Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Dola ya Kiyahudi na Kushikamana kwake na Marekani!

March 08, 2015
3254

Swali:

Katika hotuba ya Netanyahu mbele ya Kongresi ya Marekani mnamo tarehe 3/3/2015, alisisitiza msimamo wake wa kupinga kile ambacho Marekani inafanya na Iran kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran. Hiyo ilikuwa wakati wa ziara yake iliyofanyika kinyume na itifaki ya kawaida, yaani bila idhini ya Obama wala chama chake cha Democratic katika Kongresi, jambo ambalo baadhi ya waangalizi walilitaja kama udhalilishaji kwa Obama. Je, hii inamaanisha kuwa uhusiano wa Marekani na dola ya Kiyahudi umeingia katika hatua ya kutengana au hali ya uadui? Je, matukio haya yana uhusiano na uchaguzi katika dola ya Kiyahudi na Marekani? Kisha, nini matokeo yanayotarajiwa ya chaguzi hizi kwa pande zote mbili? Allah awalipe heri.

Jibu:

Ili jibu liwe wazi, tunapitia mambo yafuatayo:

1- Hakika Wayahudi hawana uwezo wa kusimama wenyewe isipokuwa kwa kamba kutoka kwa Allah na kamba kutoka kwa watu kama Alivyosema Subhaanahu:

ضُرِبَتْ عَلَيْهِمُ الذِّلَّةُ أَيْنَ مَا ثُقِفُوا إِلَّا بِحَبْلٍ مِنَ اللَّهِ وَحَبْلٍ مِنَ النَّاسِ

"Wamepigwa na udhalili popote wanapopatikana, isipokuwa (wakishika) kamba ya Mwenyezi Mungu na kamba ya watu." (QS Ali 'Imran [3]: 112)

Na kamba ya Allah waliikata baada ya enzi za Mitume wao, hivyo haikubaki isipokuwa kujipendekeza kwa mataifa mengine na kushikamana nayo ili kuendelea kuishi. Jambo hili limeonekana kwao tangu enzi hizo. Katika zama za kisasa, walikimbilia Uingereza ambayo iliwawezesha kuikalia kimabavu Palestina na wakaanzisha dola yao ya kinyakuzi, na leo wanajipendekeza kwa Marekani na kushikamana nayo. Kwa hivyo, ni vigumu kwa hali kufikia hatua ya kuifanya Marekani kuwa adui yao, hata kama kutatokea kutoelewana kiasi gani...

2- Wayahudi kupitia utegemezi wao kwa nchi nyingine wanajaribu kufikia maslahi yao. Wanatumikia mataifa makubwa na kushikamana nayo si kwa ajili ya kuyatumikia mataifa hayo pekee, bali pia ili kufikia maslahi yao. Vyama vya Kiyahudi havitofautiani katika hili; iwe mtawala ni chama cha Labor au Likud, wote wanaifuata Marekani na kushikamana nayo ili kufikia maslahi ya Wayahudi na si kwa ajili ya kuitumikia Marekani pekee... Katika suala hili, wanatofautiana na watawala katika nchi za Waislamu. Watawala wa Waislamu ni vibaraka wa Magharibi wanaotimiza maslahi ya nchi nyingine si kwa ajili ya maslahi ya nchi zao, bali ili tu wabaki kwenye viti vyao vya uongozi...

3- Wakati wa uwaziri mkuu wa pili wa Rabin kuanzia mwaka 1992, na hiyo ikiwa ni wakati wa urais wa Clinton wa chama cha Democratic nchini Marekani kuanzia 1993, Rabin aliona kuwa maslahi ya dola ya Kiyahudi ni kukubaliana na masuluhisho yaliyokuwa yakitolewa na Clinton. Baadaye, Rabin aliuawa na pande nyingine za Kiyahudi mnamo 1995... Baada ya hapo, ilionekana wazi kuwa chama cha Labor kinaelekea kwenye chama cha Democratic cha Marekani na chama cha Likud kinaelekea kwenye chama cha Republican cha Marekani. Jambo hili liliathiri uhusiano wa kisiasa kwa kiasi fulani kati ya taasisi tawala nchini Marekani na dola ya Kiyahudi...

