Swali:
Waziri wa Ulinzi wa Marekani wakati wa ziara yake nchini Japan mnamo tarehe 16-17/9/2012 alieleza kuwa "mzozo huu kati ya China na Japan kuhusu suala la visiwa unaweza kutanuka." (AFP 17/9/2012). Alisema: "Nina wasiwasi kwa sababu nchi hizi zinapoingia katika uchokozaji dhidi ya kila mmoja kuhusu visiwa hivi vinavyozozaniwa, jambo hilo litaongeza uwezekano wa kuchukuliwa kwa uamuzi mbaya kutoka upande mmoja au mwingine ambao unaweza kupelekea ghasia na kusababisha mzozo." (Chanzo hicho hicho). Hii ilikuwa baada ya Japan kutangaza mnamo 11/9/2012 kuwa imenunua visiwa vitatu kutoka kwa familia moja ya Kijapani katika fungu la visiwa kwenye Bahari ya China Mashariki ambavyo inadai kuwa ni milki yake na kuviita jina la Senkaku. Jambo hilo lilizua mvutano kati yake na China ambayo inadai kuwa visiwa hivyo ni milki yake na kuviita jina la Diaoyu. China ilituma meli mbili za kivita kuelekea visiwa hivyo...
Swali ni: Kwa nini Japan imechukua hatua hii katika kipindi hiki? Je, Marekani ina dori katika mzozo huu? Na je, inawezekana hali ikafikia kuzuka kwa vita kati yao au ni dhoruba itakayotulia?
Jibu:
Jibu la swali hili linabainika kwa kupitia mambo yafuatayo:
1- China inadai kuwa visiwa hivi vitatu kati ya visiwa vitano ni milki yake ambavyo Japan ilivikalia kwa mabavu katika vita vilivyotokea kati yao miaka ya 1894-1895. Wamarekani walivikalia katika Vita vya Pili vya Dunia baada ya kuwashinda Wajapani, ambapo waliunganisha usimamizi wa visiwa hivi na kisiwa cha Kijapani cha Okinawa ambacho walikikalia katika vita hivyo na kuanzisha kambi kubwa ya Marekani. Hata hivyo, walivikabidhi visiwa hivyo kwa Wajapani mnamo mwaka 1972 kupitia kuvikabidhi kwa familia ya Kijapani iliyovinunua kutoka kwa familia nyingine ya Kijapani iliyokuwa ikivimiliki tangu miaka ya tisini ya karne ya kumi na tisa. Eneo la visiwa hivi vyote katika fungu hilo ni takriban kilomita za mraba 6, na baadhi ni miamba tu iliyozungukwa na maji ya bahari, na havina wakazi. Lakini vina umuhimu wa kimkakati katika Bahari ya China Mashariki; viko karibu na njia za usafiri wa baharini, kando na kwamba maji yake yamesheheni utajiri wa samaki, na kuna ripoti kuhusu uwezekano wa kuwepo kwa akiba kubwa ya mafuta na gesi.
Suala la visiwa hivi limeibuliwa kati ya nchi hizo mbili mara kadhaa, na mara ya mwisho ilikuwa mwaka 2010 ambapo mvutano kama huu ulitokea.
2- Marekani iliitaarifu Japan rasmi mnamo 29/6/2012 kuwa inataka kueneza ndege "12" za aina ya Osprey katika kambi ya Marekani ya Futenma kwenye kisiwa cha Kijapani cha Okinawa, na kwamba uenezaji wa ndege hizi utafanyika mwishoni mwa mwezi huu (MENA - Masress - Al-Mashhad 1.7.2012). Vikosi vya Marekani vilitangaza kuwa moja ya ndege hizi itaanza safari yake mnamo 21/9/2012 (Arabic news CN world 20.9.2012). Haya yote yalikuja katika hali ya maandamano ya Wajapani dhidi ya uwepo wa Marekani, ambapo uwepo huu umeanza kutazamwa na Wajapani kwa jicho la kutoridhika, na baadhi yao wanadai kuondoka kwa Wamarekani nchini mwao. Kuna wanajeshi wa Marekani 47,000 nchini humo kwa mujibu wa mkataba wa usalama wa pande mbili uliotiwa saini mwaka 1960 na serikali ya Japan chini ya ukaliaji wa Marekani. Huu ni mtindo wa Marekani inayoutumia kubadilisha sura ya ukaliaji wake na kubakisha ushawishi wake katika nchi inayoinyakua, kama ilivyofanya nchini Iraq ilipofanya mkataba wa usalama na serikali ya Maliki mwaka 2008 chini ya ukaliaji rasmi wa Marekani, na pia mkataba wa usalama wa kimkakati na serikali ya Afghanistan uliotiwa saini miezi michache iliyopita chini ya ukaliaji wa Marekani ambao bado unaendelea huko.
