Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mkubwa Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Watafiti wa Ukurasa Wake wa Facebook "Fiqhi"
Ahmed Al-Qairawan
Swali:
Assalam Alaykum, ni nini maana ya Khalifa pekee kuwa na haki ya kupitisha sheria (Tabanni) za Shari’ah?
Jibu:
Wa Alaykum Salaam Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh,
Hakika jibu la swali lako lipo kwa kina katika kitabu cha Muqaddimat al-Dustur (Utangulizi wa Katiba) na katika vitabu vingine vya Hizb. Nitakunukulia baadhi ya yale yaliyokuja kuhusu mada hii katika kitabu cha Muqaddimat al-Dustur, Sehemu ya Kwanza:
- Imekuja katika ukurasa wa 110 wa faili ya Word yafuatayo:
[Ama kanuni ya nne, nayo ni kuwa Khalifa pekee ndiye mwenye haki ya kupitisha sheria (Tabanni), imethibiti kwa Ijma’ ya Maswahaba kuwa Khalifa pekee ana haki ya kupitisha sheria. Na kutokana na Ijma’ hii, kanuni maarufu za kisheria zilichukuliwa (Amri ya Imamu huondoa tofauti), (Amri ya Imamu ni yenye kutekelezwa), (Mtawala ana haki ya kuanzisha maamuzi ya kisheria kulingana na ukubwa wa matatizo yanayojitokeza).] Mwisho.
- Na imekuja katika sharhi ya Kifungu cha 36, ukurasa wa 146-153 wa faili ya Word yafuatayo:
[Ibara (a) dalili yake ni Ijma’ ya Maswahaba. Hiyo ni kwa sababu neno sheria (Qanun) ni neno la kiistilahi, na maana yake ni: Amri anayoitoa mtawala ili watu waifuate. Sheria imetafsiriwa kuwa ni (mkusanyiko wa kanuni ambazo mtawala huwalazimisha watu kuzifuata katika mahusiano yao) yaani, ikiwa mtawala ataamrisha hukumu fulani, basi hukumu hizo huwa ni sheria, watu hulazimika nazo, na ikiwa mtawala hataziagiza, basi hazitakuwa sheria, na watu hawalazimiki nazo. Na Waislamu hufuata hukumu za Shari’ah, hivyo wanafuata amri na makatazo ya Allah, na si amri na makatazo ya mtawala. Yale wanayoyafuata ni hukumu za Shari’ah, na si amri za mtawala.
Hata hivyo, Maswahaba walitofautiana katika hukumu hizi za Shari’ah; baadhi yao walielewa kitu tofauti na wengine kutokana na maandiko ya kisheria (Nusus), na kila mmoja alikuwa akifuata kulingana na ufahamu wake, na ufahamu wake huo ndio ulikuwa hukumu ya Allah kwake. Lakini kuna hukumu za Shari’ah ambazo usimamizi wa mambo ya Umma unahitaji Waislamu wote wafuate maoni mmoja, na si kila mmoja kufuata kulingana na Ijtihadi yake. Na jambo hilo lilitokea kihalisia; Abu Bakr aliona kuwa ni vyema kugawa mali sawasawa kati ya Waislamu kwa sababu ni haki yao wote kwa usawa. Umar naye aliona kuwa haifai kumpa yule aliyepigana dhidi ya Mtume sawa na yule aliyepigana naye, au kumpa maskini sawa na tajiri. Lakini Abu Bakr ndiye aliyekuwa Khalifa, akaamuru kufanya kazi kwa maoni yake, yaani akapitisha (Tabanni) ugawaji wa mali kwa usawa. Waislamu wakamfuata katika hilo, na Makadhi na Magavana wakatekeleza hilo, na Umar akanyenyekea, akafanya kazi kwa maoni ya Abu Bakr na kuyatekeleza.
Na alipokuja Umar kuwa Khalifa, alipitisha (Tabanni) maoni yanayopingana na maoni ya Abu Bakr, yaani akaamuru kwa maoni yake kugawa mali kwa upendeleo (kutofautisha), si kwa usawa, ambapo alitoa kulingana na ukongwe katika Uislamu na mahitaji. Waislamu wakafuata, na Magavana na Makadhi wakafanya kazi kwa maoni hayo. Hivyo, Ijma’ ya Maswahaba ilifungamana juu ya kwamba Imamu ana haki ya kupitisha (Tabanni) hukumu fulani zilizochukuliwa kutoka kwenye Shari’ah kwa Ijtihadi sahihi, na kuamuru zifuatwe, na ni wajibu kwa Waislamu kuzitii, hata kama zinapingana na Ijtihadi zao, na kuacha kufanyia kazi maoni na Ijtihadi zao wenyewe. Kwa hiyo, hukumu hizi zilizopitishwa (Mutabannat) ndizo zikawa sheria. Na kuanzia hapa, utunzi wa sheria ukawa ni wa Khalifa pekee, na hakuna mwingine yeyote anayemiliki haki hiyo kabisa.] Mwisho.
Natumai kuwa sasa jambo limekuwa wazi.
Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu al-Rashtah
07 Rajab al-Khair 1442 Hijri Sawa na 19/02/2021 Miladi
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Facebook wa Amir (Allah amuhifadhi)