Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Kilichotokea na Kinachoendelea Kuhusu Aleppo Kutokana na Njama, Usaliti, na Kukatisha Tamaa!

December 18, 2016
7393
استمع للمقال

Jibu la Swali

Swali: Hazijapita wiki mbili tangu kuanza kwa mapigano huko Aleppo kuanzia tarehe 26/11/2016 hadi mazungumzo ya kujiondoa na kuwahama kwa raia na wapiganaji yalipoanza... Kisha haikupita wiki moja baada ya hapo hadi sehemu ya mashariki ya Aleppo ikakaribia kuwa tupu bila wakazi wake raia, wapiganaji na familia zao: (Beirut-Amman "Reuters" - Maelfu walikusanyika katika uwanja mmoja mashariki mwa Aleppo nchini Syria wakingojea mabasi yatakayowasafirisha nje ya maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa upinzani ndani ya mchakato wa uokoaji ambao Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu inatumai utaanza tena Jumapili... Wakazi wanasema kuwa inakadiriwa watu wapatao elfu 15 walikusanyika katika uwanja mkuu katika kitongoji cha Al-Sukari huko Aleppo, wengi wao wakiwa ni raia waliobaki katika eneo la mwisho lililoshikiliwa na wapinzani, wengi wao wakiwa ni familia za wapiganaji na raia wengine, na pia kuna wapiganaji wachache. Waandaaji walitoa nambari kwa kila familia ili kuwaruhusu kupanda mabasi yatakapowasili... Reuters Arabic and International 18/12/2016). Ni nini kilichosababisha kasi hii ya (kukabidhi) Aleppo Mashariki kwa utawala, licha ya ripoti za awali kusema kuwa Aleppo ingeweza kuupinga utawala huo kwa angalau mwaka mmoja? Je, sababu ni udhaifu wa wapiganaji, au njama za wapanga njama? Ahsante.

Jibu: Aleppo imekumbwa na shambulio la kinyama na la kikatili lililoendeshwa na Marekani, likipangwa nayo na kutekelezwa na Urusi, Iran, na wafuasi wao. Licha ya mashambulizi haya kuwa mazito kiasi cha kuweza kuangusha milima imara, Aleppo ilistahimili, ikapinga, na kuyasababishia makundi hayo maumivu na majeraha makubwa. Mapambano hayo yangeweza kuendelea kwa muda mrefu... Lakini amri ya Marekani kwa Uturuki kuingilia kati suala la Aleppo kwa kufanya njama na Urusi na kuyakatisha tamaa makundi yenye mafungamano nayo, na kuyashinikiza kurudi nyuma na kujiondoa mara kwa mara, ndivyo vilivyozua mvurugano na kisha kile kinachofanana na "kukabidhi" Aleppo. Uturuki ilikuwa na jukumu la kutekeleza mpango wa Marekani kwa uratibu na Warusi ili kuuwezesha utawala kuingia Aleppo Mashariki... Hivyo, kilichoiangusha Aleppo mikononi mwa utawala si nguvu ya utawala huo, bali ni njama za wapanga njama kulingana na mpango uliokubaliwa kati ya Urusi na Uturuki chini ya usimamizi wa Marekani. Putin alifichua jambo hili na hakumsetiri mshirika wake Erdogan, bali alimfedhehesha hadharani katika mkutano na waandishi wa habari! Putin alisema kuwa kilichotokea Aleppo ni tafsiri ya kile alichokubaliana na Erdogan wakati wa ziara yake huko St. Petersburg: (Rais wa Urusi Vladimir Putin alilipua bomu la kisiasa alipofichua kuwa mchakato wa kuwaondoa wanamgambo kutoka mashariki mwa Aleppo ulifikiwa wakati wa ziara ya Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan huko St. Petersburg mnamo mwezi Agosti uliopita... Rais wa Urusi alisema katika mkutano na waandishi wa habari wa pamoja na Waziri Mkuu wa Japani Shinzo Abe mjini Tokyo, leo "jana" Ijumaa, kwamba Moscow ilikubaliana na Ankara juu ya mchango wa Uturuki katika kuwatoa wanamgambo hao watakaokubali kuweka chini silaha ili kulinda raia kwanza kabisa. Aliongeza, "Tukihukumu kutokana na kile ninachokiona, kile kinachotokea ni kile hasa tulichokubaliana na Rais wa Uturuki wakati wa ziara yake huko St. Petersburg"...) (Ilaf, 16/12/2016, Sputnik News, 16/12/2016).

