Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

JIBU LA SWALI: MATOKEO YA KURA YA MAONI YA UINGEREZA YA KUJIONDOA KATIKA MUUNGANO WA ULAYA

July 05, 2016
5443

Swali:

Kura ya maoni ilifanyika nchini Uingereza mnamo tarehe 23/06/2016 kuhusu kubaki au kujiondoa katika Muungano wa Ulaya (European Union), na matokeo yalikuwa takriban 52% ya kuunga mkono kujiondoa. Kufuatia hayo, Waziri Mkuu wa Uingereza, Cameron, alitangaza kujiuzulu kwake huku serikali yake ikisalia kwa muda wa miezi mitatu... Je, matokeo ya kura ya maoni yalikuwa kinyume na alivyotaka Cameron? Na ni nini athari za kiuchumi na kisiasa za kujiondoa kwa Uingereza katika Muungano wa Ulaya? Je, kujiondoa kwa Uingereza kimekuwa jambo la uhakika, kwa maana kwamba hakuna njia ya Uingereza kurudi nyuma? Kisha, je, kuna dori ya Marekani katika suala hili? Mwenyezi Mungu akulipe kheri.

Jibu:

Ili picha iwe wazi na kubainika rai yenye nguvu kuhusu mambo yaliyoibuliwa na swali, tunapitia yafuatayo:

1- Uingereza imekuwa ikimulika mara kwa mara, tangu mgogoro wa kiuchumi wa mwaka 2008, matatizo yake na Muungano wa Ulaya, na jinsi muungano huo usivyofanya kazi kwa maslahi ya Uingereza. Waziri Mkuu, David Cameron, alibainisha msimamo wa Uingereza kuelekea Muungano wa Ulaya katika hotuba aliyoitoa kwenye mkutano wa kilele wa Davos mnamo Januari 2016, akisema: "Muungano wa Ulaya umezidi kupoteza umaarufu nchini Uingereza. Tunahitaji kura ya maoni ili kushughulikia wasiwasi walionao watu nchini Uingereza kuelekea Ulaya: kama vile wazo la kuweka sheria nyingi mno na kuwepo kwa urasimu mwingi... na wazo la uwezekano wa muungano kuwa klabu ya sarafu moja tu; jambo ambalo hatukubaliani nalo... na wazo kwamba Ulaya inafikiria kweli muungano wa kisiasa, ambao ni muungano wa kisiasa ambao Uingereza haijawahi kuufurahia. Uingereza haijawahi kuridhika na wazo la sisi kuwa sehemu ya muungano wa kisiasa. Sisi ni nchi inayojivunia na huru, na tuna taasisi huru na za kidemokrasia tunazojivunia, na zimehudumia maslahi yetu vyema. Na tunapenda kuwa wazi kabisa kwamba haya ni mambo yetu. Ulaya ni mataifa huru yanayokutana pamoja ili kushirikiana na kufanya kazi pamoja kwa ajili ya manufaa ya pande zote, lakini si muungano wa kisiasa unaozidi kuongezeka ndani zaidi, ambao watu wa Uingereza hawaupi, na hawatautia saini." (Gov.uk, 21 Januari 2016).

Kufuatia hayo, aliingia katika mazungumzo mnamo mwezi Februari uliopita na Waulaya na akafanikiwa kupata mengi ya yale ambayo Uingereza iliyataka: alifanikiwa kulinda utambulisho wa kitaifa wa Uingereza ili isimezwe kisiasa katika muungano na kudumisha mamlaka yake huru mbali na muungano, na kutotumiwa kwa makubaliano ya Schengen kwake, hivyo mipaka yake inasalia bila vizuizi visivyohitajika, na muungano kutambua sarafu yake ya Sterling (Pauni) ili isiingie katika eneo la Euro, na kuweka vikwazo kwa wahamiaji wa Ulaya wanaoingia Uingereza katika haki ya kupata misaada fulani na nyumba za bure mpaka wakamilishe miaka 4 ya kuishi Uingereza... Cameron alisema wakati wa kutia saini makubaliano hayo akitangaza kufikiwa kwa matokeo yaliyotarajiwa kuwa "makubaliano aliyofikia na viongozi wa Muungano wa Ulaya yanaipa Uingereza hadhi maalum ndani ya muungano." (BBC, 20/02/2016). Cameron alikuwa ameuomba Muungano wa Ulaya "kuyapa mabunge ya kitaifa ya nchi wanachama mamlaka makubwa zaidi ili mabunge haya, ikiwemo bunge la Uingereza, yawe na haki ya kupinga au kufuta maamuzi ya Baraza la Ulaya" lakini ombi hili halikukubaliwa na muungano...

Uingereza ilifanikiwa kupata mengi lakini ilitaka kuyafanya maamuzi na sheria za Muungano wa Ulaya kuwa si lazima kwa Uingereza, iweze kupinga inachotaka na kukubali inachotaka kiasi kwamba Muungano wa Ulaya usiwe na mamlaka yoyote juu yake. Hiki ndicho Waingereza wanachotaka ili kuufanya muungano kuwa dhaifu sana usio na mamlaka yoyote juu ya wanachama wake. Uingereza, kama ilivyo ada yake, ilikuwa ikitaka kufaidika na muungano bila kufungwa na sheria za muungano na ilikuwa ikitumia suala la kura ya maoni na kujiondoa katika muungano kama njia ya shinikizo na unyang'anyi ili kupata upendeleo... Na kama inavyofahamika, Cameron katika kampeni yake ya uchaguzi alikuwa ameahidi iwapo atashinda katika uchaguzi wa 2015 kwamba angefanya kura hii ya maoni akifuata ada ya Uingereza ya kutishia kwa kura ya maoni ili kufikia upendeleo maalum, kwa kuitisha Muungano wa Ulaya na nchi nyingine wanachama kutokana na fujo za kisiasa na kiuchumi zinazosababishwa na uamuzi wa kura ya maoni wa kujiondoa Uingereza katika muungano!

