Jibu la Swali
Swali: Kikao cha ufunguzi wa mazungumzo ya Geneva kuhusu jaribio la kumaliza vita vinavyoendelea Sudan kwa takriban miezi 16 kilifanyika Jumatano (14/08/2024) mbele ya washirika wa upatanishi wa kimataifa: Marekani, Uswisi, Saudi Arabia, Misri, Imarati (UAE), Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa, huku Jeshi la Sudan likikosekana katika mazungumzo hayo. Je, ni nini sababu ya Marekani kuitisha mkutano mjini Geneva kama mbadala wa Jeddah na kupanua ushiriki? Na kwa nini Jeshi halikuhudhuria? Je, wito wa Marekani wa mazungumzo ya Geneva ni kupoteza muda bila nia ya dhati ya kufikia usitishaji vita? Au hilo lina uhusiano na nguvu za Waingereza ambazo bado zinakinzani? Kisha, kwa nini mapambano haya ya mara kwa mara huko Al-Fashir, na nini umuhimu wake kwa pande zote mbili? Shukrani.
Jibu: Ili kuweka wazi majibu ya maswali yaliyotajwa hapo juu, tunapitia mambo yafuatayo, na tunaanza na swali la mwisho:
Kwanza: Tulitaja katika Jibu la Swali la tarehe 19/12/2023:
[...Kwamba mzozo huo hautatatuliwa haraka, na huenda ukachukua muda fulani pia, kwa sababu lengo ni kuuzuia mzozo huo kati ya pande mbili za Marekani huko: uongozi wa Jeshi na uongozi wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF). Matokeo ya mzozo huo yanadhibitiwa na Marekani kwa kugawa majukumu kati yao, na hivyo upinzani unaofungamana na Uingereza na Ulaya unabaki umepooza kama ulivyokuwa tangu mzozo ulipolipuka katikati ya Aprili 2023, na hivyo kudhoofishwa kwa kiwango cha chini kabisa. Ili kufafanua hili, tunaonyesha yafuatayo: Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) mnamo tarehe 21/11/2023 viliteka mji wa Al-Daein, makao makuu ya jimbo la Darfur Mashariki, na pia vikateka makao makuu ya Brigedi ya 20 ya Jeshi huko bila mapigano wakati vikosi vya jeshi vilipojiondoa kwa kisingizio cha kuepuka hatari ya mapigano kati yao na madhara kwa raia! RSF ilidai katika taarifa: ("Kwamba ushindi wake unafungua mlango mpana wa amani ya kweli.. na kwamba jimbo la Darfur Mashariki na Al-Daein vitabaki salama chini ya ulinzi wake." Al-Jazeera 22/11/2023). Ikumbukwe kwamba Al-Daein ni ngome ya kabila la Rizeigat ambalo Dagalo, kamanda wa RSF, na wengi wa makamanda na wanachama wake wanatoka. Kabla ya hapo, vikosi hivi viliteka mji wa Nyala, makao makuu ya jimbo la Darfur Kusini, mji wa Zalingei, makao makuu ya jimbo la Darfur ya Kati, na mji wa El Geneina, makao makuu ya jimbo la Darfur Magharibi. Kilichobaki kwao ni kuteka mji wa Al-Fashir, makao makuu ya jimbo la Darfur Kaskazini na mji mkuu wa kisiasa na kiutawala wa eneo la Darfur. Ikiwa RSF itateka Al-Fashir, itakuwa imepiga pigo kubwa kwa harakati zinazofungamana na Waingereza na Wazungu, hususan Harakati ya Ukombozi wa Sudan na Harakati ya Haki na Usawa...].
Pia tulisema katika jibu hilohilo: [Harakati hizi zimeazimia kuulinda Al-Fashir, la sivyo zitatoweka.. hususan kwa vile mji wa Al-Fashir unashikilia nafasi ya kimkakati ambapo mipaka yake inaungana na mipaka ya Libya, Chad na miji ya magharibi ya eneo la Darfur...].
