بسم الله الرحمن الرحيم
Jibu la Swali
Swali:
Ilitangazwa kuanza kwa vita vya kuikomboa Mosul mnamo tarehe 17/10/2016, nini makusudio yake? Na tunawezaje kuelewa matamshi ya awali ya viongozi wa Marekani waliokuwa wakitabiri vita vya Mosul baada ya miaka mingi? Je, kundi la ISIS litaisha ikiwa litatolewa Mosul? Na kwa nini kuna malumbano haya kati ya serikali ya Iraq na utawala wa Uturuki? Na kwa nini Uturuki inang'ang'ania kushiriki?
Jibu:
1- Yeyote anayetafakari matukio yanayoendelea ataona kuwa ni sehemu ya mfululizo wa matukio yaliyokusudiwa kukamilisha usambaratishaji wa Iraq kwa kuunda jimbo la Masunni na jingine la Mashia, baada ya jimbo la Wakurdi kuwa wazi. Sera hii haikuanzishwa na Marekani leo wala tangu kukalia kwa mabavu Iraq, bali kabla ya uvamizi tangu Marekani ilipoweka kanda zisizoruhusiwa kurushwa ndege kaskazini mwa Iraq mwaka 1991, ambapo eneo la Kurdistan likawa nusu-dola! Na Marekani ilipoivamia Iraq mwaka 2003, mfumo uliowekwa na Bremer, gavana wa Marekani katika Iraq iliyovamiwa, ulikuwa juu ya msingi wa kimadhehebu na kigawanyo cha hisa kwa madhehebu mbalimbali... Bremer aliunda mnamo Julai kile kilichoitwa Baraza la Uongozi la Iraq, na mnamo Agosti 2003 aliteua kamati ya maandalizi ya katiba iliyoundwa na wanachama 25... Kamati hiyo iliandika rasimu ya katiba inayoifanya Iraq kuwa dola ya muungano "fedarali" kwa msingi wa mikoa (majimbo) kama vile jimbo la Kurdistan... Kisha uchaguzi mkuu ulifanyika kupiga kura mnamo Januari 31, 2005 ili kutoa uhalali kwa mchakato wa kikatiba kama ilivyoelezwa katika sheria ya utawala ya mpito. Licha ya mbinu potofu zilizotumiwa zikijumuisha vurugu, ni 58% tu ya wapiga kura waliojiandikisha walipiga kura... Na hivi ndivyo katiba hii ilivyopitishwa! Miongoni mwa vifungu vya katiba hii:
Kifungu cha (1) cha katiba ya Jamhuri ya Iraq ya mwaka 2005 kilisema kuwa (Jamhuri ya Iraq ni dola ya muungano/fedarali)... Na kifungu cha (116) kilisema kuwa (Mfumo wa kifedera katika Jamhuri ya Iraq unajumuisha mji mkuu, mikoa, mikoa isiyo na mamlaka kuu, na tawala za mitaa)... Ama kifungu cha (117/Kwanza) kiliamua kuwa (Katiba hii inatambua wakati wa kuanza kutumika kwake jimbo la Kurdistan na mamlaka yake yaliyopo kama jimbo la kifedera)... Na yeyote anayetazama mamlaka ya jimbo hili anatambua kiwango cha kusambaratika kwa Iraq katika siku za usoni! Hasa kwa kuwa kifungu cha (119) kinasema "uwezekano wa kuanzisha majimbo mengine"... Hivi ndivyo Marekani ilivyopanda mbegu za kusambaratisha Iraq kupitia katiba hii yenye sifa mbaya, bali mbaya zaidi ya sifa yenyewe...
