Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jawabu la Swali: Maana ya Al-Matlub al-Khabari katika Ufafanuzi wa Dalili

June 03, 2016
11204

 (Mfululizo wa majibu ya mwanachuoni mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut Tahrir, kwa maswali ya watembeleaji wa ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi")

 Jawabu la Swali

 Maana ya Al-Matlub al-Khabari katika Ufafanuzi wa Dalili

 Kwa: Abu Hanifa

Swali:

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh, Amir mtukufu, Allah akuhifadhi na kukulinda,

Imekuja katika ufafanuzi wa dalili za misingi (*adillat al-usul*): Ni kile ambacho kinapelekea kwenye elimu kuhusu lengo la kihabari (*matlub khabari*)... Na imekuja katika ufafanuzi wa dalili za matawi (*adillat al-furu'*): Kile kinachopelekea kupitia utafiti sahihi ndani yake kwenye lengo la kihabari (*matlub khabari*)... mwisho. Nini maana ya "*matlub khabari*"?

Je, ishara (*amarah*) inajumuisha suala ambalo dalili imelionyesha kwa njia ya yakini (*qat’i*), na suala ambalo dalili imelionyesha kwa njia ya dhana (*zanni*) baada ya kufanya juhudi katika kuifahamu dalili na kutoa ushahidi wake juu ya suala hilo?

Jazakumullah Khayra.

Jawabu:

Wa Alaykum Salam Warahmatullahi Wabarakatuh,

Hakika dalili katika istilahi ya wana-usul ni "**kile ambacho kinaweza kupelekea kwenye elimu kuhusu lengo la kihabari (*matlub khabari*)**" na kwa mujibu wa mafaqihi ni "**kile ambacho kinaweza kupelekea kupitia utafiti sahihi ndani yake kwenye lengo la kihabari (*matlub khabari*)**".

Istilahi ya "*matlub khabari*" imetajwa katika ufafanuzi zote mbili ili kuepuka "*matlub tasawwuri*" (lengo la kifikra)... Na ili kufahamu maana ya "*matlub khabari*", tunarejea kwa wenye taaluma ya istilahi hizi, nao wanatofautisha kati ya aina mbili za matakwa (*matlub*): Lengo la kifikra (*Al-Matlub al-Tasawwuri*) na Lengo la kihabari (*Al-Matlub al-Khabari*)... Ama lengo la kifikra ni kuwazia hakika ya kitu akilini kupitia ufafanuzi wake...

Kwa mfano: Unaposema "Ulimwengu" kama neno la pekee, na ukasema "Kiumbe" kama neno la pekee, basi kuwazia kwako maana ya ulimwengu na asili yake, na kuwazia kwako maana ya "kiumbe" na asili yake, hayo yanaingia katika lengo la kifikra (*matlub tasawwuri*)... Hivyo lengo la kifikra ni katika mlango wa neno moja moja (*mufrad*)... Lakini baada ya kuwazia maana ya maneno haya ya pekee, ukihusisha moja na jingine uhusiano ambao unaweza kusadikishwa au kukadhibishwa, ukisema kwa mfano: "Ulimwengu ni kiumbe", hapa umenasibisha habari ya "kiumbe" kwa "ulimwengu", yaani umetoa habari kuhusu ulimwengu kuwa ni kiumbe. Kwa maneno mengine, umethibitisha kadhia hii na kuisadiki, yaani umeihukumu kuwa ni kweli, na hili ndilo lengo la kihabari (*al-matlub al-khabari*). Limeitwa lengo la kihabari kwa sababu liko katika mfumo wa unasi-bishaji wa kihabari kwa sentensi ya jina au ya kitendo, na liko katika mlango wa muundo wa maneno (*murakkab*) na si neno la pekee (*mufrad*)...

Na kwa mfano, pombe ni haramu. Kujua kwako maana ya maneno haya, kila moja peke yake, ni kifikra (*tasawwur*). Yaani, kuijua maana ya pombe kuwa ni kinywaji chenye kulevya; ufafanuzi huu haumaanishi uhalali au uharamu, yaani hautoi hukumu, bali ni kuwazia maana akilini... Vivyo hivyo, kuijua maana ya haramu kuwa ni kile kilichokatazwa; neno hili la pekee halimaanishi hukumu bali ni ufafanuzi na ni kuwazia akilini... Na hivyo ndivyo kila neno la pekee, ufafanuzi wake peke yake bila kuliunganisha na jingine ni lengo la kifikra (*matlub tasawwuri*).

Lakini ukinasibisha neno moja na jingine ukasema: pombe ni haramu... Ukisadiki kadhia hii (muundo huu), ukahukumu kuwa pombe hakika ni haramu, au ukakadhibisha kadhia hii kuwa pombe si haramu, basi hili linaitwa katika hali zote mbili kuwa ni lengo la kihabari (*matlub khabari*).