Katika mazingira haya ya Wajapani kutoridhika na uwepo wa Marekani nchini mwao, Marekani inatangaza kueneza ndege hizo! Kawaida, tangazo hili lingezidisha upinzani wa Wajapani... Marekani ikaona kuwa kutengeneza mazingira ya uchokozaji na China na kuonyesha kuwa vita na China viko karibu kutawafanya Wajapani wakubali uenezaji wa ndege hizi, na kupunguza maandamano yao dhidi ya uwepo wa Marekani, kwa kisingizio kuwa Marekani inasimama na Japan dhidi ya China! Na hicho ndicho kilichotokea, kwani kwa makubaliano na serikali ya Japan iliyofungamana kwa karibu na siasa za Marekani, suala la visiwa liliibuliwa, na kwamba ni mali ya Japan ingawa vinazozaniwa na China. Jambo hilo lilipelekea kuichokoza China na kutengeneza mazingira ya upotoshaji ya mgongano nayo, na kwamba vita vinaweza kuzuka. Hii ndiyo inayotuliza upinzani wa Wajapani dhidi ya uwepo wa Marekani nchini mwao kama msaidizi wao dhidi ya China.
3- Kwa hivyo, kuibuliwa kwa suala la visiwa sasa, baada ya tangazo la kueneza ndege, ni hatua ya makusudi iliyopangwa na serikali ya Japan kwa mipango ya Marekani ili kuwachokoza Wachina ili kuonyesha mvutano kati ya Japan na China. Hivyo Wajapani waiogope China na kusalimu amri kwa mipango ya Marekani inayotekelezwa katika eneo lao. Ndiyo maana matamshi ya viongozi wa Marekani yalikuwa yakiashiria ukaribu wa makabiliano au ukaribu wa utangulizi wake! Waziri wa Ulinzi wa Marekani alisema wakati wa ziara yake nchini Japan mnamo tarehe 16-17/9/2012 "kwamba mzozo huu unaweza kutanuka." (AFP 17/9/2012). Na akasema: "Nina wasiwasi kwa sababu nchi hizi zinapoingia katika uchokozaji dhidi ya kila mmoja kuhusu visiwa hivi vinavyozozaniwa, jambo hilo litaongeza uwezekano wa kuchukuliwa kwa uamuzi mbaya... ambao unaweza kupelekea ghasia." (Chanzo hicho hicho). Aliziomba "pande zote mbili kuwa na utulivu na kujizuia." Waziri wa Ulinzi wa Marekani anachora picha kana kwamba vita viko karibu kuanza kati ya nchi hizo mbili, ili kutumikia malengo ya Marekani. Alikumbusha kuhusu mikataba ya usalama kati ya nchi yake na Japan ili kuonyesha kuwa Marekani iko tayari kusimama upande wa Japan, akisema: "Tunaheshimu majukumu yetu yanayohusiana na mikataba ambayo imekuwepo tangu muda mrefu na haitabadilika." (Chanzo kilichotajwa). Mashambulizi haya yote ya maneno yalikuwa wakati Waziri wa Ulinzi wa Marekani akisisitiza katika mazungumzo yake na serikali ya Japan kuhusu mipango ya Marekani ya kueneza ndege (12) za aina ya Osprey katika kambi ya Marekani huko Okinawa huku kukiwa na upinzani mkali kutoka kwa wakazi wa kisiwa hicho cha kusini kama ilivyoelezwa na shirika la habari la Ufaransa (AFP) mnamo 16/9/2012.
