Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Ombi la Pakistan la Kujiunga na Kikundi cha Wasambazaji wa Nyenzo za Nyuklia (NSG)

June 10, 2016
4436

Swali:

Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan ilitangaza kuwa (imewasilisha ombi rasmi la kujiunga na Kikundi cha Wasambazaji wa Nyenzo za Nyuklia (Nuclear Suppliers Group - NSG) katika hatua ambayo inaelekea kusababisha mpambano ndani ya klabu hiyo baada ya kupokea pia maombi ya kujiunga kwa India. Reuters: 20/05/2016). Marekani ilikuwa imepinga ombi la Pakistan... Hapo awali, Uchina ilipinga miito kadhaa ya kujiunga kwa India, lakini Marekani haikupinga... Upinzani wa Uchina dhidi ya kukubaliwa kwa India unaeleweka, lakini upinzani wa Marekani dhidi ya ombi la Pakistan bila kupinga ombi la India unazua maswali, kwa sababu serikali nchini India na serikali nchini Pakistan kwa sasa zote ni vibaraka wa Marekani. Hivyo, tunaelewaje undumilakuwili huu wa kushughulikia mambo? Kisha, nini kazi ya kikundi hiki? Naomba ufafanuzi wa suala hili, na Mwenyezi Mungu akulipe kheri.

Jibu: Tunatathmini masuala haya kama ifuatavyo:

Kwanza: Hakika jinsi mataifa ya kikafiri ya kikoloni yanavyoshughulika na vibaraka wao hutofautiana kulingana na nchi ya vibaraka hao, na tofauti ya lengo la ushirikiano huo kama ifuatavyo:

  1. Ama tofauti ya ushirikiano kulingana na nchi ya kibaraka, inategemea iwapo vibaraka hao ni watawala katika nchi za Kiislamu au walikuwa watawala katika nchi zisizo za Kiislamu. Hii ni kwa sababu mataifa hayo yanawatazama watawala katika nchi za Kiislamu kuwa ni wenye kuondoka, hivyo wanapofanya makubaliano yoyote na watawala hawa, huzingatia kwamba yatavunjwa mapema au baadaye watawala hawa watakapobadilishwa, na kwamba Waislamu hawakubali makubaliano na nchi yoyote ya kikafiri ya kikoloni isipokuwa kwa shinikizo na kulazimishwa, na hili halidumu. Kwa sababu hiyo, ingawa serikali nchini India na serikali nchini Pakistan kwa sasa ni vibaraka wa Marekani, lakini Marekani haisahau kwamba watu nchini Pakistan ni Waislamu ambao hawakubali ushawishi wa Marekani... Ama watu nchini India, wengi wao ni makafiri washirikina, na ukafiri ni milango mmoja. Hivyo, ushirikiano wa Marekani na serikali ya India ni tofauti na ushirikiano wake na serikali ya Pakistan.

  2. Kadhalika, ingawa serikali nchini India ni kibaraka wa Marekani kama ilivyo serikali nchini Pakistan pia ni kibaraka wa Marekani, lakini lengo la Marekani kwa nchi hizi mbili ni tofauti. Lengo kwa upande wa India ni kuifanya kuwa kichwa cha mkuki katika kukabiliana na Uchina, wakati kwa upande wa Pakistan, lengo ni kusimama dhidi ya mapambano ya Pakistan na Afghanistan dhidi ya Marekani. Kwa maneno mengine, lengo la kuipa silaha India ni kuidhoofisha Uchina, na lengo la kuipa silaha Pakistan ni kudhoofisha mapambano (muqawamah).

  3. Kutokana na mambo haya mawili, Marekani inaunga mkono serikali nchini India kinyuklia kwa nguvu na kwa silaha za kisasa ili kusimama dhidi ya Uchina, lakini haiungi mkono serikali nchini Pakistan kwa kuendeleza silaha za nyuklia; badala yake, ikiisaidia, huisaidia kwa silaha nyepesi na nzito za kawaida ili kusimama dhidi ya mapambano.

