Jibu la Swali
Swali:
Viongozi wa mapinduzi nchini Niger walitangaza jioni ya Jumapili 2023/8/13 (kwamba wana nia ya kumshitaki Rais aliyeondolewa madarakani Mohamed Bazoum kwa tuhuma za "uhaini mkubwa" na "kuhujumu usalama wa nchi",.. na viongozi wa mapinduzi walikariri katika taarifa yao kulaani vikwazo vilivyowekwa na Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS)... Al Jazeera 2023/8/14). Jenerali Abdourahamane Tchiani, mkuu wa walinzi wa rais nchini Niger, alikuwa ametangaza kupitia televisheni rasmi ya taifa mnamo 2023/7/28 akijitangaza kuwa rais wa mpito wa nchi hiyo, siku mbili baada ya wanajeshi wake katika kikosi cha walinzi wa rais, waliojiita "Baraza la Kitaifa la Kulinda nchi", kutangaza kumpindua Rais wa nchi hiyo Mohamed Bazoum na kumzingira katika makazi yake. Je, operesheni hii ya mapinduzi ilikuwa ni suala la ndani linalohusiana na mzozo kati ya nguvu zenye ushawishi nchini humo, au kuna nguvu za nje zinazohusika na kwamba operesheni hiyo ni sehemu ya mzozo wa kimataifa? Kisha, inaelewekaje kuhusiana na tuhuma za uhaini dhidi yake wakati bado hajamatwa bali anawasiliana na maafisa wa nje?
Jibu:
Ili picha iwe wazi, tunapitia mambo yafuatayo:
Kwanza: Usuli wa mapinduzi na watu walioyafanya:
Kanali Meja Amadou Abdramane, akiwa amezungukwa na wanajeshi tisa waliovalia sare za kijeshi, alitangaza akisema: ("Sisi, vikosi vya ulinzi na usalama vilivyokusanyika katika Baraza la Kitaifa la Kulinda nchi, tumeamua kukomesha utawala mnaoujua. Hii inatokana na kuendelea kuzorota kwa hali ya usalama na usimamizi mbovu wa kiuchumi na kijamii", na akawaomba "washirika wote wa nje wasiingilie kati" na kutangaza "marufuku ya kutotoka nje kuanzia saa nne usiku hadi saa kumi na moja alfajiri katika ardhi yote hadi ilani nyingine"... Agence France-Presse 2023/7/26).
Siku iliyofuata, jeshi lilitangaza kuunga mkono mapinduzi hayo baada ya kusita katika siku ya kwanza. Ukurasa rasmi wa Kifaransa "France 24" mnamo 2023/7/27 ulinakili tangazo la jeshi la Niger la utiifu kwa vikosi vya ulinzi na usalama vilivyomng'oa Rais Mohamed Bazoum ili "kuepuka mapigano ndani ya vikosi vya jeshi". Ukurasa huo uliongeza: "Taarifa iliyotiwa saini na mkuu wa majeshi, Abdu Sidikou Issa, ilizungumzia juu ya 'kuunga mkono tangazo la wanajeshi la kukomesha utawala wa Bazoum'". Inaonekana kwamba uongozi wa jeshi, baada ya kusita kwa siku moja, uligundua kuwa hauwezi kufelisha mapinduzi hayo, hivyo ukaunga mkono.
Shirika la habari la Al-Hurra liliripoti mnamo 2023/7/29 kwamba "Tchiani alikuwa mtiifu kwa Rais wa zamani Mahamadou Issoufou, aliyemteua kuwa mkuu wa walinzi wa rais wakati wa vipindi vyake viwili vya urais kuanzia 2011-2021". Jarida la Kifaransa la Jeune Afrique, linalojikita katika masuala ya Afrika, lilitaja kuwa "walinzi wa rais walikuwa wakipewa kipaumbele kikubwa na Rais Mahamadou Issoufou, ambaye aliwapa mamlaka na uwezo wote ili kuzuia kutokea kwa mapinduzi". Aliongeza kuwa "inasemekana kuhusu Jenerali Tchiani kwamba ni mtu mkali na anayeogopwa na jeshi". Inafahamika kutokana na hayo kwamba Rais wa zamani alikuwa akiliogopa jeshi kwani linatawaliwa na wafuasi wa Ufaransa, ambayo ndiyo iliyoliasisi tangu ilipotoa uhuru wa kimaonyesho kwa Niger. Jaribio la mapinduzi lililofeli dhidi ya Issoufou mnamo 2015 lilitokea, na haiwezekani kutenga uwezekano kuwa wafuasi wa Ufaransa jeshini ndio waliofanya jaribio hilo. Hivyo basi, alimpandisha cheo Abdourahamane Tchiani na kuimarisha nguvu zake ili awe mlinzi wake dhidi ya mapinduzi yanayofanywa na mawakala wa Ufaransa kwa sababu mbalimbali.