Ningeweza kuhitimisha jibu kwa tamko la Putin, lakini nitafafanua zaidi jinsi mji wa Aleppo al-Shahba, mji wa ushujaa na heshima, ulivyochomwa kisu cha mauti na Uturuki, ambayo ilikuwa ikichukulia Aleppo kama mstari mwekundu (ambao hauvukiki) lakini ikaigeuza kuwa mstari ulioyeyuka katika damu yake... Kadhalika, Aleppo ilichomwa kisu na makundi hayo kwa kugeuza migongo yao siku ya mapambano kutokana na utegemezi wa mali chafu waliyokuwa wakilishwa na nchi hizo zilizomfanyia hiana Mwenyezi Mungu (swt), Mtume Wake, na waumini... Kwa hivyo, nitafafanua jambo hili zaidi:

Kwanza: Wapiganaji huko Aleppo na maeneo ya kando yake hawakuwa dhaifu kiasi cha mji huo kuvamiwa kwa muda mfupi namna hiyo! Katika kipindi cha takriban wiki mbili kuanzia tarehe 26/11/2016, vikosi vya utawala na washirika wake viliingia katika kitongoji cha Hanano, kitongoji kikubwa zaidi mjini Aleppo, na vikasonga mbele na kuchukua Sakhour, kisha Al-Shaar na maeneo ya Aleppo ya kale. Kusonga mbele kwa vikosi hivyo kulikuwa rahisi kwa namna isiyotarajiwa, kwani havikukutana na upinzani ambao ungepaswa kuwepo kama si kuingilia kati kwa Erdogan. Baada ya mapumziko ya siku mbili, vikosi vya utawala vilianza kusonga mbele upande wa kusini wa mji na kukiteka kitongoji cha Sheikh Said. Katika kipindi hicho, walikuwa wakisonga mbele kupitia kampeni kali ya anga na nchi kavu bila kuzingatia utakatifu wowote wa damu za raia wala kubomoa nyumba, bali hata kuzichoma moto. Mauaji ya kimbari na kampeni za kutia hofu zilifanyika, na yote haya yalikuwa yamekusudiwa kuingiza hofu katika nyoyo za wapiganaji waliokataa kuondoka Aleppo, ili kuwalazimisha kutoka haraka mjini humo... Tangu kuanza kwa kampeni ya kijeshi dhidi ya Aleppo, Uturuki ilikuwa ikifanya kazi na Urusi kwa kasi kubwa kuhusu ulingo wa Syria. BBC iliripoti mnamo 02/12/2016 ("Mevlut Cavusoglu alisema kuwa Uturuki inashauriana na Urusi na Iran, washirika wa Assad, na pia na Syria na Lebanon ili kufikia suluhu la mgogoro wa Syria. Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alijadili suala la Syria kwa simu na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin angalau mara 3 wiki iliyopita, huku Cavusoglu akikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergey Lavrov nchini Uturuki siku ya Alhamisi kujadili mada hiyo hiyo"). Hatua hizi zilikuwa za kutekeleza mauaji ya kinyama huko Aleppo hatua kwa hatua, baada ya maelezo yake kuchorwa na Washington, kisha pande za Uturuki na Urusi na vibaraka wao wakaanza kutekeleza.

Pili: Maafisa wa Uturuki katika kipindi kilichotangulia utekelezaji walikuwa wakitoa matamko ya ajabu na yasiyo ya kawaida kuhusu kuwafukuza "magaidi" kutoka Aleppo ("Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu alitaka kusitishwa kwa mapigano huko Aleppo kaskazini mwa Syria, na akatoa wito wa kuondoka mara moja kwa Jabhat Fatah al-Sham - zamani Jabhat al-Nusra - kutoka Aleppo...") (Al Jazeera Net, 27/10/2016). Hii ilikuwa baada ya mkutano wa Lausanne ulioongozwa na Marekani kuhusu Syria. Katika kipindi hicho, Marekani ilikuwa ikitayarisha uwanja pamoja na upande wa Uturuki, ambaye ni mchezaji nyeti zaidi huko. Siku iliyofuata, ukali wa matamko ya Uturuki uliongezeka kwa kiasi kikubwa. Ittihad Press iliripoti tarehe 17/10/2016 ("Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu, alisema kuwa 'ni lazima Aleppo isafishwe na magaidi wa Al-Nusra mara moja, na wapinzani wa Syria lazima wajitenge nao', na hiyo ilikuwa siku moja baada ya mkutano uliowakutanisha mawaziri wa mambo ya nje wa Urusi, Marekani, Iran, Iraq, Misri, Uturuki, Saudi Arabia, Qatar na Jordan pamoja na mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, Staffan de Mistura, katika mji wa Lausanne, Uswisi. Msimamo huu unachukuliwa kuwa wa kwanza wa aina yake kutoka kwa Uturuki kuelekea Jabhat al-Nusra inayoorodheshwa kama shirika la kigaidi na Umoja wa Mataifa"). Ama kuhusu makubaliano kati ya Urusi na Uturuki, Turk Press iliripoti mapema tarehe 31/10/2016 ikinukuu kutoka katika gazeti la Uturuki la Yeni Safak kutoka vyanzo ambavyo havikutajwa ("Kwamba maelewano yamefikiwa kati ya Uturuki na Urusi, na kulingana na mradi mpya wa Uturuki na Urusi, hali katika miji ya Aleppo, vijijini mwa Latakia, Idlib, Al-Hasakah, Deir ez-Zor na Raqqa itarudishwa kama ilivyokuwa kabla ya kuanza kwa vita vya Syria, kwa kuzingatia muundo wa idadi ya watu katika maeneo haya"). Kisha Uturuki-Erdogan ikaanza kuchukua hatua za haraka sana na uratibu wa karibu na Urusi kutekeleza vipengele vya makubaliano ya "kukabidhi" Aleppo!.

