Home About Articles Ask the Sheikh
Dhana

Jawabu la Swali: Dhana ya Thamani (Al-Qimah)

May 19, 2017
6527

Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizbut Tahrir, kwa Maswali ya Wafuasi wa Ukurasa Wake wa Facebook "Fiqhi"

Kwenda kwa Abu Muhammad Sheikh Hamid

Swali:

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh,

Barakallahu fiika ewe Sheikh wetu mpendwa, Mwenyezi Mungu akusaidie na akunusuru.

Nina maswali kuhusu dhana ya thamani (value). Thamani ni kiasi cha manufaa kilichomo ndani ya kitu, kwa kuzingatia sababu ya uhaba (scarcity factor).

  1. Ni zana gani ninazotegemea kama mtaalamu wa bidhaa fulani ili kubainisha manufaa yaliyomo katika bidhaa hiyo?

  2. Je, kubainisha manufaa kunakuwa kwa kuelezea tu manufaa hayo, au yanathaminiwa kwa dhahabu, fedha, au kwa jitihada? Ikiwezekana, taja mfano wa jambo hilo.

  3. Je, manufaa haya yaliyomo katika bidhaa yana thamani gani na yanatambuliwaje?

  4. Nitashughulikaje na — sababu ya uhaba (scarcity factor) — katika kubainisha thamani, na kuna uhusiano gani nayo?

  5. Je, utafiti wa thamani ni sehemu ya tafiti za Nizamu ya Kiuchumi (Mfumo wa Kiuchumi) au Elimu ya Uchumi (Economic Science)?

  6. Nini umuhimu wa kufanya utafiti kuhusu mada ya thamani na ni faida gani zinazotokana na utafiti huo?

Mwisho, Barakallahu fikum na Mwenyezi Mungu awalipe kheri na awaunge mkono kwa ushindi wa karibu, hakika Yeye ndiye Mlinzi wa hilo na Muweza wa hayo. Allahumma Amin Amin.

Jibu:

Waalaykum Salam Warahmatullahi Wabarakatuh.

1, 2, na 3 - Kuhusu kujua thamani na zana zinazotegemewa katika kuibainisha, thamani hiyo ni manufaa kwa mwanadamu kama mwanadamu katika kutosheleza mahitaji yake ya kimsingi. Hali kadhalika kwa bidhaa ambazo zina thamani ndani yake zenyewe kama dhahabu na fedha. Thamani kwa kawaida hubainishwa kwa kulinganishwa na bidhaa nyingine na si kwa kiasi cha bei yake. Kwa mfano, thamani ya mkate inapita thamani ya kitu kinacholevya hata kama kileo hicho kitakuwa na bei ghali zaidi, na kadhalika.

Hili linaweza kufafanuliwa kama ifuatavyo: Thamani ya kweli ya bidhaa ni kiasi cha manufaa kilichomo ndani yake..., na thamani hii ni thabiti haibadiliki, kwa sababu manufaa yake yapo ndani ya bidhaa yenyewe. Tukitaka kukadiria thamani katika muamala miongoni mwa miamala, hii inaitwa thamani halisi (actual value), yaani ile inayorejelewa wakati wa usuluhishi au mahakamani. Tunaiwakilisha kwa bidhaa inayojulikana kwa pande zote mbili wakati wa makadirio, au kwa sarafu inayoheshimika kwa pande zote mbili wakati wa makadirio ambayo ina thamani ndani yake yenyewe kama dhahabu au fedha. Hivyo, tunasema inalingana na kiasi fulani cha kilo za ngano kwa mfano, au inalingana na kiasi fulani cha gramu za dhahabu, au kiasi fulani cha dirham za fedha. Yaani, makadirio ya thamani yanakuwa kwa kitu chenye manufaa ndani yake chenyewe, hivyo thamani haikadiriwi kwa kitu kisicho na manufaa ndani yake chenyewe kama pesa za karatasi kwa mfano... Makadirio haya yanafanywa kulingana na kulinganisha manufaa ya bidhaa inayofanyiwa utafiti na manufaa ya vitu tulivyovikadiria wakati wa makadirio. Iwe ni thamani ya kweli au thamani halisi inayofanyiwa utafiti, thamani hiyo inabaki kuwa thabiti na haibadiliki baada ya muda wa makadirio, kwa sababu ni thamani...

