allah radhi za Allah. Vilevile, ni lazima Muislamu atawaliwe na utambuzi wake wa uhusiano wake na Allah (swt), hivyo ajikurubishe Kwake kwa swala, dua, kusoma Qur'ani na mfano wake, na ni lazima Muislamu aamini kuwa ushindi unatoka kwa Allah. Kwa sababu hiyo, kulikuwa na ulazima wa ucha-Mungu uliokita vifuani kwa ajili ya kutekeleza hukumu za Allah, na ikawa ni lazima kuwepo na dua, na lazima kumdhukuru Allah, na lazima kudumisha uhusiano na Allah wakati wa kufanya vitendo vyote). Na ni wazi kutokana na hayo umuhimu wa kuoanisha dua na kuchukua sababu katika vitendo vyote vya muumini, na umuhimu huu umeongezeka kwa kukaririwa neno "lazima" (ni lazima) kuonyesha umuhimu mkubwa wa kuoanisha vitendo vyote na dua na kudumisha uhusiano na Allah...
4- Kutumia dua pamoja na kuchukua sababu ndivyo, kama tulivyosema, alivyokuwa Mtume (saw) na Maswahaba wake (ra) na waumini. Na pindi vinapounganishwa, vinakuwa na athari katika matokeo kwa idhini ya Allah, na kuvitumia pamoja hakupingani na njia ya Uislamu (tariqah), bali kinachopingana nayo ni kutosheka na dua pekee bila tariqah iliyobainishwa na maandiko kwa ajili ya kutekeleza fikra ya Kiislamu.
Ilikuja katika Al-Mafahim mwishoni mwa ukurasa wa 57 na mwanzo wa ukurasa wa 58: (Na kwa ajili hiyo, inakataliwa kata kata kwamba vitendo vyote vinavyokusudiwa kutekeleza fikra ya Kiislamu viwe ni vitendo vinavyofikia matokeo yasiyohisika, na hilo huchukuliwa kuwa ni kinyume na njia ya Uislamu...).
Yaani, kinachopingana na tariqah ya Uislamu ni "kuwa vitendo vyote vinavyokusudiwa kutekeleza fikra ya Kiislamu viwe ni vitendo vinavyofikia matokeo yasiyohisika". Ama baadhi yake kufikia matokeo yasiyohisika (dua katika hali fulani) pamoja na vitendo vinavyofikia matokeo yanayohisika (maandalizi ya kimaada), basi hili ni jambo linalokubalika na muhimu, na halipingani na njia ya Uislamu.
5- Hivyo basi, yale yaliyokuja katika Al-Mafahim kuhusu dua yako katika hali mbili:
Kwanza: Kwamba ije peke yake katika kutekeleza fikra ambayo dua si sehemu ya njia ya utekelezaji wake, bali maandiko yameweka njia nyingine ya utekelezaji wake, kama vile dua pekee katika hali ya kupigana na adui, kwa kusimama mbele ya ngome ili kuifungua bila kuandaa jeshi la vita, bali kwa dua pekee. Katika hali hii, dua haifikii isipokuwa matokeo yasiyohisika (thawabu).
Pili: Kuoanisha dua na sababu (asbab), na hili ni jambo la lazima, na katika hali hii zinashirikiana (yenyewe na kuchukua sababu) katika kuathiri matokeo kwa idhini ya Allah.
Na hakukuja katika Al-Mafahim kuhusu dua kitu chochote katika hali nyinginezo, bali hizo zinajumuishwa na hadith ya kijumla aliyoitoa Ahmad katika Musnad yake: Kutoka kwa Abu Al-Mutawakkil, kutoka kwa Abu Sa'id, kwamba Mtume (saw) amesema:
مَا مِنْ مُسْلِمٍ يَدْعُو بِدَعْوَةٍ لَيْسَ فِيهَا إِثْمٌ، وَلَا قَطِيعَةُ رَحِمٍ، إِلَّا أَعْطَاهُ اللَّهُ بِهَا إِحْدَى ثَلَاثٍ: إِمَّا أَنْ تُعَجَّلَ لَهُ دَعْوَتُهُ، وَإِمَّا أَنْ يَدَّخِرَهَا لَهُ فِي الْآخِرَةِ، وَإِمَّا أَنْ يَصْرِفَ عَنْهُ مِنَ السُّوءِ مِثْلَهَا
"Hakuna Muislamu yeyote anayeomba kwa dua ambayo ndani yake hamna dhambi wala kukata udugu, isipokuwa Allah humpa moja ya mambo matatu: ama amharakishie dua yake, au amuekee akiba kwa ajili ya Akhera, au amuepushe na ubaya mfano wa dua hiyo." Wakasema: "Basi tutaongeza (dua)". Akasema: "Allah ana vingi zaidi."
Yaani Allah (swt) anamjibu mwombaji kwa moja ya mambo matatu, na miongoni mwayo ni «ama amharakishie dua yake». Na haya ni matokeo yanayohisika.