Sera ya Uingereza ya kutishia kwa kura ya maoni ili kupata manufaa kutoka kwa muungano si ngeni, bali ni tangu miaka ya kwanza ya kuingia kwa Uingereza katika muungano huo. Uingereza imekuwa mwanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Ulaya tangu Januari 1973, na kubaki kwake na sarafu yake ya "Pound Sterling" na kubaki kwake nje ya eneo la "Schengen" yalikuwa nembo za hali maalum ambayo Uingereza iliendelea kufurahia licha ya uanachama wake katika Muungano wa Ulaya. Ilikuwa ikitumia wazo la "kura ya maoni" kuhusu kubaki kwake katika muungano kama njia ya kunyang'anya nchi za Ulaya, ili kufikia upendeleo zaidi kwa Uingereza ndani ya muungano. Ilifanya kura ya maoni mwaka 1975 ili kuboresha masharti ya kubaki kwake katika muungano, ambapo Waingereza walipiga kura ya kuunga mkono kubaki katika Jumuiya ya Kiuchumi ya Ulaya...

Kura hii ya maoni ya sasa si kitu kigeni katika kura za maoni za Uingereza ili kufikia malengo yake hata kama ni malengo maovu! Chama cha Conservative kimeendesha suala hili kwa werevu mkubwa, ambapo watu wa chama hicho waliongoza kampeni zote mbili; ya kubaki katika muungano na ya kujiondoa wakati mmoja!! Aliyekuwa kiongozi wa kampeni ya kubaki alikuwa Waziri Mkuu wa Uingereza mwenyewe, na kiongozi wa kampeni ya kujiondoa alikuwa mbunge Boris Johnson, aliyekuwa Meya wa zamani wa London, ambaye alijiuzulu wadhifa wake ili kuchukua kiti kilichohakikishiwa na Conservatives bungeni, ili kuwa na uwezekano wa kuwa Waziri Mkuu katika siku zijazo. Pia, Waziri wa Sheria wa sasa, Michael Gove, aliongoza kampeni ya kujiondoa pia... Cameron alikuwa ametangaza "kwamba tarehe ya kura ya maoni kuhusu kubaki kwa Uingereza katika Muungano wa Ulaya imepangwa kuwa 23 Juni 2016, kufuatia mkutano wa serikali. Cameron alisisitiza katika taarifa fupi mbele ya makao makuu ya serikali tena kwamba Uingereza "itakuwa yenye nguvu, salama zaidi na yenye ustawi zaidi ndani ya Muungano wa Ulaya uliofanyiwa marekebisho." (Monte Carlo, 20/04/2016).

Licha ya kuunga mkono makubaliano hayo, hakuwashurutisha wanachama wa chama chake kuyaunga mkono. Wakati ambao Cameron alisema "kwamba kuchagua kuondoka katika muungano katika kura ya maoni ya Alhamisi kutawakilisha kosa kubwa," na kutasababisha "hali ya kutokuwa na uhakika kwa hadi muongo mmoja," Waziri wa Sheria katika serikali yake, Michael Gove, aliliambia gazeti la Sunday Telegraph kwamba Uingereza itakuwa "mnara wa maendeleo" ikiwa itajiondoa katika muungano. Gove alisema: "Ni lazima wananchi wapige kura kwa ajili ya demokrasia na ni lazima Uingereza ipige kura kwa ajili ya matumaini." (BBC, 19/06/2016). Hivyo basi, Waziri Mkuu wa Uingereza Cameron na kundi la viongozi wa chama chake walikuwa wakifanya kambi inayounga mkono kubaki Uingereza katika muungano, wakati Waziri wake wa Sheria Gove na kundi la mawaziri wengine wa Cameron walikuwa wakiratibu kampeni ya "kujiondoa kwa Uingereza" pamoja na Meya wa zamani wa London Boris Johnson, kiongozi maarufu katika chama cha Conservative.

Uchunguzi wa kina wa sera ya chama tawala cha Conservative kinachoongozwa na Cameron katika suala la kura ya maoni yaliyotajwa unaonyesha kuwa Cameron alitarajia kuwa matokeo hayatakuwa yenye kuamua (yaani yangekuwa yamekaribiana sana), ili yaweze kuwa na nafasi ya majadiliano au kutumika kama uwanja wa mazungumzo mapya na muungano. Ndiyo maana chama cha Conservative chenyewe kilikuwa kikiendesha kampeni ya kubaki na kampeni ya kujiondoa... Wala hakuna kampeni yoyote iliyokuwa na nia ya dhati ya kubaki au kujiondoa kuliko ilivyokuwa na nia ya kuwa kura ya maoni iwe njia ya kupata upunguzaji wa masharti zaidi kutoka kwa muungano. Inasikitisha kwamba Cameron, licha ya kuunga mkono makubaliano, hakuwashurutisha wanachama wake kuyaunga mkono; kama angekuwa na nia ya dhati ya kubaki, angekitaka chama chake kumuunga mkono na kupiga kura ya kubaki, na matokeo yangekuwa ya kuunga mkono kubaki kwa nguvu, lakini alikiacha kijigawanye katika upigaji kura kwa sababu lengo lilikuwa si kupata wingi wa kujiondoa au kubaki, bali ni kama tulivyotaja hapo juu...

Hili pia linathibitishwa na kile kilichojitokeza kwa kiongozi wa kampeni ya kujiondoa, Johnson; kama angekuwa na nia ya dhati katika kampeni yake na kura ya maoni ikaja na matokeo ya kujiondoa, angeendelea na msimamo wake ule ule, lakini sauti ya matamshi yake ilibadilika na kuwa karibu zaidi na sera ya kubaki! Johnson alisema katika hotuba ya Jumatatu baada ya matokeo ya kura ya maoni kuwa Uingereza ni "sehemu ya Ulaya" na kwamba ushirikiano na nchi jirani "utaimarika," akibainisha kuwa kujiondoa kwa Uingereza katika muungano "hakutafanyika kwa haraka" (http://www.almodon.com/arabworld/2016/6/28/). Isitoshe, mshirika wake katika kampeni ya kujiondoa, Nigel Farage, kiongozi wa chama cha UKIP kilichojitenga na chama cha Conservative hapo awali, na ambaye alikuwa muumini mkubwa wa Uingereza kuondoka katika Muungano wa Ulaya, katika hotuba yake ya kwanza katika Bunge la Ulaya baada ya kura ya maoni alisema: "Kwa nini tusikue na kuwa wa vitendo, wenye busara na wakweli, hebu tufikie kati yetu makubaliano ya busara ya msamaha wa ushuru, na baada ya hapo mtatambua kuwa Uingereza itakuwa rafiki yenu, na kwamba tutafanya biashara nanyi, na kushirikiana nanyi, na kuwa marafiki zenu bora duniani. Hebu tufanye hivyo kwa busara, na turuhusuni tuendelee kufuata matamanio yetu ya kimataifa na ya baadaye" (The Telegraph, 28 Juni 2016). Hii inaashiria kuwa kile ambacho chama cha Conservative kilikuwa kikikipanga kupitia pande zote mbili (ya kujiondoa na ya kubaki) si kujiondoa wala kubaki, bali ni kutengeneza hali ya shinikizo kwa muungano ili kufanya mazungumzo ya kupata nafuu zaidi kwa kisingizio kuwa matokeo hayajawa ya wazi.

