Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Kuhusu Kutafuta Nusra (Talab al-Nusrah)

June 26, 2013
5104

(Silsila ya Majibu ya Mwanachuoni Ata bin Khalil Abu al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Wageni Kwenye Ukurasa Wake wa Facebook)

Kwa Okab Alhak

Swali:

As-Salaamu Alaykum.

Imeelezwa katika kitabu cha At-Takattul kuwa marhala ya kushika utawala ni kupitia Umma na vitendo vya kutafuta nusra (talab al-nusrah). Je, kutafuta nusra ni sehemu ya marhala ya tafa’ul (mwingiliano) au ni sehemu ya marhala ya kushika utawala? Tunatarajia ufafanuzi na maelezo ya kina kama tulivyozoea.

Jibu:

Wa Alaykum As-Salaam wa Rahmatullahi wa Barakatuh.

Kutafuta nusra hufanyika mwishoni mwa marhala ya tafa’ul (mwingiliano). Ikiwa wenye nguvu (ahlul quwwah) wataitikia na wakawa na uwezo wa kuleta mabadiliko, basi marhala ya tatu itakuwa imekaribia kwa idhini ya Allah. Tumeifafanua masuala haya katika vitabu vyetu, hususan kitabu cha "Mbinu" (Al-Manhaj), na hapa kuna baadhi ya mambo ya kufafanua:

1- Mtume (saw) alianza kutafuta nusra wakati wa marhala ya tafa’ul. Abu Talib alipofariki, jamii ya Makka ilikuwa imeganda na kufungwa mbele ya Mtume (saw). Kwa kifo cha Abu Talib, maudhi ya Maquraishi kwa Mtume yalizidi kiwango ambacho hawakuthubutu kukifanya wakati wa uhai wa ami yake Abu Talib, hivyo ulinzi kwa Mtume ukawa dhaifu kuliko siku za Abu Talib. Allah akamfunulia wahyi ajitangaze kwa makabila ya Kiarabu ili kutafuta ulinzi na nusra yao, ili aweze kufikisha kile alichotumwa nacho kutoka kwa Allah huku akiwa katika amani na ulinzi. Ibn Kathir ameeleza katika As-Sira kutoka kwa Ali bin Abi Talib akisema: "Allah alipomwamrisha Mtume wake ajitangaze kwa makabila ya Kiarabu, alitoka nami nikiwa pamoja naye na Abu Bakr mpaka tukaenda kwenye mkusanyiko miongoni mwa mikusanyiko ya Waarabu." Pia, Ibn Kathir amepokea kutoka kwa Ibn Abbas, kutoka kwa Al-Abbas akisema: Mtume (saw) aliniambia:

«لا أرى لي عندك ولا عند أخـيك مَنَعَة، فهل أنت مخـرجي إلى السوق غداً حتى نقرّ في منازل قبائل النـاس -وكانت مجمع العرب- قال: فقلت هذه كِنْدَة وَلَفُّها، وهي أفضل من يَحُجُّ من اليمن، وهذه منازل بكر بن وائل، وهذه منازل بني عامر بن صعصعة، فاختر لنفسك، قال: فبدأ بكندة فأتاهم»

"Sioni kwako wala kwa ndugu yako ulinzi (wa kunitosha), je, utanitoa kwenda sokoni kesho ili tukaweke kambi katika makazi ya makabila ya watu – na palikuwa ni mkusanyiko wa Waarabu – (Abbas) akasema: Nikasema: Hawa ni Kinda na washirika wao, nao ni bora zaidi miongoni mwa wanaohiji kutoka Yemen, na haya ni makazi ya Bakr bin Wa'il, na haya ni makazi ya Bani 'Amir bin Sa'sa'ah, basi jichagulie mwenyewe. Akasema: Akaanza na Kinda na akawajia."

2- Ilikuwa wazi kwa wenye nguvu (makabila) katika wakati huo ambao Mtume (saw) alikuwa akitafuta nusra yao, kwamba walichokuwa wakitakiwa ni kumlinda Mtume (saw) na kumwezesha kusimamisha chombo (dola) miongoni mwao ambacho kitatekeleza hukumu za Allah (swt). Yaani, walikuwa wakielewa kwa uwazi kabisa kuwa nusra ni kwa ajili ya kusimamisha dola inayotawala na kupigana Jihadi... Ndiyo maana Bani 'Amir bin Sa'sa'ah, Mtume (saw) alipoomba nusra yao, walisema: "Unaonaje ikiwa tutakupa baia (kiapo) katika jambo lako hili, kisha Allah akakupa ushindi dhidi ya wanaokupinga, je, tutakuwa na mamlaka baada yako? Akasema: Mamlaka ni ya Allah, huyaweka pale atakapo. Akasema: Akamwambia: Je, shingo zetu ziwe shabaha (za mishale) kwa Waarabu kwa ajili yako, kisha Allah akikupa ushindi mamlaka yawe kwa wengine! Hatuna haja na jambo lako; wakakataa kwake." Hii ina maana walijua kuwa nusra ni ya kusimamisha dola, hivyo walitaka wawe watawala baada ya Mtume (saw). Hali kadhalika Bani Shaiban walimwambia Mtume (saw) alipoomba nusra yao: "Sisi tumekaa kati ya vyanzo viwili vya maji. Mtume (saw) akauliza: «Ni nini hivi vyanzo viwili?» Akasema: Mito ya Kisra (Uajemi) na maji ya Waarabu. Sisi tumewekewa ahadi na Kisra kwamba tusizushe jambo jipya wala tusiwape hifadhi wazushi. Na mimi naona jambo hili unalolingania ni miongoni mwa mambo yanayochukiwa na wafalme. Ikiwa unapenda tukupe hifadhi na kukunusuru kwa upande wa maji ya Waarabu, tutafanya hivyo. Mtume (saw) akasema:

«ما أسأتم في الرد إذ أفصحتم بالصدق، وإن دين الله لن ينصره إلا من أحاطه من جميع جوانبه»

"Hamkukosea katika jibu lenu mlipoeleza ukweli kwa wazi, na hakika dini ya Allah hainusuriwi isipokuwa na yule atakayeilinda (itaizunguka) kutoka pande zake zote."

Basi walikuwa wakitambua kuwa nusra inamaanisha utawala na Jihadi dhidi ya Waarabu na wasio Waarabu (Maajemi), hivyo walikubali kupigana na Waarabu, lakini si Waajemi (Mafursi).

3- Kisha Allah (swt) alipoamua jambo lake, pakawa na Baia ya Pili ya Aqaba ambayo ilikuwa ni nusra ya kusimamisha dola kule Madina, na baada ya hapo ikaingia marhala ya tatu ya kusimamisha dola.

4- Ni wazi kutokana na yote haya kuwa kutafuta nusra kulikuwa kabla ya marhala ya tatu, yaani katika marhala ya tafa’ul.

5- Na hivi ndivyo chama (al-hizb) kilivyofanya kilipoanza vitendo vya kutafuta nusra katika miaka ya sitini ya karne iliyopita na bado kinaendelea navyo. Tunamuomba Allah (swt) Alikirimu hili Umma kwa kutoa Ansari watakaorejesha sira ya Ansari wa kwanza, ili isimame Dola ya Kiislamu, Dola ya Khilafah Rashidah, na ipepee juu kileleni bendera ya Al-Uqab, bendera ya Mtume wa Allah (saw). Na siku hiyo, waumini watafurahia nusra ya Allah...

Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu al-Rashtah

Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir kwenye Facebook

Kiungo cha jibu kutoka kwenye tovuti ya Amir

Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir kwenye Google Plus

Share Article

Share this article with your network