Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Khilaf al-Awla (Kinyume na Lililo Bora)

October 11, 2015
4689

** (Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata bin Khalil Abu al-Rashtah, Amiri wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Wageni kwenye Ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi")**

Kwa Numan Abo Ali

Swali:

Assalam Alaykum, je, inachukuliwa kuwa kitendo cha Mtume ﷺ kwenda kinyume na lililo bora (khilaf al-awla) ni sehemu ya ijtihadi au ni jambo jengine? Naomba ufafanuzi, Mwenyezi Mungu akubariki, aongoze hatua zako na kukunusuru.

Jibu:

Wa Alaykum Salam wa Rahmatullahi wa Barakatuh,

Labda katika swali lako unaashiria kile kilichokuja katika kitabu cha Ash-Shakhsiyyah al-Islamiyyah (Shakhsiya ya Kiislamu) Juzuu ya Kwanza kwamba ijtihadi haijuzu kwa haki ya Mtume ﷺ, bali inajuzu kwake kufanya kinyume na lililo bora (khilaf al-awla), na hivyo ukauliza tofauti kati ya ijtihadi na khilaf al-awla.

Ili kujibu swali hili, ni lazima kujua uhalisia wa "Ijtihadi" na uhalisia wa "Khilaf al-Awla"...

Kwanza:

Ijtihadi kilugha ni kutumia juhudi zote katika kufikia jambo miongoni mwa mambo yanayohitaji taabu na mashaka. Ama katika istilahi ya wanachuoni wa Usul al-Fiqh, imehusishwa na kutumia juhudi zote katika kutafuta dhana (itakadi yenye nguvu) katika kitu miongoni mwa hukumu za kisheria kwa njia ambayo mtu anahisi ndani ya nafsi yake kutoweza kufanya zaidi ya hapo.

Hii ina maana kwamba hukumu ya kisheria katika suala fulani inakuwa haijulikani kwa mujtahidi, na hivyo anafanya ijtihadi ili kuijua hukumu ya kisheria ndani yake. Anatumia juhudi katika kuelewa uhalisia wa suala hilo, anatafuta dalili za kisheria zinazohusiana nalo, anatumia uwezo wake wote katika kuzisoma na kutoa rai (istimbat) ambayo ina nguvu katika dhana yake kuwa ndiyo hukumu ya kisheria katika suala hilo.

Ijtihadi kwa maana hii haisihi kwa haki ya Mtume ﷺ kutokana na aya za wazi zinazoonyesha kuwa kila anachofikisha Mtume ﷺ kinatokana na wahyi:

قُلْ إِنَّمَا أُنْذِرُكُمْ بِالْوَحْيِ

"Sema: Hakika mimi nakuonyeni kwa Wahyi tu." (QS Al-Anbiya [21]: 45)

إِنْ أَتَّبِعُ إِلَّا مَا يُوحَى إِلَيَّ

"Mimi sifuati ila yanayofunuliwa kwangu (kwa Wahyi)." (QS Al-Ahqaf [46]: 9)

وَمَا يَنْطِقُ عَنِ الْهَوَى * إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَى

"Wala hazungumzi kwa matamanio. Hayo si chochote ila ni Wahyi uliofunuliwa." (QS An-Najm [53]: 3-4)

Hii ina maana kwamba Mtume ﷺ anafikisha hukumu za kisheria kutoka kwa Wahyi na si kutokana na ijtihadi yake ﷺ.

Kadhalika, mujtahidi anaweza kukosea; akipatia ana thawabu mbili na akikosea ana thawabu moja. Kama ilivyokuja katika hadithi ya Mtume ﷺ:

إِذَا حَكَمَ الْحَاكِمُ فَاجْتَهَدَ ثُمَّ أَصَابَ، فَلَهُ أَجْرَانِ، وَإِذَا حَكَمَ فَاجْتَهَدَ ثُمَّ أَخْطَأَ، فَلَهُ أَجْرٌ

"Mwamuzi anapohukumu na akajitahidi kisha akapatia, basi ana ujira miwili; na anapohukumu na akajitahidi kisha akakosea, basi ana ujira mmoja." (Imepokelewa na Bukhari na Muslim)

Na Mtume ﷺ ni Ma’sum (amekingwa) na makosa katika sheria, kwa hiyo, haijuzu kwake ﷺ kufanya ijtihadi kabisa. Kwani ijtihadi ndani yake mna kukosea na kupatia, wakati kila anachofikisha Mtume ﷺ katika hukumu kwa kauli yake, kitendo chake au kunyamanya kwake ni wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu pekee.

Pia Mtume ﷺ alikuwa akisubiri wahyi katika hukumu nyingi licha ya kuwepo kwa hitaji kubwa la kubainisha hukumu ya Mwenyezi Mungu. Kama ijtihadi ingejuzu kwake asingelichelewesha hukumu bali angefanya ijtihadi. Na kwa kuwa alikuwa akichelewesha hukumu mpaka wahyi ushuke, basi hii inafahamisha kuwa hakufanya ijtihadi, na inaonyesha kuwa haijuzu kwake kufanya ijtihadi, kwani kama ingejuzu asingelichelewesha hukumu pamoja na hitaji lake.

