(Silsila ya majibu ya mwanachuoni Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi")
Kwa Ahmad Nadhif
Swali:
Assalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh. Imekuja katika kitabu cha At-Taysir fi Usul at-Tafsir ukurasa wa 44: "...au kwa njia ya mapokezi (naqli), yaani kupitia mapokezi ya mkato (ya yakini) kutoka kwa Allah (swt) katika Kitabu chake kitukufu au kutoka kwa Mtume wake (saw) katika hadith yake mutawatir kutoka kwake (saw), kama vile imani juu ya mambo ya ghaibu, Malaika, Vitabu vilivyoteremshwa hapo awali, Mitume waliopita, Siku ya Mwisho, na Qadar, kheri yake na shari yake. Allah (swt) anasema katika Surat An-Nisa aya ya 136:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا آمِنُوا بِاللَّهِ وَرَسُولِهِ وَالْكِتَابِ الَّذِي نَزَّلَ عَلَى رَسُولِهِ وَالْكِتَابِ الَّذِي أَنْزَلَ مِنْ قَبْلُ وَمَنْ يَكْفُرْ بِاللَّهِ وَمَلَائِكَتِهِ وَكُتُبِهِ وَرُسُلِهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا بَعِيدًا
"Enyi mlioamini! Mwaminini Allah na Mtume wake, na Kitabu alichokiteremsha kwa Mtume wake, na Kitabu alichokiteremsha kabla yake. Na anayemkataa Allah, Malaika wake, Vitabu vyake, Mitume wake, na Siku ya Mwisho, basi hakika amepotea upotevu wa mbali." (QS An-Nisa [4]: 136)
Na anasema (saw) katika kujibu swali la Jibril (as) kuhusu imani katika hadith:
أَنْ تُؤْمِنَ بِاللهِ، وَمَلَائِكَتِهِ، وَكُتُبِهِ، وَرُسُلِهِ، وَالْيَوْمِ الْآخِرِ، وَتُؤْمِنَ بِالْقَدَرِ خَيْرِهِ وَشَرِّهِ
"Ni kumwamini Allah, Malaika wake, Vitabu vyake, Mitume wake, Siku ya Mwisho, na kuamini Qadar, kheri yake na shari yake." (Mwisho wa nukuu).
Nina swali ninaloomba ufafanuzi kwenu. Ikiwa hadith hiyo iliyotajwa ni mutawatir kiasi kwamba imani katika Qadar imejengwa juu yake, kwa nini haikutajwa katika kitabu cha Ash-Shakhsiyyah al-Islamiyyah Juzuu ya 1 wakati kikijadili kuhusu Akida ya Kiislamu? Badala yake, mwandishi wa kitabu hicho (rehema za Allah ziwe juu yake) anasema kuwa imani katika Al-Qadha wal Qadar imejengwa juu ya ushahidi wa kiakili (dalil aqli).
Jazakallahu khayran, wassalamu alaikum warahmatullahi wabarakatuh.
Jibu:
Walaikum Assalam Warahmatullahi Wabarakatuh,
Kabla ya kuanza kujibu, napenda kukuvutia kwenye mambo mawili ambayo inaonekana yanakutatiza. Mambo haya ni (Al-Qadar) iliyotajwa katika aya na hadith, na istilahi ya (Al-Qadha wal Qadar). Haya ni mada mbili tofauti na si mada moja. Mada ya (Al-Qadha wal Qadar) uliyoisoma katika kitabu cha An-Nidham (Mfumo) au Ash-Shakhsiyyah (Shakhsia) ni tofauti na (Al-Qadar) iliyotajwa katika hadith unayoulizia.
Na sasa, hili hapa ni jibu la swali lako:
1- Kilichokuja katika upokezi wa Muslim kuhusu kauli ya Mtume (saw) alipomjibu Jibril (as) kuhusu imani:
قَالَ: أَنْ تُؤْمِنَ بِاللهِ، وَمَلَائِكَتِهِ، وَكُتُبِهِ، وَرُسُلِهِ، وَالْيَوْمِ الْآخِرِ، وَتُؤْمِنَ بِالْقَدَرِ خَيْرِهِ وَشَرِّهِ
"Akasema: Ni kumwamini Allah, Malaika wake, Vitabu vyake, Mitume wake, Siku ya Mwisho, na kuamini Qadar, kheri yake na shari yake."