Lakini mambo hayakuwa kama yalivyotarajiwa, matokeo yakaja na wingi wa 52% wa kujiondoa na hapa ndipo mshtuko ulipotokea! Uingereza inataka kubaki katika muungano ili ifaidike na faida zake, hususan za kiuchumi, na wakati huo huo bila kufuata sheria zake! Kwa hivyo, katika kipindi chake chote ndani ya muungano imekuwa ikiufanyia ghasia kwa kutishia kura za maoni, kusuasua, kupinga na kutengeneza matatizo, na ujanja wake mwingi ulikuwa ukifaulu... Lakini safari hii mambo yameenda mrama! Uingereza haiwezi kujiondoa kikamilifu katika muungano kwa kukata uhusiano nao kwa sababu wakati huo itakuwa inakaribia kifo... Na wakati huo huo, inajinasibu kwa rai ya wengi ambayo kwa mujibu wa kura ya maoni inawajibisha kujiondoa... Kwa hivyo iko katika hali ya kuchanganyikiwa na imeingia katika mtego wa vitendo vyake yenyewe!

2- Mshtuko uliikumba Uingereza na Ulaya, na hata kuvuka mipaka yake, kutokana na matokeo ya kura ya maoni ya Uingereza "Brexit" yaliyofanyika Alhamisi 23/06/2016 baada ya tafiti za maoni kuashiria kuwa wapiga kura nchini Uingereza wangekubali kubaki katika Muungano wa Ulaya. Ingawa matokeo ya kura ya maoni yalikuwa na athari kali iliyovuka Uingereza hadi kwenye Muungano wa Ulaya wenyewe na kwingineko, lakini athari kubwa zaidi ilikuwa nchini Uingereza kiuchumi na kisiasa:

  • Kiuchumi: Imani kwa Uingereza na uchumi wake ilitikisika dakika chache baada ya kutangazwa kwa matokeo, ambapo thamani ya Sterling ilianguka mbele ya Dola kwa 10% na mbele ya Euro kwa 7%. Mshtuko ulitokea katika masoko ya fedha ya Ulaya na Asia, ambapo Reuters iliripoti mnamo 28/06/2016 kuwa "matokeo ya kura ya maoni yalisababisha kufutika kwa dola trilioni tatu kutoka kwa thamani ya hisa za kimataifa na bado biashara ina sifa ya kuyumba hata viongozi wa kisiasa wanapoahidi kulinda uchumi wao." Hii ilimlazimu Gavana wa Benki Kuu ya Uingereza kutuliza hali kwa kusema "kuna ukwasi wa kutosha wa thamani ya pauni bilioni 250 na kwamba hatasita kuchukua hatua zisizo za kawaida" (BBC, 24/06/2016). Mashirika ya kimataifa ya ukadiriaji wa mikopo ya "Standard & Poor’s", "Moody’s" na "Fitch" yameshusha daraja la deni la Uingereza, yakichapisha data zilizosema: "Daraja la deni la Uingereza limeshushwa kutoka 'AAA' ambayo ni bora zaidi hadi daraja la 'AA', yaani imeshuka kwa daraja mbili... Na hii ni mara ya kwanza kutokea kwa Uingereza. Mashirika haya yaliashiria kuwa "kutokuwa na uhakika kutakakofuata matokeo ya kura ya maoni kutasababisha kudorora kwa uchumi katika muda mfupi... na mazingira ya kisiasa ambayo hayaruhusu kutabiri maendeleo yake na yasiyo na utulivu na yenye ufanisi mdogo... na uwezekano wa kufanya kura ya maoni juu ya uhuru wa Scotland" (AFP, 27/06/2016). Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) lilionya juu ya kuanguka kwa bei za majengo. Ama Wizara ya Fedha ya Uingereza ilisema "bei za majengo zinaweza kushuka kwa asilimia kati ya 10% hadi 18% ikilinganishwa na jinsi bei zingefika katika kipindi cha miaka miwili ijayo" (BBC, 24/06/2016). Waziri wa Fedha wa Uingereza George Osborne, ambaye majaribio yake ya kutuliza masoko hayakusikilizwa, alitangaza kuwa "atalazimika kupunguza matumizi na kuongeza kodi ili kuhakikisha utulivu wa kifedha. Kampuni zilitangaza kusitisha ajira mpya na uwezekano wa kupunguza wafanyakazi, jambo lililovunja matumaini ya wapiga kura kwamba uchumi wa Uingereza utastawi nje ya Muungano wa Ulaya" (Reuters, 28/06/2016). Baadhi ya kampuni zilitangaza mara moja mipango ya dharura ya kuhamisha matawi yao kutoka London kwenda miji mingine ndani ya Muungano wa Ulaya, na fahirisi ya Financial Times ilianguka kwa zaidi ya 8% mara tu baada ya ufunguzi, "ambayo ni hasara yake kubwa zaidi katika siku moja tangu 2008" (Al Jazeera Net, 24/06/2016).

