Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

JIBU LA SWALI: KUWAHAMISHA WAKAAZI WA GAZA

February 25, 2025
4499

Swali:

[Al-Jazeera ilichapisha kwenye tovuti yake mnamo 26/01/2025: (Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa anazishinikiza Jordan, Misri, na nchi nyingine za Kiarabu kupokea wakimbizi zaidi wa Kipalestina kutoka Gaza, baada ya vita vya Israel dhidi ya Ukanda huo kusababisha janga la kibinadamu... Na alipoulizwa ikiwa pendekezo hili ni la muda mfupi au la muda mrefu, Trump alisema "Inaweza kuwa hivi au vile"]. Je, hii haimaanishi kuwa Trump anawaweka watawala wa Jordan na Misri katika mzunguko finyu wa aibu, haswa kwa kuwa hapo awali walikuwa wakitamka kuwa hawakubaliani na uhamishaji huu? Kisha, je, hiyo inamaanisha kuwa Trump anapanga kuufanya Ukanda wa Gaza uwe tupu bila watu wake ili kuunganishwa na umbo la Kiyahudi, haswa kwa kuwa watawala wa Kiarabu, bali watawala wote wa Waislamu, wako kimya kama makaburi bila kuchukua hatua yoyote mbele yake? Na je, hii inamaanisha kuwa kuna mabadiliko katika sera ya Marekani, au ni ile ile lakini kwa mtindo tofauti?

Jibu:

Ili kuweka wazi jibu la maswali hapo juu, tunatathmini mambo yafuatayo:

1- Trump hafichi malengo yake, bali anayasema waziwazi tofauti na mtangulizi wake Biden. Kwa mfano, Biden alikuwa akiwahadaa watu kwamba Amerika inafanya kazi kutekeleza mradi wa suluhu ya mataifa mawili, lakini ilikuwa ni kauli tu isiyo na maana! Al-Jazeera ilichapisha kwenye tovuti yake mnamo 04/01/2024: (Rais wa Marekani Joe Biden alisema jana Ijumaa kuwa kuna mifumo kadhaa ya suluhu ya mataifa mawili, akibainisha kuwa nchi kadhaa katika Umoja wa Mataifa hazina vikosi vyao vya kijeshi... Al-Jazeera 04/01/2024). Hii ina maana kwamba Biden alikuwa akiashiria dola ya aina hiyo isiyo na vikosi vya kijeshi! Lakini Trump alitaja ukweli wa juhudi zake bila kuwahadaa watu. Alitamka wakati wa kampeni yake ya uchaguzi akisema: (Ninapotazama ramani ya Mashariki ya Kati, ninaona Israel ni doa dogo sana. Kwa kweli, nilisema je, kuna njia ya kupata maeneo zaidi? Ni ndogo sana... Sky News 19/08/2024). Maana yake ni kwamba anataka kupanua umbo la Kiyahudi kwa kuhalalisha makaazi ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi na kuwapa uhuru wa kunyakua ardhi na kuanzisha makaazi mapya juu yake.

2- Hili linathibitishwa na uteuzi wake wa mtu anayeshirikiana na mtazamo wake kama balozi wa Amerika katika umbo la Kiyahudi, naye ni Mike Huckabee, ambaye Trump alimwelezea kwenye akaunti yake ya Truth Social mnamo 13/11/2024 kwamba "anaipenda Israel na watu wa Israel, na vivyo hivyo watu wa Israel wanampenda, na Mike atafanya kazi bila kuchoka kuleta amani Mashariki ya Kati." Miongoni mwa matamshi ya awali ya Mike Huckabee ni yale yaliyochapishwa na BBC mnamo 13/11/2024 yakisambazwa kutoka Channel 12 ya Kiyahudi kuwa Huckabee alijulikana kwa matamshi yake ya kuunga mkono umbo la Kiyahudi, ikiwemo kauli yake ya mwaka 2015 akisema: "Madai ya Israel ya kutaka kuunganisha Ukingo wa Magharibi ni yenye nguvu zaidi kuliko madai ya Marekani juu ya Manhattan." Ana video kwenye mitandao ya kijamii alizochapisha mwaka 2017 akisema "Hakuna kitu kinachoitwa Ukingo wa Magharibi, ni Yudea na Samaria. Hakuna kitu kinachoitwa makaazi ya walowezi, ni jamii, ni vitongoji, ni miji. Hakuna kitu kinachoitwa uvamizi."