4- Mwitikio wa China ulikuwa wa hisia, ikaruhusu maandamano makubwa mitaani katika miji yake kupinga hatua ya Japan kuelekea visiwa hivyo ambavyo havikuwa vimekaliwa na serikali ya Japan rasmi. Lakini ilipotangaza kununua vitatu kati yake kutoka kwa familia ya Kijapani ili viwe milki ya serikali ya Japan, mamlaka yakawa rasmi ni ya serikali ya Japan, jambo ambalo lilionekana kama imeviunganisha tena na Japan. Jambo hili liliichokoza China na kuifanya isogeze baadhi ya meli zake zinazolinda maji yake katika Bahari ya China Mashariki kuelekea visiwa hivyo. Waziri Mkuu wa China Wen Jiabao alitoa tamko la kihisia akisema: "Zama za kudhalilishwa kwa Wachina zimepita na hazitarudi." (AFP 17/9/2012). Wachina wanakumbuka udhalilishaji walioupata kutoka kwa Wajapani, iwe ni katika vita vilivyozuka kati yao katika miaka ya tisini ya karne ya kumi na tisa au chini ya ukaliaji wa moja kwa moja wa Kijapani nchini China katika miaka ya thelathini ya karne ya ishirini ambao uliendelea mpaka kushindwa kwa Japan katika Vita vya Pili vya Dunia mbele ya Marekani, ikajitoa China na kuiacha kwa Wamarekani. Hivyo, fundo la kushindwa na kudhalilishwa mbele ya Wajapani bado ni kichocheo kwao. Hivyo kuibua jambo kama hili kwa Wachina ni rahisi sana.
5- Hivyo basi, Marekani imepiga ndege wawili kwa jiwe moja kwa kuisukuma Japan kudai visiwa hivyo... Kwa upande mmoja, imetia sumu mazingira kati ya China na Japan ili hitaji la Japan kwa uwepo wa Marekani liendelee kuwepo na likubalike kwa watu nchini Japan. Kwa upande mwingine, Marekani inataka kuishughulisha China daima na masuala ya kikanda yenye mvutano ili kuzuia matamanio yoyote ya China katika siasa za kimataifa isipokuwa ndani ya mipaka ya eneo lake tu. Yaani, kuendelea kwa Marekani katika mipango yake ya kuizingira China na kuzuia ushawishi wake na mipango yake ya kuimarisha hadhi yake ya kikanda hadi kufikia hadhi ya kimataifa, hasa dhidi ya Marekani. Hivyo basi, mipango ya Marekani katika eneo la kikanda linaloizunguka China ni ya kufikia lengo hili. Marekani ilishatangaza mipango yake ya kuimarisha uwepo wake katika eneo la Asia/Pasifiki ndani ya mkakati mpya ambapo waziri wake wa ulinzi Leon Panetta alitangaza mnamo 1/6/2012 kuhusu mkakati huu kwa kutuma manowari sita za kubeba ndege na kuhamisha 60% ya meli zake za kivita kuelekea eneo hili katika miaka ijayo hadi mwaka 2020. Marekani inafanya kazi ya kuchochea migogoro yote dhidi ya China: katika eneo la Bahari ya China Mashariki kama ilivyotokea na Japan, na pia katika Bahari ya China Kusini ambapo kuna mvutano kati ya China na Ufilipino kuhusu visiwa na uvuvi, na pia kati ya China na Vietnam kuhusu mzozo wa visiwa ambapo Wachina waliwafukuza Wavietnam hapo mwaka 1988. Haya yote ni ili China ibaki imetingwa katika maeneo haya mawili!
Vilevile, Marekani inasimama nyuma ya nchi hizo katika maeneo hayo mawili isipokuwa Korea Kaskazini, na kuzichochea dhidi ya China ili China ibaki, kama tulivyosema, imeshughulika katika eneo lake pasina kulivuka. Hasa ikizingatiwa kuwa Marekani ina udhibiti kamili juu ya nyingi ya nchi hizi kama Korea Kusini katika Bahari ya China Mashariki, na Ufilipino katika Bahari ya China Kusini ambapo kuna kambi za Marekani, na Indonesia inayofuata siasa za Marekani, kisha Japan inayofuata mwelekeo wa Marekani.