Haya yote yanamaanisha kuwa Uingereza imeathirika na matokeo ya kura ya maoni, na hii ni ishara mbaya kwake ikiwa itajiondoa katika muungano jumla, huku ikiwa tayari inasumbuliwa na athari za mgogoro wa kifedha uliolipuka mwaka 2008. Inafaidika sana na Muungano wa Ulaya kama tulivyotaja katika Jibu la Swali la tarehe 02/05/2016: "Uingereza pia inafaidika kiuchumi na Muungano wa Ulaya, na hii inafaidisha kampuni zake na matajiri wake, kwani uchumi wa Uingereza unatawaliwa na huduma; na huduma kuu nchini Uingereza ni huduma za kifedha. Uingereza inauza nje bidhaa chache, lakini inategemea huduma za kifedha kwa ajili ya mapato, mtaji na fedha za kigeni. Pia soko la pamoja la Muungano wa Ulaya linamaanisha kuwa Uingereza inaweza kuuza nje bila vikwazo vya kibiashara kwa Ulaya nzima, jambo linalofaidisha kampuni kubwa na matajiri. Kwa hivyo kujiondoa kwake katika Muungano wa Ulaya kunaipotezea nafasi hii na kusababisha matatizo ya kisiasa nchini. Kwa sababu Muungano wa Ulaya ndiye mshirika mkuu wa kibiashara wa Uingereza, kujiondoa kwake katika muungano wakati ikiwa ni nchi ya Ulaya kunadhoofisha nafasi yake Ulaya... Hii ni pamoja na kuwa katika hali hiyo itahitaji kuupinga Muungano wa Ulaya kutokea nje na hii inadhoofisha ushawishi wake katika muungano. Ama ushawishi wake ukiwa ndani ni wenye nguvu zaidi na ufanisi zaidi..."

Tulisema katika jibu la swali lilo hilo: "Na mnamo Machi 2015, Uingereza ilishinda kesi dhidi ya Benki Kuu ya Ulaya katika Mahakama ya Haki ya Ulaya, ambapo Benki Kuu ya Ulaya ilijaribu kuhamisha kazi ya malipo ya miamala ya eneo la Euro kwenda ndani ya muungano, na hatua kama hiyo ingeweza kuiondoa London, huku Paris na Frankfurt zikiwa zenye kuvutia zaidi kama vituo vya kifedha, jambo ambalo lingedhoofisha msimamo wa kiuchumi nchini Uingereza..." Ikiwa hili litaongezwa kwenye matokeo ya kuvuja kwa nyaraka za Panama za kupunguza hifadhi za kodi za Uingereza kama tulivyofafanua katika jibu la swali kuhusu nyaraka za Panama la tarehe 05/05/2016... Basi hayo yote yanaifanya Uingereza kwa kura ya maoni ya kujiondoa, kuwa kama mtu anayejifyatulia risasi mguuni! Ikiwa kujiondoa kutatekelezwa kweli, Uingereza itapoteza hadhi ya London kuwa kituo cha kifedha na Frankfurt, hususan ikiwa mji mkuu wa kifedha wa muungano, itakuwa yenye kuvutia zaidi kuliko London kama kituo cha kifedha, na hivi ndivyo hasara za Uingereza zitakuwa kubwa na za maafa.

  • Kisiasa: Kura ya maoni ya Uingereza imeleta athari kubwa katika mshikamano wa watu wa Uingereza wenyewe. Watu wa Scotland walipiga kura kwa wingi mkubwa wa kubaki katika Muungano wa Ulaya, kadhalika Ireland ya Kaskazini, na sasa watu hawa wanadai kura ya maoni kuhusu kubaki kwao ndani ya Uingereza, yaani umoja wa Uingereza wenyewe umekuwa na mashaka. Hili si jambo ambalo Uingereza ililipanga, kwani moja ya mafanikio makubwa ya ndani ya Cameron ilikuwa ni kuzuia kujitenga kwa Scotland kutoka Uingereza katika kura ya maoni ya 2014, na Uingereza ilidhani kuwa suala la Scotland limefungwa kwa muda mrefu, lakini baada ya kura ya maoni ya 23/06/2016 limerudi tena kwa nguvu. Waziri Mkuu wa Scotland, Sturgeon, alitamka mara tu baada ya matokeo ya kura ya maoni kwamba hali imebadilika baada ya kura ya maoni ya 2014 wakati Wascot walipopiga kura ya kubaki Uingereza, na kwamba Scotland itaanza mazungumzo na Muungano wa Ulaya kuhusu kubaki kwake ndani ya muungano, na hili ni vigumu kufikiwa bila kujitenga na Uingereza. "Nicola Sturgeon, Waziri Mkuu wa Scotland, alitangaza Jumapili kwamba 'Ufalme wa Muungano ambao Scotland ilipiga kura mwaka 2014 kubaki ndani yake haupo tena', akiashiria kuwa ni 'uwezekano mkubwa sana' kufanyika kura mpya ya maoni baada ya Waingereza kupiga kura ya kujiondoa katika Muungano wa Ulaya." (Middle East Online, 26/06/2016). Ama Ireland ya Kaskazini, ambayo ni upande dhaifu zaidi wa Uingereza, "chama cha Sinn Fein, ambacho kinachukuliwa kuwa ni mrengo wa kisiasa wa Jeshi la Jamhuri ya Ireland (IRA), kilitoa mwito asubuhi ya Ijumaa wa kufanyika kura ya maoni kuhusu kuungana kwa Ireland. Mwito huu ulikuja baada ya Waingereza kupiga kura ya kujiondoa katika Muungano wa Ulaya, kulingana na matokeo ya mwisho. Chama cha Republican kilisisitiza kuwa kura ya maoni kuhusu Muungano wa Ulaya 'ina athari kubwa kwa asili ya dola ya Uingereza'" (France 24, 25/06/2016)... Hivyo, kura ya maoni ya Uingereza ya kujiondoa katika Muungano wa Ulaya imefanya kusambaratika kwa Uingereza kuwa mazungumzo ya wanasiasa tena nchini Ireland ya Kaskazini na pia Scotland.

Kwa hiyo, matokeo ya kura hii ya maoni yameleta shinikizo zinazotishia kusambaratika kwa Uingereza, pamoja na hasara za kiuchumi zinazotarajiwa. Hayo yote yanathibitisha kuwa upepo wa kura ya maoni umekuja kinyume na vile Uingereza ilivyotamani, na kwamba yenyewe - yaani Uingereza - imetumbukia katika mtego wa hila zake, na imekuwa mhanga wa kujiamini kwake kwa werevu wake. Siku zilizopita tangu upigaji kura zimeonyesha hali ya mkanganyiko wa kisiasa usio wa kawaida katika historia ya kisiasa ya kisasa ya Uingereza, pamoja na hali ya wasiwasi mkubwa ulioikumba serikali na upinzani kiasi kwamba gazeti la New York Times liliandika Jumatatu 27/06/2016: "Nchi maarufu kwa uhuru wake wa kisiasa na kisheria inazama katika fujo." Hiyo ikiwa ni maoni kuhusu kile Uingereza inachopitia baada ya kura ya maoni!

