Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Madhara ya Mgogoro wa Ugiriki

February 28, 2015
3029

Swali:

Habari ziliripoti mnamo Ijumaa tarehe 27/02/2015 kwamba Bunge la Ujerumani limeidhinisha kwa wingi wa kura kurefushwa kwa misaada kwa Ugiriki kwa muda wa miezi minne... Je, hii inamaanisha kuwa mgogoro wa Ugiriki umekwisha, na kwamba Ugiriki itaendelea kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya bila vizuizi? Kisha imebainika kuwa Marekani inajali sana Ugiriki kubaki katika Umoja wa Ulaya na kutatua matatizo yake; Obama alieleza wakati wa kilele cha mgogoro katika mahojiano na mtandao wa CNN mnamo 01/02/2015 akielezea "matumaini yake kuwa Ugiriki itabaki katika eneo la Euro" na akataja kuwa "hilo linahitaji maelewano kutoka pande zote", akisema "njia bora ya kupunguza upungufu wa bajeti na kurejesha uthabiti ni kupitia ukuaji wa uchumi". Je, ni nini msukumo wa kuingilia kati huku kwa wazi kwa Marekani katika mgogoro wa Ugiriki? Na Mwenyezi Mungu awalipe kheri.

Jibu:

Ili picha iwe wazi, tutapitia mambo yafuatayo:

  1. Mgogoro wa kifedha wa hivi karibuni wa Ugiriki ulianza kujitokeza mwishoni mwa mwaka 2009 baada ya kulipuka kwa mgogoro wa kifedha wa kimataifa nchini Marekani — kitovu cha urasilimali — na kuikumba Ulaya na ulimwengu mzima unaofuata mfumo wa kirasilimali. Mgogoro huo uliipigo Ugiriki mnamo Aprili 2010, na kufuatia hilo, mnamo 23/06/2010, serikali ya Ugiriki iliomba rasmi Umoja wa Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuamsha mpango wa uokoaji unaohusisha mikopo ili kuisaidia Ugiriki kuepuka kufilisika na kushindwa kulipa madeni. Viwango vya riba kwenye dhamana za serikali ya Ugiriki vilipanda, vilevile bima dhidi ya kushindwa kulipa ilipanda hadi viwango vya juu kutokana na hofu ya wawekezaji kuhusu "kutokuwa na uwezo wa Ugiriki kulipa madeni yake, huku kukiwa na ongezeko la upungufu wa bajeti na kuongezeka kwa deni la taifa, pamoja na ukuaji duni wa uchumi wa Ugiriki". Mgogoro huu ulitishia hali ya Euro na eneo lake, na hivyo basi Umoja wa Ulaya mzima, na kuibua wazo la Ugiriki kujiondoa katika eneo hili la kiuchumi. Hata hivyo, Ulaya iliamua kutoa msaada kwa Ugiriki mkabala na kutekelezwa kwa mageuzi ya kiuchumi na hatua za kubana matumizi (austerity) zinazolenga kupunguza upungufu wa bajeti ya serikali. Ikumbukwe kuwa mpango wa sasa wa kile kinachoitwa mageuzi ulikuwa unamalizika tarehe 28 Februari mwaka huu. Makubaliano hayo hayakuwa ya kudumu katika maudhui yake, bali yalichelewesha tu mlipuko kama ilivyosemwa.