2- Marekani ilihisi furaha ya mafanikio kwa kupitishwa kwa katiba ya kusambaratisha Iraq, na ikawaagiza mawakala wake kuiweka katika vipaumbele vyao ili kuandaa mazingira ya jumla, lakini hawakufanikiwa. Maeneo ambayo sasa yanaitwa maeneo ya Mashia na Masunni hayakuwa na harakati za kujitenga hata kwa jina la majimbo (kanda), kiasi kwamba majina haya ya maeneo ya Kishia na Kisunni hayakuwepo na yalikuwa mageni... Marekani ikaanza kuandaa mazingira kwa njia yake, ikamtegemea Maliki, ambaye ni mtu aliyejaa chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu, na ikamteua kuwa Waziri Mkuu mnamo 20/5/2006. Kazi yake ya msingi ilikuwa kuunda uhasama kati ya Masunni na Mashia kwa njia inayofanya utengano kati yao uwe wenye nguvu! Maliki alikuwa kiumbe cha Marekani na mdhehebu wa kipekee, aliwachochea wengine na kuwakasirisha, mazingira yakawa tayari kwa mgawanyiko na majimbo, na akafanikiwa katika jukumu hili. Maliki alipanda uhasama na Masunni na Wakurdi hadi mgawanyiko wa Iraq ukawa hitaji la watu wengi... Maliki alifanikiwa kuunda uhasama huu na kuandaa mazingira ya majimbo na mgawanyiko, na hiyo ndiyo kazi kuu ambayo Marekani ilimajiri kama Waziri Mkuu kuitekeleza, na ndiyo maana ilimuongezea muda wa utawala hadi Septemba 8, 2014, hivyo siku za utawala wake zilikuwa nyeusi... Hadi ilipofika mwezi Desemba 2011 na Marekani kuondoka kijeshi huku ikibaki kiusalama na kisiasa, mti wa fitina ulikuwa umeshabalehe, na Maliki akauongezea matunda maovu, akawa jeuri na dhalimu kwa namna ya kipekee. Kila moto ulipozima, aliuchochea upya kwa vitendo na maneno ya kichochezi... Na kukaongezeka hamasa ya kimadhehebu katika kuunda makundi ya wanamgambo wa Kishia wenye silaha.
Marekani ilipata alichokitafuta katika utu wa Maliki ili kutanua ufa kati ya Waislamu, kwani alikuwa akikusudia kuwachokoza Masunni kwa kila chuki, vitimbi, dhuluma na ukandamizaji aliojaliwa... Watu walipotaka kuondolewa dhuluma au kupata haki zao, aliwakandamiza na kukataa haki yoyote kwao kama ilivyotokea kwa wakazi wa maeneo ya Masunni walipofanya maandamano ya amani mwaka 2012. Madai yao yalikuwa ya kawaida yakihusu kuondolewa dhuluma, kuachiliwa kwa wafungwa wao hasa wanawake, na kuepuka uvamizi wa usiku wa kiholela... Hakukuwa na dai lolote la kuangusha utawala, lakini serikali ya Maliki iliyakataa na kuyaona kuwa madai yanayowatumikia magaidi, na akaanza kusambaratisha migogoro ya amani ili shinikizo liongezeke kwa watu wa eneo hili na wadai kujitenga au kuanzisha jimbo la kifedera. Maliki na serikali yake hawafanyi hivyo isipokuwa kwa maelekezo au ridhaa ya mabwana zao Wamarekani kwa sababu yeye anaongozwa nao. Sambamba na hilo, baadhi ya harakati za Kishia zilianza kudai kuanzishwa kwa jimbo la Mashia kusini sawa na jimbo la Kurdistan hata kabla ya kuanza kwa maandamano ya amani huko Anbar... Jambo halikuishia hapo, bali nchi jirani zilishindana katika kuibua upande wa kimadhehebu... Yote hayo ni utekelezaji wa sera ya Marekani ambayo haitaki Iraq kuwa na umoja unaojumuisha wote, bali vipande vilivyotengana na vinavyopigana, kila kimoja kikiua kingine! Na kila upande unashikilia kwa meno na kucha ili uwe na jimbo lake, na sasa wito wa majimbo unapiwa hadharani...