Kisha tukaongeza: [...Kisha RSF ikaelekea Darfur mbele ya macho ya Jeshi ili kuwa upinzani mkuu nchini. Na huenda Marekani nchini Sudan ikawa na mbawa mbili: bawa la kisiasa la RSF ambalo halitakosa silaha ili kuongoza upinzani, na bawa la kijeshi la Jeshi.. ili mabawa yote mawili yatumikie maslahi ya Marekani.. Ama kuhusu kwa nini upinzani wa RSF hautakosa silaha, hilo huenda ni kwa sababu ya mambo mawili: Kwanza, ili kudhibiti upinzani wa Ulaya unaoundwa na mawakala wa Waingereza, kwani kuuondoa kisiasa si rahisi, bali inahitajika kijeshi... Pili, ili RSF huko Darfur iwe upinzani wa kisiasa wenye nguvu ya kijeshi ili ikiwa maslahi ya Marekani yatapendekeza kujitenga kwingine baada ya Sudan Kusini, basi ifanye hivyo huko Darfur.. Inaonekana kuwa wakati wa kujitenga huku bado haujafika.. bali kuandaa mazingira ya hilo ndilo linaloendelea sasa...] mwisho wa jibu.
Hivyo, Al-Fashir ni muhimu kwa pande zote, kwa Marekani na wafuasi wake (Jeshi na RSF) ina umuhimu ili RSF huko Darfur iwe upinzani wa kisiasa wenye nguvu ya kijeshi, ili ikiwa maslahi ya Marekani yatahitaji kujitenga kwingine baada ya Sudan Kusini, iwe Darfur.
Pia, ni muhimu kwa upinzani wa Ulaya kwani hawajabakiwa na chochote cha kutegemea huko Darfur isipokuwa Al-Fashir. Wakifukuzwa hapo, upinzani huu utatoweka, hususan kwa vile mji wa Al-Fashir unashikilia nafasi ya kimkakati ambapo mipaka yake inaungana na mipaka ya Libya, Chad na miji ya magharibi ya eneo la Darfur... Kwa sababu hiyo, wanapigana huko kwa nguvu, na hii ndiyo imefanya RSF ishindwe kuudhibiti Al-Fashir hadi sasa.. Ingawa Al-Fashir inachukuliwa kuwa ngome ya mwisho ya Jeshi huko Darfur, na ingawa kwa nje wako pamoja na upinzani dhidi ya RSF, lakini hawapigani kwa dhati pamoja na upinzani dhidi ya RSF, la sivyo Jeshi lingewamaliza kwani lina nguvu ya kutosha. Lakini mpango wa Marekani unataka kubaki kwa Jeshi na RSF kwa madhumuni tuliyoyaeleza hapo juu na kuangamiza upinzani wa Ulaya au kuuweka kando!
Pili: Kuhusu maswali juu ya mkutano wa Geneva, tunaupitia kama ifuatavyo:
1- Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Blinken mnamo tarehe 23/07/2024 alitamka akisema: ("Kwamba Washington imeyaalika Jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) kushiriki katika mazungumzo kuhusu usitishaji vita kwa upatanishi wa Marekani yatakayoanza tarehe 14/08/2024 nchini Uswisi" na akasema "Mazungumzo hayo ambayo pia yanasimamiwa na Saudi Arabia yatajumuisha Umoja wa Afrika, Misri, Imarati, na Umoja wa Mataifa kama waangalizi." Alisema "Mazungumzo hayo yanalenga kusitisha ghasia nchini na kuruhusu misaada ya kibinadamu kuwafikia wote wanaohitaji na kuweka utaratibu thabiti wa ufuatiliaji na uhakiki ili kuhakikisha utekelezaji wa makubaliano yoyote" na akaashiria kuwa "Mazungumzo hayo hayatashughulikia masuala mapana ya kisiasa"... France-Presse, 23/07/2024). Ambapo Marekani haikutaka duru za awali za mazungumzo yaliyofanyika Jeddah zizae matunda yoyote kwa makusudi, kwa sababu haikutaka kusitisha mapigano kati ya pande hizo mbili. Tamko la Blinken kuwa "mazungumzo hayatashughulikia masuala mapana ya kisiasa" linamaanisha kuwa mkutano wa Geneva hautasababisha usitishaji wa mapigano kati ya pande hizo mbili, bali ni mazungumzo kwa ajili ya mazungumzo tu! Tamko la msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Matthew Miller linathibitisha hilo, kwani alisema ("Kwamba hawezi kutathmini uwezekano wa kufikia makubaliano