3- Kwa hivyo, inatarajiwa kuwa Uingereza itasuasua kwa nguvu katika kutekeleza kujiondoa katika kipindi cha karibu, bali inaweza kuchukua miaka, hii ni ikiwa itajiondoa kweli, kwani yenyewe ni bingwa wa uovu na hadaa... Na kile kilichojitokeza katika matamshi... na yale yaliyoenezwa na vyombo vya habari katika maoni... yote hayo yanaashiria kusuasua huku katika kutekeleza kura ya maoni, bali hata zaidi ya hapo kama vile kuzunguka na kukwepa kura hiyo ya maoni yenyewe. Mambo yanayoashiria kusuasua na ukwepaji huu ni pamoja na yafuatayo:

a- Maandishi ya Kifungu cha 50 cha Mkataba wa Lisbon uliotiwa saini mwaka 2007 yanatoa nafasi ya ujanja na kusuasua ambavyo Uingereza inavimudu kupitia uovu wake wa kisiasa na werevu wake. Kifungu hiki kinasema kuwa ili kuanza taratibu za kujiondoa, ni lazima Uingereza iliarifu Baraza la Ulaya linaloundwa na wakuu wa nchi na serikali za nchi wanachama kuhusu nia yake ya kujiondoa katika muungano, na kisha kufanya mazungumzo kwa muda wa miaka miwili kama kiwango cha juu katika "makubaliano ya kujiondoa". Cameron alisema mbele ya bunge la Uingereza: "Kwamba serikali haitaanza mazungumzo ya kujiondoa katika muungano katika hatua ya sasa. Na kwamba nchi lazima kwanza iamue aina ya uhusiano tunaoutaka na Muungano wa Ulaya kabla ya kutekeleza Kifungu cha 50 cha Mkataba wa Lisbon." (BNA, 27/06/2016). Cameron alisema katika hotuba yake bungeni akisisitiza kuwa Uingereza pekee ndiyo inayoamua lini ianze taratibu za kujiondoa, akisema "kwamba serikali ya Uingereza haitakiamsha sasa Kifungu cha 50 cha Mkataba wa Ulaya kinachohusiana na kujiondoa kwa nchi katika muungano" (Al Jazeera Net, 27/06/2016). Hivyo, inawezekana kurefusha muda wa kuwasilisha ombi la Uingereza la kujiondoa mpaka mazungumzo yaanze! Si hivyo tu, bali Cameron amefanya kujiuzulu kwake kusiwe kwa mara moja bali baada ya takriban miezi mitatu na kuundwa kwa serikali mpya, kisha yenyewe ndiyo iwasilishe ombi ikipenda, yaani mazungumzo yameachwa kwa Waziri Mkuu mpya atakayemrithi Cameron mnamo Septemba 2016 ambapo chama cha Conservative kitakutana kuchagua kiongozi mpya wa chama. Cameron alitaja jambo hili waziwazi katika hotuba yake baada ya kutangazwa matokeo ya kura ya maoni ambapo alisema atajiuzulu wadhifa wake mnamo Oktoba na atamuachia mrithi wake kuamua lini kutekeleza Kifungu cha 50 (http://elaph.com/Web/News/2016/6/1096000). Kadhalika, "Waziri wa Fedha wa Uingereza George Osborne alithibitisha kuwa hakutakuwa na mazungumzo kuhusu kujiondoa kwa Uingereza katika Muungano wa Ulaya kabla ya kuundwa kwa serikali mpya" (Al Jazeera Net, 27/06/2016)... Pia, mchambuzi mmoja wa kisheria alifafanua: "Ukweli ni kwamba kadiri uarifu wa Kifungu cha 50 unavyochelewa, ndivyo nafasi ya kutokitekeleza kabisa inavyoongezeka. Hiyo ni kwa sababu kadiri ucheleweshaji unavyokuwa mrefu, ndivyo uwezekano mkubwa wa matukio kuingilia kati, au udhuru kutengenezwa." (Kwa nini uarifu wa Kifungu cha 50 ni muhimu, David Allen Green, 25 Juni 2016). Kwa sababu hiyo, wanadiplomasia wawili wa Ulaya waliona kuwa Uingereza inaweza isianzishe kabisa mfumo wa kujiondoa kwake katika Muungano wa Ulaya licha ya Waingereza kupiga kura hiyo. Mwanadiplomasia huyo alisema akitaka jina lake lisitajwe: "Imani yangu binafsi ni kwamba hawataarifu kamwe Muungano wa Ulaya kuhusu nia yao ya kujiondoa," na mwanadiplomasia huyo akaongeza: "Tunataka London ianzishe Kifungu cha 50 sasa, ili mambo yawe wazi. Na kwa kuwa hatuwezi kuwalazimisha kufanya hivyo, natarajia watachukua muda wao." Aliongeza: "Siondoi uwezekano, na hii ni imani yangu binafsi, kwamba hawatafanya hivyo kamwe" (Arabi 21, 27/06/2016).

b- Hata suala la kura ya maoni lenyewe linaweza kukwepwa kwa kutafuta njia za kisheria za kuirudia au kufanya mazungumzo juu ya masharti yake. Ingawa kufanya kazi ya kurudia kura ya maoni ni jambo la aibu kwa nchi inayojiona kuwa ina demokrasia kongwe na kwamba haipingi rai ya watu, lakini werevu wa kisiasa wa Uingereza na uovu wake hautashindwa kupata njia za kutokea. Kinachoashiria hilo ni:

A- Kuna malalamiko ya kielektroniki ya kukusanya saini za wale wanaotaka kurudiwa kwa kura: "Malalamiko kwenye tovuti ya bunge la Uingereza yanayodai kurudiwa kwa kura ya maoni ya kujiondoa kwa Ufalme wa Muungano katika Muungano wa Ulaya, yalikusanaya saini milioni 3.8 hadi tarehe 28/06/2016 wakidai kurudiwa kwa kura hiyo. Malalamiko hayo yaliyoanzishwa na William Oliver Healey yanasema kwamba 'Waliotia saini hapa chini wanaitaka serikali ya Mtukufu Malkia kutekeleza kanuni kwamba ikiwa kura ya kujiondoa au kubaki itakuwa chini ya 60% kutokana na ushiriki wa chini ya 75% ya wapiga kura, basi inapaswa kufanyika kura nyingine ya maoni'." (Kutoka gazeti la Telegraph la Uingereza, 27/06/2016).