4- Nchi zinazofuata mfumo wa Kirasimali wa kidemokrasia huwa na kipindi cha uchaguzi kama kipindi cha kufichua kashfa, ambapo hakuna mipaka. Kila chama hutumia njia zake, za kimaadili na zisizo za kimaadili, wanagombana na kulaumiana, bali hata kuanika kashfa zao hadharani... Kwa sasa, katika dola ya Kiyahudi mwaka huu kuna uchaguzi wa mapema tarehe 17 Machi kama ilivyotangazwa... Na kuna uchaguzi nchini Marekani pia mwishoni mwa mwaka ujao "Novemba 2016". Pande zote mbili zinajaribu kutumia fursa zinazofaa ili kushinda, hivyo uhusiano wa chama cha Likud na Republicans na chama cha Labor na Democrats unajitokeza, ambapo kila mmoja anamuunga mkono mwenzake kwa kadiri ya uwezo wake...

5- Msimamo mkuu anaoufuata Netanyahu katika kuitumikia Marekani na kufikia maslahi ya Wayahudi uko karibu zaidi na siasa za chama cha Republican, kama tulivyotaja awali. Anapishana katika mbinu na njia na siasa za Obama na chama cha Democratic. Msuguano huu au tofauti hizi zilianza tangu Obama aingie madarakani. Netanyahu aliingia madarakani wakati uleule Obama alipoingia, na msuguano kati yao ulionekana mapema, hasa katika suala la Palestina na kisha suala la nyuklia la Iran. Katika kipindi hicho, alikuwa akijaribu kupitia kundi la ushawishi la Kiyahudi (Lobby) nchini Marekani kuishinikiza serikali ya Obama ili kupata kile kinachowezekana katika masuala haya mawili...

6- Msuguano huu unachochewa na mambo mawili: Kwanza, kama tulivyotaja awali, ni uhusiano kati ya vyama. Pili, ni tabia za Obama na Netanyahu... Yaani tofauti ya mitazamo katika kushughulikia hali ya kisiasa. Mtazamo wa Netanyahu ni mkali zaidi, na unategemea hoja inayosema kuna haja ya nguvu gumu (Hard Power - "nguvu ya kijeshi kwanza") ili kuunda matukio ya kisiasa katika eneo hili kwa maslahi ya dola ya Kiyahudi, na kufanya kazi peke yake ni sifa ya siasa zake. Mtazamo huu umeenea miongoni mwa wahafidhina mamboleo (Neo-conservatives) wa Marekani. Aidha, anajionyesha kuwa yuko pamoja na wahafidhina mamboleo katika utawala wa Bush, na wanachama wa chama cha Republican. Daniel Levy (ambaye alifanya kazi kama mshauri wa Waziri Mkuu wa zamani wa Kiyahudi Ehud Barak) alisema kuhusu mtazamo wa kisiasa wa Netanyahu: "Nadhani Bibi, yaani Netanyahu, amekuwa karibu na mrengo wa kulia wa Marekani, kwani alipata mafunzo yake ya kisiasa kutoka kwao." [Obama na Netanyahu: Tofauti ya mitazamo na siyo tu ya haiba, CNN, 2 Machi 2015]. Netanyahu anatambua hilo, na anajua kuwa chama cha Republican kinamuunga mkono.

Ama kwa upande wa Obama, yeye ni mwanahalisi kabisa (Realist), na anapinga mtazamo wa kisiasa wa wahafidhina mamboleo, ambao unatawala chama cha Republican. Yeye anafuata kanuni ya kuchanganya kati ya wazo la nguvu gumu na nguvu laini (Soft Power - "diplomasia, mikopo... na vishawishi vingine"), na anaona umuhimu wa kufuata siasa hizi ili kuunda matukio ya kisiasa kwa maslahi ya Marekani. Zaidi ya hayo, wanahalisi huepuka kutumia mbinu ya kufanya maamuzi peke yao ikiwa mazingira yanaruhusu... Hiyo ni ili kutekeleza shughuli za kisiasa kupitia ushirika na miungano inayojitolea kutekeleza mipango ya Marekani.