Hii si hadith mutawatir, bali ni hadith sahih ya mmoja mmoja (habar ahad). Pamoja na hayo, kuitumia kama ushahidi katika sehemu uliyotaja kwenye kitabu cha At-Taysir fi Usul at-Tafsir ni sahihi. Hii ni kwa sababu imetajwa kama ushahidi wa kile kinachotakiwa kuaminiwa (imani ya kijumla), na haikutumika kama ushahidi wa kuanzisha mada hiyo ya kiitikadi. Kwani takwa la kuamini Uislamu linafanyika kwa aya na hadith kutoka kwa Mtume (saw), na hata kwa barua alizozituma (saw). Mtume (saw) alituma barua pamoja na wajumbe aliowatuma kwa wafalme akiwalingania katika Uislamu...
2- Lakini wakati wa kusimamisha hoja kwamba Al-Qadar ni sehemu ya Akida na anayeikana ni kafiri, na wakati wa kuthibitisha kuwa hiyo ni elimu ya Allah na kwamba kila kitu kimeandikwa tangu milele katika Ubao uliohifadhiwa (Al-Lawh al-Mahfuz), hapo hutumiwa ushahidi wa mkato (dalil qati’i). Hivyo basi, zinatajwa aya za mkato kuhusu Qadar kwa maana ya ukadiriaji tangu milele (at-taqdir fil azal), yaani kwamba hakuna kitu ardhini wala mbinguni isipokuwa Allah anakijua tangu milele, amekikadiria tangu milele, na kimeandikwa katika Al-Lawh al-Mahfuz tangu milele... Miongoni mwa aya hizi za mkato ni:
Kauli yake Allah (swt):
إِلَّا امْرَأَتَهُ قَدَّرْنَا إِنَّهَا لَمِنَ الْغَابِرِينَ
"Isipokuwa mke wake; tumekadiria kuwa yeye atakuwa miongoni mwa watakaobaki nyuma (waangamizwao)." (QS Al-Hijr [15]: 60)
Neno "Tumekadiria" katika aya hii maana yake ni ukadiriaji tangu milele. Na kauli yake Allah (swt):
وَمَنْ يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّهِ فَهُوَ حَسْبُهُ إِنَّ اللَّهَ بَالِغُ أَمْرِهِ قَدْ جَعَلَ اللَّهُ لِكُلِّ شَيْءٍ قَدْرًا
"Na anayemtegemea Allah, basi Yeye humtosha. Hakika Allah anatimiza jambo lake. Hakika Allah amejalia kwa kila kitu kipimo chake (Qadar)." (QS At-Talaq [65]: 3)
Maana ya "kila kitu kipimo chake" ni kwamba kila kitu kina makadirio na wakati wake, na kinachokusudiwa ni ukadiriaji tangu milele. Na kauli yake (swt):
قُلْ لَنْ يُصِيبَنَا إِلَّا مَا كَتَبَ اللَّهُ لَنَا هُوَ مَوْلَانَا وَعَلَى اللَّهِ فَلْيَتَوَكَّلِ الْمُؤْمِنُونَ
"Sema: Halitatusibu lolote ila alilotuandikia Allah, Yeye ndiye Mlinzi wetu. Na kwa Allah pekee wategemee Waumini." (QS At-Tawbah [9]: 51)
Maana yake ni kwamba halitatusibu lolote isipokuwa kile alichotuandikia Allah tangu milele na kile alichotukadiria, na sisi tunamtegemea Allah. Na kauli yake (swt):
وَمَا مِنْ دَابَّةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا طَائِرٍ يَطِيرُ بِجَنَاحَيْهِ إِلَّا أُمَمٌ أَمْثَالُكُمْ مَا فَرَّطْنَا فِي الْكِتَابِ مِنْ شَيْءٍ
"Na hakuna mnyama yeyote ardhini wala ndege arukaye kwa mabawa yake mawili, ila ni umma kama nyinyi. Hatukupunguza chochote katika Kitabu." (QS Al-An'am [6]: 38)
