Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Kuhusu Taqiyya

July 09, 2013
5946

** (Mfululizo wa majibu ya mwanachuoni Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wageni wa ukurasa wake wa Facebook)**

Kwa Abu Muhammad Al-Sawalmeh

Swali:

Assalamu Alaikum Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh.

Mwanachuoni mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Allah akulinde.

Naomba upana wa kifua chenu na muda wenu kwa ajili ya kunijibu maswali yafuatayo:

"Waziri wa Wakfu na Masuala ya Kiislamu wa Jordan alisema kuwa Mtume (saw) alifanya taqiyya, na kwamba imetajwa katika maandiko ya Qur'ani na Hadithi tukufu, na kwamba kuna imani potofu kwamba inatokana na dhehebu la Shia pekee. Alitolea ushahidi andiko la aya 'isipokuwa yule aliyelazimishwa na huku moyo wake umetulia juu ya imani', na kauli yake (saw) 'Hakika katika mafumbo ya maneno kuna upana wa kuepukana na uongo'. Aliongeza kuwa Mtume (saw) alifanya taqiyya pale alipoulizwa na mbedui 'Unatoka wapi?' akajibu (saw) 'Kutokana na maji', akikusudia maji duni (manii), huku akiwauliza majaji 'Je, hii si taqiyya?'. Pia alisisitiza kukataa kwake kuwakafirisha Mashia, akisisitiza kuwa wao ni Waislamu mradi tu wanashuhudia kuwa hapana mungu apasaye kuabudiwa kwa haki ila Allah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allah.

Alisema pia kuwa tofauti kati ya taqiyya ya kisheria na taqiyya ya Kishia ni kwamba ya mwisho inachukuliwa kuwa miongoni mwa misingi ya dini (usul ad-din) na miongoni mwa mambo ya lazima katika itikadi, bali hakuna dini wala imani kwa yule asiyekuwa na taqiyya. Wakati ambapo taqiyya ya kisheria ni miongoni mwa masuala ya matawi (furu') na si misingi, na hapana ubaya ikiwa Muislamu ataiacha na kutoitumia."

Swali: Je, kutolea kwake ushahidi kwa aya na hadithi kuhusu suala la taqiyya ni sahihi?

Je, ni sahihi alichokisema kuhusu tofauti kati ya taqiyya ya kisheria na taqiyya ya Kishia?

Allah (swt) amesema:

لَا يَتَّخِذِ الْمُؤْمِنُونَ الْكَافِرِينَ أَوْلِيَاءَ مِنْ دُونِ الْمُؤْمِنِينَ وَمَنْ يَفْعَلْ ذَلِكَ فَلَيْسَ مِنَ اللَّهِ فِي شَيْءٍ إِلَّا أَنْ تَتَّقُوا مِنْهُمْ تُقَاةً

"Waumini wasiwafanye makafiri kuwa marafiki walinzi badala ya waumini. Na atakayefanya hivyo, basi hana chochote kwa Allah, isipokuwa mkilinda nafsi zenu kwao kwa tahadhari (taqiyya)." (QS Al-Imran [3]: 28)

Ibn Jarir alisema: "Taqiyya aliyoitaja Allah katika aya hii ni taqiyya dhidi ya makafiri pekee, si wengineo." Na Said bin Jubair alisema: "Hakuna taqiyya katika Uislamu, hakika taqiyya ni kwa ajili ya watu wa vita (ahl al-harb)."

Je, makusudio ya aya tukufu ni taqiyya?

Je, inawezekana kusema kuhusu Mashia wote kuwa ni Waislamu pamoja na kauli yao kuhusu kugeuzwa kwa Qur'ani, kuwatukana Makhalifa Waongofu (ra) na kumfanya bwana wetu Ali (kw) kuwa mungu...?

Shukrani na takdiri zote kwenu.

Jibu:

Wa Alaikum Salaam Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh.

Hakika huyo waziri amechanganya mambo matatu na kuyaweka katika mkondo mmoja kwa ajili ya lengo fulani nafsini mwake, hatupendi kusema zaidi ya hapo!