3- Balozi huyu amekariri matamshi yake hayo na Channel 7 ya Kiyahudi mnamo 13/11/2024 akisema: "Siwezi kusema kitu ambacho sikiamini. Sijawahi kuwa tayari kutumia neno Ukingo wa Magharibi, hakuna kitu kama hicho, nazungumzia Yudea na Samaria. Na nawaambia watu hakuna uvamizi." Alisema: "Kumbukeni kuwa katika kipindi cha miaka minne ya Trump kuwa Rais, hakujawahi kuwa na Rais aliyekuwa akiiunga mkono zaidi Israel katika historia kuliko yeye. Kila kitu kuanzia kuitambua Jerusalem kama mji mkuu hadi kuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv hadi Jerusalem na kutambua Milima ya Golan kama miliki halali ya dola ya Israel, na pia kutojaribu kushinikiza suluhu ya mataifa mawili, kwa sababu si ya vitendo na haiwezi kutekelezeka." Alisema "Siamini kuwa suluhu ya mataifa mawili ni halali, huu ni msimamo nilioshikilia kwa miaka mingi, na ni msimamo ambao Trump anakubaliana nao na nategemea utaendelea." Kupitia matamshi haya, yanaonekana wazi mwelekeo wa sera ya Trump kuelekea kadhia ya Palestina, kwamba ni kuhalalisha uvamizi katika Ukingo wa Magharibi na makaazi ya walowezi.

4- Hii ina maana kwamba utawala wa Trump hauna mradi mpya maalum kwa kadhia ya Palestina wa kuwatafutia dola ya ukubwa wowote ule, bali mambo yanaelekea kwenye utambuzi rasmi wa Amerika kwa umbo la Kiyahudi juu ya uhalali wa makaazi ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi kama yanavyoashiria matamshi ya balozi wa Amerika katika umbo la Kiyahudi, na kauli yake kuwa Trump anamuunga mkono katika hilo. Trump amemmiminia sifa, na hii inamaanisha kusifu mawazo anayobeba kuhusu kadhia hii. Hili linathibitishwa na Trump kuondoa vikwazo kwa walowezi wa Kiyahudi waliofanya makosa ambayo Amerika iliyaona kuwa kinyume cha sheria wakati wa utawala wa Biden. Kwa hivyo, amani anayoimaanisha Trump ni kukubaliana na umbo la Kiyahudi juu ya kile ilichokinyakua katika ardhi za Ukingo wa Magharibi na kujenga makaazi ya walowezi, huku akipa Mamlaka ya Palestina haki ya kubaki kwa sasa kwa kutoa utawala fulani wa ndani ili iendelee kulitumikia umbo la Kiyahudi chini ya jina la uratibu wa usalama (security coordination), na kuwachosha watu kwa kuwakusanyia kodi ili viongozi wa Mamlaka hiyo wapate riziki huku wakitoa huduma ndogondogo za manispaa.

5- Trump alijaribu kuonyesha uwezo wake wa kufikia anachotaka na kwamba yeye ndiye anayeweza kutengeneza amani ili kuwahadaa watawala wa eneo hilo na kuwapumbaza kama shetani anavyowapumbaza wafuasi wake. Al-Jazeera ilichapisha mnamo 23/01/2025: (Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa utawala wake umekamilisha katika muda wa siku 4 zaidi ya kile ambacho utawala wa Rais wa zamani Joe Biden ulikamilisha katika muda wa miaka 4, akisisitiza kuwa bila utawala wake makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza yasingefikiwa wiki hii. Pia alitaja kuwa Saudi Arabia itawekeza dola bilioni 600 nchini Marekani, lakini ataiomba ifikishe hadi trilioni moja..). Pamoja na hayo, Trump aliambatanisha "begi la zawadi" na makubaliano haya kwa umbo la Kiyahudi kama ilivyotaja gazeti la Kiyahudi la Yedioth Ahronoth mnamo 14/01/2025: (Israel itakuwa na haki ya kusitisha mapigano ikiwa itaona umuhimu wa kufanya hivyo, na Ikulu ya Marekani itaweka uzito wake kufuta vikwazo vilivyotangulia vya utawala wa Biden kwa baadhi ya walowezi waliofanya vitendo vya kihalifu, na itafanya kampeni ya kimataifa dhidi ya mahakama mbili za Umoja wa Mataifa zilizoanzisha uchunguzi au mwendendo wa kisheria dhidi ya Israel, hususan dhidi ya Netanyahu na Waziri wake wa Ulinzi Gallant.. kwa tuhuma za kufanya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu).