  2. Kifurushi kilichotolewa kwa Ugiriki tangu miaka 5 iliyopita kinakadiriwa kuwa na thamani ya Euro bilioni 240, wakati deni la Ugiriki kwa sasa limefikia Euro bilioni 323 likiwa limegawanywa hivi: 60% ya madeni haya yanatoka katika eneo la Euro, 10% kutoka IMF, 6% kutoka Benki Kuu ya Ulaya, 4% kutoka benki za Ugiriki, 1% kutoka benki za kigeni, 1% kutoka Benki Kuu ya Ugiriki, 3% mikopo mingine, na 15% ni dhamana za hazina. Kundi la Euro linaweka sharti la kufikia ziada katika bajeti ya 3% baada ya kulipa riba ya mikopo. Ugiriki haina uwezo wa kufikia hilo, lakini Waziri wa Fedha wa Ugiriki anasema kuwa nchi yake haijafungwa tena na sharti hili kulingana na makubaliano ya hivi karibuni, huku Ujerumani na kundi hilo zikiwa hazijatoa ufafanuzi wowote kuhusu suala hili. Sera ya kubana matumizi iliyowekwa kwa Ugiriki katika miaka ya hivi karibuni imesababisha hali ya kudorora kwa uchumi, kuongezeka kwa kiwango cha ukosefu wa ajira hadi 27%, na kufilisika kwa karibu theluthi moja ya miradi ya kibinafsi. Ugiriki imekuwa ikiishi tangu 2010 chini ya mpango wa kubana matumizi, na uokoaji wa kifedha wa Ulaya kwa ajili ya kulipa madeni yake umechukua zaidi ya Euro bilioni 200 za mikopo iliyotolewa hadi sasa kuokoa benki na mifuko ya uwekezaji inayoidai Ugiriki, hasa benki za Ufaransa na Ujerumani. Mikopo hii ilitolewa na Umoja wa Ulaya, IMF, na Benki Kuu ya Ulaya mkabala na Ugiriki kujifunga na hatua za kubana matumizi. Hii ina maana kwamba Umoja wa Ulaya unazilipa benki zake zilizoikopesha Ugiriki kwa riba kubwa ya haramu, wakati ambapo raia wa Ugiriki amepoteza imani na uchumi wa nchi yake; kwa mfano, Euro bilioni 18 zilitolewa tangu mwezi Desemba uliopita, na milioni 500 zilitolewa mnamo tarehe 18 na 19 ya mwezi huu. Yote haya yanaonyesha ufisadi na hatari ya kile kinachoitwa mipango ya uokoaji ya kirasilimali; kwani ni yenye kuzamisha na sio kuokoa, na ni yenye kuangamiza nchi na waja...