7- Pamoja na hayo yote ya msuguano na tofauti... vyama vya Republican na Democratic vinashindana katika kutangaza kulinda usalama wa dola ya Kiyahudi. Chama cha Republican kinaunga mkono kwa nguvu dola ya Kiyahudi, hadi kufikia hatua ya kuishika mkono dola hiyo katika uhalifu wowote inaoufanya... Chama cha Republican kinaunga mkono hilo kwa kiasi kikubwa, na uungaji mkono wa dola ya Kiyahudi wakati wa enzi za Bush kijana ulikuwa wa dhahiri... Hata hivyo, uungaji mkono wa Obama haukuwa mdogo kuliko huo, hadi Netanyahu katika hotuba yake kwenye Kongresi alitaja hilo na kumshukuru Obama akisema: "Tunathamini kila kitu ambacho Rais Obama amekifanyia Israel, pamoja na kutuunga mkono kwa makombora zaidi ya kuzuia mashambulizi wakati wa operesheni zetu msimu uliopita wa joto... na nitakuwa na shukrani kwa Rais Obama daima kwa msaada huu. Na Israel inakushukuru, pamoja na Kongresi ya Marekani, kwa msaada wenu, hasa katika msaada mkubwa wa kijeshi na ulinzi wa makombora, ikiwa ni pamoja na Iron Dome...". Matamshi haya huongezeka kadiri uchaguzi unavyokaribia kwa kisingizio cha kuhitaji kura za Lobby ya Kiyahudi, ambayo propaganda za Kiyahudi huikuza mara nyingi zaidi ya ukubwa wake halisi!

8- Kutokana na yaliyotangulia, inabainika kuwa msuguano huu kati ya Netanyahu na Obama si hali ya uadui na Marekani au kutengana nayo, bali umechochewa na uhusiano tofauti kati ya Likud na chama cha Republican kwa upande mmoja, na kati ya Likud na chama cha Democratic kwa upande mwingine... Msuguano huu umeonekana wazi kwa sababu uliendana na hali ya uchaguzi katika nchi zote mbili. Netanyahu anatambua kuwa maoni ya umma ya dola ya Kiyahudi yanahofia Iran kupata silaha za nyuklia, kwa hivyo ametumia ulaini wa Obama ulio wazi kuelekea Iran katika suala la nyuklia. Netanyahu amejifanya mlinzi wa dola ya Kiyahudi mbele ya hatari ya nyuklia. Aidha, ametumia siasa za upinzani wa Republicans nchini Marekani dhidi ya mkakati wa Obama wa mazungumzo ili aonekane kuwa upande wa chama cha Republican, hivyo vyama vyote viwili kunufaika katika uchaguzi. Kwa kufanya hivyo, amejibu mapigo kwa mkutano wa Biden na Kerry (wa Democrats) na Herzog, kiongozi wa chama cha Labor na mshindani mkuu wa Netanyahu katika uchaguzi ujao wa Israel, mkutano uliofanyika pambizoni mwa mkutano wa Munich tarehe 7/2/2015, na mikutano hiyo haikuwa katika ratiba rasmi... Herzog katika hotuba yake kwenye mkutano wa Munich, akielezea hotuba iliyopangwa ya Netanyahu katika Kongresi, alisema: "Hotuba ya Netanyahu ambayo ilizaliwa katika dhambi, ikiwa ni zao la 'uchaguzi', inatishia usalama wa raia wa Israel na uhusiano maalum kati ya Israel na Marekani"... Wakati huo huo, ofisi ya Biden ilitangaza "kwamba Makamu wa Rais atakuwa nje ya nchi na hatahuzuria hotuba yenye utata ya Netanyahu kuhusu Iran mbele ya Kongresi tarehe 3 Machi".

Muhtasari:

a- Kutokana na haya yote, inabainika kuwa Netanyahu na Obama wanavutana kwa sababu zilizotajwa, na kila mmoja wao anamuunga mkono mpinzani wa mwenzake katika uchaguzi ujao... Katika muktadha huu, ilikuja ziara ya Netanyahu kwenye Kongresi ya Marekani kwa makubaliano ya moja kwa moja na chama cha Republican bila kupitia Ikulu (White House) au angalau kukubaliana na Democrats katika Kongresi. Hivyo, ziara yake ilionyesha tofauti ya kweli kati ya watu hao wawili na vyama viwili, na tofauti hiyo iliongezeka joto kutokana na anga ya uchaguzi nchini Marekani na dola ya Kiyahudi... Hivyo ndivyo kiongozi wa dola ya Kizayuni Benjamin Netanyahu alivyoalikwa kuzungumza katika kikao cha pamoja cha Kongresi nchini Marekani tarehe 3 Machi 2015. Hili lilikuwa jambo lisilo la kawaida, kwa sababu mwaliko haukutoka kwa Obama kwenda kwa Netanyahu, bali kutoka kwa Spika wa Bunge wa chama cha Republican, John Boehner. Hili ndilo lililopelekea mvutano kati ya serikali ya Netanyahu na utawala wa Obama kuonekana hadharani, ambapo vyombo vya habari vilitoa habari hiyo kwa wingi.

Utawala wa Obama ulikosoa mwaliko huo, huku Rais wa Marekani akitangaza kuwa hatakutana na Netanyahu... kadhalika Kerry aliondoka Washington kwenda nje ya nchi wakati Netanyahu akiwa Washington... Kukatokea malumbano ya matamshi kati ya upande wa utawala na upande wa Kongresi, jambo linaloashiria kuwa chama cha Republican kinataka kuchukua hatua za kiuchaguzi kwa kujipatia idadi kubwa zaidi ya kura za Lobby ya Kiyahudi katika ushindani wake na chama tawala cha Democratic, ili kuongeza kura katika uchaguzi wa rais utakaofanyika mwaka ujao.

b- Ama Netanyahu, yeye alihutubia Kongresi dhidi ya mazungumzo ya Obama na Iran, na kuyataja makubaliano ambayo Obama anataka kuyafanya kuwa ni mabaya... Netanyahu alisema: "Nguvu za kimataifa ziliahidi kuizuia Iran kupata silaha za nyuklia, lakini inaonekana wameachana na ahadi hiyo," na akaongeza: "Naiheshimu Ikulu na Rais wa Marekani lakini katika suala la hatima kama hili ambalo linaweza kuamua kuwepo kwetu au kutokuwepo kwetu, lazima nifanye kila kitu kuzuia hatari kubwa kama hii kwa Israel." Alisema "pendekezo lililotolewa kwa Iran litaiwezesha kutishia kuendelea kuwepo kwa dola ya Israel." (CNN 10/2/2015). Haya yote ni ili ajifanye mlinzi wa maslahi ya Wayahudi ili anufaike katika uchaguzi, hasa kwa kuzingatia kuwa kuna kura za maoni zinazoonyesha mafanikio ya chama cha Republican nchini Marekani katika uchaguzi ujao kulingana na mafanikio ya chama hicho katika uchaguzi wa katikati ya muhula mwishoni mwa mwaka jana. Hivyo, Likud inapata upendeleo zaidi kwa Republicans... Pamoja na msimamo wake wa kutoiruhusu Iran kumiliki silaha za nyuklia, serikali ya Netanyahu imekuwa ikijitayarisha kwa miaka kadhaa kuishambulia Iran kwa kisingizio cha mpango wa nyuklia mwishoni mwa mwaka 2011. Ulaya ilikuwa ikiishajiisha kufanya hivyo ili kuiaibisha Marekani, ambapo Ufaransa iliipatia dola ya Kiyahudi picha za satelaiti za vinu vya nyuklia vya Iran, na Ujerumani iliitumia nyambizi za kisasa zinazobeba makombora, na Uingereza iliipatia habari za kijeshi na kijasusi ambapo Mkuu wa Majeshi wa Uingereza wakati huo alitembelea dola ya Kiyahudi na kukaa huko kwa siku tatu mfululizo kwa ajili ya maandalizi ya shambulio hilo. Italia iliruhusu ndege za Kiyahudi kufanya mazoezi katika anga yake ya kuruka umbali mrefu na kuongeza mafuta angani. Marekani ilikuwa ikifanya kazi ya "kuidhibiti" dola ya Kiyahudi na kuishinikiza isiongeze mivutano, ikidai kuwa vikwazo vinatosha na kwamba siasa za Obama ndizo zenye tija... Dola ya Kiyahudi ilikuwa chini ya shinikizo hilo hadi ilipofika ziara hii ya Netanyahu kwa uratibu na chama cha Republican katika anga ya uchaguzi...

