Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Yale Yaliyopokewa katika Hadithi Kwenye Vitabu vya Maimamu Mafaqihi

September 23, 2014
4761

(Silsila ya Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata Bin Khalil Abu al-Rashta, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Wageni Kwenye Ukurasa Wake wa Facebook "Fikhi")

Jibu la Swali

Yale Yaliyopokewa katika Hadithi Kwenye Vitabu vya Maimamu Mafaqihi

Kwa: Alauddin Abdullah

Swali:

Assalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh,

Imepokewa katika kitabu cha Ash-Shakhsiyyah al-Islamiyyah Juzuu ya Tatu, katika mada ya Hadithi Hasan baada ya kuigawanya katika sehemu mbili, yafuatayo (ikiwa ni sehemu ya pili):

"Kwamba msimulizi wake awe ni miongoni mwa watu maarufu kwa ukweli na uaminifu, isipokuwa tu hajafikia daraja ya watu wa hadithi Sahih kwa sababu ya kupungukiwa kwao. Na hadithi Hasan hutolewa hoja kama ilivyo hadithi Sahih sawasawa. Na yale yaliyopokewa katika hadithi kwenye vitabu vya Maimamu na wanafunzi wao na wengineo miongoni mwa wanavyuoni na mafaqihi huchukuliwa kuwa ni miongoni mwa hadithi Hasan na hutolewa hoja kwa sababu wao wameileta kama dalili ya hukumu au wametoa (istinbat) hukumu kwayo, hivyo hiyo ni hadithi Hasan, iwe imepokewa katika vitabu vya Usul al-Fiqh au Fiqhi, kwa sharti ya kuwa viwe ni vitabu vinavyotambulika kama Al-Mabsut, Al-Umm, Al-Mudawwanah al-Kubra na mfano wake, na si kama vitabu vya Al-Bajuri, Ash-Shanshuri na mfano wao. Ama yale yaliyopokewa katika hadithi kwenye vitabu vya Tafsir, basi hayazingatiwi wala hayatolewi hoja kwayo hata kama mfasiri ni Imamu Mujtahid, na hiyo ni kwa sababu yamepokewa kwa ajili ya kufasiri aya na si kwa ajili ya kutoa hukumu, na kuna tofauti kati ya mambo hayo mawili. Na kwa sababu wafasiri kwa kawaida hawajishughulishi na uhakiki wa hadithi wanazozitolea ushahidi, na kwa ajili hiyo hadithi hizi hazizingatiwi kwa sababu tu ya kupokewa kwake katika Tafsir kama ilivyo hali katika vitabu vya Fiqhi vya Maimamu na wanavyuoni, bali ni lazima kufanya utafiti kuhusu hadithi hiyo hata kwa njia ya kufuata (taqlid), kwa kuwauliza watu wa hadithi au kurejea katika kitabu miongoni mwa vitabu vya hadithi vinavyotambulika." Mwisho.

Swali: Tuliwezaje kufikia hitimisho kuwa kile walichokitolea dalili mafaqihi au wanazuoni wa Usul katika vitabu mama vya Fiqhi au Usul kinachukuliwa kuwa ni Hasan? Je, imani yetu juu ya elimu yao na nafasi yao inatosha kuwa kile walichokitoa kama hoja ni sahihi kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), pamoja na kujua kwetu kuwa Maimamu wakubwa wanatofautiana katika elimu ya hadithi?

Na vipi tutaielekeza kauli ya Imamu Shafi’i na Maimamu wengine isemayo: "Ikishasihi hadithi, basi ipigeni kuta kauli yangu" (itupilieni mbali)? Kwani inaonekana ndani yake kuna ishara ya kuhakiki kile anachokisema, kufanya uchunguzi na utafiti ndani yake? Na je, inatosha kupokewa kwa hadithi katika kimoja kati ya vitabu mama vya Fiqhi na Usul vinavyotegemewa, au ni sharti ipokewe katika idadi fulani ya vitabu hivyo? Na ikiwa imepokewa katika idadi fulani, je, haipasi kuwepo kwa vigezo vingine, kama vile kutopokewa tu katika vitabu vya madhehebu mmoja, bali kupokewa katika vitabu mama vinavyotegemewa katika zaidi ya madhehebu mmoja? Mwenyezi Mungu awe msaidizi wenu (Abu Hanifa)

Jibu:

Wa Alaikum Salam Warahmatullahi Wabarakatuh

Ikiwa mwanachuoni au Mujtahid anayetambulika atatolea hoja kwa hadithi, basi ni lazima hadithi hiyo kwake iwe inafaa kutolewa hoja kwayo kwa upande wa kunasibishwa kwake na Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), kwa sababu anaitolea hukumu ya kisheria na haifikiriki kuwa ataitolea hoja hali ya kuwa kwake imeshuka daraja ya kutolewa hoja. Hivyo, kutoa ushahidi kwa Maimamu kwa hadithi, hasa wale wa zamani miongoni mwao, na kutoa ushahidi kwa mafaqihi wakubwa kwa hadithi, kunatufanya tuwe na utulivu katika kuitolea hoja kama walivyoitolea hoja wao, na tuiweke katika daraja ya hadithi Hasan, na hiyo ni kwa kuamini elimu yao na ucha Mungu wao. Na hii haimaanishi kukubali kila hadithi iliyopokewa katika vitabu vya Fiqhi au vitabu vya Usul; kwani tunaweza kuichunguza hadithi iliyotajwa katika vitabu vya Maimamu ikababainika kwetu udhaifu wake kulingana na misingi (usul) yetu, hivyo tusiichukue. Bali tunaweza hata kuichunguza hadithi iliyopokewa katika vitabu vya hadithi vinavyotambulika ikababainika kwetu kuwa ni dhaifu, hivyo tusitoe hoja kwayo.

Lakini kukubali hadithi na kuikataa kuna elimu yake na misingi yake. Imekuja katika kitabu cha Ash-Shakhsiyyah Juzuu ya Kwanza katika mlango wa "Hadithi Inayokubalika na Hadithi Inayokataliwa" yafuatayo: (Inabainika kutokana na mgawanyo wa hadithi kwa watu wake kuwa ni Sahih, Hasan na Dhaifu, kwamba hadithi Sahih na hadithi Hasan ndizo zinazotolewa hoja kwayo, na hadithi dhaifu haitolewi hoja kwayo. Na kile kinachoifanya hadithi ikubalike au ikataliwe ni kuitazama Sanad, Msimulizi na Matni (Matn). Ikiwa haikuondolewa katika Sanad msimulizi ambaye kuondolewa kwake kunapelekea kutokuwa na uadilifu wa yule aliyeondolewa, na msimulizi hakutiwa kasoro, na matni haikuwa yenye makosa wala haipingani na baadhi ya Qur’an au Sunnah Mutawatir au Ijmaa ya kukata (Qat'i), basi hadithi katika hali hii inakuwa inakubalika na inafanyiwa kazi na kuchukuliwa kama dalili ya kisheria, iwe ni Sahih au Hasan.

Ama ikiwa hadithi haiko katika sifa hizi, basi hadithi hiyo hukataliwa na haitolewi dalili kwayo...

Hivyo, pasiwepo na kupituka mipaka (tanattu') katika kuikataa hadithi maadamu inawezekana kuikubali kulingana na matakwa ya Sanad, msimulizi na matni. Hasa ikiwa imekubaliwa na wanavyuoni wengi na imetumiwa na mafaqihi wengi, basi inastahili kukubaliwa, hata kama haijatimiza masharti ya Sahih kwa sababu inaingia katika Hasan. Na kama ambavyo haijuzu kupituka mipaka katika kuikataa hadithi, kadhalika haijuzu kulegea katika hadithi kwa kuikubali hadithi inayokataliwa kwa ajili ya Sanad, msimulizi au matni...) Mwisho.

Na imekuja katika kitabu hicho hicho chini ya mlango wa "Kuzingatia Hadithi Kuwa ni Dalili Katika Hukumu za Kisheria" yafuatayo:

(...Isipokuwa kwamba Khabar al-Ahad ambayo inasihi kuwa dalili ya hukumu ya kisheria ni hadithi Sahih na hadithi Hasan. Ama hadithi dhaifu haifai kuwa dalili ya kisheria kabisa. Na kila anayeitolea dalili hazingatiwi kuwa ametolea dalili kwa dalili ya kisheria. Walakini, kuzingatia hadithi kuwa ni Sahih au Hasan ni kwa yule anayeitolea dalili ikiwa anayo sifa ya kuijua hadithi, na si kwa wahadithiaji (muhaddithun) wote. Hiyo ni kwa sababu kuna wasimulizi wanaochukuliwa kuwa ni waaminifu (thiqa) kwa baadhi ya wahadithiaji, na wanachukuliwa kuwa si waaminifu kwa wengine, au wanachukuliwa kuwa miongoni mwa wasiojulikana (majhul) kwa baadhi ya wahadithiaji, na miongoni mwa wanaojulikana kwa wengine. Na kuna hadithi ambazo hazikusihi kupitia njia moja na zikasihi kupitia njia nyingine. Na kuna njia ambazo hazikusihi kwa baadhi na zikasihi kwa wengine. Na kuna hadithi ambazo hazikuzingatiwa kwa baadhi ya wahadithiaji na wakazitia kasoro, na wahadithiaji wengine wakazizingatia na kuzitolea hoja. Na kuna hadithi ambazo baadhi ya watu wa hadithi walizitia kasoro, na mafaqihi wengi wakazikubali na kuzitolea hoja. Hivyo, kama ambavyo haijuzu kuharakisha kuikubali hadithi bila kuitazama usahihi wake, kadhalika haijuzu kuharakisha kuitia kasoro hadithi na kuikataa kwa sababu tu mmoja wa wahadithiaji amemtia kasoro msimulizi wake, kutokana na uwezekano wa kuwa inakubalika kwa msimulizi mwingine, na kwa uwezekano wa kuwa imetolewa hoja na Maimamu na mafaqihi wengi. Hivyo ni lazima kufanya subira na kuifikiria hadithi kabla ya kuitia kasoro au kuikataa. Na mfuatiliaji wa wasimulizi na hadithi atakuta tofauti katika hilo kati ya wahadithiaji ni nyingi, na mifano ya hilo ni mingi sana.

Kwa mfano: Abu Dawud amepokea kutoka kwa Amr bin Shuaib, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa babu yake amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:

الْمُؤْمِنُونَ تَتَكَافَأُ دِمَاؤُهُمْ، وَيَسْعَى بِذِمَّتِهِمْ أدْنَاهُمْ، وَيُجِيرُ عَلَيْهِمْ أقْصَاهُمْ، وَهُمْ يَدٌ عَلَى مَنْ سِوَاهُمْ، يَرُدُّ مُشِدُّهُمْ عَلَى مُضْعِفِهِمْ، وَمُتَسَرِّيهِمْ عَلَى قَاعِدِهِمْ

"Waumini damu zao ni sawa (katika fidia), na anayetoa dhamana kwa niaba yao ni yule wa chini kabisa miongoni mwao, na aliye mbali zaidi anaweza kutoa ulinzi kwa niaba yao, na wao ni mkono mmoja dhidi ya wengineo; wenye nguvu miongoni mwao huwarudishia walio dhaifu (ngawira), na wanaokwenda vitani huwagawia waliokaa nyumbani."

Msimulizi wa hadithi hii ni Amr bin Shuaib, na Amr bin Shuaib kutoka kwa baba yake kutoka kwa babu yake ndani yake kuna maneno (maqal) maarufu, na pamoja na hayo hadithi yake imetolewa hoja na wengi na imekataliwa na wengineo...) Mwisho.

Na kwa hivyo, hadithi ambayo inatumiwa na mafaqihi wanaotambulika na wanavyuoni wa Usul inahesabiwa kuwa ni miongoni mwa Hasan, na si lazima kwa hadithi iliyopokewa katika vitabu vya mafaqihi wanaotambulika na wanavyuoni wa Usul kuwa ni Hasan ipokewe katika vitabu vingi; inatosha kupokewa kwa kiasi kinachotoa utulivu wa usahihi wa kuitolea hoja, lakini kupokewa kwake katika vitabu vingi na katika madhehebu mbalimbali kunaongeza utulivu katika kuitolea hoja.

Ama kauli ya Shafi’i ni sahihi, na hii haipingani na tuliyoyasema; kwani sisi tunahesabu hadithi ambayo wanavyuoni wanaotambulika wametoa kwayo hukumu ya kisheria, tunahesabu kuwa ni Hasan, lakini hii ni ikiwa hakuna hadithi Sahih yenye nguvu zaidi kuliko hiyo, vinginevyo tutazihukumu dalili kulingana na misingi (usul) inayofuatwa upande wa kukusanya kati ya dalili au kufanya upendeleo (tarjih) kati yake kama inavyojulikana katika mlango wake wa Usul al-Fiqh.

Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu al-Rashta

Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Facebook wa Amir

Kiungo cha jibu kutoka kwenye tovuti ya Amir

Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Google Plus wa Amir

Share Article

Share this article with your network