Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Ni nini kipo nyuma ya hatua ya Saudi Arabia ya kupunguza kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa mafuta?

October 17, 2022
2555

Jibu la Swali

Swali: Kwa nini Saudi Arabia, ambayo ni kibaraka wa Marekani, imeshirikiana na Urusi ndani ya shirika la "OPEC Plus" kupunguza uzalishaji wa mafuta kwa kiasi kikubwa, jambo ambalo linapelekea kupanda kwa bei kinyume na inavyotaka Marekani? Kisha, Marekani imekasirishwa na jambo hilo na kutangaza kutathmini upya uhusiano wake na Saudi Arabia: (Biden ameahidi kuwa kutakuwa na "madhara" kwa Saudi Arabia kwa kusimama upande wa Urusi katika kuunga mkono upunguzaji huo kupitia hatua zinazolenga kutathmini upya uhusiano kati ya Washington na Riyadh... France 24, iliyochapishwa mnamo 2022/10/16). Hivyo, ni nini tafsiri ya mienendo hii yote ikizingatiwa kuwa Saudi Arabia na mtawala wake mkuu Bin Salman ni kibaraka wa Marekani? Na nini kinachotarajiwa kutokana na hili?

Jibu: Ni lazima kwanza kukiri kwamba kile kilichofanywa na Saudi Arabia, kikifuatiwa na Imarati ndani ya shirika la "OPEC Plus" kwa makubaliano na Urusi, kupunguza kwa kiasi kikubwa mafuta yanayotolewa sokoni kwa kiasi cha mapipa milioni mbili kwa siku ni uamuzi wa kushtua kwa Biden na Ulaya. Hii ni kwa sababu nchi hizi zinafanya juhudi kubwa ili kuacha kutegemea rasilimali za nishati za Urusi, na hivyo zinahitaji sana kuona rasilimali zaidi za nishati zisizo za Urusi katika masoko ya kimataifa ili uhaba wa rasilimali hizo usiakisiwe kwenye bei ambazo tayari zimekuwa ghali sana, hasa barani Ulaya. Ili kuweza kujua malengo ya Saudi Arabia kutokana na hatua hiyo, ni lazima kujua ukweli wa mazingira ya kimataifa yanayozunguka hatua hiyo:

Kwanza: Mgogoro wa nishati barani Ulaya

1- (Umoja wa Ulaya miezi michache iliyopita uliidhinisha kifurushi cha sita cha vikwazo dhidi ya Urusi kutokana na vita vyake nchini Ukraine, ambavyo vilijumuisha kupiga marufuku uingizajia wa mafuta kutoka Moscow kuanzia mwezi Desemba ujao. Hakika, uingizajia wa mafuta ghafi ya Urusi katika Umoja wa Ulaya ulipungua hadi mapipa milioni 1.7 kwa siku mwezi Agosti uliopita, ikilinganishwa na mapipa milioni 2.6 kwa siku mwezi Januari... Independent Arabia, 2022/9/12). Marufuku hii ya Ulaya inajumuisha uingizaji wa mafuta ya Urusi yanayokuja kupitia baharini na haijumuishi yale yanayokuja kupitia baadhi ya mabomba. Ili kuonyesha msaada kwa Ulaya, Marekani tayari imefidia nusu ya kiasi cha mafuta ya Urusi ambayo Umoja wa Ulaya uliyaacha hapo awali (kabla ya kifurushi cha sita cha vikwazo).

2- Kwa upande mwingine, Ulaya hasa inateseka na mgogoro wa nishati unaozidi kuwa mbaya, ambapo bei za gesi na umeme zimepanda mara dufu. Hali hii inatokana na utegemezi mkubwa wa Ulaya kabla ya vita vya Ukraine kwa nishati ya Urusi. Ikiwa bei za gesi asilia zinatofautiana kwa mara nne siku hizi kati ya Ulaya na Marekani, basi hili halitumiki kwa mafuta, kwani bei za mafuta karibu zinalingana duniani kote, wakati bei za gesi zinatofautiana kulingana na uwepo wa mabomba ya usafirishaji au vituo vya kusindika gesi oevu (LNG). Hii ina maana kwamba kifurushi cha sita cha vikwazo vya Ulaya dhidi ya Urusi kitasababisha upungufu wa usambazaji barani Ulaya kwa mapipa milioni 1.4 ya mafuta, na hiki ni kiasi kikubwa kinachotarajiwa kupelekea kupanda kwa ziada kwa bei za mafuta. Ikiwa uamuzi wa shirika la "OPEC Plus" wa kupunguza kiasi cha mafuta duniani kwa mapipa milioni 2 kwa siku utaongezwa kwenye hili, basi bei zitakuwa ghali sana.