6- Kwa mujibu wa hayo, kuna matokeo yanayohisika yanayowezekana kwa dua katika hali isiyokuwa ile iliyotajwa katika Al-Mafahim, ambapo hadith imetaja moja ya mambo matatu «amharakishie dua yake» na haya ni matokeo yanayohisika. Mfano wa hili ni lile linalotokea katika swala ya kuomba mvua (istisqa) "nayo ni dua" kwa kufikia matokeo yanayohisika ya kunyesha mvua, na yanayotokea katika matibabu ya kisharia (ruqyah) "nayo ni dua" kwa kufikia matokeo yanayohisika ya kupona mgonjwa, kama inavyotokea katika kutumia dawa za kimaada...
Na Allah amewafadhili waja Wake katika aya Zake kwamba Yeye (swt) anajibu dua ya mwenye dhiki anapomwomba, na akajaalia jibu hili kuwa ni sehemu ya ushahidi kuwa hapana mungu ila Allah. Na ni wazi kutokana na hayo yote kuwa kujibiwa kwa mwenye dhiki hapa ni duniani, kwani neno "mwenye dhiki" (mudttar) ni sifa inayofahamisha uhitaji wa haja hapa duniani, hivyo jibu linakuwa la kuhisika kwa idhini ya Allah. Anasema (swt):
أَمَّنْ يُجِيبُ الْمُضْطَرَّ إِذَا دَعَاهُ وَيَكْشِفُ السُّوءَ وَيَجْعَلُكُمْ خُلَفَاءَ الْأَرْضِ أَإِلَهٌ مَعَ اللَّهِ قَلِيلًا مَا تَذَكَّرُونَ
"Au nani yule anayemjibu mwenye dhiki anapomwomba, na akaondoa dhiki, na akakufanyeni kuwa warithi wa ardhi? Je, yupo mungu pamoja na Allah? Ni machache sana mnayoyakumbuka." (QS. An-Naml [27]: 62).
Na Allah (swt) ametuamuru kuomba na akatuahidi jibu:
وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ
"Na Mola wenu amesema: Niombeni, Nitakujibuni." (QS. Ghafir [40]: 60).
Na Mtume (saw) ametafsiri jibu hili kuwa ni «moja ya mambo matatu» na miongoni mwayo ni matokeo yanayohisika. Na bila shaka, kufikiwa kwa matokeo, yawe yanayohisika au yasiyohisika, yote hayo ni kwa idhini ya Allah (swt).
Muhtasari:
- Yale yaliyokuja katika Al-Mafahim ni:
a- Tariqah ni vitendo vinavyofikia matokeo yanayohisika.
b- Ulinganifu kati ya dua pekee na jihadi katika mada ya kufungua ngome au kupigana na adui... hapa dua haileti matokeo yanayohisika, bali ni thawabu pekee, kwani dua pekee si sehemu ya njia ya kufungua ngome au kupigana na adui...
c- Haifai kwa vitendo vyote vinavyokusudiwa kutekeleza fikra ya Kiislamu kuwa ni vitendo vinavyoleta matokeo yasiyohisika, bali vinaweza kuwa mchanganyiko wa vitendo vinavyofikia matokeo yanayohisika pamoja na vitendo vinavyofikia matokeo yasiyohisika, kama vile kuandaa jeshi la vita pamoja na kumuomba Allah (swt) ushindi.
d- Dua ni jambo la lazima kwa Muislamu wakati anapofanya vitendo vya tariqah... kama alivyokuwa Mtume (saw) na Maswahaba (ra).
- Haya ndiyo yaliyokuja katika Al-Mafahim kuhusu hali ya dua ambayo haivuki zaidi ya thawabu, yaani katika hali ya kutumia dua pekee kwa jambo fulani kama kufungua ngome..., na kutoichukua njia (tariqah) iliyobainishwa na maandiko ya kisheria kwa ajili ya jambo hilo, ambayo hapa ni jihadi.
Ama hali nyingine za dua, hizo zinaangukia chini ya hadith ya kijumla ya Mtume (saw) «Hakuna Muislamu yeyote anayeomba kwa dua ambayo ndani yake hamna dhambi wala kukata udugu, isipokuwa Allah humpa moja ya mambo matatu: ama amharakishie dua yake, au amuekee akiba kwa ajili ya Akhera, au amuepushe na ubaya mfano wa dua hiyo» (Imetolewa na Ahmad katika Musnad yake).
Na kutokana nayo inabainika kuwa Allah (swt) anaweza kutimiza haja ya mwombaji hapa duniani, nayo ni ya kuhisika, au kumuondolea mwombaji ubaya mfano wake hapa duniani, nayo ni ya kuhisika, au kumuekea akiba Siku ya Kiyama nayo ni thawabu ambayo ni matokeo yasiyohisika.
Na Allah (swt) ni mwenye fadhila kuu, kwani Yeye ni Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu, anamkirimu mja Wake kwa thawabu za dua hata kama amejibu dua yake hapa duniani. Alhamdulillah Rabbil 'Alamin.