Tatu: Marekani ilijificha kidogo nyuma ya pazia, na Erdogan akaonekana huku taa zikiwa zimemulika juu yake katika jukwaa la Syria. Sambamba na kuanza kwa shambulio dhidi ya Aleppo, Uturuki ilitangaza ghafla juu ya mazungumzo yanayofanyika kati ya wahalifu wa Kirusi na ujumbe wa mazungumzo wa upinzani ambao ulishirikisha (Ahrar al-Sham, Jeshi la Mujahideen, Faylaq al-Sham na makundi ya Shamiya Front...) (Turk Press, 08/12/2016). Ujumbe huu uliingia katika mtego wa Erdogan uliokuwa umetayarishwa huko Washington. Mazungumzo haya yalikuwa ni dirisha ambapo Urusi pamoja na Erdogan walikuwa wakitupa mshituko katika ulingo wa Aleppo. Urusi ilitaka kuondoka kwa "Fatah al-Sham" kutoka Aleppo, na hiyo ilikuwa mwanzoni mwa mapigano ya nchi kavu huko Aleppo. Ingawa ni takwa la Urusi lililotangazwa tangu zamani, lakini kuliwasilisha huko Ankara mbele ya maafisa wa Uturuki na chini ya udhamini wao kuliwasilisha ujumbe mzito kwa wapinzani waliojihami kwamba Uturuki inataka wajitenge na "magaidi!". Mazungumzo yaliendelea huku kukiwa na mauaji na vitisho huko Aleppo, kisha siku iliyofuata Urusi ikatumbukiza takwa la kuondoka kwa wapiganaji wote kutoka Aleppo. Wakati wapatanishi wa upinzani waliojihami walipohakikisha kuwa takwa hili la Urusi pia ni takwa la Uturuki, walishinikiza upinzani huko Aleppo ili ujiondoe na kutoka, yaani kuukabidhi mji kwa utawala na washirika wake. Hapo ikawa wazi kuwa ujumbe wa mazungumzo huko Ankara unaowakilisha wapinzani waliojihami ndio uliokuwa ukieneza sumu ya kukatisha tamaa ndani ya Aleppo wakati wa vitisho vilivyokuwa vikifanywa na Urusi, Iran, na utawala kwa nchi kavu na anga... Jambo hili lilipokuwa wazi, wapiganaji kutoka ndani ya mji wa Aleppo waliujulisha ujumbe wa mazungumzo kuwa hawatajiondoa mjini humo na kwamba wataulinda, na kutangazwa kwa kuanzishwa kwa "Jeshi la Aleppo".

