Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Kuharakisha kuchukua Deni na kupunguza Sehemu yake

July 12, 2019
4988

(Silsila ya majibu ya mwanachuoni mtukufu Ata bin Khalil Abu al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi")

Kwa Khalid Abu al-Walid

Swali:

Mwenyezi Mungu akubariki Sheikh wetu, akuhifadhi na kukulinda... nina swali kuhusu mada hii... hivi sasa nafanya kazi katika taasisi binafsi na wananikata fedha kwa ajili ya bima na mafao ya uzeeni (pensheni), nami nataka kuchukua sehemu ya kiasi hiki cha fedha ambacho kimekatwa kutoka kwangu, lakini wananilazimisha kuchukua asilimia fulani (yaani wanapunguza) kutoka kwenye kiasi hiki ambacho ni haki yangu... Je, jambo hili linaruhusiwa kisheria?

Mwenyezi Mungu akubariki na arefushe umri wako.

Jibu:

Waalaykum Salam Warahmatullahi Wabarakatuh,

Nimeelewa kutokana na swali lako kuwa unataka kuharakisha sehemu ya mafao yako (pensheni) kabla ya muda wake wa kustahiki uliowekwa katika mkataba wako wa kazi...

Naona kana kwamba suala hili linaangukia katika mlango wa kuharakisha kulipa deni, yaani ikiwa mtu ana deni kwa mwingine na muda wa kulipa deni hilo ni baada ya miaka miwili kwa mfano, iwe ni kulipa kwa awamu hadi mwisho wa miaka miwili au ni kulipa kwa mkupuo mmoja baada ya miaka miwili, kisha mdai akamwambia mdaiwa "nilipe kiasi hicho sasa hivi na mimi nitakupunguzia kiasi fulani kinachojulikana"... Hii inafanana na suala lako, kwani wewe unacho kiasi cha fedha katika taasisi unayofanyia kazi ambacho watakupa utakapofikisha umri wa miaka (60) kwa mfano, na sasa hivi una umri wa miaka arobaini na unataka sehemu ya mafao hayo sasa hivi kabla ya muda wake baada ya miaka ishirini.

Suala la kuharakisha ulipaji wa deni mkabala wa kupunguza sehemu yake, yaani badala ya mdai kuchukua thamani ya deni (1000) baada ya mwaka mmoja, anaichukua sasa hivi ikiwa (900). Suala hili lina hitilafu miongoni mwa wanachuoni... Na tayari tulishajibu suala hili katika jibu tulilotoa tarehe 14 Safar 1434 H - 27/12/2012 M, na nakurejeshea baadhi ya yale yaliyokuja katika jibu hilo ambayo yana mafungamano na jambo hili:

(... Ama kuhusu swali lako, hili liko kwa mafaqihi kama tulivyosema chini ya mlango wa "dha' wa ta'ajjal", yaani punguza sehemu ya deni lililoahirishwa mkabala wa kulipwa deni hilo au sehemu yake kwa haraka... Na suala hili lina hitilafu:

  • Miongoni mwao kuna wale wasioruhusu na wanategemea dalili miongoni mwazo:

1- Alichopokea Al-Bayhaqi katika Sunan al-Kubra kutoka kwa Al-Miqdad bin al-Aswad amesema:

أَسْلَفْتُ رَجُلاً مِائَةَ دِينَارٍ، ثُمَّ خَرَجَ سَهْمِي فِي بَعَثٍ بَعَثَهُ رَسُولُ اللهِ e، فَقُلْتُ لَهُ: عَجِّلْ لِي تِسْعِينَ دِينَاراً وَأَحُطُّ عَشَرَةَ دَنَانِيرَ، فَقَالَ: نَعَمْ، فَذَكَرَ ذَلِكَ لِرَسُولِ اللهِ e، فَقَالَ: «أَكَلْتَ رِباً يَا مِقْدَادُ، وَأَطْعَمْتَهُ»

"Nilikopesha mtu dinari mia moja, kisha likatoka jina langu katika jeshi lililotumwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), nikamwambia: Nihesabie dinari tisini sasa hivi na nitakuachia kumi, akasema: Ndio. Nikataja hilo kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), akasema: 'Umekula riba ewe Miqdad, na umemlisha (mwingine).'"

(Kwa taarifa tu, Imam Ibn al-Qayyim amesema katika Ighathat al-Lahfan: "Katika sanad ya hadithi ya Al-Bayhaqi kuna udhaifu").