3- Katika hali hii, kulikuwa na harakati za kundi la ISIS ili kupata nafasi Mosul. Marekani iliona kuwa kuingia kwake katika mazingira haya pamoja na wanamgambo wa Kishia kutaongeza ufa kwa namna kali zaidi na yenye maumivu, jambo litakalotumikia lengo la Marekani la kuongeza utengano kati ya Masunni na Mashia. Hivyo, ikamfanya Maliki auondoe jeshi kutoka Mosul na kuacha silaha na pesa za benki, na hivi ndivyo ilivyokuwa... Mnamo Juni 2014, ilitangazwa kuanguka kwa Mosul mikononi mwa kundi la ISIS... Simulizi nyingi zimeeleza kuwa jeshi la Iraq lilijiondoa bila kupigana vita vya kweli, bali lilikabidhi silaha, vifaa, sare na kuacha pesa katika benki za Mosul, na wanajeshi, maafisa na vikosi vya usalama walitoroka licha ya kuwa wengi na wenye vifaa bora. Kila mmoja alianza kutilia shaka jambo hilo na kuashiria kuwepo kwa njama na makusudio ya kukabidhi eneo hilo kwa malengo fulani. Maoni haya ya njama yalikuwa na nguvu kiasi kwamba Maliki alikiri kuwa kilichotokea ni njama ("Kilichotokea Mosul kilikuwa ni njama" ukurasa wa Maliki kwenye Facebook, Alhurra ya Marekani 18/8/2015) lakini alijaribu kujiepusha nayo ingawa inamshika yeye, kwani alikuwa Waziri Mkuu na mkuu wa jeshi na mhusika mkuu wa vita hivyo! Jambo kama hilo lilijirudia huko Ramadi kwa kuyaondoa majeshi yaliyokuwepo hapo yaitwayo "Kikosi cha Dhahabu" bila upinzani. Kukaanza madai ya kumuwajibisha Maliki na wahusika, lakini suala hilo likafunikwa na pazia likashushwa... Inaonekana kuwa Marekani iliona ifunge suala hilo kwa sababu mkono wake umezama katika kuuondoa jeshi kwa sababu ilitaka kurahisisha kuwepo kwa kundi hilo kwa kuzingatia kuwa ni la Kisunni, hivyo kuwepo kwake kando ya wanamgambo wa Kishia kunaongeza upana wa ufa kati ya Masunni na Mashia ili kuandaa shirikisho la majimbo... Kwa ajili hiyo iliamuru jeshi liondolewe ili kurahisisha kuingia kwa kundi hilo. Si hivyo tu, bali Marekani ilikataa kushambulia kundi hilo lilipoingia Mosul; Obama alitangaza mnamo 13/6/2014 kuwa Washington "haitashiriki katika hatua ya kijeshi bila kuwepo kwa mpango wa kisiasa uliotolewa na Wairaq," jambo hili ni licha ya mkataba wa usalama uliopo kati ya Marekani na Iraq, na licha ya serikali ya Iraq kumuomba hivyo kama alivyosema Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq, Zebari, huko Jeddah jioni ya Jumatano 18/6/2014 kuwa "Baghdad imeiomba Washington kufanya mashambulizi ya anga dhidi ya wanamgambo," na hayo yalithibitishwa na Mkuu wa Majeshi ya Marekani Jenerali Dempsey katika kikao cha Congress. Hii ina maana kuwa Marekani haina haraka ya kuingilia kati bali inachelewesha hadi mazingira yawe tayari kutekeleza mradi wa majimbo kwa kupasha moto hali kati ya Masunni na Mashia, ili pande zote mbili zikubali jimbo kwa kila upande kama ilivyo huko Kurdistan ya Iraq, na baada ya hapo Marekani iamuru kupigana na kundi hilo na kulitoa Mosul.
Wanasiasa wenye uelewa wanatambua hilo na kulifuatilia, na tunakumbusha hapa habari iliyoripotiwa na tovuti ya "Iraq Today" mnamo 6/12/2015 kutoka kwa vyanzo vya kidiplomasia vya ngazi ya juu vilivyovujisha habari zinazohusiana na sharti la Marekani kumaliza kundi la ISIS nchini humo: "Kukubali kuundwa kwa majimbo makuu matatu yaliyo chini ya utawala wa kifedera huko Baghdad ndio sharti la msingi la kutatua faili la kundi la ISIS na kuisafisha Iraq nalo na kumaliza mamlaka zote ndogo ndogo zinazochukua nafasi ya mamlaka ya Baghdad sasa, hasa wanamgambo wanaoongozwa na amri za Kiirani." Vyanzo hivyo hivyo vilisema kuwa: "... Washington imeahidi kuwa itasimamia ulinzi wa utawala mpya wa kifedera nchini Iraq kwa kuungwa mkono na Baraza la Usalama...".