4- Kuhusu namna ya kushughulika na sababu ya uhaba (scarcity factor) "iliyotajwa katika ufafanuzi" na uhusiano wake na kubainisha thamani, tulishawahi kujibu suala hili na tunakurejeshea nukuu ya jibu hilo:

(Kuhusu ufafanuzi wa thamani kuwa ni kiasi cha manufaa kilichomo katika bidhaa kwa kuzingatia sababu ya uhaba, basi ndio, ni sahihi. Na kutozingatia sababu ya uhaba kama sehemu ya makadirio pia ni sahihi. Kuhusu kwa nini imetajwa, basi huu hapa ni ufafanuzi wake:

Kuzingatia sababu ya uhaba si sehemu ya makadirio ya thamani, bali ni kwa ajili ya tahadhari, uangalifu na kulinda thamani hiyo. Kwa mfano, ikiwa una mkate na ukakadiria thamani yake kulingana na manufaa yaliyomo ndani yake: viambato vyake, sifa zake, matumizi yake... na upatikanaji wake ukiwa ni adimu (scarce), basi utautunza kwa umakini na huenda ukala robo asubuhi na robo nyingine jioni, na kadhalika siku ya pili, na ikiwa "kipande kidogo" kitakuanguka, utaharakisha kukiokota... Lakini ikiwa una mikate mingi kama huo, licha ya kwamba manufaa yake ya asili yaliyomo ni yale yale—yaani thamani yake ni ile ile—hutaulinda wala kuuhangaikia kama ulivyofanya kwa ule wa kwanza, bali huenda usiokote hata kipande kikianguka, na unaweza kula mkate huo na mwingine pamoja nao kwa siku moja. Kwa sababu hiyo, kitabu kiliongeza katika "kuzingatia sababu ya uhaba" wakati wa kuelezea, neno "katika wakati huo", kikisema katika mwisho wa ukurasa wa 33: "Kwa sababu thamani ya bidhaa hukadiriwa tu kwa kiasi cha manufaa yaliyomo ndani yake wakati wa makadirio kwa kuzingatia sababu ya uhaba katika wakati huo". Yaani wakati unaoambatana na thamani wakati wa kuikadiria na kadhalika. Hii ina maana kuwa thamani ni manufaa yaliyomo kwenye kitu huku ukizingatia sababu ya uhaba kwa sababu nyingine tofauti na makadirio ya thamani, bali ni kwa ajili ya kuilinda thamani hiyo na kuijali kutokana na ugumu wa kupata mfano wake ikipotea kwa sababu ya uhaba wake. Na zingatio hili ni muhimu ili kutopoteza thamani bali kuzitumia kwa kiasi, mbali na ukweli kwamba kuzingatia sababu ya uhaba husaidia katika kulinganisha kati ya uthabiti wa thamani na mabadiliko ya bei kupanda na kushuka kulingana na sababu ya uhaba. Tarehe 21/04/2007).

5- Kuhusu ikiwa thamani ni sehemu ya tafiti za Nizamu ya Kiuchumi au Elimu ya Uchumi, hii inatofautiana kulingana na muktadha wa utafiti. Ikiwa ni upande wa mada ya kielimu kuhusu thamani na bei, yaani kutofautisha kati ya viwili hivyo, basi huo ni utafiti katika Elimu ya Uchumi. Hapo tunasema: Thamani ni kiasi cha manufaa ndani ya bidhaa yenyewe, ilhali bei (thaman) ni kiasi kinacholipwa kwa ajili ya bidhaa wakati wa kuinunua bila kuzingatia manufaa yake au kutokuwa na manufaa, huo ni ulinganifu tu upande wa ufafanuzi.