Jambo la kwanza: Taqiyya katika aya tukufu (إِلَّا أَنْ تَتَّقُوا مِنْهُمْ تُقَاةً). Jambo la pili: Aya tukufu (إِلَّا مَنْ أُكْرِهَ وَقَلْبُهُ مُطْمَئِنٌّ بِالْإِيمَانِ). Na jambo la tatu: Hadithi ya Mtume (saw) aliyoitoa Abu Bakr Al-Bayhaqi (aliyekufa 458 H) katika Shu'ab al-Iman, kutoka kwa Mutarrif bin Abdullah, amesema: Tulielekea pamoja na Imran bin Husain kutoka Basra kwenda Kufa, na alikuwa akisema: "Hakika katika mafumbo kuna upana wa kuepukana na uongo," hii ndiyo sahihi ikiwa imesimama kwa sahaba (mawquf). Na ameitoa Ibn al-A'rabi (aliyekufa 340 H) katika Mu'jam yake ikiwa imenyanyuliwa kwa Mtume (marfu') akisema: Ametuhadithia Dawud bin al-Zibriqan, kutoka kwa Said, kutoka kwa Qatada, kutoka kwa Zurara bin Abi Awfa, kutoka kwa Imran bin Husain, kwamba Mtume (saw) amesema:

إِنَّ فِي الْمَعَارِيضِ مَنْدُوحَةً عَنِ الْكَذِبِ

"Hakika katika mafumbo (ya maneno) kuna upana wa kuepukana na uongo."

Mambo haya matatu kila moja lina mahali pake, na haijuzu kuingiza lolote kati yake katika nafasi ya jengine. Ili kufafanua hilo tunasema:

Kwanza: Ama taqiyya inayojuzu kisheria ni ile iliyopo kati ya Muislamu na makafiri ikiwa Muislamu anaishi miongoni mwao chini ya mamlaka yao na akawa anakabiliwa na madhara makubwa ikiwa hatadhihirisha utiifu na mapenzi kwao... ikiwa hali ni hiyo, basi inajuzu kwake kudhihirisha mapenzi kwao kwa ulimi wake bila moyo wake. Lakini haijuzu kwa Muislamu kudhihirisha kwa Muislamu mwenzake kinyume na anavyoficha moyoni, vyovyote atakavyokuwa Muislamu huyo, awe miongoni mwa watu wa kawaida au miongoni mwa viongozi kama mtawala dhalimu; jambo hili haijuzu kisheria.

Ushahidi wa hilo ni andiko la aya tukufu na maudhui yake. Ama andiko lake, Allah (swt) anasema:

لَا يَتَّخِذِ الْمُؤْمِنُونَ الْكَافِرِينَ أَوْلِيَاءَ مِنْ دُونِ الْمُؤْمِنِينَ وَمَنْ يَفْعَلْ ذَلِكَ فَلَيْسَ مِنَ اللَّهِ فِي شَيْءٍ إِلَّا أَنْ تَتَّقُوا مِنْهُمْ تُقَاةً وَيُحَذِّرُكُمُ اللَّهُ نَفْسَهُ وَإِلَى اللَّهِ الْمَصِيرُ

"Waumini wasiwafanye makafiri kuwa marafiki walinzi badala ya waumini. Na atakayefanya hivyo, basi hana chochote kwa Allah, isipokuwa mkilinda nafsi zenu kwao kwa tahadhari (taqiyya). Na Allah anawaonya nanyi na nafsi Yake, na kwa Allah ndiyo marejeo." (QS Al-Imran [3]: 28)

Ama maudhui ya aya hiyo yako wazi katika andiko lake: nayo ni waumini kuwafanya makafiri kuwa marafiki, yaani kudhihirisha urafiki nao... Andiko ni: (لَا يَتَّخِذِ الْمُؤْمِنُونَ الْكَافِرِينَ أَوْلِيَاءَ مِنْ دُونِ الْمُؤْمِنِينَ). Na ikiwa aya au hadithi imekuja katika maudhui fulani, basi inakuwa mahususi katika maudhui hayo na haijumuishi mengine...