  3. Ujerumani ilikuwa nchi kali zaidi katika suala la mgogoro wa Ugiriki na ilikataa kuisamehe madeni. Kwa sababu hiyo, Ujerumani ilikuwa mstari wa mbele katika mazungumzo na kuyaongoza, kiasi kwamba yalitajwa kuwa ni mazungumzo kati ya Ujerumani na Ugiriki. Habari zilieleza kuwa makubaliano hayakufikiwa kupitia mazungumzo ya kweli kati ya mawaziri wa nchi 19 katika eneo la Euro na Ugiriki, bali yalifanyika kupitia mazungumzo kati ya Waziri wa Fedha wa Ujerumani na mwenzake wa Ugiriki mbele ya maafisa wa IMF na Benki Kuu ya Ulaya. Hali hii imeruhusu mrengo unaopinga Umoja wa Ulaya nchini Uingereza kuongeza ukosoaji wake kwa umoja huo ukichukuliwa kama klabu inayotawaliwa na Ujerumani ambayo inajaribu kuitawala Ulaya kupitia hiyo. Ujerumani imeanza kuhisi kuwa ndiyo kiongozi wa kifedha wa Umoja wa Ulaya kwa sababu ni nchi yenye nguvu zaidi kiuchumi Ulaya, na kila nchi inaitegemea na kuonyesha uhitaji wake kwa msaada wake. Ujerumani haitaki kulegeza kamba katika suala la mgogoro wa Ugiriki kwa sababu "maambukizi" hayo yatahamia Ureno kama hatua ya kwanza, na baadaye Ireland, Italia, Hispania na nchi nyingine za Umoja zinazokabiliwa na matatizo kama hayo. Nchi hizi ziko chini ya mpango wa uokoaji na zinatekeleza sera ya kubana matumizi iliyowekwa na Ujerumani kwa jina la Umoja. Ikiwa Ujerumani italegeza kamba kwa Ugiriki, nchi hizo zitaanza kuachana na sera ya kubana matumizi inayowalemaza raia wao. Kwa hiyo, Waziri wa Fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble, ambaye ni mmoja wa wapinzani wakali wa wazo la kuisamehe Ugiriki madeni, alisema: "Ugiriki haitapata misaada kabla ya kutekeleza masharti yaliyomo kwenye makubaliano ya sasa" na akasema: "Serikali inayoongozwa na wanajamaa inapitia nyakati ngumu" (BBC 21/02/2015). Msemaji wa serikali ya Ugiriki Panagiotis Agrafiotis alisema "Ugiriki na Ujerumani zimefikia makubaliano kuhusu kurefusha mpango wa mikopo ya uokoaji wa Ugiriki kwa muda wa miezi 4, na akasema kuna makubaliano kuhusu taasisi washirika, Ugiriki na Ujerumani" (Al-Quds 20/02/2015). Hatimaye, baada ya serikali ya Ugiriki kuahidi kujifunga na mpango huo bila masharti yoyote, Bunge la Ulaya — au tuseme Bunge la Ujerumani — mnamo 27/02/2015 liliidhinisha kurefusha muda kwa miezi minne... Schäuble alisisitiza kuwa makubaliano ya sasa "hayatajumuisha kutoa mabilioni mapya kwa Ugiriki wala hayana mabadiliko yoyote katika mpango wa sasa" (Al-Arab ya London 28/02/2015). Schäuble alijaribu kutoa uhakikisho kuwa jambo hilo halihusiani kabisa na "kutoa mabilioni mapya kwa Ugiriki" au kurekebisha masharti ya mpango wa sasa. Kamishna wa Ulaya wa Masuala ya Kiuchumi, Pierre Moscovici, aliitaka Athens "kuheshimu ahadi zake kwa washirika wake wa Ulaya na IMF" (27/02/2015 swissinfo.ch-afp_tickers).

  4. Kuhusu msimamo wa Ufaransa, ambayo ni nchi kuu katika Umoja wa Ulaya pamoja na Ujerumani, Rais wa Ufaransa François Hollande alielezea makubaliano hayo kama "maelewano mazuri kwa Ugiriki na wakopeshaji wake" (BBC 21/02/2015). Waziri wa Fedha wa Ufaransa, Michel Sapin, alisema "Athens ilikubali mwishowe kubaki chini ya usimamizi wa wadai, lakini kutakuwa na kazi ya aina nyingine, hakika kutakuwa na kazi ya kisiasa akibainisha kuwa Wagiriki hawataki tena kukutana na wataalamu wa kiufundi" (Shirika la habari la AFP 21/02/2015). Shirika hilo liliongeza "ikiwa Ugiriki itatimiza masharti yake, itapata hadi dola bilioni 2.7 kutoka kwa fedha zilizobaki za ufadhili wa Ulaya katika mfumo wa mpango wa uokoaji wa Euro bilioni 240. Ugiriki ina shauku ya kufunga ukurasa wa kubana matumizi lakini Ujerumani, mdhamini wa msimamo mkali wa bajeti barani Ulaya, iliweka sharti kwamba Ugiriki iendelee kusafisha fedha zake na kuendelea na mageuzi ya kimuundo".