6- Hivyo basi, Trump katika vipindi vyake viwili vya urais, cha kwanza na hiki cha sasa, anabeba maslahi ya Mayahudi. Hata maazimio ya kimataifa yaliyowekwa na Amerika na mataifa mengine makubwa, ambapo Amerika ilikuwa ikizifuata nchi zinazokiuka maazimio hayo, Trump ameyafuta maazimio hayo yanayopingana na maslahi ya Mayahudi. Alifuta maazimio ya Umoja wa Mataifa yanayouchukulia Ukingo wa Magharibi kuwa ardhi iliyovamiwa ambayo umbo la Kiyahudi haina haki ya kujenga makaazi humo, bali ni lazima ijiondoe hadi mipaka ya Juni 4, 1967. Pia alifuta maazimio ya Umoja wa Mataifa kuhusu Jerusalem Mashariki kuwa ni ardhi ya Palestina iliyovamiwa, na vilevile alifuta maazimio yake yanayohusu Milima ya Golan kuwa ni ardhi ya Syria iliyovamiwa, na akatambua uhalali wa uamuzi wa umbo la Kiyahudi wa kuunganisha Jerusalem na Milima hiyo. Hilo linathibitisha kuwa atatambua uhalali wa makaazi ya walowezi na kile walichokinyakua Mayahudi hadi sasa katika Ukingo wa Magharibi na kuruhusu ujenzi zaidi wa makaazi au upanuzi wake. Hilo limeanza alipotoa msamaha kwa walowezi walioekewa vikwazo wakati wa zama za Biden.

7- Trump ataendelea na mpango wake wa kuliimarisha umbo la Kiyahudi kwa kuzifanya nchi nyingine za eneo hilo zihalalishe mahusiano (normalization) na umbo hili ili kutambua uhalali wake na unyakuzi wake wa Palestina. Miongoni mwa nchi zinazopewa kipaumbele kwa hilo ni Saudi Arabia, haswa kwa kuwa uhusiano wa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi ni uhusiano madhubuti na Trump ambaye anafuatilia kwa nguvu uhalalishaji wa umbo la Kiyahudi na Saudi Arabia. Hilo linaweza lisichelewe, kwani kutii kwa utawala wa Saudi kwa kile kinachotakiwa na utawala wa Republican chini ya uongozi wa Trump kunatambulika kwa kila mwenye macho na busara. Trump alitangaza mnamo 23/01/2025 kwamba ("Saudi Arabia itawekeza dola bilioni 600 katika uchumi wa Marekani, na nitaomba zifikishwe hadi trilioni moja"... Al-Hurra ya Marekani 23/01/2025). Alitaja kuwa hilo lilifanyika katika mazungumzo ya simu na mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi, Ibn Salman, jioni ya Jumatano 22/01/2025. Yaani, kwa simu moja tu, mtawala halisi wa Saudi alitii mara moja ombi la Rais wa Amerika kusaidia uchumi wa Amerika kwa mamia ya mabilioni ya dola. Hii inaashiria kiwango cha utayari wa utawala wa Saudi kunyenyekea maombi ya Amerika katika zama za Trump. Kwa hiyo, kwa simu nyingine tu, Ibn Salman atasimama na kutangaza utayari wake wa kuhalalisha mahusiano na umbo la Kiyahudi pindi atakapoulizwa kufanya hivyo.

8- Kwa hiyo, yeyote anayetafakari mienendo ya Trump inayounga mkono umbo la Kiyahudi atapata kuwa tamko la Trump lililokuja katika swali kuhusu kuufanya Ukanda wa Gaza kuwa tupu bila watu wake na kuunganishwa na Mayahudi, haswa alipoulizwa (ikiwa pendekezo hili ni la muda mfupi au la muda mrefu, Trump alisema "Inaweza kuwa hivi au vile"... Al-Jazeera 26/01/2025), yeyote anayetafakari hayo ataona kuwa ni jambo la kawaida kwa Trump. Ama yaliyokuja katika swali: (Je, hii haimaanishi kuwa Trump anawaweka watawala wa Jordan na Misri katika mzunguko finyu wa aibu, haswa kwa kuwa hapo awali walikuwa wakitamka kuwa hawakubaliani na uhamishaji huu), ukweli ni kwamba Trump hajali kuhusu wao, wawe katika aibu au la. Haswa kwa kuwa alishatamka awali kwa uwazi zaidi ya tamko hili, aliposema: ("Ninapotazama ramani ya Mashariki ya Kati, ninaona Israel ni doa dogo sana. Kwa kweli, nilisema je, kuna njia ya kupata maeneo zaidi? Ni ndogo sana"... Sky News 19/08/2024). Tamko lake la awali lilikuwa kuhusu upanuzi wa umbo la Kiyahudi na tamko lake la sasa ni kubainisha njia mojawapo ya kupanua umbo hilo. Inaonekana Trump anataka kuandaa mazingira kwa watawala vibaraka kufuata mkondo huu wa uhamishaji wa lazima ambao hapo awali watawala waliukataa, haswa nchini Misri na Jordan. Kwa maneno mengine ni mchakato wa (kupima mapigo) ikiwa watawala hawa wanaweza kuwashinikiza watu kutekeleza tamko la Trump na kuwahamisha kutoka nchi yao ili iwe tupu na kuunganishwa na Mayahudi, au kuahirisha hilo hadi wakati mwingine ambao Trump ataona unafaa ikiwa watu watasimama kidete dhidi ya tawala hizo mbili na kuzizuia kuchukua hatua hii ambayo ni usaliti kwa Mwenyezi Mungu, Mtume Wake, na Waumini.