2- Walisema kuwa inajulikana kwamba riba ya kijahilia ilikuwa ni mkopo uliocheleweshwa kwa nyongeza iliyoshartiwa, hivyo nyongeza ilikuwa ni badala ya kuongezewa muda, Mwenyezi Mungu akaibatilisha na akaiharamisha, akasema:

وَإِنْ تُبْتُمْ فَلَكُمْ رُءُوسُ أَمْوَالِكُمْ

"Na mkitubu, basi mna haki ya kurejeshewa rasilimali zenu." (QS. Al-Baqarah [2]: 279)

Waliongeza kuwa kupunguza sehemu ya deni badala ya kusogeza karibu muda wa kulipwa pia ni haramu kwa sababu ya fidia inayotokana na muda, iwe ni kwa kuongeza au kupunguza.

Wamesema kuwa jambo hili la "dha' wa ta'ajjal" ni haramu Jamhur (wengi) wa mafaqihi kutoka kwa Mahanafi, Mamaliki, Mashafi na Mahanbali, na likachukizwa na Zaid bin Thabit, Ibn Umar na idadi fulani ya Tabi'ina.

  • Na miongoni mwao kuna wanaoliruhusu na wanategemea dalili miongoni mwazo:

1- Kutoka kwa Ibn Abbas (ra) amesema:

لَمَّا أَرَادَ رَسُولُ اللَّهِ e أَنْ يُخْرِجَ بَنِي النَّضِيرِ قَالُوا: يَا رَسُولَ اللَّهِ، إِنَّكَ أَمَرْتَ بِإِخْرَاجِنَا وَلَنَا عَلَى النَّاسِ دُيُونٌ لَمْ تَحِلَّ، قَالَ: «ضَعُوا وَتَعَجَّلُوا»

"Wakati Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alipotaka kuwafukuza Bani al-Nadir, walisema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, hakika umeamrisha tufukuzwe na hali tuna madeni kwa watu ambayo muda wake bado haujafika, akasema: 'Punguzeni (madeni yenu) na uharakisheni (kuyachukua).'" (Imepokewa na Al-Hakim katika Mustadrak al-Sahihayn na akasema hii hadithi ina sanad sahihi ingawa hawakuitoa).

(Kwa taarifa tu, Al-Dhahabi amesema katika muhtasari wake kwamba Al-Zanji ni dhaifu na Abdul-Aziz si mwaminifu. Na Ibn al-Qayyim amesema katika Ahkam Ahl al-Dhimmah: "Sanad yake ni hasan, hakuna aliye ndani yake isipokuwa Muslim bin Khalid al-Zanji na hadithi yake haishuki chini ya daraja ya hasan.")

2- Kauli ya Abdullah bin Abbas (ra): "Hakika riba ni niahirishie nami nitakuongezea" na si "niharakishie nami nitakupunguzia".

Imepokewa kuruhusiwa kwa jambo hilo kutoka kwa Ibn Abbas, al-Nakha'i, al-Hasan, na Ibn Sirin, na ni riwaya kutoka kwa Imam Ahmad na rai mojawapo kwa Mashafi, na ndio uchaguzi wa Sheikh al-Islam Ibn Taymiyyah na mwanafunzi wake Ibn al-Qayyim, na akairuhusu Ibn Abidin miongoni mwa mafaqihi wa Kihanafi kama ilivyo katika hashiya yake ya "Al-Durr al-Mukhtar".

Nasi hatupendi kufanya tabanni katika suala hili, basi mwenye suala na amfuate (taqlid) yule miongoni mwa mafaqihi anayemtumainia rai yake...) Mwisho.

Na kama unavyoona, sisi hatupendi kufanya tabanni katika hili, bali unaweza kufuata rai ya mujtahidi ambaye unamtumainia kwa usahihi wa rai yake... Na rai hizo mbili ziko wazi: rai ya kwanza inaona kuwa kuharakisha kupokea haki yako kwa kupunguza sehemu yake hairuhusiwi na ni riba... Na rai ya pili inasema inaruhusiwa kuharakisha kuchukua haki yako au sehemu yake kwa kupunguza kitu fulani kutoka kwayo... Na kama nilivyokutajia awali, sisi hatupendi kufanya tabanni ya rai yoyote kati ya hizo mbili.

Mwishoni, namuomba Mwenyezi Mungu akufungulie kifua chako kwa lile lililo kheri.

Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu al-Rashtah

8 Dhu al-Qi'dah 1440 H Sawa na 11/07/2019 M

Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Mungu amhifadhi) kwenye: Facebook

Share Article

Share this article with your network