Kumetokea mapinduzi manne yaliyofaulu na majaribio kadhaa ya mapinduzi yaliyofeli nchini Niger tangu kutangazwa kwa uhuru wake wa kimaonyesho kutoka kwa Ufaransa mwaka 1960. Mapinduzi ya mwisho yaliyofaulu kabla ya haya ya sasa yalikuwa mwaka 2010 yaliyofanywa na wanajeshi dhidi ya Rais Mamadou Tandja, wakala wa Ufaransa, na wakatangaza kuundwa kwa "Baraza Kuu la Kurejesha Demokrasia", na kumteua rais wake aliyeitwa Salou Djibo, mkuu wa kitengo cha msaada katika mji mkuu Niamey. Tulikuwa tumetoa jibu la swali kuhusiana na mapinduzi hayo mnamo 2010/2/20 ambapo tulisema: "Ishara za taarifa za Marekani kuhusu tukio la kuongeza muda wa muhula ni kuweka majukumu halisi kwa rais aliyeng'olewa Tandja na kuhalalisha mapinduzi. Vilevile, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani hakutoa wito wa kurejeshwa kwa rais huyo, wala kufanya mazungumzo kati ya waasi na rais aliyeng'olewa, bali alitoa wito wa kuandaliwa kwa uchaguzi mpya na kuundwa kwa serikali mpya. Hii inathibitisha kuwa Marekani ilikuwa nyuma ya mapinduzi hayo... Lakini ushawishi wa Ufaransa wa kila aina ulibaki, na bado kuna takriban Wafaransa 1,500 wanaoishi huko ili kulinda maslahi ya nyuklia ya Ufaransa, kwani Niger ni nchi ya tatu duniani kwa uzalishaji wa uranium. Hivyo basi, ni sehemu inayotamaniwa na Wamarekani ili kuitawala na kuondoa ushawishi wa Ufaransa kama ilivyo katika nchi nyingine za Afrika, ambazo nyingi ni nchi za Kiislamu na zenye utajiri mkubwa wa maliasili na vyanzo vya malighafi za kila aina, pamoja na vyanzo vya nishati. Kwa hiyo, imekuwa uwanja wa mzozo kati ya wakoloni wa Magharibi, Wazungu na Wamarekani."
Kweli, baada ya mapinduzi hayo kwa muda mfupi, miezi kadhaa baadaye, uchaguzi ulifanyika kulingana na matakwa ya Marekani mnamo mwaka 2011, ambapo alishinda rais wa chama cha Niger cha Demokrasia na Ujamaa, Mahamadou Issoufou, ambaye alikuwa rais wa nchi hiyo rasmi tangu 2011/4/7. Baada ya hapo, alijiuzulu uenyekiti wa chama na nafasi hiyo ikachukuliwa na Mohamed Bazoum, ambaye ni mmoja wa waasisi wa chama hicho tangu mwaka 1990 pamoja na Issoufou na rafiki yake wa karibu. Issoufou alimteua kuwa Waziri wa Nchi wa Mambo ya Nje, na kisha akamteua kuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais tangu mwaka 2015. Wakati Issoufou alipochaguliwa kwa muhula wa pili, alimteua Bazoum kuwa Waziri wa Nchi wa Mambo ya Ndani, Usalama wa Umma na Ugatuzi. Issoufou na Mohamed Bazoum walikuwa miongoni mwa wapinzani wa Rais Mamadou Tandja, na wakati Mamadou Tandja alipopinduliwa kwa mapinduzi ya kijeshi mnamo 2010/2/18, Issoufou na Bazoum walionyesha kuunga mkono mapinduzi hayo. Inafahamika kutokana na haya yote kuwa Issoufou na Bazoum ni mawakala wa Marekani.