6- Hii ni kuhusu dori ya Marekani katika suala hili na kuibuliwa kwa suala la visiwa wakati huu. Ama kuhusu uwezekano wa uchokozaji huu kufikia kuzuka kwa vita kati ya China na Japan kuhusu visiwa hivyo, jambo hilo halitarajiwi, angalau katika siku za karibu. Kuna visiwa vikubwa na muhimu zaidi kama kisiwa cha Taiwan (Formosa zamani) ambavyo China haikuvianzishia vita, huku ikijulikana kuwa Marekani ilikubaliana nayo kufanya kazi ya kukirudisha kwake kwa amani. Pia kuna mizozo na Ufilipino, Vietnam na nyinginezo kuhusu visiwa katika Bahari ya China Kusini bila kuingia vitani nazo, la sivyo ingejifungulia mlango ambao isingeweza kuufunga! China haitayadhulumu maslahi yake makubwa na Japan kwa ajili ya visiwa hivi ambapo kiasi cha biashara kati yao ni takriban dola bilioni 300 kwa mwaka. Makampuni ya Kijapani yanayofanya kazi nchini China yanaajiri zaidi ya wafanyakazi milioni 20 wa Kichina, na China inafaidika na teknolojia na utaalamu wa Kijapani. Kwa hiyo, si kwa maslahi ya China kuanzisha vita na Japan kwa ajili ya visiwa hivyo. Waziri wa Ulinzi wa China Liang Guanglie alieleza katika mkutano wake na Waziri wa Ulinzi wa Marekani mnamo 18/9/2012 akijibu swali la waandishi wa habari kama Beijing inakusudia kutumia nguvu akisema: "Bado tunatarajia suluhisho la amani la mazungumzo." (AFP 18/9/2012), jambo linaloashiria kuwa ni vigumu kwa China kuanzisha vita na Japan kwa ajili ya visiwa hivi.
7- China ikibaki imetingwa na masuala ya eneo lake, basi Marekani itakuwa imefanikiwa kuiondoa China katika siasa za kimataifa. Lakini lililo sahihi ni kwa China kufanya tishio la kweli kwa siasa za Marekani katika ngazi ya ulimwengu, na kuitengenezea matatizo yanayotishia maslahi yake. Yaani China itekeleze siasa ya tishio la kweli kwa siasa za Marekani katika kila eneo la ulimwengu, na kisha itakuwa rahisi kwa China kuwa na athari katika eneo lake la kikanda, hasa katika Bahari ya China Mashariki na Kusini.
Lakini kinachoonekana katika siasa za China ni kwamba bado inadanganyika kuwa kuingilia kwake katika siasa za kimataifa kwa namna yenye athari si kwa maslahi yake, bali inajali tu eneo lake la kikanda... bila kutambua kuwa haitaweza kutawala kikanda ikiwa haina malengo ya kisiasa ya kimataifa kwa kuitengenezea Marekani matatizo ili kuilazimisha kupunguza usumbufu kwa China katika eneo lake. Ikiwa China haitafuata siasa hii, basi itabaki mahali hapo hapo, na Marekani itaendelea kuitengenezea mvutano wa kikanda mmoja baada ya mwingine.
Vyovyote iwavyo, huenda historia ikajirudia! Khilafah itasimama kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na harakati zake za kisiasa za kimataifa "kabla ya harakati zake za kijeshi" katika kuiondoa Magharibi na Marekani kutoka eneo la Kiislamu, itakuwa mfano wa kuigwa na China katika kuondoa ushawishi wa Marekani uliyoizunguka China. Hivyo harakati za kisiasa za Khilafah zitaihakikishia China usalama kwa njia isiyo ya moja kwa moja, kama ambavyo Khilafah ilishawahi kuipa usalama China kwa njia ya moja kwa moja hapo awali. Vyanzo vya Kichina na Kiislamu vimeeleza kuwa dola ya China iliomba msaada kutoka kwa Dola ya Khilafah ya Kiislamu wakati wa utawala wa Khalifa wa Kiabbasi Abu Ja'far al-Mansur ili kuisaidia kuzima machafuko yaliyokuwa yameenea nchini humo mnamo mwaka 756 M. Khalifa alituma jeshi la wanajeshi Waislamu 4,000 na hali ikatulia huko, wakaleta usalama kwa watu wa nchi hiyo. Wachina walivutiwa na maadili ya wanajeshi Waislamu na mwenendo wao mwema, wakawaomba wabaki nao. Wanajeshi wale Waislamu walibaki huko wakiwa na sifa ya wabeba Da'wah, wakieneza Uislamu, uongofu na nuru miongoni mwa watu wa China. Na wajukuu zao leo ni Waislamu wa Turkestan Mashariki ambao China inawadhulumu hivi sasa badala ya kuwalipa fadhila!! Je, China italielewa jambo hili, na kukomesha ukaliaji wake wa Turkestan bila ya kukanusha fadhila?!
4 Dhul-Qa'dah 1433 H Alhamisi, 20 Septemba 2012 M