  5. Kuhusu msimamo wa Marekani, ulikuwa wazi kwa kuingilia kati suala hili hadharani. Rais wa Marekani Barack Obama alieleza katika mahojiano na mtandao wa CNN mnamo 01/02/2015 akitoa maoni juu ya mgogoro wa kifedha nchini Ugiriki, akisimama upande wake na kukosoa msimamo wa Umoja wa Ulaya kuelekea nchi hiyo kwa kusema: "Haiwezekani kuendelea kuzinyonya nchi zinazopitia migogoro" na akaongeza "katika hatua fulani ni lazima kuwe na mkakati wa ukuaji ili kuweza kulipa madeni". Alikiri kwamba "kuna haja ya dharura kwa Ugiriki kufanya mageuzi" lakini akasema "ni vigumu sana kuanza mabadiliko haya ikiwa kiwango cha maisha cha watu kimeshuka kwa 25%. Kwa muda mrefu, mfumo wa kisiasa na jamii haviwezi kuvumilia hilo". Obama alielezea "matumaini yake kuwa Ugiriki itabaki katika eneo la Euro" na akataja kuwa "hilo linahitaji maelewano kutoka pande zote" na alikosoa sera ya Ulaya ya kubana matumizi, akisema "wakati uchumi unadorora mfululizo, unapaswa kuwa na mkakati wa ukuaji, na si tu kufanya jitihada za kuendelea kumnyonya mwananchi anayeteseka zaidi na zaidi". Alisema "njia bora ya kupunguza upungufu na kurejesha uthabiti ni kupitia ukuaji wa uchumi". Kauli ya Rais wa Marekani ilikuja siku chache baada ya ushindi wa chama cha mrengo wa kushoto cha Syriza katika uchaguzi wa bunge nchini Ugiriki uliofanyika mnamo 25/01/2015 na karibu mwezi mmoja kabla ya kumalizika kwa hatua ya uokoaji ya Ulaya kwa Ugiriki, ili kutoa ishara ya wazi kwa Ulaya kwamba anasimama upande wa Ugiriki na kuikosoa Ulaya ili kuishinikiza iibakishe Ugiriki ndani ya Umoja wa Ulaya na kutumia msaada wake dhidi ya Umoja huo. Marekani inataka Ugiriki ibaki ndani ya Umoja wa Ulaya ili Umoja huu uendelee kuteseka na migogoro na nyufa, na kubaki kuwa umoja dhaifu unaotishiwa kusambaratika.

  6. Kuhusu Ugiriki yenyewe, ambayo ilipata serikali ya mrengo wa kushoto inayoongozwa na chama cha Syriza mwezi mmoja uliopita, inataka kubaki katika Umoja wa Ulaya. Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras alisifu makubaliano hayo akisema: "Serikali yake imezuia mpango wa nguvu za kihafidhina nchini Ugiriki na nje ya nchi wa kuifilisi nchi mwishoni mwa mwezi" yaani muda wa kumalizika kwa mpango wa uokoaji wa Ulaya. Aliongeza "makubaliano na viongozi wa Umoja wa Ulaya kurefusha muda kwa Ugiriki kwa miezi minne yatamaliza hatua za kubana matumizi zinazochukiwa nchini. Hata hivyo, serikali bado inakabiliwa na changamoto ngumu" na akidai kuwa "makubaliano hayo yanafuta kubana matumizi". Hata hivyo, makubaliano haya yalikuja mkabala na kutoa makubaliano ikiwemo kujifunga kwake na kile kinachoitwa mageuzi ndani ya siku mbili. Alisema "serikali yake itajikita katika kujadiliana kuhusu mageuzi mapya na wafadhili ifikapo Juni" (AFP 21/02/2015). Serikali ya Ugiriki ilikuwa imeomba kurefushwa kwa ufadhili kwa miezi 6 ili iweze kuwasilisha mipango ya mageuzi kwa miaka minne. Serikali ya Ugiriki ilisema kuwa imeepuka makato makubwa ya pensheni na kuepuka kupandisha kodi kwa kiasi kikubwa na kuwashawishi wadai wa Ulaya kuacha madai yao yasiyo ya kweli kuhusu bajeti. Waziri wa Fedha wa Ugiriki alichukulia makubaliano hayo kama hatua ya kwanza katika safari ndefu akiongeza: "Hakuna anayeweza kulazimisha uchumi wetu na jamii yetu hatua ambazo hatukubaliani nazo na hili ndilo jambo jipya katika makubaliano. Sasa tuna mfumo mpya, lakini tunaheshimu yaliyopita. Sasa tumeahidi kushiriki katika kuandika mageuzi haya ambayo tutawajibika kwayo". Kwa upande wake, Waziri wa Fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble alisema: "Maadamu mpango na Ugiriki haujakubaliwa kwa mafanikio, hakutakuwa na pesa na hili liko wazi" (Euronews 21/02/2015). Hiyo ilikuwa kabla ya Ugiriki kukubali masharti ya mpango huo na kisha Ujerumani kukubali kurefusha muda.