Wakati Mahamadou Issoufou aliposhika urais kupitia uchaguzi kwa vipindi viwili kati ya mwaka 2011-2021, alionyesha ukaribu wake na Marekani, akairuhusu kuanzisha kambi mbili muhimu za kijeshi nchini Niger, moja mwaka 2014 na nyingine mwaka 2018, ambapo kuna zaidi ya wanajeshi elfu moja wa Marekani na ndege nyingi zisizo na rubani (drones). Tovuti ya Noon Post mnamo 2018/9/13 ilichapisha mada iliyotafsiriwa kuhusu kambi za Marekani nchini Niger, ikinukuu taarifa za Rais wa zamani Mahamadou Issoufou katika mahojiano na gazeti la The Guardian akisema: "Sipendi kutumia neno vikosi vya kigeni, kwa sababu vikosi vya Marekani ni vikosi rafiki.. ikifahamika kuwa vilikuja nchini kwa ombi letu. Na mara tu kazi yao itakapomalizika, wataondoka Niger." Pamoja na hayo, Issoufou alibakisha uhusiano wa nchi yake na ushirika na Ufaransa na hakuviondoa vikosi vya Ufaransa, bali alishiriki katika ushirika wa nchi za Sahel ulioasisiwa na kuongozwa na Ufaransa kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi mwaka 2014. Inaonekana kuwa hawezi kung'oa ushawishi wa Ufaransa nchini Niger kwa urahisi, hivyo alienda nayo sambamba hadi ushawishi wa Marekani uimarike, ambao aliuingiza nchini kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.
Wakati Mohamed Bazoum alipochaguliwa mnamo 2021/2/21 na kushika urais rasmi mnamo 2021/4/1 kumrithi Mahamadou Issoufou na kwa uungaji mkono wake, aliahidi kuendeleza sera ya Mahamadou Issoufou. Siku mbili kabla ya kuingizwa madarakani, jaribio la mapinduzi dhidi yake lilizimwa, na mkuu wa walinzi wa rais Abdourahamane Tchiani, mtiifu kwa Mahamadou Issoufou, alikuwa na jukumu muhimu katika kulizima.. Bazoum alibaki akiidhinisha uwepo wa Marekani na alifanya kazi kuimarisha uhusiano na Marekani. Ukurasa wa Arabi 21 ulinakili kutoka kwa tovuti ya Marekani ya The Intercept mnamo 2023/7/27 katika ripoti ya tovuti hiyo kuhusu uwepo wa Marekani nchini Niger, ikimnukuu Mohamed Bazoum akimwambia Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Blinken: "Marekani inabaki kuwa chaguo bora, na inahitaji tuthibitishe kuwa tunaweza kutoa matokeo halisi." Hivyo, sera ya Mohamed Bazoum kama mtangulizi wake na rafiki yake Mahamadou Issoufou ni utiifu kwa Marekani na kutoifanyia uadui Ufaransa na uwepo wake, kwani mazingira ya kisiasa na kijeshi kwa ujumla yanailalia Ufaransa, nchi iliyoikoloni nchi hiyo moja kwa moja hapo awali kwa muda wa miaka 60, na baadaye kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwa muda unaokaribiana na huo.
Pili: Kutokana na yaliyotangulia, inabainika kuwa Mahamadou Issoufou na Bazoum ni mawakala wa Marekani, na kwamba mkuu wa walinzi wa rais Abdourahamane alikuwa rafiki wa karibu wa Issoufou na alimpa mamlaka makubwa, na alikuwa na jukumu muhimu katika kuzima jaribio la mapinduzi dhidi ya Bazoum siku mbili kabla ya kushika nafasi yake.. Hii ina maana kwamba watatu hawa wako katika mkondo mmoja, sasa kwa nini mapinduzi haya? Kuchunguza kwa kina matukio yaliyotokea na usuli wake kunabainisha yafuatayo:
Kama tulivyosema, mkuu wa walinzi alikuwa mtu wa kuaminiwa na Issoufou, wa karibu naye na mlinzi wake dhidi ya mapinduzi ya mawakala wa Ufaransa jeshini.. Vyombo vya habari, ikiwemo Asharq Al-Awsat mnamo 2023/7/28, vilisambaza habari zinazohusu kiongozi wa mapinduzi Abdourahamane Tchiani, vikitaja kuwa alijiunga na jeshi na kupata cheo cha afisa kabla ya kushika majukumu ya ndani, akiongoza baadhi ya vitengo vya kijeshi, lakini alijitokeza kwa nguvu baada ya kuingia madarakani Rais wa zamani Mahamadou Issoufou mwaka 2011 ambaye alimfanya kuwa mtu wake wa kuaminika. Wakati wa utawala wa Issoufou, Tchiani alinufaika na kupandishwa vyeo haraka kijeshi ambavyo vilimfanya afikie cheo cha Jenerali bila kupita katika mkondo uliozoeleka katika taasisi ya kijeshi kwa ajili hiyo.. Issoufou alimteua kuwa mkuu wa walinzi wa kitaifa mwaka 2015, ambavyo ni vitengo vya wasomi vilivyopewa jukumu la kumlinda Rais.. hususan baada ya jaribio la mapinduzi dhidi ya Issoufou.