Hivyo, Marekani ilimtumia Maliki kwa chuki zake za kimadhehebu kumchochea Sunna ili kuunda uhasama kati yao na Mashia, na kisha kuisambaratisha Iraq kwa majimbo na uhusiano dhaifu na kituo ambao hauchukui muda mrefu kabla ya kukatika na kuvunjika... Kadhalika ilitumia mtazamo wa kundi la ISIS kuelekea Mashia ikarahisisha kuingia kwake Mosul ili kuongeza ufa kati ya pande hizo mbili. Marekani imelitumia kundi hilo mara nyingine lilipotangaza Khilafah baada ya kuingia Mosul, ambapo Marekani ilizingatia vitendo vyake vya mauaji, kuchoma moto na kufukuza raia na ikajaribu kuhusisha vitendo hivi na Khilafah, lakini Allah alibatilisha vitendo vyao na watu wakajua kuwa Khilafah ya Baghdadi si lolote isipokuwa ni upuuzi, na kwamba Khilafah ambayo Allah amefaradhisha kufanya kazi kuisimamisha na Mtume ﷺ akabashiri kurejea kwake ni haki na uadilifu... Watu wanahajiria kwake kwa ajili ya amani na usalama, na inaeneza kheri si kati ya wakazi wake pekee bali inaibeba kwa ulimwengu mzima.
4- Ama kuwepo kwa Uturuki kaskazini mwa Iraq, ni kwa ajili ya lengo lile lile, yaani kuwapa "pumzi" Masunni nchini Iraq kama vile Iran inavyowapa "pumzi" Mashia... Hivyo hali ya kikanda inachangia katika kuhimiza majimbo (u-kanda)! Kuingia kwa Uturuki kulikuwa kwa ajili ya kutanua ufa huu ili ionekane kama inawalinda Masunni mkabala na Iran kuwalinda Mashia... Yote hayo ni kufikia lengo moja ambalo ni kurahisisha mgawanyiko.
Kuhusu Uturuki kung'ang'ania kushiriki katika vita hivi na kutokea kwa malumbano kati ya Erdogan na Abadi kuhusu mada hiyo, na Erdogan kulaani madai ya serikali ya Iraq ya kutaka wanajeshi wa Uturuki waondoke katika kambi ya Bashiqa "kaskazini-mashariki mwa Mosul" ingawa ilikuwa kwa ufahamu wa serikali ya Iraq... Jambo hili haliko mikononi mwa serikali ya Iraq wala mikononi mwa serikali ya Uturuki, bali ni kulingana na sera ya Marekani ili Erdogan aonekane kama anawanusuru Masunni katika malumbano yake na Abadi na kisha kuhimiza mradi wa Marekani wa "Majimbo". Kadhalika anafanya Abadi, kwani anaibua mada ya vikosi vya Uturuki bila vikosi vingine vinavyojaza ardhi ya Iraq na anga lake! Hiyo ni kwa ajili ya kujipatia huruma ya Kishia... Na mambo yote mawili ni kwa lengo lile lile, yaani kuongeza shinikizo kati ya Masunni na Mashia ili kutumikia lengo la Marekani la kusambaratisha Iraq katika mfumo wa majimbo... Na kuendelea kwa malumbano haya: kuendelea kwake au kusimama kwake kunaamuliwa na mradi wa Marekani. Hii si mara ya kwanza kwa serikali ya Iraq kudai kuondolewa kwa majeshi ya Uturuki; ilidai mwishoni mwa mwaka jana na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ikakutana kwa ajili hiyo na kuiunga mkono na kupeleka suala hilo katika Baraza la Usalama ili kuchukua uamuzi wa kuilaani Uturuki na kuitaka iondoke, lakini ilikuwa ni dhoruba katika kikombe cha chai na ikazima! Hivyo basi, kubaki kwa vikosi vya Uturuki ni kwa ajili ya lengo hili yaani kutekeleza mradi wa Marekani wa "Majimbo", na jambo hili halijawa siri tena, bali Erdogan alitamka akidai jimbo la Mosul sawa na jimbo la kaskazini, kwani anawalaumu wale waliokubali jimbo la utawala wa mitaa kaskazini mwa Iraq yaani jimbo la Kurdistan lakini hawakukubali kwa namna hiyo hiyo jimbo la Mosul... Alisema katika hotuba yake aliyoitoa huko "Beştepe" kuhusiana na hali ya Mosul: ("...Wale waliopiga kura ya 'Ndio' katika kura ya maoni ya utawala wa mitaa kaskazini mwa Iraq, hawakusema 'Ndio' kwa jambo lile lile huko Mosul." Gazeti la Timeturk 18/10/2016).