Lakini ikiwa utafiti ni upande wa miamala, basi ni katika tafiti za Nizamu ya Kiuchumi. Kwa mfano: Mtu akikopa bidhaa fulani yenye thamani ya dinari mia moja za dhahabu na ikasajiliwa kwenye mkataba hivyo, basi wakati wa kulipa anaruhusiwa kurudisha bidhaa ile ile au kurudisha dinari mia moja za dhahabu ikiwa bidhaa imeharibika... Hii ni kwa sababu thamani ni thabiti, haibadiliki kwa muda na mahali. Lakini hairuhusiwi kumnunulia bidhaa nyingine ya aina hiyo hiyo kwa zile mia moja, kwa sababu bei inabadilika na si sharti kwamba mia moja itanunua bidhaa hiyo hiyo... Ama ikiwa itasajiliwa kwenye mkataba bidhaa fulani ambayo bei yake ni dinari mia moja za dhahabu, basi wakati wa kulipa anaweza kurudisha bidhaa ile ile, na ikiwa imeharibika anaweza kumpa dinari mia moja au kumnunulia bidhaa ya aina hiyo hiyo kwa dinari mia moja, iwe ni kama ile au bora zaidi au yenye ubora wa chini, kwa sababu bei si thabiti bali inabadilika kulingana na mahali na muda. Lakini ni lazima pande mbili zielewe maana ya thamani na bei, vinginevyo suala hilo litahitaji usuluhishi au hukumu ya mahakama. Kwa maelezo zaidi, thamani haikadiriwi isipokuwa kwa bidhaa zenye manufaa au sarafu yenye thamani ndani yake yenyewe na si kwa pesa za karatasi kwa mfano kwa sababu thamani ni thabiti. Ama bei, inaweza kukadiriwa kama thamani na pia kwa pesa za karatasi kwa sababu bei zinabadilika; hivyo inajuzu wakati wa kukadiria kwa bei kutaja sarafu ya dhahabu, fedha au pesa za karatasi...

6- Kuhusu umuhimu wa utafiti wa mada ya thamani, unatokana na tofauti kati ya thamani thabiti katika manufaa yaliyomo kwenye bidhaa kwa mwanadamu upande wa mahitaji ya kimsingi na kwa vitu vyenye thamani asilia, na kati ya bei ambayo makadirio yake (uchache au wingi) hayategemei manufaa yaliyomo katika bidhaa. Huenda ukirejea mada ya kusajili mahari kwa thamani au kwa bei tuliyoitaja katika Nizamu ya Kiuchumi, na mfano uliotajwa hapo juu namba (4), huenda ukirejea hayo utatambua umuhimu wa utafiti wa thamani. Hili linafanya tafiti za kiuchumi zijikite kwenye mambo haya mawili:

  • Kufanya tafiti za kiuchumi zijikite kwenye thamani (values) ambapo thamani inahusiana na manufaa yanayotosheleza mahitaji ya kimsingi ya kimaumbile ya mwanadamu, na bidhaa zinazobeba thamani asilia. Hili hufanya umakini uwe kwenye bidhaa yenye manufaa. Kwa maneno mengine, hufanya utafiti uwe katika kile kinachowanufaisha watu, na hivyo kuwa ndio utafiti wa kimsingi, na utafiti wa bei unakuwa ni jambo linalofuata, hivyo kusiwe na pupa ya bidhaa yenye madhara hata kama ina bei ghali kwa sababu haina thamani...

  • Wakati ambapo kufanya tafiti za bei kuwa ndio msingi na utafiti wa thamani kuwa jambo linalofuata tafiti hizo, hupelekea kuwa na pupa ya bidhaa zenye bei ghali na kuzichukulia kuwa na thamani kubwa hata kama ni vitu vyenye madhara kama vile vileo na madawa ya kulevya kwa sababu vina bei ghali na vinaingiza kipato kikubwa...

Hivyo basi, kuimarisha mtazamo wa kiuchumi juu ya thamani kisha bei kufuata thamani hizi, mtazamo huu hueneza kheri na utulivu kati ya watu. Ama kuimarisha mtazamo wa kiuchumi juu ya bei kisha thamani kufuata bei hizi, mtazamo huu hufanya bidhaa zenye bei ghali kuwa ni bidhaa zenye thamani kubwa ingawa zinaweza kuwa na madhara kwa jamii, na hivyo mtazamo huu hueneza shari na taabu kati ya watu.

Nataraji kuwa mada hii imekubainikia, In Shaa Allah.

Ndugu yenu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

22 Sha’ban 1438 H 19/05/2017 M

Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir kwenye Facebook

Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir kwenye Google Plus

Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir kwenye Twitter

Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir kwenye Tovuti

Share Article

Share this article with your network