lakini tunataka tu kurudisha pande hizo mbili kwenye meza ya mazungumzo" akiongeza "Tunatumai hii itakuwa fursa ya kufikia usitishaji vita hatimaye"... Independent, 24/07/2024). Vilevile, Uingereza ilikuwa inatambua kuwa mazungumzo ya Geneva yaliyoitishwa na Marekani hayatapata suluhisho. Mjumbe wa Umoja wa Mataifa Ramtane Lamamra katika mkutano wa Baraza la Usalama mnamo 29/07/2024 kuhusu mkutano wa Geneva alioitisha Marekani kuufanya tarehe 14/08/2024 aliyataja majadiliano ya Geneva kuwa ni ("hatua ya kwanza ya kutia moyo katika mchakato mrefu na mgumu zaidi"... Asharq Al-Awsat, 29/07/2024). Yaani, anatangaza kuwa hakutafikiwa suluhisho katika mkutano huu, bali ni kwa ajili ya porojo pembezoni mwa Mto Rhone huko Geneva! Ikumbukwe kwamba mjumbe Ramtane Lamamra, waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Algeria, ni mmoja wa mawakala wa Uingereza anayefanya kazi ya kuushirikisha Umoja wa Ulaya na mawakala wa Waingereza katika mazungumzo yanayohusu Sudan kama ilivyotokea katika mkutano wa Djibouti uliofanyika tarehe 26 na 27/07/2024 ambapo zaidi ya nchi 20 zilishiriki pamoja na Umoja wa Ulaya. Ni vyema kutaja kuwa Marekani iliweza kuzuia kuteuliwa kwa Ramtane Lamamra kama mjumbe nchini Libya, lakini Uingereza iliweza kumteua kama mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan.
2- Hivyo, mara tu Marekani ilipoitisha kupitia kwa Waziri wake wa Mambo ya Nje mkutano nchini Uswisi, RSF iliharakisha kuitikia mara moja. Kufuatia tamko hili na jioni ya tarehe 23/07/2024, kamanda wa RSF Mohamed Hamdan Dagalo alikaribisha wito wa Blinken kupitia mtandao wa X akisema: "Tangazo la ushiriki wetu katika mazungumzo yajayo ya usitishaji vita mnamo Agosti 14, 2024 nchini Uswisi." Hii ina maana kuwa Dagalo alikuwa na habari kuhusu wito huu mapema, na alijua sababu zake kupitia njia za Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, kwa sababu hakusita kuitikia. Ingawa kamanda wa jeshi na mwenyekiti wa Baraza la Uongozi Al-Burhan naye alikuwa na habari, lakini makubaliano yalikuwa ni ajikwaze na jibu lake lichelewe, ili aonekane kana kwamba ana mamlaka (sovereignty) na anaweza kupinga. Kwa hiyo aliomba mkutano na Marekani kwa ajili ya mashauriano kuhusu mkutano wa Geneva kana kwamba Al-Burhan anaweza kukubali au kukataa bila idhini ya Marekani! Kisha akatangaza kushindwa kwa mashauriano haya: [Ilitangazwa rasmi kukwama kwa mashauriano ya Sudan na Marekani, yaliyoandaa ushiriki wa jeshi katika mazungumzo na RSF. Mashauriano hayo yalifanyika katika mji wa Jeddah nchini Saudi Arabia; kuitikia ombi la serikali inayoungwa mkono na uongozi wa jeshi ambayo makao yake makuu yako Port Sudan, jambo ambalo linatishia kushindwa kwa tukio la Geneva kabla halijaanza katika tarehe iliyopangwa ya Jumatano ijayo.. Kwa mujibu wa vyanzo vinavyoaminika, hoja kuu za tofauti zilizopelekea kushindwa kwa mashauriano hayo ni kukataa kwa ujumbe wa Sudan kushiriki kwa (IGAD) na nchi ya Imarati (UAE) kama "waangalizi", na kwamba ushiriki katika mazungumzo uwe kwa jina la serikali na si jeshi, na uanze na utekelezaji wa "Azimio la Kibinadamu la Jeddah" kabla ya kuingia katika mazungumzo mengine yoyote. "Mkuu wa ujumbe" Abu Namu aliacha jambo hilo likining'inia, na hakutoa uamuzi wa mwisho kuhusu ushiriki katika mazungumzo, bali aliuacha kwenye tathmini ya uongozi akisema: "Jambo hilo vilevile limeachwa mwishowe kwa uamuzi wa uongozi na tathmini yake." Asharq Al-Awsat, 13/08/2024].