Kabla ya Mohamed Bazoum kuingia madarakani kwa siku mbili na kabla ya kuingizwa kuwa rais wa nchi rasmi na kula kiapo cha kikatiba, alikumbwa na jaribio la mapinduzi lililofeli mwaka 2021.. jambo lililomfanya afanye mabadiliko makubwa katika kikosi cha walinzi wa rais, lakini alimubakisha Jenerali Tchiani kuwa mkuu wa kikosi hicho kulingana na pendekezo la Issoufou aliyekuwa amekabidhi madaraka hivi punde, lakini alibaki na uhusiano wa karibu na Bazoum. Issoufou anachukuliwa kuwa mtu mwenye neno la mwisho ndani ya chama tawala na alimuingiza mwanawe katika serikali kama Waziri wa Nishati na Madini.
Vyanzo vinasema kuwa watu wa karibu na Bazoum walikuwa wakimwonya dhidi ya Tchiani na kumshauri amwondoe katika uongozi wa kikosi cha walinzi wa rais ili kuimarisha utawala wake, lakini alimubakisha kulingana na pendekezo la rafiki yake rais wa zamani. Lakini katika kipindi cha hivi karibuni, wanaharakati wa kisiasa katika mitandao ya kijamii walisambaza nia ya Bazoum kumwondoa na kufanya mabadiliko katika uongozi wa taasisi ya kijeshi na walinzi wa kitaifa. Inasemekana kuwa alikuwa na nia ya kumfuta kazi mwana wa rais wa zamani kutoka Wizara ya Nishati na Madini. Haya yote yalisababisha kudhoofika kwa uhusiano kati yake na rais wa zamani.. na hata kupelekea kero kwa Issoufou na rafiki yake wa karibu Tchiani. Kisha, uungaji mkono wa kijamii kwa Bazoum ukadhoofika, na kukatokea manung'uniko kwa idadi ya viongozi wa chama tawala kutokana na kupanda kwake, kwa sababu hatoki katika kabila la Hausa ambalo linawakilisha nusu ya nchi, bali ana asili ya Kiarabu.. Hii inathibitishwa na kura chache alizopata katika mji mkuu, pamoja na jaribio la mapinduzi dhidi yake siku mbili kabla ya kuingizwa madarakani. Hakukaribishwa na makabila mengine wala na baadhi ya nguzo za jeshi.
Hivyo basi, Jenerali Abdourahamane Tchiani alikuwa mkuu wa walinzi wa rais wakati wa utawala wa rais wa zamani Mahamadou Issoufou lakini rais wa sasa alikuwa anafikiria kumubadilisha.. Al Jazeera ilichapisha kwenye tovuti yake mnamo 2023/7/28 ikinukuu ripoti ya "Mediapart": (Jenerali Abdourahamane Tchiani alikuwa mkuu wa walinzi wa rais wakati wa utawala wa rais wa zamani Mahamadou Issoufou, lakini rais wa sasa alikuwa anafikiria kumubadilisha, kutokana na kile kinachojulikana kati ya wataalamu wa jeshi la Niger kuhusu utii wake mkubwa kwa rais wake wa zamani. Mchambuzi wa kisiasa Moussa Aksar aliiambia tovuti hiyo kuwa kila kitu kilikuwa kinaashiria kwamba Mahamadou Issoufou anataka kurejea madarakani.. na alikuwa anataka kudhibiti mafuta, na ana hisa nyingi katika makampuni mengi, kulingana na ripoti ya uchunguzi iliyoashiria ubadhirifu katika Wizara ya Ulinzi ya Niger wakati wa utawala wa rais wa zamani.) Maelezo haya yanathibitisha kuwa mapinduzi yana sababu za ndani, na inaonekana ndizo sababu kuu za mapinduzi. Kwa sababu hiyo, mapinduzi yalipotokea, kulikuwa na majibu makali ya kulaani mapinduzi kutoka kwa Marekani, Ufaransa, Umoja wa Ulaya, Uingereza, Urusi na nguvu za kikanda.. kana kwamba kila mtu alishtukizwa na hilo!!
Hivyo basi, Marekani na Umoja wa Mataifa zililaani mapinduzi hayo.. na Ufaransa na Umoja wa Ulaya zililaani mapinduzi hayo.. na Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi "ECOWAS" ikalaani.. na hata Uingereza ambayo haina ushawishi nchini Niger ililaani mapinduzi hayo! Vilevile, Urusi ambayo haina uwepo huko wala kundi la Wagner, nayo pia ililaani, na haikutambua kuwa kupandishwa kwa bendera yake katika harakati hizo ni kwa ajili ya kupotosha! Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Karine Jean-Pierre, alisema ("Marekani haioni dalili zozote za kuaminika za kuhusika kwa Urusi au vikosi vya kundi la kijeshi la kibinafsi la Urusi la Wagner katika mapinduzi nchini Niger"... Reuters 2023/7/27).