Pili: Na ili maneno yasiwe ya jumla, tutatathmini jinsi Marekani ilivyoshughulika na India na Pakistan tangu kila moja ilipokuwa nchi ya nyuklia:

  1. Ushindani wa Pakistan na India ulifikia kilele chake katika vita vya mwaka 1965 na 1971, na hiyo ilisambamba na juhudi za India katika kuanzisha mpango wake wa nyuklia, ambao unatishia usalama wa Pakistan. Kwa hiyo, Pakistan ilianza kujenga mpango wa siri wa nyuklia kwa madhumuni ya kijeshi. Muelekeo huu ulifichuliwa kwa mara ya kwanza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan (Zulfiqar Ali Bhutto), ambapo alisema: "Ikiwa India itaunda bomu la nyuklia, basi sisi tutakula nyasi na kufa kwa njaa, na tutarudi nyuma miaka elfu moja, lakini tutapata letu pia... Wakristo wana bomu la nyuklia, Wayahudi wana bomu la nyuklia, na sasa Wahindu wana bomu la nyuklia, kwa nini Waislamu pia wasiwe nalo?" (Yasin, Rahil (16 January 2009). "War clouds hovering over South Asia". Weekly Blitz (Dhaka).). Pakistan ilianzisha taasisi ya utafiti wa nyuklia, inayojulikana kama (Halmashauri ya Nishati ya Nyuklia), na jitihada za Pakistan zilikuwa ni kupata nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani. Mnamo mwaka 1965, tanuri la kwanza la utafiti lilianza kazi yake, na mnamo mwaka 1972, kituo cha kwanza cha nishati ya nyuklia ya urani ya asili kilifunguliwa, na kituo cha maji mazito (Kituo cha Nishati ya Nyuklia cha Karachi), na viliwekwa chini ya uangalizi wa kina wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA)... Juhudi za Pakistan ziliendelea kawaida katika uwanja huu mpaka ulipotokea mlipuko wa nyuklia wa India mwaka 1974, ambapo hisia za Waislamu nchini Pakistan zilipanda na kuathiri kasi ya juhudi za Pakistan za kujenga vituo vyake vya nyuklia na kupata au kuzalisha mafuta ya nyuklia, ambapo ilifanikiwa kufanya hivyo kufikia mwaka 1987.

Kutokana na wingi wa silaha za kawaida za India, Pakistan ililazimika kufuata sera ya kutumia silaha za nyuklia ili kuzuia kuingia kwa vikosi vya kijeshi ndani ya ardhi ya Pakistan. Aidha, Pakistan ilianza kujenga mpango kabambe wa makombora ya balistiki (Ghauri, Shaheen, M-11, Tarmuk... n.k) yanayoweza kubeba vichwa vya nyuklia (http://www.atomicarchive.com/Reports/India/Missiles.shtml).

Hivyo basi, Pakistan ilijitahidi kwa nguvu wakati wa Vita Baridi na baada yake kupanua mpango wake wa nyuklia, ili kujumuisha mbali na uzalishaji wa vichwa vya nyuklia, mifumo ya uzalishaji wa makombora ya balistiki, na kurekebisha ndege ili ziweze kubeba vichwa vya nyuklia.

  1. Marekani pia iliunga mkono juhudi za India za kujenga mpango wake wa nyuklia wakati wa Vita Baridi na baada yake, na iliipatia tanuri la utafiti la maji mazito (CIRUS); kwa ajili ya kupata plutoniamu kwa ajili ya mlipuko wa nyuklia wa India mwaka 1974. Msimamo wa Marekani ulikuwa baridi baada ya mlipuko huo, wakati Washington ilipoamua kujadili upya mkataba wa miaka 30 wa kutoa urani iliyorutubishwa kwa ajili ya kituo cha nishati ya nyuklia huko Tarapur (nje ya Bombay).