  7. Kuhusu msimamo wa Uingereza, Waziri wa Fedha wa Uingereza George Osborne alielezea hali ya sasa katika mzozo wa Ugiriki na washirika wengine katika eneo la Euro kama "inawakilisha hatari kwa utulivu wa uchumi wa Uingereza, na akataka nchi za Euro zifikie suluhisho la pamoja ili ziweze kuzuia mgogoro unaoongezeka". Alisema "katika hali hii ngumu kuna hatari ya mgogoro ambao unaweza kusababisha uharibifu mkubwa kwa uchumi wa Ulaya na pia unawakilisha hatari kwa Uingereza" (Sky News 20/02/2015). Uingereza inataka Umoja wa Ulaya uendelee kuwepo maadamu inanufaika nao na haujengi hatari kwake. Hasa kwa vile ulimwengu wa Magharibi mzima unateseka na mgogoro wa kifedha uliokithiri, hivyo kusambaratika kwa Umoja wa Ulaya kwa wakati huu kutaipiga pigo ambalo linaweza kuwa la mwisho kwa uchumi wa kirasilimali kwa ujumla. Nayo — yaani Uingereza — inataka Umoja wa Ulaya uendelee kuwepo ili ushindane na Marekani na iweze kuutumia katika mapambano yake ya siri na Marekani na kuizuia hii ya mwisho kuwa peke yake katika siasa za ulimwengu.

  8. Tunahitimisha kutoka kwa yote hayo yafuatayo:

    a- Umoja wa Ulaya ni umoja dhaifu, kwa sababu haujajengwa juu ya umoja wa maamuzi ya kisiasa wala si chombo kimoja cha kisiasa. Hakuna utawala mmoja wa kati unaouendesha, bali ni kundi la nchi zinazokubaliana katika maeneo na misimamo fulani na kutofautiana katika mengine. Nguvu zake kuu zinashindana zenyewe kwa zenyewe juu ya uongozi wake na kulazimisha matakwa yake, hasa tukijua kwamba umejengwa juu ya manufaa (utilitarianism) kwa sababu ya kufuata kwao mabda (itikadi) ya kirasilimali inayofanya manufaa kuwa msingi na kipimo cha vitendo. Pia ni nchi za kifaunaini (utaifa) zinazojaribu kutafuta mamlaka juu ya wengine, kwa sababu mabda hii ilikubali utaifa na haikuutibu, hivyo haikuweza kuunganisha mataifa yanayoiandama katika chungu kimoja. Nchi za Ulaya, hasa zile kubwa, zinashindana zenyewe kwa mamlaka juu ya nchi za Umoja; Ujerumani inajaribu kufikia hilo, Ufaransa inatafuta jukumu kuu la kushirikiana na Ujerumani, na Uingereza inatafuta kuutumia Umoja huo kushindana na Marekani ili yenyewe inufaike pande zote mbili.

    b- Marekani inajaribu kupenya katika nchi za Umoja na kuziathiri, na inafanya kazi kuupiga na kuudhoofisha ili usiwe umoja mmoja wa kisiasa wenye nguvu inayotia athari kimataifa, na ili Euro ianguke, isibaki kuwa sarafu ya kimataifa inayoshindana na sarafu yake ya Dola. Marekani inatumia migogoro ya Umoja huo na matatizo yake na kukosoa utatuzi wake ili kushusha hadhi yake na ili yenyewe ibaki kuwa kiongozi wa ulimwengu wa kirasilimali bila mpinzani. Imetumia mgogoro wa Ugiriki, na inafanya kazi ya "kuitekenya" serikali ya mrengo wa kushoto nchini humo na kuivuta kwake, na inatetea kubaki kwake katika Umoja ili uendelee kuwa dhaifu ukiliwa na migogoro, na itafanya kazi ya kuitumia na kuichochea kuchukua misimamo dhidi ya Umoja wa Ulaya ili Ugiriki iwe sababu ya udhaifu au mpasuko kwa Umoja huo, na hivi ndivyo Umoja unavyokabiliwa na hatari ya kuanguka.