5- Ama kwa nini kung'ang'ania huku kwa vita vya Mosul sasa kinyume na matamshi ya awali ya Wamarekani, suala liko hivi:
Marekani ilikuwa ikiona kuwa wakati haujafika wa vita dhidi ya kundi la ISIS na kulitoa Mosul, na Obama hakuwa na haraka ya kumaliza jambo hili katika kipindi chake, bali baadhi ya maafisa wa Marekani walikuwa wakitamka kuwa jambo hili litachukua miaka... Lakini kulitokea mambo yaliyomfanya Obama aharakishe hilo... Obama alikuwa akipenda kumaliza kipindi chake kibaya kwa mafanikio au kitu kinachofanana na mafanikio kitakachokumbukwa kwa ajili yake... Na alikuwa akitegemea huko Syria kupitia makundi ya Iran na wanamgambo wake na kwa kuimarisha mashambulizi ya anga ya Urusi, lakini inaonekana alipoteza matumaini au karibu kutokana na msimamo huu mkuu wa watu wa Syria na hasa Aleppo, hivyo akaelekeza macho yake Iraq kuelekea Mosul labda atapata matumaini huko ya mafanikio au kitu cha mafanikio! Akakimbia kwa haraka kuingia Mosul kiasi kwamba aliacha maeneo nyuma yake yakiwemo Hawija... (Gazeti la Wall Street Journal lilisema kuwa vikosi vya Iraq vinavyoelekea Mosul vilipita baadhi ya maeneo yanayodhibitiwa na kundi la ISIS kama Hawija iliyoko katikati ya mkoa wa Kirkuk, jambo linalowapa wapiganaji wa kundi hilo uwezekano wa kuanzisha mashambulizi ya kushtukiza katika maeneo mengine nchini Iraq. Gazeti hilo lilieleza katika ripoti yake kuwa makamanda wa Iraq hawakuifanya kuikomboa Hawija kuwa miongoni mwa vipaumbele vyao ingawa iko katika barabara inayounganisha Baghdad mji mkuu na Mosul mji wa pili kwa ukubwa nchini humo... Mmoja wa makamanda wa wanamgambo wa Kishia huko Kirkuk - Maitham al-Zaidi - aliielezea Hawija kuwa ni "kisu kwenye ubavu wa kaskazini mwa Iraq," akisema kuwa serikali iliharakisha kuikomboa Mosul kabla ya Hawija kwa sababu za kisiasa na shinikizo za kimataifa... Al Jazeera 28/10/2016).
Hivyo vita vya Mosul vilianza mnamo 17/10/2016 ambapo ilitajwa kuwa wanajeshi 140,000 kutoka jeshi la Iraq, vikosi vya Peshmerga, na vikosi vya uhamasishaji wa kikabila na kitaifa na vinginevyo wanashiriki. Msemaji rasmi wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Peter Cook, alisema: ("Muungano wa kimataifa unaoongozwa na Washington unaunga mkono vikosi vya Iraq kikamilifu wakati wa vita vya Mosul" na akaashiria "kuwepo kwa vikosi vya Marekani katika mistari ya nyuma katika vita vya kuikomboa Mosul kwa lengo la kutoa msaada na msaada wa kilojistiki kwa jeshi la Iraq na vikosi vya Peshmerga..." Reuters 17/10/2016). Marekani ilikuwa imetangaza mwishoni mwa Septemba iliyopita kuwa itaongeza idadi ya vikosi vyake nchini Iraq kwa kuongeza wanajeshi takriban 600 hadi 4400 kufuatia ombi la Waziri Mkuu Haider al-Abadi. Vita vinatakiwa kuendelea wakati wa kampeni za uchaguzi wa Marekani na baada yake, ili Obama amalize kipindi chake kwa kupata ushindi utakaorekodiwa kwa ajili yake na kwa Wanademokrasia katika historia ya Marekani. Ingawa vita vya Mosul si rahisi kutokana na mivutano ya nguvu za ndani kati yao, na kutokana na mivutano ya nguvu za kikanda "Uturuki na Iran" kati yao, ambapo mivutano hii inafanya mapigano ya Mosul kusonga mbele na kusimama... Lakini maadamu sababu yenye ushawishi katika nguvu hizi ni sababu ile ile "Marekani", basi mivutano hii haitarajiwi kusimamisha vita kwa muda mrefu, bali kulingana na kile kinachohitajika na sera ya Marekani...
