Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Maana ya Mantiki ya Kuhisi na Hisia ya Kifikra

December 07, 2014
7101

** (Mfululizo wa majibu ya mwanachuoni mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amiri wa Hizb ut Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook "Fikri") **

Jibu la Swali

Kwa: Dhuha Ghufron

Swali:

Assalamu Alaikum wa Rahmatullahi wa Barakatuh, mwanachuoni mtukufu Sheikh wetu, Amiri Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah. Nina swali gumu katika kitabu cha "At-Takattul al-Hizbi" (Mshikamano wa Kihizbu); ambapo neno "mukhilisan" (mwenye ikhlasi) limetajwa katika kauli yake: "Hata kama akitaka asiwe mukhilisi (mwenye ikhlasi), hawezi kufanya hivyo," neno hili lina maana gani? Vilevile, naomba ufafanuzi wa maana ya "mantiki ya kuhisi" (mantiq al-ihsas) na "hisia ya kifikra" (al-ihsas al-fikri).

Shukrani nyingi na Mwenyezi Mungu akulipe kheri kwa kusimamisha Khilafah katika zama zako nawe ukiwa Imam wetu, Amin.

Muhammad Dhuha kutoka Indonesia, wassalaam Alaikum wa Rahmatullahi wa Barakatuh.

Jibu:

Wa Alaikum Salaam wa Rahmatullahi wa Barakatuh,

Inaonekana unamaanisha katika swali lako nukuu ifuatayo kutoka katika kitabu cha At-Takattul al-Hizbi "ukurasa wa 25-26":

(Hiyo ni kwa sababu hisia inayopelekea fikra ndani ya Hizbu, fikra hii huchomoza katika Umma miongoni mwa fikra nyingi, na inakuwa ni miongoni mwazo, na mwanzoni inakuwa dhaifu zaidi, kwa sababu ndiyo iliyozaliwa karibuni na ndiyo kwanza imepatikana, na bado haijajikita, na mazingira yake bado hayajapatikana. Lakini kwa kuwa ni fikra inayotokana na mantiki ya kuhisi (mantiq al-ihsas), yaani ufahamu unaotokana na utambuzi wa hisia, basi huzalisha hisia ya kifikra (al-ihsas al-fikri) yaani huzalisha hisia iliyo wazi kutokana na fikra ya kina. Hivyo, fikra hiyo – kwa tabia yake – humsafisha yule anayeisoma na kuathirika nayo, na kumfanya awe mukhilisi (mwenye ikhlasi), kiasi kwamba hata kama akitaka asiwe mukhilisi hawezi kufanya hivyo.) Mwisho wa nukuu.

Swali lako linahusu maana ya mantiki ya kuhisi, hisia ya kifikra, na kwa nini fikra hii inamfanya mbebaji wake awe na ikhlasi.

Sehemu kubwa ya jibu la swali lako imo ndani ya kitabu cha Mafahim Hizb ut Tahrir (Mofahamu ya Hizb ut Tahrir) ambapo pamebainishwa maana ya mantiki ya kuhisi na maana ya hisia ya kifikra. Imekuja katika kitabu cha Mafahim ukurasa wa 58-59 yafuatayo:

(Wala haijuzu kabisa kutenganisha kitendo na fikra au lengo maalum au imani, kwani katika utengano huu ــ hata uwe mdogo kiasi gani ــ kuna hatari kwa kitendo chenyewe, matokeo yake, na mwendelezo wake. Kwa hivyo, ilikuwa ni lazima kwa lengo maalum kueleweka na kuwa wazi kwa kila anayejaribu kufanya kitendo ili aanze nacho.

Na ilikuwa ni lazima kwa mantiki ya kuhisi kuwa ndiyo msingi, yaani ufahamu na kufikiri viwe vinatokana na hisia na si kwa kudhania tu mambo ya kufikirika, na hisia ya uhalisia iwe na athari katika akili, ikizalisha pamoja na habari za awali ule mchakato wa kiakili ambao ndio fikra. Hili ndilo linalofanikisha kina katika kufikiri na uzalishaji katika vitendo. Na mantiki ya kuhisi hupelekea kwenye hisia ya kifikra, yaani kwenye hisia ambayo inaimarishwa kwa mwanadamu na fikra. Na kwa ajili hiyo, hisia ya wabebaji da'wah kwa mfano, baada ya kuifahamu, huwa na nguvu zaidi kuliko hisia zao kabla ya hapo.) Mwisho wa nukuu.