Maana yake ni kuwa wao ni umma kama nyinyi, riziki zao, ajali zao, na matendo yao yameandikwa kama vilivyoandikwa vyenu. Hatukuacha wala hatukughafilika katika Al-Lawh al-Mahfuz na chochote. Hapa neno "Kitabu" limetumika kumaanisha Al-Lawh al-Mahfuz, yaani kila kitu kimeandikwa humo. Hii ni fumbo la elimu ya Allah, yaani hakuna kitu isipokuwa Allah anakijua. Na kauli yake (swt):
عَالِمِ الْغَيْبِ لَا يَعْزُبُ عَنْهُ مِثْقَالُ ذَرَّةٍ فِي السَّمَاوَاتِ وَلَا فِي الْأَرْضِ وَلَا أَصْغَرُ مِنْ ذَلِكَ وَلَا أَكْبَرُ إِلَّا فِي كِتَابٍ مُبِينٍ
"Mjuzi wa ghaibu; hakifichiki kwake hata uzito wa mdudu chungu mbinguni wala ardhini, wala kilicho kidogo kuliko hicho wala kikubwa zaidi, isipokuwa kimo katika Kitabu chenye kubainisha." (QS Saba [34]: 3)
Yaani isipokuwa kimeandikwa katika Al-Lawh al-Mahfuz, nalo ni fumbo la elimu yake (swt) kwa ushahidi wa aya hiyo hiyo.
3- Ni vyema kutaja kwamba Qadar kwa maana hii, yaani ukadiriaji wa tangu milele au kuandikwa katika Al-Lawh al-Mahfuz au elimu ya Allah (swt) kwamba jambo fulani litatokea, haimaanishi kubweteka (ittikal) na kutegemea elimu ya Allah bila kutumia nyenzo za kufanya kazi au bila kufuata kanuni za visababishi na matokeo (asbab wal musabbabat). Hii ni kwa sababu elimu ya Allah haijafichuliwa kwa yeyote ili ajue kama jambo litatokea au halitatokea. Kwa hivyo, haiwezekani kujua kitu kama kitatokea au la, isipokuwa baada ya kuchukua nyenzo za kukifanya na kukitekeleza. Baada ya hapo ndipo ukweli unadhihirika kama kazi hiyo imepatikana au la. Kutokana na hapa, si sahihi kwa yeyote kubweteka na elimu ya Allah na kuacha kufanya kazi. Masahaba walitatizika na jambo hilo, na Mtume (saw) akawabainishia wasibweteke na akawaamrisha wafanye kazi. Bukhari amepokea kutoka kwa Ali (karramallahu wajhah):
فَقَالَ رَجُلٌ مِنْ الْقَوْمِ: أَلاَ نَتَّكِلُ يَا رَسُولَ اللَّهِ؟ قَالَ: لاَ، اعْمَلُوا فَكُلٌّ مُيَسَّرٌ، ثُمَّ قَرَأَ: فَأَمَّا مَنْ أَعْطَى وَاتَّقَى الآيَةَ
"Mtu mmoja katika watu akasema: Je, tusibweteke (tusitegemee maandiko pekee) Ewe Mtume wa Allah? Akasema: Hapana, fanyeni kazi, kwani kila mmoja amerahisishiwa (kile alichoumbiwa), kisha akasoma: 'Basi yule anayetoa na akacha mungu...' hadi mwisho wa aya."
Hii ni wazi kuwa imani katika Qadar haimaanishi kubweteka, kwa sababu Qadar na maandiko (elimu ya Allah) havijafichuliwa kwa yeyote miongoni mwa viumbe; sasa atabweteka juu ya kitu gani?
Ndio maana Mtume (saw) alimwambia yule aliyemuuliza "Je, tusibweteke?": "Hapana", yaani akamkataza kubweteka, na hakutosheka na hilo bali alimwambia pia: "Fanyeni kazi", yaani akamuamuru afanye kazi. Kwa sababu hiyo, imani katika Qadar haimaanishi kuacha kufanya kazi.
Natumai jibu la swali lako kuhusu Qadar limekuwa wazi.
Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir wa Facebook