Pili: Urusi na athari za jambo hilo kwake:

1- Wakati Marekani na nchi za Ulaya zinajaribu kuuzingira uchumi wa Urusi na kuunyima fedha, nchi hizi zingependa kuona mafuta mengi yakitolewa katika masoko ya kimataifa ili kupunguza mapato ya Urusi kutokana nayo. Hata hivyo, uamuzi wa hivi karibuni wa shirika la "OPEC Plus" unafanya mafuta hayo yanayotolewa kuwa machache, jambo linalopelekea uhaba wa usambazaji, kupanda kwa bei, na Urusi kufaidika kifedha, jambo ambalo nchi hizo hazitaki. Ni kweli kwamba Marekani ina malengo ya muda mrefu yanayohusu kukata uhusiano wa Ulaya na Urusi, yaani kubadilisha minyororo ya usambazaji wa nishati, lakini kuinyonga Moscow kifedha pia kunachukuliwa kuwa lengo kubwa la Marekani. Kwa hiyo, inashangaza kuona Saudi Arabia ikifanya kazi kinyume na lengo hili la Marekani.

2- Kutokana na malengo hayo ya Marekani na Ulaya, nchi hizi zinajadili kwa bidii kuweka kiwango cha juu cha bei ya mafuta ya Urusi, pamoja na gesi. Hii ni kwa sababu nchi hizo zimeona kuwa Urusi, ambayo rasilimali zake za nishati katika masoko ya Ulaya zimepungua kutokana na vikwazo, imefanikiwa kufungua masoko mapya ya mafuta yake nchini India, China, na nchi nyingine za Asia. Licha ya bei ya chini ambayo Urusi inauzia nchi hizo mafuta yake, kupanda kwa bei ya mafuta duniani kutokana na vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Urusi kumeiruhusu Urusi kufidia tofauti hiyo. Hii ina maana kwamba mapato ya fedha katika hazina ya Urusi kutokana na mafuta hayajabadilika ikilinganishwa na kipindi cha kabla ya vita dhidi ya Ukraine kwa sababu ya kupanda kwa bei ya mafuta duniani. Kwa sababu ya yote haya, ilikuja wazo la kuweka kiwango cha juu cha bei ya mafuta ya Urusi ili kubana mapato ya fedha ya Moscow wakati usambazaji wa mafuta unabaki wa kutosha katika masoko ya kimataifa ili bei zibaki kuwa za kuridhisha machoni pa nchi hizo. Kuweka kiwango cha juu cha bei ya mafuta ya Urusi bado kupo kwenye hatua ya kupangwa na nchi za Ulaya na Marekani hazijathubutu kukiweka kutokana na athari zake kwenye bei za kimataifa wakati Urusi itakapoacha kusambaza mafuta kwa nchi zinazoweka kiwango hicho cha bei.

Tatu: Uchaguzi wa Bunge la Marekani (Congress)

1- Mnamo 2022/11/08, utafanyika uchaguzi wa katikati ya muhula wa Congress ya Marekani, na Chama cha Republican, chama cha Rais wa zamani Donald Trump, kinatumai kushinda katika uchaguzi huu na kudhibiti mabaraza yote mawili ya Congress; Baraza la Wawakilishi na Baraza la Seneti. Uchaguzi huu ni muhimu kwa sababu matokeo yake ni kiashiria cha uchaguzi wa Rais wa 2024 ambao Chama cha Republican kinapanga kurejea madarakani. Katika mazingira ya mgawanyiko mkubwa unaoikabili Marekani kati ya Chama cha Democrat na makampuni ya teknolojia yanayokiunga mkono, na Chama cha Republican na makampuni ya mafuta yanayokiunga mkono, uamuzi wa shirika la "OPEC Plus" una vipimo vya kina vinavyohusiana na uchaguzi huu. Hiki ndicho kiini cha jambo katika uamuzi wa Saudi Arabia wa kuunga mkono upunguzaji wa uzalishaji wa shirika hilo.