Nne: Urusi ilianza kutangaza habari zinazoonesha kuwa sehemu ya wapiganaji imetii shinikizo la Uturuki, hasa kwa vile uongozi wake wa kijeshi na kisiasa ndio uliokuwa ukifanya mazungumzo na Urusi na Uturuki huko Ankara. Chaneli ya Russia Today ilitangaza tarehe 06/12/2016: "Rudskoy alitaja kuwa takriban wanamgambo 3,500 wa upinzani wastani waliweka chini silaha na kujisalimisha, na 3,000 kati yao walisamehewa". Urusi ilitaja habari zinazofanana na hizo wakati wa mapigano... Yaani huo ulikuwa mchakato wa kutoka mapema mjini kwa makundi tiifu kwa Uturuki na kukabidhi vitongoji walivyokuwemo kwa jeshi la utawala na washirika wake, pamoja na makundi ya Kikurdi yaliyoshirikiana na utawala. Hivyo, makundi hayo yalijitikia ukataji tamaa wa Uturuki, na yakatii shinikizo la moja kwa moja la Uturuki au kupitia ujumbe wa mazungumzo au kupitia viongozi wake wa kijeshi na kisiasa walioko Uturuki, ambao walikuwa wamejizamisha katika mali chafu na yenye sumu iliyotolewa na Uturuki, Saudi Arabia, Qatar na nyinginezo. Wakati makundi hayo yalipoacha kupigana huko Aleppo, iwe ni kwa kuondoka katika hali ya "kujisalimisha" kwa jeshi kwa dhamana ya Uturuki, au kwa kurudi nyuma katika hali ya kushindwa na kuwakatisha tamaa wapiganaji waliobaki wa makundi mengine hasa kusini mwa Aleppo, mchakato wa "kukabidhi" Aleppo ulitokea kweli. Kama si kwa matukio haya, jeshi la mhalifu lisingeweza kuudhibiti mji wa Aleppo kwa kasi namna hiyo, mji ambao ulikuwa ngome ya mapinduzi kaskazini mwa Syria na mwiba mkubwa kooni mwa Marekani. Makadirio ya kijeshi yalikuwa yakiashiria uwezo wa Aleppo kustahimili kwa mwaka mzima. Pia kile kilichotajwa na Asia News tarehe 07/12/2016: ("Kurasa za wapinzani zilinukuu uvujaji kutoka kwa viongozi wao, zikiuelezea kama 'uhaini dhidi ya wapiganaji', ambapo habari za baadhi ya viongozi wa makundi ya wapiganaji huko Aleppo kufanya mazungumzo na Washington ili kujisalimisha na kuuhama mji mzima zilithibitishwa kuanzia Jumatano asubuhi. Jambo hilo waliliita kwenye kurasa zao kama 'makubaliano ya Kirusi-Kimarekani yaliyowalazimisha viongozi kuukabidhi mji wa Aleppo kwa serikali ya Syria na Iran'").

Tano: Katika upande wa kijeshi na sambamba na kampeni kali huko Aleppo, Uturuki ilianza kampeni nyingine katika mji wa Al-Bab dhidi ya ISIS (Daukh), ambayo ilikuwa sumu nyingine iliyoenezwa na Erdogan ili kukamilisha kukabidhiwa kwa Aleppo. Hii ni kwa sababu alikuwa akitengeneza kisingizio na sababu ya ulazima wa kuharakisha kuondoka kwa wapiganaji kutoka Aleppo kutokana na kuwahitaji katika mji wa Al-Bab, sambamba kabisa na kampeni kali dhidi ya Aleppo. Kuwalinda Waislamu huko Aleppo na kuwatetea haku thamani yoyote katika itifaki ya Rais wa Uturuki Erdogan, bali alikuwa na shauku ya kutekeleza miradi ya Marekani, bila kujali matokeo ya jambo hilo hapa duniani na Akhera... Pamoja na ukali wa Uturuki kuyakatisha tamaa makundi tiifu, na shinikizo lake kubwa la kujiunga na vita vya Al-Bab katika operesheni ya "Ngao ya Frati" (Euphrates Shield), jambo hilo liliathiri na kudhoofisha upande wa Aleppo. Ukataji tamaa ulifikia kilele tarehe 08/12/2016 kwa wapiganaji waliokuwa wakilinda kitongoji cha Sheikh Said kusini mwa mji, kitongoji ambacho jeshi na washirika wake hawakuweza kusonga mbele ndani yake na wapiganaji walikuwa wakiwakabili kwa nguvu katika wiki mbili zilizopita... Lakini kujiondoa kwa baadhi ya makundi tiifu kwa Uturuki kwa kisingizio cha kupigana Al-Bab kulivuruga uwanja wa mapambano na kuudhoofisha. Hivyo vitongoji vilivyobaki chini ya udhibiti wa wapiganaji vilipungua hadi vikaishia kusini-magharibi kama sehemu za Salah al-Din na Al-Sukari katika eneo dogo baada ya kurundikana kwa idadi kubwa ya raia waliokimbia kutoka vitongoji vingine. Hapa, na kwa mshituko usio pungua hofu, Uturuki ilitangaza kufikia makubaliano na Urusi kuwaondoa wapiganaji na raia kutoka Aleppo. ("Vyanzo katika upande wa wapinzani wa Syria vilithibitisha kuwa makubaliano yalifikiwa na utawala wa Assad kusitisha mapigano na kuhamisha vitongoji vilivyozingirwa mashariki mwa Aleppo kutoka kwa raia na wapiganaji, na utekelezaji utaanza Jumatano asubuhi. Shirika la habari la Ufaransa lilimnukuu afisa katika kikundi cha Nour al-Din al-Zenki akisema kuwa makubaliano hayo yalifanyika chini ya usimamizi wa Urusi na Uturuki, na utekelezaji wake utaanza katika saa chache zijazo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu alitangaza leo kuwa nchi yake itazidisha mawasiliano yake na Urusi ili kufikia kusitishwa kwa mapigano Aleppo, hasa ili kutoa fursa kwa raia kuondoka...") (Akhbar Al-An, 13/12/2016). Kilichokuwa cha kutisha katika tukio hili la mshituko ni kwamba mwanzoni ilitangazwa kuwa utekelezaji ungekuwa wa haraka sana kati ya saa kumi na moja na saa moja asubuhi. Lengo la hilo lilikuwa ni kuruhusu hisia za kushindwa kutawala kwa namna ya mshituko na kuzuia kufikiria chaguo jingine lolote... Na yote hayo yalikuwa yamefungwa na Uturuki katika kifuniko cha ulazima wa kuokoa raia!