Aya hii ilishuka katika hali ya Waislamu ambao hawakuhama na wakabaki Makka chini ya mamlaka ya makafiri wa Kikuraishi, wakiwa wamezidiwa nguvu, na walikuwa pindi wakidhihirisha uadui na kutokuwatii basi walikabiliwa na madhara makubwa... Kwa hiyo aya tukufu ikawavua. Maana ya aya hiyo ni:

Uharamisho mkali wa waumini kuwafanya makafiri kuwa marafiki walinzi kwa aina yoyote ile ya urafiki, na uharamisho huo umesisitizwa kwa kauli Yake (swt) (وَمَنْ يَفْعَلْ ذَلِكَ فَلَيْسَ مِنَ اللَّهِ فِي شَيْءٍ), kisha aya ikavua hali moja tu, yaani hali inayofanana na hali ya Waislamu ambao hawakuhama kutoka Makka na wakabaki chini ya mamlaka ya makafiri wa Kikuraishi, wakiwa wamezidiwa nguvu, wakawa wanahofia madhara kutoka kwao ikiwa watawadhihirishia uadui na kutokuwatii. Hii ndiyo hali iliyovuliwa.

Kwa mujibu wa hayo, kudhihirisha mapenzi kwa mtawala Muislamu kwa hofu ya madhara yake akiwa ni dhalimu, fasiki anayehukumu kwa ukafiri ni haramu. Kadhalika kudhihirisha mapenzi kwa Muislamu anayetofautiana nawe kifikra huku ukimchukia moyoni ni haramu. Na kujifanya kutofungamana na Uislamu au kutokuujali mbele ya kafiri au mbele ya fasiki dhalimu haijuzu, kwani yote hayo na yanayofanana nayo ni unafiki (nifaq) ambao Sharia imeuharamisha kwa Waislamu. Kwani maudhui ya: (إِلَّا أَنْ تَتَّقُوا مِنْهُمْ تُقَاةً), yamefungika katika uhalisia wa hali ya Waislamu waliokuwa Makka miongoni mwa washirikina, yaani yamefungika katika hali ya kuwepo kwa Waislamu chini ya mamlaka ya makafiri, na wasiwe na uwezo wa kuondoa mamlaka hayo, yaani wawe wamezidiwa nguvu.

Al-Tabari (aliyekufa 310 H) amesema katika tafsiri yake kuhusu kauli ya (لَا يَتَّخِذِ الْمُؤْمِنُونَ الْكَافِرِينَ أَوْلِيَاءَ) mpaka kauli ya (إِلَّا أَنْ تَتَّقُوا مِنْهُمْ تُقَاةً), Abu Ja'far amesema: Huku ni kukataza kutoka kwa Allah (swt) kwa waumini wasiwafanye makafiri kuwa wasaidizi, wanusurishaji na waungaji mkono. Isipokuwa muwe katika mamlaka yao mkawahofia nafsi zenu, hapo mkatadhihirisha kwao urafiki kwa ndimi zenu... lakini msiwafuate katika yale waliyomo ya ukafiri, wala msiwasaidie dhidi ya Muislamu kwa kitendo chochote.

Hivyo basi, kile wanachokiita taqiyya ambacho ni muumini kudhihirisha kinyume na anavyoficha moyoni mbele ya mtawala dhalimu au fasiki mwenye nguvu, au anayetofautiana naye kifikra au mfano wa hayo kinafutika, na kufanya hivyo ni haramu kwa sababu ni unafiki, na unafiki wote ni haramu.

*Pili: Aya tukufu (مَنْ كَفَرَ بِاللَّهِ مِنْ بَعْدِ إِيمَانِهِ إِلَّا مَنْ أُكْرِهَ وَقَلْبُهُ مُطْمَئِنٌّ بِالْإِيمَانِ), maudhui yake ni suala la ukafiri baada ya imani, yaani suala la kuritadi kutoka kwenye Uislamu, na hali husika ni hali ya kuhofia kifo, jambo ambalo mafaqihi wanaliita shinikizo la lazima (ikrah mulji'). Na hili pekee ndilo shinikizo linalozingatiwa kisheria katika hali zote ambazo hukumu huondoka kwa aliyelazimishwa. Shinikizo linalovuliwa kisheria ni lile shinikizo la lazima, ambalo ni hali ya kuhofia kuuawa kwa yakini. Aya hii ilishuka kwa Ammar bin Yasir (ra), washirikina walimkamata na kumtesa, wakawaua mama na baba yake kwa sababu walikataa kukufuru... Walikuwa wakimtesa Ammar bin Yasir mateso makali mpaka akakaribia kuuawa kama mama na baba yake, ndipo Ammar akasema neno la ukafiri.*