2- Kiini hiki cha jambo ni kipindi hiki nyeti sana kwa Marekani, yaani mwezi mmoja kabla ya uchaguzi wake: (Mnamo tarehe 5 Oktoba, muungano wa nchi zinazozalisha mafuta "OPEC+" ulitangaza kupunguza uzalishaji wa mafuta kwa mapipa milioni mbili kwa siku kuanzia mwezi Novemba ujao, jambo lililopelekea kupanda kwa bei za mafuta kwa takriban asilimia 10, kabla ya kushuka kidogo wiki hii. Anadolu, 2022/10/12). Matokeo haya ya lazima ya uamuzi wa "OPEC Plus", yaani kupanda kwa bei, ndiyo yaliyokusudiwa na uungaji mkono wa Saudi Arabia kwa uamuzi huo. Hii ni kwa sababu bei za mafuta nchini Marekani ni suala nyeti kwa mpiga kura wa Marekani na kwamba kupanda kwake kunabadilisha hisia za mpiga kura huyo na kumfanya amwepuke Rais Biden na chama chake cha Democrat na kumsukuma kuwachagua wagombea wa Chama cha Republican. Kinachoashiria hili ni kwamba Marekani ilikuwa ikiwasiliana na Saudi Arabia na nchi za Ghuba ili uamuzi wa "OPEC Plus" uahirishwe kwa mwezi mmoja, yaani hadi baada ya uchaguzi wa katikati ya muhula wa Congress ya Marekani. (Gazeti la Wall Street Journal lilisema kuwa Saudi Arabia ilikataa kuitikia maombi ya maafisa wa Marekani kuahirisha uamuzi wa kupunguza uzalishaji wa mafuta ndani ya kundi la "OPEC Plus". Gazeti hilo likinukuu vyanzo vinavyofahamu mazungumzo hayo lilisema kuwa maafisa wa Marekani, siku chache kabla ya kuchukuliwa kwa uamuzi huo tarehe 5 Oktoba, waliwasiliana na wenzao katika Ufalme huo na nchi nyingine za Ghuba zinazozalisha mafuta kudai kuahirishwa kwa uamuzi huo kwa mwezi mwingine lakini walikataa. Watu wanaofahamu suala hilo walisema kuwa maafisa wa Marekani walizindua kampeni kubwa ya shinikizo ili kuishawishi Saudi Arabia kuahirisha mipango yake, na maafisa wa White House walipiga simu kadhaa kwa Mrithi wa Kiti cha Enzi, Mwanafalme Mohammed bin Salman, na Waziri wa Hazina, Janet Yellen, alizungumza na Waziri wa Fedha wa Saudi Arabia, kulingana na gazeti hilo... Alhurra, 2022/10/11). Kwa hili, inabainika kuwa uamuzi wa kupunguza uzalishaji wa mafuta uliotajwa ni nyeti sana kwa Chama cha Democrat na utawala wa Biden kabla ya uchaguzi na kwamba utawala huo ulijaribu kuuahirisha lakini haukufanikiwa!

3- Kwa yote haya, inabainika kuwa Saudi Arabia, kupitia uungaji mkono wake thabiti wa uamuzi wa "OPEC Plus" wa kupunguza uzalishaji wa mafuta kwa kiasi kikubwa sana (mapipa milioni 2 kwa siku), haipangi kusaidia hazina ya Urusi ambayo Magharibi inaifanya kuwa adui, wala haipangi kukuza mgogoro wa nishati barani Ulaya. Saudi Arabia ni dhaifu mno kusimama dhidi ya Ulaya isipokuwa kama mabwana zake mjini Washington watatutaka afanye hivyo. Inabainika pia kuwa Saudi Arabia inapanga tu na mabwana zake nchini Marekani ili kupandisha hisa za Chama cha Republican, chama cha Trump. Hili, ingawa linaashiria kuporomoka kwa maisha ya kisiasa nchini Marekani kutokana na mgawanyiko, kuporomoka huku kunakuwa kwa kutisha kiasi kwamba chama kinafanya kazi kwa ushirikiano na pande za nje ili kupiga maslahi ya chama kingine hata kama chama hicho kingine kiko madarakani!