Sita: Makundi yenye silaha tiifu kwa Uturuki yalianza kujiondoa Aleppo katika tukio la kutelekezwa ambalo halikubaliki na Muislamu, na Urusi ikajivunia jambo hilo ("Mkuu wa Majeshi ya Urusi alitangaza Ijumaa Desemba 16, kukamilika kwa mchakato wa kuwatenganisha wapinzani wastani mashariki mwa Aleppo na magaidi"). Mapema Ijumaa, kituo cha uratibu cha Urusi cha upatanishi nchini Syria "Kituo cha Hmeymim" kilitangaza ("Kukamilika kwa shughuli za kuwaondoa wanamgambo na familia zao kutoka mashariki mwa Aleppo. Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilisema kuwa jeshi la Syria linaangamiza vyanzo vya wenye msimamo mkali mashariki mwa Aleppo...") (Russia Today, 16/12/2016). Hapa ndipo ukubwa wa njama ya Uturuki dhidi ya mapinduzi ya Syria ulipoanza kuwa wazi, kwani makundi tiifu kwa Uturuki yaliondolewa, na yakawaacha nyuma watu wa Aleppo pamoja na idadi ndogo ya wapiganaji waaminifu. Hii ilifanyika ili Urusi, Iran na utawala waweze kuwashughulikia wao peke yao na kuweza kuwaangamiza kwa sababu ni "magaidi" kulingana na matamko yaliyotajwa hapo awali ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki na pia taarifa ya kituo cha Urusi cha Hmeymim... Mbele ya matangazo haya ya wazi ya Kirusi ya kuwabana kundi la wapiganaji kwenye kona ili kuwakamata au kuwaangamiza bila kujali idadi kubwa ya raia waliobaki wamebanwa nao kwenye kona hiyo, Uturuki inatangaza kuwa shughuli za uokoaji zinaendelea, licha ya kuwa zimesimama. Hii ni kwa sababu imejikuta katika hali ya aibu sana mbele ya makundi yenye silaha tiifu kwake ambayo yaliondolewa kwa haraka kutoka Aleppo, makundi hayo ambayo yalikubali kujiondoa ndani ya mchakato wa uokoaji wa jumla kwa kila mtu. Na sasa yanajikuta yakiwa yameingizwa mtegoni na Uturuki-Erdogan, ili kutekeleza kile ambacho Marekani na Urusi zinatamani katika kile wanachoita kutenganisha wapinzani wastani na "magaidi"... Hivyo, hali halisi mpya imetengenezwa Aleppo, ambapo inakuwa rahisi kuwalenga wapiganaji waaminifu. Marekani, Urusi, na Erdogan walijivunia mafanikio ya mpango wa Marekani ili kutangaza kuhamisha uwanja wa matukio baada ya hapo hadi mahali pa mbali, Astana mji mkuu wa Kazakhstan!.

Saba: Ama Marekani, ingawa ilikuwa imejificha nyuma ya pazia kwa madhumuni yanayotokana na ufinyu wa muda uliobaki kwa serikali ya Obama, na uhakika wake wa kuwepo kwa mchezaji wa Uturuki ambaye amethibitisha uaminifu mkubwa kwake, licha ya hayo haikuwa mbali kabisa na tukio hilo. Ilikuwa ikichungulia ili kuonyesha furaha yake kubwa:

  • Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan alisema kuwa alijadili hali ya Syria na Iraq na Rais wa Marekani Barack Obama katika mazungumzo ya simu siku ya Alhamisi. Erdogan alisema kuwa Uturuki itaendelea kufuatilia uokoaji wa raia kutoka Aleppo. (Reuters, 15/12/2016).