    c- Ujerumani inafanya kazi kulinda Umoja huo na kundi la Euro na kuvitia nguvu, na karibu imekuwa na neno la kwanza ndani yake. Ni mnufaika wa kwanza kwani taasisi zake za kifedha ndizo zinazonufaika; zinaikopesha Ugiriki na nchi nyingine za Ulaya na kurudishiwa fedha hizi kwa faida (riba), hivyo kuendesha gurudumu la uchumi wa taasisi zake za kifedha kama benki, mifuko ya akiba na makampuni ya bima. Inafanya kazi kuimarisha ushawishi wake ndani yake, na kwa sasa inasifiwa kama nchi kubwa ya wastani ulimwenguni. Ufaransa ni mnufaika wa pili kwa namna ya Ujerumani na inafanya kazi kuimarisha jukumu lake la kimataifa kupitia Umoja huo. Inabaki Uingereza inayofuatilia hali hiyo kana kwamba si mwanachama ndani yake; haifanyi kazi kuuimarisha wala haijaribu kuuangusha, bali inafanya kazi ya kunufaika nao na kuutumia kwa maslahi yake.

    d- Hivi ndivyo ushindani utakavyoendelea kati ya nchi kubwa katika Umoja, na mgogoro utaendelea kati ya Umoja huo na Marekani ambayo inajaribu kuuvunja na kuusambaratisha ikiwezekana, na inajaribu kuiangusha Euro kama sarafu ya kimataifa ili kubakisha karatasi yake ya kijani (Dola) — ambayo haina thamani zaidi ya wino uliotumika kuichapa — kama sarafu ya kimataifa inayopora kwayo kheri za ulimwengu na kufadhili zana zake za kijeshi ili kuhakikisha mamlaka yake ya kimataifa kama nchi ya kwanza inayoutawala ulimwengu.

    e- Hivi ndivyo inavyothibitika mara kwa mara kwamba urasilimali ni mabda batili, na mfumo wake wa kiuchumi ni mfisadi, na matatibu yake ni hatari na matokeo yake ni mabaya; hautibu magonjwa bali unafanya kazi ya kuyatuliza tu kwa muda, hivyo matatizo yanabaki na magonjwa yanakuwa sugu. Riba ambayo inategemewa kama msingi katika miamala na mikopo ni yenye kuteketeza na kuulemea mkopaji. Zaidi ya hapo, nchi inayokopa inayotoa dhamana za hazina ili kukopa kwa riba lazima iweke bima kwa dhamana hizi, hivyo hulipa mabilioni mengine mengi mkabala na bima hiyo. Hivyo mizigo huongezeka kwa nchi inayokopa na jambo hilo haliokoi, bali inaendelea kuteseka na upungufu wa bajeti na kutokuwa na uwezo wa kulipa deni, na kuiacha chini ya udhibiti wa wadai! Na inawaacha raia wake wakiishi katika dhiki na maisha magumu kutokana na kulazimishwa kutekeleza sera ya kubana matumizi. Ugiriki ambayo inazungumziwa sasa ni mfano wa wazi wa hilo; matatibu yote ya mgogoro wake kama ilivyobainika hapo juu ni kama dawa za kutuliza maumivu kwa muda kisha hupuka tena... Ikumbukwe kwamba Ugiriki iliishi kwa muda wa karne nne katika neema ya maisha, utulivu, amani na usalama chini ya utawala wa Kiislamu.

Share Article

Share this article with your network