9- Tunatambua kuwa watawala katika nchi za Waislamu, na haswa walio jirani na Palestina, hawamstahii Mwenyezi Mungu, Mtume Wake, wala Waumini. Na kwamba kutekeleza amri ya Trump ni miongoni mwa vipaumbele vyao. Hili liko wazi kutokana na haraka yao ya kumpongeza Trump kwa ushindi wake katika uchaguzi na urais wa Marekani, licha ya kwamba alikuwa hafichi upendeleo wake kwa Mayahudi na uadui wake kwa Uislamu na Waislamu. Pamoja na hayo, watawala hawa walishindana kumpongeza:

a- RT (Habari za Ulimwengu wa Kiarabu) ilichapisha mnamo 06/11/2024: [Ikinukuu kutoka shirika la habari la Saudi "WAS", pongezi za mfalme wa Saudi kwa Trump, ambapo alisifu "ubora wa mahusiano ya kihistoria yaliyoimarika kati ya nchi hizo mbili na watu wawili marafiki, ambayo kila mmoja anajitahidi kuyaimarisha na kuyaendeleza katika nyanja zote." Vilevile ilichapisha pongezi za Rais wa Uturuki... (Akisema kupitia jukwaa la X: "Nampongeza rafiki yangu Donald Trump aliyeshinda uchaguzi wa Rais.. Tunatumai kuwa mahusiano kati ya Uturuki na Marekani yataimarika..")]

b- Kisha Al-Jazeera ilichapisha mnamo 06/11/2024 pongezi kutoka kwa Rais wa Misri: ["Natoa pongezi zangu za dhati kwa Rais mteule wa Marekani Donald Trump.. na kuimarisha mahusiano ya ushirikiano wa kimkakati kati ya Misri na Marekani na watu wao wawili marafiki." Kisha kutoka kwa mfalme wa Jordan: "Pongezi bora kwa Rais Donald Trump kwa ushindi wake katika uchaguzi wa urais wa Marekani. Tunatarajia kufanya kazi nanyi tena ili kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya Jordan na Marekani..", na pia kutoka kwa Waziri Mkuu wa Pakistan kwenye jukwaa la X: "Nampongeza Rais mteule Donald Trump kwa ushindi wake wa kihistoria kwa muhula wa pili! Na natarajia kufanya kazi kwa karibu na utawala ujao ili kuimarisha na kupanua ushirikiano kati ya Pakistan na Marekani"] ...nk.

c- Hata Ahmad Al-Sharaa, mkuu wa utawala mpya nchini Syria, alifuata mkondo huo huo na kuchapisha kwenye tovuti ya Facebook mnamo 20/01/2025: "Kwa niaba ya uongozi na watu wa Jamhuri ya Kiarabu ya Syria, nampongeza Donald Trump kama Rais wa Marekani" akisema "Tuna imani kuwa Trump ni kiongozi mwenye uwezo ambaye ataleta amani Mashariki ya Kati na kurejesha utulivu katika eneo hilo."

Hawa ndio watawala katika nchi za Waislamu, Mwenyezi Mungu awaangamize; namna gani wanageuzwa!