  • Rais Obama alitoa shukrani kwa Rais Erdogan kwa juhudi za nchi yake katika kupatanisha kusitishwa kwa mapigano huko Aleppo ili kuruhusu uokoaji salama wa wapinzani na raia. (Tovuti ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Twitter, 16/12/2016).

  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani alitoka tarehe 15/12/2016 na kutoa taarifa kuhusu mchakato wa uokoaji kutoka Aleppo, akionyesha kiwango cha kuridhika kwa Marekani na matokeo haya ambayo yalikuwa ndoto kubwa kwake katika kipindi cha "mapumziko ya wasitishaji mapigano" aliyoyatekeleza kwa damu au yale yaliyotangulia katika miaka iliyopita. Kerry alisema: ("Tunachokitaka Aleppo kwa sasa na kabla ya kuendelea mbele ni kusitishwa mara moja na kwa kudumu kwa uhasama, mazungumzo ndiyo njia pekee ya kumaliza vita na wapinzani wameonyesha nia yao ya kurudi kwenye mazungumzo...") (Tovuti ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Twitter, 16/12/2016).

  • ("Al-Qabas ilijifunza kutoka kwa vyanzo rasmi vya ngazi ya juu vilivyohudhuria sehemu ya mkutano uliofanyika Jumamosi iliyopita mjini Paris katika ngazi ya mawaziri wa mambo ya nje kuhusu hali ya Aleppo na Syria kwa ujumla, kwamba kile ambacho Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry alikisema wakati wa mkutano 'kilifikia kiasi cha kuwataka wapinzani wa Syria wa kisiasa na waliojihami kujisalimisha kikamilifu kwa Urusi, Iran na Bashar al-Assad'. Chanzo kilisema katika matamko maalum kwa Al-Qabas kuwa Kerry alitaka wakati wa mkutano huo kuondolewa kwa wapiganaji wote kutoka Aleppo, na kuwasukuma wapinzani wa Syria kwenda kwenye meza ya mazungumzo huko Geneva bila sharti lolote... Chanzo kinaongeza kuwa washiriki walipata aina fulani ya mshituko walipouliza kuhusu chaguzi zinazoweza kutumika kumshinikiza Assad na washirika wake, Kerry akajibu bila kuficha 'Rais wangu - yaani Rais Obama - aliamua kwenda vitani kupigana na ISIS tu...") (Tovuti ya gazeti la Al-Qabas, 13/12/2016).

Nane: Hivyo huu ndio mchezo wa kuigiza wa kinyama, na hizo ndizo zilikuwa zana zake, na hayo ndiyo aliyoyafanya Rais wa Uturuki Erdogan baada ya damu za Waislamu nchini Syria kuwa na thamani ndogo kwake ili kupata radhi za Marekani. Maporomoko ya damu yaliyomwagika Aleppo, na mauaji ya kimbari... sumu hizi zote zilizopenyezwa katika mwili wa mji wa Aleppo zilisababishwa na mali chafu inayochumwa na viongozi wa makundi kutoka Uturuki, Saudi Arabia na nyinginezo. Hivyo viliinamisha shingo zao kwake, na azma zao zikafifia, nao walikuwa wamedai hapo awali kuwa hawatauza watu wala damu. Na hivi leo wako katika masoko ya utumwa huko Uturuki na Saudi Arabia wakitangatanga baada ya sehemu ya kwanza ya mpango wa mauzo kukamilika, na matokeo yake ya uharibifu kuonekana. Je, kuna wa kuzingatia? Na je, kuna asiyeona kuwa kukubali mali ya kisiasa ni kujiua kwenyewe?!

