(Mfululizo wa majibu ya mwanachuoni Ata bin Khalil Abu al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook)
Kwa Ummu Sadin al-Maqdisiyyah
Swali:
Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh... Na Mwenyezi Mungu akubalie saumu na ibada zako.
Namuomba Yeye Aliyetukuka akuneemesheni nyinyi na sisi kwa nusura, tamkini (ushindi wa kudumu) na uthabiti, na akusaidie na kukukirimu kwa Ukhalifa wa pili kwa njia ya Utume, utakaokuwa ndani yake ni Khalifa wa sita miongoni mwa makhalifa waongofu, hakika Yeye ni Msimamizi wa hilo na ni Muweza wa kila kitu.
Sheikh wetu mpendwa, imeelezwa katika kitabu cha An-Nidham al-Ijtima'i fil Islam toleo la nne (1424 H - 2003 M) katika mada ya "Kuangalia Mwanamke", katika suala la sifa za vazi ambalo mwanamke huvaa juu ya nguo zake ukurasa wa 49-50: (Na inashurutishwa katika jilbab iwe imeshushwa kwenda chini mpaka isitiri miguu miwili, kwa sababu Mwenyezi Mungu anasema katika aya:
يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِنْ جَلَابِيبِهِنَّ
"Wajiteremshie shurungi zao (jilbab)." (QS. Al-Ahzab [33]: 59)
Yaani washushe jilbab zao kwa sababu neno min hapa si kwa ajili ya sehemu (tab'id) bali ni kwa ajili ya kubainisha (bayan), yaani washushe shuka au vazi la nje kuelekea chini. Na kwa sababu imepokewa kutoka kwa Ibn Umar kwamba amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema:
مَنْ جَرَّ ثَوْبَهُ خُيَلَاءَ لَمْ يَنْظُرِ اللَّهُ إِلَيْهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ، فَقَالَتْ أُمُّ سَلَمَةَ: فَكَيْفَ يَصْنَعُ النِّسَاءُ بِذُيُولِهِنَّ؟ قَالَ: يُرْخِينَ شِبْراً، قَالَتْ؟ إِذَنْ يَنْكَشِفُ أَقْدَامُهُنَّ. قَالَ: يُرْخِينَ ذِرَاعاً لَا يَزِدْنَ
"Mwenye kuburura nguo yake kwa ajili ya kiburi, Mwenyezi Mungu hatamtazama Siku ya Kiyama. Ummu Salamah akasema: Na wafanye nini wanawake na ncha za nguo zao? Akasema: Washushe kiasi cha shibri moja. Akasema: Hapo miguu yao itafunuka. Akasema: Basi washushe kiasi cha dhiraa moja na wasizidishe." (Imepokewa na At-Tirmidhi).
Hii ni bayana kwamba nguo anayovaa juu ya nguo zake - yaani shuka au vazi la nje - ishushwe chini mpaka isitiri miguu miwili. Ikiwa miguu miwili imesitiriwa kwa soksi au viatu, basi hilo halitoshelezi bila ya kuishusha chini kwa namna inayoonyesha kuwepo kwa mshuko (irkha), na hakuna ulazima wa kuifunika miguu kwani tayari imesitiriwa...):
1- Nimehisi kuna mgongano katika aya hii, pale aliposema: (Hii ni bayana kwamba nguo anayovaa juu ya nguo zake - yaani shuka au vazi la nje - ishushwe chini mpaka isitiri miguu miwili), na kati ya kauli yake: (na hakuna ulazima wa kuifunika miguu kwani tayari imesitiriwa). Je, tunawezaje kuelewa jambo hili? Je, ni lazima kwa mwanamke kuifunika miguu yake kwa jilbab yake, au kuisitiri kwa soksi inatosheleza badala ya kuifunika (kwa jilbab)?
Jambo jingine Sheikh wetu mpendwa, na unisamehe kwa kuwa nimekuwa mrefu kwako...
2- Kuhusu hadith aliyoipokea Ibn Umar amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: "Mwenye kuburura nguo yake kwa ajili ya kiburi, Mwenyezi Mungu hatamtazama Siku ya Kiyama. Ummu Salamah akasema: Na wafanye nini wanawake na ncha za nguo zao? Akasema: Washushe kiasi cha shibri moja. Akasema: Hapo miguu yao itafunuka. Akasema: Basi washushe kiasi cha dhiraa moja na wasizidishe." Imepokewa na At-Tirmidhi. Je, kipimo cha Ummu Salamah kwa jambo hili kilikuwa ni kuanzia wapi? Je, ni kuanzia kwenye kiwiko au kuanzia katikati ya mguu?