10- Pamoja na hayo, tunatambua pia kuwa Ummah wa Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ kwa wanaume wake wa kweli na waaminifu watafanya matamshi ya Trump na wafuasi wake miongoni mwa watawala hao kuwa ni mavumbi yanayopeperuka. Kushikamana kwa watu wa Palestina, Ardhi Iliyobarikiwa, na makaazi yao ni jambo linaloshuhudiwa. Kwani yeyote aliyeshuhudia maelfu yao wakitembea kwa miguu katika hali ngumu ya hewa na hali ngumu zaidi ya ardhi, na pamoja na hayo wakiharakisha hatua zao kuelekea nyumba zao ambazo wanajua kuwa uvamizi wa kikatili wa Kiyahudi umeziharibu, lakini wanachukulia kufika hapo kuwa ni ushindi mkubwa; yeyote aliyeshuhudia hayo yote na kuyatafakari, atatambua kuwa matamshi ya Trump na hila zake za kuifanya Palestina iwe tupu bila watu wake, hata kama zitachanganyika na hila za wapenzi wake miongoni mwa watawala ruwaibidhah, yote hayo yatawarudia wahusika wake:

وَقَدْ مَكَرُوا مَكْرَهُمْ وَعِنْدَ اللهِ مَكْرُهُمْ وَإِنْ كَانَ مَكْرُهُمْ لِتَزُولَ مِنْهُ الْجِبَالُ

"Na hakika walipanga njama zao, na kwa Mwenyezi Mungu ziko njama zao, hata ikiwa njama zao hizo ni za kuondoa milima." (QS. Ibrahim [14]: 46)

Na hatimaye, Ardhi Iliyobarikiwa itarejea kwa watu wake ikiwa ni Nyumba ya Uislamu (Dar al-Islam). Watawala hawa wote ruwaibidhah watatoweka, na Dola ya Uislamu, Khilafah ya uongofu (Khilafah Rashidah), inarejea kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na kupigana na Mayahudi na kuondoa uvamizi wao ni jambo litakalotokea kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Kwani mkweli mwenye kusadikiwa ﷺ amesema katika Musnad Ahmad kutoka kwa Hudhaifa:

«...ثُمَّ تَكُونُ خِلَافَةً عَلَى مِنْهَاجِ النُّبُوَّةِ»

"...kisha kutakuwako Khilafah kwa njia ya Utume."

Vilevile Al-Bukhari ametoa kutoka kwa Abdullah bin Umar (ra) amesema: Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ akisema:

«تُقَاتِلُكُمْ الْيَهُودُ فَتُسَلَّطُونَ عَلَيْهِمْ...»

"Mayahudi watapigana nanyi, na nanyi mtawatawala (mtawashinda)..."

Pia Muslim ametoa kwa tamko kutoka kwa Ibn Umar kutoka kwa Mtume ﷺ amesema:

«لَتُقَاتِلُنَّ الْيَهُودَ فَلَتَقْتُلُنَّهُمْ...»

"Hakika mtapigana na Mayahudi na mtawaua..."

Na hapo, ardhi itang’ara kwa ushindi wa Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye kushinda.

11- Lakini kama tulivyotangulia kusema, na tunakariri katika hitimisho hili:

[Lakini kanuni ya Mwenyezi Mungu imehukumu kuwa hatatushushia Malaika kutoka mbinguni kutusimamishia Khilafah itakayopigana na adui wetu huku sisi tumekaa, bali anawashusha Malaika wake kama msaada na bishara ya ushindi wake kwa wanaume walioamini Mola wao na akawazidishia uongofu, jeshi la Waislamu, wenye subira vitani, wanaojikinga kwa kiongozi wao na kupigana nyuma yake dhidi ya maadui zao:

بَلَى إِنْ تَصْبِرُوا وَتَتَّقُوا وَيَأْتُوكُمْ مِنْ فَوْرِهِمْ هَذَا يُمْدِدْكُمْ رَبُّكُمْ بِخَمْسَةِ آلَافٍ مِنَ الْمَلَائِكَةِ مُسَوِّمِينَ

"Naam! Mkivumilia na mkacha Mungu, na wakakushambulieni kwa ghafla, Mola wenu Mlezi atakusaidieni kwa Malaika elfu tano wenye alama." (QS. Ali Imran [3]: 125)

Na hapo tutakuwa miongoni mwa waliostahiki bishara:

نَصْرٌ مِنَ اللهِ وَفَتْحٌ قَرِيبٌ وَبَشِّرِ الْمُؤْمِنِينَ

"Msaada utokao kwa Mwenyezi Mungu na ushindi ulio karibu; na wabashirie Waumini." (QS. As-Saff [61]: 13)]

28 Rajab 1446 H 28/01/2025 M

Share Article

Share this article with your network