B- Kwa kuzingatia kuwa kurudia kura ya maoni kunaweza kutikisa demokrasia ambayo Uingereza inajinasibu kwayo... baadhi ya wataalamu wa Kiingereza katika sheria wameanza kutaja njia nyingine za kutokea kwa kusema kuwa bunge (House of Commons na House of Lords) linaweza kumzuia Waziri Mkuu kutoa taarifa kwa Muungano wa Ulaya. Lord Pannick QC (mtaalamu maarufu wa sheria za umma) alisema: "Bila sheria kutoka bungeni, Waziri Mkuu hawezi kuupa Muungano taarifa kisheria" (http://www.bbc.com/news/uk-politics-uk-leaves-the-eu-36671629).

c- Kuna sababu ya nje inayojali kubaki kwa Uingereza katika Muungano wa Ulaya ili kuudhoofisha, na ili ibaki ndani yake kama kiini cha mvutano, na sababu hiyo ya nje ni Marekani. "Obama alizuru London mnamo mwezi Aprili uliopita, na akawahimiza Waingereza kupiga kura ya kuunga mkono kubaki ndani ya Muungano wa Ulaya." (Al Jazeera, 24/06/2016). Kwa sababu Marekani ilikuwa ikitaka kubaki kwa Uingereza katika muungano ili ubaki kuwa muungano dhaifu. Marekani inatambua kuwa Uingereza haifanyi kazi kwa maslahi ya muungano wala kwa umoja wa Ulaya, bali inakwamisha hilo, na kuvuruga maamuzi mengi, na haifikirii isipokuwa maslahi yake, hivyo yenyewe ni kifaa cha kubomoa. Haya yote ni kwa maslahi ya Marekani ambayo haitaki kuona Ulaya ikiwa na umoja wenye nguvu unaoichangamoto au kushindana nayo katika uwanja wa kimataifa kiuchumi au kisiasa. Ikiwa kujiondoa kwa Uingereza kutasababisha kusambaratika kwa muungano, basi hilo ni kwa maslahi ya Marekani... Kwa hivyo, baada ya matokeo ya kujiondoa kujitokeza, Obama alimtuma Waziri wake wa Mambo ya Nje, John Kerry, kwenda Ulaya kufanya upatanishi kati ya Muungano wa Ulaya na Uingereza na kupunguza majibu ya nchi za Ulaya dhidi ya Uingereza. Kerry alipowasili Brussels mnamo 27/06/2016 alisema: "Ni jambo la msingi kubaki tumezingatia katika hatua hii ya mpito ili asiwepo yeyote atakayepoteza fahamu na kuchukua hatua bila kufikiri." Baada ya mkutano wake na Cameron mjini London, Kerry alitangaza akisema: "Kujiondoa kwa Uingereza katika Muungano wa Ulaya kunaweza kusitokee kabisa, na kwamba London haina haraka na hilo, na kwamba Cameron anahisi hana uwezo wa kufanya mazungumzo kuhusu kujiondoa kwa nchi jambo ambalo hakulitaka tangu awali... na kwamba Cameron hataki kutekeleza Kifungu cha 50 cha Mkataba wa Lisbon ambacho kitaanzisha mfumo wa kujiondoa utakaodumu kwa takriban miaka miwili... Kerry alieleza kuwa London haitaki kujikuta nje ya Ulaya baada ya miaka miwili kabla ya kutia saini makubaliano mapya ya ushirikiano... Alipoulizwa kama inawezekana 'kubatilisha' uamuzi wa kujiondoa na jinsi ya kufanya hivyo, Kerry alijibu: 'Nadhani kuna njia nyingi'." (France 24, 29/06/2016).

Sababu hii ya nje inaweza kuchangia kupatikana kwa mlango wa uhusiano fulani mpya kati ya Uingereza na muungano, kwani katika hili kuna maslahi kwa Marekani kama tulivyobainisha hapo awali.

4- Inaonekana kuwa Muungano wa Ulaya umeanza kutambua michezo ya Uingereza. Inataka kufikia makubaliano yasiyo rasmi ya kulinda maslahi yake kwa msingi wa mfumo wa Norway na Sweden kabla ya kuanza kutumia Kifungu (50) cha Mkataba wa Lisbon kuanza taratibu za kujitenga. Lakini kinyume na Norway na Sweden, Uingereza inataka kufika katika soko la Ulaya huku ikipinga uhuru wa watu kutembea, ambao ni suala kuu kati ya wapiga kura wa Uingereza. Merkel amelikataa hilo katakata, kwani uhuru wa watu kutembea ni moja ya uhuru unaotukuzwa na Muungano wa Ulaya, pamoja na uhuru wa kubadilishana bidhaa, huduma na mitaji. Muungano wa Ulaya unatambua werevu wa Uingereza, kwa hivyo haukukataa wazo hili tu, bali pia ulipiga marufuku mazungumzo yoyote ya siri kati ya yoyote ya nchi wanachama 27 na Uingereza. Rais wa Tume ya Ulaya (Jean-Claude Juncker) alisema: "Acheni niwe wazi kabisa, majaribio ya siri hayawezi kufanywa na serikali ya Uingereza," na akafanya jambo hilo kuwa wazi kabisa kwa wafanyakazi wote wa tume na kamati, akisema: "Hairuhusiwi kufanya mazungumzo ya siri... Hairuhusiwi kufanya mazungumzo ya siri" (Evening Standard, 28/06/2016).