Na kwa mfano: Zaid amesimama. Ukijua maana ya Zaid kuwa ni mtu fulani, na amesimama kuwa ni aliye wima kwa miguu yake, hili linaitwa tasawwur. Ukihukumu kuwa Zaid amesimama, yaani ukasadiki yaliyomo katika kadhia hii, au ukahukumu kuwa Zaid hajasimama, yaani ukakadhibisha yaliyomo katika kadhia hii, hili pia linaitwa lengo la kihabari (*matlub khabari*).

Hivyo basi, lengo la kihabari limejengeka kutokana na malengo mawili ya kifikra. Kwanza unawazia hakika ya kitu fulani akilini, yaani unafahamu uhalisia wake, kisha unawazia hakika ya kitu kingine akilini na kufahamu uhalisia wake, kisha unanasibisha kimoja kwa kingine unasi-bishaji wa kihabari, yaani kwa sentensi ya jina au kitendo, kisha unaihukumu kwa uthibitisho au kukanusha, kwa kusadikisha au kukadhibisha, kwa usahihi au makosa, kwa utekelezaji au kutotekelezwa, basi unasi-bishaji huu unakuwa ndio lengo la kihabari (*matlub khabari*)...

Na lengo la kihabari liko katika mlango wa muundo wa maneno (*murakkab*) na hufikiwa kupitia dalili, iwe dalili hiyo ni ya yakini (*qat'i*) au ya dhana (*zanni*), ya kiakili au ya kimaandishi (*naqli*). Kauli yako "ulimwengu ni kiumbe" ni lengo la kihabari ulilolifikia kwa dalili... Na kauli yako "pombe ni haramu" ni lengo la kihabari ulilolifikia kwa dalili... Na kauli yako "Zaid amesimama" ni lengo la kihabari ulilolifikia kwa dalili...

Ama lengo la kifikra (*matlub tasawwuri*), lenyewe liko katika mlango wa neno moja moja (*mufrad*) na halifikiwi kwa dalili, bali ni kufahamu uhalisia wa neno la pekee na maana yake. Kwa mfano:

"Ulimwengu ni kiumbe" inahitaji dalili ili kuthibitisha hilo kwa sababu unauliza: Ni nini dalili ya kwamba ulimwengu ni kiumbe?... Lakini huulizi: Ni nini dalili ya ulimwengu? Kwa sababu swali hili haliko sahihi... Lakini unaweza kuuliza: Nini maana ya ulimwengu au nini ufafanuzi wa ulimwengu?

Na kwa msingi huo, imesemwa katika ufafanuzi wa dalili kwa wana-usul: Kile kinachopelekea kwenye elimu kuhusu lengo la kihabari... Na kwa mafaqihi: Kile kinachopelekea kupitia utafiti sahihi ndani yake kwenye lengo la kihabari... Hiyo ni kwa ajili ya kuepuka lengo la kifikra (*matlub tasawwuri*) kwa sababu lenyewe halihitaji dalili bali linahitaji kujua maana, yaani kujua uhalisia wake.

Ama swali lako kuhusu ishara (*amarah*)... Hakika mafaqihi hawatofautishi kati ya dalili (*dalil*) na ishara (*amarah*). Dalili kwao inajumuisha ile ya yakini na ya dhana, yaani inatumika kwenye masuala ya yakini na masuala ya dhana... Ama wana-usul, wapo miongoni mwao wanaotofautisha kati ya dalili na ishara. Dalili kwa hawa ni ile tu inayotoa yakini (*qat'i*), ama ile inayotoa dhana (*zanni*) basi haitwi dalili bali huitwa ishara (*amarah*)... Kwa hiyo, ishara katika istilahi ya wana-usul haipatikani isipokuwa katika masuala ya dhana na haijumuishi masuala ya yakini...

Na kwa ajili ya maarifa, katika lugha ishara (*amarah*) wakati mwingine huitwa alama ikiwa haitengani na kitu kinachoashiriwa, kama vile *Alif* na *Lam* zinavyoashiria jina (*Ism*) kwani hazitengani nalo, basi hiyo ni alama yake. Ama ikiwa inatengana na kitu kinachoashiriwa kama vile mawingu kwa mvua, basi hiyo huitwa ishara (*amarah*). Na dalili ni tofauti na ishara (*amarah*) na alama.

Ndugu yenu Ata bin Khalil Abu Al-Rashtah

26 Sha'ban 1437 H

Mtawalia 02/06/2016 M

Link ya jawabu kutoka ukurasa wa Facebook wa Amir: facebook

Link ya jawabu kutoka ukurasa wa Amir wa Google Plus: Googleplus


Link ya jawabu kutoka ukurasa wa Twitter wa Amir: Twitter

Link ya jawabu kutoka tovuti ya Amir

Share Article

Share this article with your network