3- Hivyo, mashauriano ya Jeddah yalishindwa kukubaliana kuhusu mkutano wa Uswisi na kutengeneza sababu ya hilo kuwa ni je, mwaliko ni kwa jeshi au serikali! Kana kwamba Al-Burhan angeweza kukataa ombi la Marekani la mkutano wa Geneva kama ingekuwa na dhati na hilo! Bali ni katika mlango wa kuzishughulisha pande husika na suala la mazungumzo hadi Marekani itakapomaliza ushawishi wa Ulaya nchini Sudan, na kufikia suluhisho inalotaka ili iwe kichocheo chanya kwake katika uchaguzi ujao.. Ama kwa nini kusuasua huku kwa Marekani hadi sasa bila kupata suluhisho la tatizo la Sudan, ni kwa sababu pande za Ulaya na Waingereza bado zina nguvu nchini Sudan. Kama tulivyotaja hapo awali, Marekani ilifanya kazi ya kuonyesha mzozo kati ya Al-Burhan na Hemedti ili kuweka kando nguvu za Ulaya, lakini hadi sasa haijafikia lengo hili kwani shughuli za Waingereza zimeimarika nchini Sudan kupitia nchi ya Imarati, baada ya kushindwa kupitia Kenya ambayo ilidai kuingizwa kwa vikosi vya amani kusitisha mapigano na kushirikisha mrengo wa kiraia unaoundwa na mawakala wa Waingereza katika mazungumzo. Walishindwa katika yote mawili "kusitisha mapigano na kushirikisha mrengo wa kiraia".
4- Serikali ya Sudan na Al-Burhan wanatambua hilo. Wajumbe wa Sudan na Imarati katika Umoja wa Mataifa walirushiana maneno makali wakati wa kikao cha Baraza la Usalama mnamo 18/06/2024 ambapo mjumbe wa Sudan Al-Harith Idriss Al-Harith alisisitiza kuwa ("Ana ushahidi wa Imarati kuunga mkono RSF" na mjumbe wa Imarati Mohamed Abushahab akajibu kuwa ni "tuhuma za uongo" na kusema: "Hakutakuwa na ushindi au suluhu ya kijeshi kwa mzozo nchini Sudan na kwamba meza ya mazungumzo ndiyo njia pekee ya suluhu"... CNN, 19/06/2024). Kwa tamko hili, Imarati inatangaza kuwa inaingilia mzozo unaoendelea Sudan. Hilo lilitanguliwa na kufukuzana kwa wanadiplomasia kati ya pande hizo mbili. Uingereza ilianza mchezo uleule ambao Marekani inaucheza dhidi ya mawakala wake ili kuwadhibiti, kwa kuwafanya wawe chini ya amri ya Jeshi au chini ya amri ya RSF. Hivyo, Uingereza kupitia Imarati ilianza kuunga mkono RSF ili kuwalinda mawakala wake na kuimarisha uwepo wao, ili RSF isiweze kuwaondoa au kuwadhibiti. Mawakala wa Uingereza kwa jina la muungano wa "Taqaddum" chini ya uongozi wa Abdalla Hamdok, waziri mkuu wa zamani wa Sudan aliyepinduliwa na Al-Burhan na Hemedti mnamo 2021, walianza harakati za waziwazi. Ofisi ya mwendesha mashtaka wa Sudan mnamo tarehe 03/04/2024 ilitoa uamuzi wa kuwakamata viongozi 16 wa muungano huo wakiongozwa na Hamdok na kuwataka wajisalimishe kwa mwendesha mashtaka kwa tuhuma za ("kusaidia, kutoa msaada, makubaliano