Ama matukio yaliyobaki ya mchezo wa Aleppo baada ya kumalizika kwa "mapumziko ya wasitishaji mapigano" ya Marekani, hayapungui udhalili na aibu kuliko yaliyotangulia. Yeyote aliyebakiwa na chembe ya haya anatakiwa kuivua huko Astana, mji mkuu wa Kazakhstan. Churkin, mjumbe wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, alisema kuwa jukumu la kwanza nchini Syria, baada ya kuikomboa Aleppo, ni "kusitishwa kabisa kwa operesheni za kivita na kuanza tena kwa mazungumzo kati ya pande za Syria". (Russia Today, 16/12/2016). Putin alikuwa ametangaza kabla ya hapo kulingana na chaneli ya Russia Today tarehe 15/12/2016 kuwa alikubaliana na Erdogan kuwasilisha ofa kwa utawala wa Syria na wawakilishi wa makundi yenye silaha kwa ajili ya mazungumzo. Na kama ilivyotajwa na Turk Press tarehe 16/12/2016: ("Rais wa Urusi Vladimir Putin alitangaza kuwa atakutana na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan katika mji mkuu wa Kazakhstan 'Astana' kujadili kuimarisha kusitishwa kwa mapigano nchini Syria. Putin alitaja katika tamko lake kabla ya kuondoka kwenda Japani, kuwa makubaliano ya mazungumzo ya Geneva kuhusu Syria yaliyofanyika kwa msaada wa Umoja wa Mataifa yatatekelezwa. Rais wa Urusi alibainisha kuwa hatua inayofuata itakuwa kusitisha mapigano katika ngazi ya Syria nzima. Putin alieleza kuwa alikubaliana na Rais wa Uturuki kuwasilisha ofa kwa pande za mgogoro nchini Syria kuanza mazungumzo mapya. Rais wa Urusi aliongeza kuwa alifanya juhudi kubwa na mwenzake wa Uturuki hadi kukamilisha kufikiwa kwa kusitishwa mapigano katika mji wa Aleppo, na kurahisisha mchakato wa uokoaji wa waliozingirwa").

Hivyo njia hii, njia ya kukabidhi na kuimarisha utawala wa Assad baada ya kuufanyia ukarabati, ndiyo njia ambayo Uturuki-Erdogan inayaongoza makundi ya wapinzani waliojihami kuelekea kwayo, ikiwa ni sehemu yake ndani ya mpango wa Marekani. Na ikiwa chembe za uaminifu zimepotea kabisa kutoka katika nyoyo za viongozi wa makundi hayo, basi wanaelekea Astana mji mkuu wa Kazakhstan ili kuiweka Syria na nafsi zao kwenye kitanzi kwa thamani ndogo. Lakini ikiwa wamebakiwa na baadhi ya chembe hizo, basi ni lazima waruke haraka kutoka kwenye meli ya Erdogan na kuungana kwa ukweli na watu kabla ya kuwatema, na tayari ameanza... Ama waaminifu katika makundi hayo, ni wajibu wao kuwarudisha viongozi wao kwenye njia sahihi au kuwabadilisha, kwani inawezekanaje mapinduzi ya umma yauzwa na viongozi wa makundi kwa mamilioni kadhaa ya dola kwa adui yao Urusi na Marekani?! Hivyo bila ya kumshughulikia Mwenyezi Mungu, Mtume Wake, na waumini! Ama watu wa Syria, Mwenyezi Mungu amewaandikia mitihani hii ili kupambanua muovu na mwema katika ardhi ambayo ni makazi bora ya Waislamu, na ndani yake kuna kitovu cha dini Yake.

لِيَمِيزَ اللَّهُ الْخَبِيثَ مِنَ الطَّيِّبِ وَيَجْعَلَ الْخَبِيثَ بَعْضَهُ عَلَى بَعْضٍ فَيَرْكُمَهُ جَمِيعًا فَيَجْعَلَهُ فِي جَهَنَّمَ أُولَئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ "Ili Mwenyezi Mungu apate kupambanua walio waovu na walio wema, na akawaweka waovu juu ya waovu wengine, na akawaweka wote pamoja na akawatupa katika Jahannamu. Hao ndio waliopata hasara." (QS Al-Anfal [8]: 37)

Tisa: Mwisho na si kwa uchache, tunamkumbusha Erdogan na kila aliyefanya njama dhidi ya Aleppo na kuchangia katika kusalimu amri kwake na kuwakatisha tamaa wapiganaji ili kuwaridhisha maadui wa Mwenyezi Mungu (swt) na Mtume Wake (saw), tunamkumbusha hadithi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) iliyopokelewa na Ibn Hibban katika Sahih yake kutoka kwa Al-Qasim, kutoka kwa Aisha Mama wa Waumini (ra): Kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alisema:

مَنْ أَرْضَى اللَّهَ بِسَخَطِ النَّاسِ كَفَاهُ اللَّهُ، وَمَنْ أَسْخَطَ اللَّهَ بِرِضَا النَّاسِ وَكَلَهُ اللَّهُ إِلَى النَّاسِ "Yeyote anayemridhisha Mwenyezi Mungu kwa kuchukiwa na watu, Mwenyezi Mungu atamtosheleza na (shari za) watu, na yeyote anayemchukiza Mwenyezi Mungu kwa kuwaridhisha watu, Mwenyezi Mungu atamuacha mikononi mwa watu."