Na ni kiasi gani cha ushushaji wa jilbab ya mwanamke? Je, aifanye ibururike ardhini, au aifunike miguu yote, au materu (vifundo) ya miguu pekee? Na je, kuifunika kwa soksi kunatosheleza au vipi?
Barakallahu fika na katika juhudi zako... Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.
Ummu Sadin, Baitul Maqdis
Jawabu:
Waalaykum Assalam Warahmatullahi Wabarakatuh.
a- Wanawake, hususan wa vijijini (jangwani), walikuwa wakitembea peku au wakivaa viatu ambavyo havifuniki miguu yote. Hivyo, miguu ya mwanamke ilikuwa ikionekana isipokuwa akiburura nguo yake ardhini ili miguu yake isionekane wakati wa kutembea. Wakati Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alipokataza kuburura nguo kwa kiburi, Ummu Salamah aliona kuwa mwanamke ikiwa nguo yake haibururiki ardhini, basi anapotembea na kusogeza miguu yake wakati wa mwendo, miguu yake itafunuka. Hii ni kwa sababu miguu haikufunikwa, kwani anatembea peku au amevaa viatu visivyoisitiri... Hivyo akamuuliza Mtume (saw): "Na wafanye nini wanawake na ncha za nguo zao?" Kwa sababu wanawake walikuwa na jilbab zao au abaya zao zikibururika ardhini ili miguu yao isionekane... Mtume (saw) akawajuzia washushe kiasi cha shibri moja kisha dhiraa moja zaidi ya miguu miwili ili hata akitembea peku, miguu isionekane madamu nguo imeshushwa chini ya miguu na inabururika ardhini... Hivyo mada ilikuwa ni: (kuburura nguo kwa ajili ya kusitiri miguu...), yaani swali lilikuwa kwa ajili ya kusitiri miguu. Kwa ibara nyingine, kuburura jilbab ardhini chini ya miguu kulikuwa ni kwa ajili ya kusitiri miguu. Sababu ('illah) ya kuburura nguo ardhini zaidi ya ule ushushaji wa kawaida ni kusitiri miguu. Na hukumu inayotokana na sababu (ma'lul) huzunguka na sababu yake ('illah) katika kuwepo na kutokuwepo kwake. Hivyo ikiwa miguu miwili imesitiriwa, basi nguo haibururwi ardhini, bali inatosha kutimiza maana ya idnaa (ushushaji) uliotajwa katika aya:
يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِنْ جَلَابِيبِهِنَّ
"Wajiteremshie shurungi zao (jilbab)." (QS. Al-Ahzab [33]: 59)
Yaani kwamba nguo ishushwe mpaka kwenye miguu iliyositiriwa.
b- Ama kuhusu ni wapi Ummu Salamah alipima hiyo shibri au dhiraa, suala lilikuwa ni "kuburura nguo ardhini", hili ndilo ambalo Ummu Salamah alikuwa akiulizia. Alikuwa akiona kwamba ikiwa nguo haibururiki ardhini, basi miguu miwili itafunuka wakati wa kutembea, na hili ni sahihi. Kwani nguo ikiwa haibururiki ardhini hata kidogo, na mwanamke akatembea peku au amevaa viatu visivyofunika mguu wote, basi mwanamke wakati wa kusogeza miguu yake katika kutembea, sehemu za miguu zitafunuka... Mtume (saw) akamruhusu ashushe shibri moja ardhini kwa sababu hadith inazungumzia kuburura nguo, na neno "kuburura" (jarra) linamaanisha ardhini. Hii inaonyesha kuwa shibri inayobururika ardhini ni kuanzia chini ya mguu.
Na ninarudia kusema kuwa hili ni ili mguu usifunuke wakati wa kutembea. Hivyo ikiwa mguu umesitiriwa kwa soksi, basi inatosha kushusha jilbab mpaka juu ya mguu uliositiriwa na soksi, yaani inatosha mpaka kwenye materu (vifundo vya miguu) madamu mguu wote umefunikwa.
Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu al-Rashtah
Kiungo cha jawabu kutoka kwa ukurasa wa Amir kwenye Facebook
Kiungo cha jawabu kutoka kwenye tovuti ya Amir
Kiungo cha jawabu kutoka kwa ukurasa wa Amir kwenye Google Plus