na jinai zinazoelekezwa dhidi ya nchi, kudhoofisha mfumo wa kikatiba, jinai za kivita na mauaji ya kimbari"... Televisheni ya Sudan, 03/04/2024). Lakini haikumkamata yeyote na hakuna hata mmoja wao aliyejisalimisha, jambo linaloonyesha udhaifu wa utashi wa utawala wa Al-Burhan mbele ya mawakala wa Waingereza.. Kisha Abdel Fattah al-Burhan anakataa hata kufanya mazungumzo nayo: ["Al-Burhan, mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Sudan, mnamo Alhamisi alitangaza kukataa kwake kufanya mazungumzo na Muungano wa Nguvu za Kiraia za Kidemokrasia (Taqaddum)..". Anadolu, 06/06/2024]
5- Kuunga mkono kwa Imarati kwa RSF kunalenga maslahi ya bwana wake Uingereza nchini Sudan, na si kwa sababu kamanda wa RSF Dagalo ni wakala wa Uingereza, bali yeye ni wakala wa Marekani. Hivyo Uingereza inataka kufelisha mpango wa Marekani nchini Sudan kwa kujipenyeza kando ya Dagalo na RSF yake. Kama ilivyofanya nchini Libya ambapo ilimpa nafasi wakala wake Imarati ili ajipenyeze kwa Haftar, wakala wa Marekani, na kumpa msaada ili kumuathiri na kufelisha harakati zake dhidi ya mawakala wa Uingereza katika mji mkuu Tripoli. Na mfano wa hilo iliipa nafasi nchini Yemen, ambapo Imarati ilijipenyeza katika muungano ulioundwa na Marekani ukiongozwa na Saudi Arabia katika operesheni ya Decisive Storm kuingilia kati Yemen. Uingereza ikatumia fursa hiyo kuwaunga mkono mawakala wake na kuwawezesha kudhibiti kusini mwa Yemen na kuwafukuza Wahouthi, mawakala wa Marekani kutoka huko. Karibu ingeidhibiti Hodeidah na kisha kuelekea Sana'a kuwaangusha Wahouthi lau si propaganda iliyoanzishwa na Marekani kuwa watu wa Hodeidah wanakufa kwa njaa na magonjwa, hivyo mkutano wa Stockholm ukafanyika tarehe 13/12/2018 na kusitisha maendeleo ya Imarati na washirika wake kutoka kusini mwa Yemen... Huu ndio udanganyifu wa Uingereza katika siasa za kimataifa!
6- Hivyo, Marekani inasuausu kupata suluhisho, kisha RSF inakubali na Jeshi linakataa na kinyume chake... Mazungumzo yanahama kutoka Jeddah kwenda Cairo hadi Geneva si kwa ajili ya kupata suluhisho bali ni kusuasua katika kupata suluhisho: (...Baraza la Uongozi la Mpito linalotawala lilisema katika taarifa "Kufuatia mawasiliano na serikali ya Marekani iliyowakilishwa na mjumbe wa Marekani nchini Sudan Tom Perriello, na mawasiliano kutoka serikali ya Misri kwa ombi la mkutano na ujumbe wa serikali mjini Cairo kujadili dira ya serikali katika utekelezaji wa makubaliano ya Jeddah, serikali itatuma ujumbe mjini Cairo kwa lengo hili" na likaongeza kuwa makubaliano ya Jeddah yanataka kuondoka kwa vikosi vya RSF katika maeneo ya raia... Arabi21, 19/08/2024].