Mazungumzo haya ya mkataba na Marekani yaliipa India fursa ya kipekee ya kupanua uwezo wake wa nyuklia na upeo wake wa ulinzi, na kuachia vifaa vya nyuklia vinavyoweza kugawanyika, na kuendeleza ngao dhidi ya makombora ya balistiki na nyambizi za kurusha makombora yenye vichwa vya nyuklia, jambo ambalo linaipa India faida ya wazi... India pia ilianza mkondo wa kivita sambamba wa kutengeneza makombora (Agni, Prithvi... n.k) na kuendeleza miundombinu yake ya kijeshi. (http://www.atomicarchive.com/Reports/India/Missiles.shtml)

  1. Hivyo, India na Pakistan zikawa nchi za nyuklia, na kwa ushindi wa chama cha (Janata) kinachoiunga mkono Marekani mnamo Aprili 1998 katika uchaguzi, anga ilibadilika ghafla, ambapo chama cha (Bharatiya Janata) kilifanya majaribio matano ya nyuklia, yakifuatiwa na milipuko sita ya nyuklia upande wa Pakistan ambao serikali yake pia ni kibaraka wa Marekani. Itikio la utawala wa Clinton lilikuwa ni kuweka vikwazo kwa nchi zote mbili kuelekea mwishoni mwa kipindi chake cha urais, na hiyo inaonyesha utambuzi wa kimyakimya wa Marekani kwa nguvu hizo mbili za nyuklia katika bara dogo la India.

  2. Chini ya utawala wa Bush, uhusiano wa Marekani na Pakistan na India ulibadilika pakubwa. Marekani ilitambua uwezo mkubwa wa India, na ikawa mgombea wa kuwa kama ngome imara dhidi ya Uchina na ushirikiano wa kimkakati na nchi hiyo. Wakati huo huo, Marekani iliipa Pakistan hadhi ya mshirika mkuu nje ya shirika la NATO (Major Non-NATO Ally), ambapo Marekani iliitaka Pakistan kupigana na "ugaidi" kwa niaba yake katika maeneo ya kikabila. Sera hii ilikuja kujulikana kama (the de-hyphenation of relations), yaani Marekani ilifuata sera moja kuelekea India, na nyingine kuelekea Pakistan kama ilivyoelezwa hapo juu.

  3. Kutokana na sera hii ya Marekani kwamba India iwe mstari wa mbele wa Marekani dhidi ya Uchina, na Pakistan iwe mstari wa mbele wa Marekani dhidi ya mapambano... na kwa sababu watu nchini Pakistan ni Waislamu kwa sehemu kubwa, na watu nchini India wengi wao ni makafiri washirikina... ndiyo maana Marekani ilikuwa:

a- Inaiunga mkono Pakistan kwa silaha za kawaida ili kupigana na mapambano, na si msaada wa nyuklia... Hata misaada ya kiuchumi na kijeshi kwa Pakistan iliyoongezeka chini ya utawala wa Reagan ilikuwa ni njia ya kuzuia mpango wa nyuklia wa Pakistan. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kwa masuala ya usalama, sayansi na teknolojia (James Buckley) alieleza kwa ufupi akisema: "Badala ya vikwazo madhubuti dhidi ya mpango wa nyuklia wa Pakistan vilivyowekwa na utawala uliopita, tunatumai kuushughulikia kupitia njia za kawaida, ili kutuliza hofu za nchi kama Pakistan, ili isifikirie kujenga uwezo wa nyuklia hapo awali" (Quoted in Akhtar Ali, Pakistan's Nuclear Dilemma: Energy and Security Dimensions (Karachi: Economic Research Unit, 1984), p. 10). Njia za kawaida humaanisha misaada ya kiuchumi na kijeshi ya kawaida. Sera hii ya Marekani iliendelea kwa kutoa msaada wa nyuklia bali kwa kuhimiza kutokuendeleza mpango wa nyuklia wa Pakistan (...na Rais wa Marekani Barack Obama alihimiza Pakistan mnamo Oktoba kuepuka kuendeleza mpango wake wa silaha. Reuters: 20/05/2016).