6- Marekani imeipa Ulaya jukumu, si la kujitegemea, bali kama sehemu ya muungano, hasa Ufaransa na Uingereza, ili zifuate uongozi wa Marekani wa muungano huo, na hiyo ni ili zisibaki mbali na kuvuruga malengo ya Marekani ya vita hivyo ambayo ni kusambaratisha Iraq katika majimbo... Na kama ilivyo ada, Ufaransa inajaribu kujitokeza katika matukio kama haya kutokana na yaliyoisibu kutoka kwa kundi hilo huko Ufaransa, hivyo ikafanya mkutano huko Paris mnamo 20/10/2016 ili kujadili "mustakabali wa kisiasa wa mji wa Mosul", na ikawaalika mawaziri wa mambo ya nje na wawakilishi wa nchi ishirini na mashirika ya ulinzi wa raia. Ikaitisha mkutano mwingine wa mawaziri wa ulinzi katika muungano wa kimataifa dhidi ya kundi la ISIS mnamo 25/10/2016. Kufuatia mkutano huu, Waziri wa Ulinzi wa Marekani Ashton Carter alisema kwa kuzingatia nchi yake ndiyo kiongozi wa muungano: (Majadiliano yalilenga jinsi ya kumaliza udhibiti wa kundi la ISIS huko Raqqa... na kwamba imebainishwa kile ambacho muungano unaweza kufanya ili kuharakisha utekelezaji wa mpango huo na jinsi ya kulinda ardhi ya nchi wanachama kutokana na mashambulizi ya kundi hilo... Al Jazeera 26/10/2016), na hii inaashiria uongozi wa Marekani kwa nchi hizi ambapo inazungumzia kulinda ardhi ya nchi wanachama kutokana na mashambulizi ya kundi hilo.
7- Ama kuhusu je, kundi hilo litaisha ikiwa Mosul itaanguka kutoka mikononi mwake? Haionekani hivyo, bali kundi hilo litakimbilia vita vya kuvizia na mashambulizi hapa na pale na kuendeleza harakati zake nje ya miji. Lilitolewa katikati ya Ramadi lakini lilibaki pembezoni mwake, na hivi ndivyo itakavyokuwa likitolewa Mosul, litabaki likizunguka pembezoni mwake ili kurejea kama lilivyokuwa kabla ya mwaka 2014, na kama lilivyo sasa kivitendo, shirika la kijeshi linalopigana majangwani na milimani na katika pembe za miji na vijiji... Na kutokana na ukosefu wake wa uelewa wa kisiasa, linaweza kufanya vitendo linavyoviona kuwa ni kwa maslahi yake lakini vikatumiwa kwa maslahi ya nchi kafiri za kikoloni, na pengine litatambua hilo...