4- Utawala wa Biden ulionyesha chuki yake na hasira yake kwa Saudi Arabia na uamuzi wake. (Biden alisema katika mahojiano na mtandao wa CNN, Jumanne jioni, kwamba kuna "baadhi ya madhara kwa kile walichokifanya (Wasaudi) na Urusi". Aliongeza: "Sitajihusisha na kile ninachofikiria na kile kinachoendelea akilini mwangu, lakini kutakuwa na madhara". Biden aliashiria kuwa "wakati umefika kwa Washington kufikiria upya uhusiano wake na Ufalme (wa Saudi Arabia)". Anadolu, 2022/10/12). Vilevile (Msemaji wa White House, Karine Jean-Pierre, alisema kuwa Rais Joe Biden amekuwa wazi tangu mwanzo wa utawala wake kuhusu hitaji la uhusiano tofauti na Saudi Arabia. Msemaji huyo aliongeza kuwa Washington inatathmini uhusiano na Saudi Arabia na itafuatilia kile kitakachotokea katika wiki zijazo kwa kushauriana na Congress. Aliongeza kuwa uamuzi wa "OPEC Plus" unaonyesha kuwa Saudi Arabia inashirikiana na Urusi kuhusiana na sera za nishati. Al Jazeera Net, 2022/10/12).

Nne: Kuhusu kile kinachotarajiwa, inaonekana kuwa kama ifuatavyo:

1- Upunguzaji wa shirika la "OPEC Plus" wa mapipa milioni mbili ya mafuta kwa siku ni uamuzi unaoshinikiza kwa nguvu usambazaji wa mafuta. Hata kabla ya uamuzi huu, utawala wa Biden ulikuwa umechukua uamuzi wa kutoa pipa milioni moja kutoka kwenye akiba ya kimkakati ya Marekani kwa muda mwezi sita, ili kukabiliana na kupanda kwa bei za mafuta nchini Marekani ili utawala wa Biden usiumie katika uchaguzi wa Congress na kukabiliana na Urusi. (Rais wa Marekani, Joe Biden, alitangaza kutolewa kusiko na kifani kwa mafuta kutoka kwenye akiba ya Marekani, na kuchukua hatua za kuadhibu makampuni ya mafuta kwa kutoongeza uzalishaji kutoka kwenye maeneo ya kukodisha yasiyotumika kwenye ardhi ya shirikisho, kwa mujibu wa White House. White House ilisema: "Baada ya kushauriana na washirika, Rais atatangaza ukombozi mkubwa zaidi wa akiba ya mafuta katika historia, na kuweka pipa milioni moja la ziada sokoni kila siku kwa wastani - kila siku - kwa miezi sita ijayo." CNN Arabic, 2022/3/31).

2- Kwa haya yote, inabainika jinsi Rais wa Marekani anavyojaribu kutuliza masoko ya mafuta ya ndani kabla ya uchaguzi wa Congress wakati ambapo Saudi Arabia inakataa maombi ya Biden ya kuongeza uzalishaji. Kisha, hatimaye mwezi mmoja kabla ya uchaguzi wa Congress, inaunga mkono uamuzi wa "OPEC Plus" wa kupunguza kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa mafuta. Bali Saudi Arabia imefanya zaidi ya hayo, kwani imeongeza mara dufu kiasi cha mafuta inayoyaagiza kutoka Urusi... na data za ufuatiliaji za Refinitiv Eikon zinaonyesha (kwamba Saudi Arabia iliagiza tani 647,000 za mafuta, sawa na takriban mapipa 48,000 kwa siku ya mafuta ya Urusi, iliyoyapokea kupitia bandari za Urusi na Estonia katika miezi ya Aprili hadi Juni, na haya yanaunda mara mbili ya kiasi ambacho ilikuwa imekiagiza cha mafuta ya Urusi katika kipindi hicho cha mwaka 2021. Alhurra, 2022/7/15). Huu ni ushahidi wa njama kubwa inayofanywa na Saudi Arabia kwa makubaliano na makampuni ya mafuta ya Marekani na Chama cha Republican cha Marekani ili kupingana na sera ya Rais Biden kuelekea Urusi na kuelekea bei za mafuta duniani.

Na ikiwa yataongezwa kwenye hayo yote mawasiliano yanayofanywa na vigogo wa utawala wa zamani wa Trump na Saudi Arabia kama vile Jared Kushner, basi inabainika kuwa Saudi Arabia inaratibu sera yake ya mafuta na Chama cha Republican cha Marekani na hasa kundi la Rais wa zamani Trump na makampuni ya mafuta ya Marekani yanayounga mkono Chama cha Republican, na makampuni haya ndiyo yenye ushawishi mkubwa katika mafuta ya Saudi Arabia.