Vilevile, Marekani imekataa mara kwa mara kufanya makubaliano ya nyuklia na Pakistan na imekataa kuingia kwake katika Kikundi cha Wasambazaji wa Nyenzo za Nyuklia (NSG)... Upinzani dhidi ya kuingia kwa Pakistan katika kikundi hicho ulikuwa ni ili kuilazimisha Islamabad kutoendeleza silaha za nyuklia za kimbinu kupitia matumizi ya plutoniamu inayozalishwa nchini, kwa sababu uwiano wa plutoniamu inayotumika kwa uzito unaifanya kufaa kwa kupunguza ukubwa wa vichwa vya nyuklia (http://www.dawn.com/news/1248033).

b- Lakini inaiunga mkono India kwa silaha za kawaida na za nyuklia pia, na ili kubainisha hilo, tutatathmini baadhi ya matukio ya msaada huu:

  • Mnamo Januari 2004, Rais Bush na Waziri Mkuu wa India Vajpayee walitangaza Makubaliano ya Ushirikiano wa Kimkakati (NSSP), ambayo yanahimiza ushirikiano wa nchi zote mbili katika nyanja nne zenye utata: nishati ya nyuklia ya kiraia, mpango wa anga wa kiraia, biashara katika teknolojia ya juu, na ulinzi wa makombora... Na mnamo mwaka 2005-2006, New Delhi ilipata ahadi kutoka kwa Marekani ya kupata mafuta ya nyuklia kwa uhuru kwa ajili ya mpango wake wa nishati ya nyuklia unaohusiana na silaha, bila kujifunga na makubaliano yoyote, kama vile mkataba wa kupiga marufuku majaribio ya nyuklia kwa jumla, na mkataba wa (kusitisha uzalishaji wa nyenzo zinazoweza kugawanyika), na bila vikwazo vyovyote kwenye mpango wake wa makombora. Mnamo mwaka 2007, India ilipata mkataba (123), unaoruhusu India na Marekani kushirikiana kwa amani katika masuala ya nyuklia. Mikataba hiyo ya nyuklia inaifanya India kurutubisha urani nchini kwa ajili ya mpango wake wa nyuklia, na hii inajumuisha ukiukaji wa wazi wa ahadi ya Marekani kwenye mkataba wa kutoeneza silaha za nyuklia (NPT), ambao unasisitiza kutokuruhusu "njia yoyote inayosaidia au kuhimiza au kushawishi utengenezaji wa silaha ya nyuklia kwa nchi yoyote kati ya nchi zisizoruhusiwa kupata silaha za nyuklia" (See SIPRI, The NPT: The Main Political Barrier to Nuclear Weapon Proliferation (London: Taylor and Francis, 1980), Appendix A, p.43.).

  • Gazeti la Asharq Al-Awsat lilichapisha kwenye tovuti yake mnamo 07/05/2016 kwamba Waziri Mkuu wa India Modi ameingia (katika mkataba mkubwa wa kijeshi na Marekani baada ya kupita miaka 14 ya kukataa kwa serikali za India zilizofuatana kusaini mkataba huo. Mkataba huu unaruhusu majeshi ya Marekani na India kutumia vituo vya kijeshi vya nchi zote mbili katika kutekeleza shughuli za ukarabati, matengenezo na ushirikiano wa pamoja wa baharini. Pia vikosi vya baharini katika nchi zote mbili vinashirikiana chini ya mkataba uliotajwa katika vita dhidi ya nyambizi, ambayo ni nyanja ya teknolojia nyeti ya kijeshi na mbinu ambazo Marekani haishiriki isipokuwa na washirika wake wa jadi. Marekani inamiliki meli kubwa zaidi za nyambizi duniani wakati Uchina inaizidi India katika meli zake za nyambizi...). Nyambizi ni muhimu kwa kutoa pigo la pili katika vita vyovyote vya nyuklia kwa sababu ya kutoweza kugunduliwa na rada. Hivi karibuni India imeweza, kwa urahisi wa mkataba huo, kufanya jaribio la mafanikio la kombora la balistiki kutoka kwenye nyambizi inayoitwa (Ariana), na jambo hili limezikasirisha Uchina na Pakistan kwa sababu linaonyesha India kupiga hatua kuelekea uwezo wake wa kutoa pigo la pili (http://missilethreat.com/china-concerned-about-indian-submarine-missile/).