8- Ama Marekani, haiwezekani kuachana na mpango wake wa kuigawa Iraq katika mashirikisho (fedarali) matatu, bali hilo limekuwa sera ya dola kuhusiana na Iraq. Congress ilipitisha mwaka 2006 mradi unaohusiana na kuigawa Iraq katika majimbo matatu ya kifedera: Kikurdi, Kisunni na Kishia, lakini uamuzi huo haukuwa wa lazima kwa Rais, lakini Rais Bush alitangaza siku hiyo kuwa "hali si rafiki kutekeleza uamuzi huo". Mradi huo wa uamuzi uliwasilishwa na Seneta Joseph Biden ambaye alikuja kuwa Makamu wa Rais wa Marekani Obama mwaka 2009. Biden alikuwa akifanya kazi kwa bidii katika mwelekeo wa kutekeleza uamuzi huo bila kutangaza rasmi jambo hilo na Obama akamkabidhi faili la Iraq... Hivyo Marekani iliandika katiba ya Iraq juu ya msingi huu. Basi vitendo vyake sasa na katika siku zijazo vinaelekea kwenye kutekeleza hilo, hivyo kufuatia kuikomboa Mosul utafuata utafutaji wa mfumo wa kisiasa wa kusimamia maeneo haya yanayoitwa maeneo ya Masunni, na hiyo ndiyo hatua ngumu zaidi kwa sababu maeneo ya Mashia yana ugumu mdogo... Pamoja na hayo, si rahisi mradi huu kupita, kwani huko Iraq kuna wanaume wenye ikhlasi kwa Allah Subhanahu, wakweli kwa Mtume wa Allah ﷺ, na hawatakubali nchi yao isambaratishwe, na watasimama mbele ya miradi hiyo ili kuibatilisha kwa idhini ya Allah Mwenye Nguvu na Mwenye Kushinda.
9- Na mwisho, enyi watu wa Iraq, enyi watu wa nchi ya mito miwili, tunawahutubia kama tulivyowahutubia hapo awali: Uislamu umewakusanya kwa karne nyingi, na bendera yake imewafunika kwa muda mrefu, mkawa wenye nguvu na utukufu, mkigawana kheri pamoja, na mkipigana na shari pamoja... Nchi yenu ni ardhi ya mashujaa, ardhi ya Qadisiyah, ardhi ya Buwaib, nchi ya Harun al-Rashid na al-Mu'tasim, nchi ya Salahuddin, nchi ya wafunguzi wa awali na wa baadaye In Shaa Allah. Hakika Iraq moja ni yenye nguvu kwa watu wake, na Iraq iliyosambaratika ni dhaifu kwa vipande vyake... Na ikiwa Wakurdi wanadhani kuwa kuwepo kwa jimbo la Kurdistan au dola ya Kurdistan kutawapa utukufu, basi hautavuka muda mfupi bali itakuwa ni angamizo kwao baada ya muda... Na ikiwa Masunni wanadhani kuwa kuwepo kwa jimbo kwa ajili yao kaskazini mwa Iraq na magharibi yake kutawapa maisha ya raha, basi hautavuka kipindi kisicho na maana, kisha utafuatiwa na mashaka na dhiki... Na ikiwa Mashia wanadhani kuwa kuwepo kwa jimbo kwa ajili yao kusini kutawapa nguvu yenye ujeuri, basi hautakuwa isipokuwa kwa muda mchache, kisha mambo yatarejea kuwa udhaifu na unyonge.
Enyi watu wa nchi ya mito miwili: Acheni ubaguzi wa kimadhehebu na ukabila:
«دَعُوهَا فَإِنَّهَا مُنْتِنَةٌ»
"Iacheni kwani hiyo inanuka." (Imepokewa na Bukhari kutoka kwa Jabir). Acheni majina ya kimadhehebu na kundi, na shikamaneni na jina ambalo Allah ametuita nalo:
هُوَ سَمَّاكُمُ الْمُسْلِمِينَ
"Yeye (Allah) ndiye aliyekuiteni Waislamu." (Qur'an, Al-Hajj [22]: 78). Basi rejeeni kwake na shikamaneni nalo mtukuke, vinginevyo yatawasibuni madhila kutoka kila mahali:
إِنَّ فِي ذَلِكَ لَذِكْرَى لِمَنْ كَانَ لَهُ قَلْبٌ أَوْ أَلْقَى السَّمْعَ وَهُوَ شَهِيدٌ
"Hakika katika hayo kuna mawaidha kwa mwenye moyo (wa kuzingatia) au akatega sikio naye yupo hapa (anashuhudia)." (Qur'an, Qaf [50]: 37).
29 Muharram Al-Haram 1438 H Sawa na 30/10/2016 M