Mantiki ya kuhisi (mantiq al-ihsas) ina maana kwamba mwanadamu achukue fikra baada ya kuhisi kwake uhalisia moja kwa moja na kusimama juu yake, na si kupitia njia ya kupokea na kufundishwa (kukaririshwa) mambo ambayo usahihi wake haujathibitishwa kikamilifu, na kwa tabia yake si kupitia kudhania mambo ya khayali (kufikirika). Mantiki ya kuhisi ina maana ya kufikiri kulikojengwa juu ya kuhisi moja kwa moja, na mantiki ya kuhisi ina nguvu na imara zaidi kuliko nyingine, kwa sababu imeungana na hisia moja kwa moja. Kwa mfano, utambuzi wa mtu kuhusu kiwango cha kudidimia na kurudi nyuma kimaendeleo inakoishi Afrika kupitia habari anazozipokea, unatofautiana sana na utambuzi wake wa kiwango cha kudidimia huku anapofanya ziara barani Afrika na kujionea moja kwa moja uhalisia ulioko huko, na kufikia kupitia kujionea huku kutoa hukumu ya kurudi nyuma na kudidimia kwa Afrika.

Ama kuhusu hisia ya kifikra (al-ihsas al-fikri), mkabala wake ni hisia tupu, ambayo ni kuhisi uhalisia bila ya kuwa na fikra inayohusiana na uhalisia huo. Ikiwa ana fikra na akahisi uhalisia baada ya kuwepo kwa fikra hii kwake, basi kuhisi kwake uhalisia na uelewa wake kwake kutakuwa, bila shaka, ni imara na thabiti zaidi kuliko hisia yake tupu, yaani hisia yake kabla ya kuwepo kwa fikra. Hivyo, kupatikana kwa hisia baada ya kuwepo kwa fikra inayohusiana nayo huitwa hisia ya kifikra. Kwa mfano, hisia ya mtu juu ya uhalisia wa Afrika baada ya kujua maana ya kudidimia na kutambua tofauti kati yake na mwamko (nahdah), ni yenye nguvu zaidi kuliko hisia yake juu ya uhalisia wa Afrika kabla ya kujua kifikra maana ya kudidimia na maana ya mwamko. Na hisia yake juu ya uovu wa unyonyaji wa nchi za Magharibi makafiri dhidi ya Afrika na kupora utajiri wake inakuwa na nguvu zaidi baada ya kujua kwake kifikra siasa za nchi hizi kuelekea Afrika, kuliko hisia yake juu ya unyonyaji huu kabla ya kuwepo kwa maarifa haya. Na kwa sababu hiyo, vijana wa Hizb ut Tahrir barani Afrika wanahisi kudidimia kwa jamii huko na uovu wa unyonyaji wa nchi zao zaidi kuliko watu wengine, kwa sababu ya utambuzi wao wa maana ya kudidimia na kuona kwao siasa za nchi za kikoloni kuelekea nchi zao na kujua kwao ulafi wa nchi hizi. Ama wengineo, hisia zao juu ya hilo ni dhaifu, bali baadhi yao hata hawajishughulishi nalo.

Na fikra ya mabadiliko inayofikiwa na Hizbu ya kimisingi (ya kimabadi) inakuwa kupitia njia ya mantiki ya kuhisi inayofikisha kwenye matokeo ya kweli na sahihi, na kutokana nayo huzaliwa hisia ya kifikra inayomfanya mbebaji wake auone uhalisia na kuuhisi katika sura yake ya kweli na ya dhati. Kwa hiyo, fikra hii huzalisha, bila shaka, mofahamu za kweli kwa mwenye nayo, na haisimami katika mipaka ya habari za kinadharia tu. Mbebaji wa fikra hii anatambua ukweli wa mambo, hivyo hawezi kuwa kitu kingine isipokuwa mukhilisi na mkweli kama fikra anayoibeba. Hawezi kujidanganya na kujiaminisha kuwa uhalisia ni kinyume na anavyouona, bali yeye auona uhalisia katika uhakika wake, na anajua tiba katika uhakika wake, hivyo hawezi kuwa kitu kingine isipokuwa mukhilisi maadamu anaibeba fikra hii.

Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

Link ya jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amiri wa Facebook

Link ya jibu kutoka kwenye tovuti ya Amiri

Link ya jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amiri wa Google Plus

Share Article

Share this article with your network