  • Kulitokea majaribio ya kuijumuisha India katika Kikundi cha Wasambazaji (NSG) kwa uungaji mkono wa Marekani lakini Uchina ilipinga... Lengo la Marekani katika wito wa kuijumuisha India katika Kikundi cha Wasambazaji wa Nyenzo za Nyuklia lilikuwa kwamba kuingizwa huku kutaipatia India nyenzo za nyuklia zinazohitajika ili kuzidi idadi ya vichwa vya nyuklia vya Uchina (http://www.icanw.org/the-facts/nuclear-arsenals/).

Tatu: Ama uhalisia wa Kikundi cha Wasambazaji wa Nyenzo za Nyuklia (NSG) ni kama ifuatavyo:

  1. Kikundi hiki kiliundwa kufuatia mlipuko wa India mnamo Mei 1974, na mkutano wake wa kwanza ulikuwa mnamo Novemba 1975. Kilianza na nchi saba (Canada, Ujerumani Magharibi, Ufaransa, Japani, Umoja wa Kisovieti, Uingereza, Marekani). Mnamo 1976-1977 wanachama wake wakawa 15, kisha wakaongezeka mpaka sasa kufikia wanachama 48... Lakini ushawishi wa kweli unadhibitiwa na mataifa makuu ya nyuklia na hasa Marekani.

  2. Kikundi hiki kinalenga kudhibiti uenezaji wa silaha za nyuklia kupitia kudhibiti usafirishaji na uhamishaji wa nyenzo zinazoweza kutumika katika kuendeleza silaha za nyuklia, na kuboresha njia za usalama na ulinzi kwa nyenzo za nyuklia zilizopo. Kikundi hiki huamua nchi zinazoruhusiwa kununua nyenzo na teknolojia za nyuklia na nchi ambazo ni marufuku kushirikiana nazo.

  3. Udhibiti wa kujiunga na kikundi hiki hausalimiki na ushawishi wa mataifa makuu ya nyuklia hususan Marekani kulingana na maslahi yake... Vilevile, Kikundi cha Wasambazaji wa Nyenzo za Nyuklia hakiwezi kuunda seti ya sera zenye ufanisi zaidi za kushughulikia uenezaji wa nyuklia na kudhibiti mauzo ya nyenzo kwa nchi bila udhibiti wa mataifa makuu ya nyuklia, yakiongozwa na Marekani, kupitia ufuatiliaji wa mauzo hususan yale yanayoainishwa kama nyenzo zenye matumizi ya aina mbili (dual-use). Hapa kuna nafasi ya unyonyaji kwa ajili ya maslahi ya mataifa makuu hususan Marekani, ikiruhusu na kuzuia kwa kisingizio cha matumizi ya aina mbili...

Kwa hiyo, ingawa kujiunga na Kikundi cha Wasambazaji wa Nyenzo za Nyuklia kunarahisisha upatikanaji wa nyenzo za nyuklia na mahitaji yake jambo linalosaidia katika kasi ya uzalishaji na maendeleo... n.k, lakini jambo hili lazima liandamane na ufahamu na umakini juu ya mipango ya nchi hizo zinazodhibiti, ili kujiunga huko kuwe njia kwa nchi inayojiunga kuendeleza mpango wake wa nyuklia na si kutumiwa na nchi hizo...

4 Ramadhani 1437 H 09/06/2016 M

Share Article

Share this article with your network