7- Muhtasari:
a- Kuna uwezekano wa kutolewa maamuzi ya kupotosha yanayotaka kusitishwa kwa mapigano kati ya Jeshi la Sudan na RSF katika mkutano wa Geneva mnamo 14/08/2024, ambao umepangwa kuendelea kwa siku 10: (Imepangwa kuwa mazungumzo ya "Geneva" yaendelee kwa muda wa hadi siku kumi chini ya usimamizi wa Marekani na Saudi Arabia... Al-Jazeera, 14/08/2024) lakini yatakuwa tu bila ufanisi bali yatabaki kuwa wino kwenye karatasi. Na yakitokea, basi ni ya muda hayadumu; kwani Marekani bado haijafikia malengo yake. Itatosheka tu na kutilia mkazo ufikishaji wa misaada ya kibinadamu. (Serikali ya Sudan ilitangaza kuwa itaruhusu kupita kwa misaada ya kibinadamu kupitia mpaka wa Adre ulioko mpakani na Chad.. Na pande saba za kimataifa zilizoshiriki katika mkutano wa Geneva zilikaribisha hatua hii... Sky News Arabic, 17/08/2024).. (Marekani imeyataja mazungumzo ya Geneva kuwa ni mfano mpya ikisisitiza kuwa lengo la majadiliano hayo ni kupanua wigo wa ufikishaji wa misaada na kufungua tena njia za kibinadamu. Al-Jazeera, 20/08/2024).
b- Kutoweza kwa Marekani kuiondoa Uingereza katika ulingo nchini Sudan bado kupo, hususan kupitia mawakala wake wa kikanda kama Imarati na mawakala wake wa ndani kama muungano wa "Taqaddum". Hilo limeifanya Marekani kufanya upya mahesabu yake na kuishirikisha Imarati katika mkutano wa Geneva, ingawa hapo awali ilidhibiti shughuli zinazohusu Sudan kati yake na wakala wake Saudi Arabia katika jukwaa la Jeddah bila kuzingatia nguvu za Ulaya (Freedom and Change). Hivyo wakati (Taqaddum) ilipoonekana kuwa na ufanisi zaidi kuliko (Freedom and Change) na ikiwa na Imarati nyuma yake, Marekani iliona ni vyema kuishirikisha Imarati katika mkutano huo kama sehemu ya ujanja na upotoshaji bila ya kuwa na dhati kweli katika kupata suluhisho la kusitisha mapigano!
c- Hayo yote ni hasara kwa watu wa Sudan ambao ni Waislamu, na mwuaji na mwuawa miongoni mwao ni kama alivyosema Mtume wa Allah ﷺ:
«إِذَا الْتَقَى الْمُسْلِمَانِ بِسَيْفَيْهِمَا فَالْقَاتِلُ وَالْمَقْتُولُ فِي النَّارِ»
"Waislamu wawili wakikutana kwa panga zao, basi mwuaji na mwuawa (wote wawili) wamo motoni."
Ni wajibu kwa watu waaminifu jeshini na kwa wananchi kuchukua hatua ya kuangusha njama hizi zote na kuwaondoa mawakala, kwani wao ndio msingi wa balaa na kupitia kwao wakoloni wanaweza kutekeleza njama hizi zote.. Ni wajibu pia kwa waaminifu wote kuchukua hatua ya kuinusuru Hizb ut-Tahrir, uongozi wa kisiasa wa mwaminifu ambao haujaacha kufichua njama hizi kwa miongo kadhaa na maoni yake yamekuwa sahihi kila wakati. Hivyo, ni wajibu kwa waaminifu miongoni mwa watu wenye nguvu kuinusuru Hizb ut-Tahrir kwa ajili ya kuinusuru dini ya Allah na kuipa utukufu.
﴿وَلَيَنصُرَنَّ اللهُ مَن يَّنْصُرُهُ إِنَّ اللهَ لَقَوِيٌّ عَزِيزٌ﴾
"Na bila shaka Allah atamsaidia yule anayeisaidia (Dini) Yake. Hakika Allah ni Mwenye nguvu, Mwenye ushindi." (Al-Hajj: 40)
15 Safar 1446 H 20/08/2024 M