(Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Ameer wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Watembeleaji wa Ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi")
Kwa: Leni Marlina
Swali:
Assalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh. Nimekuulizeni mara nyingi kuhusu suala hili: Je, inajuzu kwa mwanamke mwenye hedhi kusoma Qur’an? Kwani nimesikia majibu tofauti... ni lipi jibu sahihi? Allah akulipe kheri.
Jibu:
Wa Alaikum Salaam Warahmatullahi Wabarakatuh.
Usomaji wa Qur’an kwa mwanamke mwenye hedhi ni suala ambalo lina maelezo ya kikhitilafu miongoni mwa mafaqihi; wengi miongoni mwa mafaqihi wanasema ni haramu, na wengineo wanaliruhusu kwa maelezo na masharti fulani...
Na lile ninaloliona kuwa na nguvu zaidi ni kwamba haijuzu kwa mwanamke mwenye hedhi kusoma Qur’an, kwa kauli ya Mtume (saw):
لَا تَقْرَأُ الْحَائِضُ وَلَا الْجُنُبُ شَيْئًا مِنَ الْقُرْآنِ
"Mwanamke mwenye hedhi wala mwenye janaba asisome chochote katika Qur’an." (Imepokelewa na At-Tirmidhi)
Hadithi hii, ingawa kuna maneno juu yake (kuhusu usahihi wake), lakini mafaqihi wengi wanaifanyia kazi. Pamoja na hayo, imepokelewa Hadithi sahihi kuhusu uharamu wa kusoma Qur’an kwa mwenye janaba, na mwanamke mwenye hedhi ni kama mwenye janaba katika suala hili. Abu Dawood na An-Nasa'i wamepokea, na katika riwaya ya Ibn Majah mfano wa hiyo kutoka kwa Ali (ra) amesema:
كَانَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم يَخْرُجُ مِنَ الْخَلَاءِ فَيُقْرِئُنَا الْقُرْآنَ وَيَأْكُلُ مَعَنَا اللَّحْمَ، وَلَمْ يَحْجُبْهُ - أَوْ يَحْجُزْهُ - عَنِ الْقُرْآنِ شَيْءٌ لَيْسَ الْجَنَابَةَ
"Mtume (saw) alikuwa akitoka msalani akitufundisha Qur’an na akila nasi nyama, na hakuna kitu kilichokuwa kikimzuia - au kikimkinga - na Qur’an isipokuwa janaba."
Ni wazi kutokana na Hadithi hiyo kwamba janaba inazuia kusoma Qur’an, yaani inaharamisha kusoma Qur’an kwa mwenye janaba. Na mwanamke mwenye hedhi ni kama mwenye janaba, hivyo ni haramu kwake kusoma Qur’an kama ilivyo haramu kwa mwenye janaba kusoma Qur’an.
Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah
Kiungo cha jibu kutoka kwenye tovuti ya Ameer
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Ameer wa Google Plus