Tatu: Hitimisho:
Inayopewa uzito ni kwamba mapinduzi haya yana sababu za ndani, kwani ni mzozo au mchuano kati ya mawakala wa Marekani: Issoufou na Abdourahamane upande mmoja, na Bazoum upande mwingine.. Wakati wawili wa kwanza walipogundua kuwa Bazoum anakusudia kumuondoa mwana wa Issoufou na mkuu wa walinzi, walipanga harakati hizi za mapinduzi, lakini waliacha nafasi ya mazungumzo kwa sababu wote ni mawakala wa Marekani. Hivyo, walichelewa kumkamata Bazoum na kumweka gerezani; kisha siku chache baada ya mapinduzi wakamshitaki kwa uhaini, huku akiwa bado yuko katika makazi yake, mara nyingine wakimbana na mara nyingine wakimruhusu daktari, dawa na chakula kumfikia. Wakati huo huo, Marekani na balozi wake mjini Niamey wanatafuta njia ya kutatua suala hili.. lakini mapinduzi haya yanabaki kuwa kati ya mawakala wa Marekani.
Mwathirika mkubwa wa mapinduzi haya ni Ufaransa, kwani waasi ni mawakala wa Marekani. Ili kuhalalisha mapinduzi yao, walitumia misimamo ya Ufaransa iliyochanganyikiwa na ya hasira, na chuki ya watu kwa mkoloni wa zamani na unyonyaji wake kwa nchi yao na wizi wake wa utajiri wa nchi yao bila kuwaachia chochote hata kidogo. Hivyo, maelfu ya watu waliandamana dhidi ya Ufaransa mbele ya ubalozi wa Ufaransa mnamo 2023/7/30 na kupaza sauti za kulaani Ufaransa.
Marekani itafanya kazi kudhibiti mgogoro huo huko na kuutumia dhidi ya ushawishi wa Ufaransa na kuimarisha ushawishi wake, iwe ni kwa:
Kumrejesha Bazoum ikiwezekana, ingawa jambo hili si rahisi, na kumrejesha kwake pia kuna maslahi kwake kwa sababu yeye ni mmoja wa mawakala wake, hata kama anaenda sambamba na Ufaransa, kwani maoni ya umma yako dhidi ya mapinduzi na yanatoa wito wa kumrejesha kwa sababu alichaguliwa kisheria.
Au kwa kuwashinikiza waasi kurejea katika kumaliza kipindi cha mpito na kuandaa uchaguzi mpya, na pengine rais wa zamani Issoufou akajigombeza mwenyewe ili kurejea upya, kwani waasi ni watu wake na wa kabila lake, ili kulinda ushawishi wake na ushawishi wa familia yake na kufunika wizi na ubadhirifu wao. Hususan kwa kuwa yeye ni wakala wa Marekani na ana ushawishi mkubwa katika chama chake na kabila lake linalounda nusu ya nchi.
- Hivyo basi, nchi kama hii ya Kiislamu ambayo inachukuliwa kuwa miongoni mwa nchi tajiri zaidi kwa maliasili lakini ni miongoni mwa nchi maskini zaidi, ni kwa sababu ya mawakala wanaofuata ukoloni na kutoa huduma kwa mkoloni huyu au yule mkabala wa viti vya madaraka na kupata mali ya umma. Hawafikirii maslahi ya nchi yao na namna ya kuikomboa na kuikweza, kwani wanakosa fikra yoyote hata kama ni watoto wa Waislamu, na watu wanawafuata madhalimu hawa bila ufahamu na utambuzi kutokana na uduni wa kifikra na kutawaliwa na ukabila wa kijahili.. Hali hii haileti amani, usalama wala utulivu, bali utawala wa Kiislamu, Khilafah Rashidah, ndio utukufu wa Uislamu na Waislamu, na njia ya nguvu zao, ulinzi wao na maendeleo yao.. hususan kwa kuwa Niger ni nchi ya Kiislamu na watu wake ni Waislamu.. Huu ndio ukweli.
فَمَاذَا بَعْدَ الْحَقِّ إِلَّا الضَّلَالُ فَأَنَّى تُصْرَفُونَ
"Basi ni nini kipo baada ya haki isipokuwa upotevu? Basi mnarudishwa wapi?" (QS. Yunus [10]: 32)
Mnamo tarehe ishirini na nane ya Muharram 1445 H 2023/8/15 M