3- Hapana shaka kuwa sera hii ya Saudi Arabia itaiweka katika siku zijazo kwenye shinikizo kutoka kwa utawala wa Biden uliotangaza kuwa uko katika mchakato wa kutathmini upya uhusiano wake na Saudi Arabia baada ya uamuzi wa "OPEC Plus" wa kupunguza kwa kiasi kikubwa uzalishaji. Bali maafisa wa utawala wa Biden wameanza kuhusisha kati ya Saudi Arabia na Urusi: (Rais wa Marekani Biden alisisitiza kuwa "kutakuwa na madhara" kwa Saudi Arabia kutokana na uamuzi wake ndani ya muungano wa mafuta wa OPEC Plus wa kupunguza hisa za uzalishaji, na akasisitiza kuwa wakati umefika wa "fikiria upya" uhusiano na Saudi Arabia, wakati msemaji wa Baraza la Usalama la Taifa la Marekani, John Kirby, alisisitiza kuwa Rais ameamuru kufanyike "tathmini upya" ya uhusiano kati ya Marekani na Saudi Arabia, (Alhurra, 2022/10/12). Vilevile, Seneta mwenye ushawishi wa Chama cha Democrat, Bob Menendez, ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Uhusiano wa Kigeni katika Baraza la Seneti, aliishambulia Saudi Arabia, (akizingatia kuwa Riyadh "inaunga mkono kwa ufanisi Urusi katika uvamizi wake wa kikatili dhidi ya Ukraine". Seneta Richard Durbin kutoka jimbo la Illinois alisema Jumanne asubuhi kuwa "Saudi Arabia inataka waziwazi Urusi ishinde katika vita nchini Ukraine". Aliiambia CNN: "Wacha tuwe wakweli kabisa kuhusu jambo hili, Putin na Ufalme wa Saudi Arabia wako dhidi ya Marekani", akisisitiza kuwa "Saudi Arabia si mshirika anayeweza kuaminiwa". (Alhurra, 2022/10/12). Bila shaka, Saudi Arabia haifanyi mambo haya kwa ajili ya maslahi ya Urusi, kwani ilikuwa imeweka uzito mkubwa dhidi ya maslahi ya Urusi mwaka 2020 wakati wa utawala wa Trump ili kuilazimisha Urusi wakati huo kupunguza uzalishaji (kama ilivyokuja katika jibu la swali "Mgogoro wa mafuta na athari zake" la tarehe 2020/04/29). Kwa hivyo, mtu yeyote akifikiria kuwa Saudi Arabia inaishabikia Urusi dhidi ya Marekani, basi hii ni njozi isiyo na nafasi kwa watawala wa Saudi Arabia ambao ni vibaraka wa Marekani.

Tano: Huu ndio ukweli wa sera ya sasa ya mafuta ya Saudi Arabia ambayo inakinzana waziwazi na matakwa ya utawala wa Biden, lakini inaoana na matakwa ya Chama cha Republican cha Marekani na makampuni ya mafuta ya Marekani yanayokiunga mkono, ambayo kwa upande mmoja yanataka kupandisha bei kwa sababu yanafaidika na hilo, na kwa upande muhimu zaidi yanataka kuwaangusha wafuasi wa Rais Biden wa Chama cha Democrat katika uchaguzi ujao wa katikati ya muhula wa Congress kwa matumaini kwamba Chama cha Republican kitadhibiti mabaraza yote mawili ya Congress, na kurahisisha kwao kurejea kwenye urais pia mwaka 2024.

Na kama Saudi Arabia pamoja na nchi ndogo za mafuta za Ghuba zingetaka kudhibiti masoko ya mafuta katika masoko na bei, zingefanya hivyo kwa maslahi yake na maslahi ya watu wake. Lakini hawa watawala vibaraka hawafikirii mawazo kama haya, kwani wamezama kwenye ukibaraka na unyenyekevu kwa mgeni na wamezama kwenye uadui wa Uislamu na watu wake. Na hakuna atakayefanya mafuta ya Waislamu kuwa silaha mikononi mwao na si mikononi mwa maadui zao isipokuwa Dola ya Khilafah inayokuja hivi karibuni kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.

وَيَوْمَئِذٍ يَفْرَحُ الْمُؤْمِنُونَ * بِنَصْرِ اللَّهِ يَنْصُرُ مَنْ يَشَاءُ وَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ

"Na siku hiyo waumini watafurahi. Kwa nusura ya Mwenyezi Mungu; Humnusuru Amtakaye, Naye ni Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu." (QS. Ar-Rum [30]: 4-5)

Mnamo tarehe 21 Rabi'ul Awwal 1444 Hijiria 2022/10/17 Miladi

Share Article

Share this article with your network