Al-Tabari amesema: Ametuhadithia Ibn Abd al-A'la akisema: Ametuhadithia Muhammad bin Thawr kutoka kwa Ma'mar kutoka kwa Abdul Karim al-Jazari kutoka kwa Abu Ubaidah bin Muhammad bin Ammar bin Yasir akisema: Washirikina walimkamata Ammar bin Yasir wakamtesa mpaka akawapa baadhi ya walichotaka, akamtajia Mtume (saw) jambo hilo, Mtume (saw) akasema: "Unauonaje moyo wako? Akasema: Umetulia juu ya imani. Mtume (saw) akasema: Ikiwa watarudia (kutesa), basi rudia (kusema neno hilo)." Na hivi ndivyo sababu ya kushuka aya hii ilivyokuwa tukio la Ammar na maudhui yake ni kuritadi kutoka kwenye Uislamu. Na hali mahususi kwake ni hofu ya kuuawa kwa yakini, na hili pekee linatosha kusisitiza kuwa haina uhusiano na aya ya: (إِلَّا أَنْ تَتَّقُوا مِنْهُمْ تُقَاةً). Isitoshe, aya ya: (إِلَّا مَنْ أُكْرِهَ وَقَلْبُهُ مُطْمَئِنٌّ بِالْإِيمَانِ) ni ya Makka (Makkiyya) ilishuka katika maudhui ya imani, na aya ya: (إِلَّا أَنْ تَتَّقُوا مِنْهُمْ تُقَاةً) ni ya Madina (Madaniyya) ilishuka katika maudhui ya haramu ya waumini kuwafanya makafiri kuwa marafiki na kuvuliwa kwa hali tuliyoibainisha. Kwa hiyo, hii ni tofauti na ile na wala moja haingii katika nyingine, wala haziunganishwi kwa sababu ya kutofautiana kwa hali na maudhui. Kwani Muislamu akiwa chini ya mamlaka ya makafiri na amezidiwa nguvu kwao, haijuzu kwake kuritadi kutoka kwenye Uislamu kidhahiri ili kuwapotosha, bali ni lazima kwake kuhama ikiwa hawezi kusimamisha hukumu za dini yake; tofauti na kuwafanya marafiki kwa ulimi wake bila moyo wake, kwani hilo linajuzu. Lakini ikiwa Muislamu atahofia nafsi yake kuuawa kwa yakini, na akalazimishwa kukufuru, hapo inajuzu kwake kudhihirisha ukafiri na kuficha imani moyoni, na tofauti iko wazi kabisa kati ya aya hizi mbili tukufu.

Tatu: Hadithi ya Mtume (saw) iliyonyanyuliwa na iliyosimama kwa sahaba "Hakika katika mafumbo kuna upana wa kuepukana na uongo", hii imekuja katika maudhui ya tawriyah (mafumbo). Hili si katika mlango wa uongo au kudhihirisha kile ambacho hakimo moyoni, bali ni katika mlango wa ukweli, ambapo mtu hutumia neno lenye maana mbili: moja ya mbali na moja ya karibu, akili ya msikilizaji inakimbilia maana ya karibu, lakini makusudio ni ile maana ya mbali ya neno hilo. Hii ndiyo maana ya ma'aridh.

Imekuja katika Mukhtar al-Sahah: ("Al-Ta'ridh" ni kinyume cha "Al-Tasrih" (uwazi), na kutokana nayo yanakuja "Al-Ma'aridh" katika maneno nayo ni tawriyah (kuficha) jambo kwa jambo jingine). Na "Al-Mandoohah", Abu Ubaid amesema ina maana ya wasaa na upana. Maana yake basi ni kuwa kutumia mafumbo au tawriyah ni njia ya kujiepusha na uongo. Na jibu la Mtume (saw) kwa yule mzee alipomuuliza "Mnatoka wapi?", Mtume (saw) akajibu "Sisi tunatokana na maji", hii ni tawriyah na si taqiyya:

Imekuja katika Sira ya Ibn Hisham (Mtume saw na Abu Bakr walikuwa wakitafuta habari za Maquraishi... kisha wakashuka karibu na Badr, yeye na mtu katika maswahaba zake wakapanda wanyama: Ibn Hisham akasema: Mtu huyo ni Abu Bakr Al-Siddiq. Ibn Ishaq amesema kama alivyonihadithia Muhammad bin Yahya bin Habban: Mpaka wakasimama kwa mzee mmoja katika Waarabu, akamuuliza kuhusu Maquraishi, na kuhusu Muhammad na maswahaba zake na habari zilizomfikia kuwahusu. Yule mzee akasema: Sitawaambia mpaka mniambie nyinyi mnatoka wapi? Mtume (saw) akasema: Ukituambia tutakuambia. Akasema: Je, hili ni kwa lile? Akasema: Ndiyo. Yule mzee akasema: Hakika nimefikiwa na habari kuwa Muhammad na maswahaba zake walitoka siku fulani na fulani, ikiwa aliyeniambia ni mkweli, basi leo watakuwa sehemu kadhaa wa kadhaa - akitaja sehemu aliyokuwepo Mtume saw - na nimefikiwa na habari kuwa Maquraishi walitoka siku fulani na fulani, ikiwa aliyeniambia ni mkweli, basi leo watakuwa sehemu kadhaa wa kadhaa - akitaja sehemu waliyokuwepo Maquraishi. Alipomaliza habari zake, akasema: Nyinyi mnatoka wapi? Mtume (saw) akasema: Sisi tunatokana na maji (Nahnu min ma'in), kisha akaondoka. Akasema yule mzee: Anatokana na maji gani? Je, ni maji ya Iraq? Ibn Hisham amesema: Inasemekana yule mzee alikuwa Sufyan al-Damri).

Mtume (saw) alipomwambia yule mzee akijibu swali lake "Mnatoka wapi?", "Sisi tunatokana na maji", alitumia tawriyah na mafumbo ya maneno, kwani "maji" ina maana ya maji ya kawaida na ina maana ya maji ya uhai yaani manii ambayo kijusi huumbwa kutokana nayo. Akili ya yule mzee ikakimbilia kuwa Mtume (saw) anatoka katika kijiji au eneo lililo karibu na maji fulani, kama Waarabu walivyokuwa wakifanya kwa kushuka kwenye maji fulani. Mtume (saw) hakutumia taqiyya kwa sababu taqiyya haijuzu isipokuwa katika hali ya Muislamu kuishi akiwa amezidiwa nguvu chini ya utawala wa makafiri ili kuzuia shari na madhara yao, na katika hali isiyokuwa hiyo haijuzu kwa sababu itakuwa ni uongo na unafiki, na hashingwi Mtume (saw) na hayo, kwani yeye (saw) ni mkweli mwenye kusadikiwa.

Na hakika yule waziri amekosea kwa kauli yake kuhusu Mtume (saw) kwamba alitumia taqiyya, na huenda akasoma jibu hili kisha akamwomba Allah msamaha na kutubu Kwake, na huenda akafanya hivyo, kwani sisi tunampendelea kila Muislamu aongoke kwenye haki na atubu kutokana na makosa, na kama alivyosema (saw):

كُلُّ ابْنِ آدَمَ خَطَّاءٌ وَخَيْرُ الخَطَّائِينَ التَّوَّابُونَ

"Kila mwanadamu ni mkosaji, na bora wa wakosaji ni wenye kutubu." (Al-Tirmidhi).

Ama kwa upande wa Mashia wanaofuata madhehebu ya Jafari, wao kimsingi ni Waislamu. Ama yule anayesema kuwa Qur'ani imebadilishwa au anayemfanya Ali (ra) kuwa mungu, huyo ni kafiri, na hahesabiwi miongoni mwa Waislamu.

Ndugu yenu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

Kiungo cha jibu kutoka ukurasa wa Amir kwenye Facebook

Kiungo cha jibu kutoka tovuti ya Amir

Kiungo cha jibu kutoka ukurasa wa Amir kwenye Google Plus

Share Article

Share this article with your network