c- Kuhusu matokeo yanayotarajiwa ya uchaguzi, katika dola ya Kiyahudi matokeo yatakuwa karibu sana kwani upinzani ukiongozwa na chama cha Labor unasisitiza kuwa msuguano huu kati ya Netanyahu na Obama unadhuru maslahi ya Marekani, na kwamba kukosa msaada wa Marekani kutasababisha madhara makubwa kwa dola yao. Wanajaribu pia kuonyesha matamshi ya Obama kuhusu kulinda usalama wa Wayahudi, na kwamba siasa zake za nyuklia zinaendelea kuzuia hatari ya nyuklia ya Iran kwa siasa madhubuti za kimkakati. Wanategemea kupitia hilo kupata uungaji mkono kutoka kwa Lobby ya Kiyahudi nchini Marekani, na wakati huo huo kutengeneza utulivu katika dola ya Kiyahudi ili wapate kura nyingi pia... Kwa upande mwingine, ukaribu wa Netanyahu na chama cha Republican ambacho wanatarajia kitashinda katika uchaguzi ujao wa Marekani, na kujionyesha kwa Netanyahu kama mlinzi wa maslahi ya Wayahudi na kuzuia hatari ya nyuklia, yote hayo yanampatia uungaji mkono kutoka kwa Lobby ya Kiyahudi na kura ndani ya dola ya Kiyahudi... Hivyo basi, kinachotarajiwa ni kwamba pande zote mbili, chama cha Labor na Likud, ziko karibu katika hoja, na kwamba uungaji mkono wa Obama kwa chama cha Labor na uungaji mkono wa chama cha Republican kwa Likud viko karibu kwa kiasi fulani, isipokuwa kama Obama atacheza vyema nafasi yake kama Rais na kuitumia katika uhusiano imara na chama cha Labor, na hapo anaweza kuathiri ushindi wa Netanyahu... Lakini hatua ya Obama kuwa mkali kiasi hiki na Netanyahu ni jambo lisiloelekea kutokea, hasa kwa vile Obama haruhusiwi kugombea tena katika muhula ujao. Hii ina maana kwamba kinachotarajiwa ni ushindani mkali kati ya Netanyahu na mpinzani wake Herzog kutoka chama cha Labor, na ni vigumu kwa mmoja wao kufanikiwa kuunda serikali isipokuwa iwe ya muungano dhaifu kwa sababu ni vigumu kwa vyama hivi viwili vikubwa kuungana. Badala yake, kila chama kitalazimika kushirikiana na vyama vidogo ambavyo vitaviwekea masharti makubwa kuliko ukubwa wao, na hivyo serikali yoyote itakayoundwa katika dola ya Kiyahudi itakuwa dhaifu, isipokuwa kama vyama hivi viwili vitaweza kukaribiana...

Ama kuhusu uchaguzi nchini Marekani, kura za maoni zinazochapishwa zinafanya uwezekano wa chama cha Republican kushinda kuwa mkubwa, kulingana na uchaguzi uliopita wa katikati ya muhula ambapo chama cha Republican kinadhibiti sehemu kubwa ya Kongresi, hasa kwa vile Obama hakuwa na mafanikio ya kuridhisha mbele ya migogoro ya kimataifa katika hali ya ndani ya Marekani na hali ya nje.

d- Ama kuhusu hali ya uadui au kutengana na Marekani, hili ni jambo lisilowezekana kama tulivyotaja awali. Badala yake, dola ya Kiyahudi itaendelea kushikamana na Marekani na kujipendekeza kwake, kwani hawana maisha bila kamba kutoka kwa watu, ambayo katika siku hizi ni Marekani... Lakini kamba hii itakatika kwa idhini ya Allah, pale nchi hizo zitakapohisi kuwa kamba iliyonyooshwa kati yao na dola ya Kiyahudi iliyoporwa Palestina ni balaa kwao; na hiyo ni kwa nguvu ya Uislamu, watu wake na dola yake. Na hakika hilo litatokea kwa idhini ya Allah.

وَلَتَعْلَمُنَّ نَبَأَهُ بَعْدَ حِينٍ

"Na hakika mtaujua habari yake baada ya muda kupita." (QS Sad [38]: 88)

Share Article

Share this article with your network