Bunge la Ulaya lilikutana tarehe 28/06/2016 ili kuendelea na vikao vyake kwa muda wa siku mbili. Ombi lake la kwanza lilikuwa ni Uingereza kuanza mara moja mfumo wa kujiondoa kwake katika Muungano wa Ulaya kwa mujibu wa Mkataba wa Lisbon ili kuepuka shaka yoyote inayoweza kuwa mbaya na kulinda umoja wa muungano kama ilivyotajwa. Jean-Claude Juncker, Rais wa Tume ya Ulaya, aliliambia Bunge la Ulaya: "Hatuwezi kubaki katika hali ya kutoeleweka kwa muda mrefu, nataka Ufalme wa Muungano ubainishe msimamo wake mara moja na si kesho wala keshokutwa." Alikataa mazungumzo yoyote ya siri kuhusu masharti ya kujiondoa kwa Uingereza katika Muungano wa Ulaya au kwamba London ipange ratiba yake, akisema: "Sisi ndio tunaamua ajenda na si yule anayetaka kujiondoa katika Muungano wa Ulaya." (AFP/Al Jazeera, 28/06/2016). Cameron alikuja Brussels kuhudhuria kikao cha kwanza cha Muungano wa Ulaya na kisha akaondoka ambapo alitangaza: "Natumai kweli tutaanzisha uhusiano wa karibu kwa kiwango cha juu katika upande wa biashara na ushirikiano katika masuala ya usalama kwa sababu ni jambo zuri kwetu." (DPA, 28/06/2016). Yaani, hataki Muungano wa Ulaya bali anachagua kile kinachohitajika na Uingereza ambacho ni ushirikiano wa kiuchumi na usalama. Kansela wa Ujerumani Merkel alituma ujumbe wazi kwa London akisema: "Kwamba Uingereza haiwezi baada ya kura ya maoni ya kujiondoa kuchagua kubaki na upendeleo wake na wakati huo huo kuachana na wajibu wake wote" (DPA, 28/06/2016)... Yaani, Waulaya wamekata shauri lao na Uingereza na wanataka ijiondoe haraka kabla hawajadhurika kutokana na kujiondoa kwake na kusuasua kwake katika kujiondoa.

Katika kuhitimisha mkutano huo, Rais wa Baraza la Ulaya, Donald Tusk, alitangaza kuwa "viongozi wa Ulaya walisema waziwazi Jumatano kwa Ufalme wa Muungano kuwa haiwezi kufanya mazungumzo ya kuingia katika soko la pamoja la Ulaya kama inavyopenda baada ya kujiondoa kwake katika muungano, yaani bila kukubali uhuru wa watu kutembea... wala hakutakuwa na soko la pamoja lililoshonwa kwa ajili yake pekee." Aliongeza kuwa mazungumzo ya kwanza baada ya uamuzi wa Uingereza kuondoka katika muungano yaliyofanyika Brussels hayakuchangia kufikia matokeo, kwa hivyo "tuliamua kufanya mkutano wa kishauri wa nchi ishirini na saba na tutakutana mnamo Septemba 16 huko Bratislava (mji mkuu wa Slovakia) kuendeleza mazungumzo yetu... Alisema: 'Washiriki walikubaliana kuwa tunapita katika wakati mzito katika historia yetu ya pamoja... na kupitia mazungumzo yetu limejitokeza suala moja lililo wazi: viongozi wameazimia kabisa kubaki wamoja'" (AFP, 29/06/2016).

Hii haina maana kwamba Muungano wa Ulaya haukuathirika vibaya na matokeo ya kura ya maoni hata kama athari hiyo si ya hatari ile ile iliyoisababishia Uingereza. Muungano wa Ulaya umeathirika, kwani umefungua mlango katika nchi zake kudai kura za maoni... nguvu nyingi za mrengo wa kulia zimeziwasilishia serikali zao maombi ya kura za maoni zinazofanana na hiyo, ikiwa ni pamoja na Ufaransa, kiini cha kwanza cha Muungano wa Ulaya. Wakati huo huo, Tume ya Ulaya ilihesabu maombi 32 kutoka kwa vyama vya Ulaya ya kura za maoni zinazofanana na hiyo katika nchi kadhaa za Ulaya ikiwemo Ufaransa, kwa njia inayotishia kubaki kwa Muungano wa Ulaya mzima... Nchi waasisi wa muungano huo, hususan Ufaransa na Ujerumani, nchi mbili kubwa zenye ushawishi mkubwa, zimechukua hatua na kutangaza azma yao ya kubaki kwa muungano na kuziunganisha nazo Italia, Uholanzi, Ubelgiji na Luxembourg kama nchi waasisi kufanya mkutano wa dharura... Rais wa Ufaransa Hollande alisema baada ya mkutano huo kuwa "kujiondoa kwa Uingereza katika muungano kunaupa Ulaya changamoto" na akaonyesha "masikitiko yake makubwa kwa chaguo hili lenye maumivu" akisema: "Kwamba upigaji kura wa Waingereza kwa ajili ya kujiondoa katika muungano unaiweka Ulaya mbele ya mtihani hatari, kwani haiwezi kuendelea kama ilivyokuwa hapo awali... ni lazima ionyeshe mshikamano wake na nguvu zake..." (AFP, 24/06/2016)... Kadhalika Ujerumani, mwanachama mwanzilishi wa pili, ilifanya hivyo. Kansela wake Merkel alielezea msimamo wake akisema kuwa: "Kujiondoa kwa Uingereza ni pigo kali lililoelekezwa kwa Ulaya na kwa mfumo wa kuunganisha Ulaya." Alimualika Rais wa Ufaransa Hollande na Waziri Mkuu wa Italia Renzi na Rais wa Baraza la Ulaya Tusk kufanya mkutano mjini Berlin siku ya Jumatatu (27/06/2016) na kusema: "Matokeo yatategemea sisi wanachama 27 katika Muungano wa Ulaya kuthibitisha kuwa tunatamani na tunaweza kuchukua hitimisho la haraka na rahisi kutoka kwa kura ya maoni, jambo ambalo linaweza kusababisha kuigawa Ulaya zaidi... Leo ni hatua ya mabadiliko kwa Ulaya na kwa Muungano wa Ulaya na ushirikiano wa Ulaya. Ni lazima nchi za muungano zichambue hali na kuikadiria kwa utulivu na tahadhari kabla ya kuchukua maamuzi sahihi pamoja." (AFP, 24/06/2016). Waziri wake wa mambo ya nje Steinmeier alisema baada ya kutangazwa kwa matokeo ya kura ya maoni kwenye kituo cha ZDF cha Ujerumani: "Serikali ya Uingereza imecheza na hatima ya Ulaya na imepoteza." Wajerumani sasa wanatambua uovu wa Waingereza na matokeo yake mabaya. Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani ameweka wazi ukweli wa Uingereza kuwa imecheza na hatima ya Muungano wa Ulaya na haitaki ubaki ukiwa salama na wenye nguvu. Yeye ni mmoja wa wanasiasa wa Ujerumani mwenye uelewa mkubwa zaidi kuhusu Uingereza na hataki ibaki katika muungano kwa sababu anatambua ukweli wake kwamba ni kifaa cha kubomoa.