Na huyu hapa ameona na kusikia jinsi watu wanavyozungumza juu yake kwa hasira, bali hata rafiki yake Putin hakumsetiri, bali alimfedhehesha hadharani katika mkutano na waandishi wa habari! Na hakuna ubaya kurudia kile tulichokitaja mwanzoni:

("Rais wa Urusi Vladimir Putin alilipua bomu la kisiasa alipofichua kuwa mchakato wa kuwaondoa wanamgambo kutoka mashariki mwa Aleppo ulifikiwa wakati wa ziara ya Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan huko St. Petersburg mnamo mwezi Agosti uliopita... Rais wa Urusi alisema katika mkutano na waandishi wa habari wa pamoja na Waziri Mkuu wa Japani Shinzo Abe mjini Tokyo, leo 'jana' Ijumaa, kwamba Moscow ilikubaliana na Ankara juu ya mchango wa Uturuki katika kuwatoa wanamgambo hao watakaokubali kuweka chini silaha ili kulinda raia kwanza kabisa. Aliongeza, 'Tukihukumu kutokana na kile ninachokiona, kile kinachotokea ni kile hasa tulichokubaliana na Rais wa Uturuki wakati wa ziara yake huko St. Petersburg'...") (Ilaf, 16/12/2016, Sputnik News, 16/12/2016). Hii ni mbali na adabu iumizayo aliyoiandaa Mwenyezi Mungu kwa kila aliyefanya uhalifu dhidi ya haki ya Umma wa Kiislamu, au aliyechangia kupotea kwa ardhi ya Kiislamu:

سَيُصِيبُ الَّذِينَ أَجْرَمُوا صَغَارٌ عِنْدَ اللَّهِ وَعَذَابٌ شَدِيدٌ بِمَا كَانُوا يَمْكُرُونَ "Itawafika waliofanya uhalifu udhalili mbele ya Mwenyezi Mungu na adhabu kali kwa sababu ya vitimbi walivyokuwa wakivifanya." (QS Al-An'am [6]: 124)

Ama wale waovu, ninawarudishia kile tulichokisema hapo awali: (Na pamoja na haya yote, Aleppo hata ikipata uharibifu kiasi gani itainuka tena, na ardhi ya Sham kwa ujumla na Aleppo al-Shahba haswa itabaki kuwa kisu chenye sumu kooni mwa Marekani, Urusi, wafuasi na vibaraka wao, kikiwanyima usingizi na kuwaua kwa uhalifu wao. Hawatafurahia ushindi wanaodai, kwani kutoweza kuingia katika nchi isipokuwa baada ya kuiharibu ni ushindi wa kudhania tu... Na kutoweza kumshinda mpiganaji isipokuwa baada ya kufa shahidi ni ushindi wa aliyeshindwa... Na kurundika makombora ya uharibifu, mapipa ya baruti na majeshi mbele ya mamia au maelfu machache, na pamoja na hayo wasiweze kuwakabili isipokuwa kwa ndege za kivita na meli za kivita, basi huu ni ushindi wa mwoga aliyepata hofu ya kukutana na wanaume shupavu, na ushindi huu utatoweka... Marekani, Urusi, washirika, vibaraka na wafuasi wanataka kurudia kwa uhalifu wao wa kinyama historia ya ndugu zao waliotangulia miongoni mwa wanamsalaba na Wamongolia (Matatar) kwa yale waliyoyafanya ya uhalifu nchini Iraq na nchi za Sham, lakini hawa hawakuzingatia hatima ya wale. Waislamu waliwang'oa kutoka katika nchi zao na wakainuka tena, na utukufu wa Uislamu na Waislamu ukarudi, na Khilafah yao ikaimarika, na wakaufungua mji wa Hercules na ukawa mji wa Uislamu "Istanbul", na wakakaribia Moscow na wakagonga milango ya Vienna. Na siku hubadilika, na kesho iko karibu kwa anayeisubiri:

وَسَيَعْلَمُ الَّذِينَ ظَلَمُوا أَيَّ مُنْقَلَبٍ يَنْقَلِبُونَ "Na walio dhulumu watakuja jua ni mgeuko gani watakao geuka." (QS Ash-Shu'ara [26]: 227)

19 Rabi' al-Awwal 1438 H 18/12/2016 M

Share Article

Share this article with your network