Hivyo basi, kila kilichokuja kutoka kwa Mtume ﷺ ni kwa njia ya wahyi na si kwa ijtihadi ya Mtume ﷺ.

Pili:

Ama Khilaf al-Awla (Kinyume na lililo bora zaidi), maana yake ni kuwa hukumu ya kisheria inakuwa inajulikana lakini imekuja kama "mubah" (hiari), lakini baadhi ya vitendo vyake ni bora kuliko vyengine. Au hukumu ya kisheria ni "mandub" (inayopendekezwa) lakini baadhi ya vitendo vyake ni bora kuliko vyengine.

Mfano: Ni mubah kwa mtu kuishi mijini au kuishi vijijini, lakini kuishi mijini ni bora zaidi kuliko kuishi vijijini kwa yule anayeshughulikia mambo ya utawala na kuwawajibisha watawala. Ikiwa ataishi kijijini, atakuwa amefanya kinyume na lililo bora (khilaf al-awla).

Vilevile, kutoa sadaka kwa siri au dhahiri ni jambo lililopendekezwa (mandub), lakini kuitoa kwa siri ni bora kuliko kuitoa dhahiri. Akitoa hadharani, atakuwa amefanya kinyume na lililo bora.

Kwa maana hii ya khilaf al-awla, Mtume ﷺ inajuzu kwake kufanya kitendo ambacho ni kinyume na lililo bora. Na hakika alishafanya kitendo ambacho ni kinyume na lililo bora na Mwenyezi Mungu akamkumbusha (akamtia adabu) juu ya hilo kwa kauli yake Subhanahu wa Ta’ala:

عَفَا اللَّهُ عَنْكَ لِمَ أَذِنْتَ لَهُمْ حَتَّى يَتَبَيَّنَ لَكَ الَّذِينَ صَدَقُوا وَتَعْلَمَ الْكَاذِبِينَ

"Mwenyezi Mungu amekusamehe! Kwa nini ukawapa ruhusa mpaka wakubainikie wale walio sema kweli na uwajue waongo?" (QS At-Tawbah [9]: 43)

Hii aya haionyeshi ijtihadi, kwa sababu hukumu ya kwamba inajuzu kwa Mtume ﷺ kutoa ruhusa kwa amtakaye ilishashuka kabla ya aya hii. Kwani imekuja katika Surat An-Nur, Mwenyezi Mungu Amesema:

فَإِذَا اسْتَأْذَنُوكَ لِبَعْضِ شَأْنِهِمْ فَأْذَنْ لِمَنْ شِئْتَ مِنْهُمْ

"Basi wakikuomba ruhusa kwa baadhi ya mambo yao, mpe ruhusa unaye mtaka miongoni mwao." (QS An-Nur [24]: 62)

Na sura hii ilishuka baada ya Surat Al-Hashr katika vita vya Khandaq, wakati aya ya: “Mwenyezi Mungu amekusamehe!” ilikuja katika Surat At-Tawbah na ikashuka kuhusiana na Vita vya Tabuk katika mwaka wa tisa wa Hijra. Hivyo hukumu ilikuwa inajulikana na aya ya An-Nur ni ya wazi kuonyesha kuwa inajuzu kwa Mtume ﷺ kuwapa ruhusa.

Lakini katika tukio lile ambalo ilishuka aya ya At-Tawbah, nalo ni Vita vya Tabuk na kutayarisha jeshi la dhiki (Jaysh al-Usrah), ilikuwa bora zaidi kwa Mtume ﷺ kutowapa ruhusa wanafiki kubaki nyuma. Alipowapa ruhusa katika tukio lile mahususi, Mwenyezi Mungu alimlaumu kwa kitendo hicho, yaani alimlaumu kwa kufanya kile ambacho kilikuwa kinyume na lililo bora zaidi. Aya hii si marekebisho ya ijtihadi, wala si kuweka sheria ya hukumu inayopingana na hukumu ambayo Mtume ﷺ aliifanyia ijtihadi katika tukio lile lile, bali ni lawama (kumbusho) kwa lile lililo kinyume na lililo bora zaidi.

Tatu:

Kulingana na hayo, haijuzu kwa haki ya Mtume ﷺ kuwa ni mujtahidi, bali yeye ni wahyi unaofunuliwa kwake kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Na wahyi huu ima ni kwa tamshi na maana nao ni Qur’ani Tukufu, au ni kwa maana pekee na Mtume ﷺ anaielezea ima kwa tamshi kutoka kwake, au kwa kunyamaza kwake kuashiria hukumu, au kwa kitendo chake na yote hayo ni Sunnah.

Hivi ndivyo inavyobainika tofauti kati ya ijtihadi na khilaf al-awla, na kwamba haijuzu kwa haki ya Mtume ﷺ kufanya ijtihadi kwa sababu yeye ﷺ ni ma’sum (amekingwa) na makosa, lakini inajuzu kwake ﷺ kufanya kitendo ambacho ni kinyume na lililo bora kwa sababu kitendo hicho si kosa.

Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu al-Rashtah

Link ya jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amiri kwenye Facebook

Link ya jibu kutoka kwenye tovuti ya Amiri

Link ya jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amiri kwenye Google Plus

Share Article

Share this article with your network