Mkutano wa viongozi wa Ujerumani, Ufaransa na Italia mjini Berlin mnamo 27/06/2016 ulikuja kusisitiza msisitizo wao wa kubaki kwa Muungano wa Ulaya ukiwa umeshikamana. Walipinga mazungumzo yoyote na Uingereza kuhusu kipindi cha baada ya kujiondoa kwake katika Muungano wa Ulaya madamu London haijawasilisha rasmi ombi la kujiondoa ili waweze kuishinikiza iwasilishe ombi hilo badala ya suala hilo kubaki limevunjika, kwani hilo lina madhara kwa muungano. Merkel alisema "tumekubaliana kuwa hayatapatikana mazungumzo rasmi au yasiyo rasmi kuhusu kujiondoa kwa Uingereza katika Muungano wa Ulaya madamu ombi la kujiondoa katika muungano halijawasilishwa katika ngazi ya Baraza la Ulaya" (DPA, 27/06/2016).

Lakini pamoja na hayo, wanatambua kuwa michezo ya Uingereza na ujanja wake ndio sababu. Kwa hiyo tatizo kwao linategemea uwezo wao wa kuendelea katika muungano wao na kuepuka ujanja wa Uingereza, ambayo ina uwezo mkubwa kuliko wao katika michezo ya kisiasa... Kwa vyovyote vile, ikiwa Waulaya wataweza kuachana na Uingereza haraka, na kufanya kazi ya kuchukua hatua mpya za kuimarisha muungano, basi hilo litakuwa bora kwao. Lakini Uingereza, ikiwa haitaweza kuanzisha uhusiano na Muungano wa Ulaya, itafanya kazi kutokea nje kuuvuruga muungano. Hata hivyo, yenyewe inakabiliwa na hali ya hatima kutokana na hali mbaya ya kiuchumi ambayo ishara zake mbaya zimeanza kujitokeza, kadhalika hali yake ya ndani ikiingia katika msukosuko ambapo Scotland inadai kufanyika kura mpya ya maoni ya kujiondoa katika Ufalme wa Uingereza, na Ireland inadai kujiondoa katika Ufalme wa Uingereza na kujiunga na Ireland ya Kusini. Ikiwa hilo litatokea, basi Uingereza itakuwa imekwisha kwani itajumuisha mikoa ya England na Wales pekee. Hivyo, kufanya kura ya maoni ilikuwa ni kamari ya hasara kwa Uingereza, na hila yake mbaya inaweza kuipata yenyewe kama ilivyojitokeza hadi sasa na kama inavyoonekana katika siku zijazo kwa mujibu wa data zilizotajwa hapo juu. Na ikiwa Muungano wa Ulaya utabaki macho dhidi ya michezo ya Uingereza, basi inaweza kusadikika kwayo kauli ya anayesema kuwa "itakuwa kama kisiwa cha Hong Kong, moja ya makoloni yake ya zamani, lakini katika pwani ya magharibi ya Ulaya na si katika pwani ya kusini ya China"!

5- Kwa ujumla, Uingereza imekuwa katika hali ya mkanganyiko mkubwa, na katika hali ambayo haikuipanga. Si rahisi kwake kuchukua uamuzi; kwani kurudi nyuma katika kura ya maoni kuna vikwazo vya kisheria na ni kuidharau demokrasia wanayojinasibu kwayo. Na kukamilisha safari ya kujiondoa kuna madhara kwa maslahi ya Uingereza, kwani zama za upendeleo kwa Uingereza zinaweza kuwa zimepita. Rais wa Tume ya Ulaya Jean-Claude Juncker alisema "inamlazimu yule anayetaka kuwa sehemu ya soko la pamoja la Ulaya kufuata sheria zake kali bila upendeleo." (BBC, 29/06/2016). Kutokana na hayo yote, ilikuwa ni jambo la kawaida kwa Uingereza kukimbilia kusuasua, na kukataa kuwasilisha ombi la kujiondoa, ikitumai kuwa miezi ijayo inaweza kuipatia njia ya kutokea itakayolinda sehemu kubwa ya maslahi yake.

Ama ikiwa Uingereza itajikuta inasukumwa katika njia ya kujiondoa kwa lazima, bila uhusiano wowote na muungano uwe wa kisiasa au kiuchumi, na kisha ikajikuta katika njia ya kudorora kwa uchumi na kusambaratika kisiasa, basi uwezekano mkubwa ni kwamba itafanya kazi kwa njia zake chafu kusambaratisha Muungano wa Ulaya. Baadhi ya nchi za Ulaya zenye uhusiano wa kijadi (uaminifu) nayo zinaweza kuitikia. Kiongozi wa chama cha UKIP, Farage, alitaja mnamo 28/06/2016 wakati wa malumbano katika Bunge la Ulaya mjini Brussels kuwa "Uingereza haitakuwa ya mwisho kujiondoa katika muungano," akiashiria kuwa Uingereza itakapojiondoa, wengine wataifuata... Inaweza kupata msaada katika usambaratishaji huo kutoka kwa Marekani kwa sababu maslahi ya Uingereza yanagusana kikamilifu katika hilo na maslahi ya Marekani.

Hivyo inaweza kusemwa kuwa kura ya maoni ya "Brexit" imekuja na matokeo kinyume na yale ambayo Uingereza iliyapanga, na imeleta mazingira ya kutoonekana vizuri (ukungu), na kufungua milango ya uwezekano wowote. Uingereza inaweza kuikwepa kura ya maoni na kuramba demokrasia yake, lakini wakati huo huo ina kiasi kikubwa cha hatari kinachoweza kuendelea na kuwa kifaa cha kuibomoa Uingereza kabla ya Ulaya. Na amesema kweli Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mwenye hikima:

وَلَا يَحِيقُ الْمَكْرُ السَّيِّئُ إِلَّا بِأَهْلِهِ "Na vitimbi viovu haviwapati ila wale walio fanya vitimbi hivyo." (QS. Fatir [35]: 43)

30 Ramadhan 1437 H 05/07/2016 M

Share Article

Share this article with your network